Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, August 12, 2017

DUWA LA KUKU....34


Ilichukua muda, kabla huyo mama hajazindukana, mimi sikuwa nimepoteza fahamu kabisa ilikuwa ni kizunguzungu tu, ndicho kilinifanya nidondoke na huyo mama, nikawa nimekaa nikisubiria hali irejee vyema, na mama Ntilie akaniuliza naendeleaje nikasema;

‘Mimi nipo sawa, tuendelee…’nikasema hivyo.

‘Polisi walikuwa wanataka kuongea na huyu mama, …wanamuhitajia kituoni leo hii..nilishindwa kuwapa majibu ya haraka …sasa sijui huko kuna nini…’akasema.

‘Tusubirie ikibidi nitaenda mimi mwenyewe…’akasema huyo mzee

‘Na hiyo hali , ni nani atakuelewa huko…’akasema mama Ntilie

Na muda huo ndio huyo mama akazindukana, na akawa anajaribu kuituliza ile hali, kwa kujinyosha nyosha na kutikisa kichwa, na alipoulizwa hali na kama inawezekana apelekwe hospitali akasema;

‘Hapana mimi nipo ok…sijui ni kitu gani kimenipata….ila nataka kuondoka…’akasema
‘Polisi walipiga simu, walikuwa wanataka kuongea na wewe…’akaambiwa
‘Oh, basi mimi nakwenda huko huko najua labda ni kuhusu shauri la mwanangu,…’akasema sasa akitaka kuondoka

‘Lakini kwa hali hiyo utaweza kwenda huko…?’ akaulizwa

‘Ndio nitaweza hakuna jinsi,  japokuwa, mpaka sasa sijajua la kufanya ili kwanza atoke,..lakini yeye anahitaji maelezo kujua ni nini kilimtokea, anasema anahis mimi kama mama au baba tunafahamu tatizo alilo nalo,…kwani huyo binti aliye naye kamwambia eti sisi wazazi wake tunahusika,…sasa mimi nitamuambiaje….’akasema mama

‘Mimi nitamuambia kila kitu….na ni bora nikafungwe mimi mwenyewe…’akasema yule mzee.

‘Usije kuthibutu kumwambia kitu, mpaka nihakikishe nimeshindwa kumtibia, nina uhakika tatizo hilo litakwisha, lakini sijajuia ni nani wa kulitatua hilo…’akasema huyo mama

‘Mama mimi nina imani litakwisha tu….na kwisha kwake inatokana na nyie wawili…’nikajikuta nikisema hivyo, na sijui kwanini nilisema hivyo

‘Sawa nitarudi tuyamalize haya mazungumzo, lakini sio leo tena…’akasema akijiandaa kuondoka

‘Ngoja tuongozane…’yule mzee akasema.

‘Na nani, …hapana, wewe bakia hapa hapa,…’akaambiwa na huyo mama akaondoka

Tuendelee na kisa chetu

************************

‘Natabakiaje hapa kwani hapa ni nyumbani kwangu…’akasema yule mzee na kuanza kuondoka kumfuata mkewe, na sisi tukabakiwa tukiwa na maswali mengi kichwani. Huku mama Ntilie akisema;

‘Huyu mzee bado akili haijakaa sawa, na shukuru kuwa hiyo mimba sio ya kwake….’akasema

‘Hata kama ingelikuwa ni ya kwake nisngelikubali anihudumie, sitaki kabisa…’nikasema

‘Kwahiyo sasa hiyo mimba itakuwa ya nani…?’ akaniuliza mama ntilie

‘Kiukweli mpaka sasa siwezi kujua ni ya nani…na sina haja ya kutaka kujua…’nikasema

‘Kwa maelezo ya mwanzo ya huyo mama nilijua labda itakuwa ya huyo mzee, lakini sasa anasema mumewe alianza kuumwa, akawa hana nguvu tena…je alianza kuumwa wakati umeshafika au kabla…hapo mimi sijaelewa…?’ akauliza.

‘Mimi sijui, maana ndio nimeanza kuyasikia hayo hapa kwa huyu mama, japokuwa kuna maelezo yalitolewa awali kuwa huyu baba na kijana wake wanahusika,….lakini haya ya sasa yanazidi kunichanganya,..ina maana kuna namna nyingine ilifanyika, ….hata sijui tuyaache tu…’nikasema.
‘Namna nyingine kwa vipi, kuwa ulipandikiza mbegu ..kama ng’ombe hahaha..hapana kati ya hao wawili kuna mmoja anahusika, sasa baba katoka, kabakia kijana, …haya jiandae kama ni kijana ..inabidi akuoe, au sio…?’ akauliza

‘Sitaki na simtaki kabisa…huyo wanaendana na yule binti, rafiki yangu, huoni mpaka wamefungwa, kumbe walikuwa na jambo lao la pamoja…wanafaana hao…’nikasema

‘Mhhh….hapo sasa, unalo, huyo mtoto ni wako, na huna jinsi utamzaa, bila ya kujua baba yake ni nani, lakini mimi nashindwa kuelewa, ilikuwaje, watu waingie ndani usiku, wakufanyia waliyokufanyia wewe umelala tu kama gogo,…ndio naamini kuwa ni lazima kulikuwa na mtu wa ndani alikuwa anahusika….umeona eeh…’akasema.

‘Kama ulivyosikia, wao wanakufanyia madawa unakuwa hujijui,…ndio hivyo ilivyofanyika…, kiukweli mimi sijui..naona ni mtihani tu umenikuta…’nikasema.

‘Ingelikuwa ni mimi, ningeliwaganda hao hao, maana sababu kubwa ni wao, lakini utamgandaje mtu kama huyo, mtu kachanganyikiwa,…maana bado hapo naona hajakaa vyema, akili bado haijatulia, hata hivyo, wao wanastahiki kubeba gharama zote…ngoja kama tutaendelea kuwa pamoja nitakusaidia kupambana na hao watu hadi kieleweke…’akasema.

‘Haina haja, nilishaamua nitapambana mwenyewe na maisha yangu, nimegundua kuwa ili nikae salama, basi nitafute njia ya kusimama kwa miguu yangu mwenyewe,…na muhimu nimeshamkabidhi mwenyezi mungu yote yaliyotoea, mungu…’nikasema.

***********

Ilikuwa siku nyingine huyo mama alikuja pale tunapofanyia biashara, mumewe hakuwepo, kwani alipoondoka hapo kwenda polisi na mumewe alimfuata huko, sasa hatukuwa tumejua ni nini kitokea huko, tukawa na hamasa ya kusikia kutoka kwa huyo mama.

‘Mumeo yupo wapi…?’ tukamuuliza

‘Hata sijui huko alipo, siku ile alinifuata huko polisi, hakuwaelewana, ikabidi polisi wamfukuze, wakijua yeye bado kachanganyikiwa, na nilimuambia wazi atafute sehemu nyingine ya kuishi hadi hapo matatizo haya yatakapomalizika.

‘Kwahiyo mama uamuzi wako ni upi…?’ nikamuuliza

‘Nimeshaamua sirudi nyuma,….hilo hakuna wakunishauri …..nasubiria watoto angu waje, niwaelezee maamuzi yangu na wao watajua la kufanya, ila, sio wao au wazazi wangu watakaoweza kulimaliza hili, ni mimi mwenyewe ndiye nitalimaliza…’akasema.

‘Na vipi kuhusu mtoto…?’ tukamuuliza.

‘Kulikuwa na makubaliano yafanyike kati ya walioibiwa na hao wezi, yaani yule binti na mwanangu, tukaishia kulumbana tu…, wao wanataka walipwe kila kitu…, nikawaambia kulipwa, itachukua muda, na kulipwa ina maana ni mimi sasa nibebe mzigo huo…mimi nina kosa gani…sitaweza kulipa kwa hivi sasa, na aliyeiba ni huyo binti, mtoto wangu anasema hakumshauri binti aibe, yeye alimpigia simu kuwa kafanya hivyo, wakati ameshaiba na kutoroka
‘Aliniambia mimi nina matatizo, ambayo yeye anajua jinsi gani ya kutibiwa…’akasema kijana wangu.

‘Matatizo gani…?’ akaulizwa.

‘Ya kiafya, nisingelipenda kuyaongelea hapa maana yatanizalilisha….’akasema

‘Utayaongea tu, maana hapa unatakiwa uongee kila kitu,…sasa kwahiyo wewe ukaenda huko ..kwa huyo binti?’ akaulizwa.

‘Ndio nikaenda kama alivyonielekeza….’akasema
‘Ndio ulipofika akakuambiaje…?’ akaulizwa

‘Akaniambia kafanya jambo baya sana, hakujua wakati analifanya, kuna kitu kilimsukuma afanye hivyo, kuna kitu kila siku kilikuwa kikimshawishi afanye hivyo, na ikafikia hatua kikamuambia haya muda ndio huu fanya, usipofanya sasa hutaweza tena, na utaendelea kuwa masikini maisha yako yote…akafanya na , sasa kaanza kujuta na hajui atafanyaje kujirudi na kuliongelea hilo kwa hao aliowafanyia…’akaniambia.

‘Kwahiyo mpaka unafika kwake ulijkuwa bado hujajua kuwa kaiba…?’ akaulizwa.

‘Kiukweli mimi nilikuwa bado sijajua hilo, nashangaa watu wanadai kuwa nimeshirikiana naye, mimi nilikuwa sipo, niliafiri kidogo, niliporudi sijakaa vyema ndio napata hiyo simu…’akasema.
‘Ulisafiri kwenda wapi…?’ akaulizwa

‘Kuna sehemu nilielekezwa kuwa kuna mtaalamu wa kusaidia matatizo yangu ya kiafya ndio nilisafiri kwenda kwake…’akasema.

‘Ulisafiri kwenda wapi, maana tunahitajia kuhakiki ukweli wako….?’ Akaulizwa

‘Tanga….’akasema

‘Sasa ulijua muda gani kuwa huyo mdada kaiba..?’ akaulizwa.

‘Aliniambia yeye mwenyewe nilipofika, aliniambia alitoroka pale alipokuwa akifanyia kazi, na pesa nyingi, akiwa na maana atakwenda sehemu azifanyie biashara, akizalisha atazirejesha kwa wenyewe…’akasema.

‘Nikamwambia azirejeshe haraka kwa wenyewe….’akasema

‘Akasemaje…?’ akaulizwa na polisi

‘Kaibiwa zote, walikuja majambazi na bunduki wakamvamia na kumpora kila kitu, nahapo alipo hana hata pesa ya kula na anaogopa akitoka atakamatwa na polisi…kwahiyo ananiomba msaada wa pesa, na mimi nikamwambia sina pesa, mwenyewe nahitaji pesa ,wazazi wangu hawataki kunipa pesa tena…’akasema

‘Kwanini sasa hukutoa taarifa polisi kwa haraka ulipoonana naye, mpaka tulipoonza kukufuatilia, na kuwakamata…?’ akaulizwa na polisi.

‘Muda huo nilikuwa sipo vyema, akili yangu ilishavurugika, nina matatizo yangu, nina shida zangu, na nilijua anataka kunisaidia kumbe anataka mimi nimsadie…’akasema.

‘Kwasababu ya madawa ya kulevya au sio…?’ akaulizwa

Hapo akatulia kimia, na aliposhinikizwa ndio akakubali kuwa alihitajia madawa na pesa hana, na alihitajia msaada wa huyo binti kwa vile kasema kuna namna ya kumsaidia hilo tatizo liishe…’akasema.

Alipofikia hapo ndio mama Ntilie akamuuliza huyo mama.

‘Ina maana kumbe mtoto wako anatumia madawa ya kulevya…?’ 

‘Si ndio nawaambia mume wangu kanifanya kitu kibaya kiasi kwamba nashindwa kumsamehe,,,’akasema

‘Lakini sio yeye aliyemfundisha mtoto, au sio…?’ akaulizwa

‘Sio yeye, na hata yeye alikuwa hajui kuwa mtoto kajiingiza huko…’akasema

‘Sasa kwanini unamshutumu kwa kuharibika kwa mtoto…?’ tukamuuliza

‘Ni hivi…..’akatulia akiangalia simu yake kuna ujumbe was auto uliingia, na akajibu , halafu akasema;

‘Huyo mwanaume anakuja….’akasema

‘Anakuja hapa…?’ nikauliza.

‘Ndio maana alisema tuje kwako tuhakikishe tumeliweka hili jambo vyema, nilimuambia yeye anshitajika kuhakikisha wewe upo katika hali nzuri, maana wewe kumsamehe ni pamoja na kukulipa gharama zote, unakumbuka kuna kikao tulifanya nikamuambia hivyo…’akasema

‘Lakini mama mimi sihitaji msaada wake…nisingelipenda kumuingiza mtu kwenye haya matatizo tena…nyie wawili mnatakiwa msameheane kwangu itakuwa ni faraja…’nikasema

‘Hilo halina hiari….maana yote yalifanyika ndani ya nyumba yangu na waliofanya ni familia yangu, japokuwa hatuna uhakika ni nani mwenye huo mzigo, lakini wawili hao watawajibika,...na huyo mwanaume sio mtoto…mtoto aliingizwa bila hata kujua,…’akasema

‘Kwahiyo hata wewe hujajua ni nani ambaye tunaweza kusema ndio mwenye mtoto…?’ mama Ntilia akauliza.

‘Yaani sio rahisi….maana mume wangu alianza matatizo kabla hata huyu binti hajafika,….’akasema

‘Kwahiyo basi itakuwa ni kijana wako…’akaambiwa

‘Mhh…ni kwa vile sijawahadithia ilivyokuwa baadae….’akasema na kukatisha baada ya kusikia hodi, tulijua ni wateja, kumbe sio wateja.

Waliofika walikuwa wale wanunuzi wa kiwanja wakasema ninatakiwa mimi nikafungue akaunti benki kabla ya kuanza kazi ya malipo, na walisema kwa vile bado wapo kwenye michakao ya kukusanya pesa, na haijakamilika kwanza, wao wamekuja na kiasi kidogo tu cha kufungulia akaunti, na malipo kamili yatakuja baadae, mimi nikakualiana na wao,

Niliondoka na wao nikaenda kufungua akaunti benki, na wakati nataka kuachana nao , yule kiongozi akaniuliza

‘Binti, samahani kwa hili, wewe huna matatizo yoyote…?’ akaniuliza

‘Matatizo gani…?’ nikamuuliza

‘Huyu hapa ni mmoja wa wanafunzi wangu, kajaliwa kipaji cha ajabu, anaweza kukuangalia hivi tu akajua wewe una matatizo, yeye kajua wewe una matatizo …’akasema

‘Hapana mimi sina matatizo…’nikasema

Yule anayeambiwa ana kiaji hicho, akanisogelea na kuniangalia usoni kwa muda halafu akawa ananitizama taratubu kushuka hadi tumboni halafu akasema;

‘Hiyo mimba uliyo nayo sio ya kawaida…’akasema

‘Mhh, kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui, ila nilivyokuona nikahisi kuna uchafu mwilini mwako,…na kwa vile tunajua wapi ulipotokea maisha yako, na sasa tunagundua haya tukaona tukusaidie tu, kupambana na hili tatizo, hatuhitaji malipo yoyote, usiwe na shaka na hilo…’wakasema

‘Mhh..’nikaguna tu

‘Siku tukija kukulipa tutakuja tukiwa tumejiandaa, ni kisomo kidogo tu cha kumuomba mwenyezimungu na mengine tutamuachia yeye, na hili linatakiwa , kabla hujajifungua…’akasema

‘Lakini nitajifundua salama…?’ nikauliza

‘Baada ya maombi hayo, ya kumuomba mwenyezimungu kwa uwezo wake, utajifundua salama maana hayo waliyokufanyia ni mambo ya kishetani, na shetani hatakiwi awe mwilini mwa watu, akiwa mwilini atakusumbua sana, na mtoto atakuwa akisumbuliwa sana,…sasa kabla hujajifungua tutalifukuza hilo shetani mwilini mwako,..’akasema

‘Mimi hata sijui mnaongea nini…’nikasema

‘Tukija utajua…’wakasema na kuondoka.

****************.

Siku nyingine  wakaja yule mama , sasa akiwa na yule mzee, nilifurahi kuwaona wakiwa wote sambamba…na mama akaanza moja kwa moja kuhadithia mambo ya nyumbani kwake ambayo yanamfanya asiweze kumsamehe mume wake…

‘Nimekuja naye kaniomba tuje kuyaongea yale tuliyotaka kuyaongea, kwa msemo wake anataka wewe, ambaye kukosea ujue alichokukosea, na pili, tuone jinsi gani ya kukusaidia, yeye, kukusaidia…’akasema

‘Sisi hamu yetu ni kutaka kujua, kama kuna yoyote kati ya hao wawili, yaani mume wako na kijana ambaye anahusikana na huo ujauzito,..au sio binti…?’ akasema mama Ntilie.

‘Ni sawa..mimi sikuona haja ya kuyafanya haya mambo yawe makubwa, yaliyopita yamepita, …ila nilitaka kujua zaidi kuhusu huyo kijana wako, imekuwaje hadi kufikia hiyo hali,…?’ nikauliza.

‘Ni vyema nikaelezea yote kutokea pale nilipoachia, ndio utajua jinsi gani hayo yaliyotokea yalivyoiathiri familia yangu…na kwa vile yeye mwenyewe karuhus hilo, basi ngoja niwaelezee tu, na tukitoka hapa kila mtu atajua hamsini yake..’akasema huyo mama.

‘Tutasameheana kiukweli…’mimi nikasema na nikijaribu kutabasamu lakini huyo mama hakutoa tabasamu akasema;

‘Mnajua mlipokuja nyiee mabinti wawili, yule wa kwanza,ambaye yupo jela kwa hivi sasa na wewe ndio mliowezesha haya mambo kuanza kuonekana kwa uwazi, mabinti wengine walifanyiwa mabaya lakini, labda nisema ni kwasababu ya utoto wao, sikuweza kugundua kinachoendelea, au labda kutokana na mazindiko ya kichawi hata sielewi…’akaanza kuelezea.

Yule binti wa kwanza alifanyiwa na kushika mimba,  akaja kuitoa hiyo mimba, na ..yaliyotokea yanajulikana kwa huyu binti, sasa kwa huyu, ndio nikaamua kufanya uchunguzi wakwa kuweka vifaa maalumu chumbani kwa huyu binti, na lengo langu ilikuwa kubaini yale niyowahi kusikia , na kwa vile kuna mtu alishaniambia kweli wachawi wanaweza kuingia usiku usiwaone, lakini yeye ana vifaa vya kuwezesha kuwapiga picha,au kama picha imepigwa na karibu yake yupo mchawi au shetani anaweza kuisafisha na kuona kilichojificha.

‘Ndio nikawekeza hivyo vifaa….’akasema akimuangalia mume wake.

‘Yule jamaa aliweza kufanya hayo na siku nataka kwenda kuonana naye, akaptawa na dharura akasafiri, na kabla hajarudi ndio akaja huyo marehemu na maelezo yake ambayo, tulikuja kuyaamini kuwa huenda ndio sahihi, na kwasababu hiyo ikanifanya nisihangaike tena na huyo jamaa yangu, na mambo mengi yakawa yametokea hapa kati kati..kwahiyo hilo likasahaulika.

 ‘Ina maana mume wako na huyo mtaalamu wako, ndio waliweka hayo mazindiko aliyokuwa akiyasema yule marehemu…?’ akaulizwa.

‘Ndio, na hayo ndiyo yalimfanya huyo jamaa yao, kuweza kutuona hata akiwa huko kwake, na kuweza kuja usiku kwa mbinzu zao za kichawi na kufanya mamboyao bila kujulikana..na walitafuta sehemu nyingine zaidi, ndio huko kwa wale marafiki zangu, ..kote huko waliweka ili kila ninapokwenda ijulikane ninafanya nini…’akasema.

‘Mhh…mbona hatari…’akasema mama Ntilie.

 ‘Kama nilivyosema awali, nilipogundua hayo, nilitaka ndoa yetu ivunjwe mara moja, nikahangaika kisheria,lakini wazee wakagoma, wakanishauri sana, na kunisihi sana, hasa bab yangu mkubwa, wazazi wangu kama kawaida yao walishasema huo ni mzigi wangu wa kujitakia,..basi nikafuata ushauri wa baba mkubwa kuwa siwezi kumuacha mume akiwa kwenye hiyo hali anaumwa, nihangaike naye mpaka apone kwanza,…unajua inauma ikizingatiwa kuwa alimuingiza hata kijana wangu kwenye  mambo yake ..iliniuma sana…’akasema.

‘Hapo sasa tuambie kijana wako aliingizwaje…?’ akauliza Mama Ntilie

*************

Kama nilivyosema awali, mume wangu alikuja kuathirika akawa hana nguvu tena kama mwanaume na dawa zao za kishirikina zilihitajia hivyo, kufanya uchafu wao kwa watoto wa watu wasio na hatia, wakihitajia damu..ni mambo ya ajabu kabisa,…basi mume wangu alipoona hivyo ndio akamuendea huyo mtaalamu wao,huyo mtaalamu wao, akamwambia;

‘Dozi ya dawa haikatwishi,..kwahiyo ni lazima kutafutwa namna na namna ni kumtumia mtoto wako, awe kama wewe, afanye majukumu yako..mume wangu hakukubaliana na hilo awali, baadae akakubakubali akiwa hajui mtego uliwekwa hapo.

‘Kwahiyo ili mwanao awe wewe ni lazima afanye kazi zako, kama wewe , kama mume…ashiriki matendo yote tuliyokuwa tunayafanya, …’akaambiwa.

‘Nini,…hebu hapo, una maana gani hapo…, matendo yapi maana mnapokuja usiku mimi sijiuu nimelala..au sio…?’ akauliza.

‘Lakini nilikuambia tunafanya nini, au sio,…tukifika kwanza ni lazima wewe ufanye mambo kwa mkeo kupata baraka zake..huku tunashuhudia, ili zindiko lifanye kazi, ukishamaliza kwa mkeo ndio tunakuchukua hadi kwa mwanawali, na huko tunakwenda kutafuta damu ya mizimu, ambayo itawafurahisha na kuwezesha kuhamisha nyota ya utajiri kutoka milki ya vizaz vile na kuhamia kuja hapo kwenu…’akasema.

‘Oh, hapo..hata sielewi, maana sijawahi kuona ila nahisi kuna kitu kinafanyika..na bora mfanya hivyo hivyo, nisijue kinachofanyika,…kwani naweza kuchanganyikiwa, unajua sipendi, ila nafanya hayo kwa ajili ya kutaka huo utajiri, vinginevyo nisingelifanya,..yule baba mkwe ananikera sana, moyoni mwangu…’akasema.

‘Hapana ni lazima uelewe kinachofanyika ili ifanikiwe uwe wewe unafanya jambo ambalo upo huru nalo, hatuna haja ya kukuweka wazi ulione ila kibali chako ndicho tunakihitajia…’akaambiwa.

‘Ehe niambie..mimi inakuwaje..maana ndio hivyo, na kama kijana wangu ndio anatakiwa afanye, tafadhali, naomba asije kujua au kuwa na fununu hiyo….’yeye akaomba hivyo.

‘Ni hivyo, kwa vile wewe hufanyi kazi, kijana wako atachukua nafsi yako, atafanya kazi zako, ina mama , yeye atashiriki na mkeo ili kuipata baraka kama ulivyokuwa unafanya wewe kabla hatujawaendea hao wanawali….’akasema

‘What!!!..Una maana gani hapo…ina maana, wewe hapana, huyo ni mtoto haiwezekani…..’mume alisema kwa ukali

‘Kama hutaki utajiri basi,..na hilo ni lazima lifanyike kwanza,..huwezi kupata baraka za huyo mwenye nyota bila ya kuptia kwake, na unapitia kwake kwa njia hiyo, na unakwenda kwa wanawali kuiongzea nguvu, mizumu inafurahi,…muhimu ni kuwa  mkeo hajui,..yanayofanyika nyote hamuyaoni, wewe na kijana wako mnakuwa kama magogo tu, kinachowasukuma ni mizimu inatembea na nyie,…tusipoteze muda, maana hapo hakuna kurudi nyuma tena, ukitaka kukatiza haya mambo kafara lake ni damu ya mtu, ina maana mmoja wenu anakufa..’akasema.

‘Oh, hapana, sitaki hilo litokee, sitaki mtu afe…’akasema

‘Chagua unaendelea au unakatiza…ukikatiza kijana wako au mkeo, au hata wewe kesho unazikwa, na maisha yanaendelea…’akaambiwa,

‘Hapo umeniweka njia panda…’akasema

‘Kesho tutakuja kama kawaida na kijana wako atachukuliwa na yeye ataanza kazi zako,na hakikisha binti mpya analetwa kama kawaida, mtumie huyo kijana wako awe anawaleta mabinti, usiku watapitiwa na usingizi tutachagua mmojawapo, kazi inaendelea mpaka tumalize hili zoezi, baada ya hapo nyota inahamia kweko, wewe utaanza kujaa utajiri, …unaelewa…’akaambiwa.

Jamaa alivyo mjinga,… hakuwa na jinsi ikabidi akubali hivyo hivyo..bila hata kufiria athari zake.

‘Sasa hao mabinti walipatikanaje..?’ akaulizwa na mama Ntilie.

‘Kama nilivyosema awali mwanzoni alikuwa akichukua wafanyakazi wa ndani, wa muda, leo huyu anakaa siku mbili tatu, anaondoka kesho mwingine, yeye akijifanya anawasaidia mabinti wasiojiweza, alikuwa akienda hata vituo vya kulelea mayatima kule anamchagua yoyote kuwa aje afanye kazi kwa muda…mmi sijui, kwangu mimi niliona ni jambo la neema kuwasaidia waliopo kwenye mazingira magumu, kumbe mwenzangu ana ajenda yake ya siri.

‘Sasa akaja kuongea na kijana wake kuwa afanye paty, awaalike mabinti, ..yeye alimsisitizia mabinti, na kijana akawa anajiuliza ni kwanini baba anataka jambo kama hilo, kahisi labda ni kavile baba anataka yeye aoe, kwahiyo kati ya hao mabinti atamchagulia anayemfaa, kwahiyo yeye akafanya juhudi ya kuwachukua mabinti wazuri anaowafahamu , akawaalika na mabinti wengi wakakubali …

***************

Siku hiyo ya kijana kukabidhiwa mikoba ya baba yake ikafika, usiku mabinti walioalikuwa wakafika,…na hao wachawi wakawa safarini kuja huku,..wanajua wenyewe walivyosafiri, na mimi nikapangiwa madawa ya kufanyiziwa ili niendelee kulala kama siku nyingine..ili kijana wangu mwenyewe wa kumzaa aje afanye kazi ya baba yake,..’ hapo huyo mama akanyamaza kwa muda, akiwa kainamisha kichwa chini, baadae akainua kichwa huku machozi yanamtoka akasema;

‘Hebu jamani niambieni hapo hata ingelikuwa wewe unasikia jambo kama hilo limekuja kufanyika kwako, na anafanyiziwa mtoto wako, utajisikiaje, je utakuwa radhi kumsamehe mtu kama huyu..?’ akaniuliza

Nilibakia kimia, sikuweza kutoa jibu,…hapo hapo , akili ilikuwa imganda siamini kuwa ni kweli…

‘Hebu niambie kama ni wewe ungelikuwa umefanyiwa wewe hivyo na mumeo, ungelifanyaje, ungemsamehe tu, yaishe, je una uhakika gani kama hatakuja kurudia tena, je una uhakika gani kuwa hatafanya mengine makubwa zaidi ya hayo, je utamuelezaje kijana wako….maana mpaka sasa mtoto wangu ana matatizo makubwa yaliyotokana na vitendo hivyo..na kisa ni baba yao…

‘Huyu hapa shetani mkubwa,…’akasema akimnyoshea kidole.

‘Kwahiyo hebu kwanza hapo, huyo kijana wako kwa hivi sasa ana atatizo gani ni hayo ya kutumia madawa kama ulivyosema au kuna mengine…?’ nikauliza.

‘Huko kutumia madawa, imetokana na madhara ya hayo aliyofanyiwa, na alianza kutumia baadae,kwanza alianza kuvuta sigara, akaja pombe na baadae madawa…nitakuelezea hatua kwa hatua ili uelewe vyema…..na kukuelezea huko sio kwamba umchukia huyu mtu, …hapana, ni ili uelewe pia kuwa kijana wangu hana hatia na mambo hayo, hata kama yeye alikufanyia,..na …’kabla hajamaliza smu ya huyu mama ikaita, akaangalia ujumbe wa maandishi,

‘Wazazi wangu wananipigia simu natakiwa nikitoka hapa nikakutane nao, najua moja ya maswala ya kuongelea ni hili, je nipo tayari kuwa nao, au kuwa na huyo mwanaume…’akasema.

‘Mke wangu …’mumewe akataka kuongea jambo lakini yeye hakumruhusu akasema;

‘Ulitaka niyahadithie yote subiria nimalize , nikimaliza hawa ndio watakuhukumu na hukumu hiyo ni jinsi gani wewe uadhibiwe, na wakati huo huo, wewe ujue jinsi gani ya kubeba huu mzigo wa huyu binti..na huwezi kujitetea kuwa hutaweza, kazi bado unayo, hujaachishwa… ila kwangu, sahau….’akasema.

‘Mama…’mimi nikasema

‘Unataka niendelee au niache…?’ akaniuliza mimi

‘Endelea….’nikasema

Na  huyo mama akaendelea kumalizia sehemu iliyobakia…

NB: Tutakuja kuiona sehemu iliyobakia ambayo, ndio iliyomfanya huyo mama akatae kabisa kurudiana na mumewe.


WAZO LA LEO: Hutaamini kuna watu wamefikia hadi kuwaumiza watoto wao wa kuzaa, kwa ajili ya kuutafuta utajiri, wanaenda kwa waganga wanadanganywa wafanye hivi na vile, ..kuna wengine kweli wanaupata, utajiri wa kishetani, , ikiwa ni mtihani kwao, lakini hebu wachunguze kama wana raha maisha mwao, watakuwaje na raha wakati wanamuona mtoto wao akiwa hivyo, zezeta, hajiwezi,, na wachunguzeni kwenye vifo vyao wanakuwaje, maana madhambi kam hayo adhabu yake huanzia hapa hapa duniani,..…hivi jamani tumefikia hapo…INATISHA!
Ni mimi: emu-three

No comments :