Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, August 11, 2017

DUWA LA KUKU....33


Mnajua kuna vitu vingine ukivisikia kwa watu utasema wanazusha, huwezi kuamini, kuwa binadamu anawezaje kudanganyika na kufanya mambo mabaya bila kufikiria athari zake baadae, bila kujali familia yake, bila kujali watu wengine, lakini zaidi bila kujali damu yake mwenyewe ..mimi sikuamini hilo kabla…’akasema huyo mama

Yule mzee pale akawa kainama huku kashika shavu, akiashiria kuhuzunika sana
Mimi na mume wangu tulioana bila ridhaa ya wazazi wangu, labda hilo naweza kusema linaweza kuwa ni sababu sikuwa na radhi ya wazazi wangu,labda,…imefikia kila likitokea baya wanasema tulikuambia,sasa ubebe mzigo wako mwenyewe, wanadai walishamchunguza mume wangu na kugundua kuwa hataweza kubadilika, na mimi sasa nimeliamini hilo…

‘Sio kweli….’akasema mume wake kwa sauti ya unyonge.

Kumbe mume wangu baada ya kuona hilo kuwa wazazi wangu hawamtaki, yeye akaenda mbali zaidi na kufikiria kuwa anafanyiwa hivyo kwa vile anatokea kwenye familia masikini, kakulia kwenye mazingira ya kimasikini..ndio maana hathaminiki, kwahiyo alichofanya yeye ni kutafuta njia ya kulipiza kisasi,..nakumbuka siku moja tulipokwenda kusema sisi tutaoana mume wangu wakati anajibishana na wazee aliwaambia

‘Wazee wangu, mimi sikupenda niwe masikini au familia yangu iwe masikini, yote ni maisha tu, na huwezi kujua, ipo siku naweza kuwa kama nyie, na mkawa mnanitegemea mimi…’aliwaambia wazee wangu.

‘Sawa lakini hatutaki wewe umuoe binti yetu, maana wapo wengi tu, unaweza kuwaoa, mnaoendana nao, sisi tunajiuliza ni kwanini huyu, sisi tuna kujua wewe vilivyo.., tumepeleleza nyendo za kizazi chako na hata wewe mwenyewe ulivyokulia, hutaweza kutulia wewe, una tamaa, japokuwa hapo ulipo hauna kitu, ukipata utabadilika,…sisi ni waze tunajua mengi….’wakasema.

‘Wazee ipo siku mtanishangaa, ipo siku na mimi nitakuwa kama nyie na nyie mtakuwa hamna kitu, hilo nawahakikishia,.mimi nawajali na nitawasaidia kama wazazi wangu….’akasema

‘Utafanyaje wewe…?’ akaulizwa na wazee wangu

‘Katika dunia hii hakishindwi kitu ukiwa na nia, mimi nina nia ya kufikia hapo mlipo,  na ipo siku nitafanikiwa tu wazee wangu, na huwezi jua, ipo siku na nyie mtahitajia uwepo wangu, tuombeeni tu mungu, ipo siku mtajijutia, na siku ya leo iwepo kama kumbukumbu…’akasema.

‘Kwanini unasema hivyo…hamna haja ya kubishana na wazazi wangu nimeshakuambia nitasimamiwa ndoa na baba mkubwa, inatosha, sipendi hayo maongezi yako..?’ mimi nikamwambi ili tuondoke hapo.

‘Wewe huoni wanatufanyia hivi kwa vile wao wana utajiri, utajiri wao ni nini si mali tu, mali si inatafutwa, na sisi tutaitafuta kwa njia yoyote ile,..na huenda hata hiyo mali yao hawakuipata kwa halali, ngoja na mimi nitaitafuta wewe ngoja tu…’akasema .

‘Kiukweli kipindi hicho nilijua kwa vile anasoma , kwa vile ana juhudi ya kutafuta basi atafanikiwa kwa wivu huo wa maendeleo kumbe mwenzangu alikuwa ana ajenda yake kichwani, ana wivu wa kishetani, lengo lake ni kujitajirisha kwa haraka, kwa njia za kishetani..

‘Sijui alikutana na nani akamdanganya, pamoja na usomi wake wote huo, akakubali kujiingiza kwenye mambo ya kishirikina, akaenda kwa waganga wa kienyeji, akadanganywa…sijui elimu yake ilikuwa na maana gani sijui, labda ni kweli kama walivyosema wazazi wangu….’akasema.

‘Sikutaka kuyaongea haya tena….maana jinsi ninavyozidi kuyaongea ndivyo hasira zinazidi kunijaa …nilishaamua basi bora nibakie mwenyewe na hayo yaliyopita yapite tu,….’akaashiria mikono ya kukata tamaa.

Sasa kilichofanyika kipindi hicho ni kuwa,Mume wangu akawa ananiaga kuwa anakwenda safari za kikazi,mikoani, kumbe safari hizo zilikuwa sio za kikazi hasa, niliulizia kazini kwao, wakasema hawajawahi kumtuma huko kwenye huo mkoa, haya niliyafanya kabla sijafunuliwa huo ukweli, kumbe yeye alikuwa akienda kwa mganga mmoja ambaye wanasema anaaminika kwa mambo hayo….’akatulia.

‘Sasa huko ndio wakamdanganya, kuwa akifanya hiki na kile atafanikwia atakuwa tajiri, kama wazazi wangu, na zaidi ya wazazi wangu muhimu ajitahidi aibe nyota ya wazazi wangu,..sasa sijui nyota za mtu zinaibiwaje, …wenyewe wanajua walichokifanya, ila alitakiwa afanye mambo kadha wa kaadha, kama alivyoelekezwa,..hakuwa peke yake mwenye ndoto hizo za ajabu, alikuwa na wenzake na wote hao wameishia kubaya kama alivyoishia huyu mwanaume hapa….’akasema

‘Huyo mtu waliyemuendea alitaka kuwakomoa, yeye naye alikuwa na visasi vyake akaona atumie mwanya huo kufanikisha mambo yake, sijui kwanini wanadamu tunachukiana, wajinga hawa wakaingia kwenye anga za huyo mtu….’akatulia.

‘Aliporudi nikamuona mwenzangu kabadilika, kipindi hicho sikuwa nafahamu lolote, maana nishapenda tena, namuamini sana muda huo, haniambi mtu kuhusu yeye,  kuna mambo alinifanyia mengi mabaya lakini kwa muda huo nilikuwa siyaoni, akawa ananitumia kinamna nisiyojua kuiumiza familia yangu…’akatikisa kichwa kwa kusikitika.

Ni mambo mengi mabaya ,na sikupenda kuyaongelea,…na mengi aliyanifanyia aliyafanya nikiwa usingizini, kama alivyoelekezwa, na huyo mtaalamu wao …mimi nikawa napata shida sana, nikawa naumwa, nasumbuliwa na mambo ya ajabu ajabu, nikaenda hospitalini, nikapimwa,…nikawa na magonjwa ambayo sikuyaratajia,…nikatibiwa lakini yakawa yanajirudia rudia….mpaka madocta wakanitilia mashaka…ikafika sehemu mimi mwenyewe nikawa sipendi kabisa wajibu wangu wa ndoa…’akatikisa kichwa.

‘Yote hayo nilifanyiwa ili nyota ya mali ya wazazi wangu ije ihamie kutoka kwenye familia ya wazazi wangu iende kwa huyu mtu…mimi natumiwa kama chambo…huyu ni mtu kweli au ni shetani…hivi angelifanyiwa kwa wazazi wake hivyo angelifurahi, na kwanini ufanye hivyo..ina maana gani ya kwenda shule…’akasema
Jamaa akatikisa kichwa kusikitika…

Kwa kipindi hicho nisingeliweza kuyafahamu hayo,..maana huwezi kuamini kuwa mume wako anaweza kukufanyia mambo kama hayo, baadae akasafiri tena aliporudi, sasa ikawa kazi ya kuchukua wafanyakazi wa ndani,…alikuwepo mfanyakazi wa ndani hapa mama mtu mnzima akamfukuza anasema yeye hafai, haendi na wakati kumbe waligundua kuwa huyo mama akiendelea kuwepo hapo , wao hawataweza kufanya madawa yao ya uzandiki….’akasema akitikisa kichwa.

‘Yeye akaanza kuleta dogo dogo, na basi alete wasichana wakubwa, hapana analeta watoto, vibinti vya watu hata kujielewa bado, …inasikitisha sana nikiwazia hilo, ina maana hata wazazi wa hao mabinti walikuja kugundua hayo na kuiona familia yangu ni kichawi..kuna mama mmoja alikuja kwangu akanisuta kweli, niligombana naye karibu nimfunge jela,..kwa kuniita mimi mchawi, na mume wangu, nilikuwa sijui hayo..kumbe naishi na shetani ndani ya nyumba…’akasema huyo mama.

‘Ndugu zanguni nayasema haya kutoka moyoni mwangu mkitaka kuoa au kuolewa chunguzeni sana, huyo mtu anapotokea… mkiona mtu anamuelekeo wa mambo ya kishirikina familia yao ipo hivyo achana naye, wapo wengi wazuri, ukumbuke familia yako inajengwa kuanzia hapo..kwenye ndoa yako, ukikosea hapo umeharibu kizazi chako, mshirikina sio mtu kabisa…’akasema.

‘Lakini mke wangu mimi sio mshirikina ni ibilisi tu alinipitia, na hata wazazi wangu sikumbuki kama walikuwa na tabia hiyo, hayo mengine walizuliwa tu, sio kweli….’akajitetea.

‘Si umesema nieleze kila kitu, sasa kwanini walalamika, au niache kuelezea….?’ Akaulizwa

‘Hapana endelea tatizo unahitimisha kuwa mimi sifai,..mshirikina na tabia hiyo ipo kwenye damu, hapana hiyo tabia ilikuwa ya kughilibiwa tu, mimi naweza kubadilika na nakuhakikishia nitabadilika hilo nakuahidi na ikitokea tena niua,..tuachane kabisa,…’akasema.

‘Mimi sio muuaji, mimi sina roho mbaya kihivyo, yaliyotokea hadi kuja kuwafukuza hawa mabinti ni kutokana na wewe…mimi sipo hivyo kabisa, nawapenda wote bila kujali huyu ni nani, ila sipatani na matendo mabaya hasa ya kishetani, …’akasema huyo mama.

‘Sawa endelea mpendwa, samahani kwa kukukatili…..’akasema

‘Kumbe kuwaleta hao mabinti wadogo ni moja ya masharti waliyopewa na huyo mganga wa kienyeji, mabinti wadogo ambao hawajaguswa na mwanaume, eti ndio wanaofaa kwenye hizo dawa zao za kishirikina ambazo eti  ndio hizo zitakazowaletea utajiri, ni ujinga, elimu ndogo ya kufikiri,, na nashukuru sikuwahi kuzaa mabinti maana wangelikuwepo kwa jinsi nilivyosikia,ungewatumia hao hao…’akamuangalia mume wake kwa hasira..
‘Kwani walikuwa wakifanyiwa nini …?’ akaulizwa na huyo mama Ntilia.

‘Mambo mabaya, wanazalilishwa, eti ile damu yao ichukuliwe na hao wachawi, wakachanganye na makafara yao, ni watu wa ajabu kabisa, ….sasa hebu niambie huyu sio mwanga mchawi, mimi niishi na mwanaume mchawi, jamani hamnitakii mema nyie, leo kanifanyia hivyo kesho itakuwaje,….’akatikisa kichwa kukataa.

‘Mke wangu usiseme hivyo…’akasema mume wake.

‘Wanadai dawa hizo zilikua zikifanyika kwa awamu ,eti awamu ya kwanza ni kuhamisha nyota ya wazazi wangu ije kwenye familia yetu, lakini kwanza ipitie kwangu, kama mrithi,…halafu sasa itoke kwangu iingie kwa huyu mwanaume..mimi hapo ndio natumika, usiku nafanyiwa mambo mabaya..ni mabaya kweli..sitaki hata kuyasemna.

Sasa baya zaidi, kwa laana , mwenyezimungu ni mwingi wa rehama akampiga kiboko huyu mume akashikwa na ugonjwa wa kisukari, si unajua tena kisukari, alikuwa hana tatizo hilo ghafala akaanza kuhisi hali fulani mwilini, jogoo hawiki, na kazi anayotakiwa inatakiwa jogoo awike, …kuona hivyo akaingiwa na mashaka, hapo akaniambia
‘Mkee wangu, nahisi nina tatizo…’akaniambia

‘Tatizo gani…?’ nikamuuliza hapo na mimi nilishahangaika na hali yangu mengine nilikuwa hata simuambii, sikutaka kuyaongea, nimeyaongea baada ya kupata uhakika huo, na alipotka hapo nje na kumuuliza baadhi ya maswali ambayo bado nilikuwa sia uhakika nayo, akakiri kuwa ni kweli, basi…nikajua huyu mtuu sio mtu…’akasema.

‘Watu hawa walifikia kula nyama za wafu..hawa si wanga hawa…, wachawi wakubwa…, mnakula nyama za watu waliokufa..hahaha, hapana sio mimi, nasema sio mimi..siwezi kuishi na mchawi ndani ya nyumba yangu…’akasema.

‘Lakini mke wangu nilidanganywa tu, ndio maana nilikuambia yote hayo,…kama ningelikuwa mchawi eeh, ningewezaje kukubali hayo, nilidanganywa tu,…ni shetani alinipitia, nikijua nitakuwa tajiri kama wazazi wako….’akasema .

‘Sasa tatizo likaanza mwilini mwake, alipoenda kupimwa akaonekana ana kisukari ndio sababu, jogoo hawezi kuwika hapo jasho likaanza kumtoka maana ili dawa hizo zifanye kazi anahitajika kuwazalilisha mabinti wa watu wadogo,..na alipewa muda fulani , baada ya hapo ataanza kuupata utajiri,…sasa tatizo limetokea kabla hajamaliza hiyo kazi, masharti yakaanza kumshinda…, shetani ana mbinu, lakini hawajui kuwa mungu yupo, mungu humlinda mja wake, kwa namna ambayo huwezi kutegemea.
.
‘Kuna kipindi mama aliniita, akaniambia je kweli nyumbani kwangu kuna usalama,…nilishangaa mama alijuaje kuwa nipo kwenye matatizo,…mimi kwa kujivunga nikasema, hakuna kitu kinanisumbua, sikumuelewa kipindi hicho, nikajua ni zile chuki zao, kumbe wao walishaona,..unajua tena wazee wana njozi zao, mama akaniambia, huyo mume wako hakufai, uwe makini,..mimi sitaki muachane naye, ila bidisha ibada na umuombe sana mungu wako akulinde..bila hivyo mtaangamia, …

‘Kwangu mimi  nikafuata kama alivyoniagiza mama, na mambo yangu yakaisha na ndio mume akaanza kulalamika kuwa ana matatizo, ..yeye aliporudi kwa huyo mtaalamu wao, akaambiwa kwa hivi sasa hawezi kumsaidia, ila itakuja kuisha hiyo hali akapewa, dawa, lakini akaambiwa dozi haitakiwi kukatizwa, kwahiyo inatakiwa kutafutwa njia nyingine mbadala ya haraka,…’akasema.

‘Njia gani maana hali yangu ndio hivyo, yaani sina raha…’akasema mume wangu.

 ‘Kuna njia mbili ya kwanza, ambayo ndio naiona ni nzuri kwako maana hatutawaruhudu mashetani watusaidie..ni wewe kumtumia  mtoto wako badala yako..’akaambiwa

‘Mtoto wangu, hapana mtaalamu usiingize mtoto wangu kwenye mambo haya…’akalalamika.

‘Ndio nja rahisi nyingine itakuwa ngumu sana kwako, makafara yake ni mabaya zaidi, na ukumbuke umeshaanza huwei kuacha, huoni umeshaanza kuneemeka, hali imebadilika au nadanganya…’akaambiwa

‘Ni kweli mtaalamu…’akasema

‘Na kwa mtoto wako ndio itauwa bora zaidi, ..kwasababu ni mtoto wako na mambo kama tunavyoyafanya kwako, kwani tukifika kwako unatuona, hutuoni, ila tunakuchukua wewe tunafanya yetu tunaondoka, au sio,…na tutafanya hivyo hivyo kwa mtoto wako, lakini ni lazima muwe naye sambamba, na ukubali kwa utashi wako,…wewe au yeye hamuwezi kuona, wakati hayo yanafanyika… inafanyika usiku watu wamelala,…hata nyie mnakuwa kama magoigoi tu, mnafanyizwa bila kujijua, asubuhi utaona dalili tu…’akasema.

‘Kwa vipi sasa…?’ akauliza maana ni kweli hali ya kimaisha ilishaanza kushamiri, uone mungu anavyo mpima mwanadamu unataka utajiri kwa njia hiyo anakujaribu kwa kukupa kidogo tu, kupima imani yako…wewe unazidi kusahau, …shetani anashangilia,…’akatulia.

‘Kama ilivyokuwa awali,…ina maana sasa mtoto wako ndiye atashika usukani wako, …ila wewe na yeye mtakuwa pamoja, yeye anatekeleza majukumu wewe unamshikilia mkono ili iwe kitu kimoja, iwe ni kama wewe unafanya ili kafara likamilike …’akaambiwa

‘Sawa kama ni hivyo hakuna shida…’akasema

‘Lakini ili huo usukani yeye , mtoto wako aweze kuushika ni lazima awe kama wewe, ina maana ile hali yako inahamia kwa mtoto wako, unanielewa hapo…’akaambiwa

‘Kwa vipi…sasa hapo…?’ akauliza

‘Ina mtoto anakuiwa ni wewe, si ndio hivyo..sasa takuwaje ni wewe, ina maana kuna mambo anatakiwa kuyafanya ili awe ni wewe,…’akaambiwa ..hapa nilichoka, siku nilipoambiwa hivyo, nilidondoka nikazimia, kwa hilo achilia mbali hayo yaliyopita, kunizalilisha nikiwa nimelala, kula nyama za wafu, lakini hili, haniambii mtu hapa, sitaki sitaki, ni bora niishe bila ndoa, sitaki….’akasema na akawa kama anajisikia vibaya.

‘Vipi …huwezi kuendelea?’ akaulizwa na mama Ntilie.

Huyo mama alibakia vile vile ..huku anatikisika kwa hasira…, kumbe alikuwa analia, alipoinua kichwa, usoni kulijaa machozi.

‘Niacheni jamani, siwezi,…nimesema siwezi, kama ndoa ndio hivi sitaweza, wazee wamenishi sana, lakini hapana,.. sitamki huyu mtu tena nyumbani kwangu….’akasimama akitaka kuondoka

‘Lakini ulishanisamehe….’akalalamika

‘Kukusamehe sawa nimekusamehe, hilo halina shaka, lakini sio  kwa wewe kuwa mume wangu tena, tutafanya taratibu za kuachana, na nitakupa kila ukitakacho, ukitaka nyumba, nitakupa, lakini wewe ….hapana….’akasema

‘Mama mbona unaniacha njia panda, nimesikia yote hayo, najua ni makosa makubwa sana, lakini yanaweza kusameheka,..’nikasema

‘Hujasikia hilo kubwa lao,hujasikia walivyokuwa wakija kwako usiku, walivyokuwa wakikufanyia…..hapana…ndio utaona kuwa huyu sio mtu wa kuishi naye…’akasema

‘Lakini nakumbuka yule marehemu alisema…hawa walikuwa wanafanyiwa na wachawi, na sio kwa dhamira yao…’nikasema.

‘Hivyo ndivyo walipanga , huyo mtaalamu aliwaambia najua jinsi gani y akutuweka sawa, ukumbuke zile nyumba tatu, yaani ya kwangu na marafiki zangu wawli zilifanywa ndio makao ya watu hao kukutana, na walishahisi kuwa wamegundulikana, kwahiyo ili wajilinde wakabuni uwongo huo, ….’akasema.

‘Mungu wangu ni kweli baba…?’ nikamuuliza.

‘ Ni kweli ndio maana nilitaka yeye aongee ili ….muone kuwa nimekosa na nimetubu madhambi hayo yote , sitarudia tena…’akasema.

‘Sasa wakati tunahangaika kumbe ulikuwa ukitusanifu baba, kwanini ulifanya hivyo….’nikasema.

‘Ni shetani tu,..nilitaka niwe tajiri kama wazazi wake mke wangu ili nisisanifike…na sijui kwanini akili yangu ilikuwa haiwezi kutafakari, kumbe yote yalikuwa ni viini macho huyo mjaa alikuwa akitutumia kwa masilahi yake…’akasema .

‘ Ni nani huyo…?’ nikauliza

‘Ni marehemu…’akasema

‘Ina maana kumbe ni yule yule aliyekuja kutuambia kuwa yeye atatusaidia, ….oh, sasa yule rafiki yangu alihusikinaje , mbona alimtumia yeye…?’ nikauliza

‘Yule ni binti wa adui yake mkubwa,…na binti huyo aliamua kutoroka kwao baada ya kugundua kuwa baba yake huyo ana tabia hizo chafu, na hapo hapo, alitakiwa kuolewa na huyu marehemu ambaye ndiye alikuwa mganga wa huyu mwanaume hapa, umenielewa hapo,..…lakini hakutakiwa kumuambia mtu yoyote yule…, akisema tu, atadhurika, kwa imani zao, ndio maana hata siku moja hataweza kukubali hilo…’akaambiwa

‘Ina maana anayajua yote hayo, kuwa…..’nikauliza

‘Hajui..haya ya kuwa mume wangu anahusika, hajui kabisa, haya tumekuja kuyafahamu kipindi hiki mume wangu alivyoanza kuchanganyikiwa, mume wangu alianza kutuelezea yote huku akiomba msamaha akijua sasa anakufa, kwa jinsi alivyokuwa akiteseka…, na tulijua anatania, labda ni kwa vile kachanganyikiwa, lakini nilipofika hapa leo , akiwa na akili yake vyema,  kumuuliza akasema yote aliyotuambia na kuniambia mimi mwenyewe yalikuwa ni yya kweli…kwakweli nilichoka, ndio maana nilibakia nje nikilia, …’akasema.

‘Sasa mama ina maana huwezi kumsamehe kwa hayo,..je ukifanya hivyo mimi nifanyeje…najua kakosea hata hivyo ili ajirudi na kujisikia kasamehewa, kiukweli, ni wewe kumkubali na mrejeee kwenye maisha yenu ya kawaida, na najua hatarudia tena, mimi nipo tayari kumsamehe, na nimeshamsamehe , na sina kinyongo naye japokuwa inauma sana na sasa kuna uhakika labda hii mimba haina uhusiani na yeye au shetani….’nikasema.

‘Hapana, kumsamehe sawa,… sio shida, maana yaliyofanyika yamefanyika, mimi nimeshamsamehe, lakini kutokana na hayo aliyokuja kumfanyia mtoto wangu, ..siwezi kumrejea, nitasemaje kwa mtoto wangu, nitamuangaliaje mtoto wangu…mtoto wangu sasa hivi anaozea jela, mimi nikae na mtoto niamuambie nilimsamehe baba yako kwa hayo aliyosababisha hadi upo hivyo….nitakuwa na akili kweli…’akasema.

‘Lakini mtoto si hajui hayo..?’ nikamuuliza.

‘Nitakuelezea sehemu nyingine ndio utagundua ukweli wa chuki yangu, na nikimaliza tutaagana,..maana inaumiza sana…’akasema.

‘Tumalizie basi mama….lakini umsamehe tu …au sio mama.’nikasema nikiwa na hamasa ya kusikia zaidi, lakini pale nilipo moyo wangu ulishaanza kudunda, sikuamini hayo, ina maana basi huyu mtoto anaweza kuwa ni mtoto wa huyo mtoto wake,…niligeuka na kumuangalia yule mbaba, alikuwa kainama, kama analia,..lakini kuna kitu kilianza kunijaa, kama hasira, kwanini huyu mtu akafanya hivyo, kwanini…nilijaribu kujizuia, lakini ...

‘Mke wangu kama hutanisamehe, …kama ulikuwa unanidanganya, kama..basi mimi sina maana ni bora nirejee kwenye huo ukichaa, au nikajinyonge tu…wewe unajua sikufanya makusudi , wewe unajua yote nilikuwa nataka niwe kama wazazi wako ili wasitunyanyase, niliyafanya kwa ajili yetu,…ndio nilikosea, na…yule marehemu alinitega mpaka nikaweza kumweka mtoto wetu, iliniuma hata mimi….nakuomba nipo chini ya miguu yako…’akasma sasa akimuendea mkewe,

Mkewe akamkwepa na akawa kama anamsukuma ili asimsogelee..jamaa akazidi kumuendea..niliona huyu mama akishika kichwa nahis alikuwa ana maumivu ya kichwa, au…

Mara yule mama akawa anayumba …mimi nilikuwa karibu yake nikamdaka, kabla hajadondoka chini,  na wakati huo mimi nikawa sijihisi vizuri, sijui ni kwanini, nikahisi ghafla giza likitanda usoni, mimi na huyo mama sote tukaserereka na kudondoka sakafuni…na jamaa alipoona hivyo haraka akasimama na kumsogelea mke wake.

Na muda huo huo simu ya huyo mama ikawa inaita, nani ataipokea wakati mama hajiwezi, na mama Ntilia akaichukua na kusikiliza
‘Halloh nani mwenzangu, eeh,…. polisi… ……mimi sio mwenye simu…..’

NB: Ngoja niishie hapa kwa muda, tutaendelea baadae, maana inauma,..binadamu sio wazuri, kwanini..

WAZO  LA LEO: Jinsi utandawazi unavyozidi na kuwa huru zaidi, ndivyo mwanadamu anavyozidi kutakabari, sasa ivi Mwanadamu kafikia hatua mbaya sana, anafanya mambo ambayo hata shetani atakuja kutushangaa, yanayotendeka kwa hivi sasa ni ya aibu na yamezidi hata hayo tuliyowahi kusimuliwa kwenye vitabu vitakatifu, watu wanafanya mambo zaidi ya mnyama, jamani, jamani tunatafuta nini, wakati dunia hii ni ya kupita tu, wangapi wangapi walikuwepo sasa hawapo, ina maana wao hawakutaj kuishi…tujirudi jamani, tuache, tutubu, turejee kwenye njia sahihi.


 Tumuombe mola wetu atulindie vizazi vyetu na atuwezeshe kuyashinda majaribu haya yanayotuzunguka kwa sasa, vijana wetu wanakulia kwenye mitihani mikubwa bila ya msaada wa mola wetu hawataweza. Ewe mola wetu tusaidie na utuongoze kwenye njia sahihi…..

Ni mimi: emu-three

No comments :