Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 14, 2017

DUWA LA KUKU...12


Yule mdada alipoondoka, kwanza kulipita ukimia fulani, kama vile watu wameambiwa watulie, na baadae kiongozi wa dini akasema;

‘Kuna mambo mengine yakitokea unajiuliza ni kweli au sio kweli, ..lakini kwenye hii dunia lisemwalo lipo, na uchawi upo, hata kwenye vitabu vya dini vimesema hivyo, na tatizo ni jinsi gani ya kupambana nao, au kujikinga nao, wengi hukimbilia kwenye shirki, badala ya kumuendea yule aliyewaumba. Ndugu zanguni, niliwaambia awali nimehisi hapa kuna tatizo, na hata kabla ya kuja huyo mdada, nikahisi kuna kitu zaidi ya maelezo…’akatulia

‘Unataka kusema umeamini hicho alichoongea huyo mdada..?’ akauliza mama mwenye nyumba.

‘Kuamini au kutokuamini, ni nyie wawili, ambao mumeyashuhudia hayo, na mnapata mitihani hiyo, ukijua kuwa yote hayo ni mitihani, lakini vyovyote iwavyo nimewashauri jambo moja kubwa ni kujirudi, na kuwa kitu kimoja, ili muweze kupambana na hilo tatizo mkiwa na nguvu moja, maana nyie ni kitu kimoja mke na mume na familia kwa ujumla,…’akatulia.

‘Mara nyingi adui ili ashinde hupenda kuwagawa, kutenganisha, kuwagombanisha…na hiyo ndio kazi ya shetani…kujenga fitina,..ili wanandoa wakosane, wanandugu wafarakane, majirani wasielewane…huyo ni adui yetu tupambane naye, lakini kwa njia sahihi….’akatulia, na mama mwenye nyumba akachukua nafasi hiyo na kuanza kuongea;

‘Mimi nilisema kuwa mume wangu anakwenda kwa huyo binti na nilisema nina video yenye ushahidi huo…lakini mume wangu akanikatalia,..sasa tumuulize yeye anasemaje ..?’ akasema mama mwenye nyumba na mume akabakia kimia, alikuwa kama kamwagiwa maji, hakusema kitu…hakumuangalia mke wake alionekana kuwa mbali kimawazo.

‘Huna cha kuongea…’akasema baba yake.

‘Nitaongea nini tena baba hapo…, haya yamenikuta, na kiukweli bila ya huyo mdada kuyasema hayo, nilikuwa siamini, …hata mpaka sasa bado sijaamini, lakini nifanyeje, nitajitetea vipi,..kama ni kweli, basi ni kweli…’akasema.

‘Kwahiyo unasemaje?’ akaulizwa.

‘Niseme nini hapo…kwasasa mimi namsikiliza mke wangu ..maana kiukweli itakuwa imemuumiza sana, najaribu kufikiria kama mimi ndio yeye,…lakini kiukweli mimi sijui hayo mambo, na kama kweli nilikuwa nafanya hivyo, ooh, mbona ni mtihani huu, yaani mimi kiukweli sijaamini bado…’akasema.

‘Nikuulize kitu, hali kama hiyo ilishawahi kukutokea kabla?’ akauliza kiongozi wa dini na kuwafanya watu sasa wamuangalia kiongozi huyo wakijiuliza ana maana gani.

‘Hali hiyo ya …..hapana, au una maana gani kiongozi, umesikia alivyosema, na hili kwangu ni jipya, yaani ningebisha mpaka kesho…hata hivyo, bado, jamani, yaani nitoke hivi hivi, mguu kwa mguu nisijitambue, hivi kweli nyie mnaamini hayo…!’akasema kama anauliza lakini akionyesha uso wa kutahayari.

‘Kwanini unauliza hivyo mkuu..?’ sasa akauliza mzee mmojawapo.

‘Mimi mawazo yangu, hayakuwa mbali na hilo aliloliongea huyo bint, ni kweli yanaweza kuwa ni ya ukweli kwa mtizamo wa huyo binti, kama nilivyosema awali , uchawi upo…, lakini pia, tusikimbilie huko moja kwa moja , kwa vile bado kuna utaalamu wa kihospitalini….’akasema

‘Hayo mambo yana matibabu hospitalini…?’ akauliza mzee.

‘Kuna jambo jingine nilitaka kuliongea kabla, na japokuwa nilikuwa na walakini mbili, sasa…hili limetokea likanifanya nijiuliza mara mbili, je ni mambo ya shirki, au ni tatizo la ugonjwa..’akasema kiongozi.

‘Kwani kuna ugonjwa kama huo, mimi naona ni mambo ya nguvu za giza, na hospitalini kamwe hawawezi kuyaamini hayo au una taka kusema nini kiongozi wa imani…?’ akauliza mzee.


‘Ndio, lakini hao wanatibia, madocta nk, ni wanadamu kama sisi, na hata wao wanakumbana na matatizo kama haya, je hamjawahi kuhangaika na mgonjwa wenu ikafikia sehemu huyo docta anakushauri ujaribu njia mbadala….?’ akauliza.

‘Ipo sana…..’akasema mzee.

‘Unajua mimi ni kiongozi wa dini wa eneo hili, lakini kabla ya hapo nilisomea udakitari, kuna tatizo linaitwa ‘somna-mbulism’ sijui kama nimelitamka sawa…ni neno la kitaalamu, wanajua wenyewe wazungu kwanini wakatumia neno hilo…’akatulia akiwaangalia kila mtu kwa waakti wake.

‘Ni nini hiyo…ni..ok, nimewahi kusikia kitu kama hicho, ….’akasema mzee mwingine.

‘Yaani… mtu anaota na kutenda, huku akiwa usingizi, ….na mara nyingi anachofanya hakikumbuki, anaweza akaota, akaenda kuchota maji, au kufanya kazi, na baadae akarudi akalala..bila kujijua….ndio maana nikamuuliza baba mwenye nyumba hii ni mara yake ya kwanza kumtokea hivyo…?’ akauliza kiongozi huyo wa dini.

‘Mhh…uajua umeonga jambo, ukanikumbusha kitu….’aliyesema hivyo ni mke mtu, akawa kama anawaza jambo, na kiongozi wa imani akamuuliza.

‘Kitu gani, tuambie ndio maana nilitaka mfunguke, muelezee kila kitu, huenda ikajileta yenyewe, ni kitu gani, umekikumbuka…?’ akauliza.

‘Mume wangu unakumbuka,…’ akageuka kumuangalia mume wake, ambaye bado alionekana kuwa mbali kimawazo.

‘Nini….hapana, sikumbuki….’akasema akitikisa kichwa

‘Kuna kipindi fulani humu ndani kulikuwa kunatokea maajabu, ..nilikuwa nikiamuka asubuhi, nakuta vyombo vyote vimeoshwa, kumefagiliwa kumepigwa deki, na kila kitu kimepangwa vyema kabisa, hatukuwa na mtu mwingine humu ndani, nikamuuliza mume wangu, ni nani kafanya hivyo, hata yeye akawa anashnga tu, na ilitokea mara kwa mara kipindi hicho,…’akasema.

‘Unakumbuka kwanini ilitokea hivyo..?’ akaulizwa.

‘Kipindi hicho, nilikuwa nalalamika kazi zimekuwa nyingi, na tukiongea na mume wangu anasema tuwe na subira maana hali sio nzuri kiuchumi, basi, nikawa sina raha, na hayo yakaanza kutokea, unajua, nilijua ni mume wangu anafanya kuni-shtukizia, lakini yeye akawa anashangaa, na kuniuliza, …’akasema mke mtu.

‘Mhh…nakumbuka, lakini …sio mimi, niliyekuwa nafanya hivyo..inawezekana ulikuwa ni wewe…ulipitiwa tu, maana ule usafi na jinsi ya vitu vilivyokuwa vinapangwa ni utaalamu wa aina yake, na anayeweza hivyo ni mwanamke…’akasema.

 ‘Yah, ulikataa hivyo hivyo, kama ulivyokataa hili….na sasa unajiuma uma…inawezekana ni wewe, inabidi kweli tumtafute docta,…ndio sasa naanza kukumbuka, inawezekana, sasa huyo docta tutampataje kiongozi wetu wa imani..?’ akauliza mama mwenye nyumba.

‘Lakini sioni kwamba hilo lina ukweli ndani…na hata kama lipo,  mimi sina  tatizo hilo…’akasema baba mwenye nyumba akizidi kujitetea.

‘Kama huna tatizo hilo, ina maana ulifanya makusudi,…kama ulikusudia tuambie tujua, utubu dhambi zako…’akasema mama mwenye nyumba, na baba mwenyenyumba akabakia kimia.

‘Sasa kabla ya kufikia maamuzi hayo, kuna mambo mawili ya kufanya, kwanza, nyie wawili mshuke chini, muombeane msamaha, maana mola hukubali toba za yule alietubia madhambi yake, akawa hana kinyonga na mtu, akasamehe ili na yeye aweze kusamehewa, na la pili, ndio hapo tutamkabidli yeye muumba, tutaomba kwa pamoja, ili tupate radhi zake, ulizi wake, na kama kuna jambo la shiriki, basi mwenyezi mungu aliondoe, na kuweka ulinzi wake, …sawa..?’akasema kiongozi wa imani akiwaangalia wanandoa hao.

‘Sawa kabisa…’wakasema wazee wale wawili na kijana akawa wa kwanza kusimama akiwasubiria wazazi wake, kwa uso wenye furaha.

‘Unasemaje baba mwenye nyumba, bado una mashaka na hilo..?’ akaulizwa na wazee

‘Mimi nilitaka nione hiyo video kwanza, nihakikishe kwa macho yangu maana mimi sijaamini hilo…’akasema
‘Kama ni kuiona hiyo video, basi mtaiona mkiwa nyie wawili, kama ni muhimu kwenu…, ila mimi ningelishauri muiharibu kabisa hiyo video…, isje kuleta chuki nyingine…’akasema kiongozi wa dini.

‘Ni kweli, hebu ilete hapa tuiharibu…’akasema mzee akimuangalia mama mwenye nyumba.

‘Hapana siwezi kuiharibu kwa sasa… bado nataka kuifanyia kazi…’akasema mama mwenye nyumba.

‘Kazi gani tena..?’ akauliza baba mwenye nyumba akimuangalia mke wake.

‘Nataka kuhakiki kama alichosema huyo mdada ni cha u- kweli,…’akasema

‘Kwa vipi..?’ akauliza mumewe.

‘Kuna mtaalamu mmoja, yeye kasomea, mambo ya mitandao, lakini pia ana utaalamu wa nguvu za giza, anasema yeye anapambana na hayo mambo, yeye, hatai kuitwa mganga wa kienyeji, bali anapendelea akiitwa mtaalamu, maana hapigi ramli, au…sijui tunguli, hapana, yeye anatumia mitandao…alisema yeye anaweza kupiga picha, na kwenye picha kunaweza kukawa na mtu zaidi ya mmoja,..labda, nikamuuliza kwa vipi.

‘Akasema, duniani kuna viumbe vingine havionekani, kama majini mashetani, na usiku kuna wachawi, sasa unaweza ukapiga picha bila kujua kuwa viumbe hao wapo karibu yako,..kwenye picha hawataonekana, lakini yeye akiingalia, akaweka kwenye vipimo vyake anaweza kuona vitu kama hivyo…’akasema

‘Kwanini alikuambia hayo…?’ akauliza mumewe

‘Ilitokea tu, wakati tunaongea, rafiki yangu alinitambulisha kwake, …ni mumewe….’akasema

‘Ok….kama ni hivyo sawa…’akasema baba mwenye nyumba.

‘Lakini huo ndio mwanzo wa kuamini mambo hayo, au unataka uhakikishe kitu gani sasa..?’ akaulizwa
‘Kama alichosema huyo mdada ni kweli, ina maana mume wangu alipokuwa huko chumbani, alikuwa pamoja na huyo mtu mwingine lakini, huyo mtu mwingine alikuwa haonekani, kwa kauli yake au sio…sasa kama haonekani, kwa ujuzi wa huyo mtu atamuona, kwahiyo tutagundua ukweli wa maneno ya huyo mdada, kama kweli hatudanganyi…’akasema mama mwenye nyumba.

‘Unajua ukianza kupekenyua, pekenyua hayo mambo,.. ndio mwanzo wa kujiingiza kwenye shirki, kitu ambacho ndicho tunakikwepa hapa, au sio jamani wazee wangu…’akasema kiongizi wa dini.

‘Mimi siwezi kuingia kwenye shirki hata siku moja… imani yangu ni thabiti, ndio maana hata hao mnaowaita wachawi sijui, hawajaweza kunichezea mimi,…hilo la mume wangu kufanya hayo, akilini mwangu kuwa ni uchawi sijaliafiki,…ila nilishagundua kuwa kuna tatizo kwa mume wangu,sasa sikuwa na uhakika ni tatizo gani,…kama alivyosema kiongozi wa dini, kuwa kuna hali hiyo ya kutembea kwenye ndoto, hapo naweza kuamini kidogo,…sasa mimi nahitajia muda, kuyachunguza haya…’akasema.

‘Kwahiyo bado huniamini mimi…?’ akauliza mume wake.

‘Kukuamini au kutokuamini, kunahitajia mambo mengi, na mojawapo ninalotaka kulifanya ni hilo, la pili…ni hilo la kumtafuta dakitari, na la tatu ni kumuelekea mwenyezimungu, mimi hayo yote nayapitisha, ila hilo la uchawi, bado sijaliamini, labda huyo mtu anionyeshe huyo mchawi kwenye hizo picha, …’akasema.

‘Atakuonyeshaje sasa..?’ akaulizwa.

‘Hilo niachieni mimi..sio kwamba nitaamini, lakini kama kasema anaweza kumgundua mchawi hata kama kajificha ,basi ataligundua na hilo..alisema hata picha kama kuna kitu kisichoonekana lakini kimechukuliwa na picha atakiona, alinionyesha pich alizopiga usiku akiwa piga wachawi, lakini ukiziangalia hivi huoni kitu, yeye anakiona hicho kitu,…na ana namna ya kusafisha hizo picha kwa utaalamu wake, na hizo sura za wachawi zikaonekana kabisa…..’akasema.

‘Oh, unaamini hayo..? akaulizwa na mumewe.

‘Kuamini au kutokuamini kutakuja baada ya ugunduzi huo..mimi tabia yangu ni kufanya utafiti kwanza, ndio maana nilikwenda shule…, na nikigundua basi, nitakuwa nimegundua jambo ambalo nilikuwa silijui, akili yangu itaongeza ujuzi huo, japokuwa kwangu mimi bado nayaona mambo hayo kama nguvu za giza tu, mambo ambayo hayahitajiki kwetu sisi wanadamu…’akasema.

‘Sawa, sasa mnasemaje..mpo tayari kushikana mikono na kuyamaliza haya mambo..?’ akauliza kiongozi wa dini.

‘Samahanini wazee wangu…..nisema ukweli wangu, hata kama nitakubali hapa, kuwa nimesamehe, nimshike mkono, utakuwa ni unafiki tu,  bado mimi sijawa na imani …sijakubaliana na hili jambo kuwa ni kweli, mume wangu alikuwa hajui mambo yote hayo, kuwa hakuna kitu kwenye moyo wa mume wangu, kumtamani huyo binti, …hawa mabinti, maana hata huyu kasema hay ohayo yamekuwa yakimtokea, sijafuatilia hili, ila nilishaanza kufuatilia…’akasema.

‘Sasa unataka kusema nini..?’ akaulizwa.

‘Nasema hivi, nahitajia muda wa kulifanyia kazi hili na..nikijirizisha basi , nitawaambia, lakini sio kwamba,..nimekasirika au nina nia yoyote mbaya,..naomba mnielewe hivyo, kwasababu,..nilipoona hiyo video, moyo wangu ulikufa ganzi, na mimi sio jiwe,  penzi nililokuwa nalo moyoni, silioni tena…aah, nisameheni tu, na mwenyezimungu anisamehe pia…’akasema.

‘Oh…lakini mwenyezimungu katuambia, kamwe tusiweke kinyongo moyoni, au tusiwe na kisasi au chuki moyoni, maana umauti ukikukuta ukiwa bado na kinyongo hicho, au chuki hizo,..kuuona ufalme wa mbingu, kuingia peponi kwako itakuwa ni mtihani, na mwenyezimungu anajua zaidi..ni bora msameheane,..hata kama moyoni bado una hasira, ile kusamehe,..huku unamuomba mungu, mungu mwenye atailanisha nafsi yako, nahasira na chuki hizo, zitayeyuka kidogo kidogo,…muhimu ni kumuomba mwenyezi mungu awasaidie, maana haya mambo bila muongozo wa mola wetu bado yatakuwa ni mazito kwetu,…’akasema.

‘Kiongozi,..hata kama moyoni, au kwenye nafsi yangu bado sijarizika, nikubali tu…hapana mimi bado  nina ..duku duku,…kwani jamani, siruhusiwi kujirizisha kwanza.niongoze kiongozi wangu, mimi ninachotaka ni kufany autafiti, nijirizishe, maana mume niliyemjua sio huyu tena….’akasema.

‘Hata hivyo,…mimi niliona ni vyema mkasameheana kwa leo, huku mkiendelea na michakato mingine kama nilivyosema, huku mnamuomba mungu awasaidie, maana haya yote sio kwa ujanja wetu, na hatjui ya kesho, hatujui uhai wetu upo kiasi gani….ni muhimu tukalitambua hilo…’akasema kiongozi wa imani.

Basi wote wakakubaliana tukaanza ibada ya kumuomba mwenyezimungu na kuomba hayo yote yaliyopo humo kwenye nyumba kama ni ya kibinadamu au kama ni ya kishetani..yaondoke na nyumba ibakie kwenye amani…na tuliomba mwenyezimungu atupe kinga yake, na kutuongoza kwenye njia sahihi, baada ya hapo wanandoa hao wakashikana mikono, na kijana alionekana kufurahi sana.

‘Kabla hatujaondoka nina ombi jingine na hili sitaki likataliwe, na sitarudi nyuma tena,  kwa uamuzi huo…’akasema mama mwenye nyumba.


‘Ombi gani tena..?’ akauliza mume mtu akionekana kuwa na mashaka zaidi.

‘Ni kuhusu huyu mfanyakazi wa ndani tuliye naye sasa…’akasema.

‘Ehe, unatakaje au naye ana nini..?’ akaulizwa.

 Huyo mama hakutaka hata kuniangalia machoni, akasema…

‘Mume wangu, ..hili ninataka wewe ulifanyie kazi, ..utajua wewe mwenyewe kwa jinsi gani, …’akatulia.

‘Niambie mke wangu nipo tayari, kukubalia lolote lile, najua nimekukosea sana, na sitaki niendelee kukukosea, nataka nikuonyesha kuwa mimi ninakupenda sana mke wangu...’akasema baba mwenye nyumba akitamani hata kupiga magoti.

‘Najua kwasasa utasema hivyo, siwezi kukulaumu..nimekuzoea…, ila hili, nimeliwazia sana nikaona ni bora iwe hivyo, hata kama watu wataniona mimi ni mtu wa ajabu sana…’akasema mama mwenye nyumba.

‘Sawa uamuzi ni wako, kama mnataka muongee wawili basi mturuhusu sisi tuondoke…’akasema kiongozi wao wa imani.

‘Hapana hili nitaka niliongee hapa hapa ili kila mtu alisikie na lifanyiwe kazi , ….’akasema sasa akimuangalia mume wake machoni, halafu akageuka kuniangalia mimi, na hapo moyo wangu ukaanza kudunda, nikahisi kuna jambo kubwa linakuja,..lakini siweza kubahatisha ni jambo gani!

NB: Hatimaye nimefanikiwa kuandika sehemu hiyo hivyo….kama nilivyosimuliwa na mwenyewe, tusihie hapa kwa leo.

WAZO LA LEO: Riziki haigombewi, kwani kila mja ana fungu lake.
                           Lakini pia riziki haupewi, ukilala na kusubiri fanI zake.
Jibidishe kwa amali hata kupiga kiwi, ufanye ibada na kila kitu kwa mahala pake.

 Mola ni mwingi wa rehema, atampa kila mja fungu lililo lake.
Ni mimi: emu-three

No comments :