Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, July 3, 2017

DUWA LA KUKU...-5


Ile sura niliyoiona kwa huyo mama, ilinitosha kuwa ni ujumbe kwangu, mimi nikanywea, nikasubiria kauli itakayotoka, kiukweli nilishajiandaa kuondoka, lakini sikujua wapi pa kwenda, ila nilitamani tu kuondoka hapo,…na huko ninapokwenda nitaishije, hayo kwangu akilini yalikuwa hayapo, lakini kama tuliishi mimi na mama yangu kwa kuomba, kwanini nije kushindwa kuishi. Mungu mwenyewe anajua!


‘Hii ni zawadi yako, au sio…?’ huyo mama alianza kuniuliza hivyo, huku akiwa kainua mfuko wenye kitu ndani, ni mifuko unayowekewa kitu ulichonunua madukani hasa supermarket,…hata sikujua ni kitu gani, au kimetoka wapi.

Nikajua labda ni zawadi ya kuondoka nayo, sikusema kitu wala kusimama kuipokea, nikawa nimetulia tu kimia, akilini nikiwa nashindwa hata kuwaza, mambo mengi yamepita akilini , na kichwa hapo kinaanza kuuma, lakini nikajitahidi kujituliza.

‘Nakuuliza hii zawadi ni yako, au unaogopa kusema sasa, hii zawadi amekuletea mume wetu, kakuletea wewe bi mdogo wake, ichukue, …’akasema akinirushia na mimi sikusogea kuichukua, nikawa nimetulia tu. Nilikumbuka maneno ya mama, akinikanya nisigombane na watu, aliwahi kuniambia;

Binti yangu, ukiona mwenzako kakasirika anaongea kwa jaziba wewe tulia mpe muda amalize jaziba yake, halafu akitulia ndio unaweza kufikiria jambo la kumjibu. Mara nyingi mtu kama huyo ukimjibu ghadhabu zake huongezeka, na inaweza kutokea madhara makubwa!

‘Utashangaa nimeipata wapi hii zawadi yako, na mletaji kashangaa nimeipataje,…mimi nilikuja mapema tu, nikijaribu kuchunguza kinachoendelea, …’akasogea ndani na kusimama, akageuka kuangalia mlangoni, huku anaongea.

‘Nimesikia mengi kutoka kwa majirani, ..sikutaka kuchukulia haraka, …nilijua ipo siku tu , nitawanasa,…sasa leo nimewanasa, na nimegundua kuwa ni kweli, wewe ni nyumba ndogo ya mume wangu,…unajua mimi ni mvumilivu sana, lakini uvumilivu una mwisho wake,  siwezi kuvumilia tena, maana haya yametokea mara nyingi,…sasa nasem basi, umesikia nitakuachia huyo mume, lakini sio kuwa nitawaachia, make humu, hapana wewe na yeye mkatafute wapi pa kuishi..huo ndio uamuzi wangu….’akasema na aliponiona nipo kimia, akanigeukia.

‘Unajua,…mama yako, alinikabidhi wewe, akasema nikulee kama mwanangu, nikulee kama binti yangu, kumbe nimechukua nyoka ndani ya nyumba yangu, siwezi hata kuamini,..unajifanya mpole, unajifanya hujui kitu, kumbe, umekubuhu….huwezi kusema kitu maana mimi mwenyewe, nimejionea kwa macho yangu..halafu ulipogundua kuwa nimewafuma, ukajifanya kukurupuka na kukimbia, ujanja w kitoto…’akasema.

‘Sasa nimekuambia mwenzako, afungashe, na wewe nimekuja kukuambia ufungashe…mkatafute pa kuishi, hii nyumba ni yangu ni mali ya wazazi wangu, …nina mamlaka nayo,…kama ulifikiri kuwa ni mali ya mume ..umenoa, huyo mume hana kitu hapa…unisikie vyema, mtaenda kutafuta sehemu ya kupanga, muanze maisha yenu, mjifunze maisha,….unanielewa…’akasema akiniangalia na mimi nikawa kimia, ni kama sikuyasikia hayo maneno.

Machozi yalikuwa yakinitoka,..yanatiririka kama maji, lakini sikuweza kutoa sauti ya kulia, kilio kilikuwa ndani ya moyo, nasononeka, ..naomboleza, ..lakini ni nani atalijua hilo, ni nani atamuonea huruma binti masikini…

Mara akatokea kijana wake,..akaja na kusimama mlangoni, akasema

‘Mama mbona unachukulia haya mambo kwa jaziba, ….’akasema na mama yake akamuangalia kwa macho yaliyojaa hasira,

‘Hayakuhusu haya,…’mama akasema.

‘Mama,…., kwanza naomba samahani, kuwaingilia …ila mama una uhakika na unachokisema, ….?’ Akauliza, sasa akiingia ndani kabisa.

‘Uhakika gani ninao-uhitajia mimi…., hebu niambie mwanangu, nimemfuma huyu Malaya akiwa chumbani kwetu na mume wangu, akiwa kavalia khanga moja, wapo wana, hapo unahitajia ushahdi gani mwingine, niambie wewe unayejifanya mkubwa sasa, …..yaani nasikia hata kutapika…’akasema.

‘Mama umuogope mungu, hivi kweli mama, huyu anaweza kufanya kitu kama hicho kweli mama, nakuomba mama urejeshe moyo wako nyuma, wewe ndiye uliyesema huyu ni binti wa kijijini hajui lolote, tumuongoze, leo hii unasema kayafanya hayo, mama mimi siamini hayo, hajafanya hayo unayoyasema….’akasema huyo kijana na mama yake akamuangalia huyo kijana usoni akiwa katahayari, akasema;

‘Ina maana mimi naongopa, ina maana mimi macho yangu hayaoni siku hizi, nimekulea nikakuonyesha njia, sasa umeota mapembe,…sikiliza wewe mtoto, wewe bado mdogo, haya hayakuhusu kabisa…, na hujui uchungu nilio nao mimi….subiria muda wako utafika, utaoa, na utafanyiwa hivyo ndio na wewe utajua ni kwanini ninasema haya…’akasema.

‘Mama nayasame haya kwa vile mimi namfahamu sana huyu mdada, hawezi kuyafanya hayo, na unakumbuka siku moja nilikuambia kuwa huyu mdada alishikwa na baba…alishikwa na  baba akitaka kukimbia….’akatulia akimuangalia mama yake.

‘Mama, huyu mdada ana matatizo makubwa, anapata shida, anaweweseka usiku, na wakti mwingine anadondoka na kupoteza fahamu….je ulimpa nafasi baba akuelezee kama huyo mdada hakudondoka akapoteza fahamu na baba alikuwa akijaribu kumrejesha katika hali yake, ..je mama angelikuwa ni binti yako, ungelifanyaje,…mama wewe ulitufundisha tumuogope mungu, kwa kusingiziana uwongo, je kama unachomsingizia mwenzako sio kweli, utasemaje mbele ya mungu...’kijana akasema.

‘Wewe mtoto, wewe unataka kusema nini kuwa mimi namsingizia uwongo huyu mwanamke…, kama namsingizia uwongo kwanini hajitetei…aseme yeye mwenyewe kama sio kweli…kama sio kweli sikumkuta akiwa kalala chini akiwa uchi, na mume wangu yupo juu yake, …asema yeye mwenyewe kama sio kweli….’akasema na mimi nikaendelea kukaa kimia.

‘Eti ni kweli hayo dada…?’ akaniuliza huyo kijana akiniangalia moja kwa moja, na mimi nikawa nimeinama chini, nikuendelea kukaa kimia, na mama akaonyesha ishara kama kusema

‘Unaona…’ lakini hakutamka neno….na kijana akaniangalia kwa mshangao, na kusema;

‘Sema ukweli wewe mdada, jitetee,  shauri lako…, ukikaa kimia ni nani atakusaidia….’akasema, na mama akasemaa;

‘Usimlazimishe kukana maovu yake, kukaa kwake kimia, inaashiria nini, kuwa ni kweli, na moyoni anaona haya….kwa uchafu walioufanya na ….huyo baba yako….’akasema mama.

‘Mama…usiseme hivyo, una uhakika….’akasema kijana

‘Si huyo hapo,….umemuuliza kakujibu nini, kakaa kimia, maana ukweli unauma…ni ..hata sijui niseme nini, ashukuru mungu siku hizi hasira zangu zimeenda likizo…’akasema mama.

Na mimi kwanza nilikaa kimia, nikiwazia haya mambo kwa undani zaidi, sikuwa na la kujibu, nilishindwa nijubu nini maana hayo anayoyasema huyo mama, siyaelewi, na sijui yametoka wapi, baadae sijui ilikuwaje nikajikuta nasema haya maneno;

‘Mungu pekee ndiye anayejua ukweli wa hayo yote, kama umeamua kuamini hivyo, hata nifanyeje siwezi kubadilisha imani yako, ila mwenyezimungu peke yake ndiye anayeweza kufanya hivyo….’nilipotamka maneno hayo, nilihisi kichwa kikitulia maumivu, na hapo nikaingiwa na nguvu y akuongea zaidi, nikasema;

‘Mimi sina uwezo wa kuwafanya nyie muamini ukweli ulivyo…ila mungu anaweza. Lakini ni bora niseme ukweli,…, mimi sijui hicho ninachosingiziwa nacho,…sijui mama unaongea nini, mpaka sasa naona kama umeamua kunitungia uwongo, labda ili uweze kutimiza unachokitaka….’niliposema hivyo huyo mama akataka kunikatiza, lakini sikumpa nafasi nikaendelea kuongea.

‘Mama…kilichotokea,…. mimi nilidondoka, na kupoteza fahamu…’niliposema hivyo, mama akacheka kwa kebehi, akijua labda nimesema hivyo kwa vile kijana wake alisema hivyo.

‘Mimi nilidondoka, … baada ya kuisoma barua iliyotokea kijijini kuwa mama yangu amefariki….’niliposema hivyo, machozi yakawa yananitoka utafikiri maji yana mwagwa, na mama akabakia mdomo wazi, kanikodolea macho utafikiri kasikia jambo gani, hakutarajia hilo kabisa, huenda hata hiyo barua, labda aliiona mume wake na hakuweza kumuambia mkewe kuwa mimi nimeugundua ukweli.

‘Mama, wewe umesema kuwa umenichukua mimi kama muwe kama wazazi wangu, kwa vile mama alikuomba ufanye hivyo, ..je ungeyafanya haya kwa mtoto wako,…, najiuliza ni kwanini mkanifanyia mimi hivyo, au ni kwa vile, …’nikasema hivyo bila kumalizia.

‘Mama nyie  …mlipata taarifa hiyo mkakaa kimia…’nikasema na huyo mama sasa akabadilika sura. Kutoka kwenye hasira na kurejea kwenye kushangaa…binadamu sura hujieleza ukimuangalia kwa makini.

Mama sasa akawa anatafuta njia ya kujitetea, kwanza akahema kama mtu aliyepo kwenye usingizi akibadili pumzi kwa nguvu. Akamtupia jicho kijana wake , na kijana wake akawa kainama chini, sasa ikawa zamu yao, kuhisi unyonge, maana ukweli huuma!

Lakini kama ujuavyo, mwenye uwezo, tajiri, watawala hata wakikosa hawakosi neno la kujitetea, huyo mama akasema;

‘Ni nani alikuambia upekue pekue huko ndani kwangu..si nilishakuambia kuwa wewe kazi yako ni kufanya usafi tu huko ndani…na nilishakuambia kama baba yako yupo wewe usiingie kabisa huko ndani…kwanini sasa unajiamini mpaka unaanza kupekua pekua huko unatafuta nini, je nikipotolewa na kitu utakataa kuwa wewe hujahusika, na kumbe wewe ndiye unamtia mshawasho mume wangu kwa kuingi ahuko chumbani na khanga moja,…niambie ni kwanini ukafanya hivyo?’

‘Mama, mimi sikupekua pekua vitu vyenu nilikuwa nakung’uta vitabu mavumbi, na kwa bahati mbaya ndio hiyo barua ikadondoka, na kufunguka,…na mama sijawahi kuingia ndani akiwepo baba kwa utashi wangu, kama niliingia, ni kwa muito wa baba….’nikasema na hapo akakunja uso kama anataka kusema neno, na mimi sikumpa nafasi nikaendelea kusema;

‘Wakati nakugung’uta vitabu, ndio hiyo barua ikadondoka,…na ilipodondoka, ikafunguka,…na ndio nikaona maelezo ya kutoka kijijini, na macho hayana pazia,..kuona maneno hayo,…nikavutika kuyasoma yote,…na ndio hapo nikagundua hilo,… kama ni kosa, hapo nimefanya kosa, kwa kusoma barua yako,…naomba mnisamahe, lakini najua ni mungu alitaka kunifunulia ukweli,..mlitaka kunificha mungu akataka kunifunulia ukweli…. sasa nauliza ni kwanini mumenifanyia hivyo…’nikasema

Huyo mama sasa akanywea, akahema, akageuka kumuangalia mwanae, kama vile anataka amsaidie kujitetea, lakini kama nilivyosema watu hawa wenye uwezo, hawakosi neno,…akasema;

‘Sikiliza, wewe binti, hatukuwa na nia mbaya kwako,…nia yetu ilikuwa ni njema kabisa, ya kuwa tukikuambia huo ukweli, kwanza utachanganyikiwa, utashindwa kufanya kazi, na wewe hujadunduliza kiasi cha fedha cha kukuwezesha maisha, na kwanini tulifanya hivyo, tulijua ukiambiwa utataka kwenda nyumbani, na ukienda huko unaweza usirudi kwa hali ilivyo...'akasema

'Kwanini jamani....'nikasema hivyo.

'Sisi tunaona mbali zaidi yako...hebu jiulize ungeenda hivyo kiharaka hivyo, nani angelusaidia, hpo kuna nauli..kuna matumizi, na huko je.... huko ungeenda kuishie, na maisha yalivyo huko sio kama ulivyoondoka, ..huko sasa hivi, huko kijijini eeh, we usikie tu, hali ni mbaya sana hakuna chakula watu wanakufa kwa njaa…, na isitoshe, hali ni hatari, watu wanauwawa ovyo, tuliogopa ukienda huko na wewe utauwawa…sasa nikuulize je hivyo tulifanya vibaya...’akatulia.

'Mimi najiuliza kame ingelikuwa ni wewe umefiwa, na tena mama yako, ungelifanyiwa hivyo ungelifurahi...yaani hata..hapana mimi bado sijaridhika na hilo, lakini nitafanyeje, mimi naweza kusema nini kwenu, mliamua kwa vile....'hapo sikumalizia, na huyo mama akanidakia kwa kusema.

‘Mama yako alinikabidhi wewe akasema nikulinde, na nihakikishe upo mikono salama, na ndicho tulichokifanya,…hata kama hutaelewa,…na hata hivyo, kwa mfano tungekuambia, uende…ungeenda huko ungelifanya nini, maana hata sisi wenyewe taarifa hiyo tuliipata imechelewa walikuwa wameshazika kutokana na hali ilivyokuwa huko…, mama yako aliungua sana….umenielewa, pole sana, na tuliza kichwa chako…’huyo mama akasema alipoona mimi ninalia kwa kwikwi.

 ‘Sasa pamoja na hayo najua sasa hivi upo kwenye majonzi,….wenzako sasa wameshasahau wa kusahau…lakini ni lazima nihakikishe mambo fulani, japokuwa umeweza kujitetea kihivyo,..kwa hayo yaliyotokea, nataka uniambie ukweli, ..ukweli ndio utanifanya na mimi nitulize moyo wangu, nataka unijibu bila kuogopa, …je mume wangu amekuwa akikufanyia hivyo mara ngapi…?’ akauliza na kijana akataka kuingilia lakini mama yake akamuashiria anyamaze.

‘Kunifanyia hivyo kw vipi, sijakuelewa mama..?’ nikauliza nikimuangalia huyo mama naye akawa kanikazia macho, na kwa hali hiyo mimi nikatizama chini.

‘Nilimkuta anakuwekea mdomo wake kwenye mdomo wako….unaelewa ni nini maana yake hiyo, unieleze hayo anakufanyia, hivyo ….je ni mara ya ngapi kakufanyia hivyo…?’akasema na mimi nikashtuka na kusema;

‘Kwanini afanye hivyo,…mama, mimi sijui unachoongea, kwanini afanye hivyo, hata sielewi…mimi nilipozindukana nilimkuta baba kachuchumaa, kaniinamia, kama vile yupo juu yangu, akiwa hivyo, kwa haraka nilipozindukana,,..nilijua anataka kunifanyia kitu kibaya, ndio maana nikaanza kupiga ukelele na kukimbia…’nikasema.

‘Kwahiyo yote aliyokufanyia baba yako hukuyaona, unataka kunidanganya eeh?’ akaniuliza.

‘Kwani alinifanyia nini..mama mimi sijui hayo unayoyaongea, ..sikumuona akinifanyia hivyo, maana wakati nadondoka humo ndani nilikuwa peke yangu, hata sijui huyo baba alikuja saa ngapi…’ nikasema sasa nikiwa na hamu ya kutaka kujua.

‘Wewe…unajifanya hujui, nakuuliza ni mara ngapi kawahi kukufanyia hivyo, au vitendo kama hivyo…wewe sio mtoto mdogo utake nikuffanulie kila kitu, haya labda nisema, kakulazimisha hivyo, mara ngapi, ….?’ Akauliza.

‘Mama kwakweli sijui unachotaka kukisema, kama ni hivyo, kupoteza fahamu, na labda, mimi sijui kama alifanya nini, ..sijawahi kufikia hatua hiyo, …ni huo mshutuko ulionifanya nidondoke na kupoteza fahamu….sijua lolote baadae mpak niliposhituka na kumkuta hivyo…’nikatulia nikisita kuelezea tukio lile lililopita.

‘Nakuuliza tena, maana isije ikatokea tatizo ukajuta, ..mimi ni mtu mnzima, nawafahamu sana wanaume, leo na au kesho kutwa, nije kusikia kuwa una mimba, nakuapia, utatoka humu ndani ukiwa huna sura, nitakurarua, mpaka unijue kuwa mimi ni nani…’akasema kwa hasira.

‘Mimba !!!...mama mimba itoke wapi….mimi siwezi kufanya kitu kama hicho…, kwa vipi mama,..mimi sijui kitu,….mama mimi sijui hayo mambo…sijawhi na sitaki kujihusisha na mambo hayo , mama alinikataza kabisa…’nikasema na akanisogelea kama kuninong’onezea kitu ili kijana wake asisikie…, akaniuliza jambo, sikumsikia vyema, au sikumuelewa alikuwa na maana gani, lakini nikahisi tu, na kusema;

‘Mama mimi hayo siyafahamu kabisa,…mama alinikanya sana kufanya urafiki na wanaume, hayo unayoyaongelea kwangu ni mageni kabisa siyajui mama…’nikasema.

 Mama akaniangalia machoni kwa makini kama ananipa kuwa kweli niliyosema ni sahihi au najaribu kumuhadaa, halafu akasema;

‘Sawa…ila nakuonya tena na tena, huo mwili na kupendeza usije kukudanganya, watakuambia wewe ni mnzuri, unapendeza na mambo kama hayo…..watafikia hata kukupatia zawadi,.. na ujanja wa wanaume, ili kukufanya ujione wana kupenda, wengi wao huanzia kwenye kukupa zawadi,….’akasema

‘Mama mimi sijachukua zawadi ya mtu yoyote, wakinipa huwa nakataa…’nikasema.

‘Na hiyo zawadi aliyokuletea mume wangu ilikuwa ni ya nini, kama sio mlishaanza urafiki…’akasema.

‘Zawadi gani mama, baba hajawahi kunipa zawadi nikiwa peke yangu, mara nyingi akileta zawadi, anakupa wewe ndio unanpa mimi,…kweli si kweli…?’nikasema na kumuuliza.

 Mama akahema kidogo, halafu akageuka kumuangalia kijana wake, kuna kitu alitaka kuniuliza lakini kuwepo kwa kijana wake, akashindwa kuongea, akaniangalia na kusema;

‘Haya mimi nakuambia tu…usije kudanganyika ukaingilia ndoa za watu, usije kudanganyika ukaanza mapenzi na kijana wangu, huyu kijana wangu, sio hadhi yako, usije kukudanganya kuwa anaweza kukuoa, hilo halipo na sitakukubalia hata siku moja, na…. usije kudanganyika ukaanza umalaya huko nje, ukaniletea mimba humu ndani au magonjwa, ukumbuke hayo, usije kunilaumu na kuniona mbaya,..’akasema.

Mimi nikakaa kimia, aliponiona sisemi kitu akasema;

‘Nikuambie ili kama angalizo, kuanzia sasa hivi,  nitakuchunguza hatua kwa hatua, ole wako, unasikia ole-wako, nije kugundua kuwa kuna kitu kinachoendelea kati yako wewe na mume wangu au kijana wangu….’akasema kwa hasira.

‘Mama mimi naomba niondoke humu ndani, haya ya humu ndani siyawezi,…kwani yaonekana wewe huniamini tena…, nilijua nyie ni kama wazazi wangu, sasa nageukwa,…’nikasema.

‘Uondoke , uende wapi… na ni nani anakugeuka, unaona kauli yako, nahisi kuna kitu unanificha, sema ukweli, nikusaidie, je kuna lolote kakufanyia mume wangu..?’ akaniuliza

‘Hapana, mimi naona ni bora nirudi kwetu kijijini…’nikasema

‘Hahaha, eti urudi kwenu kijijini, wenzako huko wanapakimbia, wanakuja huku , wengine wanatafuta sehemu ya kwenda wewe..unataka kwenda huko , sawa kama unataka kurudi kwenu kijijini, mimi nitakupatia nauli yako uende, lakini ukiondoka hapa ndio bye bye…waulize waliokuwepo hapa mimi sina muda wa kubembeleza mtu,…’akasema

‘Kwanza usiku mimi silali…nateseka na …sijui kuna nini humu ndani…’nikasema na hapo akashtuka na kusema

‘Kuna nini kinatokea usiku…haya anza kuongea maana nilikuwa nasubiria hilo, usiku unaona kitu gani, kunatokea nini..?’ akauliza na mara kukasikika mngurumo wa gari, mume wa huyo mama alikuwa karudi na wageni, ..

‘Nona kuna wageni, tutaliongelea hilo baadae…nataka uje kunielezee vizuri kabisa, …kwasababu kuna mwenzako alikuwa akiishi humu ndani kabla yako, alivumisha mambo mabaya sana, eti humu ndani kuna mashetani, hayo mashetani aliyaleta yeye, mbona sisi hatuyaoni hayo mashetani, acheni mambo ya kishirikina….sasa jiandae kuniambia ukweli wote …’akasema akigeuka kuondoka.

Alipoondoka, kijana wake akasema;

‘Kwanini umemuambia hayo mama yangu..?’ akauliza

‘Kwasababu ndio ukweli ulivyo, mimi usiku nateseka, silali, kwanini nisimuambie…’nikasema

‘Una uhakika kuwa kweli kuna mashetani humu ndani, mbona mimi sijawahi kuyasikia hayo mahetani …yapoje,…., au kunitokea nini…halafu kwanini iwe ni wewe, na huyo mwenzako aliyekuja leo na kuondoka…msitake kuwachanganya wazazi wangu…’akasema.

‘Mimi hayo siyajui kwasababu nimeanza kuyapatia hapa,…sijawahi kusikia hivyo nikiwa huko kwetu kijijini,…’nikasema.

‘Unasikia,….uwe makini na kauli zako, mama ni mjanja sana, anatafuta njia ya kumuona baba ana makosa, nina uhakika kuwa baba hana makosa mimi namfahamu sana baba yangu, na ikithibiti kuwa kuna kitu kinahusiana na baba, na mama akasikia kutoka kwako,…utavuruga ndoa yao,…na hapo hutapata mtetezi tena, baba ndiye mtetezi wako, na alipanga mambo mengi ya kukusaidia, …’akasema

‘Kwahiyo wewe ulitakaje,…kuwa mimi nikae kimia huku napata shida, ….hapana mimi nitasema ukweli, hata kama ukweli huo utaniumiza mimi,lakini siwezi kudanganya…’nikasema.

‘Mbona hujamuambia mama kuhusu hicho kijitabu cha huyo mdada, kama kweli wewe ni mkweli…, au kuhusu huyo mdada aliyekuja kuchukua mizigo yake, alikuambia nini..?’ akaniuliza.

‘Alinisimulia alivyopata taabu, akiwa humu ndani, mpaka akaamua kuondoka…’nikasema

‘Hivyo tu…?’ akaniuliza

‘Ndio, na kwanini na wewe unayaingilia haya, au na wewe una kitu kinakuhusu…?’ nikamuuliza

‘Mimi najaribu kukusaidia wewe, na kuisadia familia yangu, siwezi kunyamaza kama kuna tatizo linaigusa familia yangu, hao ni wazazi wangu, sitafurahi wakikosana, na mimi nimekuwa nikikusaidia hata wewe…tangia ufike hapa,mengine ..ya..ya… kukuomba urafiki ni kawaida tu, …wala usije kunifikiria vibaya…’akasema.

‘Ulisema utafanya juu chini mpaka unipate, nakumbuka sana kauli yako hiyo, nakutilia mashaka na kauli hiyo…’nikasema

‘Unanitilia mashaka, kwa nini unitilie mashaka, …najua huyo mdada kakuhadaa kwa maneno yake ya uwongo,….’akasema

‘Maneno gani ya uwongo….?’ Nikauliza.

‘Hayo, tuyaache kwasasa,… muhimu ni hali hii inayoendelea hapa, ni bora uwe makini na unachokiongea, ukiongea jambo la kumfitinisha baba, ukasababisha wao wakosane na mama. …sijui …na hata hivyo, huyo mdada alichokuambia, mimi simuamini, ..kuna mambo yake mengi alikuwa kiyafanya, na sikuwahi kuwaambia wazazi wangu, maana niliona hayana maana…’akasema

‘Kama mambo gani..?’ nikamuuliza.

‘Huyu mdada ni mshirikina..uwe makini sana na kauli zake, ukimuendekeza atakuharibu, na ukiishirikiana naye, ….utakuja kuingia kusipofaa, na mama atakugundua tu,………..’akasema.

‘Mimi sijui hayo, mimi nazungumzia hayo yanayotokea kwangu, na ambayo kumbe yalitokea na kwake, kwanini yanitokee hivyo kila siku kukabwa, kusumbuliwa, sipati usingizi….na yeye aliniambia hali ilikuw ahivyo hivyo, je hayo ni mambo ya kishirikina…?’nikasema.

‘Mimi nikushauri jambo…’akasema na mara baba na mama wakafika, na tukakatiza mazungumzo, na baba akasema;

‘Ni bora tukayaongelee chumba cha maongezi…sio huku chumbani…’akasema baba na kuondoka na mama akaingia na kusema;

‘Haya, sasa jiandae uje kuna maongezi, nataka uje uelezee kila kitu, ukinificha, basi shauri lako, ..yatakayokutokea usije kunilaumu..mimi nawafahamu sana hawa wanaume, ..unanisikia, mimi nataka nikusaidie wewe haya yasije kutokea tena…unanielewa…, kwahiyo sema kila kitu kinachotokea humu ndani, na kama uliwahi kufanyiwa jambo lolote na mume wangu, uliongee, huu ndio wakati wako…’akasema na kuondoka kumfuata mume wake.

Na kabla sijaondoka kijana akaja ka haraka, akionyesha kuwa ana jambo anataka kuniambia, lakini kabla hajaanza kuongea mara mzee mwenyewe akatokea, na kwa nyuma yake nikamuona mama akiwa kasimama,...
.
NB: Haya mambo ya familia hayo, ngoja tuone itakuwaje kwenye hicho kikao cha familia.


WAZO LA LEO: Matatizo yakitokea kukawa na msigishano, uwe wa wanandoa au uwe wa viongozi au ujirani nk… hekima na busara ni kila mmoja kukubali kushuka, na kukubali kukaa mezani na kuongea, ili muweze kujadili yale yenye sintofahamu. Kiubinadamu, tabia hutofautiana, kutokana na hisia na utashi wa kufikiri, na usipokubali kuwa kuna utofauti huo, utashindwa kushirikiana na mwenzako au kuvumiliana kwenye mambo ya kila siku. Hala hala, ili kuondoka mgongano, jambo jema ni kukubali kukaa na kuongea kwa kusikilizana, kila mmoja atoe duku duku lake, ili mwisho wake kuje kupatikana suluhu..Suluhu hujengwa kwa maridhiano, sio ubabe
Ni mimi: emu-three

No comments :