Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, June 15, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-51


                                                             KESI-HITIMISHO-2

 Hakimu aliwauliza hao watu wao ni akina nani..lakini watu hao walikuwa kama bubu, hawakutaka hata kuongea neno moja na muheshimiwa hakimu akatoa amri kuwa watu hao waondelewe hizo ngozi bandia walizojivika mwilini…, kama walivyoelezea waendesha mashitaka, …na muda huo wakili upande wa utetezi, walibakia kimia, ni nani atampinga hakimu..

Tuendelee na kisa chetu…..

*******************

Wa kwanza kufanyiwa utaratibu huo wa kuondolewa ngozi bandia alikuwa kiongozi…

‘Huyu ndiye alikuwa mtendaji mkuu , kiongozi anayesimamia shughuli zote za kila siku kwenye hilo kundi, lakini yeye sio kiongozi mkuu, kiongozi mkuu mtakuja kumuona baadae, kitu cha kushangaza pamoja na ya kuwa huyu ndiye aliyekuwa anasimamia shughuli za kila siku, lakini hata siku moja hakuwahi kuonekana ofisini mchana, ni kwanini..

‘Hii kwanini ndio iliyonifungulia njia ya kugundua mengi….

‘Wakati naendelea na utafiti wangu, huku nikichunguza, ndio nikagundua kuwa huyu mtu anafanya hivi kwa vile mchana anakuwa kwenye majukumu mengine, muhimu huenda ni ya kiserikali zaidi, na kama ujuavyo, sio rahisi mkono mmoja ukaweza kufanya shughuli mbili kwa wakati mmoja, …uwe sehemu hii na muda huo huo uonekane sehemu nyingine.

‘Huyu mtu atakuwa ni mtu anayefanya shughuli mahali fulani, na ni mtu maarufu sana, kicheo na labda hata kihali za kimaisha,....nikajiuliza huyu mtu anaweza kuwa nani…nilikuwa tayari na orodha ya watu ninaowashuku,…’akasema docta.

‘Kwahiyo wewe umeshamfahamu kuwa huyu mtu ni nani…?’ muendesha mashitaka akamuuliza docta, na docta akasema;

‘Kiukweli bado sijawa na uhakika wa moja kwa moja, ngoja tuifanye hii kazi, ili kuupata uthibitisho huo…’akasema docta akianza kualika, laptop yake ili ianze kufanya kazi, na mara yule mtu aliyewekewa huo waya, ulioungana na laptop, akaanza kufutuka, sehemu ya kichwa hadi mabegani, ….mpaka ikafika sehemu fulani, ikatulia, na mara …ikafunuka taratibu kama mtu anayefungua zipu, ikufunguka kitia sehemu ya karibu na sikio,..

Ilikuwa ni kama unaangalia,katuni fulani inavyoweza kuondoa sehemu ya uso, kutoka sura moja kwenda sura nyingin..na baadae, docta akasogea pale aliposimama huyu mtu,…na kumalizia kazi iliyobakia kwa mkono, na sasa akatokea mtu mwingine tofauti na sura ile ya awali…

Watu wakashika mdomo, wengine wakapiga ukelele, wengine wakasimama..hata muheshimiwa hakimu hakuamini, alijikuta akishika mdomo, akatikisa kichwa, akahema, na baadae akageuka huku na kule akiwaangalia wenzake, waendesha mashitaka, kama kuwauliza na nyie mumeona..akatikisa kichwa tena na tena!

‘Haiwezekani, yaani ndio wewe…siwezi kuku-bali, siamini macho yangu, wenzangu mumeliona hili, kiukweli…’hakimu aliishiwa hata na kauli.

Na mara kutoka kwa watu waliofika humo ndani, kukatokea sauti, na vurumai kidogo, na mtu mmoja alitokeza na sasa akawa anaelekea kumkabili huyo mtu, na walinzi wakamuwahi kabla hajamkaribia…

‘Yaani ni wewe , unatuhadaa kuwa …huku unanitesa mimi na familia yangu, siwezi kukusamehe kabisa,…siwezi,…’huyo mtu akasema…watu wengi walioumizwa kwasababu moja au nyingine walijawa na hasira zilizopitiliza, na kila mmoja alikuwa na lake, ikawa ni zogo, hata hakimu hakutaka kuwatuliza kwa haraka, na mwingine aliyeshindwa hata kujuzuia, akataka kwenda huko mbele alikuwa ni mpelelezi, akiwa kavalia kiraia.

Ilibidi polisi wafanye kazi ya ziada, kuwazuia watu, na kuwatuliza, ilishangaza, kwani kwa muda wote huo hakimu alikuwa kimia, hakugonga rungu lake kuwatuliza watu.

Mwingine aliyeonakana kutokuamini kabisa alikuwa msaidizi wa mkuu wa kituo, yeye kwa muda huo alikuwa ndio kaingia..inaonekana awali hakuwepo, alikuwa kwenye majukumu mengine, na sasa ndio alikuwa karudi, na kwa muda huo, alikuwa anatafuta sehemu ya kukaa…na mara ndio akamuona huyo mtu,…na alipomuona huyo mtu hakuamini..akashikwa na bumbuwazi…, akabakia amesimama, akawa kakodoa macho tu haamini…..

‘Kiukweli, sikudhania kabisa kama huyo mtu ni huyu muheshimiwa…kiukweli  hakuwepo kabisa kwenye orodha za watu niliokuwa nikiwashuku, nijuavyo, huyu mtu alisafiri nchi za nje, au sio....nilikuwa namfikiria mtu mwingine kabisa..’akasema docta, na muendesha mashitaka, akashika kichwa, na baadae hakimu akasema;

‘Haya wewe,…ina maana wewe uliyepewa dhamana ya kusimamia mambo ya serikali, ulikuwa una…aah, ….docta, ulijuaje haya..?’ hakimu akamgeukia docta, na docta akasema;

‘Muheshimiwa hakimu,..hii ni kazi ya muda mrefu sana, ..lakini mungu ndiye aliyetuongoza hadi kufika hapa tulipofikia, sio kazi  rahisi kama watu watakavyofikira, ni kazi ngumu ya kuumiza kichwa na kujitoa mhanga, na kiukweli sio kwa ujanja wetu, ni mungu peke yake aliyetuongoza na kutulinda, hadi siri hii kubwa ikafichuka…’akasema docta, na  muheshimiwa hakimu akamgeukia tena huyo mshitakiwa namba mbili, na kuumuuliza;

‘Haya wewe…sasa utajibu maswali yangu, maana sasa upo chini ya jamuhuri, nataka unijibu swali langu, nililokuuliza awali wewe ni nani…?’

Mshitakiwa huyu, akainua kichwa, maana muda wote alikuwa kainamisha kichwa kwa aibu, au kwa kuogopa watu wasimuangalie,..lakini sasa akainua kichwa na kuwakabili wanachi…akataja jina lake kwa marefu yake.  watu wakacheka waliocheka, wakaguna walioguna,wakazomea walizomea….na walipotulia muheshimiwa hakimu akamuuliza swali jingine.

‘Kazi yako..?’ akaulizwa nay eye bila kusita akaitaja,

‘Mkuu wa kituo …’akasema, na aliptaja hivi watu sasa wakamzomea, na hapo hakimu akagonga rungu lake , na kusema watu wanyamaze, kwani sasa yupo kazini, alishawapa muda wa kutoa hasira zao moyoni, sasa sheria inataka ifanye kazi.

‘Wewe kazi yako ni Mkuu wa kituo, … mkuu uliyepewa dhamana kubwa ya kusimamia usalama wa kituo, umakuwa msaliti wa nchi yako na raia wako, umetutia doa sisi tuliopewa dhamana kama hiyo, inasikitisha sana, ni kwanini,  …?’ akauliza hakimu na kabla hajajibiwa mara kukatokea ghasia ..na hakimu akainua rungu lake akitaka kuligonga, lakini akakatisha.

Mama mmoja alishajitoa mikononi mwa polisi na alikuwa sasa keshafika sehemu ya mbele, huku kashika kichwa, polisi wakamfuata, lakini hakimu akawazuia, na kusema;

‘Wewe mama una shida gani..?’ akaulizwa

‘Nilikuja kuthibitisha,….maana huyu mtu nilijua ni kaka yangu aliyepotea, nilijua ndio yeye anatutesa mimi na familia yangu…, kumbe sio yeye,..ina maana awali huyu mtu alivalia sura ya ndugu yangu, na sasa akavalia sura ya mtu mwingine, kumbe wewe sio ndugu yangu, ndugu yangu, kanipigia simu sasa hivi…yupo huko alipo anaumwa, alipotea watu wakajua kafariki, sasa kaonekana akiwa na hli mbaya sana…na nimemuona kwenye simu mbashara, ulimfanya nini ndugu yangu…’akasema huyo mama.

‘Kwahiyo huyu sio ndugu yako, wewe si ulisema awali kuwa huyu huenda akawa ndio ndugu yako, aliyepotea..?’ kaulizwa na muendesha mashitaka..

‘Huyu sio ndugu yangu kabisa,…’akasema huyo mama.

‘Ndugu yangu ni huyu hapa,….’akaonyesha picha kwenye simu yake.

 ‘Wewe ehe, …hebu tuambie hiyo yote ni kazi yenu, ni kwanini ulifanya hivyo..?’ akaulizwa;

Wakati huo mshitakiwa namba moja alikuwa kakaa kwenye kitu, katulia, kaegemea kiti,…akiangalia juu…na watu wengi wakawa sasa wanamuwazia yeye, atakuwa ni nani…na huyu mshitakiwa namba mbili akaanza kujielezea..

**************

‘ Ndugu muheshimiwa hakimu, wengi wataniona mimi ni mnyama, au mimi ni shetani, kama wengi walivyosikika wakisema,..yote ni sawa kwa uoni wao, lakini hakuna anayejiuliza ni kwanini mpaka mtu ufikie hatua hiyo,…hilo kwasasa hakuna anayejaribu kurejesha akili yake nyuma, akajiuliza…’akasema.


‘Kwanini sasa ukafanya hayo uliyoyafanya,…?’ akaulizwa.


‘Nitasema kila kitu, msiwe na shaka,..najua mwisho wa haya yote umefika, lakini nafahamu haya nitakayoyaongea yanahitajika kusikiwa na kila mtu, ili ukweli uwe bayana, kuwa mtu sio mnyama, unyama unakuja baada ya kutendwa, hasa kama tulivyotendwa sisi,….’akatulia.


‘Huyo mwanamke hapo mbele ni ndugu yangu..kwa vipi, hajui….’akasema na huyo mwanamke akasema;


‘Wewe sio ndugu yangu sikujui kabisa….’akasema.


‘Hutaweza kunijua,…lakini yoyote anaweza kuwa ndugu ya yoyote , sisi sote ni watoto wa adamu, na hawa, basi hiyo haitoshio kuwa sisi ni ndugu, sawa, kwa vile sisi hatukuwa na baba, basi hatuna ndugu, baba yetu alitukana, basi wewe hutoshi kuwa ndugu yangu, hunionei huruma, nisiye na baba, ...najua hutapenda kuwa na ukaribu na sisi, ndio maana tukatumia ndugu yako uliyemfahamu,…’akasema na watu hapo wakatulia, na kutega sikio.


‘Sikulaumu kamwe, maana nyie mlikuwa watoto wa geti kali, lakini sisi tulikuwa machokoraa, omba omba..tulikosa nini….hayo ni maelezo ya awali tu, ya kukufunulia akili yako ujue sisi tumetokea wapi, na kwanini tukawa hivyo,..sasa hebu sikia chimbuko la sisi, ombaomba, chokoraa..watoto wa haramu, tulipatikanaje, unalijua hilo, sasa leo utalijua…’akatulia.


‘Kiukweli mimi sio huyo ndugu yako aliyepotea, tulifikia hatua ya kulitumia jina lake na sura yake kwasababu ya kukamilisha haya…najua wewe unayemfahamu ni huyo ndugu yako na ndugu zako wengine, ...wewe uliyeolewa na mwanamume tajiri, aliyekuwa askari, mtoto wa askari…na kwa cha baba yake mumeo, aliwahi hata kunifunga mimi, nikiwa mdogo tu, hakutaka hata kunisikiliza…


‘Sawa hauna makosa, sawa, hata mume wako hana makosa, makosa anayo, huyo aliyesabibisha mimba ikatunga tumboni kwa mama yangu….huyo ndiye chanzo cha haya yote…’akasema

‘Sasa fungueni masikio, nieleze ni kwanini tulifikia kuayafanya haya yote,.. kabla ya kujibu hilo swali, niwakumbushe kitu kidogo,…’akawageukia wazee waliokuwa wamekaa mbele kama wazee Mahakama, kuna wawili walikuwa wazee kweli


‘Samahanini wazee waheshimiwa, nashukuru, mpo kwenye mahakama hii, maana wazee, wa mahakama, siku hizi ni vijana tu, ila hapa mpo nyie ambao mtakuwa shahidi wangu, je mnakumbuka kipindi fulani nyuma, alipatikana mama mmoja aliyekufa peke yake kwenye nyumba, iliyokuwa imeezekwa kwa makuti, nyumba ya udongo…?’ akauliza.


Wale wazee wawili wakasema wanakumbuka..


‘Safi kabisa….Nyumba hiyo ilikuwa imejengwa hapo walipojenga huyo mnayemuita mzee , ambaye mabinti zake wamejikuta kwenye mkasa huu,…mzee ambaye ndiye mume wa huyu mama, ..mzee ambaye ndiye alinunua eneo hilo kutoka kwa ndugu wa mke wake. Je ni kweli huyo ndugu alilipata eneo hilo kihalali…hakuna anayelijua hilo!


Nawakumbusha kuwa eneo hilo ilikuwa mali halali ya mama yangu, eneo la urithi kutoka kwa wazazi wake, ..lakini alikufa bila kulifaidi, alikufa ndani ya banda bovu, akiwa peke yake, huku mwanaume aliyempa mimba, tena kwa kumbaka akiwa tajiri, akiwa anakula raha na wanawake wake wa ndoa…hataki hata kumsikia.


Mnafahamu mama yangu alikuwaje,…nyie wazee, waheshimiwa huyo mama aliyekufa kwenye hilo banda alikuwaje, kihali yake,..mnajua sana…, ila hamjui kuwa huyo mama ndiye alikuwa mama yetu…’akatulia


‘Na wengine hapo wapo, wanafahamu kabisa ni kitu gani kilitokea kwa huyo mama, lakini ni nani atafungua mdomo wake, wakati ilipigwa marufuku kuliongelea hilo, eti mnamkashifu muheshimiwa, eti anasingiziwa, na atakayeongea ataishia jela kama huyo bibi,..nani alimjali huyo bibi alipofungwa, ni nani..,..alijitokeza kumtetea, ni nani, nani atamtetea, bibi mchawi..si ndivyo mlivyodanganywa..!


‘Nilishalia sana,..siku nasimuliwa maisha ya mama yangu na bibi yake…, nililia sana…sikuamini,..na nilipothibitisha hayo kuwa ni kweli,,..nikaapa kuwa sitalia tena…kilio changu kitakuwa kulipiza kisasi, ndio maana nilijiunga na kazi ambayo itanijenga ujasiri…

‘Unajua kwa historia yangu nisingeliweza kujiunga huko,…historia ya uchokoraa, mtukutu, mwizi…lakini niliweza kusoma na kujiunga na jeshi, askari polisi..ni nani aliyenisaidia hadi kufika huko…mimi nadiriki kusema ni mizimu ya mama yangu…’akatulia.

‘Na kweli nikiwa huko, niliweza kusahau ya nyuma, nikawekeza akili yangu kwenye taaluma hiyo,lakini kwa siri, nilikuwa na ajenda,…na hutaamini kila nikipata kazi ngumu ya kufanya namkumbuka mama yangu, nilivyosimuliwa,,..napambana na hilo tukio , kama ni kazi ngumu kama ni zoezi,..nalifanya hilo jambo, kama vile napambana na huyo aliyemfanyia hivyo mama yangu…’akatulia


‘Najua hata nikilia sasa,… ni nani atanisikiliza…watu huangalia mwisho wa jambo, hawapendi kuangalia chimbuko lake..mwisho huwa mtamu au mchungu kuliko mwanzo wake,…, ndivyo ilivyokuwa hivyo, hata pale mama wa mama yangu alipokwenda kushitaki,ni nani angelimsikiliza, alionekana muongo, mchochezi…’akatulia akimuangalia hakimu.


‘Hakuna haki kwenye hii dunia kwa mnyonge..’akasema akimuangalia hakimu.


‘Muheshimiwa hakimu labda ilikuwa enzi hiyo, utasema hivyo,.. mnatetea, haki za kila mtu utasema hivyo..lakini kwangu mimi, niliposikia yaliyompata mama, yaliyotupata sisi, nasema ..sio kweli,  nyie watu,  anaposhitakiwa mnyonge ndio mnajifanya mnajua sheria, lakini akishitakiwa tajiri, kiongozi mwenye heshima, mnajifanya kuwa na makengeza..ndivyo ilivyotokea kwa mama yangu.


‘MAMA YANGU, ALIBAKWA, na tena alikuwa ni kiwete, mama yake alikuwa mzee, masikini hana mbele wala nyuma,..kaenda kushitaki, anaishia kufungwa…


‘Niliapa kuwa ni lazima nitalipiza kisasi,..sitajutia kwa hilo kamwe,..najua mtanifunga, mtaniua, sawa…lakini afadhali kidogo, afadhali kidogo, angalau nimeweza kutimiza nadhiri yangu…’akasema kwa akitikisa kichwa.


Sasa sikilizeni kumuhusu huyo mama ..aliyekuwa mlemavu wa miguu, ila mzuri wa sura, …’akasema akitabasamu kidogo,


‘Ni mnzuri wa sura, ukiangalia usoni…anafanana, na  haha, ndio maana tulikuja na wazo hilo ka kutumia sura yake, kama…’mpenzi wa facebook’…hahaha, ‘hapo akacheka,


‘Ni nani angeliiona hiyo sura yake ya uso, akaacha kuvutika naye, sura hiyo nikaitumia kama ulimbo kuwanasa maadui zangu..wale wote wanaostahiki kuingia kwenye mtego wa kulipiziwa kisasi wakaingia ndani…


‘Sasa ngoja niwasimulie yaliyomkuta mama yangu na hadi sisi tukazaliwa, naomba mnivumilie…nitachukua muda wenu, lakini masimulizi haya yataaidia kurahisha kesi yenu hii, na mkiondoka hapa mtajua ni kwanini haya yote yalitokea, tofauti na uvumi, na mengi yaliyowahi kusimuliwa huko, hayo yaliyosimuliwa, ilikuwa ni propaganda, tuliyoiunda, na kweli ikanasa..


Nijua mimi sina haki tena..kama alivyoikosa haki bibi yangu na mama yangu, ..lakini haya nataka kila mtu ayasikie, na hata hapo, pumzi yangu ikikatika nijue kila mtu ni shahidi ya haya, mnawaona mayatima , chokoraa, mnawapuuza, wengine hamjui wametoka wapi, wengine walikuwa ha haki ya majumba na mgorofa yanaoota kama uyoga, ni nani atalijua hilo…’akatulia.


‘Mama yangu alipewa mimba kwa kubakwa,..waheshimiwa wazee mliambiwa atakayeongea huo uwongo, maana uligeuzwa na kuitwa uwongo, atafungwa, kweli si kweli..sitaki mnijibu msije kufungwa,..ila moyoni mnalifahamu hilo, ni nini kilitokea kwa mama yangu,mama ambaye alikuwa hajiwezi, miguu imepooza, ..sawa si sawa…’akawa kama anauliza.


‘ Mama yangu alikuwa kapooza miguu yote miwili anatembea kwa kujiburuza..ikatokea siku jamaa mmoja muheshimiwa, akapita sehemu ambapo mama hufanya kazi ya kuomba omba, tamaa bwana,..jamaa huyo akavutika na sura ya binti huyo, maana mama muda huo ni binti, na jamaa huyo …tamaa zake za kupenda wanawke wazuri, zikamvuta..akashindwa kulala


‘Haya naongea yalitokea, sio uzushi, kama nazua, waulizeni hao wazee…jamaa hakuweza kulala, au kutimiza majukumu yake akiikumbuka sura ya mama yangu..


‘Siku moja akashindwa kuvumilia, akafunga safari kwa siri hadi nyumbani kwa mama yangu , wakati huo bibi hayupo kaenda shambani,..alipofika hapo akiwa na zawadi, akamataka mama kimapenzi,..sio kumuoa, anamtaka mama kimapenzi..ni nani angemuoa kiwete…’akatulia.


Mama kalelewa, japokuwa ni masikini, lakini yeye alikuwa anajali utu wake, heshima yake, mama alikataa, akimuambia, yeye hawezi kuzalilishwa, hata akipewa pesa zinazojaa hii dunia,..alijua huyo jamaa nia yake ni kumzalilisha tu, hataweza kumuoa..ana mke wake mnzuri, japokuwa sura yake haimfikii hata nusu ya sura aliyokuwa nayo mama yangu, …huyo jamaa ana wake wengine wa nje, lakini atawezaje kumfanya huyu awe mke wake wa nje, wakati huyo mama kalemaa miguu…masikini, hajasoma…


‘Jamaa huyo, kwa vile kipindi hicho alikuwa na mamlaka, hajawahi kukataliwa, akiwataka wanawake,wanajipeleka wenyewe… akaamua kutumia nguvu, akambaka mama yangu…, mama ambaye, alipooza miguu, mama ambaye ni masikini asiyeweza kujitetea...'jamaa akatikisa kichwa, alijizuia kutoa machozi, lakini yalimlenga lenga….


‘Jamaa alipomaliza shughuli yake akamtupia mama pesa, na hizo mama hakuwahi kuzitumia,….alizichoma moto..lakini mama aliachiwa kitu kingine, uja uzito, ...ujauzito uliomtesa mama, hadi tunazaliwa sisi, ni kwanini mama aliteseka na huo ujazito, musikie sasa nyie wazee, maliojua siri hiyo mkabakia kimia…’akasema.


‘Jamaa huyo si alitumia nguvu, tendo hilo la kutumia nguvu, lilimpa mama jeraha kubwa  jeraha ambalo halikuweza kupona, kwa vile mama alikuwa akijiburuza kwa kuegeme upande mmoja ambao ndio huo ulikuwa na jeraha..jeraha likawa linafumuka kila akitaka kutembea..huwezi kuijua hiyo hali mpaka ikukute..’akatulia.


Jereha hilo likaja kutengeza usaha,, likaoza..atajitibiaje, akinda hospitalini..anaona aibu, ni sehemu ya siri…akawa anatumia dawa za kienyeji, hadi alipozidiwa sana, ndio ikabidi ajitokeze kwa dakitari, muda huo donda limekuwa donda ndugu....nataka mlielewe hili, japokuwa mimi na ndugu yangu hatukupenda kuliongelea hili, tulipanga,tulipize kisasi kimia kimia, na mambo yaishe kama yalivyo…lakini muda umefika jamii mlisikie hili, na hata tukinyongwa mjue tulifanya hivyo,kwasababu gani..

.
Mama akabeba mimba kwa shida…bibi ndiye anahangaika, ..alijitahidi awali kumgundua ni nani kamfanyia hivyo binti yake alipogundua kuwa ni muheshimiwa akamuendea,…hahaha, siku hiyo alisitiriwa, akapewa vijisenti, ili eti azibe mdomo wake.


Baadae akafuatwa na walinzi, akaambiwa asije kuonekana tena eneo hilo la muheshimiwa,…akawauliza kwanini, hiyo ni damu yake, yeye ndiye aliyesababisha hayo, kampa binti yake mimba, bibi akajitetea hivyo,…..alipotamka hivyo, ukazushiwa uvumi,…


Alizushiwa uvumi, ulioenea kama vumbi jangwani, …eti huyo bibi ni mchawi, huyo bibi anataka kumloga muheshimiwa..ok,..huyo bibi walimzuishia uchawi …ndivyo walivyosingizia huyo bibi, ….kwa vile walimzushia huyo bibi wakati kweli hakuwa mchawi, sisi ndio tukajiwa na wazo hilo,..kama yeye alizushiwa, basi katika sehemu yetu ya kulipiza kisasi, sisi tuwe ni wachawi wa kiukweli..bibi au mama hawakuwa machawi kabisa,..wala hawajui hata dawa za kienyeji, zinatengezwaje.. lakini sisi ndio tukaamua kuwa wachawi…’akatulia akijaribu kutabasamu.


‘Uchawi wetu ni wa kusomea…sio wa kurithi…kama alivyo kua yule mzee kigagula…’akasema hivyo.


 Mpaka mama anafikia hatua ya kujifungua, lile donda, lilikuwa sehemu ya siri, limekuwa kubwa, na likawa linamtafuna, si unajua tena, kidonda kisichopona,…kwa jina jingine kansa…mnasikia, mama alikuwa na kansa…ndio aliyomtesa mama, ni kansa iliyotokana na kubakwa na huyo jamaa…


Siku mama anajifungua, ndio kipindi kidonda kimekuwa ni tatizo, kinamuuma kweli kweli,..hadi uchungu unamshika, akajua hatapona, unajua alichowaambia madocta, hasa yule mama aliyemsaidia kujifungua, ..hao madocta mkitaka waiteni wawathibitishie hili…wapo, hadi leo…


‘Mama yangu alisema hivi;-


'Nataka muhakikishe, ninazaa hao watoto mapacha,…maana aliambiwa watoto ni mapacha, nataka, watoto waje kulipiza kisasi, maana mimi ni mnyonge, mimi ni kilema, mimi sina ndugu, ndugu yangu ni bibi yangu ambaye hajiwezi,…wamemfunga, ili kum-maliza asije kutoa hii siri…, sasa watoto hao mje kuwaambia siri hii, ..akawasimulia yote ilivyotokea, na huyo mama akawa kaandika kwenye karatasi, yote aliyosimuliwa, karatasi hiyo ipo, hadi leo…’akatulia.


‘Ninajua mama yangu,akisikia mimi nimekufa, na yeye hataishi tena, hao watoto wapeni wenye uwezo wa walee, na wakiwa wakubwa wasimulieni huo ukweli wote…’ ndivyo mama alisema, akiwasimulia hao manesi na madocta walishughulikia, kuhakikisha sisi tunazaliwa salama...


‘Najua wengine watasema huenda ni uwongo ulizushwa, wengine watasema tuna uhakika gani, waulizeni wazee waliowahi kuitambua hiyo familia, kama wanamuogopa mungu, watayakinisha haya maneno yangu, kawaulizeni hao madocta, na huyo mama ambaye alikuwa mkunga, kipindi hicho, sasa hivi ni mama mzee..’akatulia akiwaangalia wale wazee.


‘Kama nyie wazee mnaifahamu hiyo familia,..kama haya ninayoongea sio kweli, basi,, simameni mkanushe, kuwa nazua uwongo…’akatulia akiwaangalia hao wazee, na hakuna aliyesimama


‘Mama alijifungua kwa shida sana, ingelikuwa ni ….angelifanyiwa upasuaji, sasa mtu hana pesa…basi tena, akajifungua kwa njia ya kawaida,… akiugulia maumivu makali, mungu mwenyewe ndiye anajua ulikuwa uchungu wa kiasi gani…pimeni, fikirieni, wazeni, aina gani ya maumivu aliyokutana nayo mama..


************
 
Sisi tulizaliwa mapacha, mimi na ndugu yangu..siwezi kumtaja huyo ndugu yangu,. na kwa vile ilishagundulikana kuwa mama hatapona, sisi wawili tuligawiwa kwa wasamaria wema…tukiwa vichanga tu…’akatulia


‘Na hata hao waliotuchukua, walikuja kutushindwa, kwani walikuja kuwa na familia zao, wakawa hawana uwezo, tukatupwa mitaani, tukawa chokoraa…mnajua maisha hayo yapoje, siwezi kuwasimulia, hayo maisha yalikuwaje, maana ni hadithi ndefu ya kusikitisha....ninachotaka ni kusimulia kilichotokea kwa mama, ambacho ndicho kilituvuta mimi nije kulipiza kisasi…


Nasikia mama hakuweza kumaliza mwezi akafariki, na bibi ambaye ndiye mlezi wake, aliposikia kuwa mjukuu wake kafariki na yeye hapo hapo akafiriki akiwa gerezani, hebu fikirieni, nyie watu mnaojifanya ni malaika, maana sisi ni mashetani, nyie ni nani ni malaika, si ndio, huyo bibi alifungwa kwa kosa gani,..…’akawageukia wazee, halafu watu, watu walikuwa kimia.


Mama alifariki akiwa peke yake kwenye hilo banda la matope, lililoezekwa kwa makuti, kama wapo wazee wa siku nyingi waulizeni…walifanya nini kumsaidia huyo mama, mama anaumwa, hajiwezi, anaishia kula wadudu..acheni tu….’hapo akashindwa kuvumilia na kulia.


Nawauliza wazee ni nani aliyasababisha yote haya…nijibuni….’akawageukia hao wazee, na hakuna mzee aliyesema kitu.


‘Najua hamtasema kwa sababu mnaogopa kufungwa, kama alivyofungwa bibi, si ndio hivyo, lakini mungu anawaona…..’akatulia

Akamgeukia huyo mama aliyekuwa kasimama hatua chache, mbele ya watu waliokuwemo humo, …

‘Sasa nikuulize wewe unyejifanya kuwa sio ndugu yangu, unamfahamu huyo aliyembebesha mama yangu huo uja uzito, …najua, lakini sina uhakika, uliwahi kusimulia na bibi yako wakati anataka kukubadhi mkoba,..

‘Hapo utajifanya hukumbuki, na je, kuna tukio lilitokea,..nikiwa mdogo chokoraa, niliwahi kukuibia, wewe ulikuwa mtoto,..mimi kijana kijana …nikaja kufungwa jela ya watoto, kisa nimekuibia wewe mtoto wa muheshimiwa,..kipindi hicho sijajua wewe ni nani, na mimi nimetokea wapi, nilikuambiaje,..ipo siku nitajua ukweli wa wazazi wangu, na nitakuja kulipiza kisasi, niliongea tu, wala sijaujua huo ukweli…nilifungwa jela ya watoto,

Nashukuru sana nikiwa jela ya watoto ndio nikaanza kujifunza maisha, na nilipotoka hapo ndio, nikaanza kujitambua, nikasoma..na hapo ndio ikaja wazo la kutafuta ukweli , mimi ni nani, na kwanini ilitokea nikawa hivyo, sina baba , wala mama, wala ndugu yoyote…nitawasimulia hilo…
.

‘Sasa nakuuliza wewe mwanamke, je unajua ni nani,..aliyembaka mama yangu, akasababisha hilo jeraha…nijibu wewe mwenyewe kwa kinywa chako ili niweze kuendeela na maelezo mengine…’akamuangalia huyo mama, lakini huyo mama alibakia kimia.

‘Ninajau mna hamu ya kufahamu kwa jinsi tulivyoweza kubadilika, na kufanya tuliyoyafanya tuliwezaje, na tulifanyaje, hayo nitayaeleza yote kila mtu afahamu, hadi akatokea binti mrembo wa facebook,…huyo alikuwa ni nani, tulimtengezaje,…nitawasimulia, lakini kwanza nataka huyu mwanamke anijibu je anafahamu huo ukweli, je ni nani alimbaka huyo mama aliyefia kwenye hilo banda peke yake,,…’akamuangalia huyo mama, akisubiria jibu, mahakama ilikuwa kimiaa.

NB: Kidole kinauma, tutaendelea sehemu ijayo


WAZO LA LEO: Binadamu ana utu wake, kama mwana-adamu..ila madhila yakiwa mengi, dhuluma zikazidi,..kukawa na kuteseka kwingi, hali hiyo, humfanya binadamu akageuka kuwa mnyama..na ndio maana viongozi wanatakiwa kusimamia kwenye haki na ukweli, wakahakikisha kuwa mnyonge hadhulimiwi na mwenye nacho, …Tumuombe mungu atujalie, tuwe waadilifu, wachamungu, na tunaotenda haki na yaliyohaki, na tuwe na viongozi waadilifu,  ili tuwe na maisha mema hapa duniani na kesho ahera.

Ni mimi: emu-three

No comments :