Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, May 22, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-33



Mzee aliona mkewe anachelewa kurudi, akamtafuta kwa simu, hakupatikana, hakupenda mkewe aende huko kabla hajagundua ukweli, hakupenda kumuambia mkewe ukweli, kwani alijua akimuambia,...mke hatamsamehe, lakini hadi sasa hajaamini, ..

Na kwa jinsi mkewe alivyochelewa ndivyo alivyozidi kuingiwa na mashaka, huenda kuna jambo jingine limetokea kwa mkewe;


***********
Usiku ukaingia na Mzee hakuweza kuvumilia tena, huwezi kulala huku hujui mke kaenda wapi, au amekutwa na masahibu gani… kwa haraka akaingia ndani ya chumba chake maalumu, huko alikuwa kaweka silaha yake maalumu na vitatu maalumu.

 Hakupenda kabisa kuigusa hiyo silaha, tangia wahamie hapo, alitengeneza chumba chake maalumu cha kuhifadhia kumbukumbu zake za kazi, ikiwemo silaha hiyo na viatu hivyo. Vyote hivyo alipewa akiwa jeshini, silaha hiyo alipewa kama zawadi, alipokuwa kazini, wakati huo serikali ilikuwa na ushirikiano na Cuba, kutokana na umahiri wake wa kazi, na kuibuka kuwa mlenga shabaha mahiri kwa kipindi hicho.

Viatu alipewa wakati wa mashindano ya upelelezi maalumu akiwa msyari wa mbele, kuwachunguza maadui, siri ya viatu hivyo ukiviona ni viatu kamili vya kijeshi, lakini chini vimetengenezwa maalumu,…hata urukue juu kiasi gani ukitua chini havitoi sauti…na vinaweza kukuwezesha kutembea kwenye ukuta kama paka.

Alipoviona viatu hivyo, mara akaili yake ikamkumbusha ndoto, au tukio ambalo yeye aliliona kama ndoto, mpaka sasa hajajua kuwa ni kweli au ni ndoto,maana kama ni kweli basi, …ana kesi ya kujibu, na pia huenda kafanya kosa ambalo hataweza kulisahau maishani..

Binadamu kichwa chake ni cha ajbu sana, muda wa sekunde kadhaa unaweza kukumbuka tukio la siku nzima,..hapo akiwa ndio anakishika hicho kiatu akakumbuka ilivyotokea…

Tuendelee na kisa chetu….

***********
Alipovigusa vile viatu…, ndio akakumbuka kitu, kwanza akashindwa kuelewa, ilikuwa ni ndoto au ni kweli, anachokumbuka, ni kuwa, alipokuwa ndani…, alihisi mwili ukimlegea,…akili ikawa kama sio yake, na mara ikaja nguvu fulani inayomvuta kuwa aende mahali fulani, na bila hata kuwa na utashi wa kujizuia, akafanya hivyo, kuelekea huko anakovutika kwenda, …

‘Fanya hivyo haraka , ukamuokoe binti yako,  usipofanya hivyo bint yako atauwawa..’akaambiwa kinamna ambayo haelewi kuwa anaambiwa au anahisi hivyo.

 Na ili athibitishe hilo,…kuwa binti yake yupo matatani, basi kwanza aende kwenye nyumba yake ya zamani-makaburini! Ile nguvu ikamvuta, na kufanya hivyo akachukua bajaji na kwa haraka akafika huko…na cha ajabu kweli alimuona bint yake akiingia kwenye hilo jengo.

‘Kweli yule ni binti yangu, lakini mbona anatembea vile, ana nini binti yangu…’akawa anajiuliza kwani alimuona binti yake akitembea kiaina yake, sio utembeaji wa binadamu wa kawaida..kama roboti, kama kunyata lakini kwa haraka.

 Akataka kumuendea ili aone kama binti yake yupo sawa, lakini kuna hali ikamzuia, akiambiwa hana muda wa kufany ahivyo, anatakiwa kufanya jambo jingine ili kumuokoa binti yake.

'Ukitaka umuokoe bint yako kwa haraka, kwani yupo matatani, wewe unatakiwa uende kwenye lile gorofa kubwa linalojengwa na upande hadi juu kabisa…huko utaweza kumuona kule alipo, na utapata maelekezo zaidi!’ akaambiwa.

 Basi akafanya hivyo,…akiwa na hamasa kubwa, kwa haraka, akaanza kupanda kuelekea juu, akiwa na vile viatu alikuawa mwepesi sana, na aliweza kuruka ngazi tatu kwa wakati mmoja, na alipofika juu, akaona silaha…

‘Silaha…’ akajikuta akitamka hivyo.

‘Ndio hiyo ni silaha ya kumuokoa binti yako…hiyo ina darubini utamuona binti yako akiwa kule kwenye jango lako…’akaambiwa.

Bila kubisha akaisogelea ile silaha,uzuri wa silaha hiyo, unaweza kumuona mtu akiwa mbali na hata kumuua mtu akiwa mbali sana…moyoni akawa na hamasa, ya kumuona binti yake, na kumuhami na adui yoyote, akaiweka ile silaha vizuri.

'Unaona silaha hiyo, itumie darubini hiyo uangalie kule kwenye jengo lako, utamuona mtu aliyetumwa kumuua bint yako,…umuwahi kabla hajafanya hivyo, nia yako ni kummaliza binti yako kabisa…’akaambiwa.
 Mzee kusikia hivyo hakuchelewa, akaichukua ile darubin na kuangalia kule, kwenye jengo lake, na kwa muda huo dirisha la kile chumba ambacho bint yake alikuwa akikitumia wakati ule walipokuwa wakiishi,…alishangaa hata dirisha lipo wazi! Na walipohama nyumba hiyo, waliacha kila kitu, kitanda makabati…

Mara akamuona mtu akiingia kwenye chumba hicho cha binti yake akiwa na bastola mkononi,…sasa anatembea akionekana kulenga ile bastola muelekeo wa sehemu anayolala binti yake,..taswira ikamuonyesha binti yake kama anapiga yowe la kuogopa,..kapanua mdomo kama anataka kupiga yowe lakini sauti haitoki,…mzee akahamaki.

‘Wewe..kwanini unataka kumuua binti yangu…’akasema na mara ila hali ikamwambia;

 'Umemuona adui ya bint yako huyo…, ukichelewa tu bint yako anauwawa, sasa wewe cha kufanya umuwahi huyo binti kabla hajamuwahi binti yako…, silaha hiyo, sizani kama umesahau jinsi ya kuitumia..na shabaha unayo, kazi kwako…’akaambiwa.

 Mzee, akaichukua ile silaha ikiwa na darubini, akawa anaangalia kule ndani, nyumbani kwake. Darubin ile ilikuwa na nguvu sana, ni zaid ya nguvu za kawaida, kwani aliweza kuona vyema kule chumbani kwa bint yake…na zaidi ni taswira kama vile unaangalia video..ya kuonyesha chumba kizima...

 Yule mtu akiwa na bastola akawa sasa anajiweka sawa kulenga kule alipo bint yake, akiongea maneno ambayo hakuweza kuyaelewa na binti yake akawa kama anaomba msamaha…, na mara binti yake akachomoa bastola…

Mzee akasita..binti yake kapatia wapi hiyo bastola….

 'Mzee ukichelewa bint yako anauwawa..lakini macho yake sasa yakavutwa kuangalia kiwambo cha kufyatua bastola cha yule mtu ili aone jinsi gani anavyofyatua…

 Akaona kidole kikianza kuvuta, na yeye, akashika cha kwake, akijua sasa kachelewa, mara...yule kule akafyatua na yeye akawa keshatangulia kufyatua, aliona risasi kule ikitoka kuelekea kwa bint yake na wakati huo huo risasi ya silaha yake ikielekea kwa huyo binti…

Ilikuwa kama movie…unaona risasi inavyokwenda kwa bini yake,..anatamani kuizuia…, risasi inampiga binti na muda huo risasi kutoka kwenye bunduki yake ikimtoboa huyo mtu kichwa, lakini keshachelewa,…Yule mtu alirushwa na kulala sakafuni, kule kitandani binti yake ananyonga na kutulia..kuashiria na yeye…oh, alishindwa hata kuvumilia, akapiga ukelele wa nguvu.

'Unaona huo ni uzembe wako, nimekuambia umuwahi huyo mtu,…ukajifanya kuonyesha huruma, umesahau vita, adui yako akikuwahi umekufa,, dawa ni kumwahi yeye,…sasa jamaa kamuua bint yako , na wewe umemuua huyo mtu, lakini yote hayo ni kwa uzembe wako…ndio maana mke wako hakuamini, huwezi kulinda familia yako wewe…’akaambiwa.

Mzee akasukuma ile salaha mbali na yeye, sasa akitaka kuteremka pale kuelekea chini hadi kule kwenye nyumba aone kama anaweza kumuoko binti yake, labda risasi ile haijamuua..lakini akakumbuka alimuona binti yake kabisa akiwa na dalili za kukata roho…

‘Oh, ni nini hiki, kwanini…’akawa analalamika

 Sikiliza mzee wewe umefika vitani, risasi haina mchezo,…lakini hata hivyo ujue bado upo vitani, sasa kaa ukilia hapo askari waje kukukamata ushindwe hata kuja kulipiza ka binti yako… ondoka hapo haraka, askari watakuja kukukamata,..’ile hali ikamuambia, na hapo kweli akagundua hatari iliyopo …


 Basi akiwa hata hajielewi,..keshachanganyikiwa lakini hakuwa na mamlaka ya kujizuia amri ikitolewa fanya hivi unatii tu… akaanza kukimbia kushuka chini, na wakati anashuka kuelekea chini, mara  akamuona mtu, akiwa  kasimama kwenye ngazi,…hakujali akampita,hakuwa na muda tena…keshasikia king’ora cha polisi…na alipofika chini, akageuza kichwa kutizama juu, …kumuangalia yule mtu aliyempita ni nani, je anaelekea juu, au ni fundi tu…

Wakati anamitizama kumbe na yule mtu alikuwa akimuangalia kwa mashaka, yule mtu alikuwa akimshangaa…wakakutanisha macho…oh!

 ‘Huyu sio yule mwenye nyumba yangu ya zamani,..!’ akasema na muda huo hakuwa na muda wa kuhakikisha, alishaambiwa polis wanakuja, na keshaua, na hajui hatima ya bint yake…huyo mtu atampigia simu akifika nyumbani kutafuta njia za kumvunga, anajua yataisha lakini ni lazima amtafute huyo aliyemuaa binti yake…

 'Wewe fika kwako, lala, pumzika, mengine utasikia baadae…’akaamrishwa

‘Haiwezekani…’akataka kupinga lakini hakuweza kuipinga hiyo amri akajikuta anavutika kwenda kwake.

‘Huwezi kufanya lolote kwa sasa…’akaambiwa

**************

Na kweli alirudi kwake akaingia chumbani kwake na kulala,…baadae alizinduka wakati mke wake anamuamusha..

‘Wewe vipi mbona unalala na viatu…na hivyo viatu, si ulisema hutavivaa tena…’akaambiwa na hapo akasimama na kujikagua, hakuweza hata kumuelezea mke wake,..na muda huo ile akili ya kuingizwa kwenye nguvu za giza imeshaondoka, na hajui kama kilichotokea ni ndoto au ni kweli, lakini kama ni ndoto, mbona kavaa hivyo..viatu...viatu vyake maalumu vya kivita ...

'Kwann umelala na hivyo viatu mume wangu, na unanuka jasho, ulikuwa wapi, unachkua mazoezi, au…maana nikumbavyo, kwa kauli yako, ulisema hutaki kuviona tena hivyo viatu…na mlango wa kile chumba upo wazi,…kulikoni, mbona unavunja sheria zako mwenyewe…’mke wake akamuambia.

‘We acha tu mke, ….sijui, …hata sielewi..ngona nivirudishe huko ndani,…maana hata siwezi kusema lolote nimechanganyikiwa…’akasema na kukimbilia kwenye hiyo ofisi yake na kuvirudisha hivyo viatu,…na siku hiyo akawa mpole, hataki hata kuongea na mtu…

*********

  Ukumbuke hapo ni wakati anavichukua hivyo viatu kutoka kwenye sanduku ambalo huhifadhi hivyo vitu, na ukumbuke sasa yupo na akili zake timamu, sio kama ile awali alikuwa kwenye hiyo hali isiyoelezeka,… sasa akaiendea dhamira yake, kwenda kupambana na hao watu,…akavaa viatu vyake na sasa anaiendea silaha yake.

‘Lakini hata hivyo akajiuliza anakwenda kupambana na nani…!’

 Akakumbuka siku…kwenye hiyo ndoto, au tukio…siku kweli  alimuona  mtu wakati anakimbia kuteremka chini ya lile jengo…hajampigia simu,….na yule ana uhakika ni yule mwenye nyumba, ambapo waliwahi kapanga awali akianza maisha, ni lazma huyo mtu atakuwa anajua lolote, ni lazma atakuwa anajua kitu…ni lazima aende kwake leo hii hii…

 Na wa pili…wa kumshuku tu,  ni huyo anayemiliki super market, nduguye na marehemu, …sijui kwanini dhamira yake inamuweka huyo mtu kwenye makundi hayo mabaya, hana uhakika au ushahidi, aliwahi kumuelezea mkuu wa kituo, huyo ambaye kaenda likizo, lakini huyo mkuu, hakutilia manani,…na huyo ni lazima atakuwa anahusika, na kwa vile na huyo mkuu, alimzarau, hakutilia maanani alichokigundua yeye, japokuwa hakina ushahidi, absi hata huyo mkuu anahusika.
‘Hawa watu wana kesi ya kujibu, na watajibu tu,….’akasema akilini akidhamiria kutumia bastola ikibidi kuwatisha waseme…hatajali sasa nani ni nani..hatajali kuwa huyo alikuwa mwenye nyumba yake, au huyo ni tajiri, au huyo ni mkuu wa kituo cha polisi…

‘Hawa watu wataniambia…na wataniambia maana nitakuwa na silaha,…’akasema kwa sauti…sasa akisogeza hilo sanduku la viatu na koti lenye kuzia risasi, hakuwataka kulivaa hilo koti,…alitaka kwanza kuichukua silaha yake maalumu.

'Sasa sioni umuhimu wa kuishi, na nikishamaliza hii kazi na mimi nitajiua, ...nipotee mbai kwenye hii dunia ya mateso…’akasema akipiga piga kifua…

 Alipofikia hapo, akafunua sanduku, pale anapoweka bastola yake,…cha ajabu kwanza sanduku lilikuwa limefunguliwa, …halijafungwa na fungua…na alipolifungua kabisa , sanduku lilikuwa tupu…na bastola haipo..

Mzee akahisi nguvu…alibakia kukodoa macho yasiyoaamini…na baadae akasema kwa sauti,

'Ni nani huyu kachukua bastola yangu..'akajikuta akisema tena na tena…lakini hakuna wa kumpa jibu…,

 Na kwa haraka, na akili za haraka,.. akahisi ni mkewe,

Hakuna mtu anayeweza kufungua chumba hicho zaidi ya mkewe, hakuna anayejua ufunguo wa chumba hicho zaidi ya mkewe, na jinsi ya kuufungua mlango huo anayeujulia huo mlango zaidi yake ni mkewe!...Kwasababu mlango huo unahitajia umakini wake, katika kukizungusha kitasa cha mlango, ni kama una namba za siri, na mkewe peke yake ndio anajua.

'Sasa kwanini akachukua hii silaha,…kwanini jamani…. mke wangu, kwanini, unajitakia matatizo,na sasa hata sijui, imekuwaje, na kama ni yeye , najua ni yeye, maana …hapana ni yeye, swali ni kwanini kaichukua na …oh..?! 'akajiuliza

‘Huyu mke wangu anajitakia matatizo...sijui kafanya nini na hii silaha, maana hiyo silaha kwasasa haina, ...sijaisajili tena, nilitaka...oh, …hili sasa ni balaa jingine..sasa labda kazidiwa nguvu na hao watu wameshamuu..a....a…a..hhh!...’mzee akaishiwa nguvu kabisa.

‘Potelea mbali…..nitakwenda hivi hivi, na sime yangu, kama ni kunimaliza, wanimalize tu…, nina maana gani kwenye hii dunia, watoto wangu wote wamewaua, sasa mke...mimi nina faida gani kwenye hii dunia…siwezi kulala hapa nyumbani kama kondoo..nitakufa kama chui….’akasema sasa akiendea kabatio jingine ambalo kaweka sime maalumu….

Na muda huo tayari alishavaa hivyo viatu…bahati sime ilikuwepo, akaichukua na kuitwika kiuononi,  mara akasikia mlango, ukifunguliwa….

 ‘Oh, atakuwa mke wangu, kweli mungu mkubwa…’

 Kwa haraka akatoka kwenye kile chumba huku akihakikisha kuwa amekifunga  chumba hicho, kawaida hafanyi makosa, labda hiyo siku ya tukio ambalo mpaka muda huo hajaamini..ila ushahidi unavyozidi kutokea, anaanza kuhisi kuwa ile sio ndoto, ilikuwa ni kweli,….na kama ni kweli binti ni marehemu, na saa mke naye hayupo…labda ndio huyo kaja, kama ndio yeye, basi atamsimulia kila kitu…

Haraka haraka, akawa anakimbia kuelekea mlango wa kutoka nje,  na wakati anashika kitasa , mlango ukatangulia kufunguliwa, yaani yeye analegeza kitasa kwa ndani ili uweze kuufungua kwa nje, huyo mtu wa nje akatangulia kufungua.

 Tahamaki wanapigana kikumbo na huyo mtu anayeingia kwa kasi ya ajabu kweli ni mwanamke ..na akili yake ishajirizisha kuwa ni mkewe….lakini ule uingiaji wa kasi na mna ile kulikoni,  na kile kikumbo kililimfaya apepesuke akitaka kuanguka,:

'Aah vipi wewe mbona haraka hivyo....'akasema sasa akijihami, akijua mkewe labda anafukuzwa na kitu cha hatari….akawa anachungulia nje kwa tahadhari, mkono umeshikilia sehemu aliyofutika jamvia kiuoni…
 Akachungulia nje, hakuona kitu wala mtu, zaidi ya bajaji lililokuwa likiondoka kwa kasi…, kuashiria kuwa mkewe kaletwa na hilo bajaji.

‘Oh, mke wangu naye,…’akasema sasa akigeuka kuangalia huko mkewe alipo..

Sasa akageuka, akijua atamkuta mkewe kasimama karibu yake…., akimsubiria, akijua yeye kakasirika, kwahiyo…lakini ..kitu cha kwanza kumshtua ni nguo...

Alitangulia kuziona nguo kwasababu, huyo mtu, aliyejua ni mkewe, sasa kampa mgongo, anaelekea eneo la vyumba..na anakumbuka kabisa mkewe hakuwa amevaa hizo nguo wakati anaondoka…Na ni nguo za hospitalini…ina maana mke labda aliumizwa akalazwa..sasa katoroka hospilaini….akawaza hivyo!

Mzee akainu amguu kumfuatilia …lakini kabla mguu haujainuka,…yule mtu, ambaye sasa anahisi ni mkewe..akageuza kichwa,,...
 Mzee alihisi mwili ukiwashtuka….macho yakimtoka,..akili ..ikawa kama …kitu kikichoma kifuani, akahisi mlio fulani kichwani,..nziiiiii, na hapo hapo giza likatanda usoni!

NB: Ni kazi kweli kuiweka sehemu hii kama hivyo, lakini tupo pamoja,

WAZO LA LEO: Ukipenda kutendea wenzako ubaya, ukipenda kuwaumbua wenzako na kuwafichulia aibu zao,  ukapenda kuwatangaza wenzako ubaya hata bila ya kujua ukweli halisi, …kwako waona raha tu..ujue na wewe ipo siku utafanyiwa hivyo!


Swali,…je wewe ni kazi yako, kisheria, kufanya hivyo, hapana…ila wafanya hivyo kutafuta sifa, biashara ya mtandao wako, sawa utapata watazamaji wengi,…yawezekana kwa mtizamo wako unawakomoa hao watu,…au kama usemavyo, unawafanyia hao watu hivyo ili wajirekebishe, ..lakini je ni kweli….na je ni sahihi, kuweka aibu za wengine mitandaoni, picha za uchi, picha za kebehi, kuzalilishana…kiukweli sio vyema,sio uungwana, sio hekima, sio busara, sio utu!
Ni mimi: emu-three

No comments :