‘Mkuu,… msaidizi wangu ananihitajia sana….’akasema docta.
‘Msaidizi wako bado yupo ICU...'akajibiwa
‘Una uhakika na hilo..?’ akauliza docta.
‘Kwanini unasema hivyo..?’ akauliza mkuu
Mkuu alipopiga simu kwa watu wake huko hospitalini, akaambiwa ndio na wao walikuwa wanataka kumpigia baada ya kutafuta kila kona, ..msaidizi wa docta hajulikani wapi alipo, na wana uhakika asingeliweza kutoka, kwanza alikuwa hajaweza hata kutembea...pili ulinzi, na hadi kutoka nje, kuna sehemu mbali mbali angelipita, sasa alipitaje, wao wanahisi bado yupo humo ndani...
Mpelelezi, akamuangalia docta kwa macho ya kuuliza, akiwa kajaa hasira, hakuweza hata kuongea na mtu wake huyo akatoka nje kwa haraka na kuelekea ofisini kwake,
Mpelelezi, hakuamini..mpaka alipowapigia watu...
Tuendelee na kisa chetu..
*************
Mpelelezi alipoona bosi wake katoka akiwa kabadilika akajua kuna
jambo limetokea , na kwa jinsi amjuavyo bosi wake, basi siku hiyo iakuwa ngumu
sana, na huenda kukatokea tamko kali baadae…na yeye bila kuongea kiti na docta
, kwa haraka akatoka nje kama vile anamfuata huyo bosi wake, lakini alipofika
nje, akasimama na kuanza kuwasiliana na watu wake;
‘Vipi imekuwaje..?’ akauliza, na kusikiliza kwa makini baadae
akasema;
‘Mtafuteni haraka, haiwezekani, ina maana alipitia wapi,…kabisa
hamkumuona akitoka, haiwezekani,.. au ni ujanja wa hawa watu wamemuhamisha
kwa….ngoja nitaona…’akasema na baadae alipomaliza kuongea na watu wake akarudi
kwa docta.
‘Haya docta mpiga ramli, hebu tuambie msaidizi wako yupo wapi…?’
akauliza
‘Hata kama ningelijua wapi alipo, nisingelikuambia,..lakini
sijui wapi alipo na hilo linanipa mashaka makubwa sana, najua ni watu wenu wanafanya
hivyo…’akasema docta.
‘Watu wangu wetu kwa vipi, …nimeongea nao na wao wanashangaa kwa
jinsi gani alivyoweza kutoka bila kujulikana,…haiji akilini…’akasema mpelelezi.
‘Ndio sasa mjue kuwa mnachocheza nacho sio jambo rahisi kama
mnavyodhania, nazidi kukusihi ndug yangu…., jirudi…, hao watu sio wema, huko
ulipoingia ni kubaya sana, nakujua na najua hatari zake..’akasema docta.
‘Docta, nakuelewa sana,… lakini hata ramli wakati mwingine
zinakosea, na hiyo uliyopiga dhidi yangu umekosea sana…, sivyo hivyo
unavyonifikiria mimi ,wewe, kuwa ndivyo nilivyo, kamwe siwezi kuisaliti nchi
yangu na watu wangu, kamwe, lakini hutaweza kunielewa…’akasema mpelelezi.
‘Lakini binti yako alikuwa na matatizo kweli si kweli…?’akauliza
na mpelelezi akageuka upande mwingine akawa kama nataka kuondoka halafu akasema;
‘Ndio hilo nalikubali sana..binti yangu alikuwa na matatizo, ,..lakini
mmh, mbona wapo wengi wana matatizo kama hayo, utasema na wao wanajihusisha na makundi
hayo haramu…’akasema kama anauliza sasa akiwa amempa mgongo docta.
‘Naju mlihangaika sana,…mpaka mkakutana na jamaa fulani,..na
mipangpo tu ilipangwa iwe hivyo,…huyo jamaa ndio akakushauri jambo,..
ukamwambia, upo tayari kwa lolote lile..sawa ni sawa..?’ akauliza
‘Sasa ukiwa unaguliwa, na mtoto wako akaja mtu akakushauri
dawa..utasemaje, pesa ni nini bwana..siwezi kusema nina uwezo, lakini
…nilimuambia hivyo nikiwa na maana nitajitahidi niwezavyo…’akasema
‘Sawa, nataka kuhakiki jambo tu…maana sio mimi, ..lakini mimi
kama docta nataka kuhakiki kila kitu, ..je alikuuliza nini, baadae, ..si
alisema,…una uhakika, upo tayari,..?’ akauliza.
‘Mhh..yah, alisema hivyo, nikajua kuwa anataka kuhakikisha kuwa
nipo tayari hata kwa kutibiwa kienyeji, ….’akasema docta
‘Na wewe ukamjibuje…?’ akauliza
‘Nilimuambia …ndio…ningesemaje hapo…’akasema
‘Ndio hapo akakuelekeza wapi uende,…na ukaenda na huko,
ukaelekezwa madawa na kwenda makaburini,..sijui tambiko ..nini na nini, au sio…
ukafanya hivyo, au sio, ..nijibu ili niwe na uhakika…?’ akasema docta.
‘Ndio nilifanya hivyo…’akasema mpelelezi, sasa akimgeukia docta.
‘Na kweli ulipofanya hivyo, mtoto wenu akapona,…na wewe na mkeo
mkafurahi sana, hata mlitaka kufanya sherehe na mlipokwenda kwa jamaa kumualika
akawaambia msifanye hivyo…’akaambiwa.
‘Oh…docta..umejuaje…’akasma
‘Ila ukapewa masharti ya kutoa makafara la damu..kwanini damu,
na tena damu ya mtu, unakumbuka…?’ akaulizwa na hapo mpelelezi akageuka kumpa
mgongo docta.
‘Docta, …kuna mengine siwezi kukujibu, nielewe tu…’akasema
‘Nakueleze hilo, ili uone wapi walipokutegea, na iwe fundishi,
kwanini kafara , kwanini damu, kwanini..makaburini, kwanini..huyo ni shetani
anawachezea, ungelikuwa na imani ya dini, ungejua jinis gani ya
kujilinda…’akasema docta.
‘Wewe hujapata matatizo ambayo yanakugusa sehemu ambayo huwezi
ku…huku mtoto, huku mke hakuelewi,..unajua, we acha tu,…’akasema
‘Swali je ulikubali kuyafanya hayoo..?’ akauliza
‘Hivi..unaelewa jibu lake docta…’akasema
‘Jibi ni kuwa ulikubali, kumbuka ulishasema upo tayari kwa
lolote lile,kwao kauli hutunzwa, kama ushahidi,..kwahiyo …ukakubali, jibu ni
ndio..’akasema docta.
‘Ningefanyaje…’akasema mpelelezi.
‘Ndio tatizo lilianzia hapo…’akasema docta.
‘Docta tatizo halikuanzia hapo…lilianzia kipindi mtoto wangu alipoanza
kuumwa, ukisema lilianzia hapo unakosea…’akasema
‘Nina maana kuwa tatizo la wewe kuingia kwenye mtego wao …mtoto
angelipona, kwa njia za halali tu..sema ndio hukuelewa, hukumuweka mungu mbele,
elimu ya dini kwenu ni shida…mbona mimi nilishapata matatizo , nilikuwa
nimechanganyikiwa kabisa, ..naokota makopo..unajua…lakini imani ya dini,
mitihani hii hukufika ili kujaribiwa,…’akasema docta.
‘Sawa bwana…’akasema mpelelezi.
‘Hawa watu walikuwa wanakutafuta, ulipohamia eneo hili
wakagundua nyota yako ni kali sana…wakaanza kukutengenezea mitihani,..na wewe,
najua…ukaingia kwenye anga zao,…siku moja akakujia jamaa mwingine lakini hao
hao, kwa shauri la kutafuta kipato,…’akasema
‘Docta hayo mengine ya nini,achana nayo…’akasema
‘Sio mengine ni hao hao…walishaanza kukuharibu akili wewe hujui
tu…’akasema docta.
‘Hapana akili yangu inafanya kazi, najua mitihani hiyo
ilinipeleka kubaya, lakini sikuwahi kuokota makopo…’akasema.
‘Huyo jamaa alikuja kwako wakati huo huna mbele wala nyuma,,
umekopa pesa ofisini, unadaiwa, ulikuwa na pesa ya kikundi ya mkeo mkaitumia,
…nyuma ina deni..huku mtoto bado anahitajia dawa…anasoma, huna pesa, ulifanya
nini hapo, na ukumbuke akili yako ilishachezewa…’akasema docta.
‘Mhh…kweli wewe unajua kupiga ramli…’akasema mpelelezi sasa
akionyesha kuwa huru kuongea.
‘Ukakubali na mikakati yake ya kuingiza kipato, maana hukuwa na
jinsi,..ni mbinu zao hizo, kama sio kwenye kukutegea ugonjwa, watakuingiza
kwenye umasikini uliokithiri, madeni.., yeye akakupigia mahesabu ukakubali
..lakini ukiwa na mashaka,.’akaambiwa.
‘Ok,…’akasema hivyo tu.
‘Na ghafla mtoto akaanza kuumwa tena, na mtoto na unakumbuka
mtoto alidai nini ili apone….’akasema docta
‘We acha tu…’akasema hivyo.
‘Akawa anahitajia vitu vya thamani sana…unakumbuka,..kesho yake ukakutana
na jamaa akakuuliza una tatizo gani, ikabidi umwambia ndio akakukumbushia yale
mliyoongea ya kuongeza kipato..ukaona huna jinsi..ukakubali, ukaingia kwenye
mradi..sawa si sawa…’akasema na mpelelezi akabakia ameduwaa.
‘Lakini msharti baba..ukaambiwa nini ..kafara, sasa kubwa
zaidi…ulifanyaje, hapo utajaza mwenyewe,…’akasema docta.
‘What…docta umejua…aje hayo, …docta sikutanii, sasa upo chini ya
ulinzi, sasa nakubali kabisa kuwa wewe umetumwa…sasa sikiliza binti yangu
akiumwa tena, ama zako ama zangu…nimechoka nimechoka, unajua kiasi gani napata
taabu…’akasema sasa akionyesha kuchanganyikiwa, achue hatua kama anavyotaka au
akubaliane na docta.
‘Afande..fanya kazi yako….kama nipo chini ya ulinzi
au…unisikilize…’akasema docta. Na mpelelezi akawa sasa kashika kichwa, na kuna
hisia zinamchezea kichwani, akamuangalia docta na docta akasema;
‘Sasa hivi utapigiwa simu…binti anaumwa,…’akasema docta.
‘Ni kweli huwa nikijisikia hivi, ….haipiti muda…nina shida
docta…’akasema
‘Hahaha….sasa nikuambie ukweli, sijapiga ramli wala nini,…ndivyo
nilivyoambiwa, mimi, kila likitaka
kutokea jambo linalonigusa najiwa na njozi, sijui inakuwaje, hata mimi inafikia
mahali nashindwa kuelewa ni nani huyo ananiambia hayo yote,ndio maana nikaamua
kufanya uchunguzi huu….unielewe hapo, mimi sio mpiga ramli, mimi sio kwamba
napenda haya mambo..lakini kwa vile yanasaidia watu, kwanini nisifanye…’docta
akasema
‘Sasa utanisaidiaje…’akasema mpelelezi, na hapo docta akapumua kimoyo moyo akajua sasa
mtu keshaingia kwenye anga zake…
‘Ni hivi…jana nilijiwa na hiyo njozi..na ikanionyesha tukio lako
lote, tokea ulipohamia hapa…ulihamia hapa na moto mkali sana, maana serikali
ilikuamini, na ukaona hiyo ni sehemu ya kukupandisha daraja,….ukasahau kupiga
hodi..’docta akatabasamu.
‘Bosi wako ukawa unamwambi hiki na kile, lakini bosi wako akawa
hata hakusikilizi….mkawa sasa hamuelewani,
…sijui, nahisi alishayajua mazingiza ya hapa, akaamua kufanya kama
mazingiriza yalivyo,…najua unalifahamu hilo..’docta akasema.
‘Sawa nakuelewa, eleza jinsi gani nitamuokoa binti yangu,
nachanganyikiwa docta, ndio maana hata
kazi nashindwa kufanya, bosi wangu hapa amesha nishtukia, sitaki nikosane naye,
lakini nitafanyaje, hebu fikiria mtoto wako anapoumwa, ..hebu fikiria, mke naye
hamuelewani….aah, hata sijui nikuambieje…’akasema.
‘Kiukweli mke wako walishamteka mapema tu,…huna la kufanya juu
yake…’akasema.
‘What…una sema
nini…’akasema sasa akishika simu.
‘Sio kumteka kumchukua, hapana, walishamweka kwenye mikono yao..si
unajua wakina mama wengine walivyo rahisi kurubuniwa hasa inafikia kwenye mtoto
wake…huyo sasa hivi hata akiambia akumalize anakumaliza..ila nakuomba,
unielewe, usije kulichukulia hili kwa pupa, mke wako ni mwema sana, lakini
keshachoka,..matatizo ya mtoto yamemfika shingoni, sasa atafanyaje…’docta
akatulia
‘Kwahiyo…’akauliza mpelelezi.
‘Kwahiyo ni wewe tu….haya hata mkuu hayajui,..nimekuambia wewe
ili ujua jinsi gani ya kujitoa huko..na kujitoa kwako, ni kushirikiana na…mimi
au mkuu, lakini kwa njia ambayo..hata sijui..maana umeshajiweka kubaya…’akasema
docta.
‘Docta ningelikuwa namfahamu huyo mtu, nakuhakikishia
ningelichukua machine gun, na kwenda
kumiminia risasi,….nimechoka,..lakini nimejitahidi kumtafuta sana, lakini
sijawahi kuonana naye, na wala simjui kabisa…’akasema.
‘Kwa vipi…?’ akauliza docta
‘Ni hivi, …lakini tuyaache hayo, sitaki kumuingiza mtu kwenye
matatizo najua walivyo hao watu…’akasema
‘Mimi nimeshaingia kwenye vita na hao watu,
wananifahamu,…usiogope kuhusu mimi…’akasema docta.
‘Huwa wameshanipa masharti yao,…’akasema
‘Kuwa ukiongea utakufa, au binti yako atakufa,…haya ngoja
tusubirie ufe..’akasema docta.
‘Wewe unafanya mzaha…’akasema mpelelezi.
‘Endelea….’akasema docta.
‘Mimi kwa ujanja wangu wote, ..imefikia sehemu nafuata masharti yao
tu…nimefanya kila niwezalo, …sijampata huyo mtu…wananjia kila mahali, kwenye
facebook, ..nyumbani…yaani kila mahali natembea nao, nimechanganyikiwa docta..kila
ninalolifanya wanalijua….’akasema mpelelezi.
‘Hahaha, kwahiyo hata haya mazungumzo yetu wanayajua…au sio,
ndio wasiwasi wasi wako…’akasema docta na mpelelezi akawa kama anaangalia
hewani.
‘Sijui…’akasema
‘Nakuhakikishia, hapa umefika..hawajui lolote,…viona mbali vyao,
vimegota, haviwezi kuniona mimi kamwe, wanalijua hilo,…sasa hivi wapo matumbo
joto, hawaamini…’akasema docta
‘Kwa vipi…?’ akauliza mpelelezi.
‘Muda sasa umefika wa kulimaliza hilo kundi, najua sio kazi
rahisi, na wewe ndio njia,..unatakiwa ujitolee muhanga kwa ajili ya familia
yako na taifa lako..unielewe vyema, njozi imeniambia hivyo, wewe ndio njia ya
kufika huko kwenye uwanja wa mapambano…msaidizi wangu alikuwa nauli..alikuwa
sehemu ya kunivuta hadi hapa, sasa kazi iliyobakia ni kupitia kwako,…’akasema
docta.
‘Sijui….na sielewi kwa vipi…?’ akauliza
‘Wewe unawasilianaje na hao watu..?’ akaulizwa .
‘Kwa hivi sasa wameshaniondolea vile viona mbali
vyote..hawaniamini tena, ilikuwa kwa simu au kwa ishara, naenda mahali nakutana
nao, napata maagizo..au kupitia kwa binti yangu, wananitesea sana binti
yangu…ndio maana nasema kama ningelijua jinsi ya kumpata huyo mtu…naapa,
ningelimumaliza kwa risasi…’mpelelezi akasema.
‘Hao watu wanajua kuwa wewe ni njia yao ya mafanikio
fulani..njia ya kupata taarifa kutoka huku kwenu, njia ya kuingia kwenye mtando
wa serikali,….unanielewa, wanajua wewe una kipaji fulani…unanielewa, wewe ni
mlenga shabaha mashuhuri unanielewa….’akasema na hapo mpelelezi akashtuka na
kusema;
‘Oh..docta…sijamuua mimi , najua unapotaka kuelekea, hapo
hunipati kamwe..’akasema.
‘Sikiliza, mimi sijasema ni wewe..ila wao wametumia taswira yako
wakaiweka kwa mtu mwingine, na mtu huyo akaweza kulifanya lile jambo, ambao
ulitakiwa wewe ulifanye..uone jinsi hao watu walivyo wa hatari, kwasababu
wameshachukua kivuli chako, taswira yako, akili yako,…wewe hapo ulipo ni mtumwa
wao, kuna kitu wamekupandikizia,…’akasema docta.
‘Kitu gani, na nitafanyaje ili kiondoke…?’ akauliza
‘Ni kweli kuwa wewe ni mlenga shabaha mashuhuri,…kweli si kweli?’
docta akauliza
‘Ni kweli, lakini mimi
sijamuua huyo mtu,…naapa, mimi sijafanya hilo tendo, nimefika pale..unielewe kwa
maagizo, na baadae nikaambiwa utakuja, nifanye moja mbili tatu, ukifika wewe
ndio utaonekana umeua…nikafanya hivyo…na wakati naingia ndani ndio nikasikia
mlio wa risasi , kwa uzoefu wangu nikajua ni nini kimtokea, nikaingia ndani
kama walivyoniagiza, unapofikia kufanya maagizo yao, sijui inakuwaje,..huelewi
kitu…
‘Ehe…nakuelewa ikawaje?’ akauliza.
‘Ndio nikakuta mtu keshadondoka chini, kwa haraka ..unajua tena,
nikafanya walivyotaka, nikatoka nje, lakini nilijua kabisa walivyotaka wao
haiwezekani, …haiji akilini, nilijua utofauti wa bunduki, nilijua swala la
muda..nilijua..kwa mtaalamu atagundua kuwa haiwezekani..lakini wao walitaka iwe
hivyo ningelifanyaje…’akasema.
‘Kwahiyo unakiri kuwa mimi sijaua…?’ akauliza docta.
‘Docta unalijua hilo sana…na unajua kabisa kuwa hiyo ilikuwa ni set up..hata mkuu analijua hilo..lakini
wao wana maana yao, na sijaijua ni ipi…hawafanyi jambo ki..zembe, kila jambo,
unaweza kuliona la makosa lakini wana maana yao kubwa…nimejaribu kuwachunguza
nimeshindwa…na zaidi ni kwasababu wameniweka kwenye ndoana
yao…nimechoka,..nimeshaamua …’akatulia
‘Tulia usiamua vibaya, kujiua ndio lengo lao, …usichukulie pupa, hili jambo linahitajia
umakini wa hali ya juu..niamini mimi,…nimekuwa nikilifuatilia hili jambo hata
kabla, nilioteshwa kuwa atakuja mtu atanionyesha njia,…sasa nimefika sehemu
…natakiwa niimalize hii kazi, …sasa nataka ufanye jambo moja kubwa…’akasema
docta.
‘Jambo gani docta, ila lisiathiri familia yangu,…docta, familia
yangu ni kila kitu, nipo tayari kufa kwa ajili ya familia yangu…’akasema
mpelelezi.
‘Leo, au sijui..utaitwa..utaelekezwa..najua, wanakutafutia
mwanya wa kukumaliza, sasa ni wewe au wao…je utafanyaje, ..mimi sijui..ila
unatakiwa ujitolee mhanga, …usijali athari yake kwako, ..najua unaipenda sana
familia yako, lakini huwezi kuipenda kama bado ipo hatarini…’akasema docta
‘Mimi ninataka wewe uje kukivaa hiki kidude mwilini mwako,..sijui
utafanyaje…wapi ambapo una uhakika hutagundulikana..sijui..nataka nione nyendo
zako,moja hadi mwisho…mengine niachie mimi…’akasema.
Ilikuwa kitu kama unywele mndefu, mpelelezi huyu alishindwa hata
kuelewa, auweke wapi…anajua akiitwa mahali na hao watu, anapekuliwa hadi kwenye
chupi, sasa atafanyaje..
‘Je utaweza hilo, wewe ni mpelelezi, ni askari…una mbinu za kila
aina,…sasa sehemu iliyobakia ni hii kumjua huyo mtu ni nani..tunataka tufike
kwenye makao yao makuu,..tutafikaje, wewe utafikishwa leo,….sasa
tutakupataje…?’ akauliza docta.
‘Hata sijui..anyway, nipo tayari kufa kwa ajili ya familia
yangu, niachie ..nitajua jinsi gani ya kufanya…’akasema
Docta akatoka kitu kwenye vifaa vyake,
‘Nipe kidole chako…’mpelelezi kwa mashaka akanyosha kidole
chake, na docta akamchoma sindano kama zile za kutolea damu kwenye kidole kwa
ajili ya kupima malaria, na mpelelezi akahisi maumivu makali, …na ghafla
akadondoka chini.
Docta akampekua kila
mahali na kuhakikisha hakuna kitu mwilini mwake, na baadae akampigia simu mkuu;
‘Tayari unaweza kuja…’akasema na mara mkuu akafika.
‘Ok, umefanya ulichotaka..?’ akauliza na docta akamuonyesha mpelelezi
aliyekuwa kalala sakafuni, na mkuu akatikisa kichwa kukubali.
‘Sasa huyu mtu ni wetu..watamshuku sana.., na hatujui hatima
yake itakuwaje,..muhimu kwa sasa ni kuweka watu wako tayari…vita imeanza…na
vita hii haihitaji silaha sana ila ikibidi…hasa hapa, ni utaalamu wa kidigitali,
ulichanganyikana na …nguvu za giza…zinaitwa hivyo lakini wenzetu
wameshaziiingiza kwenye mtandao,..’akasema docta.
‘Sasa huyu msaidizi wako yupo wapi..?’ akauliza mkuu.
‘Hata mimi sijui..ila nahisi bado wanamvuta , kama walivyomvuta
binti, nia yao ilikuwa kuwakutanisha, na huyo binti, halafu wanamumaliza....na
ile dhamira yao, ya ..mpenzi wa ….wa mtandao, ikamilike, kuna ka mchezo
wamecheza, ..ni kama majaribio…bado hawajafanikiwa…, ambayo yakifanikiwa,..watu
watakuwa matatani…’akasema docta.
‘Kwa vipi…?’ akauliza
‘Mpenzi wako wa facebook, huyo huyo anaweza kuwa ni adui wako,…Itafikia
muda, tutaogopa hata kugusa mitandao, maana unaweza ukahisi mtu , au
picha,..kumbe sio mtu au picha..taswira zinachukuliwa na kuchezewa kama wanga
wanavyochezea watu usiku…unajua wachawi wanavyofanya kwenye majumba ya watu
usiku, ….sasa hawa wameamua kuyaweka kidigitali..ni hatari, …achana na wazungu
…’akasema docta.
‘Mhh, mimi hayo sielewi…na sitaki kuyaelewa…..naogopa, na
wameanza kunitisha..lakini nimeaga kwetu…’akasema mkuu.
‘Hawajataka tu,… huna nyota ya mambo yao, wanachunguza nyota…na
bahati yamtu, kuna watu wana nyota, nzuri,… na vitu kama hivyo, wakikuona hufai
hawawezi kupoteza muda na wao, ila wakikuona ni mzigo, au ni kikwazo kwao,
watakumaliza, na nahisi mkuu wako alilijua hilo ndio maana akawa hashughuliki nao…’akasema
docta.
‘Achana na mtu huyo…arubaini zake zinakuja…’akasema msaidizi
huyo huku akimuangalia mpelelezi aliyekuwa sasa akizindukana..
*************
Mpelelezi, alisimama kwa haraka na kuhakikisha nguo zake zipo
sawa, akawa kama hajui alipo baadae akasema;
‘Docta umenifanya nini mimi mbona nipo hivi..…?’ akauliza
‘Nimekufanya nini…?’ docta akauliza akionyesha kushangaa..
‘Hata sielewi,…nahisi binti yangu anaumwa..nataka kufika
nyumbani…’akasema mpelelezi akitaka kuondoka, na docta akamuashiria mkuu
amuache tu aondoke,…na mpelelezi akasita halafu akageuka nyuma, na kumuangalia
docta akatikisa kichwa kama kukubali, halafu akamgeukia mkuu wake, na kusema;
‘Mkuu naomba ruhusa nikamuone binti yangu, nilikuambia jinsi
gani anavyoumwa, sasa hisia zinanituma kuwa anaumwa…’akasema
‘Lakini hawajakupigia simu…’akasema mkuu
‘Najua tu…’akasema
‘Ok, unaweza kwenda lakini uwe na tahadhari, nakutegemea sana
wewe …’akasema mkuu.
‘Sawa afande, tupo pamoja…’akasema na kwa haraka akaondoka na
docta na mkuu wakaangaliana bila kusema neno, mkuu akatoka nje akikimbilia ofisini kwake, na docta akaingia kwenye chumb chake na kutoa komputa yake ndogo…
NB: Hii imekaaje!!!, hata sielewi, nasubiria comments zenu kwa wingi…
WAZO LA
LEO: Kila mtu kabarikiwa kipaji chake na muumba wake, wengine hujua
jinsi gani ya kuviendeleza vipaji vyao na kuvifanya mtaji, wengine kama walivyo
wezi, wanaamua kutumia vipaji vya wengine kwa manufaa yao, huo ni wizi , HIYO NI DHULUMA,……kama unajua kipaji cha mtu fulani kinaweza kuzalisha kwanini
usimwambie huyo mtu, mkaja kushirikiana naye ..kitakachopatikana mkatafuta njia ya
kugawana,..Tukumbuke kuwa, siku ya malipo, kila kitu ulichofanya utaulizwa tuweni makini sana.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment