Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, May 11, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-26
‘Binti katoweka…’akasema mpelelezi akimuangaalia mkuu wake na mkuu wake kwa muda huo alikuwa kaduwaa, akiwa bado kashikilia simu mkononi, sijui alikwua akiwaza nini, labda alikuwa akiwaza jinsi taarifa hiyo itakavyofika kwa wazazi wake, na je binti huyo yupo kwenye mikono salama , na cha muhimu kaenda wapi..kaelekea wapi, na kwanini.

‘Atatokaje pale…mlango ni mmoja, walinzi wapo mlangoni, haiwezekani, ni lazima kuna jambo la uzembe limefanyika…, ‘ akasema mkuu kwa hasira.

‘Ni kweli  mkuu…huo ni uzembe…’akasema mpelelezi.

‘Hao walinzi watakuwa wanahusika, natoa amri ukalifanyie kazi hili,, kawaulize, …waseme walikuwa wapi, wakati huyo binti anatoka, nataka kujua ukweli mara moja …’akasema msaidizi wa mkuu kwa amri na mpelelezi akatikia amri ya bosi wake akisema

‘Sawa afande,…’akageuka sasa akitaka kuondoka,… lakini kabla hajaondoka,  docta akasema kwa sauti;

‘La muhimu la kujua  huyo binti kaelekea wapi, huenda katoka kwa nguvu za giza za hao watu, hapo alipo hajijui, sasa hiyo inaweza kuwa ni hatari zaidi, lakini tukumbuke wazazi walitukabidhi huyo mtoto wao wakijua yupo sehemu salama, na kwahiyo ni muhimu sana apatikane kabla wazazi hawajaligundua hilo…’akasema docta.

‘Hahaha unamsikia huyo mtu wako na imani zake, eti nguvu za giza, kwa vipi….Mkuu huyu mtu inabidi umuweke chini ya ulinzi, anaweza kutufanya tukashindwa kufanya kazi yetu kwa imani zake hizo,..halafu umesikia alivyosema, kauli yake ni kama anajua kila kitu…’akasema mpelelezi

‘Kwanini sasa awekwe chini ya ulinzi, sijaelewa hapo…?’ aliyeuliza sasa ni wakili na mkuu akawa kabakia kimia tu.

‘Nyinyi hamlioni hilo eeh..yeye awali ya yote aliweza kuwatoroka walinzi pale aliposhikiliwa hebu muulize yeye aliwatorokaje walinzi ndio hiyo nguvu ya giza alitumia,…au..?,…na hapo hapo, alipotoka, kwa haraka akagundua wapi msaidizi wake alikuwa..nikama vile alipafahamu kabla…, ‘akasema na kabla wakili hajasema kitu yeye akaendelea kuongeaa

‘Na sasa binti katoroka, huyu mtu atajua wapi alipo, hebu atuelezee haraka, ili tusipoteze muda, yupo wapi huyo binti..au lengo lako tuonekane sisi askari hatujui kazi yetu vyema, si ndio lengo lako au?’ akauliza akimgeukia docta.

‘Kwahiyo kwa kusema hivyo , ina maana wewe unaamini hizo nguvu za giza au…?’ akauliza docta na mpelelezi akacheka kwa dharau, na kusema

‘Huyu mtu, ana jambo, inabidi tuwe makini na yeye, na mimi nimeshamuhisi kuwa anaweza kuwa kikwazo kwenye kazi yetu hii kwa kuleta imani zake, zisizofaa, ...na kama ana amini imani zake hizo, kwanini sasa hatuambii wapi huyo binti alipo, eti docta tuambie sasa huyo binti yupo wapi,.., …?’ akamuuliza docta.

‘Mimi nimetoa ushauri wangu tu na wala sijui wapi huyo binti alipo, kutoweka kwake kunanipa shida sana, nikijua kuwa mimi ni mmojawapo niliyewahakikishia hao wazazi kuwa binti yako atakuwa salama...na mimi kusema hivyo, ni sehemu ya ushahuri, , au ina maana mimi siruhusiwi kuongea, ina maana gani sasa, mimi kunishirikisha kwa hili jambo,…’akasema docta.

‘Kiukweli wewe hutufai, na ni vyema, ukawekwa chini ya ulinzi, ili tuweze kuendelea na taratibu zetu, ukiwa mbali na upeo wetu wa macho..., unaweza ukaharibu…mkuu mimi kwa ushauri wangu huyu mtu awepo hapa, au sehemu ambayo hataweza kutoka, mpaka tuimalize hii kazi, mtakuja kunikumbuka kwa hili mkuu…’akasema mpelelezi, huku akijiandaa kuondoka.

‘Lakini mimi sioni umuhimu wa kumweka huyu mtu chini ya ulinzi, yeye tunasaidiana naye au sio…nia ni kuwekeza nguvu kwa pande zote, anachokifahamu yeye, na sisi tukichanganya utaalamu wetu, itakwua rahisi kulishinda hilo kundi,..kama mlivyosema huenda wanatumia nguvu za giza…’akasema wakili.

‘Sikiliza muheshimiwa,…maswala ya nguvu za giza, ni hisia tu,..sisi tunatakiwa tutimize wajibu wetu, tuone kama kweli nguvu za giza zinaweza kutuzuia,..tusiendekeza hayo mambo ya imani zisizokubalika kisheria...’akasema mpelelezi.
‘Kwahiyo hicho kipengele cha kuwa wahalifu hao wanatumia nguvu za giza, kisikuwepo..tusihangaike kwa hilo…tuwekeze kwenye utaalamu wetu wa kawaida, hata tukifungua mashtaka hicho kipengele kiwe kama ‘kusikia tu’ akasema wakili.

‘Kwanza ni nani kaileta hiyo hoja hapa, ..ni huyu huyu docta, ndio maana kwenye kazi yangu mimi sitaki awepo,…anyway, ngojeni nikawajibike…’akasema mpelelezi.

‘Mimi naona tuwe naye, ili tuweze kuangalia na upande huo pia, na kama mpelelezi huamini hayo, kwanini sasa unasema, anajua zaidi…atajuaje zaidi wakati mtu mwenyewe, tupo naye hapa..mimi naona tusaidiane naye na kama anahusika kwa namn moja u nyingine, …ni lazima tutakuja kumgundua au sio mkuu…’akasema wakili

‘Ok, nimewaelewa wote,..ni muhimu kwa sasa tuwe timu moja, mpelelezi wewe wahi kulifuatilia hili swala la kutowekwa kwa huyo binti, kawashughulie hao walinzi, na uwahimize vijana wako na urudi hapa na taarifa kamili..’ akasema mkuu na mpelelezi akawa anaondoka, huku akisema;

‘Ok sir…ila huyu mtu sitaki awe kwenye kazi zangu kama mnamuamini sawa, atawasaidia nyie na imani zake za kishirikina,  lakini sio mimi,…’akasema mpelelezi.

‘Huyu mtu nitamshughulikia mimi mwenyewe, usijali….’ akasema mkuu, na mplelezi akaondoka, …na docta akabakia kimia akisubiria hatua za mkuu huyo.

************

Baadaye wakili akaondoka, baada ya kuongea kidogo na mkuu, msaidizi wa kituo hicho, Baadae ndio  mkuu akamgeukia docta na kusema;

‘Sasa docta sikiliza kwa hali ilivyo, wewe, inabidi ukae hapa, usiondoke kama kuna kazi ya kufanya pamoja, tutaifanya pamoja, umenielewa..haya mengine waachie polisi,..natumai hutaenda kinyume na maagizo yangu tena..?’ akasema mkuu.

‘Hamna shida…’akasema docta na mkuu huyo akatoka huku ;

‘Docta mimi nipo ofisini kwangu , kama kuna lolote usisite kuniambia…’

‘Sawa mkuu…’akasema docta huku akiombea huyo mkuu aondoke haraka kwani kuna zoezi anatakwia kulifanya haraka iwezekanavyo, na hakutaka mtu mwingine afahamu…

Docta alipoona kabakia peke yake, na kwa vile ameshaambiwa yeye hatakiwi kuondoka eneo hilo kwa sasa,…alichofanya yeye ni kuchukua mkoba wake na kuingia kwenye chumba kingine ambacho hakikuwa na mtu,  na alipohakikisha hakuna kitu cha kuweza kumuharibia mambo yake akaitoa komputa yake ndogo , kutoka kwenye mkoba wake.

 Aliiwasha ile komputa yake, baada ya kuhakikisha kuwa hakuna kiambata chochote humo kwenye chumba cha kuweza kunasa matukio humo ndani…, na alipojirisha kwa hilo, ndio akaiwasha komputa yake ndogo, na kuingia sehemu ya video mbashara, humo pia kuna sehemu yake maalum aliyoitayarisha ambayo hunasa matukio kutegemeana na jinsi alivyowekeza vinasa matukio …akaanza kufanya akzi yake huku akiombea awe hajachelewa!

 Na wakati huo huo, mpelelezi alikuwa ameshafika sehemu ya tukio na kukutana na askari ambao walikuwa wakimlinda huyo binti aliyetoweka…, na wale askari walipomuona huyo mkuu wao, wakiwa na wasiwasi wakasema;

‘Mkuu huyu mdada alitoroka kiajabu sana…hata hatuelewi alitokaje humu ndani…’akasema mmojawapo

'Mtanieleza vyema, ilikuwaje?’akauliza mpelelezi akiangalia upande pale mlangoni;

'Afande tulijitahidi kufanya kama  ulivyotuelekeza, na sijui ilikuwaje, tuliposimama mwili ulikuwa kama sio wetu, na….baadaye akili alipokuwa sawa, ndio mwenzangu akaingia ndani, ndio akakuta binti hayupo.

‘Siwaelewi, mlifanya kama nilivyowaelekeza mimi kwa vipi kuwa mlale, kuwa msiwajibike,,….mimi niliwaelekeza nini…?’ akauliza akionyesha mshangao, na hao askari wakawa kama wametahayari, na mmojawapo akasem;

‘Mkuu, sisi tulitii amri yako,kuwa tuhakikishe huyu binti hatoki humu ndani na tulifanya hivyo, hatujui ilikuwaje, ..’akasema mwingine.

‘Hamjui ilikuwaje, kama mlikuwa hapo mlangoni, kwa muda wote…aliwezaje kutoka,..sitaki maneno mengi…?’ akasema mkuu

‘Kama tulivyokueleza mkuu, muda wote tulikuwa hapa mlangoni,..kuna hal ilitutokea, mwili ukawa umelegea, huwezi hata kuinua mkono..mara tukajikuta tumesimama, mwenzangu akageuko huko na mimi huku tukawa tumepeana migongo, na mlango ukafunguka,..huwezi kugeuka, huwezi kutikisika…’akasema askari

‘Hahaha…hivi kweli nyie ni askari..’akasema mpelelezi akiwatolea macho ya hasira

‘Mkuu ni kweli kabisa,…tunahisi kuwa huyo binti alitoka kwa muda huo, na huenda yeey katufanyia kitu au kuna watu wametufanyia hivyo ili huyo binti aweze kutoka…’akasema mwingine

‘Nyie mna wazimu kweli, sasa mtaenda kunyea jela,…mtajua ni nini maana ya ulinzi..na ole wenu muongee kauli kama hiyo isiyoeleweka,…nataka kujua huyo binti akaelekea wapi…kama hamsemi mtakwenda kusemea chumba maalumu , mnafahamu huko kupoje, sawa..’akasema sasa akielekea ndani, hakuwawia sana, akatoka.

'Sasa nyie mnakwenda selo, kama hamuwezi kunieleza huyo binti kaelekea wapi, basi mtakwenda kuelezea huko kwenye mateso,, …’ akasema mpelelezi.

‘Lakini bosi…’wakaanza kulalamika, wakaambulia vibao, na kukalishwa kimia, halafu mpelelezi, akasoogea pembeni na kuchukua simu yake,
.
'Mkuu, ni uzembe umefanyika, sijui..nahisi walipitiwa na usingizi, yaonekana bint ni mjanja sana..aliwapumbaza , sijui na kitu gani…watasema wapi alipo..nakuhakikishia hili…’akasema mpelelezi, akatulia akisikiliza baadae akasema;

 'Sawa mkuu nitawawajibisha, lakini hakikisha huyo docta hatoki hapo maana nimjuavyo anaweza kuharibu hizi harakati zote.. na mkuu keshakupigia simu, alinipigia ndio,…ok, ok, sijaongea naye lolote…ndio nimekeulewa mkuu,  ni lazima kundi hili tulisambaratishwe..’akasema.

 Alipomaliza kuongea hapo , baadae alisogea pembeni, akatoa simu yake maalumu, akaingiza alama za siri, halafu akaongea lugha ya aina isiyo kiingereza au Kiswahili, lakini mwishowe akasema;

 'Wapo njiani, sawa mkuu, …wamalizwe tu..ok’ akarusidha simu yake na kugeuka kuwaangalia hao askari, akasema;

‘Inabidi…kwa uzembe wenu na kushindwa kuzuia midomo yenu, ..sina jinsi, ..’akasema kwa sauti ndogo.

 Mpelelezi huyu, yaonekana kuna kitu kikimsumbua zaidi ya hiyo kazi, akawa anawasiliana na mtu mwingine alipomaliza ndio akawageukia tena hao askari na kusema;

 'Sasa nyie, ok  naawamini maana nyie ni askari siwezi kuwachukua kama wahalifu, na nisingelipenda kuharibu ajira zenu, ingieni kwenye usafiri huo, mimi nitawafuata nyuma kwa bajaji…’akasema.

‘Sawa mkuu…’hao askari wawili wakasema sasa wakionyesha mashaka makubwa.

‘Dereva hakikisha umewafikisha hawa watu kituoni, mimi nawafuata kwa nyuma, hakikisha unapitia njia hii ya mkato…’akasema akionyesha kwa mkono njia hiyo ya mkato.

‘Lakini afande njia hiyo ina makorongo, na ni hatari, gari linaweza kukwama, na lolote linaweza kutokea…’akasema dereva

‘Wewe ndio unapanga…fuata ninachokuambia, nina maana yangu, unanielewa dereva..’akasema mpelelezi.

‘Sawa afande…’akasema dereva.

‘Nazungumza hivyo kwasababu naogopa foleni,…kwa njia hii ya mkato  kama kutakuwa na foleni kwa vile nipo nyuma, nitajua la kufanya…’akasema na dereva akasema;

‘Sawa afande..’akasema

*********

 Wakati hayo yakiendelea mkuu alikuwa naye kwenye chumba chake maalumu, akiangalia komputa yake, kama alivyokuwa akifanya docta…tofauti yake ni kuwa alikuwa akitumia komputa kubwa ya mezani…akiwa amechomeka kifaa chake maalumu ambacho kina nguvu sana ya kunasa matukio.

Mkuu alipohakikisha msafra umeondoka kwenye lile eneo, kwa haraka akatoka nje, na kwa muda huo akakutana na docta naye akitokea nje ya kile chumba.

‘Mkuu, kuna watu wanahitajia msaada wa haraka.., nahisi kuna ambushi …inabidi kuwawahi kabla hawajakutana na hatari…’akasema docta

'Watu gani hao..?’ akauliza mkuu akikunja uso

‘Wale walinzi waliokuwa wakimlinda binti, nahis kuna njama za kuwamaliza…’akasema docta na mkuu kwanza akawa kama anajiuliza ni kwa vipi docta kalipata hilo, akasema;

‘Una uhakika na unachokisema…?’ akauliza mkuu.

‘Yaonekana hivyo, …’akasema docta

‘Lakini mpelelezi yupo huko, na yeye ni mtaalam wa mambo hayo, lakini subiri, nitaongea na dereva, atabadilisha njia…na kwenye huo msafara kuna watu wetu tayari..’akasema mkuu.

'Mkuu usilizarau hili, nina mashaka na mpelelezi, ..’ akasema docta na mkuu akamtupia jicho docta, halafu akasema.

‘Huyo ndivyo alivyo…maneno yake ya awali yasikutie shaka, mimi amjulia, hata hivyo sizani kama ana lolote baya…’akasema mkuu.

Docta alitaka kumuelezea anavyohisi, lakini akaona huo sio muda muafaka, jambo la muhimu kwa hivi sasa ni kuhakikisha hakuna madhara yanayotokea.

‘Sawa mkuu mimi nakuaminia…muhimu hao askari wasije kuingia kwenye mitego ha ya hao watu…’akasema docta

'Docta mm ni mkuu, ndio maana nimeletwa huku, ukiwa na watu kwenye hii kazi kitu cha muhimu ni kuona ni nani na nani yupo na wewe, pili,…utaalamu na elimi uliyo nayo inavyoweza kukusaidia..mimi sijapewa hivyo vyeo bure bure, nimesoma na nimepitia mafunzo yote…’akasema msaidizi wa mkuu.

‘Ok, sawa…naona tusipoteze muda…’akasema docta, na mkuu akatabasamu , huku akiangalia simu yake iliyokuwa ikilia..

‘Ok, sasa ingieni bara bara kuu, msiendelee na bara bara hiyo ya mkato,..’akamuelezea dereva

‘Lakini…bosi ndiye katuelekeza hivyo, na nyuma yetu…’akasema dereva

‘Nisikilize mimi mkuu wako wa kituo, unanielewa, achana na maagizo yake, fuata maagizo yangu,…’akasema mkuu.

‘Sawa mkuu..’akasema dereva na kupindisha gari kwa haraka kuingia bara bara kuu na wakati wanapita ghafla wakaona magari mawili yakigongana, lakini kwa utaalamu wake, akaweza kuipita hiyo ajali kabla hawajazuiwa..na ikawa heri kwo,…

Huku nyuma,…Mpelelezi akaona hiyo hali ya dereva kutoka kufuata masharti yake ya kupitia njia ya mkato, na tendo hilo lilimkwanza , na kwa muda ule simu yake ya dharura ilikuwa ikiita, na alishajua ni kwanini anapigiwa, …

‘Hawa watu wameharibu…’akasema mpelelezi, na kosa la namna hiyo linaweza kumharimu, hapo akahisi hatari inayomkabili, hata hivyo, inabidi kutafuta njia nyingine mbadala, akikumbuka amri aliyopewa

‘Hakikisha hao watu hawafungui mdomo wao, na wakifungua mdomo wao wakaelezea …ujue sisi tutaifunga mdomo wako milele..’sauti hiyo ilimfanya mpelelezi ahisi matumbo yake yakimcheza- cheza,..akijua sasa hivi hata yeye yupo hatarini..

NB: Najua sehemu hiyo itakuwa haieleweki , haipo wazi …, hata mimi imenisumbua kidogo, lakini ndivyo ilivyokuwa na baadae utakuja kuelewa zaidi huko mbele.


WAZO  LA LEO: Uwongo mwingi, na kujifanya mjanja kuhadaa wengine, ukachuma jasho lisilo halali yako, kwa hadaa kugushi, veti bandia nk.., ukajijenga, nk..lkn ukumbuke mungu yupo anayaona yote hayo, na ukumbuke kuwa hayo unayoyafanya yanaumiza wengine, je wao hawana haki…je wao hawaumii, je wao hawamuombi mungu wao,..basi ni bora ukaanza kubadilika, ukatubu kabla siku haijafika, siku ambayo uovu wako, hadaa, nk..vitajulikana,.. 
Ni mimi: emu-three

No comments :