Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, April 15, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-6


 Mpenzi wangu niliyempata kwenye facebook,  , ndiye aliyenifanya nifikie hatua ya kuchanganyikiwa, ...sasa sijui ni kwasababu ya jinsi watu wanavyosema kuwa yeye sio mtu, mimi sikukubaliana na hilo, wengi waliniona ni mbishi, lakini nilikuwa na sababu zangu muhimu....je sababu hizo zitanisaidia au zitanitia matatani...

Na kwasababu hiyo docta mmoja aliyejitolea kunisaidia, akakubali tufunge safari hadi kuja huku dar, kwani hata yeye katika jinsi ya kutibia wagonjwa wake wenye matatizo hayo, yeye hupendelea zaidi kutafuta kiini cha tatizo,....

'Matatizo mengine kama haya, huwezi kuyatibia juu kwa juu, maana matatizo haya ni kama mti, ukiamua kukata matawi tu, ukiwa na maana ya kuua huo mti, miti mingine huchipua tena, ina maana haya mamatizo yanaweza kutokea tena, ni bora utafute asili yake, ili kesho na kesho kutwa yasije kurudia tena, au kumtokea mtu katika familia...'alisema docta

Ndio maana tukaandamana na huyo docta, kutoka huko mikoani hadi ndani ya jiji hili la dar, sehemu ambyo tatizo langu lilianzia,....mkumbuke tatizo hilo lilianzia ndani ya facebook, pale nilipompata mpenzi, kutoka kwenye marafiki wa facebook,  na nikaona yeye ni sahihi kwangu, simjui..sijui wapi anapotokea, ..sasa ndio ikafikia hatua hiyo ya kutaka kumjua, na wapi anatokea...

Hapo ndio nikavumbua matatizo makubwa, ..je ni matatizo tu au yana sababu za msingi, 

Tuendelee na kisa hiki...

***********

Ili kupata chanzo cha tatizo langu, ilibidi tufunge safari kutoka huko mikoani nilipokuwa natibia kienyeji na kuja tena huku Dar,...

Tukiwa tupo ndani ya daladala,hatukuweza kuongea sana, ila tulipoteremka, huku tunatembea, docta akawa ananihoji kuhusu huko tunapokwenda, kiukweli sikuwa na uhakika kuwa kweli tutawakuta hao wenyeji wetu maana kipindi hicho walikuwa wakiishi kwenye nyumba ya kupanga,…na ukumbuke dhumuni la kwenda huko ni kuhakiki tu, hakuna uhakika kuwa labda ndio sababu japokuwa docta alisisitiza kuwa tatizo ndio limeanzia hapo…

‘Inawezekana walishahama, kwasababu kipindi hicho walikuwa wakiishi kwenye nyumba ya kupanga,…na sisi tulikuwa tumepanga nyumba ya jirani na kwao,..baadae sisi tukahamia kwenye nyumba yetu,…mimi nilikuwa nawasiliana na huyo binti..mara kwa mara …si unajua tena docta…’ nikatulia

‘Mimi sijui…..nikuulize tu, huyo binti hakuweza kukuambia kama walihama au la, na kama wamehama walihamia wapi? Au labda wao walikuja kuhama kipindi wewe na yeye mumeshavunja mahusiano..?’ akaniuliza.

‘Mawasiliano yetu mara nyingi yalikuwa kwenye simu, na kukutana kwetu ilikuwa mjini…akiwa anakwenda kusoma kozi aliyokuwa akisomea, basi mimi nampitia, tunaongea,…namkaribisha chakula , siku nyingine anagoma, siku nyingine anakubali..ndio hivyo …’nikasema.

‘Ndio hivyo tu maana yake nini…ina maana wewe na yeye…mliishia hivyo tu…ongea kiukweli, hapa sio sehemu ya kufichana tena, maana huko tunapokwenda huenda ukazua kesi, kuna dalili mbaya, na dalili hiyo inaweza ikawa ndio sababu ya haya yote…’akasema docta.

‘Kesi ya nini docta, miaka yote hiyo hawajawahi kunitafuta docta…,ina maana mimi kujitokeza ndio iwe kesi..haiwezekani docta…, hata hivyo, ni mambo ya kawaida, unajua tena ujana,…kiukweli alinisumbua sana huyo binti…, mpaka nakuja kumweka sawa, haikuwa kazi rahisi, tofauti na walivyokuwa wasichana wengine, wasichana walikuwa wakinipapatikia, we acha docta, kama isingelikuwa kubadilika na kuwa mcha mungu, ningeliishia kubaya….’nikasema.

‘Kwahiyo ulikuja ukatembea naye au sio,…na wakati huo mumeshakubaliana kuwa wewe ni mchumba wake, au sio..hebu niambie hapo ilikuwaje, maana unasema mpaka anakubali ulisumbuka sana…kukubali kwa vipi, kuwa mchumba au kutimiza matamanio yako?’ akauliza docta.

‘Docta, hayo tuachane nayo…kwani yatasaidia nini , kwanza huenda sio huyo unayemfikiria kama ni yeye kwanini nisimkumbuke,....sura yake sio yeye docta...’nikasema na kutulia docta akanipiga piga begani huku tunatembea, akasema.

‘Hayo hatuwezi kuachana nayo, unasikia, kama unataka nikusaidie, wakati ndio huu..vinginevyo, mimi nafanya nini…’akasema docta.

‘Ni kweli docta, huyo msichana alinisumbua sana,…ndio alikuwa anavutia sana kipindi cha awali, kipindi kile anachipukia, akawa anaonekana mrembo sana, umbo la kuvutia, si akina dada wengi huwa hivyo kipindi kama hicho …lakini baadae aah, nilimuona wa kawaida tu, kumbe sivyo kama nilivyokuwa nawazia, nikaona kumbe wapo wengi zaidi yake…ndio nikaamua niachane naye, sasa kumbe yeye alishajua nimeamua yeye aje kuwa mke wangu…’akasema.

‘Sijakuelewa…ina maana hukuwa na lengo la kumuoa…kwanini yeye ajue hivyo kuwa atakuwa mke wako, ina maana hukuwahi kumtamkia hivyo?’ akauliza.

‘Awali wakati nahangaika kumpata, oh, docta bwana,…unajua docta, muda ule ningeoa ningeliishije na yeye,…ndio naanza kujitegemea, japokuwa kwetu tulikuwa na uwezo lakini nisingelioa kuja kuwatwika wazee wangu mzigo..unielewe hapo docta, sikufanya hivyo kwa ubishi tu, au roho mbaya…’akasema.

‘Kama ulilijua hilo, kwanini ukakimbilia, mambo hayo ya ndoa wakati hujajipanga…?’ docta akuliza

‘Oh, docta,…unajua usilinganishe wakati wenu na wetu…siku zetu huwezi ukaoa bila kujuana na msichana, mkazoeana naye ..mkatembea naye, ndio maisha ya karne yetu, sio kwamba nayapenda kwa hivi sasa akili imeshapevuka, naona ni makosa lakini kwa muda huo nilijua ndio maisha yalivyo…’nikasema.

‘Kwahiyo mlikuwaje, hebu niambia hicho kisasa, wewe na yeye ilikuwaje…mligombana au kwanini mliachana?’ docta akauliza.

‘Yeye siku hiyo alikuja, anadai nimuoe…sikutaka hata kumsikiliza, kwanza nilishaona hana lolote,…halafu docta ni kipindi kile akili haijakomaa, akili imekuja kukomaa miaka hii ya karibuni,..nilipotulia na kujitambua, nikaona kweli nahitaji muda, na kama ni kuoa, basi, nahitajika kumtafuta mke wa aina yangu…yeye hakuwa hivyo, mshamba mshamba tu…ni kitu kama hicho…nasema hivyo jinsi nilivyokuwa naona, natumia lugha hayo kwa jinsi nilivyokuwa naona, …sio kwamba namkashifu docta, unielewe hapo…’nikasema.

‘Kwanini alikuja kukuambia anataka umuoe…?’ akauliza.

‘Sijui, maana awali alikuwa anaringa, mpaka nilimpopata, tatizo yeye alikuwa wakati mbaya,, alikuja mida ya asubuhi, na begi lake la nguo, utafikiri anahamia, mimi nikamfukuza ….’nikasita kuongea.

'Kwanini ulimfukuza wakati alikuwa mpenzi wako , na sio mpenzi tu mchumba wako au sio..?' akauliza docta, hapo nikabakia kimia na docta akasema;

‘Ulikuwa na msichana mwingine..au sio?’ akauliza.

‘Kiukweli kwa kipindi kile nakubali nilikuwa sijatulia, lakini sio sasa,..nilikuwa nimeshatafuta msichana mwingine , alikuwa mkali, we acha tu,…na nilishaona huyo anaendana na mimi,..lakini ni kwa muda huo docta unielewe hapo, maana hata huyo msichana baadae tulikosana naye, hakuwa ametulia,..ndio baadae nikaamua bora niwe Single…’nikasema.

‘Oh, kwahiyo wewe una wengi mliokosana nao, wengi uliotembea nao na kuwaacha, ….?’ Akauliza.

‘Ndio…lakini sio wengi kivile... , ni watatu tu wa kiasi hicho....wengine sio wa kudumu kihivyo, ila ambaye nilifikia hatua hiyo , na hata kukubaliana naye kuwa atakuwa mke wangu ni huyo mmoja, hawa wengine wawili, hatukuwa tumefikia hapo,…wanajua, na hata leo nakutana nao, wameshaolewa…’nikasema.

‘Huyo uliyemuacha, katika kupendana kwenu ina maana wewe na yeye mlifikia hatua hiyo, ya kukubaliana kuwa muwe wachumba, mkaweka ahadi ya mafungamano kuwa mtaoana, mliwahi kufanya chochote cha kulithibitisha hilo, labda kwa wazazi, kwa marafiki…au hata yeye ulikuwa urafiki wa tamaa za kimwili tu..?’ akaulizwa.

‘Kiukweli docta, juhudi za kumpata huyo msichana zilifikia huko…siku moja ndio nikatafuta pete, nikanunua zawadi..yaani niligharamika sana siku hiyo, nikawaalika baadhi ya marafiki zangu tunaojuana pamoja, walijua, yaweza au isiweze…kuja kuoana…, maana hata wao walikuwa wakitumia mbinu hizo…basi, siku hiyo nikaamualika,…’

‘Mbinu hizo,…hebu fafanua hapo…’akasema docta lakini  kwa bahati mbaya, hatukuweza kuendelea kuongea kwani, tulikuwa tumeshafika kwenye nyumba na kabla hatuja kaa sawa mwenye hiyo nyumba akajitokeza

**********

‘Ndio hapa…..’nikasema

Pale mlangoni alikuwa kasimama mzee mmoja alionekana kama katoka kalala,  kwani alitoka huku anajinyosha nyosha…

‘Oh, unajua sijui kwanini kila nikitaka kutoka nahisi mwili mnzito, na kawaida yangu ikitokea hivyo ni lazima kutatokea ugeni, sasa sijui kama nyie ni wageni wangu au ni hisia tu…’akasema.

‘Shikamoo mzee…’mimi nikasalimia nilishamkumbuka huyo mzee alikuwa mwenye nyumba hiyo ambayo walipanga wazazi wa huyo binti ninayemfahamu.

‘Ni kweli sisi ni wageni wako, lakini tunaulizia tu, kuna mpangaji wako mmoja, sijui kama yupo hapa, …anaitwa Mashauri…’nikasema.

‘Oh, huyo aliondoka siku nyingi sana..Mashauri alikuwa mpangaji wangu wa muda mrefu, akajenga nyumba yake huko nje ya mji…, akahamia, nilimkosa sana … ni siku nyingi sana, …’akasema.

‘Oh , tulikuwa tunamtafuta yeye, sasa tunawezaje kumpata…?’ akauliza docta.

‘Kumpata mhh , kiukweli awali nilikuwa na wasiliana naye, lakini alipokutwa na matatizo, sijaweza kufahamu wapi amehamia kwa hivi sasa….dunia hii ina mitihani,..nilimuonea huruma sana….’akasema.

‘Mitihani gani tena…?’ nikauliza nikiwa hamasa kujua.

‘Mhh…mambo mengine hata kuongea inakuwa taabu, kwanza samahani niwajue nyie ni nani…?’ akauliza.

‘Mzee ina maana mimi hunikumbuki…?’ nikamuuliza na huyo mzee akanitizama kwa makini halafu akatabasamu, na kusema;

‘Sura kama naikumbuka vile…, ….nikumbushe kidogo, halafu ghafla akasema;

‘Ndio..nimekukumbuka,…sasa hivi umekuwa mtu mnzima sasa, duuh, wewe ulikuwa unagombana gombana na mtoto wangu , hahaha nimeshakukumbuka,….nahisi sasa umeshaoa maana mwenzako sasa ana watoto ana nyumba yake, katulia , sio yule wa kipindi kile …, una watoto wangapi..unajua mliondoka muda mrefu sana,….karibuni ndani …’akasema.

‘Hapana mzee, hatuwezi kukaa, maana shida yetu kubwa ni kuonana na hiyo familia.…’akasema docta.

 ‘Oh, hiyo familia ilihama muda , kitambo sana,…na mengi yametokea, sasa sijui niwasaidieje…’akasema.

‘Utuelekeze tu, huko walipohamia, tuna hamu sana ya kuonana na hiyo familia….’akasema docta, na mzee huyo akanitupia jicho, kama anataka kuuliza jambo, halafu akasema;

‘Nijuavyo mimi, ….sina hakika huko walipohamia baadae…, ila mkifika sehemu ambayo walijenga awali , na hata jingo lao bado lipo, limebakia kama gofu, kuna mpangaji mmoja tu bado yupo pale, wa siku nyingi, …yeye anaweza kuwalekeza wapi walipohamia hao watu.

‘Kwanini unasema gofu…?’ nikauliza.

‘Waliamua kuitekeleza kabisa hiyo nyumba, ni kutokana na matatizo waliyokumbana nayo..lakini muhimu mfike huko mtaelekewa wapi walipohamia, au sio…’akasema.

‘Ni wapi huko…?’ nikauliza.

‘Ni njia hiyo ya kuelekea Mkuranga, kabla hujatoka mji wa dar, kuna kijiji kimoja maarufu….’akakitaja.

‘Ehee…’nikaitikia nikiwa na hamasa.

‘Ukifika pale kuna eneo linalojulikana kama Makaburini….’aliposema hivyo, nikahisi mwili ukinisisimuka, hali kama ya uwoga uwoga ikaanza kuniingia.

‘Makaburini…?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Ndio unapafahamu sio basi mkifika huko mtaulizia nyumba ya Mashauri,..’ akasema.

‘Oh…..’nikatikisa kichwa, halafu nikamuangalia docta, nikisema;

‘Umeona docta, kumbe alikosea tu kunielekeza, nahisi labda ni sababu ya hayo matatizo…hakuna baya hapo, tukipata maelekezo mazuri tutafika na tutaonana na huyo binti…’nikasema na mara huyo mzee akasema.

‘Binti yupi huyo,….?’ Akauliza

‘Yule binti yake wa kwanza….’nikasema.

‘Kama ni huyo binti, alikuwa anaitwa Maua, au sio ndiye mnayemtafuta kwani hamna habari…’akasema.

‘Habari gani…?’ akauliza docta, na mimi hapo, nikaanza kuingiwa na wasiwasi.

‘Kama ni huyo binti mbona ni marehemu….alifariki muda sasa….walipohamia huko, kulipita kitambo,..na yakatokea yaliyotokea,…siwezi kusema zaidi, ila kwa sasa huyo binti hayupo duniani…’akasemaa na mimi nilibakiaa nimeshikwa na kitu kama ganzi

‘Unasema….?’ Nikaweza kusema hivyo, na docta sasa akaanza kuongea

‘Hebu samahani kidogo, utusaidie hapo, ilitokeaje, maana yaonekana kama kuna tukio lilitokea lislo la kawaida, au sio,..kama hutojali lakini….?’ Akauliza na yule mzee akamuangalia sana docta na baadae akasema.

‘Nahisi wewe ni dakitari…’akasema

‘Ndio…’akasema docta

‘Nilishawahi kukuona mahali ‘akasema huyo mzee

‘Yawezekana,…sisi kiukweli lengo letu ni kukutana na hiyo familia, lakini labda unaweza kutusaidia jambo moja , mimi ni dakitari na huwa nafanya uchunguzi mbali mbali, na kijana wako hapa, kama ulivyosema unamfahamu anataka kujifunza mambo…sasa kuna kazi waliwahi kuifanya yeye na huyo binti, ya kimasomo, sasa aliniambia tukikutana naye ataipata,..’akasema docta

‘Ndio hivyo, huyo binti hayupo tena duniani , japokuwa hawakutaka kusema sana, binti huyo alijiua….'akasema

'Alijiua...kwanini?'nikasema na kujiuliza

'Kwanini ni kitendawili,...na kiukweli Mashauri, ana hasira sana siku zote tukiliongelea hilo, kipindi hicho aliahidi aliyemfanyia binti yake hivyo ama zake ama za huyo mtu...walimtafuta huyo mtu sizani kama waliwahi kumpata,...'akasema

'Haiwezekani kwani hakuna aliyekua akimfahamu mchumba au rafiki wa huyo binti...?' akauliza docta.

'Huyo binti alikuwa mtoto wa getini, wanachungwa kweli kweli, mimi niliahi kumuangalia rafiki yangu huyo watoto haachungwi hivyo, sasa...ndio ni wajibu kufanya hivyo, ila yule alizidi, ndio maana hawakutaka hata kuliweka wazi hilo tukio, unajua watoto walivyokuwa wakimuogopa baba yao,....huwezi amini,...na hata hivyo huyo binti mwenyewe alikuwa mpole sana, ana tabia nzuri, hana tabia hata ya uhuni,...sijui huyo mwanaume aliwezaje kumpata, lakini ndio , sisi wanaume ni wajanja sana....'akasema.

'Sasa kwanini asema hivyo, .....kuwa ama zake ama za huyo mtu...?' akauliza docta.

'Anasema huyo mwanaume ndiye aliyemsababishia binti yake kujiua....japokuwa mpaka huyo binti anafariki hakukuweza kuusema ukweli..., ila nina wasiwasi sana, ni bora tu huyo mwanaume asijitokeze,..kuna mambo yamejificha humo wenyewe hawataki kuyasema, mpaka wanakimbia hiyo nyumba,...mimi sijui,  .’akasema.

'Mamama....sasa hilo balaa...'nikasema nikigeuka nyuma kuangalia, maana huko sasa hakuendeki

‘Sasa unasema alijia, kwasababu gani ya msingi labda....kama unaweza kujua..?’ akauliza docta.

‘Kama nilivyosema, awali  watu hao nilikuwa nao karibu sana, kwahiyo tulikuwa tunatembeleana, unajua kuna kijana wangu alitaka kumuoa huyo binti, lakini huyo binti akagoma akasema anaye mchumba wake tayari,walishaahidina naye..,basi kijana wangu akapata mchumba mwingine…..sasa ikawa kila anayekwenda hapo inakuwa hivyo siku zinakwenda…

‘Siku moja nikaamuuliza baba  yake huyo binti, kwanini binti yake anaikataa bahati, maana wanaume wanaokuja kumposa sio mchezo, ni watu wenye hadhi zao,..achilia mbali kijana wangu, baba yake akasema hata yeye hafahamu huyo mwanaume ni nani…

‘Haijapita muda,nikasikia huyo binti kanywa sumu….kakimbizwa hospitalini, ikawa ndio kwaheri, kuchunguzwa zaidi kumbe alikuwa na mimba…’mimi nikakatiza kwa kusema.

‘Alikuwa na mimba,….ooh…’nikasema kwa mshangao.

‘Ndio lakini hilo limekuwa siri ya familia wengi hawalijui hilo…’akasema mzee.

‘Labda nikuulize tu swali moja, maana ukiwa docta unakuwa mdadisi sana, alipofariki huyo binti ndio matatizo yakaanza, na walizikia, wapi..?’ docta akauliza.

‘Ndio , kiukweli matatizo ya hiyo familia chanzo kikubwa ni kufariki kwa huyo binti, na walizika sehemu hiyo hiyo maana walikuwa wamejenga sio mbali sana na sehemu ya makaburi..

‘Sehemu hiyo ya makaburi inatambulikanaje…?’ akauliza docta.

‘Unajua eneo hilo linatambulikana kutokana na hayo makaburi, panaitwa Makaburini,… kuna eneo kubwa la makaburi, …na uzuri wake kaburi hilo walilijengea vizuri sana huwezi hata kulikosea…walikuwa wanampenda sana binti yao...’akasama.

'Kwani alikuwa na watoto wangapi..?' akauliza docta.

'Wawili tu...huyo mwingine naye..ooh, ..alikuja kupata ajali mbaya sana, siku hiyo aliposikia dada yake kafariki.....' akasema

Hapo hapo nikahisi kitu kama kizungu zungu…

NB: niishie hapa kwa leo, mnasemaje


WAZO LA LEO: Kuna mambo mengine kwenye maisha yetu hasa kwenye jamii, hayahitajiki kubadilika kwasabau ya wakati, huwezi kusema kutokana na wakati, basi na tabia hizo zibadilike…, kubadili tabia hizo, maana yake ni kuharibu mustakabali wa jamii,..jamii yetu hivi sasa inakengeuka, maadili mema, nidhamu, na kumcha mungu vinabadilika, ukiiliza, jibu ni kwenda na wakati. Je huko kwenda na wakati kunaboresha au kunaharibu, tujiulize sote huku tukiangalia matokea yake kwenye jamii zetu. Tumuombe mungu tu atusaidie kwani huu ni mtihani mkubwa.
Ni mimi: emu-three

No comments :