Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, March 4, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-9


Kikao kilielekea kuvurugika

…mama anataka kuondoka, na mkwewe, …mke wa Soldier, na baba mwenye nyumba akasema;

‘Kama mnataka kuondoka muondoke, lakini mjue mnavunja sharti za ndoa, hapa tunataka kusuluhisha haya mambo nyie mnaondoka,mnadharau kikao, ukinidharau mimi mume wako sio mbaya, lakni unawadharau wanafamilia,…hamuoni pia kwa kufanya hivyo mnahalifu hata mungu…kaeni tuoni tatizo lipo wapi, kama mimi ni mkosaji si tutaona , kwanini mnakimbilia kuondoka, eeh,  …’akasema

‘Mimi nitakaa kwa ajili ya mwanangu, najua naye ana haki ya kufahamu kilichotokea…haya ya mimi na wewe, sizani kama yana ufumbuzi…najua umeshanichoka,…nina nini tena na uzee huu, hata nikiondoka kwako ni sawa tu, nyie msiozeeka,..lakini tukumbuke kila jambo lina mwanzo na mwisho wake..’akasema mama.

‘Hayo unasema wewe, labda ni wewe ni umenichoka, lakini mimi sijasema hilo, mimi bado nakupenda sana mke wangu, sitaweza kusema hilo maana abadani,...na umri huu tena tumetoka mbali mke wangu,,…sielewi kwanini usiniamini…’akasema baba mtu.

‘Kamwe, mimi siwezi kukuamini wewe tena, kipimo chako cha mwisho kilikuwa leo…

Tuendelee na kisa chetu….

****************

 Mama akarudi kwenye kiti chake, halikadhalika mke wa Soldier, na mara Soldier, akasimama na kwenda kwa mama yake na akawa anamnong’oneza kitu wakawa wanaongea kwa sauti ndogo, waliongea kwa muda..na watu wote mle ndani wakawa kimia, wakiwasubiria wao wamalize kuongea,.., halafu mama akatikisa kichwa kukubali,…

‘Sasa ni hivi, baba, na mama, na wajumbe wote mliohudhuria hapa..mimi nimekuja na wazo moja..kuhusu matatizo ya baba na mama, nimeona tuyatatue haya kwanza maana yao ni muhimu kuliko matatizo yangu…’

‘Wengi mtashangaa nikisema na mimi nina matatizo yangu…ni kweli nina duku duku kujua mtoto, huyo mdogo, …mkumbuke huko nimekaaa miaka mitatu, nilitarajjia kumkuta mtoto wa miaka miwili hivi, lakini sasa, ok…hayo ya kwangu kwanza tuyaache…’akatulia.

‘Tuyaongee hayo ya kwako kwanza…’akasema mama yake

‘Hapana mama,..ngoja tulimalize matatizo yenu kwanza , huenda litaleta tija, na kusawizisha hilo la kwangu..’akasema Soldier

‘Haya, ongea wazo lako, tunakusiliza..’akasema mzee mualikwa

‘Ni hivi, …mama mpaka sasa hajakubali kuwa Dereva sio mtoto wa baba, hata bada ya vipimo hivyo vya DNA test , maana waliopima walifanya wakiwa peke yao..mama anasema ana ushahidi kuwa baba ana mahusiano na mama yake dereva,..tuache hilo la mahusiano kwanza, mimi nina wazo kuhusu mtoto yaani Dereva…’akatulia

‘Nitampigia simu wakili wetu wa kazini, nataka yeye aje atusaidie maswala haya ya kifamilia, uzuri wake anaishi huku kwetu…namuamini, ni mwanasheria mzuri, na ni mtu mnzuri sana serikalin….’akatulia

‘Wazo langu ni hili…baba na mama yake dereva wote wamakiri kuwa mtoto sio damu yetu, ina maana kuwa hatahusikana na lolote kuhusu familia hii zaidi ya msaada wa kibinadamu..na kwahiyo sisi kama familia tunataka hilo litambulikane kisheria, ili kesho na kesho kutwa tusije kurukana..nayasema haya kwa nia njema sio kwamba nimesahau ushirikiano wetu wa kabla, maana sisi tulishakuwa kama ndugu….’kabla hajamaliza baba akadakia.

‘Sikiliza wewe mtoto, maswala ya mali, maswala ya urithi mwenye mamlaka ni mimi, nina hiari ya kufanya nitakavyo, mali na ..chochote nilichowahi kuchuma, ni vyangu…’Solder akataka kumkatiza lakini baba akamuashiria kwa mkono atulie

‘Mimi...nimeshafahamu wapi unapoelekea, kwahiyo hilo halina maana, ilimradi mimi nipo hai, naweza kuandika mirathi nitakavyo mimi…labda nifariki kabla sijaandika mirathi…na …sijui kwanini unakuja na wazo kama hilo na kitu kisichikuwa chako…’akasema baba.

‘Baba…nazungumza hili kwa nia njema, moja ya mambo yanayomtesa mama, ni kutokana na uhalisia wa maisha, haya tunaweza kuyaona sasa hivi ni mambo ya kawaida tu…, lakini yamekuja kuleta shida kwenye familia nyingi tu, nyie wenyewe ni mashahidi, baba umekuwa ukipambana na hizo kesi nyingi tu, mzazi hasa baba anapofariki,..watoto wa nje hujitokeza baadae wakidai haki ..kuwa na wao ni miongoni mwa wanafamilia, na mila zetu zinawatambua..’akatulia

‘Kwahiyo ushaanza kujipangia au sio….?’ Akauliza baba.

‘Baba naomba unipe nafasi kidogo…..Sasa kwa vile wewe baba umesema dereva sio mwanao…na halikadhalika mama yake naye kasema mtoto wake sio damu yako,..mimi sioni kwanini mlipinge hili…wazo langu ni kuwa, mwanasheria aje hapa aandikishe hilo, kuwa kutokana na kikao hiki , na vielelezo vya DNA, …na akiwemo docta aliyevithibitisha kuwa ni sahihi, dereva sio mtoto wa baba,..na hana haki za kisheria kama mtoto wa familia, …na mungu nishahidi..mama alitaka tumuite na mtu wa dini, kuwe na viapo…’akatulia

Baba akawa kashika kichwa kama anawaza, na mama yake Dereva akawa anamuangalia mwanae, ni kama kahisi kitu kwa mwanae, lakini hakusema neno…

‘Tukilimaliza hili, mama kasema atafikiria kuendelea kuwepo, maana atakuwa na amani japo kidogo…ataongezea ya kwake ya kindoa, kuwa kama baba ataendelea na mapenzi na mama yake dereva, basi ……’akasema na kabla hajamaliza baba akamkatiza na kusema;

‘Hapo siwezi kukubaliana nanyi, hamjui wapi tulipotoka na marehemu, sisi ni ndugu tulioivana na tulikubaliana na marehemu, maana aliumwa na mimi nilikuwa bega kwa bega ni kimuuguza, ..inanisikitisha sana kuwaimefikia hapa..hamuelewi tu jinsi gani niliivana na marahemu.

‘Tulikubaliana kama lolote likitokea mmoja awe mlezi wa familia nyingine,..aibebe ile familia kama yake,sasa nyie..nashanga hata mke wangu unalisahau hilo…yaani wewe upo radhi tuvunje kile kiapo tulikipa mbele ya marehemu,..hapana hilo mimi siwezi kulifanya , abadani…’akasema baba

‘Haya kama hutaki mchukue huyo mwanamke wako, muoane kabisa, ili ijulikane kuwa katika hicho kiapo marahemu alikuambia uichukue familia na mke, ….hilo mimi sikuwahi kulisikia kutoka kwa marehemu..labda kama mliongea pembeni…’akasema mama

‘Mama Soldier….mbona unasahau, upendo wenu mliokuwa nao…kwanini unarudi nyuma, hebu tumuogope mungu,..kafariki yule, ni kutangulia tu mbele ya haki, ninaweza hata mimi kufariki, haya ya kakukuta,...huyo mama hapo ni mjane anahitajia faraja zetu, hasa kutoka kwetu, kwanini mke wangu unsahau..’akasema baba

‘Kama ingelikuwa ni hivyo unavyosema nisingelikuwa na kikwazo, kama ingelikuwa ni dini inavyosema, kuwajali wajane,…nisingelikuwa na kikwazo, lakini sivyo unavyomaanisha wewe, wewe unataka kurahisisha mambo yako tu, …ili uweze kufanikisha mambo yako..na unajua kabisa kuwa mtoto huyo ni damu yako,…. na kwa vile mna ahadi zenu wawili za mapenzi ya siri…nina ushahidi wa hayo, lakini kwa leo siwezi kuutoa,..nataka kwanza mjifunge wenyewe, kwa mungu na kwa hiyo hati ya wakili,..’akasema mama

‘Una ushahdi gani wewe mke wangu, hebu …utoe sasa hivi ili tuyamalize haya mambo,..hivi niwaulize jamani, ..kuna ushahidi gani zaidi wa kuhalalisha kuwa huyu ni mtoto wangu zaidi ya DNA, mke wangu unakifahamu hicho kipimo kweli, muulize jamaa yenu huyo docta…’akasema baba mtu.

‘Muulize baba yako lile swali…?’ akasema mama akimuangalia mtoto wake.

‘Kwanza baba hebu niulize,..ulipimia wapi hicho kipimo..?’ akauliza Soldier

‘Kila kitu kimeandikwa hapo kwenye hiyo karatasi,..si unajua kusoma, au akusaidie docta, na nashangaa sana,..naona unaanza na wewe kunishuku kuwa baba yako ni muongo au sio..mwanangu uwe makini sana, nilikuamini sana, lakini leo umenivunja nguvu…’akasema

‘Baba mimi ninachopigiana hapa ni ndoa yenu, sitafurahi mkikosana na mama, sitafurahi kuingie mdudu mtu kwenye ndoa yenu, …nitalipigania hilo kwa nguvu zangu zote,kama kuna watu wanafikiri wataingia ndani ya ndoa yenu na kuivuruga,..hawatafanikiwa, hilo baba nakuahidi…uwe hai au umefariki nitailinda ndoa yenu na mali zenu…’akasema Soldier kwa ujasiria.

‘Una maana gani kusema hivyo..?’ akauliza mama wa dereva

‘Hiyo imeeleweka, alivyosema mwanangu ni sahihi, yeye kama mtoto wa kwanza wa familia hii, namuunga mkono kabisa..’akasema mama wa Soldier.

‘Hahaha..hivi nyie mnatuonaje sisi, kuwa sisi tumekuja hapa kutaka kuwaingilia, kwa lipi..ndio sina mume, lakini sio kwamba nimekuwa kilema au…muuza mwili,..nawaona watu wa ajabu sana, sasa ni hivi kama kuna haki za mtoto wangu zitalindwa, kwa njia yoyote ile, kama nipo hai, na huyo wakili wenu muiteni, na mimi nitamuita wakili wangu…’akasema mama dereva.

‘Wakili wako wa nini..wewe unataka kudai nini hapa, huyo sio mtoto wa familia hii anataka nini tena, wewe si umesema hahusiki …sasa vipi tena, huyo hatambulikani na wakili akija hapa kila kitu kitawekwa wazi, ..hana haki hapa kwa lolote lile hata kama baba ataamua kuandika urithi wake, ni lazima sisi kama wanafamilia tujue..hivyo ndio wakili tutamwambia aandike maana huenda mna ajenda za kumpumbaza akili,…sisi hilo tutalisimamia ilimradi liwekwe kisheria baba unasemajekwa hilo..’akasema Soldier.

‘Hahaha..wewe mtoto chunga ulimi wako…unajua mimi ninaweza nisikutambe wewe kwenye urithi wa mali zangu hata kama ni mtoto wangu…nikiamua unalifahamu hilo….?’akasema

‘Ukiamua hivyo hewala,.... lakini mimi ninachotaka kukipigiania hapa ni haki na sheria za familia, ulishaniambia kuwa mimi niwe mstari wa mbele kupigania, na kuilinda familia, umesahau,…sasa kama ulinipa wadhifa huo, kwanini leo unataka kunikana… upo tayari kuwakubali, watu ambao so damu yako..umkatae mwanao halali…sema baba…?’akasema

‘Ndio nilikuamini, nikijua utakuwa bega kwa bega na mimi, lakini naona sasa unaniacha njia panda…ulitakiwa uwe na mimi, ..unajua wewe mwanangu unasahau, hapa ninakuonysha njia, maana haya na wewe yatakukuta, usiponitetea mimi, na wewe utamkosa wa kukutetea..nimeshasema huyo dereva sio mwanangu, inatosha, sasa kwanini wakili, huniamini….’akasema.

Dereva aliyekuwa kimia, akakohoa kwa sauti kubwa,  na wote wakageuka kumuangalia yeye, akatikisa kichwa , akawa anathema wka nguvu , kama anajitutumua,..akawa anafanya hivyo, kwa haraka haraka sasa…..

‘Mwanangu vipi wewe…’mama mtu akasema akimuangalia mwanae, mara mtoto wake ataoa jicho, akawa sasa sio yeye tena, sauti nzito ya kutisha,..ikasema;

‘Ooooh, mnataka kunikana kuwa mimi sio mwenzenu eeh,..mnataka kuikana damu yangu eeh,..sikubali, nitaua mtu kwanza, nyie wote leo mtakuwa marehemu, na nitabakia peke yangu,….’akasema, na kwa haraka akasimama na kwa kasi ya ajabu akaruka na kusimama juu ya meza.

‘Mnaniona sasa, niangalieni vyema…mimi ni nani,…hasa wewe baba, unayeikana damu yako,…nitakutesa kwa kunikana…unanikana kuwa mimi sio damu yako…wewe ..mimi sio dmu yako….eeh,…umegushi vyeti,….umewadanganya hawa watu….hahaha…’akamsogelea baba yake Soldier.

Hutaamini, alimuinua mzee huyu hewani kutoka alipokaa,..na baba huyu ana mwili, lakini alivyoinuliwa juu, ni kama mtoto mdogo, na jamaa akasimama naye na kuanza kumzungusha hewana halafu akamrushia sakafuni…

‘Oooooooh,…ohh, yallah, oh….’ulikuwa mguno wa maumivi wa baba Soldier, akawa anagugumia kwa maumivu.

‘Oh jamani imekuwa haya tena, fanyeni la kufanya, hii sasa ni hatari,…’akasema yule mzee, akianza kuomba duwa zake, …lakini haikusaidia kitu, alishikwa na yeye akarushiwa upande wa pili na kulia ‘Yalaah, kanivunja mgongo!...’

Soldier na ubabe wake, alibakia hajui afanye nini, hajawahi kuona mtu mwenye nguvu na kasi za ajabu kama huyo….akataka amdake jamaa, lakini akawahiwa mapema akainuliwa juu na kutupiwa mbali..naye akawa anagugumia kwa maumivu…wengine sasa wanataka kukimbia.

Docta akawa anapiga simu hospitalini kwake kuomba msaada, waje na sindano, zile wanazodungwa vichaa, lakini kabla hajamaliza kuongea na simu na yeye akainuliwa na kutupiwa mbali….
Waliokuwa hawajaguswa, walikuwa hao mama wawili…na Dereva sasa akawa anawageukia wao,  na mzee akaliona hilo, akasema kwa sauti;

‘Wewe mwanamke, wewe mama yake Dereva, wewe ndiye unamfahamu mtoto wako vyema, inakwuaje ikitokea hivi, na inavyoonekana …haya umeyataka wewe, kama kuna ukweli, sema, ongea na hilo sijui ni shetani au nini…vinginevyo, hapa anaweza akatua sote..’akasema huyo mzee, …

‘Oh,mwanagu sema unataka nini....’huyu mama akawa anaongea huku anatetemeka, kwani dereva sasa alikuwa akimuendea yeye, hajui tena kama huyo ni mama yake.

‘Ninataka nini…unaniuliza mimi ninataka nini…..oooh, ….mnajua mlichokifanya…..’akasema
Mzee wa soldier alikuwa sakafuni hajiwezi analalamika maumivu, Soldier naye yupo sakafuni, akijaribu kuinuka anawahiwa, dereva alikuwa na nguvu za ajabu, kila anayemkaribia anainuliwa na kutupwa mbali kabisa..

Mke wa soldier na yaya wao walikimbilia nje mapema,….

Hali ikawa tete,….na Soldier kila mara alikuwa akiinuka kumkabili ili asiwaendee mama …alijua hao akina mama wawili wanaweza kuumizwa zaidi, kutokana na hali zao za kiafya....

‘Wewe mama hali hiyo unaiona kama unajua lolote sema, akikugeukia wewe atakuua…’kabla hajamaliza, dereva akawa sasa anamuendea mama yake..

‘Hasa wewe…nakutafuta sana..lazima nikufundishe adabu, unadiriki kusema uongo, kuwa mimi sio damu ya huyu hawara wako…..mzandiki mkubwa wewe, mara ngapi mumekuwa naye,..mimi nawaona tu…mimi sitaki uchafu huo nimechoka..sasa nakumaliza wewe kwanza…’akawa sasa anamsogelea mama yake.

‘Nisamehe mwanangu nitasema kila kitu…usinitese, usiniue mimi ni mama yako…’akasema sasa akipiga magoti huku anatetemeka.

‘Umeniuzi,…ni lazima nikufundishe adabu….wewe na mwenzako, ni kwanini mnasema mimi sio damu halali ya ….bwana wako..kwanini….’akasema sasa akiwa keshamshika mama yake na kumuinua juu, na anataka kumbamiza chini…mama huyu ana matatizo ya presha na kama hali hiyo itazidi anaweza kuathirika vibaya, sana..na kama atarushwa kama walivyorushwa wengine sizani kama anaweza kuhimili

Baba wa Soldier akaliona hili , akajua asipofanya jambo, …mke wa marehemu watamsahau, akajitutumua na kukaa vyema , akasema kwa sauti.

‘Nitasema kila kitu mwanangu…nitaitoa siri yote ya baba yako…nitasema kila kitu muachie mama yako utamuua, huyo ni mama yako…..na mimi nitasema kila kitu,…tafadhali…’akasema mzee.

‘Haya waambie ukweli, simuachiii huyu mpaka usema ukweli wote…kuwa mimi ni damu yako, kuwa wewe na mama ni wapenzi, kuwa…. Mimi ni haki sawa na familia, hii, ongea kila kitu…

‘Haya subiria, niongee…….’akasema mzee

‘Unanipotezea muda, ongea…akawa anamzungusha yule mama kutaka kumtupa chini, na baba wa Soldier, akaanza kuongea……….

NB: Aliongea nini….tutaiona sehemu hiyo baadae.


WAZO LA LEO: Watu hujidanganya kuwa wanaweza kufanya madhambi yao kwa siri, yasijulikane wakawa wanahadaana kwenye ndoa, lakini tukumbuke mkiwa wawili , kuna mwingine ambaye anawaona hata mkiwa pangoni,..akitaka siri hiyo anaweza kuibanisha kwa njia yoyote ile. Tumuogope mungu, na tufanye mambo yetu tukijua yeye hawezi kufichwa jambo lolote.

Ni mimi: emu-three

No comments :