Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, March 18, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-21


‘Halloh …sijui nikuiteje, manake mwanzoni ulikuwa dada yangu,  rafiki yangu mpendwa, lakini kwa hivi sasa, nashindwa nikuiteje,.....lakini hilo tuliache,….’akatulia muongeaji kwenye simu, na mpokeaji akawa kimia tu...

‘Nimeamua nikupigie simu tu, ili nikueleze yaliyopo moyoni mwangu,…nimekuwa nikijiuliza iweje haya yatokee, …je ni mpango wa nyie watatu au ni mpango wa wawili, na wewe ukawa mtendwaji…na sijui unajisikiaje moyoni mwako, ukiyafanya hayo unayoyafanya sasa, ni ujanja au kunikomoa mimi…sijui, labda ndivyo wanawake tulivyo kusahau,… labda…

‘Sasa mimi ninakuomba unisikilize tu…, najua mtendewa hawezi kuuhisi uchungu,kama yule aliyeathirika...kwani aisifuye mvua imemnyea, na siri ya mtungu aijuaye ni kata…'

Mpokeaji sio kwamba hawezi kujibu,,..anajua sana kujibishana, hata mpigaji wa simu anamfahamu kuwa yeye ni hodari wa kuongea, na mpigaji hamuwezi kabisa kwenye kubishana, lakini mpokeaji akaona ni vyema kubakia kimia tu, kusikiliza tu....

‘Mwanzoni nilipoambiwa una mtoto anafanana na mtoto wangu, nilijua ni kawaida tu, maana hata wanaume wetu wanafanana,..nilifurahi kuwa urafiki wetu umekomaa, na maneno ya watu nikawa nayapuuza…nikijua wewe ni rafiki yangu huwezi kamwe kufanya kitu kama hicho..lakini…

‘Nasema lakini maana haya yamekuja kujitokeza baaadaye, na baada ya kujitokeza ndio nikakumbuka jambo, siku za nyuma kuna mtu aliwahi kuniambia, kuhusu mume wako…’akatulia

‘Yeye aliwahi kufanya kazi hospitali, ambayo mume wako alikuwa akitibiwa, na yeye alikuwa kitengo cha vipimo, na siku moja aliona vipimo vya mume wako, kuwa ana matatizo …na kwa utaalamu wake, aliyagundua hayo matatizo kuwa ukiwa nayo huwezi kuzaa tena…’akatulia.

‘Kuna kipindi fulani nilikupigia simu, nikitaka tuongee, lakini kukawa na sintofahamu nyingi, tukashindwa kuongea, na hata ulipofika huko kijijini, nilikuambia hebu tafuta muda tuongee, lakini ikawa hawezekani, na nilishangaa umebeba mimba, unakumbuka niliwahi kukuambia mume ni mwingi wa rehema kaamua kuwaumbua watu na vinywa vyao,…nilikuwa na maana hiyo kuwa huyo aliyesema mume wako hazai ni mwongo,…’akatulia.

‘Kiukweli matatizo aliyokuwa nayo mume wako, yasingeliwezekana yeye kuzaa…liniambia ukweli maana hayo nimekuja kuyajua tena baadae…’akatulia

‘Baadae sasa umejifungua mtoto, na mtoto huyo anafanana na mume wangu…kama nilivyokuambia nilipoambiwa kuhusu hilo nilipuuzia,..sikuwa na akili ya kufikiria hayo maelezo ya awali…kiukweli sikulikumbuka hilo kabisa, nikajua mtoto wako, ni wangu pia, nikajawa na furaha…’akatulia

‘Watu wakazidi kunisakama, kwa hilo..mpaka kero..basi ikafikia muda nikawaambia,,,kama imetokea hivyo, mtoto wako anafanana na mtoto wangu,  basi ni bahati nzuri,  maana wewe ni rafiki yangu, na hayo wanayoyasema ni uzushi, maana wewe huwezi kamwe kunisaliti…na kama imetokea kufanana, basi ..yaishe…nikijua ipo siku tutakutana utaniambia ukweli…’akatulia.

‘Nilitamani nije tukae, nikufariji tu, tuyaache tu yapite…kama yalivyo maana mtoto wako ni wangu, ndivyo tulivyokuwa tukiishi, na…nikashukuru mungu, lakini moyoni nikawa najiuliza iweje hilo lifanyike nyuma ya mgongo wangu, kwanini usiniambie…’akatulia

‘ Nilijua kwa vile wewe ni mwanake kama mimi,  utalijutia hili, ukatubu. Nilijua wewe ni rafiki yangu, dada yangu, tuliyeshirikiana nawe, utakuja kuniambia ukweli.., nimesubiri wee, lakini haijatokea na baadae ndio ukweli ukaanza kudhihiri, kuwa kumbe haikuwa bahati mbaya, kumbe wewe na mume wangu mlikuwa na ajenda yenu ya siri…’akatulia.

‘Kwanini isiwe hivyo, mtenda kosa hutenda mara moja, akirudia kakusudia, je hujawahi kutembea na mume wangu tena na tena..kama hiyo ya kwanza ilikuwa ni bhati mbaya…, nikuulize, lakini kwasasa sitaki jibu , maana nimewaona wewe na mume wangu mara nyingi tu, yeye anajitetea kuwa anakuliwaza, haya anakuliwaza mpaka kitandani,..., nimewaona kwa macho yangu..hebu niambie kama ingelikuwa wewe ungelijisikiaje, urafiki upo mpaka kuchangia waume, mbona mimi sijawahi kutembea na mume wako kama ingelikuwa ni hivyo…’akatulia

‘Tuyaache hayo labda mimi ni mjinga,nakumbuka sana kauli yako, uliwahi kuniambia awali,  kuwa mume akitembea nje, basi mke umeshindwa kazi…labda mimi nimeshindwa kazi, kazi unaijua wewe…lakini kumbuka wewe ni mwanamke kama mimi, …kumbuka haya yanayotokea leo, yaweza kutokea kwako, kwa watoto wako …kumbuka hilo…’akatulia


'Nakupigia simu hii sikuwa na nia ya kukushutumu, najua kama umedhamiria, hata nikuambieje hutanielewa, maana sikio la kufa halisii dawa,  ila natoa neno muhimu kwako, sisi ni wanadamu tu, hapa duniani ni mapito…, wangapi waliyafanya hayo wakaishi milele, hakuna…. tutayafanya hayo na mwisho wake tutarejea kwa muumba wetu,hakimu wa mahakimu…na hata hapa duniani, muumba anaweza kutoa adhabu yake, sikuombei mabaya,..hapana , sivyo mungu alivyotuusia,ila elewa, mateso gani ninayoyapata ..elewa hilo….

‘Na sasa nakuusia wewe na kujiusia mimi mwenyewe, kuwa tumuogope mungu..najua ipo siku...haki itatendeka...

' Jingine ni hili, nimesikia mwanao ameamua kudai haki yake,…unaona yaliyokuwa ya siri sasa yanaanza kuwa dhahiri, yanaanza kututesa sisi wenyewe, nasikia kuwa kijana wako ameanza kumfuata mume wangu na kumfanyia visa, ili ikiwezekana mali yote aichukue yeye..je hamjui kuwa hiyo ni dhuluma, mnawanyang'anya hata wale wenye haki yao...

Nakuelezea hili, ninajua wewe ni mzazi kama mimi, mwanangu anarudi mungu akipenda, hivi karibuni, na haya yanaweza kuzua vita, mimi sitaki vita, mimi sitaki ugomvi..kama lengo lenu ni mali, basi fanyeni taratibu stahiki…, mje mchukue, kama ni haki yenu, ilimradi tu mtuachie amani...nawaomba tena sana, mimi sitaki fujo…umenisikia hilo njooni kwa utaraibu mseme mnataka hiki na hiki, basi mchukue..si haki yenu mnayodai…au mnatakaje!

‘Na kama wewe unamtaka mume niambie, kwanza mimi nilishaondoka hapo nyumbani ili niwaachie nafasi,..mume huyo hapo nyumbani mchukue, na mliweke hilo hadharani kuwa wewe sasa ni mke wa mume wangu, ..au mnataka nini , mimi siwaelewi,...hamtosheki jamani!

‘Dada, au mke mwenzangu, nayaongea haya maana yanazidi kuwa mabaya kila kukicha,..sasa nisipoongea leo, labda huko kesho nitakuja kulaumiwa,…mueleze mwanao, kama anahitajia hiyo haki yake,basi ajitambulishe rasmi, kwa wahusika, kuwa yeye ni mtoto wa mume wangu na anahitajia kadha wa kadhaa, au sio..tulielewe hilo, lakini sio kwa hivyo anavyofanya yeye, anatuumiza na sisi tusiokuwemo kwenye mambo yenu..

‘Yeye anapita akiimba wimbo wake, kuwa kitanda hakizai haramu…wenye akili tulishamuelewa, …sasa muulize anataka nini…..umenisikia, muulize, kama lenu ni moja, haya njooni kwa utaratibu unaofaa mseme mnataka nini…..’simu ikakatika.

Mama dereva akabakia ameshikilia simu masikioni, akahisi vitu vikimpanda na kushuka, akahisi kutapika,akihisi kulia…lakini mwili ukawa kama umekufa ganzi, akabakia vile vile kwa muda…

*********
Wakati mama anaongea na simu,  mtoto wake alikuwa kasogea na kusimama kwenye dirishani akawa anaangalia huko nje, akibuni mambo yake, na kuyaweka sawa kichwani, alijua mipango yake imeshakamilika iliyobakia ni muda tu, akiwasili wakili wake anakwenda kumaliza kazi,…

‘Mama ananiwekea kiwungu tu, lakini atanielewa, hili ni lazima lifanyike, apende mama, asipende, yeye atakuja kujua mengine baadae…’akasema kwa sauti ndogo, na hapo akageuka kumuangalia mama yake, na kumkuta akiwa kaganda..kashikilia simu sikioni, lakini haonekani kama yupo sawa, akahisi kuna tatizo

‘Mama ina maana bado unaongea na simu..bado unaongea na mama yake Soldier..?’ akauliza, lakini hakupata jibu, mama katulia tuli.

Dereva akamsogelea mama yake, na kuichua ile simu mkononi mwa mama yake, simu haikuwa hewani, akamshika mama yake mara mama huyo anadondokea sakafuni..

‘Hee mama vipi tena..’ akasema huku akili ikianza kuchanganya, akajua mama yake hayupo sawa, akamshika shingoni kuhakikisha kama mapigo yapo sawa…

' Mama nini...umepatwa na nini mama…?'akamtikisa tikisa..lakini mama alikuwa kimia..

Haraka akachukua simu yake na kumpigia docta anayemfahamu, akamuelezea dakitari jinsi ilivyo kwa mama yake, na dakitari akamuelekeza ni nini afanye kama huduma ya kwanza,  akajitahidi kufanya hivyo na, baadae mama yake akafungua macho.

'Mama kumetokea nini?'akauliza, lakini  mama yake hakufungua mdomo…alikuwa kimia tu.

Dereva akachukua simu ya mama yake na kuangalia huyo mtu aliyekuwa akiongea na mama yake, alijua kuwa ni mama yake Soldier.

Akaipiga ile namba huku hasira zikimchemka, akilini anatafuta maneno makili ya kuongea, mtu anaymemuumiza mama yake kamuumiza yeye…

‘Halloh, mimi ni dereva, umeongea nini na mama'akauliza kwa hasira.
,
'Muulize mwenyewe,…  kwani hawezi kuongea?'akaambiwa

'Mama alikuwa akiongea na wewe, na alipomaliza kuongea na wewe, akapoteza fahamu, umemfanya nini mama yangu, unajua hali yake lakini…sasa umemfanya nini mama yangu...'akawa anaongea kwa hasira


'Sikiliza dereva, nasikia wewe ndiye mshawishi mkubwa kwa mama yako, lengo na nia, ni kuhakikisha mumemfirisi mume wangu...kweli si kweli?…sasa hayo yanayompata mama yako , kwa hivi sasa sababu kubwa ni wewe…jiulize wewe mwenyewe umefanya nini….'akatulia

‘Nimefanya nini…nilishawahi kuongea na wewe kukuambia lolote..?’ akauliza

'Sasa ni hivi,..mama yako nimemuambia hivi,  kama lengo lenu ni mali, si ndio unataka hayo, mali…sasa fanyeni hivi,  tafuteni utaratibu mnzuri tu, kama ni wakili, kama ni wazee mje kwa ustaarabu, mseme mnataka nini…mnataka hiki na kile,…mtapatiwa,..au kama mnataka mali yote, sawa mtachukua,.. si ndio unalolitaka hilo, ndio nimemuambia mama yako kama kashikwa na kihoro, cha fuaraha au nini sijui...'akaambiwa .

'Mama mimi sijawahi kuongea na wewe kuhusu mali, mimi naongea na mzee, nisingelipenda wewe uingilie hayo kati, maana wewe na mama yangu hapa, nawaheshimu sana, nafahamu kabisa nyie wawili hamna hatia, na yote yaliyotokea ni sababu ya wazee wetu,…marehemu na mume wako..lengo langu ni kuwaweka kwenye mstari sahihi..baba hayupo duniani ni marehemu lakini mume wako yupo, aubebe mzigo wake...'akasema.

‘Je katika kuubeba huo mzigo unahisi anauweza kuubeba mwenyewe, wakati ana familia, unajua fika wakipigana mafahali zinazoumia ni nyasi, unafikiri ni nani anayeahirika na hayo yote,…sasa tusipoteze muda, kama mama yako keshaamuka, yupo sawa, mwambie mpange siku mje, ….unasikia, na jingine kunaweza kuwepo na sherehe ya kuwakaribisha waliokwenda huko vitani ,hakikisha kuwa unakuwepo wewe na mama yako…’akataka kusema lakini mara simu yake ikachukuliwa wangu wangu, na mama yake.

Mama yake kumbe alikuwa kazindukana vyema, na akaja kwa nyuma na kumnyang’anya Dereva simu,..

Na kwa haraka akaanza kuongea na mama yake Soldier.

‘Wewe mwanamke wewe…., nimekusikia, sitaki tena neno kutoka kwako…achana na mimi , achana na mwanagu, sitaki kuongea na wewe tena, na wala sitaki, siwataki, nawachukia..nyote nyie siwataki tena …umenisikia…’akasema

‘Ni…’mwenzake akataka kuongea.

‘Na mume wako asikanyage tena hapa kwangu, akija nitamnywesha sumu,…mwambia hivyo,  unanisikia, naona akiwa hai atazidi kunifuata fuata, je niliwahi kuja huko kwako kumfuata mume wako…yeye ndio kila siku kiguu na njia kuja hapa kwangu..nilimuita, kama umeshindwa kumuhudumia mume wako mwambie akatafute wanawake wengine, wapo wengi mitaani, kwanini ananing’ang’ania mimi..umesikia…’akasema

‘Hahaha..naona sasa umeshapona, kauli yangu ni hiyo hiyo, ..kama mnataka mali, njooni kwa utaratibu , mwambie mwanao…mje,..na kama wewe unamtaka  mume wangu, niambie..usijifanye huhusiki, usijifanye kuwa yeye ndiye anakufuata fuata, kwanini kama anfanya hivyo usiniambie mimi mwenyewe, lenu moja,,…’mwenzake akasema na mama mtu akaitupa simu chini…na kuanza kutembea, akielekea nje…

‘Mama unakwenda wapi……

NB: Haya ya akina mama yakianza …


WAZO LA LEO: Mnapoingia kwenye ugomvi,mkawa hamuelewani, muhimu kwenye ni kuvuta subira, kila mmoja atulie sehemu yake atafakari kwanza ni nini faida ya ugomvi huo, na nini athari zake, na ikizidi sana watafuteni wenye hekima wawasuluhishe, msizidi kujengeana chuki, visasi,…na uhasama, kwani kwa kutenda hayo mnazidi kumfurahisha ibilisi na mwisho wa yote nyote mtaadhibiwa mbele ya mola.
Ni mimi: emu-three

No comments :