Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, March 16, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-19


‘Hii hapa ni nakala ya DNA mzee,….’akasema akinikabidhi hiyo nakala..

‘Ya nani tena….?’ Nikauliza huku nikisita kuipokea hiyo karatasi, akili yangu ikikumbukia, ile nakala ya awali iliyothibitisha kuwa yeye ni mtoto wangu nikajua na hiyo ni ya kuthibitisha kuwa mtoto aliyeptikana ni mtoto wangu, na hapo nitakuwa sina ujanja! Mikono ilikuwa inasita, haina nguvu ya kuinuka.

‘Mzee, ipokee ni nakala yako hiyo….ni muhimu sana kwako…unishukuru kwa wema wangu huu…’akasema na mimi nikainua mkono na kuipokea,

‘Unajua mzee, mimi nakujali sana, wewe hujui tu, …hii sasa nimeitengeneza kutokana na ile halisi niliyokuwa nayo, kwa utaalamu,..unajua nilichofanya mzee, nimechukua nakala ile nikaiweka kwenye mtandao, nikabadili..pale kwenye positive nikaweka negative…’akasema.

‘Kwanin unafanya hivyo, ili iweje?’ nikamuuliza.

‘Kwasababu kwanza sitaki mimi niwe mtoto wako, pili ni siri yenu watatu,…na baba alikuwa na maana yake, siwezi kuingilia dhamira yake, namuheshimu na namuombea huko alipo, hakuwa na lengo baya, ila limekwenda vibaya…sio njia sahihi…’akatulia.

‘Mzee mimi…nitaka unielewe kuwa nakujali, nawajali, ila,…nawalaumu kwa hilo mlilolifanya kwa mama, siwezi kulaumu sana, maana mtasema kama tusingelifanya hivyo wewe ungelikuwepo, nitawajibu kwani nyie ni mungu…mnaona, ….sasa mzee ili lengo lenu liendelee kuwepo, na ili na wewe mkono uendelee kuwa kinywani, heshima yako, na …utajua mwenyewe, nimeamua kufanya hivyo …’akatulia.

‘Kwahiyo unataka nini..?’ nikamuuliza.

‘Hahaha mzee mbona haraka…kwanza tukubaliane hapo, je umenielewa, kwanini nibadilisha ukweli ukawa uwongo…lakini kwa masilahi yenu, unanielewa hapo,…?’akasema.

‘Mimi ninajua kila kitu unachofanya kina gharama, ulisema kila jambo kwenu ni Dili, au sio,,,,,sasa niambie unataka nini..baada ya haya yote, umejitolea gharama ya usafiri kwa mtoto, na yaya wake,…haya sasa umetengeneza hii DNA ya uwongo, ili ionekane kuwa kweli wewe sio mtoto wangu…ehe, nini unahitajia badili yake, ..au unataka nife, unataka nikupenini sasa..sema.?.’akasema.

‘Mzee, mimi sina roho mbaya kihivyo, unielewe hilo….najua umeshaanza kufikiria gharama na nini..lakini gharama ni nini ukilinganisha na utu wako, heshima yako…mke wako,mtoto wako….hebu jiulize hilo, ukikosana na familia yako wakakutenga, utakuwaje…’akatulia.

‘Sawa niambie unataka nini…?’ nikauliza.

‘Mzee mimi sitaki kitu kibwa saana…, ninachotaka ni haki yangu kama mtoto wako, lakin sitaki niwe mtoto wako.. maana bado nathamani usiri wenu, wewe na marehemu… ila haki yangu lazima niipate …’akatulia.

‘Mhh…sasa nimekupata, nilijua tu, huwezi kufanya hayo yote bila sababu bila marejesho, sasa nikiulize, wewe unadai haki, haki gani wakati mimi sio baba yako…?’nikamuuliza

‘Mzee,ili hilo la mimi sio mtoto wako,liendelee kuwepo,…kuwa mimi sio mtoto wako… hii nakala 
ya DNA, ya uwongo, utakuwa nayo wakati wote…kama ushahidi wako, au sio.., yoyote atakeyakuuliza sema mimi sio mtoto wako, ushahidi huu hapa..nani atagundua kuwa umebadilishwa, hebu niambie ichunguze vizuri…hata docta akiangalia atakubali tu, lakini ili mimi nisahau hayo, nifunge mdomo wangu, nahitajia kitu kidogo tu, haki yangu…’akasema

‘Haki gani, kiasi gani..niambie sasa..’nikauliza nikijua lazima itakuwa gharama kubwa sana.

‘Mzee, unajua kwanini mimi ninataka mama awe na …a-ma-ni,…hii ni namna ya kumfanya mama arudi katika hali yake, asiwe kama alivyo sasa,..unanielewe hapo..nina uhakika kabisa ukifanya itakawavyo,, mama atafurahi…’akasema

‘Sawa…niambie kwanini unazunguka,…sema unataka nini mali yangu, nyumba, mashamba, au unataka nini sasa, sema lengo lako…’nikasema

‘Mzee nimewaza sana hilo, nikajiwa na wazo sahihi kabisa…’akatulia

‘Ehe…sema..’nikasema

‘Ninajua wewe unaiitikia kirahisi tu sawa,..sema nk…ukifikiria kwa uwoni wako lakini moyoni mwako sio kweli, hapo ulipo kama ungekuwa na bastola ungeniua,..’akasema kama amenisoma moyoni mwangu.

‘Lakini umesahau uliyoyafanya,je ni mazuri,…hapana, nikuambie ukweli, sasa hivi mama ana wasiwasi sana na mimi, kuhusu maisha yangu ya baadae,..anyway, mimi ni mtoto wa kiume, nitahangaika kivyangu, lakini kwa mama hawezi kuelewa,….’akatulia

‘Sasa nikajiwa na wazo, ili mama awe na amani, ni lazima kuwe na kitu kama dhamani fulani ya kumrizisha mama yeye…,mzee unanielewa hapo, hili sasa ni kati yangu mimi na wewe…sawa unaweza ukaongea na mama kumuambia umefanya hivyo kwa upendo wako na rafiki yako, ila mimi na wewe tunafahamu ukweli upo wapi.., nafikiri tukifanya hivyo mama atafurahi sana…’akasema

‘Unataka nifanye nini..sijakuelewa bado?’ nikamuuliza

‘Uandike hati ya urithi,..hati hiyo ieleze kiasi gani mimi nitakipata kama mtoto wako wa kiume…si unajua mambo ya kimila mtoto wa kiume anapata nini….hilo sio siri, nyie watoto wa kiume mnawatahamini sana, na wanapata sehemu gani katika mali…, kwa vile mimi ni mtoto wako, lakini kwa makubaliano yako na rafiki yako, ulinitoa kwake niwe mwanae, lakini hiyo hainifungi mimi kupata haki yangu kama mmoja wa watoto wako wa kiume au sio,..?’akasema

‘Mhh….mtoto acha tamaa…kwani unataka nini kwenye mali zangu, baba yako alikuachia mali, mashamba, tatizo lako kwa tamaa zako umeuza,..mumebaiwa hamna kitu, sasa unakimbili kwangu….wewe mtoto acha tamaa, utakufa kabla ya muda wako…’nikasema

‘Mzee, sifanyi mdhaha….lichukulie hili jambo kwa umuhimu wake, unajua nifunge mdomo, nihakikishe siri zote za ukweli hazionekani,..siwezi kuziharibu maana sijui leo na kesho, ila nitahakikisha zipo sehemu nyeti…’akatulia

‘Sasa mzee tusifanye maneno marefu….mwanasheria wangu atakuja kesho, yupo njiani, kesho anatua na ndege,..ni gharama hizo mzee lakini zitaleta faida, faida kwangu na kwako, kila kitu tulenge kwa faida, au sio….umenielewa mzee, mimi nitaziba mdomo, hutaumbuka, utaendelea kuneemeka na uongozi wako, na mimi na mama tutapata haki yetu..au sio….?’akawa kama anataka kusimama.

‘Mhh, hati ya mirathi….siwezi kuamini…’nikasema nikitikisa kichwa.

‘Usiulize hiyo hati ya mirathi itaandikwaje, mwanasheria,…eeh, atajua jinsi gani ya kuiandika,…muhimu ni kila kitu kiwe wazi, mali yako warithi wako..nk. nia hapa ni ili kila mtu wa familia yako apate haki yake, na mimi nipate haki yangu na mama naye apate kifuta jasho chake, ukifanya hayo, aaah, mimi na wewe tunashikana mikono, hutanisikia tena katika maisha yako….’akasema

‘Najua hilo utasema tena na tena,…mtoto una tamaa wewe, sijui umetoka wapi, najua kila ukiwa na shida, utakuja, na usifikirie hilo ni rahisi kihivyo, niandike urithi, kwanza wa nini, uliwahi kuona huku kijijini wanaandika urithi, eeh, …hapana, wewe una lako jambo, unataka kuniua…’nikasema

‘Mzee, sikulazimishi,… ila ukilala leo lifikirie kwa makini mzee ni mangapi nimekufanyia,..na sasa nataka kuziba mdomo wangu kabisa,..hivi mzee, jiulize kwanza, hivi nikiamua nikianza kutangaza kuwa wewe ni baba yangu, ulitembea na mama pasipo na hiari yake.., nikianza kusema wewe umetembea na mke wa mtoto wako…si utaumbuka…fikiria sana hilo mzee’akasema

‘Lakini yote hayo ni uwongo…ni ujanja ujanja wako tu…sijafanya hivyo’akasema

‘DNA, haidanganyi mzee…uwongo kwa vipi, ….wewe umesoma mzee, unafahamu maana ya DNA,…au sio…na uwongo kuwa hukutembea na mke wa mwanao, ....muulize, kama kweli atakubali kusema ..na atakuja kusema, kama hutakubaliana na mimi...’akasema

‘Kama umeweza kubadili,…hiyo hati ya DNA,..utashindwaje kudanganya hayo..’nikamwambia

‘Sikiliza mzee, kamtafute dakitari wako unayemuamini, tukapime, kama kweli hiyo DNA, ni ya uwongo..uone utakavyoumbuka…’akasema

‘Nitamtafuta..hilo nakuahidi, ni lazima niuafute ukweli…’nikasema kwa kujiamini.

‘Sawa tuahidiane hilo, na likifanyika hilo kuwe na mashahidi..na likimalizika hilo liwe wazi watu wajue, kuwa kweli mimi sio mtoto wako wa damu au ni mtoto wako wa damu,…haitakuwa siri tena, upo tayari kumsaliti rafiki yako…marehemu, upo tayari kujiumbua, sema mzee…kama upo tayari haya, kesho akija wakili, tuanze michakato, twende hadi mahakamani…’akasema

Nilikaa kimia kwa muda nikiwaza, halafu nikasema;

‘Nia na lengo lako ni nini hasa…?’ nikamuuliza

‘Nimeshakuambia mzee…, mama yangu anahitajia amani,…amani yake ni kuona haki yangu imelindwa, hakujua mlichomfanyia..huo mliofanya ni unyama, unajua kubaka..nyie mlifanya njama, ukambaka mama yangu…huku hajitambui….kesi ya kubaka, kesi ya kumnywesha mtu ulevi….kesi ya….’akatulia

‘Acha,….usinitishe, maana mimi sikupenda hilo, hata baba yako hakupenda hilo, wewe unalikuza tu….’nikasema

‘Mzee, chukulia mfano hayo yangelifanyika kwa mkeo..ukaja kuyafahamu, …au uchukulie wewe ulikuwa ndio mama..ukafanyiwa hivyo, hebu angalia katika nadharia hiyo…’akasema

‘Najua wewe na mama yako mumekaa mkalipanga hilo..ok, haya sasa yeye anataka nini kwangu, wewe unataka mali yangu, sijui kiasi gani, na yeye anataka nini,…hivi yeye kama yeye hashukuru kuwa ana mtoto au hilo hamlioni, mnaona mali tu…?’ nikauliza

‘Mama anahitajia kifuta jasho…najua hakuna thamani ya kurejesha utu wake…ila wewe unahitajika sana tena sana, ukamuombe msamaha,..na hayo hayawezi kufanyika kwa maneno tu, hayo yaatafanyika kukiwa na dhamana fulani, itakayo mfurahisha,……hati..ya urithi ndio dhamana stahiki, …kesho nakuja na wakili wangu…’akasema akianza kuondoka.

‘Wakili wako! Sasa unataka kuniweka uchi , ndio lengo lako au…?..mimi nitamuaminije huyo wakili wako.., si ndio hao watakwenda kuniharibia maisha yangu..unataka kuniweka mtegoni ndio lengo lako au sio, umemtafuta tapeli mwenzako huko aje ..kama wakili wako au sio….’nikasema

‘Mzee..niamini, wakili wana kiapo, hawezi kuwa tapeli.., utamuona mwenyewe akifika hapa, na ni kwanini afanye hivyo, unasema utapeli, hapana, hana shida hiyo,… wewe mtafute wakili wako ukitaka,..na mimi anakuja huyo wakili wangu…tutaandikishana basi, …hiyo ndio dhamana yetu…nini…, hati ya urithi, kuwa mimi nitapata kiasi gani kwenye mali yako, kama itatokea ukatangulia, au hata ukiwemo, lakini mali hii na hii ni yangu, kimaandishi, ya kisheria,…umenielewa mzee…?’ akasema kwa kuniuliza

‘Achana na mimi…siwezi kukuelewa kamwe..ngoja huyo wakili wako aje, ..tutapambana naye, na nakuahidi haya sasa yamekwenda mbali…unataka mali si ndio…, nitakupa… si ndio unataka hicho…mali, haya…, lakini utakuja kujua kuwa mimi ni nani kwako, kama hukutoka kwenye hii damu….tutaona,..wewe si unataka mali, haya nitakuandikishia kila kitu tuone kama mtakuja kuutumia…

‘Mzee, tumemalizana, kwa leo, kalale,..lakini ukumbuke,..nina orodha ya mali yako yote,kuanzia huko ukweli kwako,..hadi hapa…yote hiyo iwepo kwenye Hati ya urithi,..’akasema

‘Oh, …’nikaguna hivyo tu.

‘Hilo ndillo jambo litakalomfanya mama yangu awe na amani, aache pombe. Atulie…na asidhalilike, anaumia, kwa hicho ulichomfanyia,na niliapa…., siku nikigundua kuwa ni kweli, …’ akatikisa kichwa.

‘Haya nayafanya kwa ajili ya mama yangu,…nilidhamiria kufanya mabaya zaidi ya hili…, lakini nimeona haina haja,..muhimu mzee, wewe andika hiyo hati na hakuna kupunjana kati yangu mimi na wanao hilo siwezi kulifanya haki kwa haki, sawa kwa sawa, kwa watoto wa kiume, sawa…kwaheri……’akasema na kutaka kuondoka. Na mara simu yangu ikalia…

‘Ni nani mwenzangu…?’ nikauliza nikiwa nimejichokea...

‘Ni mimi mwanao Soldier, baba…tunatarajia kufika huko kesho kutwa au mbele yake kidogo, nitawajulisha, …’ ilikuwa sauti ya Soldier

NB: Raha si raha, ….jamani mbona nimekatiza..


WAZO LA LEO: Tamaa za mali, tamaa za utajiri, tamaa za maisha zisivuke mpaka, tukumbuke kila kitu kina haki zake..tusiporidhika na haki zetu, itafikia mahali tutamani hata utajiri wote wa dunia na hata tukiupata bado hatutatosheka…hakuna utajiri mnzuri kama kutosheka, na pato la jasho lako halali, tumuombe mungu turidhike jasho la pato letu halali,..Aaamin.
Ni mimi: emu-three

2 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Nami naweza nikasema jamani ndugu wangu bona umekatisha utamu ilipoanza kukolea?...haya tusubiri kinachoendelea....

emu-three said...

Utamu unakuja ndugu wangu, soma sehemu ya 20