Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, March 15, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-18


‘Mzee hilo peke yake la kuwa ulifanya hivyo ni kashfa kwako, ulifanya nini na mke wa mwenzako , tena rafiki yako,..ni swali ambalo litakuharibia sifa yako, ...je ni kwa makubaliano, kama ni kwa makubaliano mbona mama hajui....au ulimuhadaa baba, kwa vile mnafanana naye,..haingii akilini...'akatulia

Sasa hilo ni tisa, kumi , hili....hili la sasa mzee, sijui utaiambiaje jamaii, mzee, utakufa kwa presha,…fikiria sana, lakini nipo kijana wako nipo, nitakusaidia , ila…’ akasema.

‘Acha nife…’nikasema nikiwa natamani kusema maneno mabaya lakini sikuwa na ujanja, huyu kijana anajua jinsi gani ya kumshika mtu pabaya, nishaanza kumuogopa,...na umri huu tena, sikutaka changamoto za namna hii...ningekuwa na bastola, lolote lingelitokea...kanimaliza....

‘Mzee usiseme hivyo, wanaoo tunakupenda, …. ndio maana nataka kukusaidia,...'alisema.

Kweli msaada aliotoa ulikuwa wa namna ya kumfanya huyo mtoto aweze kupata maziwa, yaya wa kumlea, tiketi zao..lakini najua gharama hizo nitakuja kuzibeba mimi, najua kuna jambo lipo mbele yangu..nikawa nasubiria, hata nikiwa kwenye ndege, nikajua kuna mtego, hilo la kupewa huyo mtoto nk..ni sehemu tu, ni lazima kuna jambo kubwa litatokea huko mbele, sijui ni jambo gani

Tuendelee na kisa chetu…

                   **************
Mtoto alipoanza kulia tu, mara mwanadada mmoja akatokea, akiwa na kikapu..ndani yake kuna vifaa vya mtoto, maziwa nk...akanisalimia, na kujitambulisha,... sikuwa na zaidi, nikafungua mlango wangu na kuingia ndani, baadae naye akaingia...

 Mipango ya mtoto kuondoka na mimi ilishapangwa na Dereva, ajabu kabisa, na hata huyo yaya aliyeletwa huo usiku alikuwa keshakatiwa tiketi yake…kweli jamaa alijiandaa, alikuwa na uhakika kuwa hayo yote yatafanyika na mimi nitakubaliana nayo,..na najua ana maana yake, na gharama hizo nitakuja kuzililipa, sijui kwa vipi..

Hata hivyo nilishukuru, maana ningelifanyaje na huyo mtoto, na alishaanza kulia…

Huyo yaya…alipofika tu,  akamnywesha huyo mtoto maziwa aliyoyatengeza kwa muda mfupi tu, naona alikuwa kaisomea hiyo kazi..., mtoto akanywa na hatimae akalala…,

‘Kwahiyo huyo mtoto utakwenda kulala naye chumbani kwako…’nikamwambia

‘Wapi bosi, ...?' akaniuliza

'Hakukuambia aliyekutuma...?' nikamuuliza

'Hapana yeye kasema nije hapa, nianze kazi ya kumhudumia mtoto na mengine yatafuata , ndio nasubiria,....bosi 'akasema

'Haya mimi najipumzisha, sasa wewe ...utalala wapi, ...?' nikauliza
'Mimi nitakaa hapa hapa kwenye sofa,...kwasababu, nasubiria maagizo, yenu....'akasema

'Sawa...'nikasema nikiliza kichwa kwenye mto.

Mawazo mawazo..usingizi wa mang'amu ng'amu, tunasubiria,....muda ukafika, tukaondoka kwenda uwanja wa ndege, taxi ilishafika, ...

Tuliondoka hapo kama kawaida na kufike maeneo ya kwetu, na nilipoteremka uwanja wa ndege tu haraka, nikachukua usafiri wa kuelekea huko kijijini anapoishi mke wangu, sikutaka kufika kwangu na huo ugeni, nitasemaje watu wakiniona na huo ugeni na watu ni wepesi sana kunasa mambo.

Haya haraka tukafika ukweni, na uzuri huko nilikuwa na nyumba yetu niliyojenga na hapo ndipo mke wangu alikuwa akiishi, ni hatua kidogo kutoka hapo ndio makazi ya wazazi wa mke wangu.

Mke wangu aliponiona, alinipokea tu kama mgeni, huku akionyesha macho ya mshangao na huo ugeni, hakusema kitu, akahakikisha huduma muhimu zipo, hasa kwa mtoto,…mimi nilikuwa nimekaa sehemu ya nje kwenye mti, sikutaka hata kuingia ndani.

‘Mbona huingii ndani..?’ akaniuliza

‘Kuna mambo nataka tuyaongee kabla sijaingia huko…’nikasema

‘Ina maana unaondoka leo hii..?’ akaniuliza

‘Ndio, nahitajika…kufikisha kile nilichotumwa huko ….leo hii, …’nikasema, akilini nikijua nina mambo yangu natakiwa kuyaweka sawa, na nikiendelea kukaa hapo, maswali yatakuwa mengi, ambayo sina majibu yake. Na ….

Mara mke wa Soldier akatokea….

 ‘Hee huyu mke wa Soldier yupo huku….?’ Nikamuuliza mke wangu, na moyoni nikawa nakumbuka maneno ya Dereva…

‘’….Ndio maana nimekuambia wewe ulifanye hivyo, kwa kukusaidia,..mchukue huyo mtoto maana ni damu yako, rudi naye kijijini kamtafute mke wako…na huko utamkuta mke wa kijana wako ameshafika,kwanza muulize alikuwa wapi…’’

‘Ndio amekuja huku, anaogopa kuishi na wewe , umemfanyia vituko vya aibu…hata sijui wewe mwanaume wa namna gani…hata mke wa mwanao…..’akasema.

‘Amefika tokea lini…’ nikamuuliza bila kujali hicho alichoongea, maana kweli nikilewa nakuwa ….hata sielewi.

‘Sio muda mrefu, lakini hana raha kabisa, nimejaribu kumuuliza ana nini hataki kuniambia…nafikiri ni mambo yako, hebu niambie ulimfanya nini..?’ akaniuliza.

‘Mke wangu mimi sijamfanya kitu, na wala sielewi, kuna muda nilikuwa nalewa..kuondoa mawazo, sasa sijui…..naombe mke wangu unisaidia…nahitajia msaada wako mkubwa sana…’nikasema.

Pamoja na yote ninayoyafanya, mke wangu ananipenda sana, ni mwanamke mwenye huruma, sana, na nilivyoongea hivyo akawa keshanielewa kuwa nipo katika hali gani. Kukawa na ukimia kidogo, halafu mimi nikasema;

‘Oh…kumbe ni kweli..’nikasema, na wakati huo mke wa mwanagu alikuwa anakuja kunisalimia.

‘Kweli kuhusu nini, kwanza hebu niambie huyo binti na mtoto mchanga umetokea wapi, usiseme umempa mwanamke mwingine mimba na unataka kuniletea mizigo huku…huyo mtoto mchanga mnafanana naye….uniambie ukweli, ili tuachane kwa amani…’akasema

‘Huyo ni mtoto wa Soldier..’nikasema kwa kujiamini.

‘Eti nini…?’ aliyeuliza hilo swali ni mke wa Soldier alishafika mbele yangu kunisalimia.

‘Eti nini…mtoto wa nani,…?’ akauliza mke wangu, sasa naye akianza kuchanga changanya macho, najua sasa anamuhofia mke wa Soldier, atalichukuliaje hilo...na huenda moyoni atakuwa akinilaumu kwanini nimeongea hilo mbele ya mke wa Soldier

Tukasalimiana na mke wa mwanangu, halafu yeye akasogea pembeni akisubiria maelezo, na mimi sikutaka kuongea naye kwa muda huo, nilitaka kwanza niongee na mke wangu , niyaweke mambo sawa, hata hivyo, bado nilikuwa na maswali muhimu kwa huyo mkwe wangu:

‘Ngoja niongee na mama yako, atakuja kukuambia kinachoendelea, msijali tutayamalizia haya mambo ambayo yametokea huko…, sijiu kinachoendelea mpaka sasa…maana habari ni nyingi sana, muhimu tuzidi kumuomba mungu mtoto wetu awe salama..unasikia, muombee sana mume wako…’nikasema

‘Kwani ulisikiaje…?’ akauliza huyo mke wa Soldier.

‘Mengi tu…..atakuja kukuambia mama yako, nikimaliza kuongea naye, au unasemaje,..?’ nikamuuliza mke wangu.

‘Sawa, hata sielewi, umeshanichanganya….’akasema mke wangu.

‘Ile mke wa mwanangu, nakuomba sana, ufanye utakavyoagizwa, kuna mambo nitakubaliana na mama yako, ujitahidi kuyafuata …vinginevyo, sijui itakuwaje, mume wako anaweza kuwa matatani..’nikasema

‘Mhh…mimi sielewi…mambo yenu, nimekuja mara moja tu kumsalimia mama, nitaondoka…’akasema

‘Kwani wewe ulikuwa wapi muda wote huu, mwaka na kitu...hujui wewe umeolewa...?' nikamuuliza

‘Nilikuwa kwa wajomba zetu, nchi ya jirani…’akasema

‘Nchi ya jirani, huko wanapoishi wakimbizi…!!!?’ nikamuuliza na kichwani nikaanza kuhisi huenda aliyoyaongea Dereva yana ukweli, lakini ..haiwezekani kuwa kulewa kwangu niliweza kumfanyia ….hapana, siwezi, huwa kweli nalewa, mpaka napitiwa, lakini…oh, mbona ni aiabu hii…!

‘Lakini mbona hukutuambia,unajua bado upo kwenye mamlaka yetu, ulitakiwa ukisafiri umbali huo tujue, unajua kiasi gani nilivyohangaika kukutafuta…nikipiga simu kwenu hawataki kupokea…, mtu umeondoa nyumbani..unasema una kwenda kwenu, kwenu haupo, kuna nini ulikwenda kufanya,huko…?’ nikamuuliza na niliombea kama kuna ukweli wowote asije kuusema mbele ya mke wangu.

‘Baba, ..ilibidi niondoke, ..wewe mwenyewe unajua, nisingeliweza kuvumilia, …na kuna jambo muhimu nilitakiwa kwenda kulifanya huko kwa wajomba..nilikuwa sina jinsi…’akasema.

‘Mambo gani..?’ akaulize mke wangu kwa hasira kidogo.

‘Siwezi kuyasema,…mama nilishakuambia, muda ukifika nitayasema yote, lakini sio sasa, naombea huyo mume wangu arudi salama, akiwepo, ….ndio nitaongea,…naombeni mnielewe hivyo…’akasema.

‘Ulikuwa na nani huko nchi za jirani…?’ nikamuuliza, na akawa kimia, mke wangu ikabidi aingilie kati na kusema;

‘Mimi naona hayo niachie mimi, nitaongea na mwanangu, najua anahitajia muda, sisi wanawake tukikwazika, huwa hatutakiwi kulazimishwa…ila kama kuna lolote uelifanya kwa mwanangu hapa, tafadhali, …ujue itakuwa haina mjadala, hivi sasa nipo tu, sijaweza kuyaongea yote kwa wazazi wangu….’akatulia.

‘Ina maana umewaambia wazazi wako kuhusu matatizo yetu...?' nikamuuliza.

‘Niwaambie nini, ..huo uchafu wako, kama wengelisikia, sizani kama wangelinikubalia tena, nirejee kwako, nasubiria muda muafaka mwanangu arudi, akirudi, ..hapo nitatoa kauli yangu ya mwisho…’akasema.

‘Mke wangu unajua tumetoka mbali, unanifahamu sana , na siwezi kuishi bila yaw ewe, mengi yanayotokea ni kwa vile upo mbali na mimi..nakuomba sana, usije kunifanya nikapoteza maisha,…ooh…’nikataka kupiga magoti mbele ya mke wangu, lakini nilipogundua kuwa mkwe wangu bado yupo hapo, nikasita.

‘Samahani ….naomba faragha…’nikasema na huyo mke wa mwanangu akaondoka shingo upande, najua alikuwa na mambo …na alikuwa hakafahamu kuwa kuna ugeni mwingine, mtoto…alikuwa hajaonana nao hadi muda huo.

‘Nasikia kama kuna sauti ya mtoto mchanga..’akasema akimuangalia mke wangu.

‘Ndio,…sijajua ni nani hao, nitakuja kukuelezea, nenda wapo chumba cha wageni…’akasema mke wangu.

Baada ya mke wa Soldier kuondoka,….nikakimbilia kupiga magoto mbele ya mke wangu, yeye akageukia upande mwingine akisubiria maelezo.

‘Mke wangu mimi nitakueleza kila kitu, muhimu ni subira, tuombe mungu mtoto wetu arudi salama maana taarifa za huko hazieleweki,…lakini pamoja na hayo, nakuomba sana, univumilie mke wangu, naapa kuanzia sasa nitabadilika…...’nikasema.

‘Hayo ulishayaongea sana..utabadilika ndio wimbo wako ukikosea, sasa yabidi na mimi nichuke hatua, nasema mtoto wetu akirudi, hutaamini nitakachokifanya, na…hilo …la huyo mtoto, kama ni wako, ndio itakwua ushahidi wa uchafu wako,…..’akasema.

‘Huyo ni mtoto wa Soldier, hunielewi…’nikasema.

‘Na huyo mke wa Soldier ulimfanya nini…?’ akauliza

‘Je kuna kitu kakuambia kuwa nimemfanya lolote?' nikamuuliza kwa kujihami, nikiombea kusiwepo na kitu kama hicho...labda sio kweli, labda..labda..hata mimi sijui ukweli halisi!

**********

Ilikuwa kazi kubwa ya kumshawishi mke wangu kuwa huyo mtoto ni wa Soldier, na haijulikani alimpataje, kwahiyo yeye afanye juhudi za kuhakikisha mke wake anampokea huyo mtoto kama wake na kumlea, na afanye hivyo,..mpaka hapo mume wake atakaporudi, na yoyote atakaye muuliza aseme huyo ni mtoto wake…

Mimi ikabidi niondoke nirudi nyumbani kwangu,…

Wakati nakaribia nyumbani kwangu nikaona mtu amekaa kwenye kiti changu cha enzi, kuna kiti changu nimekitengeza kwa magogo, huwa napumzika hapo nikiwa napunga upepo, na huyo mtu alikuwa kava kofia kubwa, kama la yule mtu niliyemuona kule hotelini.

Nilihisi mwili ukiniisha nguvu…nikahisi hatari, nikahisi mashaka…ni nani huyu, ni yule jamaa, nikazidi kusogea, na mara yule mtu akajua ni mimi, akajigeuza na kunielekea, akavua kofia, na kusema;

‘Shikamoo mzee, nimekusubiria sana….’akasema.

 Alikuwa ni Dereva, mtoto wa rafiki yangu, alikuwa nje ya nyumba akinisubiria, utafikiri alijua kuwa nitarudi siku hiyo…unajua imefikia hatua nikimuona huyu mtu naanza kuingiwa na mashaka, shinikizo la damu linaongezeka,…ananipa shida kweli, natamani nifanya jambo…nim-malize, keshakuwa ni adui yangu moyoni.

'Hiyo kofia uliyovaa, ni kama yule mtu uliyemtuma kule hotelini....'nikasema

'Yah, ...ni kofia zetu, za kujikinga na jua...'akasema

Na kiukweli kwa hali niliyokuwa nayo, sikutaka kuongea na mtu, lakini niliona niongee naye ili nihakikishe mambo fulani fulani,..niujue ukweli na ni ni dhamira yake, kwahiyo nikawa mnyonge.

‘Umefika saa ngapi..?’ nikauliza.

‘Mzee, nimefika tokea asubuhi,…niliwasili…na ndege ya pili, baada ya nyie kuondoka na mimi niakingia ndege ya pili yake…kuna mambo muhimu nmekuja kuyaweka sawa… nilikuwa na mama nyumbani nimemalizana naye…, baadae nikaja hapo kwako, nikasema siwezi kuondoka mpaka tuongee…’akasema.

 ‘Haya sasa umekuja na kipi kingine, maana nia yako ni kutaka kunimaliza, si ndio..unimalize kimaisha, nifiriskike,….si ndio hata nikifa ni sawa kwako…’nikasema.

‘Mzee, nilitarajia wewe ungenipongeza kwa juhudi niliyoifanya, kwanza nikuulize mama (mke wako) na mke wa Soldier wamesemaje..?’ akaniuliza, najua anafahamu nimetokea huko.

‘Watasemaje,…mambo hayo umezua wewe, na haijulikani ukweli wake ni upi..’nikasema

‘Mzee, hivi kweli huyo sio mtoto wako,..niambie ukweli mzee, maana nikitaka kuutafuta huo ukweli nitaujua tu, na si unanielewa zangu..’akasema akiniangalia usoni.

‘Unajua uwe na heshima, mimi nawezaje kutembea na mke wa mwanagu, nimelogwa…’nikasema

‘Haaah, labda ulikuwa umelewa ukapitiliza...mimi hata sielewi..ni aibu sana mzee, ni jambo ambalo unatakiwa ucheze karata vyema vinginevyo , utaumbuka,…sasa  hayo yapo mikononi mwako kwa hivi sasa,mimi nimejitahidi kufanya hivyo ili kukusaidia,…’akasema

‘Kunisaidia au kuniangamiza….?’ Nikauliza

‘Mzee, utaelewa tu, ila,…kuna kitu nimekuja nacho hapa…’akasema

‘Kitu gani tena…?’ nikauliza

‘Ile nakala ya DNA, unayo..?’ akaniuliza

‘Nimeichana..’nikasema, ni kweli niliichana-chana kwa hasira.

‘Hahaha, …nilijua kuwa utafanya hivyo, ile ni nakala tu, halisia yake bado ninayo…lakini ulichofanya ni sahihi kabisa…sasa nimekuja na nakala nyingine ya DNA, ya kuthibitisha jambo jingine,…’akasema.

‘Ya nani, ya mtoto…?’ nikauliza sasa miguu ikinicheza cheza, na wakati huo, jamaa alikuwa akiitoa kwenye kibegi chake, taratibu.

‘Usiwe na wasi wasi mzee, unajua nilishakuambia mimi ni mtoto wa mjini,..na kila jambo kwetu ni dili..umeonaeeh, sasa, utaniamini kuwa mimi sijazaliwa leo, naona mbele na nyuma, na ujue, kuwa mimi sifanyi mchezo, nikuakuambia jambo ujue nimeshalifanyia kazi..’akasema.

‘Ohh..kijana...unanitafuta sana, hatasijui nisemeje,...lakini we ngoja tu...'nikasema na yeye akatabasamu tu.

‘Usichoke mzee..ngoja tuyamalize haya kwanza, halafu utakwenda kulala, upumzishe kichwa chako ukiwazia, ni nini ufanye, …’akasema.

‘Hii hapa ni nakala ya DNA,….’akasema akinikabidhi.

‘Ya nani tena….?’ Nikauliza huku nikisita kuipokea,

NB: HAYA, NINGELIENDELEA LKN MUDA, NA SALIO.


WAZO LA LEO:Ulevi ni mbaya, ulevi huondoa akili ya kawaida ya kufikiria kihekima, na wengine huchanganyikiwa kabisa,…na wanaweza kufanya mambo ambayo wakiwa na akili zao za kawaida hawawezi kufanya… na wengine wanajitetea kuwa wanakunywa ili kupunguza mawazo. Hivi unapunguza mawazo au unayasubirisha mawazo…ulevi ni moja ya silaha ya shetani,..ukiingia kwenye shabaha yake umeangamia!

Ni mimi: emu-three

No comments :