Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, March 11, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-15


Unajua kuwa kuna mambo ukiguswa, hata kAma upo na ujasiri gani, utatikisika tu, unaweza ukajibaragua lakini moyoni, utakuwa na vishawasha vya uoga, kiukweli nilianza kuogopa, ..kwanza nikaanza kujishuku mwenyewe, je kweli mimi nipo sahihi….nikajikuta nikijilaumu kuwa mwenendo wangu usio mnzuri, ndio maana haya yananitokea..

Ikafika nikaamua niongee na familia tuweze kuuza sehemu ya ardhi tuliyokuwa nayo..tuliwahi kununua mashamba, na mwenzngu yeye aliuza uza maeneo yake ili kupata pesa ya matibabu. Kutokana na hali ngumu, nikaona na sisi ni wakati muafaka wa kuuza sehemu ya shamba,…

Wanafamilia hawakulipinga hilo ombi langu, ila hawakufahamu kuwa mimi pamoja na hayo nina ajenda ya siri…sikuwa na namna nyingine ya kupata pesa, tukauza eneo, na pesa ilipofika mkononi, nafsi ikaniambia hii pesa ni jasho la familia, usiigawa bure, ..nyingine ikaniambia, fanya uliyoagizwa, utakuja kuumbulia na kazi , umauurufu wako wote utaingia nyongo, na wakati nawazia hayo mara simu yangu ikaita,  kuangalia mpiigaji ikawa ni ile namba isiyo na namba..

‘Haya niambie unataka nini tena..?’ nikauliza

‘Hiyo pesa ifikishe kwa muuza duka yule chotara,  mwambie ni deni la kijana wa marehemu rafiki yako atakuelewa…’akakata simu, hata kabla sijaweza kuongea lolote.

 Oh, sasa akili ya kiaskari ikaanza kufanya kazi, ukitaka kumshika mwizi, kwanza anza na yule unayemshuku, huyo anaweza kuwa ni njia ya kumpata mwizi wako, kwahiyo mimi moja kwa moja nikamuendea muuza duka kwa vitisho..

‘Mzee mbona unanichanganya,…mimi mwenyewe nimepokea ujumbe kuwa wewe mwenyekiti utanileta pesa, ya sehemu ya deni ninalimdai huyo jamaa’ akasema.

‘Kwahiyo mpo kundi moja…’nikasema.

‘Mzee ni hivi huyo jamaa mimi namdai sana, pesa nyingi tu,…na sijui kwanini isku hizi hanilipi kama zamani, alikuwa mwaminifu sana, anakopa analipa……….na jana ananitumia ujumbe wa maneno, tana sijaufuta kuwa wewe utakuja kuniletea hizo pesa yeye kasafiri, nashukuru sana kama umekuja kupunguza hilo deni..

‘Unamdai shilingi ngapi…?’ nikamuuliza

‘Milioni mbili…’ akasema.

‘Milioni mbili!!! …wewe, alikopa pesa zote za nini hizo..?’ nikamuuliza,na yeye akaanza milolongo mrefu, kumbe deni hilo limeanzia kipindi baba yake akiwa hai , yeye derva alikuwa akifika hapo, na kukopa bila baba yake kujua, kwa ajili ya kununua dawa,..au mahitaji amengine,  akawa analiendeleza hilo deni, akipata pesa anapunguza, ikafika muda anakopa tu…mara hiki au kile…

‘Kumbe hata hiyo ajenda ya kuwa anadaiwa ada ilikuwa ni sababu tu ya kupata pesa ili kupunguza hilo deni, na mara ya  mwisho ndio akaja kukukopa kwa ajili ya safari…na wewe ukamkubalia tu, kwanini ukubali na deni unaliona ni kubwa sana..?’ nikamuuliza.

‘Bosi mimi namuamini sana huyu mtu, analipa,..huwa anakopa analipa, ..sina wasi wasi na yeye, sema kwa sasa hivi naona kafikwa…sijui ana tatizo gani, kwani hata alipokuja kuniona alionekan hana raha…’akasema.

‘Na alikuambia anafanya kazi …maana kukopwa pesa nyingi hivyo, utakuwa na uhakika kutokana na kazi anayoifanya…?’ nikamuuliza.

‘Mimi sijui kazi yake,….ila anakuwaga na pesa nyingi, na siku nyingine anakuwa hana pesa kabisa, ndio anaishia kukopa…’akasema.

‘Sasa nataka uniambie ukweli, la sivyo nitawapeleka polisi…’nikasema kwa ukali.

 ‘Kwa kosa gani mzee, kwa mimi kudai haki yangu,..?’akasema akishangaa.

‘Kudai haki yako kwangu mimi, kwani mimi nilikuja kwako kukopa, au kuwa madhamini, wa huyo tapeli mwenzako …’nikasema.

‘Mzee mimi kama kuja kwako ningelifika kukuuliza tu, kutokana na taarifa hii ya ujumbe wa simu, vinginevyo, ningemsubiria tu mwenyewe akija, mimi sina shaka naye, nina uhakika jamaa atakuja kunilipa pesa yangu, mimi sijui kwanini kasema wewe ndiye utamlipia, hayo ni juu yako wewe na yeye…’akasema

‘Kwahiyo mnafahamiana naye sana..?’ nikamuuliza.

‘Ndio..nafahamiana naye kama mteja wangu..alikuwa akifanya shughuli zake anakuja dukani kwangu anakopa, analipa, yeye ni fundi mnzuri wa magari, na mimi napeleka gari langu analitengeneza vizuri,…namkopa, namlipa tumejuana hivyo tu, lakini undani wa maisha yake mimi sijui…’akasema.

‘Unamwaminije mtu kama huyo ambaye hujui wapi anapotoka maisha yake yapoje..nahisi kuna kitu kati yako na yeye..’nikasema.

‘Mzee,..mimi sina zaidi, najua ipo siku atakuja kunilipa deni langu, kama alikosea kukutaja wewe kuwa ndiye utamsaidia, kulipa, basi samahani mzee, hakuna shida, mimi ninayemdai ni yeye, sio wewe…ila aliniambia nitazipata kutokea kwako…’akasema

‘Alikupatia picha uniletee mimi..?’ nikamuuliza

‘Picha!...mzee picha gani …mara ya mwisho kuonana naye ni kipindi alisema anasafiri, na hakuwahi kunipa picha zozote, mzee. samahani je hizo pesa unazo, au huna, nilitaka kupunguza deni kwenye dafutari la madeni…’akasema akiwa anafungua fungua hilo daftari, nikalichukua hilo daftari, nikaanza kulikagua kweli niliona mtiririko wa hilo deni, tokea tarehe za nyuma, linalipwa linaongezeka..

Kiukweli, ikabidi nitoe pesa, japokuwa sio kwa kiwango hicho alichodai yeye…, lakini, zilinitoka, nikasema ahueni kumba nasaidi kitu ambach hata rafiki yangu angelikuwepo ningakifanya…baada ya kutoa pesa hiyo,..nilipofika nyumbani nikapokea ujumbe wa kushuru, na hali ikapoa,…ila moyoni nikaahidi kulifuatilia hilo mpaka nijue mwisho wake, hawawezi kuchukua pesa yangu hivi hivi tu...

Kiukweli badae kukapoa, sikuwahi kuona rabsha nyingine kutoka kwa huyo kijana hadi karibia mwaka mnzima, kuonyesha kweli alikuwa kasafiri,...Tatizo kubwa lilikuwa kati yangu na mke wangu,  familia yangu hatuongei na huko kwa shemeji nako nikawa najiiba siku moja moja..nikifika huko kuna wakati naambulia matusi, kuna wakai tunaongea..siku zinakwenda.

************

Muda ukafika Soldier akaja nyumbani kuoa…

'Ehe, unataka kuoa mchumba unaye  tayari au tukusaidie kutafuta?' nikamuuliza

'Ninaye tayari keshakubaliana na mimi..nilionana naye kwenye safari zangu...'akasema

'Wa huku huku au huko maeneo mengine?' nikamuuliza
'wa huku huku mzee..'akasema

'Ni nani au anatokea familia gani..?' nikamuuliza.

'Ni kutoka familia ya Matatizo,...'akasema

'Nani...wewe una laana...'nikasema kwa mshangao, tulikuwa tunakuala hamu yote ya kula ikaisha..Maana hiyo familia, haina maelewano na familia yetu tokea kizazi na kizazi,...ila huyo binti yao, alikuwa msichana mnzuri tu...mwenye tabia nzuri wengi wanamfahamu.

‘Kijana..hilo unalolitaka ni laana, unajua mababu watatulaani, maana haijatokea hata siku moja familia yetu kwenda kuoa huko au wao kuja kuoa kwetu, ni mwiko....ni wewe wa kwanza..’nikamwambia.

‘Basi mshukuru kuwa mimi nimeondoa hilo tatizo,..hayo ni mambo yenu ya kizamani, tufike mahali tuachane na tabia hizo za chuki...sasa tuwe marafiki…’akasema.

Pamoja na sisi kukubali, upande wao ilikuwa nishida, kuna kaka yake na huyo binti, ni aadui mkubwa sana wa familia hii, na waliwahi kugombana na soldier, na uhasama wao ukawa wa kudumu,  haya mwanangu anataka kuoa huko..ilikuwa ni kazi kweli, lakini watoto wameshapendana, utafanyaje..

Huku na huko ikafikia hatua, inabidi maadui wakae meza moja,…kujadili maswala ya ndoa huku tumekunjiana sura…huwezi amini, tukaja kukubaliana na tendo hilo likafanya familia yangu na familia ya huyo adui yangu wa siku nyingi, tuweze kusahau ugomvi wetu na kuwa kitu kimoja, kwa ajili ya kufanikisha sherehe ya watoto wetu..ila huyo mtoto wao mkubwa, alisema moja kwa moja yeye, na familia hii ni kama maji na mafuta..

 Kiukweli hata mimi nilikubaliana na familia hiyo, ilimradi tu yaishe, kumrizsiha kijana wetu maana alishafikia sehemu kijana wetu hataki kuoa tena, sasa alipokuja na ombi hilo, tukamkubalia, ila pale alipotaja ni nani anataka kumuoa kutoka kwa familia gani, hapo, ilikuwa ni kazi kutushawishi.
Familia hiyo tulikuwa hatuelewani nayo tokea enzi, kisa ni ardhi, mipaka, na huko nyuma mababu zetu waliwahi kupigana na kumwaga damu, kwahiyo kukajengeka visasi…

 Mwisho wake, tukakubali tu, watoto wakaoana,..na haikupita muda, mara taarifa inakuja, kuwa Soldier ni miongoni mwa watu waliochaguliwa kwenda vitani kwa kupitia mikataba ya kimataifa,..safari hizo wengi wa maaskari wanazitaka sana kijana wetu alikuja kutupatia hiyo taarifa akiwa na furaha nyingi tu…, maana japokuwa ni hatari lakini ukirudi angalau unaweza kuitwa mtu..

Ilikuwa sio furaha kwetu kama wazazi, hasa mimi ninayefahamu ni nini maana ya vita, lakini moyoni, kimaongezi, nilikuwa nawaambia watu huo ni uzalendo. Na ukumbuke ndio kijana wetu katokea kuoa, hata miezi mitatua haijaisha,..tuliombea angalau atupatie mjukuu, sasa ndio anamuacha mkewe mikononi mwetu, anakwenda vitani, na vita ni vita…mama yake alikataa kata kata, lakini atafanyaje, mwisho wa siku tulikaa pamoja kama familia tukamuombea duwa, akapata baraka zetu, akatuachia mkewe…

************

Mwaka ukapita , na sasa familia ya mkewe kijana wetu ikawa inaleta malalamiko , kwanini tumemuoa mtoto wao anakaa tu na wakwe, kwani sisi ndio tulimuoa,… mume wake yupo wapi,… kama kafa huko vitani kwanini hatusemi, binti yao arudi kwao,....ikawa ni shida kweli…lakini tunamshukuru mungu kwani mkwe wangu, binti huyu  alijitahidi sana kuvumilia kwani alikuwa akimpenda sana mume wake..

Mimi kama kawaida yangu nilijitahidi kuwa karibu naye, inafika sehemu najifanya sio mkwe, ilimradi tu asijisikie mpweke, nahisi tabia kama hiyo, yeye na wengine, ndio wakaanza kuitafsiri vibaya, lakini ndio tabia yangu ya ucheshi,....ndio siwezi kukataa, kuwa katabia kwa kuchepuka sikuweza kukazuia..lakini sio mkwe wangu!

Basi mwaka wa pili tukapokea taarifa kuwa kikosi kilichopelekwa huko, kimevamiwa na kuna baadhi ya askari wetu wameuwawa….hapo tukawa tumbo joto, tukawa tunawasiliana na makao makuu, laki hakukuwa na taarifa rasmi…, lakini tetesi zikaja kuwa miongoni mwa waliouwawa ni mwanangu…siku hiyo ilikuwa ni kilio..nyumba ikabadilika,..mama, mke wa kijana wangu….mimi kiukweli niliiona taarifa hiyo kama sio kamilifu.

Nilijua akilini mtoto wangu hajafa, na kama ameuwawa, basi amekufa kishujaa,..si yupo vitani…ndio nitaumia sana moyoni, lakini ndio mungu kapanga iwe hivyo utafanyaje…, lakini hata hivyo, jambo kama hilo likitokea ni lazima tutapewa taarifa iliyo rasmi,hatukuwahi kupokea taarifa kama hiyo, ni tetesi tu, uvumi tu..siku zikaenda..

Siku moja,…nikapata safari ya kwenda nchi ya jirani,.. jirani yetu ana wakimbizi wengi wa vita, unajua vita vinavyoendelea huko, kwahiyo huko kuna kambi za wakimbizi, ..nilifika huko kwa mualiko, kama kiongozi mmojawapo,..na tulipofika huko nikawa mmoja wa waongeaji, …mimi ni mpiganaji mstaafu kwahiyo nafahamu mambo ya kivita..ndio maana walinipatia nafasi hiyo...

Baada ya vikao, ..kukutana na watu ikafika muda wa kujipumzisha, kwahiyo nikaelekea hotelini kwangu,..nilipofika nikahisi nywele zinanisisimuka,..ni hulka yangu tu, ikitokea hivyo, naweza kukutana na kitu kisicho kuwa cha kawaida, ningekuwa vitani, ningechukua ‘cover..’ kujihami, lakini nipo uraiani,..nikajipa moyo, ..nikaangalia huku na kule,..baadaye nikajirizisha, na kuelekea hotelini kwangu.

Nikiwa natembea kwenye corido za hiyo hoteli,..mbele ya chumba changu niliona mtu kakaa nje ya mlangoni wa chumba changu,..kwanza nilitaka kurudi kuwauliza mapokezi, ni nani huyo, ..akili ya hatari imeshanicheza, lakini nikasema labda ni muhudumu tu, nikatembea kwa tahadhari hadi pale mlangoni.

Kwanza nilihisi mwili ukinicheza,…ni mtu au ni jinni…kafikaje hapo, kapitaje kule mapokezi, maana kuna sheria ngumu hapo hotelini, huwezi kuja kumuona mtu hapo mpaka huyo mwenyeji apewe taarifa, akubali, na wanapingwa sana kuingia humo hotelini ni wakimbizi, na jinsi nilivyomuona huyu mdada, yawezekana akawa na mkimbizi, vinginevyo, basi sio binadamu!

Nilijiuliza maswali mengi kichwani huku natembea mwendo wa taratibu, kuvuta muda, kabla sijafika pale mlanngoni, nikajiuliza ni kwanani wakati nachukua ufunguo pale mapakozi, wahudumu hawakuniambia kwua nina mgeni, labda sio mgeni wangu, sasa ni kwanini aje kukaa kwenye mlango wangu..…yawezekana ni mtego…hapo nikasimama kidogo..

Lakini baadae nikaanza kutembea kumkabili huyo mtu, kwani ni mwanamke..nilivyomuona kwa mbali..hiyo hoteli ni kubwa,…ina vyumba vingi vya wageni,…nikasogea hadi kwenye chumba changu, nikamuangalia huyo mtu…

Alikuwa mdada, kajifunika kitu kama shuka nyeupe, imechakaa,..na kuna sehemu ya nyingine kwenye hiyo shuka ni kama imeungua,…na kuna alama za damu damu, hapo mwili ukazizima, damu zimetokea wapi,  na ule mkao ni wa masikitiko, mtu anakaa miguu inakuja karibu na kichwa, kainama hataki kuniangalia… inatia huruma kumuona, ..

Na kitu kilichonivuta hisia zangu zaidi ni pale nilipoangalia pembeni yake, kuna kitoto kichanga..

NB: Tuendelee baadae.


WAZO LA LEO: Kuna watu maisha yao ni Ujanja ujanja, kuwarubuni watu, kuhadaa kudanganya, kutumia mbinu za mdomo kupata kipato kutoka kwa wengine..ukimuuliza anasema, anatumia elimu yake, anatumia ujuzi wake kupata riziki…huo ni wizi, tujaribu kupata kipato halali, kwa njia halali, zisizo za hadaa, mtu alipwe kutokana na huduma, tusiweke mitego, mfano utakuta watu wanaandika, mwishoni masharti kuzingatiwa wakiwa wameka mitego kuwa ukikosea kidogo, pesa yako imeliwa. JAMANI tumuogope mungu.
Ni mimi: emu-three

No comments :