Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, March 10, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-14


‘Lakini mzee mimi sitaki shida, …sipendi mabaya yakukute, …tumalizane tu…, si unajua cha kufanya, ada tu…basi usisahau, samahani mzee kwa usumbufu, kwaheri, lakini usisahau….’akageuka na kuanza kuondoka huku anaimba imba wimbo...

Mimi pale nilibakia nikiwa nimeishiwa nguvu….akili ikawa inawaza mengi sana,...


‘Sasa hili ni tatizo…’Mzee mzima alishika kichwa.

Mzee alibakia hivyo akiwaza, hakujua kuwa muda umepita sana,..., na mara alishtuka mtu anamshika begani, ..kwa akili za haraka haraka, akajua ni yule kijana karudi tena..., akasimama kwa hasira, sasa akitaka kumpiga vibao...hasira zilikuwa simemzonga, ....

'Umerudi tena, sasa....' akakatisha kauli yake alipoona mtu mwingine akiwa kamsimamia mbele yake.

‘Mzee vipi mbona upo hivi…na kule nyumbani vipi, mbona naona watu kuna nini kimetokea, mama yupo wapi..?’ ilikuwa sauti ya Soldier

Tuendelee na kisa chetu....

**************

'Mwanangu mbona umekuja,....?' nikamuuliza mtoto wangu maana alishatupigia simu kuwa wapo kwenye mafunzo, na itachukua muda kwa wao kurudi nyumbani...

'Nimeomba ruhusa ya dharura...'akasema

‘Ya dharura, kuna tatizo gani…?’ nikamuuliza kijana wangu.

‘Ndio baba, twatarajia kusafiri..na nilitaka kabla ya kuondoka nihakikishe nimefunga ndoa, kuna kitu kaniambia mchumba wangu kimenifanya nirudi, na ikibidi tufunge ndoa haraka iwezekanavyo...’akasema.

'Mbona sisi hatuna habari hiyo ni nani kakuambia...?' nikamuuliza

'Mimi huwa nawasiliana naye mara kwa mara..japokuwa mawasiliano ya shida, ila kuna namna natumia...'akasema

‘Mhh, mimi sielewi lolote, na kama kuna tatizo kwanini wazazi wake hawajatuambia..?’ nikamuuliza

‘Ndio maana mimi nimeona, ili kumaliza yote haya, nije nifunge ndoa...baba niambia ukweli, mama hajambo, ngoja nikamsalimia…’akasema, na mimi nilitaka kumzuia, lakini nikaona haina haja.

Kiukweli ndoa hiyo aliyotaka kijana wangu haikufanyika, kwani binti alimtaka kumuoa alikutana na mtoto wa rafiki yangu, akahadaiwa na kuja kuchumbiwa na kijana huyo, nikamshauri Soldier aachane naye, nahadithia tukio hiki ili muone uhasama ulivyokuwa unadhidi kati yangu mimi na familia ya rafiki yangu ambayo nimeachiwa mimi.

Soldier akarudi jeshini akiwa hana raha, kamkosa mke, mchumba wake aliyempenda sana , na kwasabbau hiyo akaachana kabisa na wazo la kuoa, na hata nilipojaribu kumshawishi aoe tena,akasema kwa hivi sasa hafikirii kuoa tena, na miaka ikapita…

************

Turudi huku nyumbani kidogo …., shemeji yangu akawa anaendelea kunywa, mpaka watu wakamzoea kama mama mjane mlevi, kisa ni mimi, kisa ni hayo niliyokubali kuyafanya kwa ajili ya rafiki yangu.

Ukumbuke Dereva alishaahidi kunifanyia jambo, kwa vile nimemfanya mama yake abadilike na kuwa hivyo alivyo, mama mlevi…na hata nilipojitahidi kumpa pesa kidogo ya ada, hakurizika, kila siku akawa anakuja na jambo jipya, ..na kila akija huja na mambo mengine yaliyojaa vitisho ndani yake, mpaka nikamzoe, nikaona ni vitishio tu.

Na kweli kumbe alikuwa kasafiri, kazi sasa ikawa kumtafuta huyo anayefanya hiyo kazi ya kunitishia kwa jina la huyo kijana...ina maana kuwa Dereva katafuta msaidizi wake..na hiyo inazidi kuniweka pabaya kuwa sipambani sasa na mtu mmoja, huenda napambana na kundi la watu..na kiongozi wao ni dereva.

Siku moja nikiwa nimetokea kwenye vikao vyetu...huko tunakula , tunakunywa, unajua tena mambo ya kisiasa...wakati nipo njiani, wazo likanijia, nikaona nimtembelea shemeji,...ni muda sijafika kwake, niliamua nifanye hivyo, japokuwa nilikuwa nakiuka makubaliano yangu na rafiki yangu, na nilifanya hivyo ili kumridhisha mke wangu, kwani ilishafika muda hatuelewani...nilikuwa nasiki tu jinsi gani huyo mjane anavyolewa,...

 Siku hiyo ndio nikaamua kwenda kwake,  nipofika nilimkuta huyo mama mjane akiwa keshanunua vilevi vyake, nilisikia kuwa japokuwa analewa, lakini hunywa akiwa nyumbani kwake,  kwahiyo siku nilipofika, nilimkuta tayari ameshanunua vilevi vyake, anakunywa,..aliponiona tu…

‘Ehee leo umejileta mwenyewe..hawara yangu…’akasema alikuwa tayari ameshaanza kulewa.

‘Shemeji tuyache hayo, usitake kuchokoza mambo..’nikamwambia

‘Nichokoze mambo gani,  wakati nyie ndio mumenianza, kuanzia sasa wewe ni bwana yangu, sio yule wa kunipa mada nikalewa, nikapoteza fahamu, nataka uwe bwana wa kiukweli kweli,… 'akasema

'Shemeji naona haupo sawa, ....'nikasema nikitaka kuondoka.

'Hahaha,...najua kawaida yenu, kwa kuvia wake za watu muwapoteze fahamu kwanza ndio mfanye mtakavyo, au sio...hivi hivi unaogopa, ....ukumbuke wewe ndiye uliyeamua kumchangia mume mwenzako, unasikia, ...sasa ni hivi leo hutoki hapa mpaka unitimizie haja yangu…’akasema akiwa anayumba yumba.

‘We shemeji niache kabisa, haya yaliyopo sasa yameshanifika shingoni, usianzishe mengine..’nikasema nilishamuona hana jema, sasa nikawa naondoka akanishika shati,..kiukweli siku hiyo hata mimi nilikunywa kidogo kwenye pati zetu za kikazi…, na kilichotokea hapo,…siwezi kusimulia, lakini ndio ikawa ukurasa mwingine ambao …ninaujutia sana…hadi leo.’akatulia

Hali hiyo ikiwa inandelea kwa siri sikujua kuwa kuna mtu ananichunguza nyuma ya kisogo, na siku moja nipo ofisini kwangu, muda huo nimeshakuwa kiongozi tena…, mara nikaletewa bahasha na ndani yake kuna picha..nikashangaa ni nani huyu kaniletea bahasha yenye picha, basi kwa vile ni kiongozi nikajua labda ni picha za mikutano na kazi kwa ujumla.

Nilifungua na picha ya kwanza, ilinifinya nishutuke na kujikuta nimezirusha hizo picha chini ni kam vile umeona kitu cha kutisha, sikuamini,….nikaangalia huku na kule kama kuna mtu ananiona, hakukuwa na mtu karibu, nikaziokota zile picha kwa haraka, na kuzifutika kwenye meza, nikawa natoa moja moja…

‘Aaah, ni nani kafanya hivi…nitamuua…’nikasema huku naanza kuzichana chana,..zile picha na kabla sijamaliza simu yangu ikaita, nikaipokea nikiwa na hasira.

‘Naona sasa hivi utakuwa unazichana-chana hizo picha, kuna nakala kama mia hivi..ni gharama kuzitengeneza, lakini lazima kazi hiyo ifanyike, na gharama hiyo lazima irudi,... unasikia sana kiongozi,..natumai hutapenda wananchi wako wazione hizo picha…na zaidi mke wako, ..au wakwe zako, au watoto wako…na …shemeji yako ambaye umemgeuza nyumba ndogo…’ nilitaka kukata simu lakini.

‘Sikiliza mzee kwa makini, ulishindwa kuuza kiwanja, sasa utakiuza…nahitajia shilingi laki nane tu,..' akasema

'Wewe una wazimu sikupi hata senti moja...'nikasema kwa hasira.

'Hahaha..kweli eeh, ngoja tuone ubabe wako,....nasema hivi utatoa laki nane,..kamili..kiwanja chako ukiuza ni milioni moja na nusu, hizo laki kadha itakuwa kifuta jasho..' akasema

'Kwa kazi gani uliyonifanyia au ndio utapeli wenu ,....nikuambi haupati kitu wkangu fanya upendavyo...'nikasema nikitaka kukata simu.

'Unajifanya mjanja mzee,...hiyo laki nane ni ya kuzinunulia hizo nakala za picha..umeniskia,..nilikuonya mapema , na naendelea kukuonya kwangu mimi sipungukiwi na kitu, nikifanya utakavyo, nitawapelekea vyombo vya habari, au sio..lakini kwanza familia yako..mke wako..sasa jiweke tayari kwa mapambano…’akakata simu.

Nilijaribu kuipiga ile namba lakini hakukuwa na namba, alipigia kwenye namba isiyojulikana..

‘Ni huyu mshenzi..ngoja nikaongee na mama yake,..’nikasema na kutoka hapo ofisini nikiwa na hasira, na wakati natoka mke wangu akaniona, ofisi yangu haipo mbali na nyumbani,..
Hakusema kitu, na mimi sikumjali, tulishafikia sehemu hatuna masikilizano kwa kipindi hicho japokuwa kiukweli alijitahidi sana kuwa name bega kwa bega hadi nikapata huo uongozi…

Nilifika kwa shemeji na kama kawaida yake nilimkuta akiwa na chupa anakunywa, nilimuangalia nikamuonea huruma,…nilitaka kugeuka kuondoka, akasema;

‘Umenichoka sasa eeh, mimi si mwanamke mlevi,...mwanamke wa kuchangiwa na wanaume wengi..nina thamani gani tena mimi, mama mjane , mlevi....sasa masikini... lakini nikuambie kitu, ukumbuke ulevi huu chanzo chake ni nyie, sikupenda niwe hivi,…,…au …?’ akauliza.

‘Shemeji, nakuomba umkanye mwanao, anachotaka kukifanya sasa hivi kimevuka mpaka, nakuomba ukae naye uongee naye, atakuweka uchi mbele ya jamii.’nikasema.

‘Aniweke mimi uchi hahaha, nikae uchi mara mbili..mlichonifanyia nyie si sawa tu na kuniweka uchi,..nina tahamani geni tena , kila mtu akiniona ananinyoshea kidole kuwa nimemsaliti mume wangu..naonekana mimi ndiye nilitenda hilo….’akatikisa kichwa.

‘Lakini shemeji twende mbele turudi nyuma…kama mume wako asingelikuja na hilo wazo ungelikuwa na kijana kama huyo, mfano mume wako angeamua kukaa kimia,…mengine tumuechie mungu, tu, mimi nazidi kusema unisamehe, na umusamehe mume wako…unachokifanya sasa cha ulevi, ni kujiadhibu tu mwenyewe kwa kosa ambalo hujalifanya..’nikasema

‘Leo ….nimemkumbuka sana mume wangu..pamoja na mengine nilimpenda sana mume wangu kaniacha, nateseka, kiniachia mtihani, nitafanya nini mimi jamani, nimewakosea nini jamani, ..najishi mpweke, najihisi kinyaa, nafanya machafu…sasa natamani nimfuate huko alipo,…mtoto sasa naye ananipanda kichwani, anadai nimuambie ukweli…’akasema

‘Umuambie ukweli gani?’ nikamuuliza
‘Anasema watu wanamuambia kuuwa huenda baba yake wa damu sio mume wangu ….aah, inanipa shida sana, ndio maana nimeamua kulewa tu,..nitamjibu nini mimi,…nimemwambia aachane na hao watu, lakini yeye anasema ni lazima autafute ukweli, na ataupata tu…mimi kiukweli nitamwambia nini huyu mtoto, maana hata mlivyonifanyia mimi sijui, nitaanzaje kumuambia…’akatulia

‘Oh, hii sasa imekuwa ni balaa, …mtoto wako anaharibika, Unajua alichokufanyia mwanao..?’ nikauliza

‘Mimi sijali atakachofanya…nimemwambia afanye atakavyo, mimi nimeshachoka..’akasema.

‘Mtoto wako kajiingiza kwnye utapeli…ananitishia mimi akidai mapesa mengi, na moja ya jambo analonitishi anlo ndio hilo, kuwa ….mimi ni baba yake, na tena katengeza mapicha mabaya…’akatulia

‘Mapicha, mapicha gani hayo…?’ akauliza.

‘Yaani hata siamini,..unajua..aah sijui walipigaje hizo picha…’nikawa naangalia mle ndani kama kuna sehmeu mtu anaweza kujificha na kupiga picha, sikuweza kupaona nikajaribu kuchunguza huku na kule kama kuna vyombo vya kunasia matukio humo ndani, sikuweza kuona.

‘Unatafuta nini…?’ akaniuliza

‘Kapigaje hizo picha…?’ nikauliza

‘Nani sasa,…mimi sijui, maana hata hizo picha zijaziona, huenda umekuja na stori zako za uwongo, nitaaminije...?’ akaniuliza.

‘Hili sasa ni balaa, ..unasikia hizo picha zikisambaa tu, nime…na hata wewe..., mwambie akupatie hizo picha, vinginevyo, utaadhirika, sio mimi tu….na wewe pia…’nikasema na yeye, akasema;
‘Ni nani katupiga picha…kamwambie aje atupige tena, mimi sijali, wewe ndio utaumbuka, …zipo wapi hizo picha..?’ akauliza akionyesha kutokujali.

‘Ninajua ni mwanao…hakuna mwingine anayeweza kufanya jambo kama hilo maana alinitishia kuwa atanifanyia kitu kibaya kama nisipo mpa, pesa anazohitajia…’nikasema

‘Lini kafanya hivyo,…maana mtoto wangu hayupo , aliniaga anasafiri, akawa anahangaikia paspot, kaipata, sasa …hapana huyo sio yeye, .na hata hivyo mtoto wangu hawezi kufanya jambo la kuniadhiri mimi mama yake mimi namfahamu sana mwanangu...hilo nalipinga….’akasema.

‘Kanipigia simu yeye mwenyewe…’nikasema.

‘Sio yeye, mimi nakuambia ukweli mtoto wangu kasifiri, jana tu nimeongea naye, kasema amefika salama, yupo huko nchi za wenzetu…’akasema.

‘Haiwezekani…mtoto wako atakuwa ni jambazi wa kimataifa…na kama anatumia watu, ..ohooo., mimi nitalifikisha kituo cha polisi, watamshughulikia,….’nikasema

‘Hiyo utajua mwenyewe, ila ninachokuambia ni kuwa mtoto wangu hayupo, kuna kazi aliahidiwa, wanakwenda kujifunza mambo ya kuhudumia wakimbizi…kwahiyo hata akimaliza hayo mafunzo,…atakuwa mtu wa kuzunguka zunguka,..’akasema.

‘Sasa ada alikuwa anataka ya nini..?’ nikamuuliza na mama yake akawa kakaa kimia kama anawaza jambo, nikajua hilo jambo limemgusa sana.

Nikatulia kidogo, ndio nikakumbuka jambo…

‘Vipi ile kadi na diary ya mumeo umeshanitafutia, unajua ile akiipata huyo mtoto wako anaweza kuharibu kila kitu…?’ nikamuuliza.

‘Nimetafuta nyumba nzima sivioni hivyo vitu na vilikuwa pale pale…na funguo ninazo, lakini …hata sijui ni nani alifungua lile kabati, hawakuchukua kitu kingine...ina maana huyo mtu anajua ni nini anakitafuta, nina wasiwasi na wewe…’akasema

‘Ningevichukua ningekuulizia, …una uhakika hukuvihamisha, maana hilo sasa ni tatizo kubwa sana, utanifanya niishi kwa mashaka…’nikasema.

‘Mimi sijui…sijawahi kuvihamisha,…sijui ni nani kavichukua…’akasema na kunifanya sasa mwili uanze kutetemeka na akilini nikawa nakumbuka maneno ya dereva:

Sikiliza mzee kwa makini, ulishindwa kuuza kiwanja, sasa utakiuza…nahitajia shilingi laki nane tu,..kamili..kiwanja chako ukiuza ni milioni moja na nusu, hizo laki kadha itakuwa kifuta jasho..ununue hizo nakala za picha..umeniskia,..nilikuonya mapema …na nilikuambia nini,… ipo siku nitaujua ukweli…sasa jiweke tayari…’’

‘Nimekwisha….lakini nakuambia, mimi ni askari, mwanao si anataka kupambana na mimi, tutaona…’nikasema na kutaka kuondoka, yeye kwa haraka akanishika…na kabla sijajitetea, mlango ukafunguliwa,..

‘Nilijua tu umekuja huku…haya niambie ukweli, hujatosheka na umalaya wako, umeamua kunitumia na mpicha yenu michafu…eeh, sasa umevuka mipaka, hii mipicha nitaifikisha kwa mabosi wako, serikalini…’’

Nilibakia nimeduwaa…..na mara ujumbe ukaingia kwenye simu yangu, hakuna namba,..nikaufungua

‘Hapo ndio nimeanza….nahitajia hizo pesa haraka iwezekanavyo, uza kiwanja…na kutokana na gharama kuongezeka, sasa nahitajia milioni moja…’

NB: Ni nini kitatokea


WAZO LA LEO: Mtoto umleavyo ndio akuavyo, walisema wahenga, lakini watoto wengine huharibika kutokana na matendo yetu wenyewe, kwani dhambi nyingine hulipwa hapa hapa duniani, kama ulimfanyia mwenzio ubaya, ipo siku utalipiziwa kwa namna hiyo hiyo, na huenda mikono yako, mtoto wako au hata ndugu yako akawa chanzo cha kulipiza dhambi hiyo uliyomtendea mwenzio, kama unakumbuka nenda haraka ukamuombe msamaha kabla milango ya toba haijafungwa. Tumuombe mola wetu atuepushie madhambi hayo…

Ni mimi: emu-three

No comments :