Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 8, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-12



Nilisoma kile kilichoandikwa, ..aliandika kila kitu,…sijui alikuwa na maana gani kuandika hivyo, naona baadae aliona kakosea, akafuta futa kwa kuchora chora juu yake, karibu ukurasa mnzima alindika mipango yake, baada ya kugundilikana kuwa hatazaa… na jinsi gani ya kuutekeleza...

'Rafiki yangu atanisaidia kwa hili...amekubali,...

Hata kabla sijamaliza kusoma, nikainua uso kumuangalia shemeji, ambae alikuwa kavimba kwa hasira…kanitolea macho…sijawahi kumuona shemeji katika hali kama hiyo..

Nilishindwa hata kumuangalia shemeji usoni, nikazuga zuga kuendelea kusoma, lakini akili yangu haikuwepo hapo tena,..na hakukuwa n anjia nyingine ya kumdanganya,..nikageuza uso pembeni, na mara shemeji akaninyang’anya hiyo diary na kuwa nayo mkononi mwake,mimi nikaishia kusema;

‘Kwanini kafanya hivi,….kaharibu…’ nikasema

‘Sasa ..kaharibu eeh…mliniona mimi mjinga sio..oooh, …aak…’akasema shemeji kwa sauti nzito, na alionekana kama hayupo sawa.

‘Lakini shemeji unajua mume wako alikuwa anajaribu kutunga story, unaona hapo….kakosea akafuta, kwani wewe unafikiria nini…?’nikajikuta nimeongea, na shemeji yangu akawa ananiangalia kwa macho yaliyojaa hasira, na hata kabla sijasema kitu akadondoka chini, …na kupoteza fahamu. 

Oh, tatizo, shemeji amekuwa hivi, kupoteza poteza fahamu, lakini hali hiyo ilishaanza kutoweka, sasa kutokana na hili, kapoteza tena fahamu, nitasemaje kwa watu…

Nikajikuta kwenye wakati mgumu kweli…, maana hata nikimuita docta, atauliza ilitokeaje,…nikaona ngoja nifanye kazi ya ziada, nikaanza kumfanyia huduma ya kwanza,…ya kifuani, maana tukiwa jeshini hayo yote tumefundishwa…nilifanya mara tatu, haikuleta matunda.

Nikaona sasa nitumie njia nyingine ya kumpuliza mdomoni hapo ni mdomo kwa mdomo…nikasita, lakini nikasema, …..ni lazima nifanye, kumuokoa huyu mtu, nikashusha mdomo wangu, mara ya kwanza ikaleta matumaini, mara pili…

Mara mlango ukagongwa, na haraka ukafunguliwa,…na wakati huo shemeji alishaanza kuzindukana, kainua mkono kama anataka kunisukuma…

Kwa jinsi nilivyokuwa, nimemuinamia huyo shemeji yangu, na yeye akiwa kainua mkono yake akinishikilia kifuani kunisukuma…na momo wangu upo karibu yake,na kwa jinsi nilivyokuwa nimekaa , mtu akija haraka anaweza kujua hawa watu wapo kwenye mapenzi yao…na kwa vile huyo mtu aligonga kwa haraka , sikuweza kujiinua na kujiweka vyema, na tahamaki nakutana uso kwa uso na mke wangu..

‘Oh..kuna nini hapa, yaani kumbe ndio zenu…?’ akauliza na kabla sijamjibu akageuka akiwa kashika kichwa, na kuondoka kwa haraka, nikabakia nimeduwaa,…baadae nikazindukana na kutoka nje kwa haraka, sikumuona, ina maana atakuwa kakimbia,..au ..sio yeye, haiwezekani atoweke kwa haraka hivyo…nikatoka pale na kutembea huku na huku, sikumuona mtu.

Nilirudi ndani na kumkuta shemeji kakaa..keshazindukana,…hakutaka hata kuniangalia machoni, mimi nikasogea ili nimsaidie ainuka, akaniashiria kwa mkono kuwa hataki hata kuniona,niondoke

‘Shemeji bado haupo  vyema…’nikasema

‘Ondoka…nikikuona nasikia kichefu chefu..ondoka, ina maana nyie wawili mlipanga kunifanyia hivyo…wewe na rafiki yako…sitaki kukuona tena machoni mwangu…’akasema akigeuka pembeni.

‘Lakini shemeji,..ni vyema kwanza ukajua ni kwanini hayo yalitokea…’nikasema

‘Hakuna sababu ya msingi, hakuna utetezi wowote ambao utaweza kuniondolea aibu hiyo na uchafu huo mlionifanyia, kwanini….’akasema akianza kulia.

‘Shemeji ngoja nikuulize, kwani wewe ulikuwa humtaki mtoto..hebu niambie ukweli..?’ nikamuuliza akageuka na kuniangalia kwa macho yenye hasira, akatikisa kichwa kusikitika,…na alichosema ni hiki:

‘Mimi na mume wangu tulikuwa kwenye kiapo cha ndoa, kuwa waaminifu, na kusaidiana kwa shida na raha, ni wapi ulisikia kitendo kama hicho kimefanyika, au nyie ni watu wa pekee, mnaochangia wake zenu..kwahiyo hata wewe ulikuwa radhi mkeo atembee na mume wangu au sio…” akaniuliza

‘Sio hivyo shemeji, hatukuwa na lengo kabisa…na sivyo unavyofikiria wewe, nia na lengo letu ilikuwa….’kabla sijamaliza, akasema

‘Sitakia maelezo yake tena,..sitaki kusikia kitu tena, ina maana mimi naishia kwenye maombi, ibada, nafunga, kumuomba mungu, ili tupate mtoto kumbe mwenzangu ana mipango yake.. mimi nilijua mungu hajapenda kutupa mtoto, na aliponipatia nikajua ni maombi yangu yametimilizwa,..’kumba kuna ushetani umechezwa…’

Akashika kichwa na kujiinamia

‘Shemaji, nakuomba unielewe, mume wako hakutaka kabisa kukuvunja nguvu, hakutaka kukuambia kuhusu afya yake, na alitaka akupatie zawadi muhimu ya mtoto, alishajua kuwa hataishi ..na hata akiishi, hata weza kupata mtoto, ndio akaona aniombe tufanye hivyo…’nikasema

‘Maana nyie ni miungu, mnaweza kujibunia mbinu zetu, mwenyezimungu angalitushauri tufanye hivyo kama ingelikuwa ni njia sahihi, …mnataka nifanyeje sasa, huyo mtoto nitakuwa nikimtimaje, je akija kugundua ukweli atanionaje mimi,..kwakweli mnanipa wakati mgumu, natamani kabla hajaniuliza hayo maswali niwe nimeshaondoka hapa duniani…’akasema

‘Shemeji usifikie hapo..kwanini unawazia hivyo..muhimu ni kuliacha kam lilivyo, tumuombe mungu atusamehe, na kamwe usija kumuambia chochote mtoto wako…’nikasema

‘Nilijua mungu hajapenda..na nilipopata uja uzito nikafurahi sana, lakini kumbe, kwanini ,…kwanini tumkufuru mungu…haya kama alikuwa na tatizo kama hilo kwanini hakuniambia, ningemshauri njia sahihi..sio ya madhambi kama hayo…kwakweli shemeji sitaki kukuona tena maishani mwangu, na huyo rafiki yako kama angelikuwa hai, sijui kama …ningeishi naye tena…’akasema akilia.

‘Shemu, huu sio muda wa kumlaumu marehemu, muhimu ni kumuombea, na hayo aliyafanya kwa ajili yako,…akili yake ilifikia hapo na akaona hiyo ndio njia sahihi,  hakupenda kabisa iwe hivyo, hata mimi aliponiambia nilikuwa na wakati mgumu, lakini ….nilimuonea huruma sana rafiki yangu basi ikabidi nifanye alivyotaka yeye, vinginevyo, nahisi angezidi kuwa na wakati mgumu…’nikasema

‘Kwahiyo mimi ni hawara wako, au ni mkeo..au ni nani kwako..?’ akaniuliza akiniangalia usoni.

‘Shemeji..hayo hayana msingi kwasasa maji yameshamwagika hayazoleki…, nakuomba tafadhali..hifadhi ulimi wako, itunze hii siri kama alivyotaka marehemu,…tafadhali sana,… huyo ni mtoto wenu wawili, hata iweje, usije kusema tofauti, na hakikisha ushahid huo umeuharibu kabisa…nakuomba nipo chini ya miguu yako…mtoto wenu huyo ni halali kabisa,…’nikasema huku nikimpigia magoti.

‘Tatizo sio mtoto, tatizo ni hicho mlichonifanyia mimi…, usikwepeshe hoja ya msingi, mtoto wa watu hana kosa,kosa ni matendo yenu mabaya,..najua mwenyezimugu kama alitaka tuwe na mtoto, angezaliwa kihalali tu, nyie mkatumia njia ya haramu, mkaona kuwa kitanda hakizai haramu…niwaambie ukweli mimi ninawachukia,…’akasema

‘Usiseme hivyo shemeji muombee mema mume wako…’nikasema

‘Nakuomba utoke humu ndani haraka, kabla sijakutapikia…’akasema akiwa kakunja uso kwa hasira

‘Kabla sijatoka niahidi kitu shemeji…, kama hutaweza kuvichoma hivyo vitu moto, nipe mimi niondoke navyo,  nikavichome moto maana vikifika mikono isiyo salama, itaharibu kila kitu, nakuomba….tafadhali,..niahidi shemei kuwa hii siri haitavuja kamwe…’nikasema na yeye….

Akatikisa kichwa, akawa kama anatabasamu, …huku uso ukiwa na huzuni, akaniangalia usoni, huku akiendelea kutikisa kichwa, na kusema;

‘Kwa hili utajuta….’akasema hivyo, akiwa kavishikilia vile mkononi kama anaviinua juu kunionyesha, halafu akageuka kunipa mgongo…

‘Utajua kwanini ulikifanya hicho kitendo….’akasema hivyo

Akakimbilia chumbani

‘Nitajuta…’nikabakia nikisema maneno hayo, nikiwa sielewi shemeji ana maana gani.

***********

Nilibakia pale nje, ….nikitamani hata niingie ndani nivichukue vile vyeti na ile diary,..lakini haitawezekana kwani shemeji aliondoka navyo kuelekea chumbani kwake,…na sijui lengo lake baadae litakuwa ni nini…..na akilini nikasema, nitajitahidi mpaka nivipate hivyo vyeti na diary nihakikishe nimevichoma moto, nihakikishe vimepotea kabisa mbele ya macho yangu…

‘Hivyo vitu ni ushahidi na vitaathiri mambo mengi sana..huyu rafiki yangu kafanya nini…’nikawa najiongelesha mwenyewe huku nikigonga gonga ukuta.

‘Nitajuta…’nikarudia maneno ya shemeji, nikijaribu kuwaza ana maana gani

Baadaye wazo likanijia, nitupe karata yangu ya mwisho, nimshawishi shemeji nitumie lugha ya uwongo, nivipate hivyo vyeti….Nikasogea pale mlangoni, nikitaka kumgongea shemeji ili atoke tuongee, nijaribu iwezekanavyo, anipatie hivyo vyeti..lakini kabla sijagusa mlango…

Mara simu yangu ikalia, kuangalia ni simu ya mke wangu, nikasita kuipokea,…nikajua hapo itakuwa kubishana kwenye simu, mpaka basi na sikutaka shemeji afahamu kuwa mwenzake aliwahi kufika hapo, akiwa kazirai, na akaniona nikiwa namfanyia huduma ya kwanza lakini akatafsiri vibaya na kukimbia..angejisikia vibaya.

Nilipoona simu inaendelea kuita, nikatoka nje na kuipokelea huko…, nilianza moja kwa moja na kujielezea, ili mke wangu asije kunikatili, nikawa naongea kwa haraka haraka;

‘Mke wangu mwenzako kapoteza fahamu na nilikuwa namfanyia huduma ya kwanza, naona ajabu wewe ulipofika pale…uliamua kukimbia, badala ya kuja tusaidiane,…kwanini,..…’kabla sijamaliza nikasikia sauti ya mtoto wangu ikisema kwenye simu;…

‘Baba njoo haraka mama kadondoka, hapumui….’ilikuwa sauti ya mtoto wangu.

‘Kafanya nini…?’ sikusubiria jibu, nikageuka kushoto , kulia…

Hapo sikuaga…., nilitoka nje na kuanza kukimbia, kulekea nyumbani..nilitamani nichukue usafiri wa kunipaisha, japkuwa sio mbali kutoka hapo na kwangu, lakini kwa tukio kama hilo nilipoana ni mbali , kuna uzio ulijengwa, katikati, kwahiyo inabidi uzunguke hadi barani ndio upate njia ya kuingia kwangu.

Niliwapita watu kama upepo, na kile aliyeniona alijua kuwa kuna tatizo,..watu wengine wakawa wananifuatilia kwa macho..

Nikafika nyumbani, na kuwakuta watu wameshafika, wakijaribu kumpepea mke wangu

‘Kuna nini jamani..?’ nikauliza

‘Tulisikia mtoto wako akipiga ukulele, akisema…`mama, mama kadondoka…’ basi ikabidi tuje hapa kwa haraka, na kuikuta hii hali, yaonekana kuna jambo limemshtua..’akasema jirani yetu mmoja

Nilijaribu kumshika shka mke wangu, nikaona anaanza kupumua, akafungua macho, na aliponiona tu akanisukuma akisema;

‘Usiniguse,..tafadhali ondoka mbele yangu…’akawa anajitahidi kuinuka kunikwepa lakini mwili haukuwa na nguvu, watu wakamsaidia akatulia.

Ile hali ilizua maneno mengi, na kuzidi kuniweka mahali pagumu, na wakati huo watu wanafuatilia sana viongozi watarajiwa…na wakati najaribu kutafakari, mara nikasikia hodi, maana kwa muda huo tulikuwa ndani, …sauti hiyo ilinifanya damu ianze kuchemka…nikawa nataka kusimama ili nikamzuie huyo mpiga hodi, ili asiingie ndani, lakini nilikuwa nimechelewa, akawa keshaingia ndani….

Mke wangu alikuwa wa kwanza kumuona,…..macho yakamtoka pima…!

‘Wewe ni soldier….oh, hapana…’alisema kwa mshangao na mashaka…!

NB: hapo inatosha kwa leo


WAZO LA LEO: Mkiwa wana ndoa jaribu kuwa wakweli, muelezane mambo yenu, kwani nyie ni kitu kimoja, msipende kuweka siri na watu wengine wan je, mkafichana nyie wawili kwani hapo ni kama kuudanganya mkono wako wa kushoto huku ukifikiria mkono wako wa kulia hautafahamu. Mkeo ni ubavu wako, kwanini umdanganye. Ndoa ya kweli hujengwa kwa kuaminiana, kushirikiana na kuambizana ukweli na upendo wa dhati.

Ni mimi: emu-three

No comments :