Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, March 11, 2017

HAKI YA MTU HAIPOTEI BURE,-3
Nikasogea mezani na kuchukua ile barua, taratibu nikaitoa kwenye bahasha, na maandishi ya kwanza niliyoyaona, ni….’ninasikitika…’ kichwa kikaanza kuuma, nikawa sioni maandishi..mara giza…nilichokumbuka ni kauli …

‘NISAMEHE MAMA, sikufanya makusudi…’, nikazama kwenye giza! Nilipoteza fahamu,………..
Nilijikuta nipo hospitalini…nikatibiwa siku kadhaa baadaye nikatoka, na nilipofika ofisini, kama barua ilivosema, mimi sasa sitakuwa bosi tena, na nafasi yangu ataichukua mwenzangu, na mimi nitakuwa msaidizi wake, ..huku uchunguzi ukiendelea, na ikibainika kuwa ni uzembe wangu, hatua zaidi zitachukuliwa, nikawa sina jinsi ….

Basi siku zikaenda, nikakubaliana na hiyo hali…

 Siku moja narudi nyumbani jioni,  mtoto wangu kipenzi analalamika macho yanamuuma,..hapo nimechoka na kazi za ofisini ambazo zinanichanganya sana bosi wangu ananifanyia vitwimbi, lengo niondoke kabisa…sasa nimerejea nyumbani sijaweka hata mkoba, mtoto analalamika macho, …kwahiyo hilo la mtoto kulalamika macho, nikalidharau tu, na sio kawaida yangu, mimi huwa nawajali sana watoto wangu, lakini siku hiyo nilichoka sana.

Nikajilaza kwenye kochi, kausingizi ka mang’amu ng’amu,…namuona mtoto wangu ananililia anatoa machozi ya damu…ilikuwa ndoto fupi tu, nikafunua macho,..kweli mtoto alikuwa kasimama pembeni ya sofa, analia..macho, mama macho…

Nikamnawisha, na kumweka dawa ya macho, nikijua ni matatizo tu ya kawaida, huenda kaingiwa na michanga…

Inafika usiku mtoto wangu analia,…anasema haoni vizuri..nikaanza kupaniki, hapo sasa nikawa sina ujanja, ikabidi nimkimbize hospitalini usiku huo huo..,..walimuangalia, wakaona hakuna tatizo..akapewa dawa, tukarudi nyumbani akalala hadi asubuhi..nikajua akimuaka atakuwa safi..

Kesho yake mtoto analalamika haoni vizuri…unajua,kuchanganyikiwa… nilianza kuwaza mbali, kwanza kazini kuna matatizo, sasa shida ya mtoto….nilianza kulia, …nililia, nikikumbuka kuwa nina tatizo jingine mimi na mume wangu hatuelewani kabisa, na imefikia kama tumetengana naye, anaishi kwake na mimi kwangu, hapo sina mtu wa kunisaidia…! Utaona umuhimu wa mume kipindi kama hiki cha shida…

Hapa naingia natoka….nifanyeje.

Na siku hiyo kazini kulikuwa na kikao muhimu sana, nikikosa kufika siku hiyo, nitaeleweka vibaya sana,..na huenda nikafukuzwa kazi kwani nimeshaonywa mara nyingi kwa barua, na utakuta makosa yenyewe sio makosa hasa ni uzembe wa watu wengine nabeba mzigo wa lawama mimi,…baadaye sijui kwa vipi…nikakumbuka…

Iilinijia tu kama fikira… , nikamkumbuka yule mama aliyekuja ofisini siku ile,…sijui ilikujaje mpaka nikamkumbuka…,

Unajua nilichofanya, nikasema hayo ya mwanangu namuachia mungu,, nikaondoka kwenda kazini, nikamuachia mfanyakazi wangu maagizo ya kumuhudimia mwanagu,…nikawahi ofisini…, nilipofika ofisini tu.., nikaitafuta ile barua ya yule mama, nikaanza taratibu za kufuatilia kuhakikisha yule mtoto anasoma…nikamwandikisha ‘private candidate…’

Pamoja na kipato changu kidogo… , lakini nilimsomesha huyo mtoto , bila ya hata yeye kujua, au wazazi wake kujua hadi akafikia chuo kikuu…wao wanajua labda ni huduma za hiyo ofisi,…ofisi isingeliweza kumsaidia, kwani alishafeli….mimi nikatumia gharama zangu akasoma hadi chuo kikuu, huko nikamuachia mungu, maana alifanikiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi waliopewa mkopo…

Sasa tukirudi kwa mtoto wangu hali ya macho ilimtesa sana..nilihangaika naye, ikafikia sehemu nikakakata tamaa kabisa kabisa.., maana,..alishafikia sehemu haoni, ni kama kipofu…anaona kidogo sana….basi ikawa mimi na ibada tu kumuomba mungu tu…

**********

Siku moja nipo nyumbani mara mtoto wangu anakuja, keshakuwa mkubwa kiasi, yupo kidato cha nne, anakaribia kufanya mitihani…nashangaa mwanangu anafuraha ya ajabu, nikamuuliza ni nini kilichomfurahisha hivyo, maana yeye muda wote ilikuwa kulalamika tu.., kwanini mama, kwanini imekuwa hivyo, ina maana mimi sitaona tena…maneno ya kunitesa tu,..sina la kufanya mimi ni kulia tu.

Sasa leo anakuja na furaha tele,…nikamuuliza ‘mwanangu umefanikiwa nini huko shuleni,..?’

‘Mama mimi naona kabisa…’akasema kwa kujiamini.. na kwa kunihakikishia, akaanza kunisomea kwenye kitabu chenye maandishi ya kawaida,…sikuamini, nikamuuliza imekuwaje…maana kusoma ilibidi atumie lenzi kubwa anaishikilia mkononi ndio asome….

Akasema; Alikuja kijana mmoja, yeye anasoma chuo kikuu, ni mtu wa dini sana, …akasema yeye anaombea watu wenye matatizo ya macho maana hata yeye alitibiwa kwa kuombewa, na alimuomba mungu ampe kipaji hicho cha kuwaombea watu wengine..na kweli mungu akamjalai akapata hicho kipaji, kwahiyo yeye sasa anapita mashuleni kila akipata nafasi,  kuwaombea wenye matatizo kama hayo, ndio kaniombea na mimi nimepona mama…ahsante mungu…’akasema binti yangu.

‘Anaitwa nani…?’ nikamuuliza nikiwa na furaha moyoni, unajua furaha…

Akanitajia jina,…nikamkumbuka yule kijana niliyemsomesha, jina lake ni hilo hilo…nilimwambia mwanangu twende kwa huyo kijana, ..ukumbuke muda huo sijawahi kukutana naye, na wala hajui kuwa mimi nilijitolea kumsomesha hadi akamaliza kidato cha sita…na sikutaka afahamu kabisa, maana nilikuwa nalipa dhambi nilizozifanya..

 Unajua mpaka leo, sijaonana na huyo kijana,  maana alisafiri kwenda nje, kwani alipata msaada zaidi wa kusoma nje, …ila bado natafuta siku nije nionane naye…nina hamu sana ya kumuona, hasa mama yake pia angalau niwaombe msamaha..’ akamaliza.;

‘Kwahiyo hayo yaliyokupata usikate tamaa, mkabidhi mungu, yeye anajua ni kwanini imetokea hiyo, kama wamekufanyia hujuma,…mungu mwenyewe anajua cha kufanya,..muombe mungu tu…na amini nikuambiayo, malipo ni hapa hapa duniani..na kamwe haki ya mtu haipotei bure, hata aweje, hata yule unayemuona hafai, ana haki yake, usiwe wewe ndiwe chanzo cha kumfanya ateseke.....’akamalizia.

WAZO LA LEO: Enyi mlio kwenye madaraka, ogopeni kuwatendea vibaya wenye madhaifu ambayo hawakupenda yawapate,..ogopeni kuidhulumu nafsi ya mja…waja wa mungu nikiwa na maana wale wenye madhaifu ambayo hawakupenda yawapate, ….kuwatendea ubaya watu kama hao, ni madhambi makubwa sana,…na adhabu yake huanzia hapa hapa duniani,…utazaa, au wewe mwenyewe yatakukuta,..timiza wajibu wako, lakini usije kuweka chuki yako kwa waja wa mungu, ogopeni sana dhambi hiyo ya kiburi na dharau…!


NIMEWAKILISHA TUKIO NA UJUMBE HUO
Ni mimi: emu-three

No comments :