Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, February 28, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-5


  Ilikuwa usiku sana, watu wengi walishaondoka, na ndipo Soldier akapata nafasi ya kwenda chumbani kwake, kulala,…mkewe akawa bado anashughulika na wenzake, bada ya muda mkewe akafika,…alitaka kumuongelesha, lakini alikumbuka mkewe alivyomuomba kuwa leo hataki kuongea kitu chochote,…kibusara akaona sawa, ngoja avute subira tu, lakini ikafika muda akaona anashindwa kuvumilia,alimuangalia mkewe alivyolala, akatamani kumuamusha waongee, lakini akasita…akasema.

‘Kesho itafika,….mtaniambia kila kitu la sivyo…’akasema na kujigeuza upande mwingine, ...macho yalikuwa manzito sababu ya usingizi, lakini kila akijaribu kulala anajikuta akiwaza hili na lile, kichwa kilikuwa hakina amani kabisa

‘Kwanini mama hajaniambia kitu…sasa anaumwa, sijui anaumwa nini…mke wangu naye hataki kuongea, halikadhalika baba, wote wanasema kesho kesho ..kuna nini hapa..?’ akajiuliza, hakuzoea mambo ya kusubiria,…akajiinua pale kitandani, na kusimama, akachungulia nje dirishani,…

‘Natamani nitoke nje….’akasema, lakini akaona akitoka nje, anaweza kuondoka na kwenda sehemu nyingine na huenda akajikuta akifanya mambo ambayo hakutaka kuyafanya…’sitaki nije kushawishika kulewa….’ Akasema na kurudi kitandani…

Tuendee na kisa chetu…

************
Alipofika kitandani akasogeza mkono akitaka kumuamusha mkewe, ili angalau waongee kidogo…lakini akasita, mkewe anapenda kulala sana, akiweka ubavu kitandani usingizi tayari, na hapendi kuamushwa…akasita kufanya hivyo, kwa vile alijua mkewe alikuwa kachoka sana, kazi walizofanya siku nzima ya leo, ni lazima takuw akachoka sana,…na wakati anamuangalia mkewe, mawazo yakarudi nyuma, akakumbuka alipokwenda kuonana na mama yake kwenye shughuli, pale alipomfikia na kumkuta analia, alimsalimia akaitikiwa,…lakini baada ya salamu, mama yake hakutaka kuongea zaidi.

‘Mama anaonekana ana jambo nzito sana, ni jambo gani..ni kuhusu mke wangu na mtoto, je ni kuhusu baba….mmh, hata sijui, lakini lazima nifahamu, na najua nisipoingilia  kati mama ataumia sana…lakini kwanini baba anafanya hivi…mimi sijui baba anafaidikka nini na hali hii…?’ akawa anawaza..

‘Ngoja nijaribu kulala…’akasema kwa sauti ndogo, na kuanza kuutafuta usingizi, …na mara taswira ya mama yake ikamjia akiongea….

****************

‘Mwanagu nashukuru umerudi salama, najua kuna mengi umekutana nayo huko ulipotoka na sasa unahitajia muda wa kupumzisha kichwa chako….kapumzike mwanagu, mengine yaacha kwanza kama yalivyo….nafahamu kabisa una maswali mengi na unahitajia majibu na ufafanuzi…, lakini nakuomba kwa leo usiniulize kitu,..hapa nilipo sina amani,..unielewe hivyo,…’mama yake akasema na kusimama

‘Mama lakini siwezi kuwa na amani nikikuona katika hali kama hiyo…kuna nini, na kwanini unalia?’ akamuuliza mama yake akimuangalia usoni, na mama yake akawa anamkwepa wasiangaliane.

‘Hata mimi siwezi kuwa na amani nikikuona katika hali hiyo, mimi ni mama yako, japokuwa umekuwa mkubwa, lakini bado hisia za umama zipo ndani yangu…naumia nikikuona, …ila nielewe tu, amani yako ndio itanifanya mimi nitulie…’akasema

‘Mama kuhusu mimi usijali, nimeshakuwa mkubwa sasa, .na kama kuna matatizo nina haki ya kuyafahamu, maana matatizo ni sehemu ya maisha, nimetoka vitani, huko ilikuwa ni kufa kupona, sembuse hapa, …hapa hakuna milipuko ya mabomu au bunduki, zijazungukwa na maadui, kwahiyo mama, nawaomba….mama nakuomba kuhusu mimi usiwe na shaka…’Soldier akajaribu kkumpoza mama yake, japokuwa moyoni alijua hana amani.

‘Mwanangu, ya vita ni mengine,..hayo yanaonekana na yana mwanzo na yana mwisho wake…, ila haya ya hapa sijui kama yatakuja kwisha, nimechoka nayo ….oh, hebu kwanza niache, nikapumzike kidogo…wewe nawe kampumzike tutaonana kesho mungu akituamsha salama…’mama yake akasema akianza kuondoka.

‘Lakini mama, mimi nakutegemea wewe, uniambie kinachoendelea, tuongee kwanza kabla hujalala, unajua mama tukiweza kuyaongea matatizo ndio inakuwa mwanzo wa kujua jinsi gani ya kupata ufumbuzi, ..baba kaniambia ..’ kabala hajaendelea mama akamgeukia na kumkatiza maneno…

‘Sitaki kusikia maswala ya baba yako hapa….sitaki hata kuongea naye leo,..huyo achana naye, isingelikuwa ni wewe, ..na huyo mkeo, na…na mtoto, ningelisharudi kwetu, lakini mimi ni mama, mimi ni mwanamke, nimeumbwa kupata mateso na kuyavumilia,..mangapi tunaumia nayo, ya maumbile na hata ya kimaisha,..haya ndio maisha yetu, uchungu, kuumia na kuvumilia, yanapita na tunayasahau, ndio maana nimevumilia ili kupatikane muafaka kwanza,kabla sijaamua la kufanya…’akaanza kuondoka.

‘Mama..mama…inaonekana kuna tatizo kwanini unasema hivyo..’Soldier akawa anamfuata mama yake kwa nyuma,… lakini kabla hajafika mbali, akashikwa began a mtu…hakumuona alipotokea, maana sehemu ile kulikuwa ni varanda ya kuelekea sehemu ya vyumba….alihisi maumivu kutokana na huo mkono ulimshika,  ulikuwa kama wa chuma, na huyo mtu aliyemshika anaonekana hana amani naye, …Soldier akageuza kichwa kwa hasira kumuona huyo mtu …

‘Vipi mbona unanishika….’akasema na kabla hajamaliza uso wake ukakutana na uso wa shemeji yake, kaka wa mke wake,Mshari…

‘Karibu kijijini kwetu, …mimi Mshari, umenisahau…’akaambiwa, sasa wakiangaliana uso kwa uso.

‘Ahsante, lakini,…tutaongea baadaye nataka kuongea na mama kwanza…’Soldier akasema akitaka kuondoka lakini jamaaa akamshika mkono, …huyu jamaa mkono wake ni mkavu, una nguvu, na akikushika lazima uhisi maumivu, ..

‘Mama hawezi kukusaidia , najua kuna tatizo, lakini matatizo mengine huwezi kumkimbilia mama, wewe ni mwanaume,pambana kiume, usidekedeke hapa kwa mama…’akasema shemeji mtu.

‘Sikuelewi…unataka kusema nini, na tafadhali sitaki kuivuruga siku yangu, unajua umuhimu wa siku hii…’akasema Soldier, maana anamfahamu huyo jamaa kila wakikutana wanaishia kugombana.

‘Aaah..nani kasema anataka vurugu,..mimi nipo nyumbani kwenu, mimi ni mgeni tu hapa,…sikupenda kuja hapa ni bab tu kanisihi, ..na hasa aliposema mdogo, hana raha, ninajua kweli hana raha….sasa mimi sitaki kuvunja heshima ya ugeni, ila ikibidi sitaacha kufanya lolote, na sitajali kuwa wewe ni askari, uaskari wako ni huko huko…unanielewa, ninachotaka kuuambia ni hiki..…’akawa sasa akimtoboa toboa kwa kidole kifuani, ..mpaka soldier akahisi maumivu, na kusoge nyuma huku mkono mwingine ukitaka kuzuia mkono wa huyo jamaa asiendelee kumtoboa toboa na kidole.
.
‘Unataka kusema nini…?’ akauliza Soldier, sasa akiwa tayari kwa lolote, alishaona jamaa anataka kumkalia kichwani.

‘Ni kuhusu mdogo wangu… namuona hana raha, hataki kuniambi ana tatizo gani,…mimi sipendi…unasikia, kwanza ni kwanini ….unajua mdogo wangu alitoweka mwaka na kitu, hatujui yupo wapi,…, anarudi na mtoto,…ok, sijui,  na kwa ile alikuwa na mama yako, sikuwa na shaka sana…sasa tunahisi humu kwenu kama nilivyowahi kuwaambia awali ndugu zangu, dada hana amani…mimi namuheshimu sana mama yako, nilishataka kuleta vurugu, nimchukue dada yangu ‘akatulia
‘Kwanini umchukue…?’ Soldier akauliza
‘Nisikilize kwa makini, mimi sitaki kujua ni nini kinachoendelea kati yako wewe na dada yangu au kati ya dada yangu na familia yako, hasa baba yako…mimi simuamini baba yako kamwe kama nisivyokuamini wewe, wakati wote nyie wawili nai maadui zangu….unanisikia sana…nikipata mwanya tu, moto utawaka…’akajitutumia kifua.

‘Mhh..sielewi kitu, na uadui wako huo usioo maana haunistishi,..unasikia, ushari wako wa kishamba, hauna maana kwangu, kwahiyo tuachane…’Soldier akasema.

‘Hata baba yako alitamka maneno hayohayo..mtasema hivyo hivyo, hamuelewi kitu huku mnatesa dada yangu, sawa ushari wangu ni wa kishamba, sijasoma, si ndio maana yake hiyo ila mimi nakuambia hivi hatua nitakayochukua mtakuja kuniona mbaya, nimeshamuambia baba yangu…, niliwaonya mapema tu..leo wanataka msaada wangu…niliwaambia kabisa, nyie watu hamfai kumuoa mdogo wangu, hamfai…lakini baba hakunisikia, sasa haya yanatokea wameanza kuyakumbuka maneno yangu..’akasema

‘Lakini kwani kuna tatizo gani hebu tuongee kuna tatizo gani, mama na baba yangu wana, kuna nini….?’Soldier akataka kujua zaidi.

‘Sitaki kusikia kudeka deka kwako,..mimi sidekewi,..kamdekee mama yako ..maana naona unamuhitajia sana, wewe ni mwanaume pambana na matatizo yako kama mwanaume,..achana na kutegema familia yako ooh mama , oo mama, kila kitu mama, kila baba ..mpaka lini,..unaniona mimi, …simtegemei baba wala mama, ninaishi kwangu , mbali kabisa na familia,..kwanini, sababu..mimi ni mwanaume wa shoka..’akasema sasa akitaka kurusha ngumi kama kawaida yake mkono wake ni mwepesi kupiga, na Soldier anamfahamu jamaa, akasogea pembeni.

‘Hahaha…mama, mama…gangamala mwanaume...’akageuka kuondoka na Soldier akaona asimuachie kuondoka hivi hivi bila kumjibu neno, akasema;.

‘Lakini shemeji sikiliza, hayo maneno yako mimi siyapendi, kwanza mimi sideki, pili mimi siwategemei wazazi wangu kama unavyofikiria wewe,..nimeshakuwa mkubwa nina familia yangu ndio maana nikamuoa dada yako, na tatu, dada yako na mimi tulioana kwa kupendana, hakuna kulazimishana hapo, na dada yako hana matatizo, na kwa ufupi ni hivi, mimi nimerudi nitahakikisha yote yamekwisha…kwahiyo sipendi wewe kuingilia maisha yangu na familia yangu, wewe una family yko na mkeo sijawahi hata siku moja kukuingilia, kuwa mstaarabu na..kaa mbali kabisa na mimi na familia yangu.unanielewa….’Soldier akasema na jamaa aliyeanza kuondoka ghafla akasimama.

‘Unasema….?’ Akauliza bila kugeuka

 Soldier alijua jamaa akigeuka hapo atamjia kama mbogo, aliyejeruhiwa,..anamfahamu huyu jamaa alivyo.., hawezi kuachana naye kabla hajaanzisha shari,…na hii shari ya sasa kainzisha yeye, kwani jamaa alishaamua kuondoka,..hakutaka iwe hivyo, ila aliona bila kusema neno, ataonekana mjinga,…Soldier akajiandaa kwa mapambano, anamjulia, jamaa huwa anakuja bila mipangilia, …, na kabla jamaa hajageuka mara mke wake akatokea, na kusema;

‘Oh, kaka, uko huku , baba anakutafuta wanataka kuondoka wenzako…’akasema na kaka mtu akahema kama mtu aliyeshusha mzigo mnzito…

‘Waambie nakuja…’akasema kwa hasira.

 Na dada mtu akahisi kuna tatizo, anafahamu wawili hao wakikutana ni vurugu, akaona njia pekee ni kuhakikisha wanatengana, akasogea hadi kwa mumewe na kumshika mkono.

‘Twende, kuna wageni Wanaka kukuaga…’akasema akimshika mumewe mkono na kaka yake akiguna akatembea mwendo wa kasi kuondoka eneo hilo

‘Vipi kuna nini tena,..najua nyie wawili mkikutana hamuishi kugombana mnagombea nini jamani, mbona hamkui…?’ mkewe akamuuliza.

‘Hatujagombana tulikuwa tunaongea tu..’akasema Soldier.

‘Unafikiri mimi ni mtoto mdogo sio nimewaona muda tu, na niliwahi kumuondoa kaka hapo nikijua kitakachofuata ni nini..na mama naye hayupo vizuri, …sijui ana tatizo gani..?’ akasema mkewe

‘Mama hayupo vizuri..?, ana tatizo gani , anaumwa..?..yupo wapi…?’ Soldier akauliza maswali mengi akiwa na mashaka

‘Sasa hivi kaenda kulala, hataki kuongea na mtu…’akasema mkewe

‘Ok ….sasa , kabla hatujaenda huko, nikuulize kitu,...’ akasema akimshika mkewe mabegani na wakawa wanaangaliana uso kwa uso, na kwa haraka Soldier akasema.

‘Hebu niambie kuna nini hapa nyumbani….ni nini kinachoendelea hapa nyumbani,…nataka majibu ya haraka kabla kichwa changu hakijapasuka kwa mawazo?’ akamuuliza mkewe akimuangalia kwa macho makali,mpaka mkewe akashikwa na butwaa,..kama kutahayari, hakupenda jinsi mumewe alivyomshika,watu wanaweza kuwaona, akaondoa mikono ya mumewe mabegani na kusogea pembeni..

Mkewe kwanza alibakia kimia kwa muda, halafu akasema;

‘Hata mimi nina maswali kama hayo hayo…..nilimuuliza mama, hakuweza kunipatia majibu, akaishia kulia…na wewe unaniuliza mimi, aah, inafikia najuta, kwanini niliolewa,…ooh, sitaki kuyaongea sasa hivi,…na sitaki kuyaongea kabisa, mimi naona kwasasa wa kukupatia majibu hayo ni baba yako, na mimi sitaki uniulize zaidi, nimejitahidi kuvumilia ili urudi, na sasa umerudi, subiria muda muafaka utapatiwa majibu na baba yako, na ninajua baada ya hapo, hutakiwa na shaka na mimi, nitaondoka zangu…’akasema
‘Utaondoka zako…!!? Una maana gani kusema hivyo! Kuondoka …, kwenda wapi.? Na , na…Baba anahusikanaje na mtoto, baba anahusikinaje..na na…hebu niambie haraka, kabla sijabadilika….niambie…’kabla hajamaliza mara baba yake akatokea…
Kokorikooooh…..kumekucha!...

NB: Bora niishie hapa,

WAZO LA LEO: Hakuna kitu kinatesa kama mawazo, mawazo yasiyokuwa na ufumbuzi wa haraka,na mwazo yakizidi sana, inageuka kuwa ni ugonjwa, na madhara yake huweza kuwa makubwa zaidi ya mawazo yenyewe! Ni muhimu sana kutafuta suluhu ya mawazo kabla hayajageuka kuwa ni tatizo..Ni kweli mtu mwenyewe unaweza ukasema nitayamaliza tu, lakini kuna shinikizo la nje,..ni kwanini mbona nk…haya kama hakuna subira na uvumilivu, haya..ndio yanayofikia kuwaumiza watu hadi kufikia kupatwa magonjwa ya shinikizo la damu. Tumuombe mungu sana atulinde na matatizo ya mawazo!
Ni mimi: emu-three

No comments :