Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, February 24, 2017

HAKI YA MJA HAIPOTEI BURE-2


‘Mama mimi nimechelewa kikaoni…’nikasema sasa nikianza kufunga funga vitu vyangu ili niweze kuondoka. Lakini yule mama ni kama hakunisikia,..na pale ofisi kulishajaa harufu ya jasho lake,…nikasogea kwenye kipozoe na kukiwasha, sikuwa na nia mbaya ya kumzarau..lakini ofisi ni ofisi, huyo mama alipoona hivyo akasema;

‘Najua unakerwa na jasho langu, jasho hilo lina thamani kubwa mbele ya mungu na ni ushahidi kwako, ili ujue ninavyoteseka, uone kuwa nimetembea maili nyingi hadi kufika hapa sina nauli nitafanyaje..….'akasikitika kwa kutikisa kichwa

'Lakini hayo hayana maana kwako, maana utafikiria nimekuja kukuomba, hapana ninachotaka ni haki yangu, haki ya mtoto wangu, na najua imeshachelewa kama ulivyosema, lakini hata kama imechelewa, nataka wewe usikie hii kauli yangu kwako…..

Muda huo mimi nimeshakasirika,....sikutaka hata kumsikiliza nilitaka atoke, ili nione nitafanya nini, maana nilishachelewa hata hicho kikao,...nitafute namna ya kumdanganya bosi wangu kama atanielewa....namfahamu sana huyo bosi mkuu, kwake muda ni kitu muhimu sana,hapotezi hata sekunde moja, ukichelewa dakika moja tu, keshafunga kikao, kitakachofuata hapo ni barua…

‘Nisikilize kwa makini, najua sana kuwa sisi watu wa chini hatuna maana kwenu, tunanuka mijasho na tutasema nini, ndio maana hatutakiwi kuja kwenye ofisi zenu, sawa nashukuru..., lakini hata hivyo tuna sehemu ya kimbilio letu, ..huyu hawezi kamwe kututupa, na kauli yangu na ujumbe wangu ni kituma kwake yeye, asiyeangalia mwili au mijasho yetu,... mola ..kwa mola wangu..….’ Akanikazia macho na huku anainua mikono juu.

Wakati huo nilishasimama mlango kumuashiria atoke, nifunge mlango, yeye akawa kasimama pale pale, na kuendelea kuongea;-

`Kauli yangu ni hii….

‘Kama kweli barua hiyo haikuwahi kufika kwako…, wewe ni mzazi kama mimi wewe ni mama kama mimi, unazaa kama mimi, mungu anaona,…hakuna anayefahamu uchungu wa mtoto zaidi ya mzazi, hasa mama….’akaweka mikono hivi kama atafanyaje.

‘Nasema hivi , kama kweli haijafika kwako, basi nisamehe,..lakini kama kweli ilifika kwako ukafanya uzembe, ukadharau, maana unaona huyo ni kilema tu, anafaa nini,..mungu anakuona…mimi sasa naondoka,..samahani sana kwa kukupotezea muda wako…’

Hayo ndio maneno aliyatamka huyo mama kabla hajaondoka, halafu alipomaliza taratibu akaanza kuondoka, kwanza, nilibaki nimeduwaa, nikakumbuka kikao, nikakurupuka lakini kabla sijafungua mlango mara katibu muhutasi wangu ananijia kwa kasi akisema;

‘Samahani bosi mimi sikumuona huyo mama akiingia….alipitia wapi, ooh, nilikuwa nimekwenda maliwatoni, samahani bosi…’akasema na mimi sikumjibu kitu..ila aliposema…..

‘Na…bosi mkuu amepiga simu anasema anakuja…’aliposema hivyo, mwili mzima ukanywea, maana hicho kikao kilikuwa kinakwenda kufanyikia ofisi kwake, sasa nimechelewa,…lishapita nusu saa sijafika huko, ..niliangalia simu yangu, nikakuta missing call tano, simu nilikuwa nimezima kutoa sauti...nikajua sasa kimenuka, ajira haipo tena!

Nikataka nitoke tu, nimuwahi huyo bosi kabla hajafika,....na kabla sijafunga mlango, mara mlango wan je ukafunguliwa, na aliyeingia alikuwa bosi mkuu… kakunja uso utafikiri sio yeye..alikuja moja kwa moja kwangu pale nilipokuwa nimesimama..

‘Kwanini hujafika kwenye kikao…?’ akaniuliza, na kabla sijamjibu vyema, akasukuma mlango wangu, ukafunguka, akawahi kuingia ofisini kwangu, na hakukaa, akanibwagia barua mezani, nilijua ni barua ya nini….nikashika kichwa,…

Huyo bosi hakusema zaidi, akatoka, na hakuaga, akatoka nje, kuondoka zake,…sikuisoma ile barua kwanza,…akili yangu ilinituma kuhakikisha jambo fulani kwanza, kwahiyo nikaliendea trei langu la barua zinazotoka, na kuingia nikawa nakagua sehemu ninapoweka barua za kuja kwangu,…haikuwa mbali,  nikaiona ile barua.

‘Oh..’nikaguna, hapo ndio nikaikumbuka tatizo la huyo mama na barua iliyotumwa kwangu, kumbe ndio huyo mama…

‘Kiukweli…, ile barua niliwahi kuisoma, kukawa na ucheleweshaji fulani, katika kufuatilia kumbukumbu zake, hazikuwa zimekamilika na ilifika ikiwa imechelewa mezani kwangu,…na mimi nilitingwa na kazi nyingine…, mpaka muda ukapita, nilipoiona tena, muda ulishapita,..hatungeliweza kufanya lolote,… kwahiyo tukaacha kama ilivyo,….leo hii huyu mama amekuja na maneno kama hayo..Ilinipa wakati mgumu sana, lakini sikuwa na la kufanya!

Nikageukia mezani, barua aliyoleta bosi ipo mezani, huenda ndio ya kufukuzwa kazi,..sasa nikaanza kukumbuka mbali…

‘Unajua kwanza niliwazia watoto wangu,..ile kauli ya huyo mama ililenga haswaa…mimi kama mama ilinigusa pale pale,..mama ukitaka kumpata gusia watoto wake,..laana ya huyo mama imeshaanza kufanya kazi, kwanza nimeshafukuzwa kazi, ya pili sijui itakuwaje…mimi nina imani sana ya dini,..lakini hapo nilitikisika kiimani… nilijikuta nikalia,..nilifikiria, sina nitawakleaje hao watoto,..

Nikasogea mezani na kuchukua ile barua, taratibu nikaitoa kwenye bahasha, na maandishi ya kwanza niliyoona, ni….’ninasikitika…’ kichwa kikaanza kuuma, nikawa sioni maandishi..mara giza…nilichokumbuka ni kauli …

‘NISAMEHE MAMA, sikufanya makusudi…’, nikazama kwenye giza! Nilipoteza fahamu,………..

NB: Kwa wale wanaotaka kujua ni nini duwa ya mja inafanya kazi soma kisa hiki, tuonane sehemu nyingine mungu akipenda.


WAZO LA LEO: Usimdharau mja wa mola..hata kama kakosea, hata kama wewe ni mubwa namna gani, kipato chako cheo chako, hakina thamani mbele ya muumba, ambaye anajua ni kwanini kamuumba mja wake hivyo..
Ni mimi: emu-three

No comments :