Ni kisa amenisimulia bosi wangu mmoja, nilipokuwa naongea
naye maswala ya mtoto wangu..,…akaniambia,…
‘Ndugu yangu wewe muombe mungu wako tu…, utafanikiwa, kama
njia hiyo imefungwa ipo nyingine itafunguliwa..nikuambie ukweli, haki ya mja
haipotei bure….’akatikisa kichwa na akawa kama anakumbuka jambo…
‘Nikuambie tukio lililonikuta mimi mwenyewe…’akanigeukia
kuniangalia usoni.
‘Sijamsimulia mtu…’akageuka kuangalia huku na kule kama
kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayemsikiliza.
‘Mimi niliwahi kuwa bosi sehemu,..nikawekwa kwenye kitengo
cha kuwasaidia watoto wenye matatizo mbali mbali ambao wanahitajia kusaidiwa
kwa namna moja au nyingine. Nia hasa ni kuwawezesha na wao waweze kusoma, maana
bila hivyo hawatasoma, jamii haina wema na watu wenye matatizo…hasa unapogusia kwenye
swala la elimu, sanasana uwaamabie michango ya harusi, watakuchangia sana.
Basi mimi kwa elimu yangu nikawa mkuu wa kitengo hicho na
baadaye nikateuliwa kuwa mkurugenzi wa kampuni nzima,…na moja ya kazi zetu ni
kuhakikisha watoto wenye mapungufu fulani, ..ulemavu, matatizo ya macho,
nk…wanapatiawa huduma maalumu ya kuweza kufanya mitahani yao vyema..kama vile
kupewa maandishi maalumu..,na vitu kama hivyo,…’akatulia kidogo.
‘Siku hiyo nilikuwa nimefika ofisini asubuhi…kama kawaida
yangu. Na hata sijakaa vyema kwenye kiti changu, ghafla mlango ukafunguliwa na
akainga mama mmoja, ni mtu mnzima, nilishangaa yeye kuruhusiwaje kuja kuniona
maana enzi zangu, kuja mpaka unifikie mimi kuna hatua kidogo, sio kwamba
nilitaka iwe hivyo, hapana ni utaratibu wa kazi ulivyo, kiutandaji,..wapo
wadogo zangu ki vyeo, inabidi wao kwanza wafanye hizo kazi, kabla hazijanifika mimi…
Sasa asubuhi hiyo na mapema hata sijajiweka vyema…na
ilitakiwa kabla mtu hajafika kwangu nipigiwe simu,…na nadra watu kuletwa
kwangu, maana shughuli nyingi zinamalizwa na walio chini yangu…lakini kama ni
lazima mtu kuniona inatakiwa apangiwe siku na mimi niwe nimeshapitia mlolongo
mzima wa matatizo yake….sasa siku hiyo ikawa ni ajabu ya aina yake…na haijawahi
kutokea.
Basi huyo mama, akiwa kasimama, akaanza kutoa machozi,…nilihisi ana tatizo
labda la kufiwa, au… ni omba omba tu maana hapo ofisini tulikuwa tunakutana na
mitihani mingi, watu wenye shida ni wengi sana, huwezi hata kuamini, lakini
hawaruhusiwi kufika kwangu….mimi kwa tahadhari, nikasogeza mkono ili nishike
simu niwapigie mapokezi , niwaulize kulikoni,…lakini hata kabla sijafanya hivyo
huyo mama akasema;
‘Usihangaike mdogo wangu,…najua wewe ni bosi mkubwa sana
hapa, najua wewe kukufikia ni shida, najua wewe ni muheshimiwa, lakini kwanza
jiulize nimewezaje kukufikia wewe…lakini hiyo sio hoja yangu , ila ninaomba
dakika tano tu, nikufikishie huu ujumbe, ….’akasema na kutulia, na mimi
nikareejsha mkono wangu na kutulia.
‘Kuna barua yangu nilikutumia, nina mtoto wangu, yeye ni
mlemavu, ..ana matatizo mengi, ni mtihani wa maisha tu umetukuta,…nami siwezi
kulalamika sana…mtoto wangu, ana ulemavu wa viungo, pia ana matatizo ya macho
hayaoni vyema ..haya hata kusikia kwake ni
kwa shida,lakini anatakiwa na yeye asome, ndio maana kukawa na maidara kama
haya, ya kuwasaidia watoto kama hao, na nyie mkapewa dhamana hiyo, mnalipwa kwa
ajili hiyo…mtoto anasoma kwa shida sana,anateseka,..lakini nitafanya nini…’akatulia.
Mimi pale ninatakiwa kujiandaa na vikao, nahitajika
nitayarishe muhutasari wa kazi zetu , ..huyu mama hajui hilo,lakini nashindwa
kumtoa, …akilini hasira zinachemka, hasira kwa watendaji wangu wa chini,
wanajua majukumu niliyo nayo….
‘Lakini namshukuru mungu, mola kamjalia angalau ana
akili..huko nyuma kajitahidi sana,…lakini tatizo mtihani huu wa mwisho,…wa
kumaliza kidato cha nne,… sikuwahi kupata msaada kama nilivyoomba, kwasababu
yenu….wewe ukiwa bosi wao…’akasema akininyoshea kidole.
‘Sasa mwanangu hajaweza kufanya mitihani yake, atfanyaje
wakati hakutayarishiwa kama ilivyo kawaida yake, sababu nasikia umesema
vithibitisho havikukamilika..vithibitisho gani, wakati miaka yote anasoma,
miaka yote anapata hizo huduma, leo hii….hapana, wewe huna uchungu,….’akawa
anatoa machozi.
Pale nikaangalia saa, nimebakiwa na muda mchache tu
niondoke, sijatayarisha chochote, na kikao hicho kilikuwa cha migogoro ya
kikazi nilitakiwa kwenda kujieleza..
‘Nyie kwenye maelezo yenu awali, mlisema tutasaidiwa kila
kitu tukaorodhesha majina ya watoto wetu kumbe nia yenu ni ili mfaidike kwa
kupitia migongo yetu,…mtoto wangu hajafanya mitihani, nyie ndio mumesababisha hayo……’akasema
kwa huzuni..
‘Lakini mama samahani sana, nina kikao maalumu naomba
tafadhali…’nikaanza kujitetea, lakini hakunipa nafasi akawa anaongea tu.
‘Nikuambieni ukweli, mwanangu hakuomba yeye awe hivyo…hii ni
mitihani tu, hata uwe tajiri au masikini haya yaliyomkuta mwanangu yanaweza
kukuta hata wewe, hata mtoto wako,…au nyie kwasababu ni matajiri, hayo hayawezi
kuwakuta au sio…niwaulize maana mimi sijui…nimewakosea nini jamani, umasikini
wetu ndio tunapata adhabu kama hii…..’akawa analia.
‘Mama samahani kidogo…’sasa nikashindwa kuvumilia…na yeye
akawa anazidi kuongea…
‘Labda, mnaona atakuwa na fadia gani kwenye hii dunia..,
mwili wenyewe umelegea, macho hayaoni,..atafanya kazi gani..au sio…, si ndivyo
mnavyofikiria au sio…..ndio maana mnatufanyia hivi sisi watu wa hali ya chini..hamjui
jinsi gani tunavyohangaika na haya maisha, mnafikiri tumeomba…’akajifuta
machozi.
‘Mama, mimi nina kikao..nina matatizo makubwa, nielewe
kwanza…’nikasema lakini hakutaka kunisikiliza akaendelea kuongea…
‘Sasa nikuambie ukweli, wewe hayo kwako waona matatizo, hebu
nifikirie mimi,…mimi naishi huko,…Pugu, nimekuwa nikiamuka saa kumi alifajiri,
namuandaa huyo mtoto kumleta huko Masaki kwenye shule yao alipokuwa akisomea….ni
mtoto wangu nitafanya nini,..mume alinikimbia, kisa huyu mtoto, eti kwanini nimezaa
kilema….leo hii jamani,…mnanifanyia hivi….’akatulia akilia.
Hapo hisia za huruma zikanijaa..., lakini nikiangalia saa ninachelewa ni kazi za kuandaa, nitahitajika kwenye kikao na wakubwa kujitetea,..nina matatizo makubwa,....
‘Mimi nimehangaika na huyu mtoto tokea anazaliwa, lakini
nilisema hata kama yupo hivyo ni kiumbe wa mungu, mpaka anafikia miaka minne
hawezi hata kukaa, kalegea tu kama hana mifupa…alipofika mika sita akaweza
kukaa, kutambaa, lakn kusimama shida, miguu haina nguvu.
Nikahangaika naye,..umasikini huu tena, unakwenda wapi,
lakini kila hatu akaonyesha ukomavu, na hata alipofika miaka sana akaanza kudai
kuwa na yeye anataka kusoma,...
‘Mwanangu kwa hali hi shule gani watakupokea…’nikamwambia,..lkn
ya mungu mengi, akatokea jirani mmoja akanielekeza shule moja, nikampeleka huko…ikawa
namshikili hadi shule, anasoma jioni namfuatilia,…ni shida….mpaka akamaliza la
saba, alipewa mtihani wa maandishi makubwa, akwa miongoni mwa watoto waliofaulu. Ilikuwa furaha iliyoje, hakuna aliyeamini...
Sasa sekondari…ikawa wapi, maana kapangiwa shule za kata ni mbali, na hali yake itakuwaje…ndio
huyo huyo jirani yangu akanielekeza kuwa kuna shule hiyo ya huko Masaki…nikaenda huko nikaomba
nikapata nafasi,..mdogo wangu usione hivi, nakuambia haya unielewe,…nimeuza kiwanja cha urithi, kumtibia
huyu mtoto.., lakini wapi…
Lakini namshukuru mungu, kidogo ndio sasa anaweza kusimama,
kutemba kwa shida,…nimekuwa nikimleta kutoka Pugu hadi Masaki, kuanzia kidato cha kwanza, mimi
mwenyewe,..nagombea daladala hadi shuleni,…na jioni namfuata namrejesha
nyumbani, hadi kafikia kiwango hicho,….mama ni mama tu..,..sasa imefikia
hatua hii ya mwisho,….mnakatili jamani,…niliomba kwa mungu asome hadi chuo kikuu awe
shahidi…jamani sasa ndio mnanifanyia hivi..?’ akasema huyo mama kwa uchungu.
'Najua hapo moyoni kwako unasema;
‘Si kilema tu huyo, hata akisoma atasaidia nini..lkn nyie wenyewe ndio mlitushauri, wasome, sasa mumeona wamekuwa wengi au sio…mnataka watoto wenu tu ndio wasome
wasiwazibie nafasi za elimu ya juu, mnaongoza kwa kishindoa au sio…hewala bwana, acheni watoto wenu tukafe nao
majumbani,..nyie acheni watoto wenu, wasome wafika hadi ulaya….’akasema huyo mama hajui mimi nipoje,...watoto wangu wenyewe wanasoma shule za kawaida tu...
Alipofika hapo nikaona nami nisema neno, nikamwambia,….
‘Mama sielewi unachoongea, unanilamu bure tu...kwanza hebu niambie kwa kifupi tatizo ni nini… na kwani
huko ulipopita wamekuambiaje, maana
kiutaratibu, na kwanini ukasubiria mpaka matokea yakatoka …..?’ nikamuuliza
lakini kabla sijamaliza akasema;
‘Unajifanya kuwa hujapata barua ya maombi yangu kuwa
mwanangu ana matatizo,..alihitajia mtihani wa maandishi maalumu, tofauti na wengine, makubwa sana…, ....mwanangu anasikia kwa shida, ana matatizo ya macho anaona kwa
shida…ni nusu kipofu…, ni kilema, namshikilia kila siku kuja
shuleni,..nimefanya hivyo miaka mine, leo kafika kidato cha nne mnasema eti
vielelezo havikukamika, eti….mbona huku nyuma hakumsema hivyo, na kwanini na
nyie hamkuniambia mapema, mkaacha mpaka mtihani umefika,…?’akasema
‘Lakini mama..kwanza , mimi sikumbuki vyema hiyo barua yako..., basi samahani subiria nitaongea na
wenzangu..lkn hata hivyo umeshachelewa sana mama kutoa malalamiko yako,… na kama
barua yako ingelifika kwangu kwa wakati kwanini nisikupatie hizo huduma…, tusingeliacha kumfanyia itakiwavyo, mbona
tunafanya hivyo mara kwa mara lakini nahisi kulikuwa na tatizo…oh, …sijui kwani ilitokea
hivyo…’nikajitetea huku hata sijui nifanyeje,…
‘Muheshimiwa, kwanza unakana kuwa barua yangu haijafika kwako.huo
ni uwongo,tatizo la mwanangu linajulikana muda mrefu, miaka minne sasa, yeye alikuwa anasomaje hapo shuleni,ilikuwa na haja gani ya kuomba tena,…lakini ndio hivyo, kama ulivyosema muda umeshapita,
nitafanyaje, kakosa kakosa, hata nikilia, dua la kuku sasa,…lakini nataka unisikie,...ujumbe wangu,…’akasema
‘Mama nimechelewa kikao, yaani mama hujui tu…’nikasema sasa nikianza kufunga
funga niondoke.
‘Nisikilize kwa makini, huu ujumbe lazima upenye masikioni mwako,...sisi watu wa chini hatuna neno,
kilio chetu ni kwa mola..sasa nasema hivi,….’ Akanikazia macho na mimi nikawa simsikilizi sasa nimeshachukua mkoba wangu nataka kuondoka, na yeye akayaongea haya maneno....
NB: Hebu sikiliza maneno ya mja wa mungu, na je maneno haya
yataleta athari gani...
WAZO LA LEO: Kila
jambo hutokea kwasababu, na mara nyingi likiwa ni kinyume na matarajio yetu
anglabu hatushindwi kujitetea, hata kama tunafahamu tumekosea..lakini
tukumbuke, mwenyezimungu mungu hadanganyiki…mwenye haki mpeni haki yake, na
kama ikichelewa, msiendelee kumnyanyasa, adhabu za mungu zitashuka ukiwa umechelewa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment