‘Dada mimi simtaki huyu mtu,…,
simtaki…ataniua…’
‘Ananibaka ananibaka, njoo nisaidie….niokoe
niokoe…simtaki simtaki,….’
Ni sauti
zilizonivunja nguvu kabisa, zilicheza kwenye ubongo wangu na kunifanya nihisi kuwa huyu mdada sitaweza
kumshawishi kwa vyovyote vile, na nashangaa kitu gani mke wangu alimpendea, na
wakati anafahamu kabisa nilivyokuwa
namchukia huyo binti.
‘Kwa
taarifa yako tu, …nimesikia juu juu, kutoka kwa wife wangu, kuwa huko kijijini
watu wengi wanamtaka huyu binti…, sasa kazi kwako , chelewa chelewa utamkuta
binti sio wako,….
‘Ina maana wenzangu
wameshajipanga, watamchukua, na kiukweli ni binti mnzuri, ana sifa zote za kuwa
mke mwema, ila mimi tu….
Kuna muda nilitaka
kusema , vyovyote iwavyo, mimi sitaki kuoa, lakini je ni kweli kuwa nitaweza
kuvumilia kuishi bila mke…na hata mfano ndio nikataka kuoa, na wakati huo huyo binti
keshaolewa, sioni kuwa nitaumia sana, …
‘Aaah, …’nikasema
hivyo nikiwa na maana haina haja sana, kwani ni lazima niti kila kitu
wanachosema watu…
‘Unayapuuza maigizo ya mke lakini..mkeo
ambaye kafa kwa ajili yako,..mkeo aliyekupenda sana, na usia wake ndio huo
umuoe huyo binti, huyo binti ndiye anayekufaa…..
Ni kweli kwa tabia
yangu, sidhani kama mtu anaweza kunivumilia, japokuwa kiukweli nilikuwa
nimeshabadilika sana, …nilikuwa mtu mwingine, nilikuwa nimeshaanza kuzisahau
zile hasira, …je kweli nitaweza kuvumilia hivyo,.
Hapo nikabakia njia
panda,…
Niliwaza hayo nikiwa
nimekaa upenuni mwa nyumba, sikutaka kuondoka kabisa, niliogopa huyo binti
atatoka na begi lake aondoke.
Siku hiyo hakuweza
kutoka nje, hali yake ikawa imebadilika, akawa sasa anaumwa kweli...
**********
Huyo binti hali yake ikawa sio nzuri, akawa
hawezi hata kusimama, ikabidi nimuite, na docta akasema hali hiyo itakwisha ni
kutokana na shinikizo la damu, ila anahitajia uangalizi wa karibu na kukwepa
kitu chochote kitakachomshtua tena..
‘Sasa docta
inavyoonyesha binti huyu kaniogopa mimi, na wala sijui ni kwasababu
gani..’nikasema.
‘Huenda kuna jambo
uliwahi kumfanyia, na muda mwingi amekuwa akiogopa…sasa ilishafikia kikomo,
akashindwa kuvumilia tena…ndio ikatokea hivyo…’ akasema huyo docta.
Kwa maelezo hayo ya
docta , nikakata tama kabisa na huyo binti.
Nilijitahidi
kumsaidia, kumuhudumia, alikuja mzazi wake akitaka kumchukua , nikamuomba
asimchukue, aendelee kutibiwa hapo hapo, na mimi nitamsaidia,…sasa ikawa zamu
yangu kufanya yale yale aliyokuwa akinifanyia mimi.
Usiku sasa ikawa
nakesha kumuomba mungu wangu, nilimuomba anisaidie, huyo binti apone, na
anisamehe yale yote niliyomfanyia, na amsafishe moyo wangu uwe na ujasiri wa
kuweza kuishi na mimi asiniogope, na ikiwezekana awe mke wangu…hayo ndio
yalikuwa maombi yangu.
Akawa anaanza
kupona, na hata kutembea tembea japokuwa kwa shida…..
*************
Sijui hiyo siku ilitokeaje,…kuna matukio mengi kama haya ya
ajabu ajabu yalikuwa yakinitokea lakini hili liliacha kumbukumbu kubwa katika
maisha yangu…
Ilikuwa mchana
mchana, nikawa nimekaa nje, navuta hewa kwenye bustani ya nje, na akili
ikanikumbusha enzo hizo, mke wangu alipokuwa akihudumia hayo maua, nikawa
nimezama kwenye mawazo …na ghafla nikaona tena taswira ya mke wangu akitokea
upande wa pili..
Yaani pale niliposimama
nyuma ya hayo maua, ndipo nilimuona sasa akiwa kasimama, na alikuwa
akiniangalia, lakini kwa kujificha,…nikashangaa,…na akili pale ikawa imetaharuki,
akili inawaza kuwa hilo ni kweli, huyo ni kweli mke wangu, haraka nikasogea…ili
nimuone vyema, lakini kila nikisogea na yeye hujisogeza kujificha..
‘Mke wangu
umerudi…’nikasema
Nikafanya haraka
ili niende kumlaki, nikasogea upande ule wa pili..yaani huwezi amini, akili
yangu iliona hivyo,… na kilichofuatia baada ya kumkaribia huyo mke wangu,
nikamvaa na kumkumbatia…nikawa nimemganda, na kilichonishtua ni sauti..
‘Shemeji
unaniumiza….’oh, shemeji tena…kumbe alikuwa huyu binti, huyu binti alishajiweza
na akajikongoja kutoka nje, …mimi nilipohisi kuwa ni yeye kwa haraka nikamuachia,
nikageuka kutaka kuondoka. Na sauti nyuma yangu ikasema;
‘Shemeji mimi naona
nimepona nataka niondoke, maana kwa hivi sasa nionavyo mimi hata wewe
umeshapona, na kwa hali ilivyo mimi siwezi kuendelea kukaa tena hapa, …kama
unavyoona, vituko vyako vinanitisha, hadi nafikia hivi..na zaidi sasa nimekuwa
nikiota ndoto mbaya-mbaya dhidi
yako,nyingi zikinikumbusha kipindi kile ulichotaka kunifanyia mambo mabaya, kwakweli
shemeji mimi siwezi tena kukaa hapa….’akasema
‘Najua shemeji
yangu, nilikukosea sana…lakini ..’nikajitetea.
‘Shemeji yangu
hakuna cha lakini..mimi bado hali hiyo inanitesa..kumbuka sana,..ilikuwa mbele
ya dada, sasa nipo peke yangu, hivi likitokea la kutokea, atalaumiwa nani,
wakati nilishaambiwa niondoke…hapana shemeji , ngoja niondoke tu….’akasema
Nilijilamu sana, kwanini mimi ilinifikia hali
ile, kiukweli kipindi kile nilishakuwa mnyama….hapo ndio nikakumbuka tukio la
siku ile , siku ile ambayo nilimfanyia huyu binti jambo la aibu, na athari yake
ndio inaendelea hadi leo….
************
Binti huyu alikuja hapa kwangu, kama kawaida
yake alikuwa akija kumsaidia dada yake,…awali alikuwa mdogo, lakini jinsi siki
zilivyokwenda akawa anakuwa haraka
haraka, kajaliwa mwili wa kukua haraka,..ikawa sasa akija ni binti mrembo na
mimi baba tama, nikawa naanza kumtamani, lakini muda wote alikuwa karibu na
dada yake, nikaanza kumtongoza kiaina mara namletea zawadi hii na ile…, na hata
ikafikia muda nikaanza kumuomba awe mpenzi wangu…
Siku nilipomtamkia
hivyo, alishtuka sana na hakuamini …alishawhi kusikia kuwa nina tabia mbaya,
lakini hakutarajia kuwa na yeye yanaweza kumkuta hayo…
Sasa siku hiyo aliposikia
namtamkia hivyo, alibakia mdomo wazi,…baadaye akakimbia na kwenda kwa dada
yake, sijui waliongea nini… ila sasa akawa hataki kabisa kunikaribia mpaka dada
yake akahisi kuna jambo, lakini sijui kama aliwahi kumuelezea dada yake au vipi,
mimi kwa kipindi hicho sikuwa najali!
Moyoni sikukubali
kushindwa,…nikawa kila nikipata mwanya namuandama, na yeye ananikatalia, kwangu
mimi kukataliwa ni kutangaza vita…nikaanza kumchukia, maana sio kawaida yangu
kukataliwa…, wengi nikiwabembeleza kwa pesa wananikubalia tu, sasa kwanini huyu….sikukubali.
Siku moja nilibakia
mimi na yeye, ili kuondoa aibu nikanywa pombe, na alipojitokeza tu, kwanza
nikampa zawadi niliyokuwa nayo, akaikataa, nikaanza kumbembeleza akakataa,
nikaona asinipoteze e muda nikamdaka, ikawa kukuru kakara, ilichukua kama
dakika kumi, huyo binti akipambana na mimi....hakukubali
Nikaanza kumpiga,
kumpiga kweli mpaka akadondoka chini, …akiwa sasa hajiwezi, na mimi na pombe
tena, hata sijui ninachokifanya, kichwani sio mimi, alipodondoka, sikujali kama
kapoteza fahamu au vipi, nikataka kuanza kufanya mambo yangu….
Mara nikasikia
sauti ya mtu akipiga hodi,..
Binti alikuwa
kalala sakafuni, mimi nikawa sasa nasita kuendelea, … hapo ikawa salama yake,
huyo binti aliniponyoka akakimbia,….na siku hiyo hiyo aliondoka, hata bila
kumuaga dada yake… na dada yake alikuja kuhisi , lakini kipindi hicho mke wangu
hakuwa na nguvu za kunikabili..nilikuwa siambiliki..mbogo, …nina pesa, utasema
nini kwangu…
Baadae iliwahi
kuja, lakini hakutaka hata kunikaribia, na kipindi alichofika ilikuwa mimi na
mke wangu tumeshakwaruzana, na alipofika yeye ndio ikawa zaidi , ni kama
alikuja kuongeza mafuta ya taa kwenye moto..mimi hapo nikajua yeye ndiye
chanzo,…nikampiga marufuku kuwa simtaki hapo nyumbani, lakini mke wangu akasema
;
‘Huyu ni ndugu
yangu, atakuja kila nikimuhitajia…’sikuweza kuipinga hiyo kauli, lakini moyoni,
ikatokea kumchukia sana huyo binti…
Kumbe yaliyotokea
kati yangu na uyu binti mke wangu alikuja kuyafahamu, lakini mke wangu
aliniacha hivyo akijua ni nini nilichokuwa nahangaika nacho kwa kipindi kile,
japokuwa kiukweli alikuwa akiumia sana.
***********
‘Umenisikia shemeji….mimi naomba kesho
niondoke…’ sauti hiyo ilinizindia kutoka kwenye hayo mawazo
Nilimuangalia yule binti….sasa angalio langu
kwake, lilikuwa la aina yake, angalio la sasa lilikuwa la macho ya huruma na
upendo, moyo wangu kwakweli ulikuwa umeshalainika,. Huyu sasa alikuwa sio yule
binti niliyemchukia tena, huyu ni mwanamwali mwingine kabisa, binti ni mrembo,
na nikimuangalia sana, simuoni yeye, ila ninyemuona ni aliyekuwa mke wangu,…
‘Sasa nifanyeje…?’
nikajikuta najiuliza , kumbe nimeongea kwa sauti.
‘Hamna cha kufanya
shemeji,..naelewa hali yako, ama kwa swala la nauli kila kitu kwasasa ninacho..
mimi nikutakie tu maisha mema, na nashukuru sana kwa yote, wala usijali shemeji
yangu…, kwa hayo yaliyotokea huko nyuma,..nikijaliwa nikipata muda nitakuwa
nakuja mara moja moja, lakini hilo siwezi kukuahidi kabisa…maana sijui ya huko
mbele…’akasema.
Moyoni nikasema
kwanza huyu mtu anastahiki nimuombe msamaha kwa yale niliyomtendea, hajawahi
kusema kuwa keshanisamehe, hilo ni muhimu sana kwangu…nataka kwanza nisikie
kauli yake ya kusema kanisamehe.
Kama kawaida yangu nikitaka
kumuomba mtu msamaha nafanya hivyo… nikapiga magoti mbele yake…na kwa muda huo
huyo binti alikuwa kasimama tu, akiniangalia , na hilo tendo la mimi kupiga
magoti mbele yake akalipokea kwa mshangao mkubwa, niliona machoni mwake…
‘Nisamehe sana …shemeji
nakuomba, nipo chini ya migu yako, nakuomba sana sana, unisamehe,..kiukweli
kama sio wewe hadi leo ningekuwa mtu mwingine, ..na nimegundua kuwa bila wewe
sizani kama nitaweza kuishi peke yangu humu kwenye hii nyumba,sitaweza kuishi kwa
amani…nakuomba sana unisamehe, na nakumba usiondoke tafadhali….’nikasema
Kwanza alitulia,
akibabaika…halafu akasema;
‘Shemeji ….naomba
usinipigie magoti,…mimi sio mtu wa kupigiwa magoti, sina hadhi hiyo kabisa,…..ama
kwa kukusamehe, mbona mimi nilishakusamehe tu shemeji yangu..najua sio wewe,
nilijua sio wewe ni ibilisi tu, na kila siku nimekuwa nikikuombea, ili mungu
akuongeze,…lakini sasa shemeji..naomba uinuke, …na ujue ukweli kuwa sasa muda
umefika, wa mimi kuondoka, na unielewe kuwa na mimi nahitajia maisha yangu…’akasema.
‘Maisha yako…eeh, ehee,
unajua shemeji hapo na mimi nilikuwa na maongezi tena mazuri sana, kuhusu
maisha yako,…unajua wewe ndiye mtu wangu uliyebakia,..unaona ndugu zangu wote,
wamenikimbia,sina kitu, hata marafiki wapo tena, sina kitu…umebakia wewe tu…,
wewe ni zaidi ya ndugu….na nataka maisha yako yawe hapa, uishie hapa…’nikasema
‘Hapana shemeji…wewe
unastahiki uje uoe,…na hilo dada alilisisitizia sana kuwa akiondoka hapa duniani,
atafurahi sana ukioa mapema, nakumbuka kabisa alisema hivyo, …ila kwa mimi shemeji
haitawezekana kabisa kuendelea kukaa humu, ninaomba unielewe tu...’akasema.
‘Umekumbuka sasa
eeh, dada yako kumbe aliwahi kukuambia hayo,..japokuwa sikutaka kuoa, lakini
kwa ajili yake, basi mimi nataka nije kufanya hivyo, sasa unaonaje ukikaa hapa
ili niweze kulifanikisha hilo…?’ nikasema na kumuuliza.
‘Nakumbuka sana
jinsi dada alivyosema, kila nikipokuwa naye karibu aliniambia mengi,na moja
wapo ni hilo kuwa mimi nijitahidi
kukusaidia mpaka hapo ukiwa na hali nzuri ndio mimi nirudi kwetu
kijijini…ndivyo alivyoniomba hivyo…, hakuna zaidi, hajasema niwe naishi hapa na
wewe milele,…mpaka uje kuoa tena… hapana, halafu siwezi kuendelea kukaa zaidi
humu, maana mimi sio ndugu yako, watu wananifikiria vibaya…’akasema
‘Sasa nakuomba kitu
kimoja, nakuomba uniache niwazie hilo, ila nakuomba sana usiondoke kesho,
nitaka tuongee, tafadhali sana….’nikasema.
‘Kesho shemeji mimi
naondoka….siwezi kukaa zaidi hapa tena…’akasema huku akiondoka kurudi ndani.
************
Ilikuwa kwenye chakula cha usiku, aliniandalia
yeye, ..maana sasa alishaweza kufanya kazi zake kama kawaida, …na aliweka
chakula mezani kwa haraka akataka kuondoka, hapendagi kula na mimi mezani…
‘Shemeji nakuomba
leo ..tule pamoja hapa mezani, nataka kuongea na wewe jambo moja…’nikasema na
yeye kwanza alionekana kusita, lakini kwa heshima akafanya hivyo.
Nilimuanzia
maongezi ya mbali..kwa kuongea mimi najua sana, najua jinsi gani ya kumweka mtu
sawa…na hatimaye nikamuelezea dhamira yangu,..kuwa mimi ninataka kumuoa yeye,
awe mke wangu wa ndoa…hapo sasa…
‘Eti nini…wewe baba
wewe..hapana,….mimi nimekuwa nikiishi hapa , kwasababu tu ya dada, na wala
sikuwahi kuwa na wazo kama hilo hata siku moja…, nakuomba tena sana ondoa wazo
kama hilo, usije kuja kuumia moyo wako….mimi sitaweza kuishi na wewe, siwezi na
haitawezekana…’akasema akionyesha kweli ana nia hiyo.
‘Shemeji….nakuomba sana
sana, urudishe moyo wako nyuma,..najua mengi yamepita, lakini niangalie na
mimi, ..na kiukweli kama ukiondoka, ukaniacha… huku nyuma utasikia mengine,
siwezi kuishi bila ya wewe..nakupenda sana …na nakuona wewe kama mke wangu,
kila nikikuangalia nakuona wewe kama jilio jipya la mke wangu ’nikasema
‘Mhh.. shemeji huko
umeenda mbali, siwezi kuwa mke wako.. hapana..nimekuwa mimi nikikusaidia wewe
kwa vile dada nilimpenda sana, lakini kiukweli sijawahi kufikiria kitu kama
hicho, nakuheshimu sana shemeji yangu,.. eti leo mimi nije kuolewa na wewe,
hapana..hata wazazi wangu hawatakukubali hilo…’akasema,
‘Kwanini sasa..kwa
vile mimi …nina matatizo au..nitakufanya kitu kibaya..shemehi mimi
nimeshabadilika,..mimi sio yule mtu wa zamani,…nimetubu, nimemrejea mola wangu,
..na toba yangu,..inatoka moyoni..nakuomba unielewe…’nikasema
Mdada huyo
akatikisa kichwa kukata, kata kata….
Ikawa kazi kubwa
sana ya kumshawishi huyu binti, nilitumia kila njia ninayoifahamu mimi, na
ikafikia hatua ya kupiga hata magoti..mimi nikitaka kitu, naigiza kila jambo,..hutaamin,
hata chozi lilinitoka,
Baadaye huyo binti akasema anahitajia muda wa
kuliwazia hilo, na hapo ikanipa moyo kuwa huenda atanikubalia ombi
langu..unajua tena.., ile hali ya kuishi naye karibu-karibu, nahisi hata yeye, ilishamjengea namna fulani ya upendo..lakini
huenda uwoga…
Basi asubuhi ndio
nilitarajia ataondoka, akaja kuniaga, kiukweli alishapanga kuwa ni lazima
aondoke, ..ila sasa hata akiondoka najua anaondoka na jambo jingine kichwani,…aliniambia
anaondoka na wazo hilo kichwani mwake, yeye kama yeye anaweza asiwe na maamuzi,
anaomba kwanza aende nyumbani akaongee na wazazi wake kwanza .
‘Shemeji unipe
muda, kwanza ni swala la kunishtukizia,…najua , nakufahamu, kiukweli,…sina la
kusema,..itakuwa vigumu sana kuja kukuzoea,..lakini siwezi pia kusema hapana,
sikutaki,..ngoja kwanza nilifikishe hilo ombi kwa wazazi wangu na kama wao watanikubalia,
basi …kwa heshima ya dada yangu nitakubali niishi na wewe….’ Akasema
‘Uishi na mimi kama
mke na mume…’nikamalizia mimi, na yeye kwa aibu akageuka pembeni.
‘Tuombe mungu tu…’akasema
hivyo, na siku hiyo akaondoka kurudi kwao…
NB: Mhh, mbona
inazidi kuwa ndefu hii stori….msijali, tutakuja kumalizia sehemu iliyobakia,
tukijaliwa
WAZO LA LEO: Ili tufanikiwe kwenye shughuli zetu, shughuli za kimaisha,
zenye hitajio la mafaniko fulani, yawe ni ya kumtafuta mwenza wa maisha, yawe
ni yakutafuta maisha bora, yawe ni ya kuishi na familia yako vyema, ujirani mwema
nk…tukumbuke sana kumweka mungu wetu mbele, tuombe sana, tumuombe mola ukweli
wa kumuomba, kwani yeye ndiye anayefahamu shida zetu na njia ipi sahihi ya
kufanikiwa, yeye ndiye anayemfahamu mwenza wetu wa kimaisha,..omba na usichoke
kuomba.
Mola wetu
tunakuomba, utukubalie maombi yetu, tuwe na wenza wema, maisha mema, afya njema
na Baraka tele…Aamin.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment