Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, November 2, 2016

TOBA YA KWELI-16


‘Na mimi siwezi kuondoka bila kukuambia yote aliyotuagizia mkeo…maana hayo maagizo hayataki kuchelewesha, kama ni kucheleweshwa iwe ni juu yako….na lolote likitokea tusije kuja kulaumiwa sisi kuwa hatukuweza kukuambia, na hata mbele ya mungu tuwe tumenawa mkono, yeye ndiye atakuwa shahidi wetu…’hayo yalikuwa maneno ya docta, yakiwa yananielea akilini
Nilifika nyumbani kwangu nikiwa nimejaa hasira, na sijui kwanini,…kwa muda huo sikujijua, na sikujua sababu, zaidi ya kuwa hivyo.

Nilifungua mlango kwa haraka, na kama mtu angejitokeza hapo kwa muda huo, sijui ningemfanya nini.. akili ilikuwa imesahau kabisa kuwa nilikuwa na jukumu la toba,…toba ambayo masharti yake ni kuwa uwe mbali na jaziba, uwe mbali na husuda, chuki…visasi..kwa kifupi ilitakiwa moyo uwe safi, lakini kutokana na hayo waliyoniambia docta na mkewe, vikanifanya nisahau kila kitu…

 Niliingia ndani kwangu na kujipweteka kwenye sofa,  nikiwa nimeangalia juu, kama nahesabu vilivyopo huko juu, japokuwa akili haikuwepo hapo, ilikuwa mbali kimawazo…na mara nikahisi kuwepo kwa mtu mwingine, ..
ILIVYOTOKEA, wakati nikiwa nimelala hivyo,.. ilikuwa kama nimeshikwa na usingizi , au ganzi fulani hivi,  na hii hali imekuwa ikinijia vipindi hivi vya majaribu,  yaani kinakuja kitu kama kausingizi ,  halafu mwili unalegea kabisa, na baada ya hapo kunatokea kitu kisicho cha kawaida…

Sasa,..ninachokumbuka mimi ni kuwa,  macho yangu yalikuwa mazito, na mwili ukawa umeshikwa ulegevu, kwa hali kama hiyo unachopweza kukifanya ni kuyazungusha  macho kutizama huku na huku, lakini viungo vinakuwa havina nguvu ya kuinuka, ila unaweza ukajiwa na hisia ya kuwa umeinuka, ukafanya jambo…

Haya….hali hiyo ilipotokea kwa muda huo, ndio nikaona jambo la ajabu..

 Nilimuona mtu kaja kusimama mbele yangu, kwa mbali kidogo,..na haraka nikatambua kuwa ni mke wangu, yaani ndivyo nilivyoona kitaswira na kiakili…!

Sikuwa na haja ya kujua mke wangu katokea wapi, ila nilichojiwa nacho akilini, ni kutaka kuinuka na kwenda kumpokea, kumkumbatia..lakini mwili hauwezi kuinuka,…hata hivyo akili ikanivuta kuwa nimeshasimama…sasa namsogelea, lakini simfikii…nikawa namkodolea macho t.
Mke wangu hapo alionekana wa ajabu kabisa, alikuwa kavalia vizuri, nguo nyeupee na nyepesi ambayo niliweza kuona maumbile yake ya ndani…kwanza nikataka kumuuliza kwanini mke wangu kavalia hivyo, sio kawaida yake, lakini nikasema moyoni, hizo labda ni nguo za kulalia, haina shida,…lakini  kulikuwa na kitu kingine cha ajabu…..

Pamoja na y a kuwa mke wangu kavalia hivyo, na niliweza kuona maumbile ya ndani, lakini sikuweza kuyaona yalivyo, maana, yalikuwa yakimeta meta, kwahiyo huwezi kuona mwili, unachoona ni kama mchoro wa mwili wake wenye miale kama ile ya jua na macho yanapata shida kumuangalia , nikainua uso ili nimuangalia usoni,…alikuwa ndio yeye…, nikahema

‘Sasa kwanini simfikii mke wangu…’nikasema huku nikimsogelea kihisia, lakini kila nilivyosegea alionekana kwa umbali ule ule….

 Sasa yeye akawa ananiongelesha jambo…, lakini sikusikia anachosema,..ni kama ananionya au kunisuta, au kuniashiria nifanye jambo fulani ..na kuna muda alionyesha kama kukasirika,…na ghafla nikasikia sauti…

‘Shemeji nikutangenezee chakula gani…’ Ilikuwa sauti iliyonishtua, …na hapo hapo ile hali ikaisiha, na haraka nikazindukana na nilipogundua kuwa aliyekuwa kasimama mbele yangu ni yule mtu nisiyetaka kuongea naye, kwa haraka nikasimama,..hasira chuki, vikauteka tena ubongo wangu…

‘Aaaha,  …kumbe ni huyu mshe—nzi,….’ nilisemea akilini haku nasonya..nikatembea kuelekea chumbani.
 Nilipofika chumbani kwangu, nikajitupa kitandani, na wakati nafanya hivyo, maneno ya docta yakatanda kwenye ubongo wangu:

‘Na mimi siwezi kuondoka bila kukuambia yote aliyotuagizia mkeo…maana hayo maagizo hayataki kucheleweshwa, kama ni kuchelewesha ucheleshe wewe mwenyewe….na lolote likitokea tusije kuja kulaumiwa na mbele ya mungu, ….’.
Nilijiunua kichwa changu na kuangalia darini, sasa nikaogopa ile hali ya kuona taswaira isije ikanirekjea tena,…nikajiinua kwa haraka, halafu nikasimama na kutembea kuelekea dirishani, na wakati natembea akili yangu ikawa inaendelea kukumbuka mazungumzo ya docta na mkewe,….maneno waliyokuwa wakiongea wakati huo mimi nilikuwa natembea kutoka nje kwa hasira, lakini  niliyasikia, baadhi…

‘Mkeo alikupenda sana…hakujijali yeye mwenyewe…sikia kwanza usiondoke…yeye alikujali sana..hakuijali nafsi yake kama wewe… kwani alifiki hatua ya kukutafutia hata mke gani umuoe,….’ Hayo aliyasikia, lakini sikutaka kusikia zaidi, ila kuna neno la mwisho lililonifanya nikimbie kabisa humo ndani…

Mara nikasikia mtu akigonga mlangoni, nikajua ni nani, sikuitikia nikakaa kimia, na mara simu yangu ikaita….

Nikabakia kujiuliza niitikie huyo wa mlangoni au kwanza niangalia ni nani anayepiga simu, ….mara yule mlango akaacha kugonga, na mimi nikaisogelea ile simu, ilikuwa namba mpya kwenye simu yangu…nikaiangalia ile simu, moyoni sikupenda kuipokea, sikutaka kuongea na mtu……..lakini ikaonyesha mpigaji , kweli kadhamiria kuongea na mimi

Nikaiweka hewani..na sauti ya docta ikasikika,…. alikuwa ni docta, alikuwa katumia namba ngeni,..huenda alijua akitumia simu yake, nitagoma kuipokea.

 ‘Jirani nisikilize kwa makini usikate simu kwanza, hili ninalokuambia ni la muhimu sana, mimi nipo safarini, lakini sitakuwa na amani kama hutalisikia hili jambo, uliondoka kabla sijakumalizia,….’ Ni kweli nilishajiandaa kuikata simu,lakini nikaona nisikilize tu…

‘Nimekuambia kuwa mkeo, alituambia ni nani uje umuoe…  na sio mimi au mke wangu, hilo lielewe wazi, na ni vyema ukamsikia huyo mtu…najua kwa hivi sasa huna unayemfikiria, lakini tuna uhakika ukituliza kichwa chako utagundua kuwa kweli huyo aliyemtaka mkeo umuoe ndiye stahiki yako,…kwahiyo usije ukakasirika ukiona labda sisi ndio tumempendekeza, labsa kwa masilahi yetu…
Akilini nilitaka kusema sitaki kumsikia, lakini kwa namna nyingine iliuliza ni nani kwa nini anachukua muda kumtaja,…
‘Mkeo aliona mbali , anakufahamu na yeye aliliona hilo kwenye njozi zake, anakujua kitabia, anajua unahitajia nini…kama nilivyokuambia awali kutokana na imani aliyokuwa nayo mkeo kwa mungu wake, mwenyezimungu alimpa dalili fulani fulani..na mojawapo ni hiyo kuwa hatapona,..na nyingine ni nani anayekufaa kuwa awe ni mke wako…

‘Sasa ….mkeo alituambia kuwa, wewe una hasira sana, wewe una hamaki, wewe una tamaa, na wewe unataka kile ukitakacho ukipeta, kwahiyo unahitaji mke mwenye subira….na ndio maana akaona kuwa, mke anayekufaa, si mwingine ni huyo huyo unayeishi naye humo ndani ya nyumba,…

‘Unasema nini…’hpao nikajikuta ninaongea

‘Ndio alisema mke anayekufaa …  ni huyo huyo binti anayekusaidia kila siku hapo nyumbani kwako, mkeo anamfahamu sana, mkeo alishampima, lakini hakuwhi kumwelezea huyo binti kuwa wewe ndiye unayefaa kuolewa na mume wangu, ila alimuomba awe karibu nawe, akusaidia mpaka uwe umejiweza mwenyewe, tatizo ni je atakubali, hiyo ni kazi yako……’akaendelea kusema.

Hebu fikiria mwenyewe…mwanzoni ilikuwa nikimuona huyo binti na hisi hasira, nahisi kama ndiye mbaya wangu, ndiye…aliye..oh, sasa naambiwa kuwa ndiye mke wangu alitaka nimuoe…..haiji akilini, na upendo utatoka wapi wakati chuki zangu zimejaa tele dhidi ya huyo binti, …haiwezekani….hapo, nikasema;

‘Nyie watu kweli mumenichoka,…,kwanini mumenidharau kiasi hiki,hata kama sasa nimeishiwa kiasi hiki,….lakini hamuwezi kuni, eti nimuoe mfanyakazi wangu wa ndani mnahisi kuwa labda mimi natembea naye, au sio, sitaki kusikia zaidi, nakata simu….!’ Nikawa sasa nikitaka kuikata ile simu,lakini kila nikibonyesha kitufe cha kukata simu ikawa haizimiki na sauti ya docta ikawa inaendelea kuongea;.

‘Hili ninalokuambia mimi sio uwongo, ni mkeo mwenyewe, alituambia hivyo, kuwa huyo ndiye chagua lake na huyo ndiye anayeweza kuishi na wewe, wengine hawatakuweza, kutokana na tabia yako..na zaidi ya hayo, yeye kwa njozi zake, alivyoonyeshwa kwa ishara huyo ndiye atakupatia kile ulichokuwa ukikitafuta siku nyingi….’akasema docta.

‘Huyo ndiye ataweza kukupatia mtoto…’akasema na mimi hapo nikahisi kama kitu kimemwagiwa kichwani , kitu cha baridi.

‘Jirani mimi kama nilivyokuambia, huwa naota tu, na ndoto kwangu ni ndoto tu, lakini ndoto ya jana imenifanya nifikiri sana… jana usiku, hutaamini mkeo ainijia tena kwenye ndoto,…ndoto kwangu ni ndoto tu, lakini kwa hii nimelichukulia kuwa ni kweli…alikuja akiwa kavalia vaza la ajabu, anameta meta mwilini…..sijui nikuelezeje…’akasema docta
Baadaye nikawa sina mawasiliano na docta, nahisi walifika sehemu hakuna mtandao…nikaiweka simu kitandani na sikutaka kulala tena, nikatembea hadi dirishani na kuangalia nje

Nikawa najiuliza ilikuwaje, ina maana ,..ndoto ile ile niliyoota mimi, na docta naye kaiota hivyo hivyo…maana docta kanisimulia vile vile kama nilivyoona mimi…alimuona mke wangu akiwa na vazi lile lile, akiwa na maumbile yale yale….hapa sasa kuna jambo, nikahema kwa nguvu…
**********
‘….na ndio maana akaona kuwa, mke anayekufaa, si mwingine ni huyo huyo unayeishi naye humo ndani ya nyumba,…’ maneno haya yakawa yanajirudia sana kichwani mwangu, mpaka nikahisi vibaya, …

‘Mimi siwezi kumuoa huyo….sitaki sitaki….’nikawa nasema huki najikuna kuna kichwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Baadaye nikatulia, na kuanza kuchanganua hilo jambo, kwanza nikajiuliza kulikoni..

‘Kwanza sitaki kuoa, ..pili simtaki aliyependekezwa, tatu….’hapo nikasikia mlango ukigongwa, nikajua ni nani..sikutaka kuitikia nikakaa kimia, huku nikizama kwenye mawazo…

‘Mfano..nasema mfano, naamua kumuoa ili kumrizisha mke wangu, nitauweka wapi uso wangu…’nikasema kimoyo moyo

Niliwaza mbali nikikumbuka maneno ya watu, walivyokuwa wakinihsi vibaya kuwa mke wangu kafariki, na sasa nakaa na kimada, najifanya ni mfanyakazi wangu wa ndani kumbe ni kimada wangu…najifanya naombeleza kumbe naendekeza zinaa…., sasa wasikia kuwa nimemuoa, si ndio watasema, `mnaona tulisema…huyu jamaa anatembea na mfanyakazi wake ndani sasa kathibitisha kabisa, ….’ Nikawaza hivyo.

‘Ndio….kaniambia uoe, na usioe mtu mwingine zaidi ya huyo binti mnayeishi naye huyo ndiye chaguo lake, sasa kama unataka kumkaidi mkeo sawa, na huyo ndiye atakaye kupatia mtoto…..’nikakumbuka maneno ya mke wa docta.

****************
 Siku hiyo ikapita, na nyingine na nyingine, mawiki , mwezi..miezi…

Kiukweli sikupenda kuoa tena..lakini hata mimi ndoto za mara kwa mara za kunijia mke wangu kuwa nifanye kile alichokita zikawa zinanitesa sana, siku zikawa zinakwenda, nikawa natokewa na ndoto hizo zingine mbaya, mpaka napiga kelele, kama mtu aliyechanganyikiwa.

Hali hi iliendelea mpaka siku moja huyo binti akamuita docta wa akili, huyo docta alifika, nikiwa hata sina habari…na akaja kujitambulisha kuwa yeye ni docta wa mambo ya akili, na amefika hapo kuja kunisaidia..
‘Nani kakuambia ninaumwa akili..mimi sijachanganyikiwa…’nikasema

‘Unaweza kusema hivyo, lakini ukijiangalia kwenye kiyoo utagundua kuwa wewe haupo sawa..unahitajia matibabu…’akasema

Sikutaka kubishana naye sana, nikatulia, na yeye akaanza kunihoji, kwanza nilimtolea nje kuwa mimi siumwi, lakini baadaye akaniweka sawa, nikamuelezea mengi yanayonitokea…mengi kuhusu maisha yangu..lakini sikumuelezea hilo la kuwa natakiwa nioe, na …nimuoe….

‘Sikiliza..hali uliyo nayo, unahitajia mke,..labda nikuulize ni kwanini huoi…?’ akaniuliza,

‘Mimi sitaki kuoa…aliyekuwa mke wangu ndio huyo kafariki, na mimi nilishakufa kimwili, kihisia…sina hisia za mke mwingine yoyote….’nikasema na docta kwa utaalamu wake, akanielezea mambo mengi, kuwa hayo yanayonitokea ni kuwa akili yangu haitaki kuondokana na kumbukumbu za mke wangu na kwahiyo ili hizo kumbukumbu ziondokane na mimi dawa yale aliyoiona yeye, ni mimi kuoa.

‘Oa mke ambaye atakuliwaza, wake mungu kawaleta humu dunia, kutusaidia, na kutuliwaza sisi wanaume..mchague ambaye atakupendezesha, ambaye anaweza kuchukua nafasi ya mke wako…vinginevyo, hali hii haitakwisha, na huko unapokwenda ni kubaya  tena kubaya zaidi, umeshafikia hatua mbaya sana, chukua hatua kabla hujachelewa…’akasema docta na baadaye akaondoka.

'Na ningeshauri, awepo mwanaume....huyu binti..ni hatari kuendelea kukaa na wewe humu ndani....'akasema docta, na nilimuangalia yule binti, akionyesha wasiwasi machoni.

 Docta baadaye akaondoka....

Docta alipoondoka tu, nikamvaa huyo binti, nilimfokea sana huyo binti mpaka akawa analia.., na hata nikafikia hatua ya kumsema vibaya kuwa hizo ni mbinu zake,..

‘Kama ni mbinu zako za kutaka kuendelea kukaa hapa …basi utaondoka tu, sikutakia humu ndani, uondoke ...nani kasema anakuhitajia humu, uondoke..…’na huyo binti alibakia kimia,a yeye akabakia kimia hakujibu kitu zaidi ya kulia tu.

Ikapita miezi, hali ile ikawa inaendelea kunitesa, na kweli kila mtu aliyeniona alijua kuwa mimi sasa nimechanganyikiwa, haikupita muda wakawa wanakuja ndugu zngu , hata wazazi wangu, na kila mmoja aliyefika aliishia kunishauri nioe..., lakini sikuweza kuwasikiliza,…

Sasa siku moja ndio niliota ndoto mbaya zaidi….ndoto iliyonifanya nipige ukulele sana,…na nilipozindukana, nikahisi moyo kama unatolewa pumzi ..ikawa kama nimebanwa..ilichukua muda mpaka kujisikia vyema, nikatulia. Na ujue kwa muda wote huo anayenisaidia ni huyo binti.

 Hata sijui ilitokeaje…nakumbuka tu...ilikuwa siku huyo binti keshaamua kuondoka, …alikuwa ameshafungasha kila kitu,…akawa sasa anaiga, nilishamkubalia aondoke, kwangu mimi kwa uoni wangu huo wa kuchanganyikiwa,....sikuwa naona umuhimu wake, ..

NAFSI, AKILI,…ile kuwaza kuwa huyo binti sasa ndio anaondoka kabisa, maana alishasema yeye anaondoka na hatarudi tena,na nilimwambia ni bora afanye hivyo maana akifanya hivyo itanisaidia hata mimi...huyo binti alisema sawa kwa sauti ya unyonge, hakuwa na jinsi...

Sasa ndio huyu kweli....keshafungasha, ananiaga.

Sijui ilikuwaje,nilihisi upweke fulani ghafla. nilihisi kumkosa mtu muhimu kwangu …ilikuwa kama vile namuona mke wangu ananiaga, ghafla nikajikuta nimemkumbatia huyo binti….huku nasema;

‘MKE WANGU USIONDOKE,…usinieche peke yangu…..’ Huyu binti alibakia kaduwaa, na kwa vile alishanizoea kuwa nimechanganyikiwa, yeye alitulia tu, akiwa anaogopa, unajua huyu binti japokuwa anaishi hapo lakini ananiogopa kweli, hasa akikumbuka siku zile za zamani nilipotaka kumbaka....

Baadaye huyo bnti akasema;

‘Shemeji mimi sasa naogoa kwa hali uliyofikia,...hata hivyo, pia haifai wewe kubakia peke yako, hutaweza, ni bora nipitie kwa ndugu zako mmoja aje kukaa na wewe hapa…’akasema

Oh….nikakumbuka, kumbe sio mke wangu… nikakurupuka, nikasimama pembeni,nilikaa kimia kwa muda, na ghafla machozi yakaanza kunijaa machoni, nikajikuta nikilia..nililia sana,..unajua kulia..., nililia sana siku hiyo…mpaka nikawa sina nguvu tena..halafu nikasema;

‘Mke wangu…nakupenda sana, haya yote ni kwa ajili yako, sijui nifanyeje nini, kukuonyesha pendo langu kwako, namuomba mungu aichukue roho yangu, ili nije huko ulipo…ooh,…’nikatulia ..na nilihisi yule binti akiwa karibu yangu, alifanya kama vile mama anavyofanya kwa mwanae..akawa kaniwekea mkono wake begani, kama kuniliwaza  akasema;

‘Shemeji,..mungu atakusaidia, utapona tu,..haya yana mwisho, lakini usifikie hatua ya kumkufuru mungu, kwani yaliyotokea ni kwa mapenzi yake, sio kwa mapenzi yetu, mimi na wewe hatuna la kufanya, ila shemeji inabidi mimi niondoke...ila nakuahidi nitajitahidi mmoja wa ndugu zako waje..'akasema

'Mimi ...najua nakwenda kinyume na maagizo ya mke wako, alisema niskuache peke yako, maana hakuna anayekuweza.... lakini mimi sasa naanza kuogopa…ninaogopa chochote chaweza kunipata, ..samahani sana shemeji, kwa kweli kwa hali kama hii sina jinsi, ni lazima niondoke,  kwaheri shemeji…’akasema sasa kiwa keshabeba mizigo yake.

Nilibakia nimeshikwa na butwaa…na nilianza kuhesabu hatua za yule binti, akiondoka... moja , mbili tatu,..huyo anaondoka…alipofika mlangoni, sikuweza kuvumilia, nikajiinua , na kwa haraka nikaanza kumkimbilia huyo binti, kabla hajavuka kizingiti cha mlango..nikamfikia na kumshika begani.

Huyo binti alishtuka sana, mpaka akadondosha lile begi, na karibu apige yowe....

‘Binti tafadhali, nisamehe….kabla hujaondoka nakuomba unisamehe..nipo chini ya miguu yako….' nikasema sasa nikimpigia magoti.

Huyo binti akawa anatetemeka kwa uwoga,..akabakia kuniangalia macho yalikuwa na wasiwasi, kaduwaa, hajui hata fanye nini,  lakini mimi niliendelea kumuomba msamaha….na mara nikasikia gari nje likisimama, na mara nikasikia sauti ya mtu akipiga hodi…. Na kabla sikajaa sawa,…. huyo binti, akalegea, na kudondoka chini,  sakafuni na kupoteza fahamu…

NB: Nashindwa kuimalizia leo, kuna mambo mengi hapo yalitokea na ili kisa hiki kiishe vyema, ni wajibu kuyaandika, samahani sana tukutane sehemu ya mwisho

WAZO LA LEO: Akili zetu za kibinadamu zinapokutwa na mitihani , iwe ya misiba, iwe ya njaa, shida, au matatizo mbali mbali kama ya kukataliwa, …kumkosa uliyempenda, nk..hufikia kujilaumu sana, na hata kujiona hatuna faida,..na wengine hufikia kubaya na kusema bora waafe…hii sio sahihi, tujue kuwa mambo hayo hutokea kwa mapenzi ya muumba.

Tujue kuwa mola wetu, yeye ndiye anayejua ni kwasababu gani, hayo yanatokea, huenda mengine hutokea ili iwe ni heri kwetu, na mengine hutokea maana muda wake umefika. Sasa sisi kama wanadamu watiifu kwa mola wetu kinachowajibika kwetu kwanza ni kumshukuru mola wetu…na, pili ni kuzidi kuomba rehema zake, maana yeye ndiye mjuzi wa yote.


Ewe mola wetu, tupe subira , tuondolee mitihani hii ya maisha na ikitukuta tupe moyo thabiti wa kuweze kusubiria, na utujalie mafanikio mema…bila wewe mola wetu, sisi hatuwezi kitu, …sote tuseme Aamin…. 

Ni mimi: emu-three

No comments :