Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, August 2, 2016

TOBA YA KWELI-8

   

  Marejeo..niliamua kuikimbia nyumba yangu kuepusha shari...niliondoka huku nikijua huenda nimeshamu-ua mke wangu, ..na docta aliyekuja kumtibia alikuwa taabani kwa kipigo changu...nikaenda kupata hifadhi kwa rafiki yangu, na kufika huko tu nikapotewa na fahamu..

 Baadaye hali ilirejea , nikakutana na mshauri wangu wa kiimani, akanikumbusha kile nilichoahidi,..kutubia madhambi yangu ili iwe ni tiba ya matatizo yangu, matatizo yaliyonifanya nisiwe na raha hapa duniani, japokuwa nina mali, mke mnzuri...lakini...

Je nitaweza, kulifanikisha hilo.. kwani kila hatua ilikuwa ni ngumu na yenye mitihani migumu,...na sasa nipo kwenye kizingiti kigumu...KUSAMEHE WALIONIKOSEA..!

Walikosea hadi kuingilia ndoa yangu..na kuharibu, ...na kuharibu kile nilichokuw nikikitafuta!

                        Tuendelee na kisa chetu

                                             *************.

 Nilipofika nyumbani kwangu, kabla hata sijalifikia geti la kuingilia, nilihisi mwili ukinisisimuka,  kwangu mimi hiyo ni ishara kuwa sipo salama, kuna adui karibu..mimi ni mpiganaji, na nilipokuwa jesini, nikijihisi hivi, najua sipo peke yangu, kwani adui karibu, na natakiwa nijihami kwa haraka,lakini sasa sipo vitani…nipo uraiani, natakiwa nisionyeshe hali yoyote ya mashaka.

Nilichofanya kwanza nikujaribu kuchukua tahadhari zote,..nikavuga nikichunguza mzunguko wote wa eneo langu kwa macho huku natembea , kuelekea mlangoni, na hadi nafika mlango wa geti nilishajua kuna nini kuzunguka eneo.

Kulikuwa na watu ….lakini hakuna niliyemtilia mashaka, kwani walikuwa wakiwa na shuguli zao pembezoni mwa ukuta,…nikawa kila mara nawatupia jicho kw uficho kuona kama kuna yoyote anashauku na mimi, lakini hakuna aliyeonyesha dalili hizo.
Nikashika mlango wa geti na kuusukuma,..siku hizi hata mlinzi hakuna!

Nikaingia ndani na kukagua maeneo yote ya kuzunguka nyumba yangu, lakini kwa macho,  mpaka nilipojirizisha kuwa hakuna tatizo, ndio nikashika kitasa cha mlango, ile na ile nakigusa tu,nikasikia sauti ikilia nyuma ya nyumba.

Kwa haraka nikakiachilia kile kitasa  na kwa haraka nikakimbilia nyuma ya nyumba…nilisikia mtu akidondokea nyuma ya ukuta, nikajua kweli kulikuwa na mtu huku nyuma, nikachunguza sehemu zote, na nilipoona hakuna zaidi, nikarudi mlangoni nikafungua mlango, kwa ufunguo wangu ninaotembea nao.

Kwanza nilishikwa na butwaa, …

 Ndani kulikuwa shangala baghala… utafikiri kulikuwa na vita vya dunia, vitu vimevunjika, …hakutamaniki..sikuamini kuwa ni mimi niliyefanya yote hayo, nahisi kama kuna mtu alikuja akaongezea kama anatafuta kitu…

Nikajaribu kupanga panga vitu,lakini akili haikunikaa sawa, nikajiona nimechoka, napoteza muda…haraka nikaacha hiyo kazi na kutoka nje, nikitafakari la kufanya kwanza.. Nikaona kabla sijafanya lolote nijua hali ya mke wangu.

Simu sikutaka kuiwasha kabisa,….ukiwa kwenye shughuli zangu, simu ni nzuri sana, lakini pia ni chanzo kikubwa cha kukufichua wapi ulipo, nikaona niachane na simu kwa muda, haraka nikaelekea kwa jirani yangu ninayelewana naye..huyu mara kwa mara tunakutana na kuongea…, nilipofika kuulizia kama wana taarifa yoyote kumuhusu mke wangu nikaambiwa;

‘Si nimesikia kuwa mke wako yupo hospitalini anaumwa,…na ana hali mbaya sana, kwani wewe ulisafiri, kweli jana pia nilisikia watu wakijaribu kukutafuta sana, hupatikani umezima simu yako, ni kwanini unafanya hivyo..’akasema kwa kunilaumu.

‘Kwani umesikiaje, kuwa mke wangu ana hali gani…?’ nikauliza

‘Sijasikia zaidi.., nilitaka kuja kwako kuukulizia, lakini niliposikia kuwa haupo, nikaona nisubirie tu…hata hivyo, mbona watu wanasema ndani kwako, yaonekana kama kuna majambazi waliingia, kwa jinsi kulivyoonekana, nilitaka leo nifike mwenyewe niingia maana tunajuana, lakini ndio bahati hii umekuja…’akasema

Lakini kuna watu waliamua kuingia ndani na kuchungulia dirishani wakikutafuta, wakaona ndani vitu vimevunjwa vunjwa….kwani kulitokea nini..?.’nikaambiwa na jirani huyo na mimi sikutaka kusema lolote nikauliza;

‘Mke wangu kalazwa hospitalini gani?’ nikauliza, na jamaa akataja jina la hospitali ambayo, inamilikiwa na mbaya wangu, niliposikia hivyo kwa haraka nikageuka kuondoka,na huyo jirani yangu akasema;

‘Na pia nimesikia kuwa unatafutwa na polisi…’ akasema akiniangalia kwa mashaka.

‘Natafutwa na polisi kwanini…?’nikauliza nikijifanya nashangaa, huku nikianza kutembea kuondoka.

‘Mimi sijui…unajua mimi naumwa sijaweza kutoka nje wiki sasa.., hayo nimeyasikia tu…sasa sijui umefanya nini….’akasema huyo jirani yangu akiniangalia kwa mashaka wakati huo mimi nilishafika mlangoni naondoka zangu.
‘Uwe makini jirani…’akasema

Sasa moyo ukaanza kunienda mbio, nikajua yawezekana jirani yangu huyu naye anajua jambo, kumuhusu mke wangu, lakini hakutaka kuniambia moja kwa moja…na kama polisi wananitafuta yeye ndiye atakuwa wa kwanza kuulizwa, kwani wengi wanajua tunafahamiana kwa karibu kama majirani…sasa hawa polisi wananitafutia nini..ni kuhusu mke wangu au…ooh, yawezekana,

‘Kwa kumuumiza dakitari…’nikasema

‘Sizani kama mkewe wangu ataweza kunishitaki, kuwa nimempiga..na kama ana hali mbaya, au …hwezi kuwa kafariki, haiwezekani…, sasa natafutwa na polisi kwa kosa gani?’ nikajiuliza huku nikitembea kurudi nyumbani kwangu, na kabla sijafungua mlango nikahisi kuna mtu ananichunguza, nikafanya kama nafungua mlango halafu kwa haraka nikageuka kuangalia nyuma…hakuna mtu.

‘Ni lazima kuna mtu ananichunguza..’nikasema, lakini sikutaka kuchunguza zaidi , nikaingia ndani. Nilikaa ndani kwa muda, nikijaribu kuwaza,..sikutaka kuwasha simu yangu kwanza, baadaye, nikatoka nje,wazo jingine likanijia kichwani.

‘Niende huko hospitalini…’nikasema

Nilipotoka nje, nikaona mlango wa geti ukifungwa kwa haraka, kuashiria kuwa kulikuwa na mtu ndani, sasa alikuwa akitoka, ..kwa haraka nikakimbilia pale getini na kufungua mlango kuangalia huyo mtu ni nani…..sikumkuta mtu yoyote.

‘Hawa watakuwa ni polisi au ni watu gani, au wezi nini…’nikasema niktamani niwashe simu nimpigia mlinzi wangu aje..lakini sikuona haja, kuna mlinzi wa jirani huwa akija usiku anaangalia sehemu zote, na mimi nachangia katika malipo, ndio maana sikuwa na haja na mlinzi wangu binafsi.

‘Nina uhakika nikienda hospitalini, nitaishia mikononi mwa polisi, na kama hawa watu wananitafuta kuna jambo… na jinsi wanavyonitafuia visa vya kunikamata, sasa naona wamenipata, lakini sikubali….’ Nikafunga mlango na geti, nikatoka nje …hutaamini nilikuwa na gari langu, nililiuza, …

Nikatembea kuelekea kituoni….,lakini kabla sijafika mbali nikahisi kuna mtu ananifuata kwa nyuma!

                                          ************

 Nilichukua bajaji , lakini kabla sijaingia kwenye bajaji , jamaa wawili wakaja wakanishika, wakajitambulisha kuwa wao ni watu wa usalama, wakasema ninahitajika kituo cha polisi kwa kuhojiwa. Sikufanya ubishi, nikaongozana nao hadi kituoni.

‘Umeshitakiwa kwa kupiga na kujeruhi…’akasema askari

‘Nimempiga nani…?’ nikauliza

‘Dakitari…’akasema

‘Amesema ni kwanini nimempiga..?’ nikauliza.

‘Hajui sababu…, yeye anasema alikuja kwako kumtibia mke wako , ukaanza kumpiga,…’akasema polisi.

‘Sio kweli…’nikasema , nikadanganya, nikawa nimevunja miiko ya toba, kwani niliambiwa kipindi chote hiki niwe ninasema ukweli…nisidanganye,  lakini kwa hali ilivyokuwa sikukubali kwenda jela.

‘Sio kweli kwa vipi una maana docta anaweza kuja kukusingizia  uwongo, unafahamu ni docta gani tunayemzungumzia..’akasema.

‘Yawezekana…kutokana na jinsi tunavyoishi, mimi nimekuwa na maadui wengi, kila mmoja anataka kuniharibia maisha yangu,…na huyo ni mmojawapo, huenda kapigwa na watu wengine akahisi ni mimi nimewatuma…’nikasema.

‘Hata hivyo docta alikuja baadaye akasema kaifuta kesi, ila kutokana na uchunguzi wetu kunaonekana kuna tatizo, wewe mtu una matatizo, …tuambie ukweli, ni nini kinachoendelea, maana tulifika kwako hali tuliyoikuta yaonyesha wazi, hakuna usalama, ..’akasema polisi.

‘Kuna jingine lolote au niondoke..’nikasema, na Yule askari aliponiona sitanii, akasema;

‘Sawa unaweza kwenda, lakini bado tunakuchunguza kama kuna jambo linaloondelea na hutaki kutoa ushirikiano , ujue utakuwa hatiani…tumekuwa tukikufuatilia, na mara kwa mara umekuwa ukiponyoka kwenye mikono yetu,lakini nakuhakikisha ipo siku….’akasema huyo askari.

 Mimi sikumjibu nikaondoka zangu hadi hospitalini.

                                                                             *************
 Nilipofika hospitalini, sikuruhisiwa kumuona mgonjwa, niliambiwa docta amesema mgonjwa asisumbuliwe, na yoyote Yule.

‘Lakini mimi ni mume wake…’nikasema.

‘Tunafuata amri ya docta…’akasema nesi.

Nilikaa pale kwa muda, na mara docta akafika, ..Nilimuangalia huyo docta akishuka kwenye gari lake, alikuwa na plaster puani, nikakumbuka ile ngumi niliyompiga…nikahisi vibaya, kiukweli nilifanya vibaya lakini hasira, hata ingelikuwa ni wewe, unaambiwa huyu ndiye mwizi wako..

Docta, akawa anakuja usawa na pale nilipokaa, aliponiona wala,hakuonyesha dalili za kunikasirikia, akanisalimia ,…na akanitafadhalisha kuwa nimpe muda kidogo aingie ofisini kwake baadaye ataniita, ..na kweli haikupita muda, baadaye alinikaribisha kwenye ofisi yake,

‘Mkeo bado hayupo vyema..na kwa hali aliyo nayo, tunashindwa kuendelea na matibabu mengine..ila tangia jana alikuwa akitaka muonane naye…’akasema.

‘Kwani ana tatizo gani?’ nikamuuliza.

‘Mhh…siwezi kukuambia lolote kwasasa maana bado yupo kwenye uchunguzi, lakini mengie alisema,…atakuja kukuambia yeye mwenyewe…’akasema.

‘Sijakuelewa…kwanini wewe kama docta usiniambie tatizo lake ni nini….?’ Nikamuuliza.

‘Mimi natii agizo la mteja wangu ambaye ni mgonjwa wangu..hata kama ni mkeo siruhusiwi kumwambia lolote mpaka yeye mwenyewe atoe hicho kibali, ilimradi ana fahamu na akili zake timamu…’akasema.

 Nikasimama kutaka kutoka,..na yeye akasema;

‘Kuna jambo nilitaka kuongea na wewe, lakini naona ukaongee kwanza na mke wako ila nikuambie ukweli,…mimi sipendi ugomvi mimi na wewe,…yaliyotokea sawa, labda ulifanya ukijua ….au ukitaka kulipiza kisasi,..lakini nikuambie unafanya makosa sana…’akasema.

‘Umesema hutaki kuongea na mimi mpaka niongee na mke wangu, ..unataka tuongee kwanza….?’ Nikamuuliza.

‘Aaah,.. hilo ni juu yangu mimi na wewe..ulichonifanyia jana kimeniuma sana, kuwa wewe umekimbilia hasira,..unafikiri mimi siwezi kupambana na wewe...unataka mimi na wewe tuonyesha ubabe si ndivyo unavyotaka, lakini kwanini umesahau, … nilitaka kukushitakia lakini baadaye nikaona haina maana, maana huenda sio kosa lako…’akasema.

‘Ni kosa la nani….?’ Nikauliza.

‘Ufahamu!…ufahamu wako ni mdogo sana….’akasema na mimi nikawa napambana na hasira, niliona kanizarau,..lakini nikaona nikiendelea kujibishana na yeye nitaharibu kila kitu, kwanza nipo ofisini kwake, pili keshanishitakia….basi nikasema;

‘Naweza kwenda kumuona mke wangu tafadhali..’ nikasema

‘Sawa unaweza kwenda kumuona, ila wewe na mimi hatujamalizana...mimi na wewe tutapambana kiume..wewe si unajiona mbabe sio....tutaona...kwa mahali pake, sio hapa, nakuapia umeingia choo cha kike, hayo unayoyataka hutayapata na nitahakikisha unakuja kunipigia magoti.....'akasema na mimi nikatikisa kichwa dharau.

'Usijali....'nikasema

' Na kama angalizo, uwe makini sana na kauli zako mbele ya mkeo.., hakikisha huongei jambo la kumkwanza..ndio maana sikuhitajia mtu yoyote kuonana na yeye, lakini kwa vile anahitajia kuonana na wewe, sikuona kwanini nikuzuie, bado yupo kwenye uchunguzi, ….’akasema

‘Sawa , usiwe na wasiwasi na mimi, huyo ni mke wangu..’nikasema na kuondoka kuelekea huko kwenye chumba alicholazwa mgonjwa, nikiwa na mafundo mengi kichwani…niktamani nirudi nipambane na huyu mtu, katika maisha yangu sipendi kutishiwa, ni bora tupambene nijue moja...moyoni nikaahidi kupambana na huyu mtu ...

Nilifungua mlango alipolazwa mke wangu….chumba kilikuwa cha baridi, na mlio uliokuwa ukisikika ni wa kipozoe cha hali ya hewa, na mbele yangu kulikuwa na kitanda,..lakini kimezungushiwa pazia,..moyo ukanilipuka…


NB: Ni nini kitaendelea, jamani tuombeane heri, maana mitihani ni mingi, ndio maana nachelewa sana kukiendeleza hiki kisa

WAZO LA LEO: Katika maisha ya ndoa kunaweza kutokea mitihani kwa wanandoa, kiasi kwamba kila mmoja akawa na chuki na mwenzake. Yaweza ikawa ni sababu za kiuchumi, au ikawa ni sababu yoyote ile, tahadhari, kwa vyovyote iwavyo, sio vyema mmojawapo kwenda kumtangaza mwenzake nje ubaya.


 Kufanya hivyo ni kukiuka miiko ya ndoa, muhimu nyote wawili, kaeni ongeeni, ikishindikana watafuteni wakubwa, wazazi wenu, au washauri wa kidini. Msiwape watu faida kwani wengine watautumia mwanya huo kuwaharibia kabisa.

\Ni mimi: emu-three

No comments :