Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, August 9, 2016

TOBA YA KWELI-10Rafiki yangu hutaamini , nilipoteza fahamu siku tatu,

‘Siku tatu, kwa vipi…?’ nikamuuliza msimuliaji wa hiki kisa

‘Yaani … siku nipo , madocta wanahangaika huku na kule, hadi ikafikia watu wakajua sasa nimeshakufa...na wakiwa wameshakata tamaa ndio nikazindukana. Na nilipozindukana kwa muda huo sikujua nipo wapi, mara nikasikia sauti…

‘Docta. Docta…njoo  mgonjwa kazindukana…’ hapo nikajua kumbe nipo hospitalini, lakini kwanini…akili ilikuwa haiweze kutambua, .

Nilijua huyo aliyeita ni mwanamke, kutokana na hiyo sauti, lakini sikujua ni ya nani…, kuna wazo liliniambia huenda ni sauti ya mke wangu, nikawa sijielewi elewi,…sijui nielezeje hapo,…

‘Basi muacheni atulie msimwambie au kumuuliza kitu chochote…’nikasikia sauti ikisema hivyo,…hapo nilikuwa nasikia wanavyoongea, lakini ile akili ya kutafakari, ilikwua haipo, nilikuwa kama buwa, akili haielewi kitu!

Nilikaa hivyo hivyo kwa siku nzima, nageuza macho tu…na ilionekana kama nimepatwa na tatizo jingine, mwili hauosegei zaidi ya kutembeza macho, akili haifanyi kazi zaidi ya kusikia wanavyoongea na kuwasa hapo kwa hapo, baadaye nasahau,..nikawa kama mtu aliyepooza viungo….

Docta akawa anakuja na kunipima pima, anajaribu kkuninyosha viuongo, lakini sikumuelewa ni kwanini…akiinua mkono kuuwek hewani, akiachia unadondoka kama sio wangu….

‘Kwa hali hii anahitajika mtu wa kukaa naye karibu…’akasema docta na jamaa zangu wakawa wanashauriana, ilionekana kila mtu alikuwa na shughuli muhimu kwake, na akabakia binti mmoja , kwa muda huo sikumtambua, yeye akasema;

‘Mimi nipo tayari kukaa naye…’akasema

‘Lakini huyu ni mwanamke atamsaidiaje..’wakaulizana

‘Sawa hamna shida atasaidiana na manesi , ni muhimu tu kwa mtu wake wa karibu kuwepo, kazi nyingine wapo watu wa kuzifanya..’akasema docta

Basi siku , wiki ,hadi miezi ikapita mimi sijijui, hata ukiniuliza jina langu nilikuwa siijui ninaitwa nani, na hata wakati mwingine wakiniita kwa jina , nilikuwa siitiki maana sikujua kuwa wananiita mimi… hapo sasa ikaonekana nina tatizo jingine…

Baadaye nikaanza kuinuka,..hata kutembea kidogo kidogo…lakini akili bado ilikuwa haijafunguka…

‘Hili ni tatizo lakini litaisha taratibu…’akasema docta

Docta akashauri nirudishwe nyumbani lakini mara kwa mara kuwepo na mtu karibu wa kunichunga, na Yule yule binti ambaye aliyejitolea kule hospitalini akawa tayari kunisaidia sijui kwanini….

Nilikuja kujua baadaye kuwa huyu alikuwa binti kwa upande wa mke wangu, ambaye kipindi hicho cha nyuma alikuwa akifika hapo nyumbani kumsaidia mke wangu. Alikuwa akimpenda sana mke wangu!

********
 Siku moja nikiwa nimepumzika ndani, nikiwa peke yangu, nikaanza kufungua fungua makabati, napekua pekua kwenye droo za kabati, sijui natafuta nini,  mara nikaona shajara(diary), nikavutika kuisoma,….akilini nilikuwa najisomea tu,…

Sasa kitu cha ajabu kila nikisoma kilichoandikwa humo ilikuwa kama mtu anayenikumbusha jambo fulani, akili inakuwa kama inajenga hoja ya kujiuliza na kujiuliza huko kunazua ,maswali mengi, nikiaona nimechoka naiacha naanza kutembea tembea huku na huku nikitafakari, baadaye nairudia tena.

‘Nikawa kila mara navutika kuitafuta sajara hiyo na kuanza kuisoma,..ninasema naitafuta , maana nikitoka pale ninakuwa nimesahau kabisa niliiweka wapi…ila kuna kitu kinanishitua kuwa niende pale kwenye kabati nitafute tafute halafu nakutana nayo tena naanza kuisoma, ikawa sasa ndio sehemu ninayopenda kukaa kwa muda mrefu..

Huyo binti akawa ananishangaa , maana ananiona mara nyingi nipo hapo kwenye kabati natafuta tafuta baadaye ananiona nimetulia, na nikiwa hivyo sikupenda aniulize jambo, basi ananicha mpaka mimi mwenyewe niwe nimechoka, nainuka hapo naanza kutembea tembea..

Siku moja, nikaisoma sana hiyo shajara ….huku ninawaza sana, mimi ni nani, ilitokeaje, nikawa nawaza kwa bidii sana…..ikafika muda hata kichwa kikaanza kuniuma sana, huku najilazimisha kujua, kujiuliza… kuna kitu kinanijia kunaipatia majibu, lakini hakikai, nikawa najilazimisha kujua….sasa yakawa yanakuja maumivu makali kichwani mpaka nikapoteza tena fahamu…

Huyu binti anayenisaidia akanikuta nimelala sakafuni, nimepoteza fahamu, niliambiwa aliwaita watu, wakajaribu kunihudumia lakini zikuzindukana, wakaamua kunipeleka hospitalini…nikalazwa tena…

Huku hospiatalini ilipita siku nzima sizundukani, wanasema kuna muda nakuwa kama nataka kuzindukana lakini inaishia kutikiswa-tikiswa, halafu natulia…, lakini sifungui macho, nipo tu..docta alisema ni dalili kuwa akili inaanza kufanya kazi ya kukumbuka mambo…ndivyo walivyoniambia hivyo baadaye…siku mbili , baadaye nikazindukana,sasa niipozindukana,  mambo yakawa tofauti.

‘Mke wangu yupo wapi…?’ ilikuwa kauli yangu ya kwanza  siku hiyo, na watu waliokuwepo humo ndani wakawa wanaangaliana…alikuwepo docta, na baadhi ya ndugu zangu na huyo binti aliyekuwa akinihudumia huko nyumbani.

‘Ni mimi hapa….’akasema mdada mmoja..Nikamuangalia kwa makini, nikajaribu kukumbuka nilimuona wapi,

‘Wewe ni nani…?’ nikamuuliza nikimuangalia kwa mashaka

‘Umenisahau mkeo….’akasema akionyesha aibu aibu

‘Mhh..mke wangu siwezi kumsahau, mke wangu yupo wapi..?’ nikauliza na watu wakabakia kimia

‘Si huyo hapo,….’sauti ikasema na nilimuangalia mzungumzaji alikuwa akimnyoshea huyo mdada kidole, nilimuangalia huyo mdada kwa makini, na kumbukumbu zikaanza kunijia, nikakumbuka kuwa ni mdada aliyekuwa akija nyumbani kipindi cha nyuma..lakini sikukumbuka kuwa muda wote ndiye aliyekuwa akinihudumia.…

 ‘Acha utani unafikiri mimi simfahamu huyu, …’nikasema

‘Huyo ni nani..umemsahau mkeo, hukumbuki kuwa ndiye mliyekuwa naye siku zote akikuhudumia…’nikaambiwa
‘Akinihudumia, mimi…hapana..kama nikuja labda amekuja leo...ila mimi ninamkumbuka kuwa yeye ni shemeji yangu! Mimi ninauliza dada yake huyu yupo wapi…?’ nikauliza sasa nikijitahidi kujiinua.

Na watu walibakia kimia, nikamgeukia huyo mdada na kumuuliza

‘Ulikuja lini, je uliweza kuingia kumuona dada yako huko alipolazwa…?’ nikamuuliza, na yeye sasa akainamisha kichwa chini kama aibu fulani, na mara nikasikia sauti ya mzee ikisema.

‘Docta unaonaje tumwambieni ukweli…?’sauti hiyo ilitokea nyuma ya kitanda sikuweza kumuona vyema aliyeuliza, ila nilijua kuwa ni sauti ya mzee .

‘Mnaweza….’sauti nyingine ikajibu, ilikuwa ni ya docta , yeye aikuwa pembeni mwa kitanda, sikutaka kugeuka kumuangalia, kwa wakati huo macho yangu yalikuwa kwa huyu mdada, ambaye nimeshamtambua sasa kuwa ni yule binti aliyekuwa akija kumsaidia mke wangu kazi za nyumbani.

‘Tajiri…, tunaomba uwe mvumilivu, kiukweli ni kuwa  mungu keshamchukua mja wake,…mke wako hayupo tena duniani na sasa ni inakaribia miezi mingapi..saba au nane hivi,…hatukuweza kukuambia mapema  kutokana na matatizo yako uliyokuwa nayo awali….’akasema

‘Nyie waongo, mwaka!...mnasema nini…, hohoho…acheni utani…., hahaha, leo sio sikukuu ya wajinga, mhh…mnasema nini, mbona mimi siwaelewi, hebu nisaidieni niinuke, ni- nataka kwenda kumuona mke wangu…’nikasema nikijaribu kujiinua kitandani lakini sikuwa na nguvu za kufanya hivyo.

‘Sikiliza Tajiri…hayo tunayoakuambia ndio ukweli wenyewe…! ‘sauti ikasema

‘Ukweli gani…wewe unayezungumza ni nani kwanza..wewe ni mwanga nini.., ni jana tu nilikuwa naongea na mke wangu, nyie mnaniambia nini, aah, hebu acheni utani,…’sasa nikajitutumua hadi nikaweza kukaa vyema kitandani.

‘Sikilizeni sasa niwaambie ukweli, mke wangu amepelekwa thieta.kufanyiwa upasuaji, hajarudi …mnajua hata mimi sikuwa naelewa tatizo ni nini…wamesema baada ya upasuaji wataniambia, sasa ….hata mimi, ninataka nijue tatizo lilikuwa ni nini, hebu muiteni dakitari mumuulize, yule jirani yangu, sio huyu…, huyu hajui..muulizeni yule dakitari jirani yangu anafahamu vyema…’nikasema

‘Mliongea na mke wako wapi, lini..?’ nikaulizwa nikamuangalia muulizaji kwa macho ya kushangaa

‘Wapi lini..jana,…niliongea naye Hospitalini,….mke wangu alikwenda huko, akalazwa kwa ajili ya upasuaji, nia ni kusafisha kizazi, …ninajua baada ya upasuaji huo atakuwa hana tatizo tena..tutapata watoto…nyie hamjui kwa vile hamukuambiwa hayo..mimi najua, ..yupo thieta…’nikasema

Watu wakabakia kuangaliana…

 Kwakwei ilichukua muda mimi kuikubai hiyo hali…dakitari alisema nizidi kupewa muda,…

Siku ya pili yake niliruhusiwa kurudi nyumbani, ilikuwa ni kazi, maana nilitaka kwanza nikamuone mke wangu..hata hivyo baadaye nikakubali, na kurejeshwa nyumbani…,

Ikawa sasa kila siku nadamka asubuhi nadai nataka kwenda hospitalini  kumuona mke wangu…hapo hakukaliki , inabidi waniruhusu, tunakwenda hadi hospitalini , nikifika nawauliza madakitari, kuhusu hali ya mke wangu,…

Ilifikia hatua watu wakaona kama nimechanganyikiwa…, lakini docta alisema akili yangu ipo sawa, ila hiyo hali bado haijakubaliana na ubongo wangu.

Na siku moja, jamaa wakanipeleka makaburini na kunionyesha kaburi la make wangu, hapo ndio kidogo akili ikaanza kukubali-kukubali…lakini haikuwa kazi rahisi..

Naikumbuka sana siku ile,..sijui kulitokea nini, na ndio nikaanza kukubali kuwa kweli mke wangu hayupo tena duniani…, ilikuwa siku niliyoumia sana,… siku hiyo ilikuwa ndio kama vile msiba umetokea kwangu, nililia sana ..mpaka nikawa sijiwezi…

Basi siku zikapita, …mwaka na kitu sasa…nikawa siongei na mtu…yule binti au mdada ndiye anafanay juhudi za kunisaidia,..wakati mwingine nakataa kula..anafanya juhudu mpaka nakula..nikaisha …mwii ukawa kama sio mimi…

                        *********

Siku moja….nipo ninaongea na mke wangu, na katika kuongea mke angu akanituma nikamchukulie kitabu kidogo kwenye kabati, alisema hivyo, na mimi nikasimama sasa kuelekea kwenye kabati…mara nikazindukana kumbe ilikuwa ni ndoto…
Nilipoamuka niliwaza sana hilo..kijitabu kidogo, kijitabu kidogo, ni katabu gani hicho,…basi nikaenda kwenye kabati, wakati napekua pekua, ndio nikakutana na shajara ya mke wangu.
Ukumbuke awali niliisoma hiyo shajara bila kujua ni nini ninachokisoma, na kwa muda ule sikukumbuka kabisa kama niliwahi kuisoma, …sasa kwa hivi naisoma nikiwa na akili zangu timamu, naelewa kila kitu,… ndipo hapo nikaanza kugundua ukweli halisi kumhusu mke wangu,….kumbe mke wangu alikuwa akiandika kia kitu , katika maisha yake….

Hapo nikamjua mke wangu vyema, nikamjua kwa yale ambayo sikuwa nayafahamu….
‘Mungu amlaze mahali pema peponi….’ Akasema na sote tukasema kwa pamoja
`Aaamini…’
                             ************

Mke wangu awali kabisa aliandika wasifa wangu, jinsi gani anavyonipenda,..na aliapa kuwa hataweza kuishi na mtu mwingine zaidi yangu….aliandika maneno mengi ya kunisfikia, ila kitu alichokiona ni tofauti, na anakiombea kiniondoke ni hasira..na kupenda sana mali…

Nikawa naisoma hiyo shajara kwa hisia ….aliandika jinsi gani anavyotamani kuwa na mtoto, lakini hampati, akaeleze jinsi gani tulivyohangaika mimi na yeye, ikafikia sehemu akaona mimi nimekata tamaa,akawa anahangaika kivyeka…ndugu zangu upande wa kiumeni wakawa wanamsakama sana ….

Ikafikia sehemu ya ugonjwa,…..aliandika kuwa alianza kuhisi maumivu hasa ikifikia siku zake..ilikuwa ni mateso sana kwake..hali hiyo iliendelea kumtesa sana….

Kumbe Mke wangu alianza kuumwa tumbo, muda,…nikakumbuka awali  kuwa ni kweli mke wangu alikuwa akilalamika kuwa tumbo linamsumbau, na kuna kipindi tulikwenda mimi na yeye hospitali, na akatibiwa, na baadae sikusikia tena hilo tatizo, kuna muda analalamika, mimi nikawa simtilii maanani…najuata sana nikiliwazia hilo…

Kumbe mke wangu baadaye akawa anahangaika peke yake, na huko akagundua kuwa ana tatizo kwenye kizazi, lakini kwa jinsi nilivyokuwa bize na maisha ya kutafuta mali, hakuweza kuniambia zaidi…na kumbe tatizo hio ilifikia mahali akaambiwa hatakiwi kushika mimba…akishika mimba itakuwa ni hatari kwake, hakuweza kuniambia hilo…aliongea na docta , na akamwambia docta asije kuniambia kitu!

Katika kupimwa pimwa walikuja kugundua kuwa alikuwa na uvimbe kwenye kizazi, akatumia dawa za kienyeji, na ule uvimbe ukaondoka, lakini kumbe kulibakia tatizo humo humo kwenye kizazi…shimo au kidonda…,na tatizo hilo lilikuja kuharibu  kizazi kabisa, na mke wangu aliposikia hivyo, alijitahidi sana kutafuta njia za kuniambia lakini alishindwa...

Mimi nilikuwa nataka mtoto, sasa akiniambia hatanipatia mtoto itakuwaje, ina maana nitamfukuza, au nitatafuta mke mwingie…alisema kutafuta mwingine sio hoja, lakini anajau kabisa nitakuwa simpendi tena…basi akawa anamuomba mungu huku akivuta subira kuwa ipo siku mungu atajali,atapona, au ipo siku ataweza kuniambia ukweli…

Mtu aliyemtaja kama dakitari, alikuwa ndiye msaada wake mkubwa, na mshauri wake mkubwa, alisema kama asingeikuwa yeye, huenda  angelikuwa keshakata tamaa ya maisha kabisa…alimtaja kama mtu ambaye ana deni kubwa kwake kwa fadhila….docta..docta…akawa anamtaja sana…

Siku baada ya siku ndio ikagundulikana kuwa kumbe  kile kidonda kimekuwa kikubwa kimekula na mirija ya uzazu..kimekuwa kidonda , na hakitaki kupona,…na ndipo akaanza utaratibu wa tiba na aliyekuwa akimsaidia ni huyo docta.

‘Docta..docta..docta….’ alimtaja sana kwenye shajara hiyo mpaka nikaanza kujisikia vibaya, wivu….alionekana kama yeye ni mtu muhimu sana, hata kuliko mimi, ..mimi nikawa simjali anayemjali ni huyo docta…

‘Nampenda sana mume wangu, lakini yaonekana anapenda mali zaidi kuliko mimi, na inafikia muda najaribu kuongea naye hanielewi, tofauti na ilivyo kwa docta, ..alinijali sana…’kauli hii iliniuliza sana, na zile hasira dhidi ya docta zikaanza kunijia tena akilini.

Mke wangu hakutaka kabisa niambiwe, akijua kuwa nikiambiwa nitaumia sana, na kwa mawazo yake ningemuacha kwa hasira, kwasababu ananifahamu nilivyo, na kama ningemuacha, asingeliweza kuishi bila mimi..na akawa anaumia sana pale nilipoanza harakati za kutafuta mtoto. ….

 Kumbe …aligundua kuwa ninatembea na wanawake wengine ili nipate mtoto , lakini hakutaka kuniambia, aliombea tu, nijaliwe nipate huyo mtoto, lakini haikutokea…na kwa jinsi alivyohangaika, alijua ni yeye peke yake anayeweza kulifanikisha hilo..lakini kwa vipi….

Sikutaka hata kumalizia hiyo sehemu, nikairudisha ile sajara kwenye kabati, haraka nikiwa nimeshaanza kupaniki, nikatoke nje, moja kwa moja nikaeleeka nyumbani kwa docta, ..docta alikuwa jirani yangu….

NB: Naishia hapa kwa leo, nina imani sehemi ijayo itakuwa ni hitimisho…

WAZO LA LEO: Kuvumiliana ni kitu muhimu sana kwenye mahusiano, kwani akili za kutafakari mambo hutofautiana mtu na mtu, haiwezekani kile unachofikiria wewe au kukitaka wewe kikawa sawa na mwenzako. Pia tukumbuke kuwa, uwezo wa kujieleza, hutofautiana mtu na mtu, kwasababu mbali mbali, mmoja anaweza kushindwa kuelezea jambo, labda kutokana na malezi ya huko alipotoka, au labda kutokana na sababu mbalimali...


 Sasa basi mnapokutana wawili, mnatakiwa hili mliangalie kwa makini,kwa mfano  tatizo likitokea, mjaribu kukaa, kuulizana na kila mmoja apate nafasi ya kuelezea aonavyo, na kama kuna ugumu wa kujieleza, au hata kutekeleza, basi kuwa na namna ya kuvumilia, kuchunguzana tatizo lipo wapi…huenda kuna sababu ..na sio vyema kukimbilia kwenye jaziba, mkaanza kugombana na wengine hata kuingia kwenye uadui, na wengine hukimbilia kuachana huku moyoni wanapendana, au wengine wanateseka ndani kwa ndani, lakini wanashindwa kusema,kama ilivyotokea kwenye kisa chetu…
Ni mimi: emu-three

3 comments :

Anonymous said...

Safi sana mkuu

Anonymous said...

Lini tena, like a movie

Anonymous said...

Mtu wangu, hongera sana