Mzee aliondoka nikabakia peke yangu…nakajua sasa mimi ni
mpweke, sina wa kumtegemea tena, na sina majaliwa mengine ya hapo kijijini.. na
kabla sijatanabahi ndio mlango ukafunguliwa…..!
Lakini kabla ya tendo hilo la kufunguliwa mlango, ulipita
muda mchache kama dakika kadhaa…na muda huo ulinifanya niwaze sana,
nilie..nisononeke…..
************
Akili ya mwana-adamu ni ya ajabu sana…mzee alipoondoka tu
hapo hapo akili ikaanza kufanya kazi, ni kipindi cha muda mfupi tu, lakini
niliweza kuwaza mambo mengi na niliwaza
hayo hata kabla mlango haujafunguliwa…!
Jambo la kwanza lilinijia akilini ni kuwa natakiwa niondoke
hapo nyumbani haraka kabla sijakutana na
mama mwenye nyumba,…..yeye alikuwa hanitaki….najua hilo akilini,….chuki na
hasira alizokuwa nazo mama huyo angeliweza hata kunifanya chochote, nilishindwa
kuelewa ni kwanini alipotukuta pale kitandani na nikiwa na mumewe hakufanya
fujo, ilivyo kwa wengi wangelileta fujo, yeye hakufanya hilo kabisa ni kama vile alijua
nini anachikifanya.
Hakutaharuki, zaidi ya kusema maneno aliyosema na kutupiga
picha… ni kama vile ulikuwa mpango wa kuninasa…na hii ilinipa mawazo mengine
akilini kuwa huenda hili lilipangwa…..ina maana walifanya mpango huo na mumewe,
hapana…sizani!.
Wazo la kuwa huenda mumewe alifanya hivyo ili upatikane
ushahidi halikuniingia akilini, …kwasababu mume huyo alikuwa mkarimu, mwenye
huruma sana kwangu, sasa iweje wapange
na mkewe kuwa kupatikane ushahidi nifukuzwe….
Kwa jinsi ilivyotokea pale…mume mtu ndiye alianza uchokozi
na mimi sikuwa na mpango huo, nilimuheshimua sana huyo mbaba…na kama
angelichelewa kuja huyo mke mtu, mumewe,alikuwa
akielekea kubaya,….alishashindwa kuvumilia, lakini mimi sikuwa tayari kwa hilo…
‘Sasa mimi nilikuwa na kosa gani hapo….kwanini wanione mimi
ndiye mbaya,…lakini hapo hapo nikazidi kujiuliza ni kwanini mkewe asilete
vurugu..hili lilinisumbua sana kichwa kuliwazia,hata hivyo sikuwa na uwezo wa
kulipatia jibu, sikuwa na muhimu ni
kuondoka hapo nyumbani haraka…
Kitu kingine nilichojiuliza kwa haraka, ni kuhusu kuonekana
kuwa mimi ndiye mkosaji, ni kwanini wao walikimbilia kuniona mimi ndiye
mkosaji, ni kwanini wasimshutumu mume mtu… labda ni kutokana na historia iliyopandikizwa
kwangu kuwa mimi ni mbaya huko kwetu,…. sina cha kujitetea sina wa kunitetea,
mtetezi wangu alikuwa huyo mzee, sasa
naye kajitoa, sasa kweli nakamilika…. mimi sasa nimekuwa…sikio la kufa….
‘Sasa nitakwenda wapi!....hata kama nikiamua kuondoka…?’
nikajiuliza
‘Hata kama sina pa kwenda ni lazima niondoke kwenye hii
nyumba kabla mambo hayajaharibika…’nikasema
Hakukuwa na jingine bali ni kuanza kupanga vitu vyangu ili niondoke kwa haraka na ikiwezekana wakiingia
humo wakute nimeshaondoka…tatizo ni muda, tatizo nilikuwa sijui waliongea nini
huko,..na nini kitafuata….ila hisi ziliniambia kuwa…kwa muda wowote watafika na
kunitimua sizani kama baba mwenyenyumba anaweza kumshawishi mkewe…..
Nilijua kwa hivi sasa alikuwa na wakati mgumu wa kuitetea
ndoa yake,….na hata kama ingelikuwa mimi , ningetetea ndoa yangu kwanza, sasa
sijui walikubaliana nini, na huenda baba mwenye nyumba keshanigeuka, huenda kapindisha maneno, au walipanga ili
niondoke hapo nyumbani….sijui, labda…niliwaza hilo nikijaribu kuhisi jinsi
mbaba huyo atakavyojitetea ili kuikoa ndoa yake,..nasema huenda japokuwa huyo
mbaba hakuonekana kuwa na tabia hiyo.
Nilikumbuka kuwa mke mtu alimwambia mumewe aende akampe
talaka yake, …nilijua kabisa kauli hiyo ni ya kutingsha kibiriti…..,lakini kwa
vyovyote itakavyokuwa, mume hawezi kufanya hivyo, asingelikubali kuitoa hiyo
talaka ..na ndivyo ilivyokuwa ndio maana huyo mzee aliitwa haraka,
Nilijiuliza ni kwanini huyo mzee aliitwa, badala ya wawili
hao labda kuwaita wazazi wao, ili wasuluhishwe, kwanini aitwe huyo mzee kwanza, kuna sababu ya msingi….kama mpango
wao tu, basi walitaka kuutumia ushahidi huo ili mimi niondoke…lakini kwanini….!
Kwa tabia ya huyo mbaba, nimjuavyo mimi….yeye sio muongeaji,
pili hapendi majungu kukaa na kuanza kuteta mtu, na siku zote ikitokea tupo
wawili, haongei sana labda kwa swala la wajibu….na alijitahidi sana kujiweka
mbali kama hakuna ulazima, isipokuwa siku nikiwa naumwa…na hata mkewe
alipofikia kumshuku hivyo, niliona ajabu sana…
Sasa ni sababu gani ya kuweza kufanya mipango ya pamoja ili upatikane ushahidi ili nifukuzwe humo ndani…, sizani, hiyo
itakuwa mbinu ya mama mwenye nyumba, …sikutakiwa kuliwaizia hilo nilichotakiwa
kukifanya ni kuondoka, maana sitakiwi tena kuwepo hapo...
Najua mzee aliitwa, kama kweli sio mpango, mume alimuita
huyo mzee, au mke ndiye aliyemuita huyo mzee ili kuwe na suluhu, na ili suluhi
ipatikane ni mimi niondoke…kwani tatizo ni mimi, na sio mume aliyenitaka …..na waliamua
kumuita huyo mzee kwani ndiye
aliyenidhamini,au kama ni mkewe alimuita huyo mzee, nia yake ilikuwa kuonyesha huo ushahidi alioutaka huyo mzee.
Mzee alipofika, mama mwenye nyumba hakuwa na la zaidi
….sijui labda mama mwenye nyumba alisimamia kwenye msimamo wake kuwa anataka
talaka yake na mumewe akaanza kujitetea, na mama mwenye nyumba akaamua kuutoa huo
ushahidi….
Nakumbuka mzee alipoingia tu, alionekana kukasirika,
hakuonyesha ule uso wa upendo tena, ina maana alishakabidhiwa mtu wake, na mzee
hakuwa na jinsi ….kwa jinsi alivyoonekana ni wazi kuwa huenda alishaafiki uamuzi kuwa mimi niondoke hapo japokuwa mzee
hakunitamkia hayo,hakusema ni nini walikubaliana huko…hakutaka hata kusikia
hiyo siri niliyokuwa nimekusudia kumwambia…yeye alisimamia katika kuiokoa ndoa
ya watu. Mawazo haya yalikuja kwa haraka sana kabla mlango haujafunguliwa
'Hivi kwanini mzee hakutaka kunisikiliza nalo lilinikwanza sana, utafikiri huyo mzee ni baba
yangu, nilijiuliza sana kwanini mzee hakutaka kunisikiliza kama ilivyokuwa
kawaida yake, hakutaka kunielewa, hata
kama kuna maamuzi hayo…ya kuwa mimi niondoke,…kwanini hata hakutaka kusikiliza
hiyo siri….
‘Kwanini ..kwanini…mzee hukunisikiliza….’
‘Kwanini mzee…mimi nilitaka unielewe,…’ nilisema kwa
sauti,..sikupenda mzee wa watu ajisikia vibaya kwa maamuzi yake ya kunitetea,
sikutaka mzee aungane na wengine ili nionekane mimi ni mbaya kama walivyokuwa
wakiniona wengine..kama ni kuondoka iwe ni kwa nia njema tu, ya kuikoa ndoa ya
watu ,mzee huyu umenisaidia sana, kwa ujumla ananidai….,kwa fadhila zake… hata
kama nikiondoka lakini ingelikuwa ni vyema angenielewa, tu…
‘Sasa kwanini mzee
umeondoka….hata bila kukushukuru…’ nikajikuta naongea mwenyewe tu….ni kiukweli,
sikutaka tena…kuwepo hapo, sijui…maana ningeenda wapi,….na kama nikiondoka
kwenye hiki kijiji, sizani kama nitaweza kurudi tena…ni vipi nitakutana na
nyuso za watu wa kijiji hiki…., nilijiona mchafu, nilijiona sifai kwenye jamii,
lakini nikajiuliza kwa kosa gani, kwani mimi nilifanya nini kikubwa ambacho wengine
hawajakifanya
Labda mimi sikustahiki kuwemo humu duniani, na hapo wazo la
kujiondoka hapa dunia, hata kufa likaanza kunijia akilini…nilitamani kabisa
nitoweke hapa duniani, nisionane na nyuso za watu….
‘Bora nife tu….’nikasema na hapo hapo nikasema kwa sauti
‘Ina maana hata mzee, na yeye kayaamini hayo…..’nikasema
huku sasa nikiwa naanza hatua za kwenda kuanza kupanga vitu vyangu niondoke…..
‘Hata mzee jamani….ni yeye peke yake aliyewahi kunielewa…’
nikasema tena huku kichwa kikianza kuniuma, niliwaza sana…na wazo la mzee
likaaka sana kichwani, nikimuoena huruma jinsi nilivyomsumbua ….. mzee wa watu,
Nitamlipa nini mzee wa watu….hata shukurani sijawahi kumpa….,
na sasa keshaondoka, na sitaweza kumshukuru .., mzee ambaye alionekana mwenye
hekima, huruma na upendo, alinifanya mimi kama binti yake na alinisikiliza yale
niliyomuambia awali,…
‘Sasa kwanini mzee hukuvuta subira kidogo, nikakufichulia
siri…siri ambayo…ooh,..’nilijikuna kichwa nikitafuta wapi pa kupenya , wapi
…dunia ipasuke nimezwe…..
Niliona nisiendelee kulia, kujitesa na mawazo… kwani nilijua
mzee ana sababu kubwa ya kuyafanya hayo yote, na kwa haraka nikajua sababu hizo….nilichanganua
sababu hizo kichwani kwa haraka, ujue hayo ni mawazo yaliyonijia kichwani kwa
muda mfupi,hata kabla mlango
haujafunguliwa…na kipindi hicho sikuwa nimejuwa kuwa kuna mtu angelikuja, na mimi sikupenda mtu
aje, nilihitajia muda wa kujiandaa na kuondoka, na kutokomea kusikojulikana…
Niliyachanganua sababu za mzee kuamua hivyo
alivyoamua,..haya niliyachanganua kichwani, ili kujirizisha kuwa mzee wa watu
hana hatia, hajaamua tu….nikawaza kichwani kwa haraka…
Kwanza, ukumbuke mzee alishapata ushahidi kutoka kwa mama
mwenye nyumba,…sijui walichoongea wakati mzee alipofika kusuluhisha hilo tatizo
ili kuiokoa hiyo ndoa,…na sikujua mzee
huyo aliitwa saa ngapi, nahisi alipigiwa simu.
Ila ninachojua ni
kuwa mama mwenye nyumba huyo kabla….hilo nililijua kabla kuwa mama huyo aliwahi
kwenda kwa huyu mzee kumlalamikia kuwa mimi sio mtu mwema, na mzee hakulichukulia
haraka, ila nakumbuka niliambiwa kuwa mzee alimuahidi huyu mama kuwa kama
utaupata ushahidi unaonyesha kuwa mume wake ana mahusiano na mimi, na akamuonyesha
mzee huo ushahidi, basi mzee hatakuwa na msamaha na mimi, yeye
mwenyewe atanichukuliwa hatua kali, na hatua hiyo ni mimi kufukuzwa hapo
nyumbani…
‘Ushahidi…mmh, najua tu, picha…!’ nikasema kwa sauti.
Nilijua kwa vyovote huyo mama atakuwa
alimuonyesha huyo mzee huo ushahidi wa picha.
Pili kutokana na taarifa alizozipata huyo mzee kutoka huko
kijijini kwetu alipokwenda kutafuta ukweli, huko alikutana na hao wanaume wanne
na pia wazazi wangu,na watu wengine mbali mbali, na wote walisadikisha kuwa
mimi nilikuwa na tabia mbaya, nilishindikana, sikuwasikiliza wazazi wangu….
lakini kubwa zaidi ni kuhusu kuwa eti…
‘Eti mimi nitakuwa nimeambukizwa ugonjwa wa ukimwi na nimeambukizwa
na mmoja wa hao wanaume, kwani nilitembea naye na wengi wanaamini hata hiyo
mimba ni huyo mwanaume sijui kwanini wanaamini hivyo…’nikasema kwa sauti ndogo
Nilisikia kuwa huyo jamaa alikuja kujitangaza baadaye wakati
mimi nimeshaondoka huko kijijini kuwa kaathirika,…mimi niliposikia uvumi huo
kwa mara ya kwanza sikuamini…lakini sasa imekuwa hivyo, lisisemwalo lipo…wanakijiji
wameambiwa,…na hata kuthibitisha.
Kwahiyo mzee alichokuwa akihitajia kutoka kwangu ni kauli yangu
tu, kuwa kweli nimetembea na hao wanaume
wanne..,na mmojawapo ni huyo jamaa….. na zaidi ya hayo yeye alishawaahidi
wanakijiji kuwa kama nimeathirika kweli, na kama nilitembea na hao wanaume
wanne …na ikagundulikana kuwa lengo langu ni kuusambaza huo ugonjwa, hatua kali
dhidi yangu zitachukuliwa…na hatua hizi ni mimi kufukuzwa hapo kijijini, kauli
hiyo aliitoa kwa raia-wanakijiji, waliofika kumlalamikia.
‘Mimi nawaahidi kuwa itagundulikana kuwa ni kweli…huyo binti
katembea na hao wanaume wanne, mimi sitakuwa na msamaha kwake,…na ikizingatiwa
kuwa mmojawapo kaathirika, …basi nitasimamia upande wenu, …hilo
nawaahidi,..’akasema mzee
‘Mzee chonde chonde…’wakazidi kusisitiza
‘Kwani pamoja na hayo, huyu binti ana tofautii gani na
mabinti zetu hapa kijijini, au ni kwa vile ….?’ Akauliza mzee
‘Mzee huyu binti ni mrembo, ana mvuto, na ni kishawishi
kikubwa hapa kwetu, anaweza kuutumia urembo wake huo kuwashawishi vijana wetu,
au waume zetu, huoni hilo ni hatari kabisa, mzee, tumia hekima zako umuondoe
huyu binti….’aliambiwa
‘Sasa niwaambie kitu…kama ni mkosaji, kama mnahisi ana tabia
hiyo, ya kuweza hata kuwarubuni waume zenu, na sijui kwanini waume zenu warubuniwena
huyo binti kwa hali kama hiyo…hawana huruma….sawa, sasa nipeni ushaidi wa
kulithibitisha hilo...’aliwaambia
‘Sisi tulifika hadi huko kijijini kwao, kuna taarifa
zimeenea kuwa huyo mwanamke ni mhuni kupundikia, tunaweza kumuita malaya,…katembea
na wanaume zaidi ya mmoja, …yaani mzee, huyo ni kicheche…ana tabia mbaya na la
kuogopewa tumesikia kuwa mmoja wa mwanaume aliyetembea naye keshagundulikana
kuwa kaathirika, …kama huamini nenda mwenyehuko kijijini ukalithibitishe hilo….kuna ushahidi wa
kutosha,..utauona mwenyewe….’akaambiwa
‘Hayo mumesikia…hayo ni ya kuambiwa, mimi naongea na huyo
binti mara kwa mara, niliwahi kumuulizia kuhusu hilo na alisema hayo ni maneno
ya huko kwao,…ni tabia za atu kuwavumishia watu uwongo,….ni kwa vile tu wanamchukia, yeye yupo mbali na
tabia hizo…sasa sijui, kwanini hakuwahi kuniambia ukweli huo…’akasema mzee
‘Uliwahi kumuuliza kuhusu hao wanaume wanne, kuwa aliwahi
kutembea nao…?’ akaulizwa
‘Kwanini niingie undani wa hayo, nitakuwa kama simuamini,
yeye kaniambia kuwa hana tabia hizo chafu,nikimuhoji sana kihivyo, ataniona
simuamini,….na kiukweli mimi nimemuamini..na kutokana na hali aliyo nayo,
sikutaka kumweka kwenye hali ya majonzi…jaribuni kujiweka kwenye hiyo hali
yake…’akasema mzee
‘Sisi mzee tunakuhakikishia hilo, na ushahidi utakuja
kuupata…lakini hata hivyo, ni lazima tukutane tulijadili hilo, maana naona wewe
mzee unalichukulia kirahisi tu…huwajui hawa vijana wetu wa siku hizi….waongo,
hawana ukweli…’akaambiwa
Kwa malalamiko hayo, wazee na wajumbe wa kijijji walikutana,
na mzee akawekwa kiti moto kuuliziwa,na
Mzee mbele ya baraza la kijiji , aliwathibitisia kuwa huyo binti hana makosa ,
mambo yote nasingiziwa tu;
‘Huyu binti ni mhanga wa udhalilishaji, akina mama, mabinti
zetu wanadhalilishwa,…wanabebeshwa mimba na wanaume waliofanya hivyo
wanawakana.. na wanakuwa hawana namna ya kujitetea, watakwenda wapi…niambieni,…
huyu binti nimemchunguza nimegundua kuwa ni mmoja wa wahanga hao, ndio maana mimi
nimeamua kumtetea, ili tuweze kuangalia jinsi ya kumsaidia, na ikibidi tuonane
na wazazi wake, na huyo aliyembebesha mimba awajibike…’akasema.
‘Lakini mzee…..’wakazidi kumlalamikia, hapo ni kabla
ushahidi haujapatikana, ushahidi wa watu na mzee kwenda huko kwetu, na ushahidi
wa mama mwenye nyumba….
‘Sasa ushahidi umepatikana, na mzee keshaniona mimi ni
muongo….. unatarajia nini hapo, mimi nina usalama hapa kweli, kwanza nitapitaje mitaani, nikikutana na watu
nitakuwa nikinyoshewa vidole , …..hapana ni lazima niondoke hapo haraka, lakini
niondoke niende wapi…’ nikazidi kuwaza
Vyovyote itakavyokuwa nitamshukuru sana huyu mzee, kwani
hata Wanakijiji wa hapo waliona ajabu sana kwa jinsi mzee huyo alivyoamua
kunitetea, kwa jinsi nilivyosikia mzee
huyu ni mmoja ya wazee wanaoheshimika hapo kijijini kwa msimamo mkali, msimamo
wa kupinga mambo machafu yanaoharibu vijana na wanajamii hapo kijijini,…yeye
akachaguliwa kuwa mzee mshauri na kiongozi wa kusimamia tabia njema za hapo
kijijini.
Lilipotokea hilo na mzee kuonekana tofauti na tabia yake,
wenzake wakajiuliza kulikoni na wabaya wake wakaona ndio sehemu ya kumuharibia,
wakaomba kikao kiitishwe kulizungumzia hilo jambo, na wao wakaonyesha msimamo
wao kuwa wanapinga huyo mdada kuendelea kukaa hapo kijijini.
Kwa shinikizo hilo
ndio maana mzee akawa hana budi, akaona ni heri kulifuatilia hilo tatizo kwa undani zaidi
licha ya kuwa ndoto yake ilikuwa imemuonyesha kuwa mimi sina hatia.
Yeye mzee hata hivyo aliwaambia wenzake, ….hasa wale ambao
muda mwingi walikuwa wakitafuta mwanya wa kumchafua …aliwaambia wazi wazi kuwa
yeye kama yeye hawezi kukubaliana na
hizo shutuma mpaka kuwe na ushahidi wa dhahiri,….akawapa changamoto wapinzani
wake hao kuwa walete huo ushahidi kulithibitisha hilo;
‘Kama mkileta huo ushahidi na kugundilikana kuwa huyo binti
ana kosa mimi sitasita kuwa pamoja nanyi, ilii huyo binti achukuliwe hatua
stahiki kutokana na taratibu zetu za hapa kijijini, na hatua ya juu, inayomfaa kuhakikisha
kuwa tumemfukuza huyo binti hapa kijijini…lakini kwa hali kama hii, ya maneno
tu, hatuwezi kufanya hivyo, tutakuwa tumekosea sana….’akasema
Baadhi ya wajumbe, waliamua kuutafuta huo ushahidi, ….
Haya wajumbe wakafanya kazi yao japokuwa sikuambiwa
zaidi..ila tetesi zilinifikia kuwa kwa uchunguzi uliofanywa uliashiria kuwa
mimi nina makosa…hakuna aliyekuwa na tafsiri nyingine,…walisema huko kwetu
ukinitaja mimi ni gumzo la binti aliyepotoka…na nimekimbia kwa kashfa…
Nilishindwa kujua kwanini, kwani mimi ni wa kwanza, wapo
wengi waliopata ujauzito hata bila kuolewa, wakakataliwa na waliosadikiwa
kuwapa mimba, na taratibu zilifanyika yakaisha, lakini kwanini mimi ikawa
tofauti…huko kijijini na sasa hapa.. hakuna aliyeangalia utu au ubinadamu, kila
mmoja aliyesikia hayo alikuja na msimamo mmoja kuwa mimi niondoke hapo
kijijini, sifai, nitaharibu jamii….nitawaambukiza vijana na waume wa watu ukimwi..
‘Eti mimi nina ukimwi,
sijawahi kupimwa,..kama kweli ninao, mimi sijui kama nina huo ugonjwa, lakini
watu wameshaanza kuninyanyapaa…oh…eti ni kuwa huyo mwanaume, kati ya hao wanne
kaniambukiza, lakini angalau wangetafuta ushahidi wa kitaalamu, nipimwe
basi…ili, nionekane ninao….’nikawaza hilo huku nikijawa na wasiwasi,
‘Huenda kweli ninao, mimi sijui, labda kwa vile naumwa umwa
hivi,…kiukweli kila mara naumwa hiki, mara kile, mara damu inanipungukia, lakini mbona hata
docta alisema ni kawaida tu, inatokea tu….,na
sijui…na hata hivyo...sijawahi kupimwa, kwa ajili ya ugonjwa tu….. maana mara
zote ninapokwenda kupimwa, sikumbuki kuchukuliwa kipimo hicho,…ila nakumbuka
wakati naongezewa damu….sijui , ila docta mmoja aliwahi kuniuliza kama niliwahi
kupima huo ugonjwa nikamwambia hapana…na hakusema zaidi
Inawezekana ninao…lakini kwa vipi..ooh, hata sijui…jamani
sijui…ilikuwaje,…hata mimi najiona kinyaa, kwa hicho cha kutembea na hao wanaume
wanne..ilikuwaje,….nawaambia kiukweli hata mimi sjui, ni siri…ni siri ambayo
nilishindwa kuing’amua, lakini ipo siku …ipo siku kama nikikutana na hao
wanaume wawili
Kwahiyo kwa hivi sasa msiniulize kwanini ilitokea hivyo……jamani
sijui ilikuwaje….lakini kama ni hivyo kama kweli ilitokea hivyo…., basi ninao,
na nashindwa kuelewa kwanini madocta hawakuniambia…au ndio wamevujisha kuwa
ninao…sasa kwanini hakuniambia mimi mwenyewe…nikaanza kuingiwa na mawazo
mengine, wasiwasi..mashaka ambayo sikuwa nayo, kuwa huenda kuwa kweli nina huo
ugonjwa.
Ndio maana wanakijiji waliofuatilia kuchunguza kuhusu hizo
kashafa dhidi yangu waliona kuwa kweli mimi ni mkosaji, na hakukuwa na dalili
za kuonyesha kuwa kuna kusingiziwa au unyanyasaji, taarifa zilikuwa kuwa mimi
nilikuwa mjeuri, sikuwasikia wazazi wangu nikawa natembeza uhuni mitaani, na
mambo ya aibu,hayo ndiyo yamezagaa kijijini kwetu,….kwahiyo huko nikionekana
itakuwa ni kuzomewa tu,….…na mzee wa watu aliposikia hilo akawa hana namna
tena, na yenye kama kiongozi muaminika,akatakiwa
kutoa kauli…
Yeye kabla hajachukua hatua yoyoye aliamua kujirizisha ndio
maana alifunga safari ya kwenda huko kwetu, na alikwenda huko baada ya mama
mwenye nyumba mfadhili wangu kuja kwake tena kumlalamikia kuwa mimi sasa
nayafanya hayo hadharani, nimekuwa mkaidia nimekuwa kama mke ndani ya nyumba, sifanyi
kazi, nasingizia kuumwa, natumia nafasi ya kuumwa kwangu ili nikutane na mume
wake…
‘Una uhakika na hayo unayoyasema ina maana humuamini mume
wako…’mzee akasema
‘Wanaume hawaaminiki..hasa wakipata uchochoro…huna mwanamke
ni rahisi sana akiwambiwa , na hata bila kutongozwa anajiuza..anajirahisi, na
mume wangu sio malaika, ni lazima katekwa na huyo binti..ule urembo
umemzuzua..mtu anakaa khanga moja, hajali kujisitiri, unafikiria
nini…’akanisingizia mengi, kitu ambacho sio kweli, mimi nikiwa hapo nyumbani nikijua
wapo, nahakikisha nimevaa gauni kubwa , pana, siunajua magauni ya akina mama
wakiwa wajawazito..sikuwahi kuvaa nguo fupi….labda kama ilitokea siku chache!
‘Mimi nimeshaongea na mume wako kanihakikishia kuwa hawezi
kufanya uchafu huo,…na mume wako namuamini sana…lakini kama una uhakika,
..nitafutie ushahidi,…kama utaniletea ushahidi, ….siwezi kuvumilia tabia hizo
nitamfukuza, sitajali kuwa mimi nilimdhamini…’nasikia alisema mzee huyo siku
alipokutana na huyo mama.
Haya limetokea, na
mama mwenye nyumba keshaupata huo ushahidi….mzee alipoitwa ina maana
alionyeshwa huo ushahid, ushahidi wa picha, na kuambiwa haya mtu wako uliyekuwa
ukimtetea ndiye huyu, ona anachofanya na mume wangu, ….mzee kuiona hiyo picha
hakuamini, akamuuliza baba mwenye nyumba…vipi kulikoni…
‘Wewe , si uliniambia ….’ukumbuke haya nayawaza tu kichwani,
sikuwa nimeyafahamu kwa muda huo…lakini ndivyo ilivyokuja kujulikana baadaye,
kwa siku hiyo sikuwa nimekijua walichokiiongea, ila kwa pale niliwaza hivyo …..
Nahisi baada ya malumbano makali, ikaonekana kuwa mimi
sifai, na mzee akaona ni heri mimi niondoke, lakini kabla hajaungana na wengine
akaona kwanza aje kulithibitisha hilo kwa kutaka
kusikia kaulii yangu..kauli yangu tu, ndiyo aliyoitaka kama ningelijua hilo
ningetafuta mbinu za kutokumjibu, lakini nilimuamini sana huyo mzee nikaona
nimuambie ukweli …nimjibu anavyotaka yeye...ila mengi ya nyuma ya pazia yalikuwa
ni siri ambayo hakuvuta subira nimsimulie, angeliyajua hayo, nahisi angepasuka
kwa hasira….sasa itabakia kuwa siri yangu
Hata hivyo mimi nilijua kuwa ujio wa mzee ungelilenga moja
kwa moja swala la hiyo ndoa, kuwa nimefumaniwa,….. Lakini cha ajabu mzee
hakutaka kuliongelea hilo la mimi kutembea na mume wa mtu, hakutaka kunitupia
shutuma hizo , yeye akaja na jambo jingine kabisa, kutaka kujua kama kweli nilitembea na hao
wanaume wanne.. na aliposikia kauli yangu akaaondoka
Je ni hiyo kauli tu!,…hapana ni zaidi ya hilo,..mimi kwa
muda huo sikutaka kuyajua zaidi, nilichotakiwa kukifanya ni kuondoka
hapo,…sikutaka kukabiliana na wenye nyumba tena, nilijua ni nini kitatokea,
naogopa nitazidiwa kwa maneno nitajibu na majibizano yatazaa vita, …na mimi
sikuwa na nguvu tena ya kugombana na mtu, niliyo nayo yanatosha, nikakumbuka
kauli ya mzee wakati anaondoka alisema;
‘Kwa jibu lako hilo, kwa kauli yako hiyo kuwa ulitembea na
wanaume wanne, na si mmoja, si huyo mwanaume wako tu, na nilijua hao
wanakusingizia, ndio niliona ushahidi lakini waweza kutengenezwa..nilitaka
kauli yako, na wewe umelithibitisha hilo, mmmh, sasa….hapana, hapoo tena siwezi kuvumilia….’ na ndio, akaondoka
Kumbe alipoondoka hapo alikwenda moja kwa moja kuitisha
kikao chao cha wajumbe wa kijiji. Wajumbe hao walikuwa wakisubiria kikao hicho,
kwani aliyekuwa kikwazo cha kufanyika kikao hicho cha maamuzi ni huyu
mzee, ….ni huyo mzee,…
Sasa kikao kinaenda kuitishwa, je mzee atasema nini kwenye
hicho kikao, kwani yeye ndiye aliyekuwa kaweka pingamizi, je atanitafutia
sehemu nyingine…niende kuishi kwake, yeye hana uwezo wa kunichukua kwake kwani
nyumbani kwake kumejaa, ana familia kubwa…siwezi kwenda kwake, kamwe..ni aibu,
nitaishije huko… nitakuwa mzigo mwingine kwake…
Kwa vyovyote iwavyo, uamuzi wa kikao hicho, ninajua utakuwa nifukuzwe hapo kijijini, na nikifukuzwa
nitakwenda wapi….Nirudishwe kijijini kwetu..na je mzee anaweza kunitetea tena
kwa lipi…sizani…! Labda watapanga kunirejesha nyumbani kwetu….!
‘Hapana kwetu siwezi kurudi hata kama ni kwa dawa…..’,
nilishawaambia,
‘Kwetu hasa kwa wazazi wangu sirudi , ni bora kufa….’
Niliwaambia mapema, kwahiyo wazo la kunirejesha kwetu halipo,…wanalifahamu hilo,…labda
watumie nguvu, na wakitumia nguvu, je wazazi wangu wapo tayari kunipokea, hasa
baba , baada ya kashifa zote hizo …sizani ,mimi namfahamu mzee wangu ana
msimamo mkali, akiamua kaamua….
‘Hapana huko sirudi,….na kama wakifanya hivyo,watarudisha
maiti yangu….’nikajisemea na ndipo mlango ukafunguliwa..na kukatiza mawazo
yangu, nikatoa macho ya uwoga….!
NB; Hii ni nyongeza kabla ya kukutana na huyo mtu
aliyeingia, sijui ni baba mwenye nyumba au mama mwenyenyumba au ni mzee alirudi
tena, au ni walinzi wa kijiji walikuja kunifukuza.
Nimeamua kuifafanua sehemu
hiyo kwa undani zaidi ili watu waelewe, kuna watu wameniuliza nafikiri sasa
watakuwa pamoja nami.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment