Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, October 1, 2015

RADHI YA WAZAZI-45Hiyo ndio sehemu niliyomuhadithia kaka yangu, ndugu zanguni,...’akasema huyo mzee tuliyemkuta kwenye hiyo nyumba, akaendelea kusema

‘Sasa mengine yalikuja kutokea baada ya huyo kijana kurejea hapa nchini,.....’akasema

‘Kijana yupi..?’ nikamuuliza

‘Kijana ambaye alikuwa akiishi na profesa huko nje, kijana ambaye alikuja kuungana na mama mtemi .....’akasema

‘Kwanini alirejea nchini,..?’ nikamuuliza

‘Unajua hayo yalitokea kama mapinduzi, ....kila taifa lina hili tatizo, la vijana wengi kukosa ajira, na wenyeji wa nchi husika mara nyingi hudhania kuwa ajira zao zimechukuliwa na wageni,.....ndio maana wao hawana kazi....hili lilitokeapia huko ....’akasema

‘Huko Ulaya!?’ nikamuuliza

‘Ndio, huko Ulaya,.... vijana wa nchi hiyo aliyokuwa akiishi profesa nao walikuja juu, wakiandamana kutaka wageni waondolewe makazini...ili wao wenyeji wawezi kuajiriwa,...kwanini wageni wakapate ajira wakati wao wenyeji hawana ajira....na ukumbuke kuwa wenzetu, wana taratibu za kuwalipa watu wao wale wasiokuwa na ajira japkuwa kiasi wanacholipwa ni kidogo....’akasema

‘ Basi kutoka na ghasia hizo, wanasiasa wakainglia kati, ikabidi upite mchujo wa raia wa kigeni upite, na wale walioonekana kuwa wanaweza kurejeshwa makwao, warudishwe, na wengine walifanyiwa utaratibu wa kupata ajira kwenye balozi za nchi  hizo kwa wale walioonekana wanafaa kufanya kazi hizo, na mmojawapo alikuwa kijana wetu,...’akasema huyo mzee

‘Kwahiyo kijana wetu  akarudi na mkewe...’akaongezea

‘Na mkewe....?’nikamuuliza kwa kushangaa

‘Ndio walishaoana na huyo mtoto wa mama mtemi na wakati wanakuja huku walikuwa tayari wana mtoto mmoja, na wa pili walimpatia wakiwa huku huku kwetu...’akasema huyo mzee na kutulia kama vile keshamaliza kisa , na mimi nilipoona hivyo nikamuuliza;

‘Sasa hiyo hali ya kuchanganyikiwa ilitokeaje maana katika maelezo yako tumesikia zaidi kuhusu wewe, hukutuelezea kuhusu huyo kijana ambacho ndicho tunachokihitajia...?’ tukamuuliza

‘Najua...ila nilitaka muone chanzo halisi , ni wapi kijana wetu alitokea....kama angelikuwa na uwezo wa kuongelea mambo yake angeliwaelezea zaidi kwa upande wake,...’akasema

‘Kwahiyo ....?’ nikataka kuuliza na huyo mzee akaonyeshea mkono kama kuninyamazisha akasema;

‘Nitawaelezea msijali, ...jinsi ilivyokuja hadi kijana akawa hivyo....si mlimkuta barabarani kapanga  mavitabu, anatoa ‘lecture’...moja baada ya nyingine au sio.....’akawa kama anauliza

‘Ndio baadaye akaanza kuporomosha matusi...’mwenzangu akasema

‘Yah...ndio muone nini maana ya mzazi...na sio kwamba mzazi, au wazazi wake walisema au walitaka awe hivyo..hapana mungu mwenyewe kataka kuonyesha uwezo wake....’akasema

‘Kwa vipi....?’ nikamuuliza

‘Hii ni sehemu ya pili,...ambayo nitawaelezea yaliyotokea huku Tanzania......’akasema huyo mzee

******************

‘Ilibidi niwaelezee kuhusu Profesa , maana yeye ndiye aliyesababisha hayo yote...’akaendelea kusema

Profesa kila mara alikuwa akikiri hilo, na hata kufikia kutubu, kuwa bila yeye hayo yote huenda yasingelitokea...hata hivyo, hadi kufikia kijana kuchanganyikiwa hiyo ili ni baadaye ni kipindi ambacho kijana ana fahamu zake ana utashi wake, usingeliweza tena kumbebesha lawama profesa

‘Muda ulifika Profesa akawa sasa anaendelea vyema, na mara nyingi alikuwa akitumia dawa zake za mitishamba, na ikafikia hatua afya yake ikaanza kuimarika, na hata akaanza biashara yake ya kuuza dawa za kienyeji, na hata kupeleka mjini.

Na mara ya kwanza alipofika hakutaka kabisa kupitia eneo alipokuwa kajenga, alijitahidi kufuata masharti ya kaka yake, lakini mara pili hisi zikamvuta, akashindwa kuvumilia.

Siku hiyo, alimua kupitia tu angalau aone hiyo nyumba ipoje, kwani alishasikia kuwa imekarabatiwa na kutengenezwa upya.....

‘Ngoja nipitie tu nikapaone...’siku hiyo akasema na kweli akapitia huko.

 Alipofika eneo hilo, kwanza alijiona kama kapotea kwani mji ulikuwa umebadilika, mitaa mingi ilikuwa imeboreshwa , bara bara ambayo kipindi hicho ilikuwa haina lami, sasa ina lami, akajisema moyoni, kweli maendeleo yapo.

Akatembea hadi pale kulipokuwepo nyumba yake,  hakuweza kuamini, japokuwa nyumba yake kipindi hicho ilionekana kubwa ya kisasa, lakini sasa alichoona ni nyumba nyingine iliyojengekea kisasa zaidi....na hakuna mabanda ya mbele tena, kilichoonekana ni ukuta mkubwa wenye nyaya za usalama juu yake..

‘Mhh, hawa wajanja wamefanya hivi ili nione kuwa ilikuwa sio nyumba yangu..’akasema huku akiisogelea, na alipofika kwenye eneo la geti la kuingilia ndani, akagonga hodi na mara akatokea mlinzi, kwanza hakumsemesha akawa anaangaza macho ya kushangaa.

‘Unasemaje...?’ akauliza huyu mlinzi na profesa akawa anaendelea kukagua akitafuta mwanya wa kuangalia kwa ndani.

Nyumba ilikuwa imebadilika kabisa, imefanyiwa ukaratabati wa hali ya juu, sio ile nyumba yake tena aliyokuwa akiifahamu, ni nyumba imara ya kisasa zaidi, ikiwa na kila kitu cha nyumba ya kisasa.

‘Mhh kweli ni kama imejengwa upya....lakini hawawezi kunipiga changa la macho, hii ni nyumba yangu...’akasema kwa sauti na yule mlinzii aliyekuwa kasimama akimuangalia akabakia kushangaa, akamuuliza

‘Nyumba yako kwa vipi,...umechanganyikiwa nini. wewe....?’ akauliza huyo mlinzi

‘Hahaha nimechanganyikiwa, ..hebi nikuulize wewe umekuja lini hapa mjini...?’ akauliza

‘Hata kama nimekuja jana, juzi au mwaka juzi, inakuhusu nini wewe, ....?’ akauliza huyo mlinzi

‘Maana hufahamu chochote kuhusu hii nyumba awali ilikuwa ni ya nani....?’ akauliza profesa

‘Mimi nafahamu hii nyumba ni ya wenye hii nyumba ....’akasema

‘Wewe ulikuwepo eneo hili wakati hii nyumba haijakarabatiwa..?’ akaulizwa

‘Sikuwa nafanyakazi hapa, nilikuwa sehemu nyingine, lakini nilikuwa napita mara kwa mara.....’akasema huyo mlinzi akionyesha hamasa ya kutaka kujua zaidi.

‘Kabla haijakarabatiwa ulikuwa ukifahamu kuwa nyumba hii ilikuwa ni ya nani.....?’ akauliza

‘Mimi sijui, na hainihusu....kwanini unauliza hivyo...?’akasema na kuuliza

‘Basi kwa taarifa yako hii nyumba ilikuwa ni ya jamaa mmoja aliyejulikana kama profesa....’akasema

‘Hahahaha....unanichekesha kweli, mimi nijuavyo hii nyumba ilikuwa ya mzungu, ambaye alikuja kuwauzia hawa wenye hii nyuma kwa hivi sasa.....ambao ndio wameamua kuikarabati kama inavyoonekana kwa sasa....’akasema

‘Sawa, ipo siku mtakuja kuujua ukweli.....’akasema Profesa na kutulia kidogo.

‘Ukweli wa nini.....ili iweje, aah,....?’akasema huku akitaka kugeuka kuendelea na shughuli zake

‘Samahani nilikuwa naulizia huyu mtu anayeihi hapa yupo wapi?’ profesa akamuuliza huyo mlinzi

‘Hayupo kaenda kazini....’akasema huyo mlinzi bila hata kugeuka kumuangalia muulizaji.

‘Na mkewe, au hana mke?’ akauliza Profesa  na huyo mlinzi akageuka sasa akiwa mkali, akasema;

‘Kwanini unawaulizia, unataka nini kwao...una shida gani kwao?’ akauliza kwa hasira

‘Mimi ni mgeni wao, nahitaji kuonana nao...’akasema profesa.

‘Ndio hivyo, nimekuambia hawapo wamekwenda kazini....umenielewa au...’akasema huyo mlinzi akiwa kakunja uso, na profesa hakutaka kuongea zaidi akageuka kutaka kuondoka, halafu akasimama akageuka tena kuangalia muelekea wa hiyo nyumba, hakuweza kuona ndani kwasababu ya hilo geti moyoni akawa anasikitika, na baadaye akasema;

‘Mhh, hiki ndio ilitakiwa iwe kinua mgongo changu, kwa umri kama huu, ningekuwa na kiota cha kunisitiri, naona mabanda yote yaliyokuwa hapa mbele wameyabomoa, yalikuwa yakinisaidia sana kwa kukodisha.....lakini ...ipo siku, na ...tutapambana tu....’akasema na yule mlinzi akawa anamuangalia huyo mgeni kwa macho ya kujiuliza, halafu akasema;

‘Kwani  wewe ni nani...?’ akauliza huyo mlinzi

‘Ipo siku utajua tu....’Profesa akasema na kugeuka kuondoka , alirudi sehemu ambapo alikuwa akiuzia dawa zake, akaendelea kutafuta wateja, maana kazi ya kuuza dawa kama hizo inahitaji kuhangaika kweli, na ilibidi kufanya mazingaumbwe na vioja mbali mbali ili kuwaita watu waje kuvutika nazo.

Siku hiyo hakutaka kurudi mapema kijijini, sio kwasababu ya biashara, lakini alikuwa na hamu ya kuwaona wamiliki wa nyumba yake, aliendelea kuuza dawa zake hadi jioni., Na ilipofika jioni, akafunga funga shughuli zake na haraka akarudi tena mitaa ya iliyokuwa nyumba yake.
Alipofika akamkuta mlinzi mwingine sio yule aliyeonana naye mchana, ikabidi kwanza aanze kumdadisi.

‘Samahani afande, eti mwenye nyumba hii kesharudi....?’ akauliza

‘Kwanini unauliza hivyo, wewe ni nani?’ mlinzi akauliza

‘Mimi natokea huko kijijini, mwanzoni alikuwa akiishi jamaa yangu hapa, ndio nataka kujua kama yupo au kasafiri...?’ akauliza

‘Jamaa gani...?’ akauliza

‘Alikuwa mangaji wa hii nyumba, lakini kabla hajakarabatiwa....’akasema

‘Alishandoka, mbona siku nyingi sana...hii nyumba sasa hivi inamilikiwa na watu wengine kabisa....’akasema

‘Inamilikuwa sio imekodishwa, sio kuwa hawa wanaoishi hapa ni wapangaji, na wenyewe wanaishi ulaya...?’ akauliza

‘Walikuwa wakiishi ulaya ndio, sasa wamekuja kuishi wenyewe, hakuna mpangaji, wanaishi wenye nyumba....’akasema

‘Ohoo, kumbe wanaishi wazungu, ndio maana wameitengeneza hivi...’akasema profesa na huyo mlinzi akataka kuachana naye, lakini profesa akamuuliza swali jingine.

‘hivi unamfahamu aliyekuwa mumiliki wa hii nyumba kabla haijauzwa....?’ akaulizwa

‘Namsikia tu, mimi sikuwahi kuonana naye.....’akasema

‘Unamsikia tu,...alikuwa nani, unamsikiaje?’ akaulizwa

‘Namsikia tu, alikuwa naye anaishi huko Ulaya, akaishiwa , akawa naumwa sana, ikabidi auze nyumba yake ili awezi kujitibia, nasikia alikuwa tapeli,...akaja kuumwa huu ugonjwa, akarudishwa huku akiwa kazidiwa, na ameshafaiki dunia,....huu ugonjwa unawamaliza sana watu wetu....’akasema huyo mlinzi

‘Nani alikuambia hivyo?’ akaulizwa

‘Watu wengi wanaomfahamu mbona wanalifahamu hivyo, ....’akasema na mara akaangalia kwa ndani, akasema

‘Ulikuwa na shida gani ndugu...?’ akauliza sasa

‘Nataka kuonana na huyo mumiliki wa hii nyumba, umesema ni mzungu au?’ akauliza

‘Kama ni kazi hakuna kazi , walishaniambia hawataki watu kuja kuwasumbua, niwaeleze kabisa kuwa hakuna kazi....’akasema mlinzi

‘Mimi natokea kijijini, nahitajia kuonana na mwenye nyumba hii nina mashitaka dhidi yao....’akasema profesa kwa ukali

‘Mashitaka , mashitaka gani...?’ akauliza mlinzi

‘Wewe niitie au niingie nionane nao mimi mwenyewe....’akasema kwa ukali, na mlinzi akaingiwa na hamasa, akamuangalia huyo mgeni kwa makini, halafu akasema;

‘Niwaambie wewe ni nani..?’ akauliza

‘Profesa.....’akasema na huyo mlinzi akamuangalia huyo mgeni kwa makini na kusema,

‘Wewe ni profesa,...mmh, najua maprofesa ni watu waliosoma, wana kazi zao, ....sasa wewe mbona ....’akasema na profesa akasema

‘Unaniitia su niingie mwenyewe....’akasema kwa ukali

‘Hebu subiri...’akasema na kufunga mlango vizuri, akarudi kibandani kwake akachukua simu na kupiga, akawa anaongea, na sauti ilikuwa haisikiki vyema ila alisikia jina lake likitajwa;
Baadaye mlinzi akafungua mlango akasema;

‘Kaniuliza maswali mengi, kwani mwenyewe alikuwa na miadi ya kuonana na rafiki yake anasoma chuo kikuu, lakini anasema huyo mtu hajafikia ngazi ya uprofesa, sasa akahisi anatania tu kwani ana ndoto ya kusoma hadi uprofesa, lakini wewe sizani kama unasema chuo kikuu......’akasema

‘Niingie au nikaje na askari, ndio utaniruhusu niingie...?’ akauliza profesa

‘Ingia ndugu, Profesa......wanakusubiria ndani...’akasema sasa akimpisha huyo mgeni huku akimuangalia kwa mashaka

‘Huko kwenye mfuko umebeba nini....?’ akauliza

‘Dawa zangu, nauza dawa....una matatizo ya ngiri,...tumbo kijaa gesi, nguvu za kiume,....’akaongea kama anavyonadi dawa zake akiwa kazini..

‘Hapana ndugu, kama lengo lako ni hilo kuwauzia dawa, watu hao hawahitaji dawa hizi za kienyeji, ...’akasema

‘Sitaki kuonana nao kwa ajili ya dawa, kama una shaka na hilo, nahifadhi mzigo wangu hapa, nataka kuonana nao kwa maswala mengine kabisa...’akasema sasa akikagua mandhari ya ile nyumba maana alikuwa ameshaingia kwa ndani, akageuka upande ambapo kulikuwa na mti na kiti cha kubembea, mti ule na kiti kile bado kilikuwepo, akasema

‘Kiti changu bado kipo, naweza kwenda kukaa kidogo....?’ akauliza yule mlinzi akamuangalia huyo mgeni kwa mashaka,akasema;

‘Unaweza kwenda kuwaona, kama hunatajali, maana siruhusiwi kuongea na wageni hapa getini, ...’akasema na profesa akaona asipoteze muda, akatembea huku bado akikiangalia kile kiti, hadi alipofika kwenye geti jingine la nyumba.

Lilikuwa ni geti la nguvu, unabonyeza kitufe linajifungua, na hapo unaiona nyumbe yenyewe sasa, na kulikuwa na mtoto akicheza mpira kwenye bustani, alikuwa na sura ya kizungu ,moyoni akajua kweli wenyeji ni wazungu.

Akasoegelea mlango akagonga mara mbili tatu na mara mlango ukafunguliwa na binti, ambaye alimuangalia huyo mgeni akionyesha mshangao usoni, akasema

‘Wewe ndiye profesa...?’ akauliza

‘Ndio, wenyeji wapo wapi, na wewe ni nani?’ akauliza kwa sauti la lafudhi ya kizungu, kuonyesha msisitizo, na huyo binti akawa kama anajizuia kucheka, akashika mdomo.

‘Kwanini unacheka....?’ akauliza

‘Hapana samahani unavyoongea tu, unanichekesha...’akasema

‘Wewe ni nani...?’ akauliza

‘Mimi ni mfanyakazi wa ndani wa nyumba hii subiria nikuite wenyewe....’akasema sasa akionyesha mashaka...

‘Kama nakufahamu vile....’akasema Profesa , alijisemea tu kiutani

‘Hapana hunifahamu....’akasema huyo binti, na kufunga mlango, hakumkaribisha ndani, ukapita muda, na baadaye akarudi na kusema;

‘Karibu ndani....’akafungua mlango na profesa akaingia ndani

‘Wenyeji wapo wapi...?’ akaendelea kutumia lafudhi ile ya kizungu, na yule binti akafanya vile vile akitaka kucheka lakini akaweka mkono mdomoni kujizuia

‘Wanaogelea....’akasema

‘Kwani hii nyumba imewekwa bwana la kuogelea ...!?’ akauliza Profesa kwa mshangao na huyo binti akatabasamu na kusema

‘Ndio....lipo kwa nyuma huko,...’akasema huku akiendelea kunyosha nguo kwa haraka yanekana zilihitajika kuvaliwa na wenyewe nyumba.Na kwa muda huo profesa alitarajia kuulizwa unatumia kinywaji gani, lakini binti alikuwa akihangaika na kunyosha nguo tu....

‘Naweza kupata maji ya kunywa...au..?’ akauliza profesa na binti akaangalia nyuma ya profesa kama kutoa ishara, hakusema neno, na profesa akageuka nyuma na akaona mashine ya maji iliyoandikwa Cool Blue, na vikombe vya plastiki vya kutumia mara moja, akasema

‘Oh, afadhali,yaani nina kiu.....basi wewe endelea tu na kazi yako mimi nitajisaidia mwenyewe...’akasema na kuanza kunywa maji, alikunywa maji kwa tani yake, halafu akasema

‘Sasa basi tumbo limejaa,....maji baridiiii...mmh ’akasema na kurudi kukaa kwenye sofa akakunja nne akimuangalia yule binti akiendelea na usafi na kwa nje kwa kupitia dirishani akamuona binti au mwanadada wa kiziungu akiwa na vazi la kuogelea, akipita na kuotea alikuwa kabalia mawani usoni, akajaribu kuchunguliza zaidi kwa nje lakini hakumuona tena.

‘Huyo mwanadada huko nje mzungu ndiye mwenye nyumba au....?’ akauliza profesa akichungulia kule dirishani na yule binti akageuka kuangalia huko nje kwa kupitia dirisha hilo la viyoo lakini hakuona kitu, hata hivyo akatikisa kichwa kukubali.

‘Mhh, nilijua tu, hata hivyo nitapambana nao...’akasema profesa na huyo mdada akawa anaendelea kunyosha nguo hakusema kitu.

‘Wewe ulianza kufanyakazi na hawa watu toka lini?’ akauliza

‘Siku nyingi, tangu walipofika toka huko ulaya....’akasema huyo binti

‘Kwahiyo kumbe unawafahamu sana....nitafurahi nikipata muda tukaongea wote kama hutojali...’akasema

‘Kuhusu nini...?’ akauliza huyo binti, bila kumuangalia

‘Nitakuja kukuambia, ngoja nionane nao kwanza....’akasema na kuendelea kuangalia humo ndani kwa makini, halafu akasema;

‘Mhh, kweli wameiboresha, mwanzoni haikuwa na ukubwa huu, na humu wamepaongezea......’akasema na huyo binti akainua uso na kumuangalia, Profesa lakini hakusema kitu.

Profesa sasa akawa anaendeela kukagua mandhari ya hapo ndani kwa macho, .....na binti akawa anaendelea na shughuli yake, wote wakiwa kimia.

Kilikuwa ni chumba kikubwa cha maongezi kilichopangiliwa vizuri kabisa na kulikuwa na masofa ya kisasa makubwa kweli....na katikati kulikuwa na meza kama ya mkutano, imepangwa viti kuiznguka, na maua yasio asili yakiwa yamepangwa vizuri juu ya hiyo meza...kulikuwa na matunda kwenye mabeseni,

Profesa akaingiwa na hamu ya kutaka kuchukua moja, lakini akavutiwa na kitu kingine, kwenye, ukutani kulikuwa na runinga kubwa, ikionyesha matukio mbali mbali, na moja ya tukio na jamaa aliyefukuzwa huko ulaya kwa makosa mbali mbali, akawa na hamasa ya kutaka ni wapi huko, na akilini na yeye akawa anakumbukia tukio lake....

‘Mhh, mbona sisi hatuwafukuzi huku kwetu, kwao wanatudharau, wanatufukuza huku kwetu tunawakumbatia, tunawaita tunawaona kama mungu mtu.....’akasema akisonya, na huyo binti akatabasamu.

Akiwa bado anaangalia kwenye runinga ambayo iliwekwa kwa sauti ndogo, mara sauti ikasikika , ilikuwa sauti ya kike , na ilikuwa ni lafudhii ya kizungu ikiongea, na ilionyesha alikuwa akimuongelesha huyo mfanyakazi.

‘Huyu mgeni yupo wapi...’sauti ikauliza

Profesa ambaye alikuwa kazama kwenye mawazo, akiangalia runinga, akajiinua pale alipokuwa amekaa, kwani alikaa mkao wa kujiegemeza kama kulala upande upande, na haraka akageuza kichwa kuangalia wapi sauti hiyo imetokea.

Profesa  hakuweza kumuaona huyo aliyeongea, akahisi hueda huyo mtu alishapitiliza na kuingia kwenye chumba ambacho kilionekana mlango wake upo wazi, akamtumpia jicho huyo binti mfanyakazi, ambaye kwa muda huo alikuwa akiendelea kunyosha nguo kwa haraka, ili kuwa na uhakika Profesa akauliza,....

‘Yupo wapi....?’ akawa anamuuliza huyo binti huku akiagalia kile chumba ambacho mlango uo wazi, na huyo binti aliendelea na kazi yake bila kusema kitu.

Profesa akawa sasa kakaa vizuri akijua kuwa mwenyeji wake sasa hivi atajitokeza na kwahiyo anahitajika kujipanga jinsi gani ya kukabiliana naye, kwanza alishajiandaa kutoa vitisho, kuwa nyumba hiyo alitapeliwa, kwani hati yake bado anayo....kwa vile mauzo yalifanyikia ulaya, hati ya nyumba ilikuwa haikuchukuliwa, lakini yaweza ikawa imepitwa na wakati..

‘Nitaanza na hilo kujaribu,....’akasema na mara akasikia mtu akikohoa, ilikuwa ni kutokea chumba kile ambacho mlango upo wazi...

Taratibu, akageukia upande ul na kumuona huyo mwanadada wa kizungu akiwa kasimama mlangoni, akiwa kageukia mlango wan je, kama vile anajua kuwa mgeni huyo bado yupo huko nje. Profesa akataka kusimama ili amuone vizuri, lakini huyo mwanadada akawa anatembea kuelekea pale alipokuwepo huyo mfanyakazi wa ndani..

‘Huyo mgeni bado yupo nje....?’ akauliza huyo mwandada wa kizungu na huyo mfanyakazi akanyosha mkoni kuonyesha pale alipokuwa amekaa Profesa na huyo mwanadada wa kizungu, akataka kama kugeuza kichwa mara moja kwa haraka na kurejea kuangalia kile alichokuwa akikiangalia, alikuwa akiangalia nguo alizokuwa akinyosha mfanyakazi, halafu akachukua nguo mojawapo akasema

Kulikuwa na kizuizi pale alipokaa Profesa na hao wenyeji wake, na ilimfanya Profesa asiweze kuwaona vizuri, kama huyo mwanadada angelikuwa kasimama pale alipokuwa kasimama huyo mfanyakazi ingelikuwa ni rahisi kwa profesa kumuona vyema.

‘Hii kamwekee mume wangu ,ndiyo atakayoivaa...sawa eeh...’akasema huyo mwanadada wa kizungu, halafu sasa akawa kama anataka kugeuka upande ule alipokaa mgeni, lakini akasita na kuendelea kupanga hizo nguo alizokuwa akinyosha huyo binti,  na kusema;

‘Mgeni samahani kidogo, ...,sijui tukusaidie nini...’

‘Nashukuru, wewe ni mwenye nyumba nataka kuongea na mume wako .....?’ Profesa akaanza kusema akitaka kusimama, lakini alipoona huyo mwanadada anaendelea kufanya jambo a huyo mfanyakazi, akarudi kukaa, profesa akajipa moyo akisema kimoyo moyo;

‘Mambo mazuri hayataki haraka..’akasema huku moyo ukimuenda mbio, akilini alihisi kitu lakini hakuwa a uhakika nacho, akawa anasubiria....

Profesa akiwa anasubiria moyoni akijaribu kujipa uhakika kuwa nyumba hiyo inamilikiwa na wazungu, aligeuza kichwa chake kuendelea kuangalia runinga, alijua kabisa huyo mwanadada wa kizungu hawezi kuongea lolote mpaka huyo mwanaume wake aje, huyo mwanaume wake alikuwa bado akiogelea au akifanya jambo huko nje, na moyoni akasema

‘Ni lazima nipambane nao, hata kama ni wazungu.....’akasema na wakati anaongea kimoyo moyo huku akiangalia kitu kwenye runinga, akahisi kuwa kuna mtu yupo karibu yake, ni yule mwanadada alikuwa tayari keshafika kwenye sofa lililokuwa upande wa pili, .kuliani kwake, akageuza kichwa ili kumuangalia huyo mwanadada wa kizungu na sasa wakawa wanaangaliana uso kwa uso na  huyo mwanadada,....

Profesa alijikuta akishtuka, na kubakia kutoa macho ya kutokuamini hicho anachokiona

‘Ni wewe....’profesa akasema huku akibakia mdomo wazi, na yule mwanadada aliyekuwa ameshakaa, akasimama akionyesha wasiwasi naye akiwa katoa macho kuashiria kuogo,akawa kashika mdomo, na kwa sauti yenye kigugumizi akasema;

What the hell,... Who is this man..?’ aliuliza huyo mwanadada wa kizungu akiwa bado katoa macho na kule kwenye mlango wa kutokea nje, kukatokea sauti ya kiume, huenda alikuwa ndio mume wa huyo mwanadada wa kizungu ikiuliza:

‘Kwani kuna tatizo gani....’sauti ikasema,na hiyo sauti ikamfanya Profesa azidi kupatwa na mshituka,...na kwa vile alishakuwa na tatizo la shinikizo la damu, akahisi mapigo yakienda mbio,....pumzi ikawa kama haitshi, ila alijitahidi na sasa yeye akasimama huku mkono mmoja ukishikilia lile sofa, akitaka kugeuka kuangalia huko sauti ya kiume ilipotokea....

NB: Ni nani huyo


WAZO LA LEO:Tabia njema ni pamoja na jinsi gani ya kukirimu wageni, ..hata kama tuna haraka, au hatuna muda wa kuongea na huyo mgeni lakini tuwe na namna njema ya kumfanya mgeni ajisikie vyema, asione kadharauliwa, ..kwani kwa kufanya hivyo, kuonyesha hutaki mgeni, huna muda wa kuongea, au kwa wenye uwezo kuhisi kuwa mgeni kaja kuomba, tunajikosesha baraka.
Ni mimi: emu-three

No comments :