Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, September 11, 2015

RIZIKI HAIGOMBWI-UTANGULIZI


RIDHIKI HAIGOMBWI-utangulizi

Baada ya kusikia tetezi kuwa kuna jamaa mmoja alikuwa freemasoni, na akakiukamiiko, na hatimaye kufirisika,mimi nikaingiwa na hamasa ya kumjua na kujua ni nini nyuma ya pazia

Ndio chanzo cha kisa chetu

Siku hiyo ndio nikaamua kumuendea huyo mtu, ajulikanaye kama Mzee tajiri, lakini kwa siri walikuwa wakimuita mzee wa freemasoni , kwanini walimuita hivyo, kwanini ilikuwa hivyo, ndio chanzo cha kisa chetu,..

Na tulivyofika kwake ndio akaanza kunisimulia kisa cha maisha yake, akianza hapa kama utangulizi tu, alianza kwa kusema,

'Wengi walihisi mimi ni freemason, lakini hapana...’akaanza kusema.

'Kwanini walikuhisi hivyo?' Nikamuuliza kwani hata lengo la kuja kuonana naye ilikuwa hivyo,kuwa tumesikia kuwa yeye alikuwa ndani ya taasisi hiyo, na mimi nikavutika kutaka kujua zaidi ndio nikafika hapo nikielekezwa na rafiki yangu

'Walifikia kusema eti utajiri wangu niliokuwa nao ulitokana na taasisi hiyo na imani zao, eti baadaye nikakiuka masharti ndio maana nimefirisika,...' akasema na mwenzangu aliyekuwa karibu akanifinya kuniashiria kuwa huyo mzee anadanganya

'Ni kweli nilikuwa tajiri sana,..nikafikia kumiliki kampuni kubwa tu,.., na sio kampuni moja.kampuni hiyo kubwa ilikuja kuzaa kampuni nyingine zikiwa zipo chini ya kamuni hiyo tanzu....'akasema.

Nilimuangalia huyo mzee jinsi alivyo, akiwa kavalia shati kuukuu, iliyogimbaa kwa jasho, tai shingoni,..kuashiria alikuwa akijpenda, au ...ndio hivyo, kama walivyosema watu alikuwa mtu mkubwa, mashuhuri,..lakini nilipotupa macho miguuni, nikakuta kavalia kandambili, zilizokwisha na zikiwa na rangi tofauti...

'Sasa sina utajiri tena., sina cha kampuni wala dalili ya hizo kampuni, ukifuatilia utagundua ni kampuni yenye madeni yasiyolipika,ikiwa na maana nilifirisika.., sasa sina mbele wala nyuma, nimekuwa masikini wa kutupwa, hata pesa ya kula naipata kwa kuomba omba...'akasema kwa uchungu 
‘Ilinichukua muda kuamini hivyo, kuwa sasa sina kitu,...huwezi amini, mimi aliyekuwa tajiri, nijifunika ili nisionekane, nakwenda barabarani kuomba...kweli hujafa hujaumbuka..’akasema kwa uchungu

Unaweza ukafikiria kuwa huyu mtu ni muongo, ukimuona kwa hali aliyokuwa nayo,unaweza ukafikiria anajitukuza tu, kuwa alikuwa tajiri , akawa anamiliki kampuni, alikuwa mkurugenzi, ..lakini mimi mwenyewe niliona kwenye gazeti, likionyesha enzi zake, akiwa mkurugenzi, akiwa anaongea na mawaziri, akifungua vituo mbali mbali vya watoto mayatima...leo hii ukimuona unaweza kusema ni kizee cha wapi.
'Mimi nilikuwa mkurugenzi, naheshimika, najuana na mawaziri...na hata mkuu wa nachi' Akasema sasa akinitupia jicho na kuangalia chini kama anaona aibu.

'Lakini, leo, unavoniona ndio hivi,...natamani hata kujiua...lakini kwanini nijiue, nilijiuliza mara mbili tatu, nijiue, wakati siku yangu itafika, nitakufa tu...'akasema kwa sauti ya unyonge.

'Mimi nilikuwa na mke wangu mrembo kweli..nikisema mrembo ni mrembo kweli, kila nikipita naye mitaani, watu hugeuza shingo kumtizama, na alivyokuwa na maringo, basi ikawa hata waandishi wa habari wanamfuata kila anapokwenda ili kupata picha zake....' akasema
'Lakini leo hii unavyoniona hapa nilipo sina cha mke wala mtoto...’akasema
‘Wamekwenda wapi...?’ nikamuuliza na hapo akainua uso kunitizama na machozi yakaonekana yakimlenga lenga.
‘Usinikumbushe mbali...mke hayupo na wala sijui katoweka wapi, .....na aliondoka na mtoto wangu, ...’akasema

‘Kwanini aliondoka...?’ nikamuuliza
‘Hivi hali niliyo nayo unaweza kuishi na mke mrembo kama huyo...mtu aliyekuwa kazoea kula chakuala kutoka ulaya , maji kutoka ulaya, na kila upande kazungukwa na wafanyakazi wa ndani, akikohoa anaulizwa ‘madame unataka nini...’akasema kwa mikogo.

‘Mke wangu nilimpenda sana, ...kila alichotaka nilimpa, na alikuwa mshauri wangu mnzuri sana, alijua jinsi gani ya kunifanyia...lakini ooh, jinamizi likavamia maisha yetu, balaa ikatuvamia,..kisirani kikatuvamia...furaha, amani..upendo vikapotea...’akasema

'Lakini mzee kwanini ikatokea hivyo...?' nikamuuliza nikipoona anazidi kulalamika tu, kwani nilivyosikia kwa watu ni kuwa jamaa huyo utajiri wake ulikuwa unahusishwa na taasisi hiyo inayojulikana sana duniani....ya freemason.
'Lakini mzee mimi nimesikia kuwa wewe ni mwanachama wa taasisi ya frimasoni, ila ulikiuka masharti...'
'Wengi wanasema hivyo, lakini kiukweli hawafahamu kitu....' akasema.

Na jamaa yangu akanifinya na kuninong'onezea sikioni, akisema;

'Alikuwa frimason huyo, asikudanganye, kakiuka mashart, ndio maana kafirisika,...'

'Mke wangu alinikimbia, nilimpenda sana, alinikimbia na mtoto wangu kipenzi changu, ua la moyo wangu nikabakia mkiwa, hata sijui wameenda wapi, angalau ningejua wamekufa, angalau ningejua wamekimbilia wapi, lakini hata fununu hakuna,....’akasema kwa uchungu

'Siku wameondoka nilitaka kujiua....nililia usiku kucha, na niliendelea hivyo hadi mwaka ukapita...nikawa sina machozi tena, ikabakia kulia moyoni...' akasema kwa uchungu

‘Najiuliza kwanini...umasikini sio kilema,...eti ukiwa masikini hutakiwi kuwa na mke,  wangapi ni masikini lakini wanaishi mtu na mke wake, ...ina maana mimi kuwa masikini ndio wanikimbie...’akasema kwa uchungu.

'Samahani mzee unaweza kunisimulia ilivyokuwa, kwanini ulipanda kuwa tajiri na baadaye ukashuka kuwa masikini kwa kiasi hicho kikubwa...' nikamuuliza.

‘Mengi nilikuwa siyajui,...kwani nilikuwa nimetekwa na anasa, nimetekwa na ile hali ya utajiri,..nikajua mimi ndio mimi, utajiri huo ni kwa ujanja wangu,...lakini baadaye nilikuja kutambua kuwa utajiri huo ulikuwa sio kwa ujanja wangu...’akasema

‘Ina maana utajiri huo ulitokana na nini...?’ nikamuuliza, na mwenzagu akanifinya na kusema unasikia

‘Huwezi amini, hata mimi sikuwa naamini hivyo, maana nimesoma, unajua mimi maisha yangu mengi yalikuwa ulaya, nilikulia huko nikasomea huko, nilikuja huku nikiwa mkubwa tu, ndio nikawekeza...’akasema
‘Ila nilipokuja nilianzia chini sana.nilikuwa mtu wa kawaida tu, biashara ndogo ndogo, nikawekeza..huwezi amini hilo, nilianza na wafanyakazi wachache ambao nilikuwa nawalipa mshahara midogo sana, kutokana na kipato, na tulipanda tukiwa nao...’akasema

‘Walirizika na kipato chao.., na nilikuwa nao, kuanzia naanza biashara hadi nakuwa tajiri, na sikuwa nawalipa mishahara mikubwa sana kiukweli, walikuwa hawana makuu, hata nilipofikia kuwaajiri wazungu, wafanyakazi waliosoma,, mishahara yao haikuwa mikubwa sana...’akasema

‘Ni kweli ilibidi niwaajiri mameneja utawala,...mameneja fedha, masoko, na nikawa nawalipa mapesa mengi tu, lakini hawa nilioanza nao,...aah, sikuwakumbuka tena...unajua..’akasema

‘Sijakuelewa, kwanini ikawa hivyo, wakati mulianza pamoja, na ungeliweza kuwaendeleza,...?’ nikamuuliza

‘Ukitaka uyafahamu hayo, inabidi nianza kukusimulia maisha yangu toka mbali....ili uje kuoana kuwa kumbe utajiri wangu haukuwa ni ujanja wangu,...utajiri huo niliupata kwa kupitia kwa watu ambao hata sikuwathamini, , ...mungu alinipatia utajiri huo kwa vile nilikuwa na hao watu, ...’akasema

‘Mhh, hata sikuelewi,labda unisimulia ilivyokuwa ...kama hutojali....’akasema na mwenzangu akanifinya akiniambia tuondoke

‘Unajiingiza hivyo..’akasema huyo rafiki yangu

‘Hutaweza kuamini hayo mpaka na wewe ya kukute, kwani hata mimi sikuamini hayo hata sasa inaniwia vigumu kuamini...,kuwa kumbe kweli,..usije ukajiona wewe ni tajiri, ukajisifu, ukawazarau wale uliokuwa nao,...huwezi kujua kuwa kumbe utajiri huo ni kutokana na wao

‘Unajua nilikuja kuyafahamu hayo, wakati nimeshafirisika, wakati sina kitu, wakati mke keshanikimbia wakati nilipoiona barua ya mke wangu ikielezea kilakitu, niliumia sana,....' akatulia.

Ndio maana nimeamini kuwa riziki mtoaji ni mungu, mambo mengine, ni sababu tu, na riziki unaweza kuipata kwa kupitia mtu mwingine usiyemthamini kabisa, usiyemtegemea kabisa, unayemdharau tu, na kumuona si chochote kwako, kwanza hana hadhi kuishi na wewe,....

‘Kiukweli nimegundua kitu, hata siku moja riziki haigombaniwi., kuwa wewe ni mjanja sana, utaipata riziki kwa ujanja wako,kuwa wewe utashindana na wengine upate zaidi,...utawadhulumu watu jasho lao,kiujanja ujanja ili upate zaidi,... ‘akatulia

‘Ndio ni kweli, kwa muda huo utapata uteneemeka , utajijenga, utakuwa kama nilivyokuwa mimi,majumba ya kifahari, magari...,lakini itafika muda riziki hiyo itakukimbia...’akasema

‘Maana wewe si utajiona wewe ni mjanja,...wewe unapata kwa ujanja wako, kumbe sio, kuna jinsi fulani mungu anakua hiyo riziki, .....huwezi kujua na huwezi kuelewa, inaweza kuna sababu, kuna mtu, mungu aliyemuweka hapo ili iwe sababu ya riziki yako huwezi kumjua, anaweza akawa mtu hohehahe tu, mtu usiyemjali tu, na hata huyo mtu hajijua kuwa ndiye sababu ya riziki yako, huwezi amini hilo, hata mimi sikuamini hilo..,' akasema.

‘Huwezi amini hilo, kamanilivyokuwa siamini mimi,maana nimesoma, mimi ni mjanja, ...utaniambia nini,ila kiukweli, nikuambie kitu...hata siku moja 'Riziki haigombwi.....' akasema.

‘Riziki haigombwi, kwa vipi....?’ nikamuuliza

‘Nitakusimulia kisa cha maisha yangu, lakini kwanza nina njaa....’akasema

NB: Huo ni utangulizi wa kisa kipya, ambacho nitakuwa nikItoa ndogo ndogo kwenye facebook, lakini kwa marefu na mapana utakipata kwenye blog, ndani ya diary yangu....na hili ni kutokana na maombi ya wapendwa wengi, kuwa pia sasa niwe natoa visa moja kwa moja kupitia hapa FACEBOOK, mnasemaje?

Najua wapendwa mpo tayari na mimi, ili nijua hayo, naomba mlike diary yangu,.....

Ni mimi: emu-three

No comments :