Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, September 28, 2015

RADHI YA WAZAZI-44


Bro, unajua mimi nilipoteza fahamu siku tatu,...nikiwa kama mfu, maana nilikuwa sijijui,kabisa ..’akaanza kusema Profesa.

‘Siku tatu, unasema ulikuwa kama mfu,..halafu ukafufukaje..!?’ akauliza kaka mtu

Kisa kinaendelea...

*********

‘Ni siku ile alipokuja wakili nikiwa nimelazwa hospitali, akiwa na wazo la kutaka mimi kurudishwa huku kwetu...alipoondoka kumuita dakitari , mimi huku nyuma, hali ilizidi kuwa mbaya, nikapoteza fahamu....’akasema

‘Ndio ulisema hivyo,....sasa ikawaje..?’ akauliza kaka mtu

‘Unajua pale mwanzoni alipokuwa akinielezea makusudio yake alidhania kuwa huenda nimedhira kuongea naye, kwani alishaambiwa na docta kuhusu hali yangu...kiukweli kutokana na hasira, masononeko, shinikizo la damu lilikuwa limepanda juu,nikawa nakufa kisabuni, maana ndani kwa ndani hali yangu ilikuwa mbaya,...’akasema

‘Mhh....’akaguna kaka mtu

‘Na ndipo alipoondoka tu, nikapoteza fahamu, na nilipozindukana na kuweza kutoa kauli kwa mara ya kwanza tangu hali hiyo itokee ni siku nimeshafika hapa nyumbani, ...’akasema

‘Sasa aah.....  siku ile, kama hali ilikuwa mbaya kiasi hicho kwanini,hukumwambia yule wakili maana alikuwa ni wakili wako au sio?’ akaulizwa

‘Ni wakili wangu ndio, na ndiye aliyetakiwa kunisaidia, lakini kwa jinsi nilivyokuwa nimekasirika,...siku ile sikutaka kuongea naye kabisa, niliona wananipotezea muda wangu tu huku mimi naumia,...bro, niliteseka sana jela, hakuna maelezo nitakayokuambia yaweze kuelezea hiyo hali,.. hata hivyo japo nilidhamiria hivyo, lakini ilipofikia nahisi kufa kufa, nilitaka nimuelezea kuwa hali imekuwa mbaya, hapo nilishindwa kabisa, sikuweza kuongea tena kiukweli....’akasema

‘Sasa ikawaje...?’ akaulizwa

‘Kwa vile lengo lao lilikuwa mimi niondolewe hapo nchini haraka iwezekanavyo,walitafuta kila hila...ningelikufa ingelikuwa ni aheri kwao wangelitimiza dhamira yao,lakini wakakuta sifi, maana hali kama hiyo ilishatokea mara nyingi, ...’akasema

‘Hali gani..?’ akauliza kaka mtu

‘Hali hiyo ya kupoteza fahamu, nakuwa kama mtu anataka kukata roho,....lakini baadaye wanakuta mimi bado nipo hai, kwahiyo walishachoka, ...na wasingeliweza kuniua...’akasema

‘Kwanini sasa..., unasema walishindwa kukuua?’ akauliza kaka mtu

‘We acha tu, ...bro, binadamu ni mtu wa ajabu sana, akiwa na malengo yake, atatafuta kila mbinu, bila kujali kuwa na yeye ni binadamu tu...hayo anayoyataka kuyapata kwa njia ya dhuluma, ni masilahi ya muda tu, ipo siku na yeye yatamkuta, atayaacha tu....hapo kulikuwa na ajenda ya siri, na walishajua kuwa mimi nikipata mwanya tu, nitawaumbua....lakini mungu anajua,...mimi nilikuwa mnyonge, sina wa kunisaidia, ningelifanya nini...’akasema kwa sauti ya unyonge.

‘Mhh, sasa ilikuwaje...?’ akauliza kaka mtu

‘Nikasafirishwa kiaina, kurudishwa huku kwetu....’akasema

‘Mhh, sasa aaah, mimi hapo sielewi, ulisafirishwaje ukiwa huna fahamu,.?’ akaulizwa

‘Bro, wajanja hawashindwi kitu, walifanya walichofanya nikajikuta nipo bongo ...’akasema

‘Walifanyaje sasa..??, walikubeba kwenye jeneza...’akasema

‘Walinifanya kama msukule....’akasema mdogo mtu huku akicheka kama mdhaha

‘Hahaha,...sasa wewe unachelewesha tu, hebu elezea kitu kinacheleweka,  ina maana hata wazungu nao ni wachawi.....?’ akauliza kaka mtu.

‘Walipojua kuwa mimi nipo hai, ni nguvu tu sinam walinidunga sindano ya kuongeza nguvu, hali ile ya kupoteza fahamu, kuzindukana ilikuwa inakuja mara kwa mara...wakaona isiwe taabu,...wakanipiga hiyo sindano...’akasema

‘Mhh, ipoje hiyo...?’ akauliza

‘Ni ya kuongeza nguvu, kwa muda....’akasema

‘Ina maana hata wenzetu wanaweza kuwa na roho mbaya kihivyo...?’ akauliza kaka mtu

‘Nimekuambia watu wakitaka jambo lao liwe, wanajisahau kuwa na wao ni binadamu tu,,...kuna mambo walitaka kuyafukia, na mimi ningekufa ingesaidia, ....lakini ikwa mimi sifi, na wakaona isiwe taabu, kufa nitakufa tu, lakini lini, na je kama nikiweza kuongea, watu wa habari, au..’akasema na kukatisha akikohoa.

‘Njia gani hiyo, kwani wangetaka si wangekuua tu, una nini wewe , wewe ni nani mpaka wasumbuke hivyo...?’ akaulizwa kaka mtu sasa akimtizama mdogo wake kama yupo salama kwani alikohoa mfulululizo.

‘Bro, sheria ipo, na sheria inaogopewa, sema watu ni kutikisa kibiriti tu, hata uwe nani, ukijua kuna sheria inakubana, hata ukifanya makosa bado moyo utakusuta, utakuwa na mashaka...kuna watu wanafuatilia sana mambo hayo,...usione hivyo, hata kama mimi sio kitu, lakini watu wanatafuta visababu vidogo tu, kuangushana hasa kisiasa.....’akasema

‘Sasa ilikuwaje...na je inaruhusiwa?’ akauliza kaka mtu

‘Kuruhusiwa kwa vipi?’ akauliza Profesa

‘Yaani mgonjwa kuchukuliwa katika hiyo hali uliyokuwa nayo?’ akaulizwa

‘Hilo mimi sijui, ..ninachojua na ndivyo ninavyohisi walifanya hivyo, wakitaka mambo yao yawaendee vizuri,...’akasema profesa

‘Akina nani, maana hapo nahisi walichoogopa labda ni gharama za kukusafirisha ukiwa maiti...au, hebu elezea ilivyokuwa...’.akasema kaka mtu.

‘Hivyo ndivyo ilitakiwa ionekane hivyo, lakini kiundani kulikuwa na ajenda ya siri,...ukiangalia mlolongo mnzima wa hiyo kesi, hadi kushikwa mimi, ....kuna mambo mengi yemejificha hapo, kwani mpaka naondoka bado muuaji halisi alikuwa hajapatikana....’akasema

‘Si ulisema alishapatikana, ...au alikuwa sio yeye?’ akauliza kaka mtu

‘Alikuwa ndio yeye kwa kushukiwa tu, .. lakini ilikuwa haijathibitishwa mbele ya mahakama kuwa muuaji ni nani, jinsi walivyoshukuwa hao watu wawili ni kama nilivyoshukiwa mimi tu,...lakini je walikuwa ndio wauwaji, kweli, na huyo mtu wa pili alikuwa ni nani...’akasema profesa

‘Sasa muuaji alikuwa nani....?’ akauliza kaka mtu.

‘Mimi nilishaondoka huko,..wao walitaka mimi niondoke huko mapema maana kukaa kwangu huko kungelifichua mambo mengi...hasa kama hao watu wanaoitwa wa haki za binadamu wangeliingilia kati, najua wangelidadisi kutaka kujua zaidi, na hapo bomu lingewalipukia...’akasema

‘Haya tuyaache hayo, hebu niambie wewe ilikuwaje hadi ukafika huku kwenu..?’ akauliza kaka mtu.

‘Ili uelewe vyema turudi siku ile pale alipoondoka wakili kumuita dakitari , alipoondoka mimi huku nyuma nikapoteza fahamu kabisa,nilishakuambia hilo ...., kwahiyo dakitari alipokuja, sikumuona, na sikuwa na ufahamu ni nini walikifanya kujaribu kunizindua,....najua watakuwa walifanya hivyo,  lakini ilishindikana, wakajua labda ndio kwaheri, muda wakakuta nacjezesha mkono...’akasema

‘Hayo uliyajuaje, ni nani alikuja kukusimulia hayo ya huko, wakati ulishaondoka, na unasema ulikuwa hauna fahamu...?’ akauliza kaka mtu

‘Haya nilikuja kuambiwa ni hao watu walionisindikiza kunileta huku..’akasema

‘Ina maana ilibidi usindikizwe na watu wao, au ni akina nani hao walikusindikiza, na ulipata wapi mwanya wa kuwauliza,?’ akauliza

‘Ni watu wao wa usalama,...kama nilivyosema ilibidi kuwe na watu wawili ambao walikuwa kiegemeo wakati naletwam wanakuwa pande zangu mbili, ili nisije kudondoka...na watu hao walipewa kazi ya kuhakikisha nimefikishwa nchini kwangu na kuandikisha maelezo yangu....’akasema

‘Maelezo gani sasa...?’ akauliza kaka mtu

‘Maelezo..! ni lazima kuwe na melezo ya kuejeshwa kwagu huku nyumbani nikiwa mgonjwa,...’akasema

‘Sasa waliandikaje...?’ akauliza

‘Waliandika kuwa mimi ni mhalifu wa biashara za mlungula, na pia nilikuwa kule kinyume na sheria, na nikawa najishughulisha na matendo kinyume na sheria za nchi hiyo,...nilihukumiwa kufungwa, lakini kutokana na hali ya kiafya kama ilivyoonyeshwa na dakitari wameona waniwahishe huku.....blablabla...’akasema

‘Najiuliza sheria inasemaje kuhusu hilo....inakubalika kweli, watu wa huku kwetu hawakulihoji hilo...?’ akauliza kaka mtu

‘Walihoji hilo, wawahoji wazungu,...lakini ndio hivyo, mimi sijui....ninachofurahi ni kuwa nimerudi nyumbani na najua dawa zangu za kienyeji zitaniponyesha tu, si unaona sasa hivi nimeshaanza kuonekana binadamu...japokuwa bado natisha....’akasema akiendelea kujiangalia.

‘Sasa hao watu waliokusindikiza walikusimuliaje, na wewe ulisema ulikuwa unasikia tu, ...?’ akauliza

‘Ndio,...wakati napelekwa hospitali ya hapa.nilipata nafuu nikaweza kuongea kidogo, nikamuuliza  huyo jamaa mmoja ilikuwaje, ndio akanielezea kwa haraka,...namfahamu sana huyo jamaa....’akasema

‘Alikusindikiza hadi hospitalini, au alikusimulia wapi?’ akauliza

‘Walifanya hivyo ndio, walinisindikiza hadi pale nilipofikishwa hospitali, kuhakikisha wanaondoka kila kitu kikiwa kama walivyotaka wao, wasije kuonekana walipanga kwa nia mbaya....’akasema

‘Mhh, ....alikuambiaje...?’ akauliza

************

'Turejee siku ile nilipopoteza fahamu, pale hospitalini.....'

'Wakati wakiwa wanaulizana wafenye nini, hapo fahamu ikanirejea, lakini mwili haukuwa na nguvu kabisa....hapo tupo sawa..?.’akaanza kuelezea mdogo mtu sasa akielezea mkasa mzima.

‘Fahamu zilinirejea kwa namna ambayo siwezi kujiinua, naona, nasikia lakini siwezi kujibu kitu, mwili ulikuwa kama sio wangu, akili tu ndio inafanyakazi....

‘Huyu mtu kapooza mwili mzima, hapa alipo ni kama mzigo tu....’akasema dakitari, nilimsikia na kiukweli sikuipenda hiyo kauli yake lakini sikuweza kumjibu.

‘Kwa hali kama hiyo tunaweza kumsafirisha kumrejesha huko kwao....?’ akauliza mtu mwingine sikuweza kumfahamu maana alikuwa kwa pembeni.

‘Inawezekana lakini mhh ...au mnatakaje...’akasema dakitari  wakawa wanaongea kwa sauti nisiyoisikia, na baadaye dakitari akatikisa kichwa kama kukubali.

‘Kwahiyo inawezekana,mkitaka iwe hivyo, lakini, sijui maana si mumesema huyu mtu ana kesi ya kujibu, hakimu kalirizia hilo ...?’ dakitari akauliza akionyesha mashaka.

‘Hakimu kaizinisha, huyu mtu arudishwe kwao,...ili kukwepa gharama hasa kutokana na hii hali yake...’sauti ikasema

‘Unajua docta, kama ulivyosema , kuendelea kumfunga huyu mtu hali yake itazidi kuwa mbaya, basi maelezo hayo yalisaidia hakimu kukubali, maana kama unavyoona, ina maana itabidi kila muda awe analetwa huku hospitalini au sio,...sasa tunachotaka huyu mtu asifie huku kwetu...’sauti ikasema

‘Kwahiyo mnatakaje....?’ akauliza na maneno waliyokuwa wakiongea sikuyasikia, ila docta baadaye akasema

‘Kama mnataka hivyo, Inawezekana tutaona jinsi gani ya kufanya...’sauti ikasema

*******

 Profesa aliandaliwa na kweli ikaja nguvu ya aina yake, akaweza hata kukaa, lakini cha ajabu, pamja na nguvu hiyo kurejea, lakini profesa hakuweza kuongea, aliweza kuona kinachoendelea, na kusikia tu, na kwa msaada wa watu aliweza kusimama, akaweza kutembezwa akiwa kashikiliwa huku na huku, na hata wakati anaingizwa kwenye gari, kupelekwa uwanja wa ndege aliweza kufahamu hayo yote , lakini kila mara kulikuwa na watu wawili wakumsaidia kushoto na kulia, ili asije kuanguka.

‘Nilikuwa naona, nasikia, lakini siwezi kutamka kitu, nilikuwa kama bubu, mdomo haufunguki,...mwili unaweza kutembea kwa msaada wa mtu huku na huku, unafikishwa kwenye kiti unakaa kama kawaida, ila ni lazima kuwe na mtu wa kukuzuia huku, na huku, ili kukitokea mtikisiko usiangukie upande mwingine....’akasema profesa

‘Nilifikishwa kwenye ndege nikitembea, kwa msaada wa watu huku na huku walihakikisha sianguki, ila ionekane nipo hai, nipo mnzima, ni kuchoka tu ...na hao watu wawili ndio nilikuja nao hadi huku nyumbani...’akasema profesa

Ndani ya ndege nilipigwa sindano nyingine nahisi ni ya kuniongeza nguvu, na hadi tunafika hapa nchini, bado nilikuwa na zile nguvu za kuongezewa, na nikakabidhiwa kwa watu wa usalama wa huku, na ikatakiwa kuwahishwa hospitalini haraka,...’akasema

‘Huyu mtu ni mgonjwa, ni muhimu afikishwe hospitalini....’wakasema, waliongea walichoongea, na kweli nikachukuliwa na gari la wagonjwa, kuelekea hospitalini na tukiwa njiani ndio nikaweza kuongea, na kumuuliza mtu aliyenisindikiza, kwanza hakuamini, halafu alipoona kweli nimezindukana vyema, akanisimulia ilivyokuwa

‘Alinisimulia kwa haraka, ....nikawa nasikia tu...aliniambia kuwa yeye alitakiwa aondoke kesho kurudi kwao lakini kwanza alitakiwa kuhakikisha kuwa nimefikishwa hospitalini,...ili kutoa maagizo kwa dakitari atakeyanipokea’

‘Maagizo,..maagizo gani hayo.....’akazidi kusema

Profesa alifikishwa hospitalini na kukabidhiwa kwa dakitari, haikuchukua muda profesa akapoteza fahamu...

Profesa alilazwa hapo hospitalini wiki nzima, kabla hajaweza kujitambua vyema na alipojitambua ndio akawaomba madocta wajaribu kuulizia kuhusu ndugu zake,  ndio ukafanywa utaratibu hadi kaka yake akapatikana, ....

‘Bro ndio ilivyokuwa hivyo...’akasema akimuangalia kaka yake.

‘Sasa vipi kuhusu huyo kijana wetu...?’ akauliza kaka mtu.

***********

‘Bro mimi hata sitakia kusikia, kuhusu huyo mtoto wako,  na kwa angalizo bro...nakuonya uachane kabisa na huyo mtoto...’akasema

‘Kwanini unasema hivyo...?’ akauliza kaka mtu

‘Kutokana na msimamo wake, nina uhakika kama atarudi hapa mkaonana naye, atakutia hasira na itakuwa ndio mwanzo wa kuchukiana kabisa na yeye...’akaambiwa

‘Mimi sina haja naye, ...kama amekwisha kusema hana baba, baba yake alikufa, basi...ila kinachoniuma ni huyo mama yake maana kila mara nikikutana na ndugu za huyo mama ninachoulizwa ni hicho,wanasema huyo mama sasa hivi kawa kama kachanganyikiwa kisa ni huyo mtoto, sijui kwanini hamsahau, yeye anadai mtoto wake yupo hai, lakini mbinu zimefanywa ili asimuone....’akasema na Profesa akatikisa kichwa kwa kusikitika, halafu akasema;

‘Inaniuma sana, najuta kwanini nilifanya hivyo, wakati nayafanya hayoo nilijua natenda jambo jema, kuwa nitamsaidia huyo mtoto, apate elimu, na mimi hapo hapo ndio nikapata mwanya wa kutokea, ...nisaidie na mimi nifaidikie  sikujua haya yote yanaweza kutokea....’akasema

‘Ndio hivyo umeniharibia mwanangu kwa tamaa zako, na hivi sasa utafanyaje, maana..majuto ni mjukuu....hebu fikiria kama ni mtoto wake angefanyiwa hivyo ungelifanyaje...’akasema kaka mtu.

‘Lakini hata mimi ni damu yangu, ...nilifanya kile nilichoona ni sahihi kwa wakati huo,...mfano kama mambo yangekuwa mazuri, akawatambua nyie, ...faida ingelikuwa kwa nani, tatizo ni kuwa amekataa kuwatambua au sio...’akasema

‘Nikutokana na malezi uliyomlelea, wewe umeishi maisha hayo ya utapeli, mali na pesa ipo mbele zaidi ya utu,...hiyo ni tabia mbaya sana, ...nakufahamu sana bwana mdogo, tokea ukiwa mtoto, ...lakini tuyaache hayo, wewe jitahidi ufuate masharti usije kujiona umepona...’akaambiwa na kaka mtu.

‘Nitajitahidi sana, na nataka nianze ile biashara yangu ya madawa, nikipata nafuu nitakwenda mjini, kuangalia soko langu...’akasema

‘Huko pasahau,..maana ukienda huko utataka kuiona nyumba, na itakutia hasira...mimi ningekushauri uweke akili yako kwenye kutunza afya yako....’akaambiwa

‘Ni lazima nikaione hiyo nyumba, na ...sijui. bro.....labda mungu asinipe uzima,..mhh, sijui....’akasema

‘Utafanya nini wewe, nyumba utakufa nayo, unanishangaza kweli...?’ akaulizwa kaka mtu akimuangalia ndugu yake kwa jicho la dharau, akitabasamu.

‘Ile ni haki yangu bro, wematumia mbinu kuniibia...lakini ngoja nipone,...na ole wao,,nipate afya njema, nipate nguvu, bro, usinione nipo hivi, ,...'akasema

'Utafanya nini na hiyo hali, hivi hujioni eeh...?' akauliza kaka mtu

'Mhh, nitafanya nini,...wao waombee tu nife,...lakini kama mungu atanipa afya angalau kidogo..., nikarudi kwenye hali nzuri, bro, utayasikia mambo yangu, ile nyumba itarudi.....mimi sio profesa wa bure bro, nafahamu mambo ambayo wewe huyajui..'akasema

'Ya uchawi...?' akauliza kwa dharau

'Kinachoniuma ni kuwa ile nyumba nilijenga kwa jasho langu, halafu watu waje waichukue kilaini tu, hivi hivi, hata sikubali...nitaizungukia kwa udi na uvumba....’akasema akijiinua pale alipokuwa amekaa, akasimama, kaka mtu akamuangalia akitabasamu

‘Haya bwana, ....nakujua ulivyo, unapenda sana ligi, mwili wenyewe upo wapi, ni maneno tu. Yamebakia sahau, wajanja wameshakuzidi...utarudi ukapambane na mama mtemi, au....wewe, kubali tu yaishe..’akasema kaka mtu

Na mara mlango ukagongwa, akaja mgeni, wakasalamiana, na huyo mgenii akasema katokea mjini

‘Umetokea mjini....?’ akasema kaka mtu akisalimiana na huyo mgeni

‘Ndio nilikwenda kuchukua mzigo...’akasema

‘Kuna nini huko mjini...cha zaidi?’ akaulizwa

‘Hakuna cha zaidi...mambo ni ya yale yale, kampeni za kisiasa...si unajua tena, vipi mgonjwa wetu anaendeleaje, maana naona uzima unaanza kurejea, kweli binadamu wa ajabu, mimi nilijua ni maandalizi tu ya kuzika,..’akasema akigeuka kumuangalia mgonjwa, na Profesa akacheka

‘Sifi bwana, mtakufa nyie kwanza....’akasema kiutani

‘Kweli wewe una roho ya paka...’akasema mgeni

‘We acha tu cha moto nimekiona...hata mimi hapa nilipo siamini kuwa bado nipo hai....’akasema  na huyo mgeni akawa kama anakumbuka kitu akasema

‘Hivi ile nyumba yako,mjini  uliiuza...au?’ akauliza huyo mgeni na ndugu hawa wawili wakaangaliana, na baadaye kumuangalia huyo mgeni kwa macho ya udadidi na Profesa akawa wa kwanza kutamka neno

‘Kwanini unasema hivyo...?’ akauliza profesa

‘Mhh,...nimepita pale sikuweza kuitambua tena,imezungushiwa mabati, nahisi...kuna matengenezo yanaendelea humo ndani, ...’akasema

‘Oh, hata sijui....’akasema kaka mtu akitikisa kichwa na huyo mgeni akageuka kuondoka akasema

‘Jamani mimi sikai nilikuja kumuona mgonjwa mara moja mimi naondoka...’akasema na kuondoka zake.

‘Ngoja nipone...ngoja nipone...tutaona.’akasema Profesa akitikisa kichwa

Kaka mtu akamtizama mdogo mtu  kama kutaka kuuliza kitu, lakini akamuona mdogo wake kainama , akajua mdogo wake huyo sasa roho inaanza kumuuma, na akajua sasa kuna vita nyingine inakuja huko mbele...

NB: Profesa karudi nyumbani, ni nini kitaendelea huku, na huko je ilikuwaje...na ni vipi hiyo radhi ya wazazi ikaja kutokea...tuzidi kuwepo kwenye hitimisho la kisa hiki.....

WAZO LA LEO: Roho inauma pale unapokikosa kitu, hasa kama kilikuwa chako na sasa kimechukuliwa na mtu mwingine kwasababu mbali mbali..... , kama ilivyo kukosana kwenye ndoa, ukaacha mke, na mke akaja kuolewa na mtu mwingine na ukaja kukutana naye na kumuona kawa mnzuri zaidi...moyoni utaumiaje...thamani ya kitu inaonekana pale unapokikosa.
Ni mimi: emu-three

No comments :