Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, September 7, 2015

RADHI YA WAZAZI-39


‘Hamna cha wakili mnzuri hapo ushahidi upo wazi, yeye ndiye kaua, kutokana na vielelezo tulivyo navyo,  ....’akasema muendesha mashitaka

‘Ukiangalia video inaonyesha wazi, anaonekana mshitakiwa akiwa anakimbia akiwa na silaha,kwanini akimbie, ndilo swali la kujiuliza hapa, na anakimbia akiwa kashikilia hiyo silaha...hapo hana sehemu ya kuokokea, hata akiwa na wakili mnzuri,...

‘Na mara nyingi kama silaha ina alama za vidole za mtuhumiwa, ni ushahidi wa kutosha wa kumtia mtu hatiani, labda ithibitike kuwa alishikishwa, kwahiyo huo kwetu ni ushaidi muhimu unathibitisha na kuhalalisha kuwa huyo mshitakiwa ndiye muuaji, sasa mnataka ninii zaidi....’akasema. muendesha mashitaka wakiwa wanajadiliana na wenzake

‘Lakini hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa ndiye aliyefyatua risasi, yeye mshitakiwa anadai alipigwa na kitu kichwani akapoteza fahamu na kweli jereha linaonekana kichwani,..hatuwezi kusema kajipiga mwenyewe ili kuharibu ushahidi,...sehemu kama ile mtu huwezi kujipiga mwenyewe,....’akasema mpelelezi.

‘Yah....’akasema muendesha mashitaka

‘Na pia anasema alipozindukana alikuwa kachanganyikiwa, ...., akaiona hiyo silaha karibu yake, kwa kutaharuki akaichukua na kukimbia nayo....’akasema mkuu kuongezea

‘Hapo unaweza kusema anajitetea tu, na hoja kama hiyo ni ya kufundishwa na huyo wakili wake,...japokuwa kweli ana jeraha kichwani,..labda alipigwa na marehemu wakati wanapambana, labda alipigwa na mtu mwingine baada ya kutoka hapo....’akasema mpelelezi.

‘Na labda tungesema huenda alipigwa na marehemu wakipambana, lakini kwenye eneo la tukio  hakukuwa na dalili za watu kupambana, tumechunguza hilo...inaonyesha muuaji, alifika na kumpiga marehemu risasi, bila hata maehemu kujitetea, ni mauaji ya dhahiri ....’akasema mpelelezi

‘Ana jeraha kichwani, lakini hakuna dalili ya kuwa walipigana na marehemu,....hapa inamaanisha nini.....’akasema mkuu aliyekuwa akiwasikiliza.

‘Hapa ina maana kulikuwa na mtu wa tatu, na huyo mtu wa tatu anaweza kuwa ndiye muuaji,...sasa huyu mtu wa tatu ni nani.....’akasema mpelelezi.

‘Kwahiyo kazi yote uliyofanya ni bure, inabidi kumtafuta muuaji, au...?’ akauliza mkuu

‘Sio bure, hapa tukithibitisha kuwa yeye sio muuaji, yaani mshitakiwa, tunaangalia njia nyingine ya kumpata muuaji, na atapatikana tu, kama sio huyu mshitakiwa , akiatikana ni kiasi cha kuunganisha ushahidi na huyo muuaji mpya, matendo na sababu ni zile zile...’akasema mpelelezi

‘Yaweza kuwa tofauti, kutegemeana na mtu mwenyewe, huenda katumwa tu kuua,...muuaji wa kukodiwa,.....na hapa tunacheza na muda...’akasema muendesha mashitaka

‘Ok,...tusipoteze muda, mimi naona tuanzie kwenye orodha ya majina ya watu walioingia pale kwenye jengo siku ile..., maana hapa ndipo wakili wao, alipoweza kukushika shati wakili,.....ilikuwaje kwenye saa zisiendane, na kuonekana kama zimebadilishwa, maana hapa yaonyesha kabisa kuna jamboo limefanyika,.....’akauliza mkuu.

‘Tulipowauliza wahudumu waliokuwepo, walisema mara nyingi, yule mtu anayeingia ndiye anayeandika saa , na wao huwa makini kuthibitisha hilo kuangalia kama kweli aliyeandika kaandika muda sahihi, lakini wakati mwingine kuna kupitiwa...’akasema mpelelezi.

‘Kwahiyo kweli, hakuna aliyejaribu kubadili mtiririko wa saa kwa makusudi..?’ akauliza muendesha mashitaka

‘Hakuna,....saa hizo waliandika wenyewe watu walioingia, na hata tulipowaonyesha wale walinzi waliokuwepo hao mapokezi wakisimamia hilo, walishangaa, hawakuwa wameligundua hilo kabla....’akasema

‘Yawezekana hili limefanywa kwa makusudi, au huyu wakili mtetezi, asije akawa kafanya ....’akasema mkuu na kukatiza

‘Hapana , wakili huyo hajafanya kitu, maana kama ingekuwa kumebadilishwa ungeooana, hakuna dalili kama hizo...’akasema mpelelezi.

‘Sasa ni nani kafanya hivyo...maana mshitakiwa hawezi kufanya hivyo, ukiangalia yeye kaandika sawa tu, tofauti kidogo na mtu wa juu yake,...angekuwa kaweka saa tofauti na mtu wa juu yake, kama walivyofanya hao waliopotosha saa tungesema ni yeye....’akatulia mpelelezi kama kagundua kitu

‘Hapa tuwaangalia hawa watu wa juu, hawa watu watano, walioleta tofauti ya saa, ni akina nani....hawa wanaweza kuwa na sababu...ni nani hawa watu....?’ akauliza

‘Mmoja ni kijana wetu, na yupo kijana mwingine walikuwa naye....’akasema

‘Kijana wenu! Ni nani huyo...?’ Na, ina maana mlikuwa na mtu humo, wakufuatilia au ilikuwaje mbona hujaniambia hilo....?’ akauliza muendesha mashitaka na mkuu naye akawa kama ndio kwanza anasikia hiyo taarifa

‘Siku ya kuchukua huo mzigo ambao ni pesa, hatukuwa na uhakika ni saa ngapi,au ni wapi....na hatukuwa na uhakika kuwa watatumia jengo hilo, mwanzoni walipanga kuwa huyo mpelekaji atapeleka hizo pesa kwa huyu marehemu, na kuna mtu atakuja kuzichukua....’akasema mpelelezi

‘Lakini wakaja kubadili, kuwa marehemu azipeleke kwenye hilo jengo, tatizo walipobadili hivyo, marehemu hakutupa taarifa kuwa kaambiwa apelike hizo pesa maeneo hayo....’akasema

‘Unahisi ni kwanini alifanya hivyo?’ akaulizwa

‘Hapo hatujui ni kwanini, maana alikubali kushirikiana nasi...’akasema mpelelezi

‘Yawezekana marehemu alishakuwa na mpango wake,..unajua alishafahamu kuwa huo mzigo una pesa,...kwahiyo huenda, alitaka kufanya awezevyo nay eye aambulie kitu....’akasema mkuu.

‘Hiyo yawezekana...maana wakati anaondoka hapo alimuaga mwenzake kuwa anakwenda kufanya dili.....’akasema

‘Dili, akiwa na maana gani?’ akauliza mkuu

‘Dili ni namna ya kuingiza pesa kwa mpango fulani, uwe wa kujadiliana au kibiashara,....’akasema

‘Mwenzako hakusema lolote, kama alifahamu ni dili gani na kama aliweza kuona ni kitu gani mwenzake aliondoka nacho....?’ akaulizwa

‘Mwenzake anasema kulikuwa na mzigo ,na mwenzake alipokea simu, ikimuelezea huo mzigo aupeleke wapi, na .....kwa vile yeye hashughuliki sana na mizigo ya kutoka nje, hakuwa makini ni kitu gani...’akasema

‘Huoni kwamba mwenzake ana kitu anaficha, maana pale mambo mengi yapo kimaandishi au sio....?’ akaulizwa

‘Ndio na ndizo taratibu zilivyo, lakini cha ajabu huo mzigo, haukuwa na kumbukumbu yoyote, kama ilivyo kawaida yao, mzigo unaandikishwa umetoka kwa nani, unakwenda kwa nani,...lakini mzigo huo ulikuwa ni wa maneno tu, fanya hivi, peleka hapa, na kwahiyo walikiuka taratibu, kisheria....’akasema mpelelezi.

‘Je marehemu alipofika kwenye hilo jengo alipoambiwa apelike huo mzigo, aliandikisha jina lake muda gani?’ akaulizwa

‘Cha ajabu basi marehemu hakuandikisha jina lake halisi.....na tulipowauliza walinzi, waliokuwepo, walisema kwa muda huo kulikuwa na watu wengi,...kulikuwa na hali ya msongamano , kila mtu akitaka kuwahi, kwahiyo hawakuwa makini sana,....

‘Sasa kilichotusaidia ni kamera, kamera ilionyesha marehemu akiandika jina lakini tulipoangalia hakukuwa na jina lake, ina maana aliandika jina la  uwongo....’akasema mpelelezi

‘Kwanini....?’ akauliza muendesha mashitaka

‘Angalia mtiririko wote huo,huko kazini, hawakufuata taratibu za huo  mzigo, ina maana alikuwa na ajenda fulani, ama kwa masilahi yake au kutokana na hao walivyomuelekeza...na huenda ndicho kilichosababisha kifo chake...’akasema mpelelezi

‘Ok, kwenye hiyo kamera, hakuna namna ya kunasa muda,...ni kamera ya namna gani, kwani nyingi unaweza ukafuatilia tukio, unapanga kwa masaa, kwa sehemu nk...hiyo kamera ipoje,...ili tujue hasa huyo mshitakiwa alifika saa ngapi.....?’ akauliza muendesha mashitaka.....

‘Kamera waliyoweka sio za kisasa, huyu mtu aliweka kamera ili tu kuonyesha kaweka kamera,...ni ya kizamani na kuukuu....tuliliangalia hilo tukio kwa utaalamu wote, lakini, hatujaweza kufanikiwa...’akasema mpelelezi


‘Kamera yake ni ile ya kuchukua tukio kama video tu, inaonyesha tuki kwa muendelezo, na huwezi kulichambua hilo tukio kwa saa, kwa eneo nk...tulijaribu kuingia ndani zaidi kuona kama tunaweza kupata ule mtiririko wa picha moja moja..lakini hatukuweza, maana hata mashine yenyewe ni mbovu....’akasema mpelelezi

‘Ni mbovu, lakini hilo jengo ni jipya, au sio, sasa Iliharibika kwa vipi,..iliharibika muda gani, au iliharibiwa makusudi...?’ akauliza mkuu

‘Inavyoonyesha ni kipindi marehemu akiandika,.... maana wakati anaandika utaona ile kamera ikicheza cheza, halafu, ikazima,....halafu ikawaka, halafu ikazima,...kukawa hakuonyeshi kitu, sasa toka hapo hadi watu kama ishirini hivi hakukuwa na picha yoyote....’akasema

‘Mhh....kwanini iharibike kipindi marehemu anaandikisha jina....hapa kuna sababu, ni nani anayesimamia huo mtambo, hawakujisajili idara ya usalama....?’ akauliza mkuu.

‘Kwa muda huo, mtambo huo ulikuwa unajiendesha wenyewe, ....huwa yule mtu wa kuhudumia huo mtambo, akisha uweka sawa, anaondoka, na kama kuna tatizo ndio anaitwa,....’akasema mpelelezi.

‘Lakini mtambo wao haukusajiliwa kwenye watu wa usalama kama wengi wanavyofanya, maana nijuavyo mitambo hii lazima iwe na uangalizi makaoni mwa ofisi za usalama kwao kama wana kampuni ya ulinzi au kwa usalama wa kipolisi,...?’ akaulizwa

‘Niliwauliza hilo swali, kwanini, wakasema ndio walikuwa mbioni kufanya hivyo, hata fomu wanazo walizokuwa wamejaza kwa ajili ya kujiunganisha kwenye usalama wa kipolisi...’ akasema mpelelezi

‘Kwahiyo sasa walikuwa wanatumiaje hiyo kamera, ipoje...?’ akauliza mkuu

‘Wao kamera yao ilikuwa humo kwa mumo,wana mtambo wao na unatumika humo humo ndani, na walinzi waliopo ni wafanyakazi wao, waliowaajiri kwa kazi hiyo, kwahiyo wanalipwa mshahara kama wafanyakazi wa kawaida...hawakukodi kamuni za usalama, ..ndio tatizo hapo...’akasema mpelelezi

‘Sasa huyo aliyekuwa akishughulika na hiyo mitambo, siku hiyo alikuwa wapi...?’ akauliza

‘Alitoka kama kawaida yake, huwa anakuja muda kwa muda, akihitajika, hasa mtambo ukileta matatizo,..na ilipotokea matatizo siku hiyo alipigiwa simu, lakini simu yake haikuwa hewani, hakupatikana mara moja, na baadaye yeye mwenyewe akapiga simu kwa kutumia namba tofauti akasema simu yake imeibiwa  ....’akasema

‘Je ni kweli hayo anayoyasema, kuwa aliibiwa simu,  maana mimi nimeshaanza kumuhisi vibaya...’akaulizwa

‘Ni kweli simu yake ilibiwa,....kuna ushahidi,... alipoibiwa alitoa taarifa kwa mawakala wa simu,...wakazuia takwimu zake,..na ni muda kabla ya muda wa haya matukio, na kumbe wakati anahangaika huko kutoa taarifa, na kupata line nyingine huku wanamtafuta...’akasema mpelelezi.

‘Hapa kuna jambo...huyu mtu tunahitajia kumweka chini ya ulinzi, nahisi anafahamu kitu,....nyie mnaonaje,... inawezekana huyu mtu kapangwa...’akasema mkuu

‘Na pia yawezekana kuwa huyo mtendaji, muuji, alijua kuwa huyu ndiye mtaalamu wa hapo, akamwibia simu yake, akijua hakutakuwa na mawasiliano, akaingia kwenye hilo jengo akaharibu mawasiliano ya kamera..lakini je yawezekana hilo, tukiangalia muda wa kufanya hayo yote....’akauliza muendesha mashitaka

‘Aliibiwa mitaa ya .....mmh, kweli hapo ni lazima kuwe na ushirikiano zaidi ya watu wawili, kwa minajili hiyo basi kulikuwa na mtu mwingine wa kufanya hayo, akiwa kwenye jengo, wakati huyo mwingine akiiba simu nk, ...’akasema mpelelezi

‘Mshitakiwa hawezi kuwa mshirika....?’ akauliza mkuu

‘Mshitakiwa?... Mimi naona kama hivyo,...niliona hivyo, lakini nitalipompekenyua zaidi,nikagundua kuwa huyo hana utaalamu wa hiyo mitambo.....’akasema mpelelezi

‘Kwa minajili hiyo, huyo mshirika awe na sifa ya utaalamu wa hiyo mitambo...ni nani tunaweza kumshuku, aliyewahi kuingia hapo mwenye utaalamu huo, hebu tuangelia katika  walioingia kabla ya marehemu, hata baada lakini wawe karibu na huo muda...’akasema mkuu

‘Tukiangalia kwa mshitakiwa, yeye alifika baadaye, kuna watu walikuwa wakimfuatilia, wanasema alifika hoteli ya karibu, akaingia na kutokea mlango wa nyuma, hawakuligundua hilo hadi walipoona muda umekwisha, wakawa wamempoteza na kumpata kwake ndio muda huo anakamatwa....’akasema mpelelezi.

‘Kwahiyo hao hawakuweza kutusaidia, ....eeh, hebu turudi kwenye hili dafutari la mapokezi..hawa watu watano,ni nani na nani....nahisi hapa tunaweza kupata kitu, hisia zangu zinanituma hivyo’ akasema mkuu

‘Mmoja ni kijana wetu, wengine hawa wawili ni wateja wa humo  humo,na wengine wawili....mmoja tumempata, ni mtu wa kuingia na kutoka, hana lolote,alifika kuuza bidhaa zake tu, na huyu mwingine hatujampata , jina ni geni...yawezekana hakuandika jina sahihi....’akasema mpelelezi

‘Na kamera ndio hiyo ilikuwa haifanyi kazi...huyu huyu, ambaye yaonekana aliandika jina bandia, ni nani...., walinzi wanasemaje kumuhusu yeye, hawana kumbukumbu yoyote ya kutusaidia...?’ akauliza mkuu na muendesha mashitaka akaongeza kwa kusema

‘Na je kamera za nje hazikuweza kunasa mtu wa kumshuku aliyeingia, tukiangalia kumbukumbu za watu wakorofi...?’ akauliza muendesha mashitaka akijikuna kwa kutumia kalama  kichwani

‘Unajua kamera hii nje  imenasa hao watu walioingia eneo hilo, lakini watu walioingia eneo hilo, kuelekea kwenye hilo jengo ni wengi sana...labda tungekuwa tunamuhisi mtu fulani, tungeliweza kumnasa kwa kumsearch--- kwa picha,  hilo lingeliwezekana, lakini ukumbuke ni watu zaidi ya mia waliingia eneo hilo, na katika kutafuta watu tunaoweza kuwashuku, hakuna tuliyempata...’akasema mpelelezi.

‘Huyu ambaye hakuandika jina halali ni nani, mpelelezi, fanya kazi hiyo tumpate, na nilikuwa nauliza huyu kijana wako aliyekuwa kwenye hilo jengo ni nani, na alikwenda kwa matilaba yenu, au alikuwa na mambo yake binafsi...?’ akauliza muendesha mashitaka.

‘Huyu kijana wetu, alikwenda kwa mambo yake na huko akamkuta huyo kijana mwingine, ....na kijana wetu anasema huyo mwenzake aliondoka akamuacha yeye hapo, ....’akasema

‘Ok, tujue kwanza kuhusu kijana wa mshitakiwa, ....’ akasema muendesha mashita na mkuu akionekana kuwaza jambo.

‘Huyu kijana wa mshitakiwa  alipomuona mshitakiwa anaingia akatoa taarifa kwetu, na huyu ndiye aliyesaidia, maana watu wetu walishampoteza huyu mshitakiwa, kwahiyo sisi tukawasiliana na  watu wetu kuwa mshitakiwa kaonekana akiingia kwenye hiyo hoteli,na wao wakaelekea huko, lakini walikuwa wamechelewa....’akasema mpelelezi

‘Ni nani huyo kijana wenu, ni maofisa usalama, au ni hawa wa kupachika siku moja moja....?’ akauliza muendesha mashitaka

‘Sio ofisa usalama, unakumbuka nilikuambia kuwa kuna vijana tuliwashirikisha na wakawa tayari kuisaidia polisi, huyu alikuwa mmojawapo, yeye anafanya kazi kwenye ile ofisi ya yule mtaalamu,....’akasema

‘Mtaalamu huyu mwenye kampuni ya mitandao ...?’ akauliza mkuu

‘Ndio mkuu...’akasema mpelelezi

‘Ni nani huyo?’ akauliza muendesha mashitaka akimuangalia mkuu,halafu mpelelezi

‘Ni kijana wa huyo mshitakiwa...’akasema mpelelezi, na aliposema hivyo, mkuu akainua kichwa kumuangalia mpelelezi, kama kuonyesha kushutika hivi, lakini hakuonyesha dalili ya moja kwa moja, akamgeukia muendesha mashitaka kama kutaka kumuuliza kitu, lakini akasita, akamgeukia mpelelezi na kumuuliza.

‘Mbona hukuniambia hilo hata kwenye ripoti yako hukuyaandika hayo, sikuona hilo kabisa au nimekosea,...?’ akauliza mkuu, na mpelelezi akawa kama anatafakari jambo, na muendesha mashitaka akauliza

‘Huyu kijana wa mshitakiwa anasemaje ulipomuuliza, alifika hapo kwasababu zake,  au alifika kwa kazi maalumu,,...?’ akauliza muendesha mashitaka.

‘Sisi hatukumtuma, alitumwa na mtu mwingine,...’akasema

‘Alitumwa na mtu mwingine !? ni nani huyo alimtuma...?’ akauliza mkuu

‘Alitumwa na Mama mtemi!! ...’akasema mpelelezi

‘Alitumwa nini,au kufanya nini....maana haya sasa nayaona megeni hukuyaandika, hukuniambia...?’ akauliza  mkuu

Wakati huo muendesha mashitaka akawa anaandika kwenye kumbukumbu zake na mkuu akawa anaangalia jinsi muendesha mashitaka anavyoandika, kwa kuonyesha wasiwasi,  na mpelelezi hakujibu hilo swali kwanza japo mkuu wake ndiye aliyemuuliza, akisubiria muendesha mashitaka amalize kuandika anachoandika.

‘Mkuu, haya sikuyaandika kwasababu.....’akatulia, akisita kuongea na muendesha mashitaka akamkatiza kwa kumuuliza swali jingine.

‘Samahani kwanza hapo,....umesema huyu kijana wa mshitakiwa alimkuta kijana mwingine , huyo kijana mwingine sio miongoni mwa vijana wenu...?’ akaulizwa

‘Hapana, ...yeye ni rafiki wa huyo kijana wa mshitakiwa,...’ akasema mpelelezi, akimtumpia jicho mkuu wake, aliyekuwa akiangalia saa

‘Ni nani huyo kijana mwingine rafiki yake kijana wa mshitakiwa, na mlimuuliza huyo kijana mwingine alifika hapo kwa shughuli gani, haiingiliani na hili tatizo....au walipanga kukutana na huyo kijana wa mshitakiwa au ilikuwaje...hebu weka sawa hapo nikamilishe ninachoandika...samahani mkuu kwa kukukatiza?” akauliza muendesha mashitaka.

Mkuu akatikisa kichwa kukubali, huku naye akionyesha shauku kusikia jibu la mpelelezi, wote wakawa wanamuangalia mpelelezi, wasubiria...mpelelezi akawa anafungua makabrasha yake hakutaka kulijibu hilo kwa haraka,na hapo kumfanya mkuu wake aonyeshe kama kukerwa, na kabla mkuu hajasema neno, kwani alitaka kusema neno, mpelelezi akageuka kamuangalia muendesha mashitaka akasema, ....

‘Ni kijana wa mkuu...’akasema mpelelezi na mkuu akashituka kiasi kwamba kule kushituka kwake kulimfanya atake kama kusimama

‘Ni kijana wangu! Kijana wangu mimi,.... haiwezekani, ...una uhakika na hilo,...ilikuwa saa ngapi, nakumbuka alikuja kwangu, tukawa.... no no, ungeniambia mapema, kwanini hukuniambia mapema, kabla huja.....siwezi kuamini, sio yeye....’mkuu akasema sasa akishindwa kuficha hisia zake, akasimama huku akiangalia saa

‘Kwanza nimechelewa kikao,...na mpelelezi,umenichanganya,..hukutenda majukumu yako ipasavyo, itabidi tuliongee hilo, sipendi kazi ya namna hiyo, ya kunificha ficha baadhi ya mambo.....sasa mimi naondoka, nina kikao na wakuu...’akasema akipanga panga makabrasha na kuweka ndani ya mkoba wake.

‘Mkuu, ngoja tumalize hili kabla hujaondoka...’akasema muendesha mashitaka alipomuona mkuu huyo akijiandaa kuondoka, lakini mkuu hakumsikiliza akainua mkoba wake na kuanza kundoka

Naye mpelelezi akawa anafungua makabrasha yake kama vile anataka kuendelea kuonyesha ushahidi zaidi...akasema

‘Mkuu  nina sababu za kufanya hivyo....’akasema, na mkuu alishaanza kuondoka akageuka kumuangalia mpelelezi akasema

‘ Sijarizika na utendaji wako,...sina muda tena, wekeni mambo sawa tutakutana baadaye, na mara simu ya mkuu ikalia, na mkuu kwa haraka akainua simu yake kuangalia mpigaji, na kusema....

‘Ni mke wangu! Oh, nilisahau kumpigia simu,...`sory mke wangu..nilikuwa kwenye kikao....nani, kijana wetu,.... yupo hapo,mwambie asiondoke mpaka nije,nina mazungumzo na yeye....’akawa anaongea huku anatembea kutoka nje...na wenzake wakawa wanaangaliana,  macho yakiongea .....


WAZO LA LEO: Kuna wazazi huwa wepesi sana kuwatetea watoto wao, hata kama wanajua kuwa watoto wao ni wakorofi, wakiambiwa `mtoto wako ni mwizi, au mtoto wako ni muhuni au ni jambazi....’, yeye (mzazi) huja juu na kumtetea mwanae....,badala ya kuungana na jamii kumsaidia huyoo mtoto, yeye hukimbilia kujenga chuki na jamii,...tukumbuke kuwa kufuga mwizi, kutetea maovu, hata kama yanafanywa na mtoto wako ni sawa na kufuga nyoka mwenye sumu kali, ipo siku atakugeukia wewe mwenyewe...
Ni mimi: emu-three

No comments :