Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, July 6, 2015

RADHI YA WAZAZI-15


 Siku hiyo nilikuwa nimekaa sebuleni, nikiwa nimekunja nne, pembeni kuna chupa ya kinywaji, sina wasiwasi pesa zipo japo kidogo,..unajua tena masikini akipata inakuwaje...na wakati nainua gilasi ya kinywaji kwa madaha,  mara nikahisi mwili ukinisisimuka, nikainua kichwa na kutizama ujio wa mlangoni. Huwa sijui ni kwanini, ....

‘Unajua bro, kutokana na utaalamu huu wa madawa, na mazoezi,...huwa nimeshajengeka kuwa na hisia fulani,...najua wengi, ingelikuwa huku watasema una kitu kama mashetani au ...vyovyote iwavyo ila nina hiyo tabia,...ni tabia ya kuhisi jambo kabla halijatokea, hasa ikiwa ni hatari,...kwahiyo nilivyohisi mwili unasisimuka, nikajua kuna jambo, na kweli haikupita muda mara  kule mlangoni, nikaona watu wakiingia.

Pale nilipokuwa nimekaa nilikuwa naona mlango wa kuingilia, na nilichagua sehemu hiyo mahususi kwa ajili ya kujihami, ...nilitaka mtu yoyote akiingia nimuone, ni kujihami tu maana muda mwingine nikiwa chumbani siwezi kuona anayeingia na kutoka
Hata hivyo wakati nachukua chumba, kwa siku mbili tatu, nilishawaambia kuwa sitaki mgeni.

‘Nina kazi naifanya sitaki usumbufu, kwahiyo akija mgeni au mtu yoyote kuniulizia msimwambie nipo hapa, ....’nikawaambia

‘Sawa bosi, upendavyo, jisikie upo nyumbani...’akasema huyo muhudumu, lakini ka hisia zile nikahisi kuna jambo..

‘Mhh, nahisi hatari....’nikasema na kusimama kidogo, lakini nikajipa moyo kuwa hata kama ni hatari, bado huyo mtu hawezi kuja kuniona moja kwa moja, ,...ni lazima muhudumu, atakuja kuniambia kwanza. Nikainua chupa kabla sijapiga fundo, nikahisi hiyo hali tena, nikatikisa kichwa kuondoa hiyo hali, nikasema kwa sauti ndogo

‘Hata hivyo, huku nani atanifuata, ....mmh nihahisi ni owoga tu, .....’na kabla sijamaliza kujiongelesha kichwani,nikaona mlango wa sehemu ile niliyopo ukifunguliwa, hapo nikatega macho, na masikio...

 Alikuwa ni mtu wa mapokezi ! Kwanza nilijua yupo peke yake , nikajiandaa kumwambia sitaki wageni, ....lakini kumbe nyuma yake kuna mtu!

Ni nani huyo yupo nyuma yake, huyo mtu alisimama nyuma ya huyo mtu wa mapokezi, kama  vile anajificha nyuma yake, sikumuona mapema....

‘Oh,....alikuwa ni mwanamke...., mwili ukanizizima, nikataka kuinuka niende chooni, lakini isingeliwezekana kwani choo, kipo muelekeo wa  huko wanapotokea hawo watu.

‘Nimekubamba....’ilikuwa sauti ikitokea nyuma kwa  huyo mwanamke, na sauti yake ilinifanya nidondoshe ile gilasi niliyokuwa nimeshikilia, na kushikwa a kikohozi cha muda.

‘Mhh,...kohokoho... u-u-u-menibamba! Kwanini, karibu...hamna shida, unajua , nipo hapa nasubiri kukutana na bosi wangu mpya...kohokohokoho, karibu madame.....’nikasema huku nikijikanganya.

‘Najua....yah, , tena sana, kila bosi wako lazima aingie mkenge wako au sio...ndio zako hizo,..., hahaha....angalia usitie hasara kwa kuvunja gilasi za watu kwa uwoga...’akasema huku akimuashiria yule mtu wa mapokezi aondoke, utafikiri ana mamlaka naye, na yule muhudumu kweli akageuka na kuondoka.

Huyu mama alisubiri kuhakikisha yule muhudumu kaondoka kabisa ,halafu akasogea pale nilipokaa, akasema huku akitabasamu kwa dharau.

‘Siku hizi huonekani eeh,....umepotea kabisa maeneo ya kule kwetu,....’akasema akishika kidevu huku akibenua mdomo kwa dharau...

‘Mbona nipo tu, ni kwa vile umesema huna kazi na mimi,sasa nitakuonaje huko kwako,....au kuna kazi nije...’profesa akasema sasa akijitutumua kuondoa ule uwoga uliokuwa umemtinga.

‘Mhh,... kumbe umekuja kujificha huku, ukitumbua pesa za mlungula...au sio...?’akaniambia huyo mama huku akivuta kiti na kukaa , alikaa mkabala na mimi, ili tuwe tunaangaliana,sikupenda akae hivyo .Akawa sasa ananiangalia moja kwa moja usoni,bila kupepesa macho.

‘Hapana,...sio pesa ya mlungula,... nilifanya kazi sehemu moja,nikapata vijisenti, na kwa vile nina miadii na bosi wangu mmoja ndio nikaona nije nipumzike hapa...ni kawaida tu..leo hapa kesho pale, si unajua mimi sina kazi ya kudumu....’nikazidi kudanganya

‘Hahaha,...watu kama nyie mtapata kazi ya kudumu,...halafu unasema eti umekuja hapa kupumzika wakati umepanga kwenye hii hoteli, leo siku ya ngapi....usinifanye mimi mjinga....’akasema akizidi kumuangalia profesa moja kwa moja usoni.

'Ndio hivyo...’akasema profesa akishindwa kuendelea kuongea

‘Ok, sina haja ya maneno mengi,....ila nafahamu unajua kwanini nimekuja hapa kukuona au sio...?’ akasema

‘Aaah, kuhusu pesa yako au sio...’akasema profesa huku akitoa pesa mfukoni, ilikuwa dola elifu tano, akaziweka mbele ya huyo mama, na huyo mama akaziangalia kwa macho ya dharau na kusema;

‘Unakumbuka deni langu,.... ulisema utalipa sehemu nyingine mwisho wa mwezi huu uliopita, na mwezi umeshapita sijapata hizo pesa,unataka nikuelewe vipi...na hiki ni kitu gani unanipa.....hiyo ndio malipo yangu, naona unanitania...’akasema huyo mama akizingalia zile pesa bila kuzigusa.

‘Ndio maana nipo hapa kukutana na bosi wangu, nitakuja kwako nikitoka hapa kama sio leo ni kesho...huyo bosi wangu, ananizungusha kidogo, lakini nina uhakika ...’nikasema nikitikisa kichwa kama kukubali.

‘Bosi wako ,bosi wako..huyo bosi wako ni nani....?’ akauliza

‘Huna haja ya kumfahamu,...si unajua tena...’akasema profesa

‘Nataka pesa yangu, wakati unaichukua hukunipa muda...unakumbuka...ukajifanya mjanja,..hahaha, utaninyaa, nakuambia, utanisimulia..bado,.....’akasema

‘Nakuomba uniamini, nipe wiki moja hivi...ukiniona kimia, nakuahidi nitakuwa nimeshapata pesa yako usijali...nilipanga kila wiki niwe napunguza, lakini mambo hajawa safi,....lakini ipo njiani inakuja...’nikasema nikinyosha mkono kuzichukua zile pesa, nikijua hataki kuzichukua.

‘ Wiki moja!,...nikupe wiki moja...hahaha,  unanitania sio,....Sikiliza wewe mwizi wa mlungula,....’akasema sasa akiwa kasimama, na jinsi mkono wake ulivyokwenda haraka na kuzichukua zile pesa utafikiri  ulimi wa mjusi ukidaka wadudu wanaopita hewani.

‘Labda wewe hujanielewa, sipendi utani, usione nimefika hapa ukafikiri nimebahatisha, nafahamu nyendo zako A to Z, najua sasa mpo kwenye mpango wa kumla mtu pesa zake, sasa sijui kwa vipi,....’akasema akizifutika hizo pesa sehemu ya maziwa yake bila kuzihesabu.

‘Hizi hazipo kwenye mahesabu,ni gharama ya kukufuata...unasikia....’akasema

‘Hapana napunguza deni,.....’akasema profesa

‘Mimi hilo sijui,na sijali jinsi gani unazipata hizo pesa,  na wala sitaki kuingilia wizi wako....., ilimradi unanilipa pesa yangu kama ulivyoahidi...’huyo mama akasema

‘Nitakuletea pesa yako madame,..., wewe uniamini tu....na sio za wizi ni jaso langu...’akasema profesa hukuu akichelea huyo mama asije kuleta vurugu hapo, na watu wakawaona.

‘Poa,...mimi naondoka, nakupa siku hizi mbili, au tusema tatu, nikija , au popote utakapokwenda ujue ninakuja kwa shari... sitakuja hivi hivi,nikuache hivi hivi...leo nimeiheshimu hii hoteli, wananifahamu na nawafahamu ni watu wangu...’akasema sasa akiwa sasa anasimama.

‘Ila kumbuka, safari nyingine nikija, ...nitakuja nikiwa nimekamilika, usinione sasa ni mtu mzima ukafikiri siwezi kukumudu...kwanza wewe hunipi shida...ni mdwebedo tu...hujai hata kiganjani...’akasema na kugonga meza kwa nguvu, hadi vinywaji vilivyokuwepo vikamwagika

‘Oh...tafadhali madame...utafanya watu wanifikirie vibaya....’nikasema , na yeye bila kujali,huyoo, akaondoka zake nikabakia najikunguta kinywaji kilichonirukia, usoni na nguoni. Mwili ulikuwa umeanza kunietemeka.

*********

Nilibakia nimeduwaa maana sikuweza kafahamu vipi huyu mama aliweza kugundua kuwa nipo hapo,kwani hapo ni sehemu niliyoitafuta ya kujificha, nikiwa nafanya vitu vyangu, na kiujumla pesa nilikuwa nayo kidogo tu, lakini ilikuwa haitoshi kumlipa huyo mama, kutokana na makubaliano yetu ...akawa sasa kachukua kaakiba kangu niliko kuwa nak...

Nikaangalia huku na kule kuhakikisha kama hakuna aliyewahi kuona hilo tukio, na hakukuwa na watu sehemu hiyo, watu walikuwa wamekaa kwa nje,....na ukiwa kwa nje huwezi kuona huku ndani.

Hapo sasa nikaona hakuna amani na siku imesharibika, nikasimama na kuanza kutafakari la kufanya.

‘Huyu mama kanipa  siku tatu,...na mzigo mwingine tuna utarajia lini, oh,...ni baada ya wiki,...baada ya wiki,  sasa nifanyeje..’nikajikuta nakuna  kichwa, nikiwazia la kufanya.

‘Nitapatia wapi pesa za kumnyamazisha huyo mama, japo kidogo....?’ nikawa najiuliza
Mara wazo la haraka likanijia kichwani, nikachukua simu yangu ya mkononi  kutaka kupiga simu, lakini nikakumbuka jambo, nikarudisha hiyo simu mfukoni, ...nikatembea hadi mapokezi

‘Muhudumu,...umefanya nini sasa, nilikuwambia sitaki mgeni, mbona unamleta yule mama bila taarifa...maana yake nini....,mnakiuka masharti ya mteja au...?’ nikauliza kwa hasira

‘Huyu mama kasema mliwasiliana naye, na huyu mama huwa ni mteja wetu mkubwa wa hapa,tunamuamini sana, hawezi kutudanganya, na kasema upo hapa ukimsubiria, hatuwezi kumdanganya...na alishakuona ukiingia mara kwa mara hapa, kwahiyo anafahamu kuwa upo hapa...’akasema muhudumu

‘Ina maana anaingia hapa hotelini mara kwa mara, kufuata nini...?’ nikauliza na yule muhudumu akakaa kimia,

‘Mhh...ina maana kila siku yupo hapa,na alishaniona nikiwa humu...haiwezekani...!? 'nikasema.

‘Ndio...alishakuona na akasema wewe ni mfanyakazi wake, na kwa vile ni  mteja wetu mkubwa tukamuamini..’akasema

‘Mhh,mbona hamkuniambia....ooh, itabidi niondoke hapa haraka, siwaamini tena nyie watu...’akasema

‘Kwanini tukuambie, kwani kuna tatizo...mimi najua ni mtu wako mnafahamiana...na kasema wewe ni mfanyakazi wake...anajua wewe upo japa kwa kazi maalumu aliyokupa....umfanyie...’akasema

‘Kwani nadaiwa shilingi ngapi, nipeni bili yangu...nadaiwa shilingi ngapi?’ profesa akauliza

‘Kwanini uondoke haraka hivyo...na akija tumuambieje...?’ akauliza huyo muhudumu akionyesha uso wa mshangao

‘Nataka sehemu nyingine, sehemu ambayo sitaki wageni, na nikisema sitaki wageni kweli sitaki wageni, ...’akasema profesa

‘Sawa kama ni hivyo, tutafanya hivyo...endelea kukaa, akija tutamwambia haupo....au tusemeje bosi...’akasema muhudumu

‘Unajua umenivurugia mipango yangu ya pesa,  nipeni bili yangu niwalipe niondoke zangu...hamna maana nyie kabisa...’profesa akasema na muhudumu akaenda kuongea na bosi wao, haikupita muda akaleta bili na profesa akalipa,na kuondoka zake.

********

‘Lakini bwana mdogo, naona kama umeruka sehemu, unakimbilia kusema umepata pesa, hujasema umezitoa wapi, ulizipata wapi,..ilikuwaje...?’ kaka mtu akauliza, alipoona mdogo wake msimuliaji akijinyosha.

‘Nitakuelezea tu bro..., wewe usijali, naongea kutegemea na kumbukumbu zinavyokwenda imebidi nianzie hapo maana tukio la kuzipata pesa mwazoni lilikuwa rahisi lakini hatua ya pili iliingia nyongo...’akasema huku akiashiria kwa mkono

‘Ilikuwaje ikaingia nyongo...?’ kaka mtu akauliza

‘Unajua dili hii haikutakiwa kuharakisha kihivyo, lakini tamaa zetu zilitufanya tufanye hivyo,  na matokea yake, ikaharibu mambo...’akasema

‘Kwa vipi hebu anzia pale mlipokuwa mkipanga jinsi gani ya kufanya, mkakutana na yule msichana wa bar....halafu ...,  hatujaona hilo tukio, jinsi mlivyofanya hadi mkaweza kumtoa huyo mtu pesa...’kaka mtu akasema

‘Hilo utalisikia tu huko mbele..., ngoja twende ninavyotaka mimi,...’akasema mdogo mtu

‘Haya endelea utakavyo....’kaka mtu akakubali kwa shingo upande.

‘Ni hivi bro,...kiukweli tulipopata mkupuo wa kwanza,...lakini haikuwa pesa ndefu kama ilivyotarajiwa,....maheabu yetu mwanzoni kutokana na mtaalamu yalikuwa makubwa,... lakini hatukufanikiwa.

Unajua kazi hizi za dhuluma, hakuna kuaminiana kwani hata nilipompelekea mtaalamu, kiasi hicho hatukuelewana, yeye akaendelea kudai ushuru wake, lakini ningepata wapi hicho kiwango alichokuwa akidai, hakuniamini  kabisa hadi pale alipohakiki kwa njia zake....

Basi tulichopata ndicho tulichogawana, nikajikuta nina pesa ndogo tu,...nikaona cha kwanza kwenda kumlipa huyo mama...nina penda sana pesa ikiingia mkononi, ninakuwa mchungu kuitoa, lakini nikikmbuka ya huyo mama, sikuweza kuvumilia, kwa haraka nikakimbilia kwake...

Nilifika kwa huyo mama huku mabega yapo juu, kwa madaha,nikamuuliza

‘Hivi unanidai shilingi ngapi...?’ nikamuuliza

‘Unataka kusema nini, umekuja na pesa yangu au..?’ akauliza na kabla sijamjibu nikatoa bulungutu la dola elifu ishirini,...nikawa nahesabu na huyo mama akawa ananiangalia kwa macho yenye uchu

‘Nakuda-dai,....hesabu vizuri....dola,laki-, eeh, ....aah, hebu vizuri....’akawa ananifuatilia ninavyohesabu, na akishindwa kunitajia kiasi anachodai, kwa uchu wa zile pesa,mpya mpya kutoka benki

‘Hizo ni za mkupuo wa kwanza,...baada ya wiki mbili hivi nitakuletea mkupuo mwingine, nataka tumalizane kabisa...kukuonyesha kuwa sina shida..ilikuwa ni namna ya kukuweka sawa....siuanona mwenyewe...’akasema profesa

‘Umepatia wapi hizi pesa, ohoo,umemuibia mtu mwingine nini  eeh...sawa,mimi sijali,ninachotaka ni pesa yangu,...’akasema akiwa haamini, akiwa kazishikilia hizo pesa mkononi

‘Mhh, uliuliza nini, ...ok,..nilishakupa jumla ya deni langu sitaki kurudia rudia tena, ....madeni ya wengine mtajuana nao,ila....wakisema niwasaidie,nitawasaidia, na tutakuja kwako...’akasema

‘Aaah,....wewe angalia chako..ukiwasemea wengine...nitashindwa kukulipa deni lako, hao wengine achana nao,....,unasikia, ...tutaongea mimi na wewe nikija kumalizana, au sio....’nikamwambia, lakini kwa muda huo alikuwa akianza kuzihesabu zile pesa.

‘Unasema ...ndio tutaongea, ngoja kwanza nizihesabu hizi pesa, maana kwenye pesa hakuna kuaminiana...’akasema akihesabu

‘Wewe niamini tu, nikipata nyingine, ambazo natarajia hivi karibuni, nitakuja , ni kama baada ya wiki moja hivi,...’nikasema nikianza kuondoka

‘Aaah, unanichanganya, hebu subiri.....’akasema mimi sikutaka kumpa nafasi maana anaweza kunza kudai nyingine na mimi nikakosa hata salio,

‘Nina haraka, kuna miadi mingine mahali, wewe niamini tu, kuwa nitakuletea nyingine kama hizo au zaidi ya hizo....’nikasema huku nikiharakisha kuondoka, na huyo mama akabakia akihesabu pesa yake.

‘Unaona bro, hayo ndio mambo ya mlungula...unapata pesa, lakini pesa zenyewe ni haramu hazikai...’akasema mdogo mtu akishika kidevu akikumbukai hiyo enzi

*********

‘Ina maana huyo mama mlishakubaliana kulipana hizo pesa...au ilikuwaje na ulikuwa unadaiwa kiasi gani na huyo mama....?’ akauliza kaka mtu

‘Kiasi gani ...hahaha alikuwa akinidai pesa nyingi, aliweka na riba juu kunikomoa....tatizo ndio hilo , unapata pesa, na aliyekupa hizo pesa akikuzidi ujanja, inabidi umlipe, na unamlipa pesa nyingi zaidi...sasa uone ubaya wa kazi kama hizo ulivyo,  sasa nalipia pesa nilizowahi kuzila, napata huku narejesha huku, nabakiwa sina kitu,..

‘Bro hayo ni maisha ya shida, maana huyo mama alishanikaa kooni, na nilijua nisipofanya hivyo, nitauhama huo mji, na sio kuuhama tu, huenda nikaishia jela,na hakuna sehemu ninayoiogopa kama jela, asikuambie mtu jela sio mahali pa kwenda

‘Nilishawahi kufungwa kabla..., lakini sikuwahi kukaa sana, nafungwa nakaa wiki, wiki mbili, na muda mrefu ulikuwa mwezi mmoja, kabla ya kifungo hicho kikubwa nitakachokuja kukusimulia ilivyokuwa...lakini bro, huo muda mfupi wenyewe..., nilikiona cha moto,mtu kama mimi, profesa kulala jela, niliumia sana, lakini ndio maisha,...’akasema

‘Hebu kwanza nikuulize,unaposema uliwahi kufungwa kabla,...ina maana maisha yako ya ulaya ilikuwa hivyo,maisha ya wizi......ukamchukua mtoto kwa maisha hayo -hayo, ,...?’ akauliza kaka mtu kwa hasira.

‘Bro,nilishakuambia kuwa mwanzoni, sikuwa na shida, kipindi wahisani wananipa pesa za mtoto,sikuwa na tatizo, matatizo yalianza pale kijana alipoanza kazi...

‘Naa, ni kweli kuwa niliwahi kufungwa kabla,hiyo ilikuwa kabla sijamchukua huyo mtoto,  ilikuwa  ni tatizo la madawa , kuna mteja nilima dawa, akakosea matumzi, yakamuathiri huyo mteja, nilikaa wiki moja tu, akaja huyo mteja kunitoa mwenyewe, ...akanisamehe, yakaisha....’akasema

‘Haya endelea na simulizi la maisha yako ya dhuluma, kwani nina hamu ya kusikia kuhusu kijana, ilikuwaje, ...’akasema kaka mtu

‘Bro...maisha ya huko ni ujanja ujanja tu...’akasema

‘Ujanja gani huo, dhuluma ni ujanja, hayo ni maisha ya kujitakia, na hayo yaliyokukuta, wala usimlaumu mtu....unalipa kile ulichovuna, ....na bado hujafika mbele ya muumba,...hujatubu, maana kutubu kwake, ni hao uliowadhulumu, wakusamehe, sasa wapo wapi....’akasema kaka mtu.

‘Bro, we acha tu,...nani arudi ulaya,...eti niende kuwatafuta ili nitubu, ..hahaha,  sijui kama nitarudi hai....hao walichukua pesa za mnada wa nyumba ni bahati yao...ila kiukweli, ulaya sio mahali pakukimbilia hivi hivi tu, kama huna utaratibu maalumu, ukienda huko, utaumbuka....’akasema

‘Umeona eeh.....’akasema kaka mtu

‘Nione mara ngapi bro,..niulize mimi,maana nimeishi maisha yote, ya raha, ya shida, ya jela...kila aina ya maisha huko nimepitia, nimewahi kuajiriwa,nikafanya kazi za ofisini, nikaona ugumu wake....na kule hufanyi siku nzima, ni masaa, ukitoka hapa unakwenda hapa, ukipata pesa inashia kwenye kodi,hakua ujanja wa kukwepa kodi huko .....kwahiyo hakuna mtu wa kunidanganya...’akasema

‘Ehe endelea.....’akasema kaka mtu.

‘Niendelee sio....’akasema kinywa maji

******

‘Pesa tuliyopata kwa huyo jamaa ilikuwa kiduchu tu..., na yule binti ilibidi aondoke,...sio tu kutokana na vitisho, lakini hata muajiri wake, alishapata malalamiko kabla,kumbe muajiri wake alikuwa akisiburia kisingizio, ili apate mwanya wa kumfukuza kazi huyo binti.

‘Basi tukamlipa pesa huyo binti, kiasi, sio zote,..na akafanyiwa mpango sehemu nyingine ya kazi..., kutokana na urembo wake, haikuwa ni tatizo, akapatiwa sehemu nyingine, ikawa ni ahueni yetu, lakini bado kulikuwa na tatizo, kwani bado alikuwa akinidai, na akasema kaka yake ndiye atakuwa mkusanyaji wa hilo deni...ikawa ni tatizo

‘Bro,nikajikuta kwenye wakati mgumu,maana wote wanaonidai, walishaona dalili kuwa nina pesa,kwahiyo wakawa wananiandama,ndio maana nikatafuta sehemu ya kujificha,ili nikionekana tu,niwe na cha kudanganyia....’akasema

‘Pesa tuliyopata ikawa ndio hiyo, kinyume na tulivyotajia, kwani ilikuwa ni ndogo sana...lakini jamaa alishaingia kwenye anga zetu, na alishaahidi kulipa nyingine baada ya wiki moja

‘Kwanini sasa,..... unajua bwana mdogo unachanganya mada...hujaenda kimpangilio...’akauliza kaka mtu

‘Kulikuwa na tatizo lilitokea...hasa kuanzia huko benki na likaja kumuhusisha mkewe...’akasema

‘Kwa vipi na wewe ulisema huyo jamaa anaweza kutoa pesa nyingi tu bila matatizo...na bila mkewe kujua,?’ akauliza kaka mtu

‘Kutokana na mtaalamu ndivyo ilivyokuwa , lakini kumbe akaunti ya huyu jamaa ilikutwa ina matatizo, benki walikuwa wanahitaji maelezo ambayo alikuwa hajakamilisha, na barua kutoka benki, ikaja na aliyeipokea akawa ni mkewe,hilo ni la kwanza

Pili, jingine kubwa likatokea,ambalo liliharibu, na kusababisha sintofahamu, kati yao wawili, yaani jamaa na mkewe, ikabidi akaunti hiyo sasa ijulikane rasm kwa mkewe na mke, na azimio jingine likapitishwa...na sio hayo tu kuna kisanga kwa familia hii, utakuja kuona ndio maana tulikuwa na uhakika wa kupata hizo pesa....’akasema

‘Ilikuwaje...?’ akauliza kaka mtu

‘Bro, Subiri nitakuhadithia, sehemu ijayo,ngoja nipumzike kidogo....

NB, UTAKUJA KUONA SEHEMU HIYO, SEHEMU IJAYO, NGOJA TUWEKE MAMBO SAWA, SIUNAJUA MAMBO YA SALIO NA MIMI BADO NIPO KWENYE MAWE


WAZO ZA LEO: Toba ya kweli kwa mkosaji, kwanza ni kukiri kuwa kweli umekosea, ukakiri kuwa hutarudia tena, halafu ukamwendea uliyemkosea ukamuomba msamaha, ukamrejeshea ulichomdhulumu,...wengi wanadhulumu, mafisadi, wanatajirika, lakini hawajui kuwa chumo hilo ni deni, hapa duniani na kesho ahera, kamwe asikudanganye mtu, kuwa kuna mtu wa kubeba dhambi za wengine, ..! Kumbuka, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe! 
Ni mimi: emu-three

No comments :