Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, June 16, 2015

RADHI YA WAZAZI-5


‘Unajua bro nilikweda kwa yule mke mtaliki wako, na cha ajabu akagundua kuwa huyo mtoto ni wake....’akasema akiwa anaongea na kaka yake ambaye alikuja siku hiyo mjini kununua bidhaa zake za biashara, na akampitia mdogo wake kumtembelea, sio kawaida yake mara kwa mara kufanya hivyo, ila kwa vile anafahamu mdogo wake huyo ypo na mtoto, basi akaona apitie ajue kinachoendelea.

Alishapanga afanye utaratibu wa kumchukua huyo mtoto akaishi naye, na alishajipanga kuhakikisha anambadili tabia yake, lakini kulikuwa na tatizo kuwa ataweza kujikuta matatani, kuwa yeye ndiye alimuiba huyo mtoto, na wakati sheria, na watu wa usalama walishafika kwake mara nyingi, na kuwaambia hajui wapi alipo

‘Ni kweli nilikuwa sijui wapi alipo....’akawa anajisemeza mwenye kichwani

‘Ni huyu kichwa maji, sijui kwanini alifanya hivyo, hata aliponipigia simu kuwa akimpata huyo mtoto afanyeje, nilijua anafanya mzaha, kumbe...mmh, sasa hili ni tatizo, lakini sijali,..lazima nimchukue huyu mtoto, vinginevyo ataharibika kabisa....’akasema

Basi akaona siku hiyo apitie kwa mdogo wake huyo na alipofika alimkuta mdogo wake akiwa kwenye harakati zake za kuuza madawa zake, akiwa na wasaidizi wake..

‘Oooh, bro, umakuje leo kwangu, ajabu kabisa....karibu, ngoja nimuachie huyu muuzaji wangu aendelee, karibu ndani....’akasema

Na ndipo wakaanza kuongea

‘Kwanza mtoto mwenyewe yupo wapi?’ akauliza

‘Kaenda shule, hatakiwi kukaa nyumbani, japo yupo likizo, lakini nimeoana awe anasoma soma, hili litamsaidia na yeye kujichanganya na wenzake na ataweza kukifahamu Kiswahili vyema zaidi..japokuwa ni kichwa, Kiswahili keshakifahamu hutaamini,...’akasema

 Tuendelee na kisa chetu

                                  *************

‘Sasa kwanini ulimpeleka mtoto huko kwa mama yake, mimi nilikuambia kuwa, sitaki wale watu wafahamu kuwa huyo mtoto tunaye,....kwani ulichofanya ni makosa,....sasa kwanini ulkampeleka huko bila idhini yangu?’ akauliza

‘Bro, huyu mtoto amekuwa mikononi mwangu miaka yote hiyo wewe hujui kuwa ninaye, na nimekuwa nikifanya lolote bila idhini yako, ....sasa kukuambia hilo ndio imekuwa kosa,....unanishangaza sana bro...’akasema

‘Vyovyote iwavyo huyo ni mtoto wangu, sikukutuma wewe kwenda kumuiba, mimi pale ni mjumbe, najua taratibu zote, naaminika, ..na kama taratibu zingelifuatwa,  nilijua kabisa mwisho wa siku nitakabidhiwa huyo mtoto wangu, wewe kwa kiherehere chako ukaenda ukamchukua bila idhini yao, hujui hilo ni kosa, hujui kuwa taarifa za kupotea huyo mtoto zilifikishwa polisi ....’akasema

‘Lakini ningewezaje kumuacha aliwe na mamba au kwa vile sijakusimulia ilivyokuwa, unafikiri mimi nina akili mbovu ya kuchukua watoto wa watu bila idhini yao....’akasema akiangalia saa, hakutaka huyo mtoto aje akutane na huyo baba yake.

‘Mimi sihitaji kujua, kwani haitanisaidia kitu, ....na sitaki ushahidi hapa, cha muhimu ni kuwa mtoto yupo, ubaya zaidi umemuharibu, huyo mtoto hastahili kukaa na wewe tena, anahitaji kuja kijijini ili apigwe msasa....’akasema.

‘Sikiliza bro, siku ile kule porini, nilimuokota huyo mtoto akitaka kuliwa na wanyama wakali, na mwanzoni sikujua kabisa kuwa ni mtoto wako....’ akasema

‘Hahaha hivi unafikiri nitakuamini na hadithi zako za kutunga...’akasema

‘Bro hili ninalokuambia ni la uhakika, ....unaufahamu ule msitu,ungelijua  huo msitu ulivyo,na bahati mbaya ni kuwa humo kuna mto ambao wanakijiji wanautumia kwa kuchota maji, kwa mbele yake kuna mamba, kuna mikenge mikubwa, ..kuna michatu na wanyama wakali, hebu fikiria, ...’akasema

‘Sasa huyo mtoto alifikaje huko, kama sio uwongo wako....?’ akauliza

‘Nimekuambia huko ndipo wanakijiji wanapochotea maji yao ya matumizi, si ndio serikali yako, kuna vijiji wana taabu ya maji...’akatulia

‘Najua ndio kauli zenu wapinzani, kwa vile mimi ni mjumbe wa chama changu utanishambulia kwa poroj zenu, na siwezi kukuamini kwa hadithi zako hizo...’akasema

‘Bro hii sio hadithi, ni kweli, mimi nilimuona huyo mtoto huyo akitembea peke yake, ..., huku analia, isingelikuwa ni mimi mtoto huyo angelikuwa ni kitoweo cha wanyama wakali....mimi kwa macho yangu nilimuona chatu akiwa eneo lile lile alipokuwa akitembea huyu mtoto....’akasema

‘Wewe ulifuata nini huko?’ akauliza huyo kaka yake sasa moyoni akiwa kajawa na jaziba, sijui kwanini ahisi hivyo kwa muda huo.

‘Nilikwenda kufuata dawa zangu, nilikuwa nimeshamaliza kuzipata dawa, nikawa sasa nachukua picha za video kwa kumbukumbu....na wakati namalizia, mara nikasikia sauti kama ya mtoto analia, nikaelekeza kamera yangu hiyo na huku na huku nafuatilia,....’akasema akionyesha kwa vitendo

‘Nikafuatilia, ndio nikamuona huyo mtoto akitembea kuelekea barabarani, kwanza nikamtizama kwa makini, kuhakikisha kuwa ni binadamu, hebu fikiria msitu kama ule unamuona mtoto mdogo peke yake, huwezi kuamini kwa haraka, ...nilipohakikisha kuwa ni binadamu sio kibwengo,, nikamwendea,....’akasema

‘Ina maana hao watu wanaishi karibu na hicho kisima, au ilikuwaje wamuachie mtoto atembee peke yake na kwenda huko msituni, ndio maana nilitaka nimchukue mtoto nimlee mwenyewe, ....siku nikikutana nao watanitambua, hilo halivumiliki, watu gani hao wasiojua kulea, hukumuona mama yake....?’ akaulizwa

‘Kwa muda ule sikumona mama yake, nilichojua ni kukimbia hadi pale alipokuwa huyo mtoto kabla hajadakwa na hilo lichatu....yaani hata mimi mwili ulinizizima kwa hofu, sina uwoga kabisa na midudu hiyo maana ninayo dawa ya kuyalewesha manyama makali kama kama hayo yasiwe na nguvu, huwa naileweshaga nikitaka kuchukua sumu zake, kwa dawa zangu, lakini kwa kitendo kilee...haaah, ...’akasema

‘Mhh,.....sitaki uendelee kunisimulia unanifanya nizidi kukasirika, na kuwachukia hao watu, ... ninachowaza ilikuwaje huyo mtoto awepo huko msituni peke yake.....?’ akauliza

‘Siku hiyo nilikuwa nimeweka kambi yangu ...kawaida nikitafuta dawa zangu sitaki mtu afahamu kuwa nipo hapo msituni mpaka nizipate....uzuri wakati namuona huyo mtoto nilishamaliza kazi zangu, ilikuwa ni bahati ilinijia, kwani ndio ulikuwa muda nachukua picha, na hizo picha ni biashara huko ulaya...’akasema

‘Unasema  ilikuwa ni bahati kukujia, unaona ni kitu kizuri hicho...!’ akasema kaka yake kwa mshangao

‘Basi bro, nilipomchukua huyo mtoto, sijui ni wa nani....nikawa sasa nawaza nimpeleke wapi huyo mtoto. Nilimpa chakula nilichokuwa nacho akala akalala, alikuwa na njaa, ungeona alivyokuwa anakula...’akasema.

*********

Nilkiwa sasa nataka kuondoka, mara wakaja watu;

‘Profesa kumbe leo upo huku....?’ akauliza mmoja wa askari pori huwa nafahamiana naye, wakati huo mtoto yupo kwenye hema kalala, hawakumuona na kwa muda ule ningewaambia, lakini haikutokea hivyo....ningewaaminije..., nikaoea nao kwanza

‘Ndio nipo nilikuwa namalizia kuchukua dawa zangu na nika....’kabla sijamaliza tukasikia kelele zikiita, walikuwa aksri wenzake, wakiwaita hao askari pori, wananifahamu sina shida nao sana, basi wakakimbia kuelekea huko walipoitiwa

‘Mhh, hawa wanatafuta nini, au ndio wanamtafuta huyu mtoto....?’ nikabakia kujiuliza
 Baadaye nikaona haina haja, muda wangu wa kukaa hapo ulishapita, nikamchukua yule mtoto nikaingia kwenye gari langu nikaondoka, na ni wakati naondoka ndipo nilikutana na mtu akanihadithia tukio zima, na uzuri, wakati huo mtoto alikuwa kalala kiti cha nyuma, na hakuweza kuonekana na mtu

‘Unajua sana kutunga hadithi wewe, na sikuamini katu, na mambo yako ya uganga hayo, ya utapeli utapeli ni nani atakuamini ..usije kuwa ulitaka kwenda kumuuza huyu mtoto kwa mambo yako ya kichawi....’akasema kaka yake.

‘Bro...sikiliza kwanza, waliponisimulia kuwa mtoto huyu ni wa mama mmoja aliye na mtatizo ya kifafa, nikamkumbuka shemeji,...na kweli alikuwa ndio yeye, nikaona ooh, sasa ndio muda muafaka wa kufanya kile ulichokuwa ukikitaka

‘Kile nilichokuwa nikikitaka...wewe hebu acha uzushi, nilitaka kumuiba mtoto...?’ akauliza kwa mshangao.

‘Nakumbuka ulisema kuwa unataka kuirejesha damu yetu mahali pake , ulitaka mtoto huyo achukuliwe arejeshwe kwao, yaani kwenye familia yetu...utajifanya umesahau, mimi nakumbuka vyema, uliwahi kuniambia hivyo....’akasema na kaka yake akabakia kimia

‘Niliposikia hivyo nikamchunguza mtoto nikagundua kuwa kweli anafanana na wewe, basi nikaona kumbe naweza kufanya jambo,....lakini sikutaka wewe uingie matatani...ndio maana sikukuambia mapema....’akasema

‘Tatizo lako unajifanya una akili sana, unafikiri ulichofanya ni ujanja na ujasiri, ..huoni kuwa ndio ulijiweka kubaya, sasa wakija kugundua kuwa wewe ndiye uliyemuiba huyo mtoto, wakafungua mashitaka unafikiri itakuwaje....?’ akaulizwa

‘Bro, mbona unakatiza utamu wa maelezo,.....wakati nipo porini mara nyingi ninakuwa na kamera yangu ya video, siunanijua zangu,...nimekuwa nikipiga picha nyingi za wanyama wa hapo msituni, sasa hilo tukio hahaha, kwanza liliniingizia pesa nyingi ajabu ...’akatulia

‘Wakati huyo mtoto anapita pale alipolala huyo chatu.....ndipo utamu ulipokuwepo, japokuwa nilikuwa na wasiwasi mkubwa,  ikanasa hilo tukio bara bara...utaliona lile chatu likijitutumua,..bro, unajua hilo tukio limeniingizia pesa nyingi, mtoto anapita karibu na chatu, na yule chatu anajitutumua kutaka kummeza....hebu weka akilini,....’akatulia

‘Na tukio hilo ndilo lililowezesha huyu mtoto kusoma huko ulaya, niliwaambia nilimuokota huyo mtoto akitangatanga msituni, hana wazazi, ...wazungu wana huruma , walipoona lile tukio kwenye kanda ya video, wakatokea wadhamini kibao wakuhakikisha huyo mtoto anapata elimu na matunzo....’akasema

‘Kwa ushahidi gani...?’ akauliza kaka yake

‘Ushahidi si hiyo kanda ya video..sasa nambie kama mimi sio mjanja...mimi ni profesa bro.’akasema

‘Kwahiyo mtoto wangu anajulikana huko kama mtoto yatima hana baba wala mama...?’ akauliza akiwa kakunja uso.

‘Huko ulaya ni mtoto yatima aliyetekelezwa msituni, ......na atakuwa hivyo mpaka anamaliza shule hadi chuo kikuu,,....si umeona mwenyewe anavyoongea kiingereza kile cha kwao....halafu, alisoma shule yenyewe inayotambulikana, ..’akatulia kuendelea hakutaka kusema anasoma shule ya watoto yatima.

‘Nakuambia wewe utafungwa, hayo maisha yako ya ujanja ujanja,mimi siyaungi mkono,...kumbuka uliponea chupuchupu kunyongwa huko uchina kwa madawa ya kulevya,karibu mama afe kwa shinikizo la moyo....sasa hili linaweza kukupeleka kubaya usipoangalia....’akasema kaka mtu

‘Baada ya miaka kumi na sita, ni nani ataweza kunifungulia mashitaka na kwa kosa gani, ni nani anajua sheria kwenye ile familia, wote sio waongeaji,.. ni nani pale, wote wapole-pole, watu wa kukubali tu, na kusema, namuachia mungu...hahaha, wacheza na profesa wewe...’akasema

‘Mimi sipendi kabisa hiyo tabia, sipendi kabisa...’akasema kaka mtu

‘Sikiliza bro, nilichofanya kwa muda ule kilitakiwa kiwe hivyo, na nina ushahidi,..., na kama unanilaumu kwa hilo, basi ..., hilo niachie mimi mwenyewe, mimi nimesoma naifahamu sana sheria, na mimi ni mjanja, ...’akasema

‘Huo sio ujanja, ni dhuluma, ujinga, a utapeli, na ukumbuke kuwafanyia watu hivyo, usione umeshinda....malipo ni hapa duniani, wangapi wangapi waliishi maisha ya namna hiyo wakajenga, wakatajirika,....’akasema akizungusha macho kuangalia paa la nyumba na kuzungusha macho kuangalia vilivyomo humo ndani, kweli mdgo wake, alikuwa kajijenga, nyumba ya maana, na vitu vilivyomo humo ndani ni vya thamani tupu.

‘Utajiri wa namna hiyo,...hii, mmh haina mwisho mwema,mwisho wake unakuwa mbaya...., ukumbuke malipo kama hayo ni hapa hapa duniani, kamwe dhuluma haidumu...na mengie huenda yakalipiziwa kwa familia yako mwenyewe....sasa mmmh....,mimi namtaka mtoto wangu....’akasema

‘Hahaha bro, badala ya kunishukuru, unaanza kunilaumu, kunionea wivu, huuku unasema eti..sasa namtaka mtoto wangu, ungempataje, kama angelibakia kule, ungempataje kama angeliwa na wanyama wabaya, angewezaje kufika ulaya..hivi bro, hulioni hilo....na kwanza mtoto mwenyewe hataki  kabisa kusikia habari za wazazi wake....’akasema

‘Eti nini, kumbe wewe ndiye ulimfunza huyo kijana, atukatae, sisi wazazi wake.....naona akikaa na wewe ataharibikiwa kama wewe, ...kwanza yupo wapi huyo mtoto, umesema kaenda shule, anarudi saa ngapi, nataka niondoke naye...’akasema

‘Analala huko huko.....’akamdanganya

‘Atalalaje huko huko, wakati umesema anasoma kwa muda,...na kwanii uhangaike kumpeleka shule hizo, wakati yupo likizo....anatakiwa kuwajua wazazi wake, anatakiwa kujifunza maadili mema...?’ akauliza

‘Bro unakumbuka nilikuambia kuwa nikipata bahati ya kumpata huyo mtoto nifamfanyeje, uakumbuka, na  uliniambia nini?’ akauliza

‘Nilijua unaongea kwa utani wako.....sikuwa na uhakika kuwa umedahamiria kulifanya hilo,..ningelijua kuwa unaye huyo mtoto, ningekuambia umrejeshe kwa mama yake haraka, maana najua utaratibu ulivyo....’akasema

‘Hahaha, bro, sasa unanigeuka, sema ulivyoniambia siku ile...’akasema

‘Nilikuambia nini...?’ akauliza kwa hasira

‘Hukusema ikiwezakana nimuibe na nimfiche wasimuona, ....akae mbali kabisa na hiy familia wasije kumuambukiza huo ugonjwa wa mama yake

‘Kipidi kile niliongea tu kwa jaziba tu...’akasema kaka mtu

‘Mimi nilijua umedhamiria na ndivyo nilivyofanya, nikamchukua huyo mtoto nikakaa naye, na bahati nilikutana na huyo mzungu aliyekuwa akishughulika na watoto yatima, nikamwambia nina mtoto yatima mkononi mwanagu, nikamuonyesha hiyo kanda ya video...na akasema tuongzane naye hadi huko kwao, na kwa vile na mimi nilikuwa na safari ya kwenda huko mambo yakijipa....’akasema

‘Tatizo lako, ujanja-ujanja na kuongea sana, kunakuzuzua...na ukome kabisa kusema huyo mtoto ni yatima, huwezi kuniua mimi, kwa kisingizio, hicho,....huna akili kweli wewe, yatima kwani mimi nimekufa, kwani mama yake amekufa....’akasema

‘Ndio ilikuwa njia muafaka ya kumweka mbali huyo mtoto na nyie wazazi wake amba hamualewani, nataka kwanza hl tuelewane, maana ukitoka hapa na kwenda kuongea ovyo, utaharibu kila kitu, ....’akasema

‘Kwahiyo yeye mtoto, anafahamu hivyo kuwa hana baba wala mama....?’ akaulizwa

‘Nilifanya hivyo ili asome, na ili aweze kuishi huko ulaya , na kweli akapata shule nzuri, na kusomeshwa huko,..tatizo kubwa ndio hilo hakuweza kupata mtu wa kumuongoza ili ajue asili yake mapema, hilo bro ndilo tunatakiwa tulifanyie kazi, tuelewane hilo, ....’akasema

‘Unajua bro, baada ya kwenda naye ulaya, sikuweza kuonana naye kwa miaka kma saba hivi, na siku nilipokutana na huyo mzungu  akaniambia maendeleo ya huyo mtoto ni makubwa sana...ana akili sana darasani.., nikamwambia nataka niwe karibu naye, nikitaka ajue lugha yao, na .....hata asili ayake, akanikubalia, kwahiyo nikawa namtembelea, tukaanza kuzoeana, na baadaye nikaja kumuambia mimi ni baba yake......’akasema

‘Wewe ndiye baba yake,....?’ akauliza kaka mtu

‘Mwanzoni....si alikuwa bado mdogo, kwahiyo nilitaka kumpeleka taratibu, ili anizoee, ilikuwa ni hatua kwa hatua za kumrejesha kiakili kuwa yeye sivyo kama ilivyo..unielewe hapo....’akasema

‘Ina maana hata huyo mzeungu hukumueleza ukweli...?’ akauliza kaka mtu

‘Yeye anafahamu kuwa mimi ni baba wa kufikia, ...mtu niliyemuokota huyo mtoto akitangatanga msituni..... hadi sasa inajulikana hivyo, ila ni rafiki yangu mkubwa, ndiye kaniwezesha kuwa karibu a huyo mtoto, na kwa vile kule nilipata soko la dawa zangu, nikawa naishi huko na yeye anakuja mara kwa mara kwenye dula langu,....tumezoeana sana, hana shida...’akasema

‘Nikuambie kitu, wewe kwanza huna adabu kabisa, ....mimi sitakuelewa, mpaka nimchukue huyo mtoto, nataka nikakae naye mwenyewe...’akasema

‘Bro huyo kijana bado anasoma, na anatambulikana huko kama yatima, ukijitia kimbele mbele utafanya asisome tena,...utamwaribia maisha yake ya baadaye na mimi utanifanya nionekane ...eeh tapeli...’akatulia

‘Mhh...umeanza kujileta mwenyewe, kumbe eeh...’akasema kaka yake

‘Bro, wewe mwache asome hadi tuone mwisho wake..mtot ana kili darasani,  ana kipaji sana cha lugha,...ana akili sana, hata nilipomtembelea hapo shuleni kwao,mwalimu wake aliniambia kuwa darasani ni miongoni mwa vijana wanaofanya vyema....’akasema

‘Lakini hata akiwa na akili. Kama hanifahamu mimi, kama hana adabu unafikiri huko mbele itakuwaje...?’ akaulizwa

‘Bro, kumbuke kuwa huyu mtoto hadi kwa wazazi wake , mama yake hajulikani wali alipo, kapotea, ...kafa, na hata wewe uljua huyu mtoto yupo wapi.....na nakuambia hivi ukilazimisha kumchukua huyu mtoto utampoteza kabisa, ..anaweza kutoroka, na hata asionekane tena, wewe niachie mimi nitampeleka hivyo hivyo na ipo siku atakuja kukutambua wewe kama baba yake, sasa hivi usilamishe....’akasema

‘Hilo sikuoelewi,...mimi naondoka, ila nikirudi tena ujue nitakuja kumchukua,....’akasema na kuondoka, na wakati anageuka kuondoka mlango ukagongwa

‘Dad am back....am hungry...’ sauti ikasikika

NB: Haya haya, japo kwa shida, lakini tutafika tu, kwa leo ni hayo , tuzidi kuombeana heri...


WAZO LA LEO: Kizazi chema ni kile kinachojengwa kwa maadili mema, elimu yenye manufaa, na msingi mwema wa maisha. Wazazi ni jukumu letu kujitahidi kwa hilo, maisha ya ubabaishaji, utapeli, kudanganya tusiyaingize kwenye akili za watoto wetu, kwani baadaye tutakuwa na taifa lisilojua sheria, na muelekeo mwema. 

Ni mimi: emu-three

No comments :