Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, May 19, 2015

NANI KAMA MAMA-79


Nikiwa chumba alicholazwa mama, dakitari akafika akiwa na faili la mama, akaniangalia usoni halafu akasema;

‘Vipimo vyote vya mama vipo tayari…’akasogea na kumkagua mama kwa macho halafu akanielekea huku kashika faili

‘Kama ulivyoambiwa, mama yako ana uvimbe kichwani..na uvimbe huo unahitajika kuondolewa, …kunahitajika upasuaji…’akatulia

‘Na kama unavyojua hapa nchini kwetu hatuna huduma kama hiyo, wataalamu wa upasuaji wapo eeh, lakini, bado hatujafikia hatua ya kufanya upasuaji huo…’akatulia

`Ili mama yako apone anahitaji kupelekwa India huko ndipo upasuaji huo unawezekana…kiujumla tatizo alilo nalo mama yako,likiachiwa litasababisha matatizo mengine,…sio na kutisha ila ndio hali halisi, uvimbe huo ukiachiwa,mama yakoataathirika ki-akili, hatakuwa sawa, atapooza viuongo…, lakini wenzetu huko India wanaweza kulitatua hilo tatizo kwa upasuaji, na nimewasiliana nao wanasema hilo linawezekana….’ Akasema

Tuendelee na kisa chetu

***********

‘Oh docta kumbe mama anaweza kupona na kumbe tatizo lake linawezekana kutibiwa, …Sasa docta si nyie basi ndio mnaweza kufanikisha hiyo safari ya mama ili akafanyiwe huo upasuaji au,…’nikasema nikionyesha furaha, na docta akaniangalia akafanya kubenua mdomo kama anatabasamu, akasema

‘Mhh, …kufanikisha ..mmmh hapana sisi kazi yetu tumemaliza…’akasema docta sasa akiendelea kulikagua lile faili (kabrasha)

‘Lakini mama yangu anahitajika kwenda India…si ndio na huko atafanyiwa upasuaji, na nyie ndio mnaojua taratibu zote au sio...’nikasema nikimuangalai docta, na docta akanitupia jicho , halafu kwa haraka akaendelea kulikagua lile faili.

‘Ndio hivyo,..mama yako anahitajika kwenda India, na safari hiyo ni gharama ,...'akasema

'Si ndio docta mtu kama mimi nitawezaje,....najua serikali, itasaidia au sio docta...?' nikauliza na docta akatabasamu akaniangalia na kusema;

'Mimi, kama docta nimekamilisha kazi yangu,  kazi iliyobakia ni wewe kutafuta uwezekano wa yeye kufika huko…'akasema

'Ina maana ni mimi natakiwa kufanya kazi hiyo,...docta mimi, nitawezaje ....mhh?' akawa kanivunja nguvu.

'Ndugu, nikuambie ukweli, kuna wagonjwa kama mama yako wengi..na matatizo kama hayo na mengine na wanahitajika kwenda huko huko,...wanasubiria ruzuku ya serikali, lakini lini, siunajua tena, serikali kama serikali haina pesa, fungu la namna hiyo ni dogo, sana sana wanategemea ufadhili,…'akasema

'Si ndio hapo, wao watatafuta wafadhili , mimi nitawapatia wapo hao watu...'nikasema

'Unajua kwanini nimekuambia ... tatizo la mama yako linahitajia uharaka..ndio maana nikakuambia wewe hivyo, ili uweze kufanya juhudu za ziada, vinginevyo haya, subiria hiyo ruzuku ya serikali,..sasa sijui lini….’akasema docta

Yalikuwa maneno ya dakitari ambayo niliyaona kama sindano ndani ya moyo wangu. Nikajiuliza kwanini hii mitihani yote iniandame mimi, nilijiuliza mara mbili tatu kichwani,

Hivi huyu dakitari kasema hivi kwasababu anajua kuwa mama hatapona au kasema hivi kwa vile anajua kuwa sina uwezo huo na kwahiyo mama ataishia kufa tu bila msaada wowote. 

Nikamwangalia yule dakitari huku machozi yakinilengalenga, na huyo dakitari akanitizama usoni halafu akatizama lile faili aliloshika, halafu akamwangalia mama pale kitandani alipolala, na aliponiona amchozi yakilenga lenga machoni akaniuliza 

‘Kwani wewe huna jamaa mkaambizana mkachangishana, kwasababu kwakweli upasuaji kama huo hapa nchini hakuna, na huo upasuaji unahitaji umakini sana, mimi nimemchunguza mama yako kwa makini na ninauhakika kama atakwenda India atapona kabisa,..’akasema

‘Kwahiyo ninachokushauri wewe nenda katafutaneni wanandugu..mchangangishane..., au njia nyingine, tafuteni wafadhili, ili ipatikane hiyo pesa, kwa haraka zaidi, `the sooner the better’, umenielewa lakini…’ akatikisa kichwa, na kuangalia saa yake, hii iliashiria kuwa nampotezea muda wake, kwani dakitari kama yeye ana wagonjwa wengi, ana hosptalini nyingi za kwenda kuwahudumia wagonjwa, na pengine, wagonjwa ambao wana uwezo wao!

‘Sawa dakitari kuhusu hiyo safari nimekuelewa,...tatizo ni hizo gharama... na sijui niseme nini, ina maana kama hazikupatikana hizo pesa, kwa ajili ya gharama za usafiri, eeh na matibabu…, hakuna njia nyingine ya kumtibu mama yangu? nikamuuliza na docta akaangalia saa yake

'Njia sahihi ni upasuaji,...nimeshakuelezea 'akasema

'Sasa docta utanisaidiaje, unaniona nilivyo, hali kama hii,..docta yaani mimi sina kazi kabisa..., sina ndugu, sina pesa, na sina uhai....nipo kama mfu….oh,..nakuomba docta mnionee huruma, nisaidieni....’nikafikia hadi kupiga magoti

Docta akaniangalia na kutiskia kichwa, akageuka na kuanza kuondoka;

‘Sasa docta,…utanisaidiaje….maana ndio nitajitahidi kuombaomba, lakini nakuomba na wewe kama una njia za kunisaidia unisaidie tu, mama yangu akifa na mimi ni heri nife tu…’ nikajikuta nalia kama mtoto mdogo. Niliposema kauli hiyo dakitari akasimama na kunigeukia akasema;

‘Sikiliza ndugu kulia hakusaidii, …njia zipo nyingi za kufanya kaam nilivyokuambia,ni kweli tatizo kama hili ni gharama, mtu mwenyewe ni shidaah...sasa kama huna ndugu, huna uwezo,…nakushauri nenda kwenye redio au runinga tangaza kuwa una tatizo kama hili, linahitaji msaada wa haraka, kuna watu wakisikia hivyo watatoa misaada, wapo watu wanasaidia…’akasema na kuniangalia kwa makini sijui kwanini alikuwa akiniangalia hivyo

'Docta nimeshakuelezea hali halisi.....mimi ni masikini, ukijua tulipotokea huwezi amini, mimi na mama tulikuwa omba omba...basi nikapata mfadhili nikasoma nikapata kazi, ..baadaye nikapunguzwa kazi, na hapo matatizo yakaanza kujipanga, hili baada ya jingine, unavyoniona hapa, ......watu wanahisi nina ukimwi..lakini hii ni shidaa tu docta...'nikasema

'Uliwahi kupima afya yako hilo ni muhimu sana..'akaniambia

'Ndio nimeshapeleka vipimo, na leo natakiwa kwenda kuchukua majibu ya vipimo...lakini docta mimi siumwi...'nikasema

'Anyway, tuache hayo ya kwako, muhimu kwasasa ni mama,...fanya kama nilivyokuambia..'akasema

'Lakini docta sina jinsi..naomba msaada wako....nipo chini ya miguu yako, nisaidie, nakuomba sana docta..'nikawa sasa nalia kiukweli.

‘Nikuambie kitu, usijiweke katika hali ya unyonge kihivyo...., matatizo hayo yapo, watu wanaipitia kwenye matatizo mbali mbali, ...lakini matatizo yasikufanye uwe mtumwa wake...tatizo likitokea muhimu ni kutafuata njia ya kulitatua,....sio kukata tamaaa, jaribu kila njia..'akatulia


'Sasa docta nyia ndio wenye nafasi ya kunisaidia..'nikasema

'Sikiliza, matatizo hayaepukiki, sasa hivi tatizo lipo mezani kwako,..unalo… huwezi ukabakia kulia tu...ujue matatizo ndio changamoto ya kukuwezesha wewe kufanya jambo…ukilia itasaidia nini, na tafadhali usinipigie magoti, maana mimi sio mtatuzi wa hilo tatizo, nakuomba uinuke..’akasema akinishika mkono niinuke lakini sikuwa na hata nguvu ya kufanya hivyo nikabakia vile vile nimepiga magoti…na yeye akasema;.

‘Wapo watu wanaweza kukusaidia , tatizo watajuaje kama wewe unahitajia msaada kama huo, cha muhimi ni wewe kwenda kulitangaza hilo tatizo lako, ili wasikie….mimi kazi yangu nikukusaidia kutafuta tatizo na nimejitahidi sana kwa kutumia vifaa vyangu binafsi, gharama zangu binafsi, ...'akawa anafungua fungua lile faili.

'Nimefanya zaidi ya uwezo....kama ungelikuja kwenye hospitali yangu gharama ingelikuwa kubwa sana, lakini kwa vile nimeamua kumsaidia mama, ndio maana nimejitolea kutoa hadi vifaa vyangu binafsi kwa vipimo toka hospitali yangu mwenyewe ambavyo ni gharama sana,…je ulitaka nikusaidiaje…au unataka nikuambai kile kitu na gharama zake ili ujue nimekusaidiaje...’akasema

'Nashukuru sana docta kwa msaada wako lakini bado nakuhitajia..'nikasema

‘Nimeshakusaidia vya kutosha,…zaidi ya hapo mimi sina uwezo huo, huko sio sehemu yangu tena kuna wahusika wengine…natumai umenielewa…samahani nawahi wagonjwa wengine….’ akasema yule dakitari nakuomba tafadhali kuwa anawahi sehemu nyingine. Sikuwa na jinsi bali niliinuka pale nilipokuwa nimepiga magoti, huku nikipepesuka nikiwa kama bua, nilitembea hadi pale alipolala mama, nikamshika mkono.

‘Mama nifanyeje mwanao, hapa nilipo sina kazi, sina ndugu wa kutegemea…, sina pesa …mama sasa, oh, nifanyeje, mama ukifa na mimi nitakufuatia nyuma, maana sitakuwa na raha maisha yangu yote, nitakosa raha kwasababu nimeshindwa kuokoa maisha yako…mama nifanyeje mwanao, ningelikuwa na nguvu, ningelikwenda hata kuiba,…ningefanya dhambi hiyo….lakini nikaibe wapi…’nikajikuta machozi yakinitoka kama maji

‘Mama hapa nilipo sina nguvu,…sijala, siku ya ngapi leo naishia kula kitumbua…na maji… hata kutembea natembea kwa shida, watu wanadhani nina ukimwi kwa jinsi nilivyokonda,..lakini sio ukimwi, ni shida, njaa,…na yote haya ilikuwa ni kuhakikisha wewe na family yangu mnaishi vyema, lakini imekuwa bahati mbaya. …’nikatulia kidogo nikiamuangalia mama alivyolala, hatikisiki..kinachoonyesha yupo hai ni yale mashie tu.

‘Mama, mke wangu ndio huyo kanitoroka na mbaya zaidi kaondoka na mwanangu…ni sawa uzalendo umemshinda, ni sawa, huenda mtoto angelikuwepo ingekuwa ni tatizo jingine…lakini najua kabisa mama, kama ningelikuwa mimi naumwa kama wewe hivyo, katu usingeliweza kuniacha, kama ningelikuwa mgonjwa kama wewe najua  wewe ungelikuwa pembeni mwangu ukiniuguza, maana wewe ni mama yangu, mama nakupenda, lakini nifanyeje…’nikatulia nikivuta kwikwi.

‘Mama watu wanakimbia wakidhania, nina ukimwi…mama jana nilikwenda kupimwa, na leo nikitoka hapa nakwenda kuchukua majibu kama kweli ninao basi mama nakuaga kabisakuwa hatutaonana tena, na kama sina huo ugonjwa nitahakikisha kuwa nazipata hizo pesa ukatibiwe,….  ikibidi nitakwenda kuiba….’ Nikamshika mama mkono na kuubusu mkono wake huku machozi yakimdondokea mkononi.

Nilitoka mle hospitali nikiwa kama nipo gizani, macho yalikuwa yamejaa utando wa giza na machozi, akili ilikuwa haifanyi kazi tena, mwili ulikuwa kama sio wangu.

Nilitembea huku na yumbayumba, na kuelekea barabarani, nafikiri watu walikuwa wakinishangaa, nilishazoea kushangawa na watu, nilijonea sawa tu.Nilikuwa hata sijui naenda wapi, kwani wakati huo akili zangu zilikuwa zikiwalaani wale mgambo waliomkanyaga mama kichwani, niliwaona kama wao ndio wamemsababishia yote hayo kwa mama yangu . Moyoni nijaa chuki, na nilidhamiria kama nikiwakuta hawo mgambo tena nitafanya la kufanya nikafie gerezani.

***********

 Nikiwa natembea kutoka pale hospitalini, mara ghafla nikasikia magari yakifunga breki miguuni mwangu, nikabakia kubabaika, nisijue nifanyeje, kumbe nipo katikati ya barabara bila kujijua…, na hali kama hii ikanikumbusha siku ile nilipodondoka kwenye lori ambalo nilipanga kutoroka nalo siku ile nilipotoroka shule ya watoto watukutu.

Kumbukumbu hizo zilinijia muda huo nipo kati kati ya barabara, sijui kwanini kumbukumbu hizo zilijia muda ule, nikawa kama nipo kwenye ndoto, niliwazie lile tukio la siku ile, jinsi nilivyokuwa nimelala kwenye kile kisehemu nyuma ya lile lori, na jinsi nilivyopitiwa na usingizi …ndani ya usingizi ule niliota ndoto mbaya…

Ndoto ile ndio iliyonifanya nizindukane na kusahau kuwa nipo kwenye shemu ambayo ni hatari…unajua ilikuwa ni sehemu ndogo sana, na kwa vile nilikuwa bado mtoto, niliweza kujibanza mle, bila wasiwasi.

Jamani, ….niwakumbushe kidogo siku ile…kuna tukio muhimu sikuwahadithia….

Nilijikuta namedondoka chini ya barabara ya lami, na kwa vile gari lile lilikuwa kwemye mwendo, nilidondoka na kuserereka, na ukumbuke nyuma, yalikuwepo magari yanakuja kwa kasi na mojawapo lilikuwa `land cruiser’, ambayo ilikuwa karibu sana na lori letu.

Kwahiyo nilipodondoka, …yule dereva wa `landcuiser’ akawa kashikwa na mshituko kwani hakutegeema kitu kama hicho, alijaribu kufunga breki, na kulipindisha gari pembeni mwa barabara, na kufanya vile akawa kanigonga kidogo na kunusumia nje ya barabara huko huko anapotaka kulipindishia gari lake, kwahiyo nikawa nimetupwa kama mpira.

Sikujua nini kiliendelea baadaye zaidi ya maumivu kwenye kichwa na begani, yalikuwa hayakadiriki na giza likatanda usoni na kilichofuata baadaye ni kupoteza fahamu. Nilipozindukana nilijikuta nimevalishwa mavitambaa mwili mzima, na shingoni kuna limhogo, mkononi hadi begani nimevalishwa POP, pia. Nilikuwa kama sanamu fulani lilofungwa mavitambaa kila mahali. Nikafunua macho kwa shida na mbele yangu nilimuona kasimama mama mmoja.

‘Docta naona kama vile mgonjwa kafungua macho, …ahsante sana mungu, nilijua tumeua…docta tafadhali mwangalie kama anahitaji msaada wowote..’ akasema yule mama.

Docta alinijia na kunitizama , halafu akaangalia mashine yake ya mapigo ya moyo, halafu akafunua mboni zangu za macho, akamgeukia yule mama, na kusema, kuwa mgonjwa bado hajawa vyema, inahitajika muda kidogo kusema lolote. Nikatamani kuwambia kuwa mimi nimepona, wasiwe na wasiwasi , niliona heri nipone haraka niondoke mahali hapo, wasije wale mgambo wakaja kunikamata na kunirudisha huko kituo cha kulelea watoto.

Baadaye nikashikwa na usingizi na ndani ya usingizi huo nilimuota mama yangu akinikanda kwa maji ya moto mwili mzima, na kunibembeleza kuwa nitapona, ilikuwa ndoto iliyoanzia kwa mimi kudondoka kwenye mti na kutegeuka mkono, sasa mama akawa ananikanda maji ya moto, na kuniambia nisitoe kitambaa alichonifunga, kwani nikikitoa mkono hautopana, …’ mara nikashituka toka usingizini na kujikuta nimeshikiliwa na docta…alikuwa akinibadilisha vile vitambaa vya vidonda.

‘Docta nipo wapi mama yangu yupo wapi, namataka mama yangu haraka..’ nikawa napiga ukulele na kutaka kuinuka, lakini yule docta akanishikilia na kuniambia nitulie kwani nitajitonyesha, nilale hivyohivyo…., na wakati nahangaika na yule docta mara akaja mama mmoja, nilikumbuka nilimuona kabla , alikuwa kaongozana na mwanaume, walikuwa wamebeba matunda na vitu vingine, nilitamani kuwaambia nina njaa lakini mdomo ukawa mzito.

‘Docta vipi mgonjwa wetu anaendeleaje…? Akasema yule mwanamke. Nilijiuliza kwanini wanasema `mgonjwa wetu’

‘Hali yake inatia matumaini, unajua kwasababu ni mtoto, haitachukua muda mrefu …atapona haraka sana, sio kama mtu mzima…’ akasema docta.

‘Unanipa matumaini sana docta, kwani tulikuwa na wasiwasi sana, …na natumaini…, hakutakuwa na matatizo zaidi kwani askari wamaona kuwa sio kosa letu, ni kosa la huyo mtoto, sijui alirukaje kwenye lile lori,…unajua hatukujua kabisa katoka wapi, karuka toka juu ya lori au…hata hatuelewi, sisi tuliona mtu huyu, yupo mbele yetu anaserereka, cha ajabu hata lile lori halikusimama kabisa…’ akasema yule mwanaume.

Wale watu walipomaliza kuongea na dakitari waliondoka, na sikuweza kuwajua ni watu gani.

Nilikaa pale hospitalini karibu wiki tatu halafu… nikaruhusiwa nasiku naruhusiwa alikuja yule mwanamke na mume wake, wakanichukua hadi nyumbani kwao na waliniambia kuwa nitaishi nao mpaka watakapokuja ndugu zangu. Niliwaambia kuwa sina ndugu, kwani mama yangu nilisikia wakisema aliruka kwenye gari, na haijulikani kuwa kafa au yupo hai.

Na nyie ndio nawaona kama ndugu zangu , maana msaada mlioutoa hakuna mtu angadiriki  kufanya hivyo..’nikasema

‘Basi usijali wewe tunatishi na wewe hapa na jisikia kama upo nyumbani..’wakaniambia.

Basi ndio ikawa ahueni yangu maana kweli niliishi nao, wakanipa kila huduma ninayostahili, utafikiri mimi ni mtoto wao wakanisomesha, nikamaliza darasa la saba, na nilifaulu kwenda sekondari hadi kidato cha nne,…hapo nikawa mzembe, kujiamini kuwa nina familia ya kifahari, kila kitu napata, matokeao yake nikafeli, sikupata matokea mazuri ya kuendelea mbele…

Maisha ni kupanda na kushuka, hutaamini hawa wafadhili wangu kumbe walikuwa wamejenga na miradi yao yote hiyo ilikuwa ya mikopo, sijui ikatokea nini, na muda huo ndio namaliza kidato cha nne,

Nakumbuka siku nimetoka kufanya mitihani, nikiwa sijui hili wala lile narudi nyumbani nakuta watu wanabeba vitu, na jamaa zangu wamesimama pembeni, nikawasogelea , na kuwauliza kulikoni.

‘Wewe tulia tu, maisha ni kamari leo tumekosa kesho tutapata..’akasema baba yule huku akionyesha hana wasiwasi tofauti na mkewe.

Kumbe kipindi hicho mambo yao yalikuwa sio mazuri, lakini hawakutaka kuniambia, biashara zao zilikuwa haziendi, na walikuwa na tabia ya kucheza kamari kwenye makasino, huko ndipo kulipowaweka pabaya zaidi,  wakawa wamefirisika, lakini walijitahidi kunipa kila kinachowezekana na sikujua kabisa hadi siku hiyo… kiukweli kumbe walikuwa na hali mbaya ya uchumi. Na kumbe walizembea kulipa madeni waliokopa benki na kwa watu mbali mbali, na kwahiyo nyumba yao ya kifahari, magari yao waliokuwa nayo yakapigwa mnada.Wakabakia hawana kitu..

‘Kwahiyo sisi ndio hivyo, tunajaribu kuangalia njia nyingine ya maisha, sasa..hatuna uwezo wa kukusaidia zaidi, kama unavyoona…’wakasema

‘Oh, sikujua, ….’nikasema

‘Lakini usiogope yote maisha,..’wakasema

‘Basi kwa vile hali halisi inaonekana…na mimi nimeshakuwa mkubwa niacheni mimi nikahangaike kivyangu..’nikasema

‘Hapana wewe bado hujaweza kuishi peke yako, kaa na sisi,..kuna sehemu tutajisitiri hadi tujua la kufanya,chochote kitakachowezekana tutasaidiana..’wakasema

‘Hapana ndugu zangu,...wazazi wangu, mimi naona nikizidi kukaa na nyie nitazidi kuwapa mzigo..mimi niacheni nikahangaike, ..., nitajua cha kufanya….’ nilikataa na kuingia mitaani kutafuta maisha.


WAZO LA LEO: Matatizo kwa binadamu ni changamoto ya kusonga mbele, matatizo hukomaza akili na kuweza kufikiria zaidi. Tusiyachukulia matatizo kama bahati mbaya, kuwa labda nimelogwa , labda nina bahati mbaya, tuyachukulia matatizo kama ngazi ya kutupeleka juu, kutufikisha sehemu nyingine ya zaidi, ambayo ni kufanikiwa kutatua lile tatizo na ni maendeleo.

Ni mimi: emu-three

No comments :