Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, May 15, 2015

NANI KAMA MAMA-77‘Kwahiyo mama ikawaje…?’ nikamuuliza nilipoona anataka kuhadithia jambo jingine

‘Mnataka tuendelee na hali ya mama, ok…..’akasema na kutulia vyema.

‘Siku ile marafiki zangu wakanisaidia hadi mama tukafika hospitalini. Mama alikuwa vile vile, na hata wakati tunamteremsha na kumbemba hadi ndani kwa dakitari,  sote tulijua ndio mwisho wa kumuona mama tena. Lakini cha jabu docta alipomchunguza akasema mama kapoteza fahamu tu,.

‘Usiwe na wasiwasi mama yako yupo hai, sijui kwanini unalia…’akaniambia docta aliponiona nikilia.

‘Mhh, …’nikaguna tu huku nikimuomba mungu mama yangu sije akafariki na kuniacha kwenye madeni ya fadhila,…nsjua hakuna anayeweza kulipa fadhila za mama, lakini angalau nipate muda wa kukaa na mama kidogo nimuonyeshe kuwa mimi ni mtoto wake.

Mama akalazwa hapo hospitalini wakimuwekea dripu za maji, mimi nikiwa nimekata tama kabisa, baadaye dakitari akanijia na kuniambia, mama yangu kapoteza fahamu tu, wao wanajaribu kuona kwanini fahamu za mama zimepotea, na wanajaribu kumzindua kwa vifaa vyao lakini hajazindukana bado…je ni kitu gani kilitokea hadi mama yako akapoteza fahamu…?’akaniuliza

‘Hilo la kupoteza fahamu sijui maana imetokea baadaye sana,..ila alidondoka akagonga kichwa ..nikampa dawa ya maumivu, na akaendelea vyema tu, tukawa tunaongea kwa muda mrafu sana,  baadaye ndio hivyo akapoteza fahamu….’nikasema

‘Pamoja na hilo yaonekana mama yako ana matatizo kichwani, …hujui lolote kuhusu historia yake ya nyuma,..labda ana matatizo ya kupoteza fahamu mara kwa mara au ana matatizo mengine…?’akaniuliza

‘Kiukweli mimi sijui sana ila alinihadithia kuwa huko nyuma mimi nikiwa mchanga alipoteza kumbukumbu, akawa hakumbuki chochote, na hilo tatizo lilikuja kumalizika....’nikasema

‘Basi ngoja tumlaze hapa tuone tatizo nini, vipimo vingine bado….’akasema huyo docta, na kuniambia kuwa mimi naweza kuondoka na nije kesho yake, lakini mimi sikuondoka, nikabakia hapo hadi usiku,  mama hakuzindukana kabisa hata baada ya juhudi  mbalimbali walizomfanyia madakitari. Mama alibakia hivyo hivyo kwa siku mbili na ikaonekana hawezi kuzindukana tena, lakini wakimpima bado yupo hai…

Siku ya pili nilikawia sana kurudi nyumbani, kwani ilibidi nihangaike na madakitari kuhakikisha kuwa wanampima mama na kuona tatizo hasa ni nini, na hatimaye nikaahidiwa kuwa yupo dakitari bingwa atakuja kumuona, na huenda ikajulikana tatizo lake ni nini...

Mimi moyoni nikahisi kuwa huenda wanapoteza muda tu, kwa vile sina kitu cha kuwapa, kama ningekuwa na kitu nina uhakika mama angelikuwa keshapimwa na kugundulika tatizo lake…. Na fikira hizi ziliniandama kichwani na kujiona sina maana. Sina maana maana mimi nimeshindwa kumsaidia mtu aliyenisaidia kwa hali na mali….niliumia sana moyo wangu.

Nilijaribu kutafuta vibarua ili nipate chochote, lakini kutokana na hali yangu ya kimwili, kila ofisi niliyofika, waliniangalia mara mbili na kusema `wewe nenda tutakuita baadaye kama kuna nafasi..’ Niligundua kabisa kuwa hawo waajiri walishanihisi vibaya. Ni kipindi kile mtu ukikonda sana wanajua unao…

Siki zilivyozidi kwenda hali yangu ilizidi kuwa mbaya sana, kwani udhaifu wa mwili ulikuwa umenijia kwa kasi, mwenyewe nilijiona kama buwa, mwili hauna nguvu, na hata akili ikawa haifanyi kazi vizuri, kwani nilijikuta naongea peke yangu bila kujijua kama mtu aliyechanganyikiwa. Na watu walishaanza kuninyanyapaa wakijua mimi ninao. Ilifikia muda nikienda kuongea na watu kwenye kundi, ili kupoteza muda, watu wanaanza kutafuta mwanya wa kuondoka eneo hilo na baadaye najikuta nimebakia peke yangu.

‘Rafiki yangu nakushauri kitu kimoja, ulishawahi kupima afya yako, kwani nakuona hali yako sio njema, kwani unasumbuliwa na nini hasa?’ aliniuliza yule rafiki jirani yangu aliyenisaidia kumpeleka mama hospitalini.

Siku hiyo rafiki yangu alikuja hapo ninapokaa, ili kunijulia hali na kunipa pole ya kuibiwa na kutaka kujua hali ya mama, japokuwa walikuwa wakijitahidi kwenda hospitalini kumuangalia mama, lakini siku nyingine wanashindwa, wanakuja kuniuliza mimi.

Hutaamini kuwa, siku ile niliyokawia kurudi nyumbani, nikiwa hoapistlini kumbe huku nyuma, watu tena walikuja wakakusanya kila kitu kilichokuwepo mle ndani. Na nilipodadisi nikagundua kuwa alikuwa ni mke wangu.

‘Sasa kwanini huwaambii polisi kuhusu kuibiwa , maana mtu unayemshuku ni mke wako, na ni kweli alionekana, … watu walimuona akija na gari, hata mke wangu kasema alimuona lakini wakati huo ndio anatoka,..na alipokuja kutaka kujua, mke wako akamwambia mke wangu kuwa hayamuhusu, yeye anajua ni nini anachokifanya, basi mke wangu hakutaka makubwa akanipigia simu, nilimwambia amuambie mjumbe, ..mjumbe hakuwepo…na muda huo mke wako alishaondoka na gari na vitu…’akatulia

‘Nilikupigia simu na ukawa haupatikani..basi tukashindwa la kufanya ,na mke wangu hakuweza kumzuia, …’akatulia

‘Unaju mke wangu yeye alijua labda ni makubaliano yenu, au mumepanga muhame…’akaniambia rafiki yangu.

‘We acha tu…hii safari ya pili, alikuja kumalizia vitu vilivyokuwepo,hata sijui kavihamishia wapi,…wala sihangaiki kwasasa, na siwezi kwenda polisi..’nikasema

`Safari hiyo ya mwisho alihakikisha anachukua kila kitu, hata kitanda hakuna hata sijui nitalala wapi’…nikasema

‘Hata kitanda hakukuachia, sasa utalala wapi…?’ akaniulizia rafiki yangu, baada ya kuniuliza swali la kwanza kuwa naumwa nini, nikawa kimya ..

‘Mimi nakushauri nenda polisi,….’akasema

‘Hapana, hata polisi hawataiamini..’nikasema

‘Kwanini wasikuamini na hali inaonyesha, au unajua kwanini mke wako kafanya hivyo, labda katafuta sehemu nyingine ili muende mkaishi naye huko…?’ akauliza

‘Hata sijui,  mimi hapa najiona kama mfu tu, naona kama walimwengu wameamua kunitenga, yaani kuacha wewe rafiki yangu, sijui kama kuna mtu atakuwa karibu na mimi tena, watu wananikimbia watu wanaogopa hata kunipa mkono kusalimiana na mimi…’nikasema

‘Mhh, lakini ni muhimu ukapime, unajua siku hizi wapo wataalamu wakijua una tatizo wanajua jinsi gani ya kukupa ushauri nasaha…utajiona huna tatizo kabisa…’akasema

‘Mhh,….mimi hapa mawazo yangu ni kwa mama, sijui kama atapona, yeye ndiye mtu wangu wa karibu anayefahamu tatizo langu,…sijui ..sijui rafiki yangu, nahisi kama siku zangu nazo zinahesabika..mama akifa na mimi namuomba mungu aichukue roho yangu….sizani kama nitaishi tena..’ nilijikuta nasema hayo maneno ambayo yalimfanya rafiki yangu aniangalie kwa wasiwasi.

‘Nakushauri tena rafiki yangu, nenda ukapime ujue hali yako…mimi nahisi una tatizo la kiafya, na huwezi ukalijua mpaka ukipima, hata kama ni huo ugonjwa wanaokudhania watu, si ndio itakuwa bora, kwani ukijijua unajipanga vyema, na hata hivyo nasikia kuna dawa za kurefusha maisha…’akasema

‘Mimi sina huo ugonjwa, uhakika huo ninao…labda kama kuna tatizo jingine..’nikasema na rafiki yangu aakniangalia kwa mashaka.

‘Lakini utajuaje kama hujapima..kwani kuna tatizo gani kupima, wanapima bure tu..nenda hospitali ya Lugalo nitakuunganishia kwa jamaa yangu mmoja askari…’akaniambia huku akiniangalia kwa mashaka. Nilishamshuku kuwa hata yeye keshaingiwa na wasiwasi na mimi, sikumlaumu sana, kwani yeyote ambaye angeliniona kwa muda huo angelijua lazima nina tatizo, ninao….

‘Nitakwenda kupima na majibu yangu nitayabandika usoni , ili kila mtu ajue kuwa sina huo ugonjwa kama watu wanavyonidhania mimi, labda…siwezi jua , kama huo ugonjwa unaweza kuingia akilini na kunidhoofisha kia-akili , ukapunguza nguvu za kufikiri …..’nikamwambia huyo rafiki yangu.

‘Unajua rafiki yangu haya yote yametokana na msongo wa mawazo, matatizo mengi yaliyofulululiza…imefikia hatua nikashindwa hata kufikiri jinsi ya kuishi, jinsi ya kuondokana na umasikini nilionao,…labda huo ugonjwa umepitia huko na kama ni hivyo basi ninao, …’nikasema nay eye akaniangalia tu

‘Kama ni huo ugonjwa, … wa kupunguza kinga za mwili , na unapatikana kwa zinaa, au ….labda niupate kwa mke wangu, na nakiri kuwa tangu tuanze matatizo na mke wangu tuna zaidi ya mwaka hatujuani,…sasa , ok, nitapima tu rafiki yangu kama ulivyonishauri…ili niwathibitishie wanajamii, waache kuninyanyapaa’ nikasema nikiwa nimedhamiria kufanya hivyo.

Alipofika hapo akakaa kimia kwa muda kama anawaza jambo halafu akaniangalia na kusema;

‘Unakumbuka siku ile tulipokutana kule Lugalo Hospitali…’ akaniuliza huku akitabasamu, nikatikisa kichwa kumkubalia kuwa kweli nakumbuka.

‘Basi nilikwenda baada ya ushauri huo wa rafiki yangu, nilipofika hospitalini nikakutana na dakitari nikamwelezea nini dhumuni langu, na yeye akanipa ushauri nasaha, akijua kuwa kweli nimeathirika, Nikamsikiliza , huku akilini nikimuomba Mungu, kuwa kama kweli ninao namuomba sana anipe ujasiri wa kuishi ili niweze kuhangaika ili mwisho wa siku nipate hela za kumtibia mama yangu.

Nikajikuta natoa machozi, mbele ya dakitari, hakujua kwa nini natoa hayo machozi, yeye nahisi alihisi kuwa huenda nawaza kuhusu huo ugonjwa, akasema

‘Nakuomba usijali kwasababu kuumwa ni kawaida tu, na ukimwi ni sawa na magonjwa mengine, na dawa yake kubwa ni kufuata masharti, kwahiyo usihofu na usianze kujitwika mzigo kabla haujatua kichwani…’ alisema mengi , lakini kiakili nilikuwa sipo hapo kabisa.

Yaani hata ungeniuliza mengi aliyooongea hapo, nisingeliweza kukuambia, maana sikujua kaongea nini, akili ilikuwa inawaza jinsi gani ya kupata pesa za kumuuguza mama yangu tu..Hata hivyo kama akitokea dakitari , nitamlipa nini ….


Basi siku ile nilipofika kwa dakitari, damu imeshatolewa, sikujua muda ulivyokwenda,….nilisikia tu nesi akisema

‘Twende huku ukachukuliwe damu…’ akasema yule dakiatri, na tulitoka naye hadi chumba cha maabara, wakaanza kutafuta mishipa ya damu, ilikuwa taabu, maana mwili umekunjamana utafaikiri mzee wa miaka nenda rudi..hatimaye wakchukua hiyo damu, nikaambiwa nirudi kesho yake kuchukua majibu. Niliwaomba kama inawezekana niyapate muda ule ule, lakini wakasema haiwezekani muda ulikuwa umekwisha na kulikuwa na matatizo ya umeme. Basi nikatoka kuelekea nyumbani.

Nilifika kwangu , nikatandika mkeka ambao ndio peke yake alioniachia mke wangu, hakuna cha nguo wala kipande cha shuka, nikanyosha ule mkeka na wakati nauweka vizuri nikaona barua ndefu kidogo, nilipoiangalia vyema nikagundua kuwa ni barua kutoka kwa mke wangu.

‘Uliyekuwa mume wangu, natumai hustahili kubakia na chochote zaidi ya huu mkeka, kwani utakufaa wakati  wa kwenda kuzikiwa, na najua kuwa wasamari wema watakusaidia sanda yako. Nasema haya sio kwa kuwa nakuchukia kiasi hicho, la khasha ila ni kwasababu ya kusimamia upande wa mama yako ambaye ndiye chanzo cha hali mbaya tuliyo nayo. Utakubalije mtu aje akuangamize wewe na familia yako, kama na wewe sio njama moja.

Nimeamua kuchukua kila kitu ili mupate muda wa kuwanga usiku, na sizani kuwa mnastahili kulala, kwasabau usiku hamlali…. Mama yako kakulogezea ukimwi, angalia unavyokwisha,…mimi nimeshapima na kuonekana nipo salama, kwani nilikuwa na wasiwasi kuwa huenda umeniambukiza na mimi. Nakushauri uende ukapime, ili uhakikishe kuwa ninachokuambia ni sawa, kuwa mama yako kakulogezea ukimwi..lakini humwi…wewe hulioni hilo,….

Nakutakia maisha mema ..ipo siku utanikumbuka kwa haya ninayokuambia

Mimi niliyekuwa mke wako

*********

Niliichana-chana ile karatasi kwa hasira huku nikumkumbuka mama yangu ambaye alijitolea maisha yake kwa ajili yangu, mama ambaye alinipenda sana, eti leo ageuke kuwa mchawi wa kumloga mwanae, ….

Niliyawaza hayo maneno ya mke wangu kwenye barua, ….nilitamani huyo mke wangu angelikuwa mbele yangu, ningelimfanya kile ambacho asingeliweza kukisahau maishani. Nikiwa pale kwenye mkeka mbu wakinitafuta kumbukumbu za maisha yangu na mama hasa tulipohamia sehemu nyingine baada ya kufukuzwa na mgambo zikanijia…zilinijia kaam njozi…

Tulipokimbia siku ile kuwakimbia mgambo, tulihamia sehemu ya mbali kabisa na pale ,kwani tulisikia kuwa mgambo wanatutafuta sana, wakisema wanamtafuta mwanamke mmoja anayevaa kininja. Nikajua kuwa ni mama, lakini mama hakuwa na wasiwasi akasema waacha waje wanikamate lakini mwanangu sitakutupa, nitakulea hadi uwe dume, dume litakaloniletea wajukuu..basi akianza kuongea na mimi tunacheka, na kusahau machungu ya dunia.

Maisha ya makazi mapya yalikuwa magumu sana, kwani tulikuwa hatuna njia ya kupata kipato, hatuna mtaji wa kuanzia biashara, hatuna eneo la kulima hata mchicha. Basi tukaona ni bora tugeuke kuwa ombaomba mitaani. Na hali ya kuomba ilikuwa ngumu, tulikuwa tukinyanyaswa na hata kupigwa. Na wakati mwingine unaomba unapata kitu kidogo, mwisho wa siku jamaa wenye nguvu zao wanakuja kutuibia, na nilishamwambia mama asipigane nao, maana wanaweza kumuua, na mimi nitabakia na nani, akakubaliana na mawazo yangu, akawa hapigani tena.

Siku moja tulihangaika kutwa nzima hatukupata chochote, mimi nikawa na njaa sana, nikaanza kumlilia mama kuwa nisikia njaa, siwezi kuvumilia, mama akanionea sana Huruma mwanae, akaniambia tuondoke pamoja , ilikuwa jionijioni, tukafika makazi ya watu. Ujue mara nyingi tunajificha nje ya makazi wa watu kwasababu tunatafutwa na mgambo.

Basi tulifika kwenye nyumba, maeneo yanayojulikana kama uzunguni, tukijua huenda hawa matajiri watatupa chochote hata makombo, kwani wao wanakula na kusaza, mabaki wanayatupa majalalani, hawajui kuwa kuna ambao hayo mabaki wanayatafuta lakini hawayapati.

Tulikwenda nyumba moja, akatokea mama mmoja wa Kihindi, au kisomali au Kizungu, hakuwa na sura mbayo moja kwa moja ungesema ni taifa gani, lakini ni Mtanzania, kwani anaongea Kiswahili vizuri, ila lafudhi yake utajua sio Mtanzania asilia. Mama akamuomba atupe chochote, akasema basi subirini niingie ndani nitawapa chochote.

Yule m-mama akaingia ndani , na alikawia kutoka nje, mama machale yakamcheza, akaniambia;

‘Mwanangu hapa naona hakuna usalama, na kama kutatokea fujo kimbia moja kwa moja hadi mfichoni kwetu usijali litakalo tokea….mungu atakulinda…’akaniambia

Wakati anamalizi yale maneno mara ghafla, ikasimama nyuma yatu landrover, ikiwa imejaa mgambo na askari wa kawaida, nikageuka kushoto , halafu kulia ili nipate mwanya wa kukimbia, …wakanidaka kabla sijakimbia.

Mama alipoona hivyo akawa mbogo, wakaanza kumpiga mama kama wanapiga mwizi, na ajabu kubwa niliyoiona ni kuwa mara nyingi wakimkamata mama walikuwa wakipenda kumkanyaga mama kichwani. Mtu wamekamata kadondoka chini wanamkanyaga kichwani. ..Nililia sana,

Na leo hii nalikumbuka hili tukio ni kijua kuwa , hawo mgambo na wanadamu wengine ndio waliomfikisha mama yangu hapo alipo, ndio walionifikisha hata mama hapa nilipo, dunia ilitutenga kwasababu ya umasikini wetu, kwani jamani tuliomba tuwe hivi…tulikosa nini. Wakati nalia na kuomba wasimuue mama yangu, nikawa naimba wimbo wa Huruma nikisema;

‘Mama nakupenda mama, mama naomba usife, nitaishi na nani kwenye hii dunia..,’

Rafiki yangu , machungu ni mengi yaliyonipata siku ile, ila kwa uhakika nakumbuka dakitari aliniambia mama ana matatizo sana kwenye kichwa, kuna athari zimejitokeza kichwani kuna uvimbe kichwani…, ila bado waanzidi kuchukua vipimo vingine kuhakikisha kama hakuna tatizo jingine …

‘Sasa tutafanyaje kuhusu huo uvimbe..?’ nikamuuliza dakitari

‘Kwakweli kwa hapa nchini,mmh …wewe subiria kwanza vipimo vingine kama ni huo uvimbe tu, mama yako atahitajika kufanyiwa upasuaji, na tatizo ni kuwa upasuaji kama huo, hauwezekani hapa kwetu, ….unapatikana India..’akasema.

‘India…?’ nikauliza

‘Ndio..utakuja kuambiwa kila kitu baada ya vipimo vyote kukamilika..’akasema


WAZO LA LEO: Urafiki mwema ni ule unaokuja wakati wa matatizo wakati mtu hujiwezi, hana mbele wala nyum,au wakati mtu unaumwa, anahitajia msaada wa hali na mali, hapo ndipo utakapogundua ni nani rafiki yako wa kweli.  Wengine wanasubiria mtu afe ndio wanafunga safari toka walipo na kujifanya wanajali, waanupendo, upendo gani wa kupenda maiti…ukishaondoka duniani, upendo kama huo hauna maana tena kwa marahemu.
Ni mimi: emu-three

No comments :