Mama wa mitaani , mama ambaye kalazwa
hospitalini, kwa tatizo la kukatwa na mapanga na kuungua kwa moto, moto
uliochuma sehemu aliyokuwa akiishi kwa nia ya kumuangaliza kisa ni kuwa mama
huyu ni mchawi.
Mama huyu hana kumbukumbu za nyuma, huenda
ni kutokana na matatizo aliyokutana nayo, madakitari wamekuwa wakijaribu kila
njia kuzirudisha kumbukumbu zake na pia kujua chanzo cha matatizo yake.
Dakitari anayemshughulikia ni moja watu
waliotumwa kuchunguza matatizo yanayoikumba hiyo sehemu hadi kutokea wazee
akina mama kunyanyapaliwa, kuteswa na hata kuuwawa, kwa visingizio mbali mbali
ikiwemo imani za kishirikiana.
Mama huyu keshaanza kurudisha kumbukumbu,
na kumbukumbu zake zimeanza kumrejea kwa njia ya njozi, kila anchoota ndio
kilichowahi kutokea huko nyuma, japo njoiz hizo hutokea kinamna , isiyo moja
kwa moja, lakini ukiziunganisha na kutumia hekima unajua ni kitu kilichokuwa
kikielezea kwenye hizo njozi.
Mama akawa anaendelea kusimulia hicho
alichokiona kwenye njozi zake, je njozi
hizi zitatufikisha kwenye ukweli wa huyu mama, je huyu mama ni mama kutoka
mbinguni, au ni mzimu, au shetani kama walivyodai watu,
Tuendelee na kisa chetu…
‘Mama yetu, ndoto ndio njia ya kukuelekeza yaliyopita, na kutokana
na hiyo ndoto tunaweza kugundua wapi ulipotoka,…mpaka sasa hatujui mume wako ni
nani, au sio, hatujui ndugu zako halisi ni nani…ndio maana watu wanafikia
kusema wewe ni mama kutoka mbinguni,na wengine wanafikiria vingine….’akasema
docta
‘Wanafikiria kuwa mimi ni mchawi, mzimu au sio..’akasema huyo mama
‘Ndio maana tunahitajia ukumbuke, utuambie kuhusu ndoto
yako,..hata hizo za nyuma, hapo umesema ndoto zako zilianzia siku ile ulipotaka
kuchomwa moto, na hebu kumbuka ndoto hiyo ya mwanzo….’akaambiwa
Siwezi kuikumbuka vyema…ila ninachokumbuka, mmh ehe, ilianzia kama
hivyo tukioa lenyewe, kuwa nipo kwenye moto, nataka kuungua, mara akaja huyo
rafiki yangu..’akasema
‘Nani huyo rafiki yako…?’ akaulizwa
‘Nazungumzia rafiki wa ndoto, sio ukweli, mnielewe hapo…ilionekana
kuwa huyo ni rafiki yangu, maana alikuwa
karibu sana na mimi, ndivyo ninavyokumbuka
‘Ilivyotokea ni kuwa nilikuwa kati kati ya moto, nguvu
zimeniishia..nikawa siwezi hata kuinua mkono,..moto ukawa mkubwa kweli
unazunguka unanisogelea..nikaanza sasa kuungua mguu, …’akasema
‘Mguu uliungua kabisa kama nyma ya kubakika, moto ukazidi
kuongeza, kwahiyo nikajua sasa nakufa….nikahisi mtu ananisaidia kuinuka,
nikajua ni wale wale waliotaka kuniunguza, lakini mkono wa huyu mtu ulikuwa ni
baridi sana, na aliponishika ukawa unaondoa ule ukali wa moto…ni kama maji ya
baridi yamekuja kuuzima huo moto mwilini mwangu, …’akatulia
‘Mhh, hapo siji ilikuwaje, ila baadaye nikapiga ukelele, wa kuomba
msaada nikihidi huyo mtu ni miongoni mwa hao waliotaka kuniua…lakini sauti
haitoki, nikapiga kelele…kelele…kelele…na mara nikahisi nazama kwenye shimo
refu, na kuelekea dunia nyingine...yenye giza....sikumbuki zaidi.
‘Kwahiyo huyo rafiki uliyemuona hhukumuona kwa sura , yaani
kukumbuka kuwa ni mtu gani?’
‘Mhh,…sikumjua kabisa,…kwa
muda huo kwenye ndoto sikujua ni nani, ila nilimuona sura yake,..lakini cha
jabu sikujua ni nani…ila nilipozindukana nikamuona huyo mtu…’akasema
‘Ukamuona kuwa ni baba wa nyumba, baba wa mtoto unayemlea…au sio?’
akaulizwa
‘Ndio ajabu yenyewe, kwenye njozi sikijua kuwa ni yeye alionekana
mtu tofauti, mtu nisiyemfahamu, ila nilipozindukana na kumuona kuwa ndio yeye
ndio nikakumbuka kuea ndiye huyo niliyemuota kwenye njozi..’akasema
Nesi ambaye alikuwa akijifanya kufanya usafi bado alikuwa
akiliwazia hilo na alitamani dada yake awe hewani asikili anachooongea huyu
mama, ..akakumbuka jinsi alivyoambiwa na dada yake..
‘Yaani shemeji yako kabadilika sana, …amekuwa mpole, ..’
‘Kwa vipi..?’ akauliza
‘Hata sijui,..’dada yake akasema
‘Labda na mawazo yake ya kimaisha, muulize maana huyo ni mume wako unatakiwa ujua kama
kuna tatizo msaidiane, vipi kuhuus mtoto…’walipofikia kwenye mtoto wakasahau
kuendelea kuhusu huyu baba mwenye nyumba, na kipindi hicho mawasiliano yalikuwa
madogo, na hawakuweza kuwasiliana tena hadi aliporudi kwenye kozi yake.
Anakumbuka aliporudi, ndio wakakutana na tatizo la huyo mama, na
siku moja dada yake alimuambia tena kuwa shemeji yake amekuwa kama
kachanganyikiwa na hataki kabisa kusikia lolote kuhusu huyo mama…
‘Unamjua shemeji yako,
hapendi kuongea kitu kwa kubahatisha, anaweza akasikia jambo au akahisi
jambo…akakaa kimiya… lakini nina uhakika kuna jambo ambalo linamkera na huenda
linahusiana na huyu mama…maana kuna muda nilimuona kiongea pake yake..na
akaonekana ana jaziba kweli kwelii…mmh mpaka niliogopa…lakini ngoja tusubiri
tuone…
Nesi akakukumbuka swali
aliloulizwa mama, …
‘Unahisi ni kwanini ulimuota huyo mwenyeji wa hiyo nyumba….je
ulimpenda, au yeye unahisi alikupenda…’swali hili lilipoulizwa akatega sikio
kupata jibu, lakini jibu lililotoka halikusaidia kuondoa duku duku lake
‘Hahahaha, hivi mimi kwa hii hali,
…hapana…akili na mawazo yangu muda wote ulikuwa kumtafuta mtoto wangu mapenzi
yangu yote yapo katika kumpata mtoto, sio vinginevyo, na sijui kwanini ikatokea
kumuota,..siwezi kujau hilo..’
‘Hebu tauambie maisha yako ulipokuwa hapo nyumbani , kwa wafadhili
wako ilikuwaje, hukuwahi kuota kuhusu hilo, je hukuwahi kukutana na baba mwenye
nyumba mkaongea, hukuwahi kuota lolote kuhusu kukutana na huyo baba..?’
akaulizwa
‘Kwakweli sikumbuki…..maisha ya hapo siyakumbuki sana, zaidi ya
tukio hilo la moto na jinsi nilivyo fika hapo, na kuwa mtu wa kuletewa watoto,
lakini mengine kuhusu huyo mwenye nyumba, mama na baba,..mmh, hata sura zao
naona kama zimenipotea..’akasema.
‘Huyu mama nahisi anaficha
kitu, sizani kama hakumbuki yote…mimi nikipata muda wa kuongea naye
nitamuuliza…nahisi kuna jambo..., nahisi huyu atakuwa katumwa kuchunguza..huenda ni
kuhusu huyo mtoto, akapewa maneno ya kutungwa kwa watu waliowahi kusikia historia ya tukio hilo, ndio
maana akajifanya hakumbuki..’akawa nesi anawaza akilini.
‘Vinginevyo huyu ni shetani, ….lakini siwezi kuamini hayo moja kwa
moja... sikubaliani na kuwa huyo mama ni yule aliyekuwa kafa na sasa kafufuka....mimi msimamo wangu ndio huo huyu mama simjui , na siwezi kukubali lolote
kuhusu huyo mtoto,…’akaweka msimamo huo.
Na siku hiyo ikapita hivyo
*********
Nesi alipofika kazini akawa na nia ya kumuona huyo mama, lakini
alipofika aliambiwa na manesi kuwa huko wodini hakuna usalama huyo mama
kachachamaa, asiende kuonana naye
‘Eeeh, anasemaje?’ akauliza
‘Hatujui…lakini inavyoonekana kuna tatizo walikuulizia,. Wakasema
ukifia uende ofisi kwa mkuu, ..’akasema
‘Mhh…na huyu docta hapatikani kabisa..’akasema
‘Docta yupo ..?’ mwenzake akamuuliza
‘Aaah, we acha tu…’akasema na kutembea kuelekea kwa mkuu ,
alipofika ofisini kwake, akaambiwa yupo wodini, na maaigizo ni kuwa akifika
hapo aelekee wodini.
********
‘Unajua huyu nesi anajua
mengi…na katuficha mengi….nilimwambia yule mpelelezi ajaribu kumhoji huyo nesi,
lakini huyo mpelelezi anasema muda wa kufanya hivyo bado, anashindwa kumuhoji
kwasababu atamwambia anamuhoji kwa kosa gani….’akasema
‘Lakini tatizo silimeshaonekana, mimi sioni kwanini ashindwe
kumuhoji,….’akasema mwenzake.
‘Sasa sisi kama utawala inabidi tuchukue hatua..maana kama
unavyoona huyo mama kachachamaa…na zipo kila sababu kuwa kweli alikuwa na
mtoto, lakini sasa cha gujiuliza ni kwanini hakumbuki maswala ya mume
wake…’akasema mwenzake.
‘Hilo naona limejifunga sana..kama angefunguka akakumbuka ya
nyuma, tungekuwa na ushahidi wa kutosha, maana mpaka sasa hatujui wapo
alipotokea, na hili linatia mashaka,…na kiukweli hata sisi japokuwa tunatafuta
ukweli, japokuwa tunakubaliana kuwa huyu mama madai yake yanaweza kuwa kweli,
lakini hatuwezi kufanya lolote maana mfano huyo mtoto anapatikana…tunaweza
kweli kumkabidhi mtu wa namna hiyo?’ akauliza mwenzake.
‘Mhh, bado..hatuwezi, japokuwa vipimo vyangu havionyesho kuwa huyu
mama kachanagnyikiwa vinaonyesha kuwa huyu mama kapoteza kumbukumbu…kwahiyo
…kwa tahadhari kwanza ni kujua ukweli tu, ..na huu ukweli tutaupaat kwa nesi,
sasa kwa vipi, na kwanini nesi hataki kutuambia ukweli…’akasema
‘Ngoja akija inabidi tumbane, ikibidi sheria ya utawala ifanya
kazi yake..’akasema
‘Utafanyaje, maana huwezi kumtungia kosa, ana kosa gani , na
huwezi kujua kwaninia nafanya hivyo huenda ni kwa masilahi ya
hospitali…’akasema
‘Tutaona….’akasema na mara mlango ukagongwa
**************
Nesi alipoingia na kuwakuta
wakubwa zake akajua swala ni lile lile, akasalimiana nao na kutulia kusubiri atakalo
ambiwa…
‘Nesi hata iweje usije kuliongelea hilo kwa yoyote
yule hadi muda muafaka ufike, hiyo kwa ni kwa masilahi ya mtoto na usalama
wake..kama mama yake amfariki basi wewe ndiye unabeba hiyo dhamana..’akakumbuka
kauli ya docta kijana
‘Mhh, sasa ina maana muda muafaka ndio huu… na kama muda mufaka wa
kutoa hiyo siri umefika,ni nani wakuamua kuwa lifanyike nini,..’ akajiuliza
nesi, huku akitizama dirishani kukwepa macho ya mabosi wake ambao walikuwa
wametulia wakimtizama yeye.
‘Nesi naona umepita hapo na kuiona hali halisi ya huyo mama, ina
maana hakuna muda tena wa kusubiria…’akaanza kusema bosi wao.
‘Kwahiyo nyie mnataka nifanye nini…?’ akauliza nesi, baada ya
kufikiri kwa mapana na kuona kazi inaweza ikaota mbawa. Bosi wake akakunja uso,
akageuka kumuangalia mwenzake halafu akamuangalia nesi, akasimama na kuanza
kuongea kwa sauti ya ukali.
‘Hivi wewe una akili kweli,..unauliza swali kama hilo eti nyie
mnataka nifanye nini, unamuona yule mama alivyo,…’akasema akionyeshea kidole
kuelekea kule waliokolzwa huyo mama na mgonjwa mwingine akaendelea kusema;
‘Mimi ni dakitari,…mimi ni bosi wako wa kazi, … nahitaji maelezo,
ili niweze kumtibu mgonjwa,…imefikia hatua kumkawiza huyu bingwa, unajua na
majukumu mngapi, anahitajika kwenda kwenye hospitali nyingine, lakini siku ya
ngapia nafika hapa kwetu , ni kwa ajili ya huyo mama…’akasema
‘Na wewe kama nesi wangu ni msadizi wangu wa karibu, siri za
kazini hapa unazijua wewe, leo hii unanificha maelezo ambayo yataweza kumsaidia
mgonjwa, kwasababu zenu za kibinafsi…nesi mimi sasa nakuonya kwa mara nyingine,
kabla sijachukua hatua za kinidhamu,…niambie yote unayoyajua kuhusu huyo mama....na
huyo mtoto yupo wapi….’akasema docta kwa ukali
‘Docta….hapa unaulizia mama yupi, huyu mama au huyo mama
ninayemtambua mimi…?’nesi naye hakutaka kukaa kimia kwa vile bosi wake kaja juu
akajitetea hivyo.
‘Nesi hebu mwangalie yule mama, pale tumemnyamazisha kiaina
akipandisha hasira zake itabidi ukapambane naye wewe mwenyewe, hili sio swala
la kusubiri, ni swala la kujua ukweli, na ulivyosema inaonyesha wazi unajua
kitu, kuhusiana na huyo mama, na huyo mama anaweza akawa ndiye huyu mama.
Nakuuliza tena huyo mtoto ambaye alizaliwa hapa wa huyo mama,….wewe si una
mashaka na huyu mama, lakini unajua wapi
mtoto alipo au sio, hata kama sio wa huyu mama kama unavyodai wewe, huyo mtoto wa
huyo mama unayemjua wewe yupo wapi..?’ akaulizwa
‘Alikufa..’akasema na kuwaacha wale madakitari wameduwaa. Docta
bingwa akageuka kumuangalia nesi, kwa mshangao na huyu mkuu wa hospitalia akawa
kamkazia nesi macho sasa kwa kuonyesha mshangao akasema;
‘Eti nini..nesi unajua unachokisema….na kama ni hivyo, kwanini
hukutuambia hilo muda wote huo, tukamwambia huyo mama, ..hivi kwa hivi sasa
unaweza kumwmbia huyo mama kitu kama hicho akakuelewa..’wakasema.
‘Ndio maana sikutaka kusema, nilijua nikiliongea hilo mtamuambia
huyo mama, na huyo mama ataumia sana, na huenda asiamini…’nesi akasema na
wakati anaongea hilo alisema alikuwa akiiona sura ya dada yake akiwa kalala na
kitoto akionyesha furaha, na aliona huruma kuja kuikatisha hiyo huruma kwa mama
asiyetambulikana na huenda kwenda kumtesa mtoto kwa mama ambaye huenda sio
kweli mama wa huyo mtoto.
‘Mimi siamini kuwa mtoto huyo alikufa, nesi usitake kuharibu
ushahidi, sema ukweli kwanini unaficha hilo tukio je ulimuiba huyo mtoto..?’
akasema docta huyo mwingine, akionekana kweli haamini kauli ya huyo nesi, na
docta mwenzake akamtupia jicho halafu akamuangalia nesi.
‘Ina maana mumefikia hatua hiyo ya kutokuniamini mimi, mnamuamini
huyo mama, mama ambaye hajulikani wali alipotokea,…mama ambaye hana kumbukumbu,
inaonyesha anayoyaongea ni ya kubahatisha tu…hivi mfano kama ningelikuwa na
huyo mtoto tunamkabidhi huyo mama, mtoto huyo anakwenda kuwawa, mtakuja kusema
nini….mimi, nawashangaa sana mabosi zangu au ndio mnatafuta visa vya kunifukuza
kazi..’akasema
‘Nani kazungumza maswala ya kufukazana kazi hapa…, hili ni jambo
la utendaji na kama itafikia huko basi mahakama ndio itaamua, maana kuna madai,
na haya madai yamekuja hapa kwenye utawala, na huyo mama keshasema akitoka hapa
anakwenda mahakamani kushitaki,…sisi tumeamua kwanza kumzuia kiaina tukijua
kuwa bado yupo kwenye mamlaka yetu yupo kwenye matibabu..’akasema
‘Kwanini mumuzuia muacheni aende mahakamani, na huko ukweli
utajulikana…’akasema nesi, moyoni akijua kuwa hilo kalitamka tu ili kuonyesha
msimamo lakini aliogopa hilo lisije kutokea.
‘Nesi unatupotezea muda,
mimi ni mtaalamu wa mambo ya akili, huyo mama alikuwa kapoteza kumbukumbu, na sasa
kumbukumbu zake zinaanza kurejea hatua kwa hatua, na ili kuweza kumsaidia zaidi
ni kumpata huyo mtoto, hili litampa faraja na ataweza kukumbuka yote ya nyuma…unanielewa..’akasema
docta.
‘Nimekuelewa bosi haya niambia huyo mtoto mnayemtaka nyie yupo
wapi ili tumuambia huyo mama, maana mimi nimeshawaambia ukweli..’akasema nesi
na wale madocta wakaangaliana na mkuu akasema;
‘Nesi, chunga sana hiyo kauli yako unajua nikiiweka kwenye
maandishi ni jambo jingine…’akasema
‘Nesi wewe hapa, ni mwenyeji kuliko sisi, na huyo mama
keshakunyoshea kidole wewe kuwa ndiye uliyemchukua mtoto wake, na lile kovu
tumboni linadhihirisha ukweli kuwa alijifungua kwa upasuaji ,je kwani kuna siri
gani iliyopo kuhusiana na huyo mama uliyesema unafahamu tukio lake…? ‘ docta
akawa anasema kwa sauti ya chini.
‘Docta ndio ni kweli mimi nipo hapa kwa muda ukilinganisha na
nyie…na nilisema kuwa kulikuwa na tukio la mama moja lilitokea miaka iliyopita, nakubali na
nilikuwepo,na mama huyo alikuja kufariki.. ..lakini mimi sikuwa mhusika mkuu,
wahusika wakuu waliokuwepo kipindi hicho, akiwemo docta bingwa wa akinana mama.
wote hao kwasasa hawapo hapa kwanini mje kunitupia lawama hizo, kwanini
mnanibebesha mzigo ambao sio wangu…, ‘nesi akasema.
‘Ok, hata hebu tuambie huyo mama unayemzungumizia wewe alijifungau
mtoto kwa upasuaji, mtoto wake akachukuliwa na nani?’ akaulizwa
‘Watakujibu wahusika, mimi sio msemaji wao..’akasema nesi
‘Wewe unajua fika kuwa madocta waliokuwepo hapa hawapo, aliyekuwa
mkuu kakimbilia nchi ya jirani kutokana na makosa mbali mbali..tunafanya
taratibu za kumrejesha kuja kujibu mashitaka…..na wewe mama kakunyoshea kidole
akuwa ndiye uliyemchukua mtoto wake, hata kwenye ndoto kakuona….’akasema
‘Unasema anaitwa kuja kujibu mashitaka!?’ akauliza kwa mshangao.
‘Ndio ulijue hilo…uliwaona watu wa usalama walikuja hapa,
hujiulizi kwanini…kuna mambo mengi yalifanyika hapa ubadhirifu, na kushiriki
katika kuficha ukweli kwa matukio yanatokea huko kijijini yakiwemo ya mauaji…ni
mambo mengi kidogo, na hayo yanafanyiwa uchunguzi, huyu mama anadhihirisha hayo…sasa
je upo tayari kuwalinda wahalifu…?’ akaulizwa. Nesi kwanza akabakia kimia
akiwaza, lakini akakumbuka kuwa hilo analolifanya ni kwa masilahi ya mtoto, ni
masilahi ya dada yake….na huyo mama siye muhusika, kwahiyo akikubali basi
atakuwa kavunja ahadi na litakalotokea kwa huyo mtoto atakuja kujialaumu maisha
yake yote..hapo akasema;
‘Mnaposema mashitaka, na mimi mkaniunganisha, si mlitakiwa
kunifahamisha kwa maandishi,…kuwa nashutumiwa..mbona hamjaniambia hilo….halafu
mimi nitajuaje hayo….kuwa kuna mashitaka…je mimi name nimo kwenye kundi la
washitakiwa..?’ akauliza?’akasema
‘Kwahiyo wewe unataka uarifiwe kwa maandishi kuwa ni mshukiwa…unataka
hilo sio….?’ akaulizwa
‘Lakini mabona wangu mbona siwaelewi, mumesema kuma mashitaka,ndio
maana hawa watu wa usalama walikuja, na
kiutaratibu kama kunamshitaka, ningelifahamishawa ki maandishi….’ akasema yule
nesi huku akikunja uso kwa kutafakari.
‘Kama ndivyo unavyotaka sawa..lakini usije kutulaumu kuwa
hatukukusaidia, mimi naona tuachie sheria ifanye kazi yake ..si ndivyo
unavyotaka nesi….?’ Akauliza docta
‘Hapana mkuu, tusikimbilie huko, hili tunaweza kulimaliza kwanza
hapa,..muhimu tuone tutamsaidia vipi huyu mama, tukikimbilia huko…nahisi hata
nafasi ya kumsaidia huyu mama itakuwa ni ndogo..’akasema bingwa
‘Lakini si mumesema mashitaka tayari kinachofanyika kwa sasa ni
uchunguzi au sio,…basi mimi naomba nikamtafute wakili ..’akasema.
‘Ok, nesi wewe unaweza kwenda, tuache tuangalia tutakachoweza
kukifanya, ila kaa ukifikiria kuwa wewe ni mwanamke, hebu fikiria umejifungua
na yakakutokea kama ya huyo mama, unatafuta mtoto wako,…..’akawa anaongea
dakitari
‘Naombeni muda nikalitafakari na kama limefika mahakamani niweze
kutafuta wakili maana naona mnanibebesha mzigo ambao sio wangu…..’akasema
Na wakati nesi anatoka,
akaona mama mmoja akitokea kwenye ile wodi ambayo alilazwa yule mama na
kukimbilia wodi ya wazazi , mama huyo alijifunika kama yule mama wa mitaani,
nesi akaamua kumfuatilia huyo mama kwa nyuma
akihisi ni yule mama katoka. Alikimbia hadi kwenye wodi hiyo ya wazazi, na
kukuta mhusika pale naye katoka, akaaanza kuhisi wasiwasi.
‘Vipi mbona upo mbiombio…’ akagutuka na kugeuka nyuma, na nesi
aliyekuwa zamu kwenye wodi hiyo ya wazazi alikuwa kabeba sinia la dawa na vifaa
vingine.
‘Nahisi kuna mama kaingia humu, ambaye hastahili kuingia humu,
na…’ akasema nesi mkuu kumuelezea huyo nesi mwenye zamu na wodi hiyo, na kabla huyo nesi hajajibu kitu mara wakasikia sauti ikiita kutokea ndani kwa ukali...
‘Wewe nesi upo wapi, nataka mtoto wangu…’
NB : Hapa tulikuwa tunamalizia sehemu iliyokuwa imebakia, kabla hatujaingia sehemu nyingine muhimu, tuwepo pamoja.
********
WAZO LA LEO: Maswala ya dini na imani ni kama sheria,
huwezi ukayajua mpaka uyasomee na ujue mantiki yake. Watu siku hizi hujifanya
kujua maswala hayo ya dini wakawa wasemaje wakuu, na hata kuzua mambo bila
kujua athari zake,….
Tukumbuke kuwa kila fani ina namna zake, masharti yake, na maana zake, ndio maana kuna wataalamu wa
hiyo fani, tunapoingilia dini nyingine na kujifanya tunajua zaidi kuhusu hiyo
dini, na hata kuweka uwongo ili dini hiyo ionekane mbaya sisi tunakuwa waongo, tujiulize
tunamdanganya nani, na kama ni kiongozi au wa imani nyingine ukaweka uwongo kwa
dini nyingine, huoni kuwa unakiuka uadilifu wako, wewe sio mkweli hata mbele ya
mungu, …..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment