Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, April 14, 2015

NANI KAMA MAMA-57 Yule mama alipofika pale mlangoni akasimama, hakushika mlango,...alishika kichwa , halafu akashusha mkono,  dakitari akasogea na kushika kitasa cha mlango, akafungua mlango na kusema;

‘Haya unaweza kuingia,usiwe na wasiwasi….'akaambiwa 

Yule mama alionekana kusita, kwanza akabakia amesimama, …dakitari akamshika mkono, wakaingia wote …

Walipoingia ndani jicho la kwanza la huyo mama lilitua pale alipokaa nesi, na ghafala akasimama..., akaupachua mkono wake kutoka kwa yule dakitari,  akawa kasimama na na taratibu akaanza kutembea kuelekea pale alipokaa nesi…

Mkuu wa hiyo hospitali akasimama, na yule ofisa usalama naye akafanya hivyo, ambaye hakuonekana na wasiwasi alikuwa dakitari aliyekuja naye alikuwa kasimama mlangoni akimuangalia nesi,


Nesi, akawa anaonyesha wasiwasi, macho ya woga yakamtanda …..

 Nesi alipoona huyo mama anamjia yeye, huku akijaribu kumuangalia macho yake kwa kupitia sehemu ile iliyoachwa kwa ajili ya macho, na kujaribu kuhidi kuwa macho ya huyo mama yalikuwa yamebadilika kwa hasira...na macho hayo, yaliweza kupenya hadi nyoyoni mwake, na kujua kila anachokiwaza....ndivyo alivyohisi huyo nesi kwa sekunde chache zile, akahis yupo hatarini..

Tuendelee na kisa chetu...

Nesi akiwa katulia akajipa moyo,...kwa uapnde mmoja hakuamini kuwa huyo mtu , kama kweli ni huyo mama, ambaye alikuwa kafa na sasa kafufuka basi huyo ni shetani na kama ni shetani hamuwezi mwanadamu mwenye udhabiti, ila anaweza kumshinda mwanadamu kama moyo wake ukiingiwa na hofu, na yeye hapo akajitahidi kujidhatiti, akaiondoa hofu

Nesi akamnyoshea kidole huyo mama na kuanza kuongea kwa sauti...

‘Hata kama wewe ni shetani sikuogopi, mungu atanilinda, hata kama wewe ni mwanga umekuja kutaka kunidhuru, sikuogopi , mungu atanilinda ... 

'Wewe ni mwanga, au shetani au mzimu, angamia kwa jina la mwenyezimungu....najua wewe ni mzimu, umekuja kutaka kumchukua mtoto ambaye sio wako, ukamnyonye damu yake..., mimi siwezi kukubali...mungu atanilinda, mungu atamlinda huyo mtoto unayemdai......’nesi alijikuta akiongea, na kuwafanya waliokuwepo humo ndani kumuangalia kwa mshangao.

‘Kwa nguvu za muumba kama wewe ni shetani, kama wewe ni mzimu, rudi huko ulipotoka,...angamia na tokomoea huko ulipotoka...’nesi akawa anaongea akinyosha mkono kama anakemea, wakati huo wengine wote walikuwa kimia.

Yule mama aliyekuwa akimsogelea, amabye sasa alishakuwa karibu na huyo nesi, akawa anainua mikono kumkabili nesi,...sijui ni kutokana na hayo maneno, au sijui ni kitu gani kilimfanya asite, kwani ghafla alisimama...

 Ghafla akatulia na mikono iliyoanza kuinuka kutaka kumshika huyo nesi,ikarudi chini,....na mara akainua mikono na kushika kichwa na haikupita muda akaanza kuyumba, na kama asingelikuwa yule dakitari kuwa karibu naye huyo mama angelidondoka , lakini dakitari akamshika na akawa anahangaika naye kumweka sawa

‘Vipi tena....’aliyesema hivyo alikuwa ni askari, na wote wakasimama sasa wakihangaika kumshika huyo mama, ambaye alionekana kama hayupo sawa...

‘Mnaona...mnaoona.......’ilikuwa auli ya nesi ambaye alikuwa kasimama pale akiwa haamini, japokuwa aliyatamka hayo maneno, lakini bado akilini alikuwa hayaamini hayo aliyoyasema, lakini kwa namna nyingine akajua yamefanya kazi,.....

‘Ina maana huyu mama ndiye huyo mama...ni mzimu wake,.....kama ni yeye sikubali hata mara moja kumchukua mtoto wetu...’akasema kimoyo moyo

‘Naona hali sio nzuri..’akasema dakitari aliyekuja na huyo mama..., na ikawa kazi ya kumweka huyo mama kwenye kiti, lakini haikuwezekana....wakamlaza sakafuni, na haraka dakitari mwingine akaitisha kitanda maalumu cha kubebea wagonjwa, ....na baadaye yule mama akabebwa na kurudishwa chumba maalumu cha wagonjwa wa dharura...

 Yule mama akafanyiwa huduma ya kwanza, na alionekana kama kapoteza fahamu....waliokuwa wanahangaika walikuwa madocta, kwani kwao wao walijua kuwa huyo ni mwanadamu tofauti na dhana iliyjijenga, ...

********

Nesi , docta wa magonjwa ya akili na mkuu wa hospitali, walikuwa wamekaa kukizungua kitanda, alichokuwa kalala huyo mama, na wale watu wa usalama bado walikuwa kule ofisini kwa huyu mkuu wa hiyo hospitali, wakisubiria taarifa kwa hamu kutoka kwa wataalamu hawa;

Wao kama watu wa usalama wasingelwieza kuingia chumba hicho maalumu cha wagonjwa mahututi, lakini pale walipoachwa kila mmoja alikuwa na lake kichwani, hasa walipona nesi anakemea, …kama vile huyo mama ni shetani au mwanga, na ghafala mama huyo akadondoka, basi kila mmoja alipeleka akili yake kwa runinga jinsi watu wa dini wanavyokemea mashetani na watu kudondoka..

‘Yawezekaan huyu mama kweli alitekwa na shetani….’akasema ofisa huyo wa polisi

‘Kwanini…?’ akauliza mwenzake

‘Huoni nesi kamkemea, kasema kama ni shetani lishindwe..na ghafala mama akayumba na kudondoka..wewe huoni kuwa huyo mama ana mtindio wa namna hiyo..’akasema

‘Unaamini hayo mkuu..?’ akauliza

‘Aaah,unajua kuona kunaweza kukupelekea kuamini,nimekuwa nikifuatilia tatizo hili na nimesikia mengi…na kama nilivyokuambia niliambiwa huyu mama katekwa na shetani, sasa kwa hili linanionyesha kuwa kunaweza kukawa na ukweli..’akasema

‘Mhh, mimi sijui…sina uhakika,…lakini ..mmh haya mambo siyakuamini sana,…ngoja tuone wanasema nini hao watalaamu, lakini ulisema huyo mama hilo shteni likimtoka anakufa, au sio…’akasema

‘Ndio wasiwasi wangu huo..’akasema

‘Sasa kama hakufa, …’akasema

‘Ina maana …kuna uwongo, ina maana halijatoka, ina maana..oh, unajua mambo kaam haya ya kiimani, yasiyo naushahidi, mmh hayatufai, kama wataalamu wa usalama, cha muhimu tusubirie..ila nataka nipate muda wa kuonana na yule mama tena..’akasema

‘Mama yupi?’ akauliza

‘Yule niliyeongea naye na kuaniambia kuwa huyu mama sio binadamu wa kawaida,…’akasema

‘Kwanini, atakusaidia nini mama kama huyo aliyetekwa na imani za kishirikina..?’ akauliza

‘Mimi nahisi yeye ndio hao hao, wale watu wanaodanganya wenzao kuwa ukipata mwili wa mwanadamu unaweza kuwa tajiri….’akasema

‘Oh…umefikia kuamini hivyo lakini yeye sio mganga wa kienyeji….utamshukuje…?’ akamuuliza

‘Lakini watu wanakwenda kwake kutabiriwa mambo yao, keshakuwa mpiga ramli yule..na anachowaambia watu wanaamini….kwa vile mengi aliyosema ynakuja kuwa kweli…kibahati nasibu na huenda..ndio nguvu za giza…na anaweza kutumia mwanya huo kufanya lolote…’akasema

‘Mhh…, ngoja tuone, ngoja tusubiria huyu mama atakuwaje, ..’akasema

‘Ni sawa..ila hayo ndio malengo yangu, nataka haya mambo tuyaangalai kiundani zaidi nahis yanajengwa kuanzia mabli sana, kuna mtu, kuna kitu…..’akasema

‘Ok, nimekuelewa, sasa na huyu nesi, unamwamini…?’ akauliza

‘Mhh,… nahisi kuna jambo anaficha…na leo tulitaka tulibaini kwakupitia kwa huyo mama,....lakini naona haliimevuruga, na sijui kafanya hivi ili kuvuruga huo mtegoo…ila kwa vyovyote iwavyo,...na yeye ni lazima afike kituoni huko tunaweza kumbana vyema, nahisi ana jambo anaficha…’akasema

‘Yah…nahisi…..’akasema mwenzake.

************

Huku kwenye chumba maalumu nako kulikuwaje…


‘Naona keshazindukana....’akasema docta bingwa wa magonjwa ya akili na mwenzake akathibitisha hilo, wakamsogelea huyo mama, nesi akawa kasimama pembeni, kdogo akiwaachi hao wataalamu wafanya kazi yao, na kama kuna kitu cha kufuatilia awajibike.

Nesi alikuwa amesharizika kuwa huyu mama sio mtu wa kawaida na kama ni mtu wa kawaida basi atakuwa alitekwa na mapepo… na akili ya kusema huyo mama ni mzimu, haikuwa ikikubali.

‘Lakini kama ndio yeye, ….kama anavyodai, basi huu ni mzimu, huyu ni shetani na akianza kuniandama tu, nitamkemea,..nitamuomba mungu amuangamize, akawa sasa anakumbuka mengi jinsi ya kuomba kinga kwa mungu kwa mambo kama haya…moyoni akawa anaomba, anamuomba mungu ampe kinga…

‘Mama hebu tuambie..unajisikiaje....?’ akauliza docta akimuangalia huyo mama, nesi akshituka kutoka kwenye maombi yake, ina maana huyo mama keshazindukana, na sasa anaweza akaanza kumuandama tena,…..hapana…

‘Kichwa .....kichwa kilikuwa kinaniuma sana...na kilianza pale tu nilipoingia kwenye kile chumba, sijui ni harufu ya madawa, sijui …hata sielewi…na hata huyo nesi alipoanza kuongea…, yaani alikuwa kama anakizidisha kichwa kwa maumivu, na maneno yake yakazidi kunipandisha hasira, …’akasema

‘Hasira za nini?’ akaulizwa

‘Hasira za nini, ina maana hamjaniamini…’akasema
‘Tunataka tusikie ukweli wote, ..sio kwamba hatujakuamini, lakini ni vyema ukatupa ushahidi ili tuweze kutimiza wajibu wetu…’akasema

‘Najua huyo ni mwenzenu, na ni lazima mumtetee, lakini mimi sitakubali,…tutafikishana mbali....’akasema

‘Tunakuomba utilize kichwa chako, unajua ukizidi kupandisha hasira na ndio kichwa kitazidi kuuma, hebu tuambie sasa unajisikiaje?’ akaulizwa na alikaa kimia kwa muda, halafu akasema;

‘Mhh.....bado....’akatulia

‘Unasikia maumuvu wapi,kichwa au unajisikiaje..?’ akaulizwa

‘Maumivu hapana…kichwa kimepoa,… lakini nahisi kama sipo sawa, nahisi kuna kitu bado hakipo sawa… akili inaniwanga ....’akatulia

‘Akili inakuwaje, unakumbuka vyema yaliyotokea…?’ akaulizwa

‘Mmmh nayakumbuka sana, ndoto imenisaidia,…ndoto imenipa imenikumbusha mengi sana, nilijua tu hiyo ndoto inanielekeza jambo.....na ni kweli ilikuwa hivyo.....’akasema

‘Hiyo ndoto imekuelekeza nini?’ akaulizwa

‘Ni kweli kuwa....nina mtoto....na kitu kinachonisumbau ni kama nilikuwa na mtoto , mtoto wangu yupo wapi, nilimuona nesi akimchukua,  huyu nesi...nesi...nesi...kwanini…nitamfanya kitu mbaya…’akasema akionyesha kukasirika, na nesi pale aliposimama, akawa hana amani, yule mama alikuwa hajamauona kwa jinsi alivyolala.

‘Kwani hiyo ndoto ni ndoto gani,.....?’ akauliza docta mwingine, akiwa anamuangalia huyo mama kwa mashaka, akamtupia mwenzake jicho, kutaka uhakika kwani waliona huyo mama anastahili kupumzika, lakini kwa hali aliyo nayo hatakubali kufanya hivyo.

‘Au upumzike kidogo, tutakluja kuongea vyema baadaye….’akaambiwa

‘Ni pumzike,…nyie mna akili kweli, nimewaambia akili hapa inaniwanga, nataka …..namtaka mtoto wangu…hilo ndilo la kunifanya nipumzike, …ndoto itanirudia tena na tena…mpama nimpate..’akasema
‘Basi hebu tuambi kuhusu hiyo ndoto yako….’akasema docta

‘Hiyo ndoto hahahaaah…ni ndoto ya ajabu, na nimekuwa nikiiota mara kwa mara.... , na hayo niliyoota japokuwa yanakuwa katika hali ya kimaajabu, kinamna ya tofauti ...lakini yananionyesha ukweli fulani,...na imenisaidia kukumbuka mambo yangu ya yanyuma….kutoka na hiyo ndoto sasa nimeamini...’akasema akawa kama anataka kuinuka.

‘Wewe tulia tu,...wala usisumbuke kuinuka, mwili bado unahitajia kupumzika... hebu tuambie umeota nini…?’ akauliza dakitari wa magonjwa ya akili....na nesi aliyekuwa kasimama akashika kidole shavuni akitabasamu kuonyesha dalili ya kutokukubaliana na hayo anayoongea huyo mama.

 ‘Unajua hata nikiwaelezea ilivyokuwa mnaweza hata msinielewe ‘ akasema

‘Wewe tuelezee tu...tutakuelewa....sisi ndio kazi yetu mimi hapa ni docta mtaalamu wa mambo hayo …’akasema docta na huyo mama akatulia kama anawaza jambo

‘Ilianza ghafla tu…nipo sehemu... nipo sehemu yenye ubaridi sana, ...sijui ni wapi, lakini kwa akili yangu nilijiona kama nipo kati kati ya msitu mkubwa....maana kulikuwa kumetulia kimya,...’akasema na kutulia kidogo kama anajaribu kukumbuka kitu.

‘Msitu!,. Msitu gani huo....?’ akaulizwa

‘Sijui...nilihisi hivyo tu, akili ilinituma nifikiri hivyo...’akasema

‘Ehe, hapo msituni ulikuwa unafanya nini…?’ akaulizwa

‘Ni kama nimelala….sasa sijui ni kitandani aua kwenye majani..lakini nimelala
nimenyooka,...siwezi kuinuka....ilikuwa kama ...sijui lakini nilijua kuwa nimelala hivyo, na siwezi kufanya chochote zaidi ya kulala, na kuwaza tu...kuna muda nilitamani niinuke, lakini mwili ulikuwa kama sio wangu.....kiwili wili kilikuwa kama sio change, change ni akili ya kuwaza tu..’akatulia

‘Lakini ulijiona ukiwa mtu kamili, au ulikuwa mfu, au ulikuwaje....?’ akauliza docta

‘Hapana, sio mfu....sikuwa nimekufa,labda nilikufa, lakini hapa sijui......sio hivyo kutokana na hiyo ndoto nilikuwa nimelala...mwili ulikuwa hauna nguvu ya kufanya chochote..., nilichokuwa nacho ni akili, kuwaza tu...’akasema

‘Ulikuwa peke yako..?’ akaulizwa

‘Ndio nataka kukuelezea ilivyokuwa baadaye…’akasema

‘Ehe….’akasema docta

‘Nikiwa hapo nimelala, ghafla nikajiona nimezungukwa na watu warefu waliovalia majoho ya rangi…kama hayo mnayovaa mkienda kufanya upasuaji na usoni wamejifunika kuficha sura zao, na kuachia sehemu ya macho tu,... na wote walinizunguka mimi.

‘Hao watu uliwaona..ina maana ulikuwa macho...unawaona kwa macho yako hao watu...au ndio ukiwa nusu mfu...au ..unawaza?’ akaulizwa.

‘Hapana, sio kuona kwa macho haya...usiseme neno mfu, sikuwa nimekufa bwana..mnielewe, hakuna cha kufa hapo, ...ila, macho yalifumba, si nipo usingizini,... naota..kinachofanya kazi hapo ni akili, mwili umetulia kabisa..lakini unajiona kwenye matendo, ila mimi kwa upande wngu sikuweza kufanya matendo...naona kama mwili ulifungwa, sio kwamba hapana hauwezi kufnya kitu....hauna nguvu ya kuinuka...ila naona kila kitu kwa macho ya ndani akilini ...na ninaowaona watu wanavyofanya kazi, wanatenda, ila mimi sikuweza kufanya lolote.....’akasema

‘Ina maana wenzako uliowaona kwenye ndoto wanafanya kazi kama kawaida, na vitendo kama kawaida, ila wewe huwezi kufanya hivyo, ....na hao watu walikuwaje...?’ akaulizwa

‘Watu hao...wao walikuwa wanafanya  kazi, vitendo kama kawaida...ila sasa maumbile yao, ni ya ajabu kabisa.....’akatulia kidogo

‘Wao walikuwaje, ni binadamu au mashetani…?’ akaulizwa

‘Wao walikuwa warefu, wakubwa,..ni mijitu.....na siweza kuwaona kwa ukamlifu,..kwa muda ule kwanza sikujua ni nani na wanataka kufanya nini kwangu, lakini zikanijia hisia,...kuwa hao ni wachawi, au ni mjitu tu....na wanachotaka kwangu ni kula nyama yangu, ....’akasema

‘Kwanini wale nyama yako....au ulihisi tu hivyo?’ akaulizwa

‘Nilihisi hivyo tu....lakini kitu kingine kilichonifanya nihisi hivyo ni kwa vile walikuwa na vifaaa, kama mavisu na mikasi mikubwa sana...masindano makubwa sana..yaani kila kitu kilikuwa kikubwaaaa.....’akatulia

‘Sasa kwanini ulihisi kuwa ni wachawi...?’ akaulizwa

‘Hata sijui, nahisi ni akili za kibinadamu zilivyo,...jambo la ajabu akili zetu zinakimbilia huko, kwahiyo kwa hisia zangu nikajua ni wachawi, au mashetani....au mijitu kama nioliyowahi kusoma kwenye vitabu vya Sinbad…’akasema

‘Walikuwa wanavitu gani zaidi ambavyo wachawi wanavitumia....?’ akaulizwa

‘Mhh, zaidi ya kuvaa nguo nyeupe, na kujifunika nyuso zao...sikuona kitu kingine ambacho wachawi tunaambiwa ndivyo walivyo....hisia tu  ndizo zilinituma hivyo.....zaidi walikuwa na mamikasi makubwa....mavisu...yaani kwa ukubwa naona kama mapanga....’akasema

‘Ehe,...walifanya nini?’ akaulizwa

‘Kwa hisia nilijua wanataka kugawana mwili wangu....’akasema

‘Walifanya nini mpaka ukahisi hivyo..hebu elezea walivyokuwa wakifanya?’ akaulizwa

‘Kuna mmoja wao alikuwa karibu yangu akiwa kainamia upande wa tumbo langu...tumbo lenyewe nilikuwa silioni, nahisi tu kuwa nina tumbo..., na ilionekana kama anaagiza visu na vifaa vingine ambavyo vilionekana kama mapanga yenye ncha kali, ...akilini mwangu nilijua ndiye kiongozi wa kugawa nyama kwa wenzake...’akasema

‘Nilimuona  huyo aliyeinamia kwenye tumbo langu,  kila mara alikuwa akikirudisha kifaa au kukisogeza pembeni kifaa alichotumia kikiwa kimejaa damu. Nikajua ni damu yangu, inatokea sehemu anazokata nyama yangu...Niliwaona ni watu wasio na huruma...walionekana hivyo, japokuwa walikuwa wameficha nyuso zao....niliyemuogopa zaidi ni huyo aliyekuwa kaniinamia, maana niliona hasiti kufanya anachokifanya...’akasema.

‘Wakati wanakata nyama, ...ulihisi maumivu....?’ akaulizwa

‘Hapana..hakuna hisia yoyote ya maumivu....hakuna ninachokisikia kama kagusa kitu, hapana, sihisi kitu,akili tu inawaza hivyo...’akasema

‘Kuna muda nilijaribu kuinua kichwa kuwaomba wanihurumie na kuniacha huru, lakini sikuweza kuinua hata sehemu  ndogo ya mdomo wangu, nilikuwa nimelegea mwili mzima, na hata akili ilikuwa ikiwaza tu kuwa sasa wanafanya hiki au kile, kwa macho naona, lakini sio kwa macho haya, ni macho ya akilini.

‘Nilijua kabisa huko tumboni au sehemu yote ya chini kutakuwa hakuna kilichobakia tena, na sikuweza kuhisi maumivu, kwani ilikuwa kama sio sehemu ya mwili wangu, akili tu ndio ilikuwa ikifanya kazi....mnielewe hivyo…’akasema

‘Muda ukawa unapita, nikajua sasa labda wameshatoa utumbo na kila kitu sehemu ya tumbo langu..., maini, na sehemu za ndani, lakini sikuona hizo nyama, au utumbo vikitolewa nje, ial nilihisi tu kuwa wamefanya hivyo

‘Na kuna muda niliona kama wanatafuta kitu ndani ya tumbo langu ambalo nilihisi kwasasa hakuna kitu, ni kama boksi tupu....nikaona kama wanatizama  na kuonyesha hali ya kushangaa,...nikaona wakibadilishana vifaa!

 Wakati wanaendelea hivyo, nikaoana jambo la ajabu,....’akasema na kutulia

‘Uliona kwa hisia au kwa macho ya hisia...ehe hebu tuambie uliona nini.....?’ akaulizwa na docta akitabasamu kuonyesha ni jambo lisiloingia akilini lakini yeye alishaelewa anachokiongea.

‘Mhh...unajua kipindi chote nilijua wanatoa utumbo, maini, sijui na vitu gani tumboni mwangu ..lakini sikuona hivyo vitu vikitolewa na kuwekwa pembeni, labda kwa vile nilikuwa siwezi kuinua kichwa...’akatulia

‘Lakini safari hii kwa mara ya kwanza nikaona wakitoa kitu nilichokiona,...’akasema

‘Ulikiona kwa macho au kwa hisia?’ akaulizwa

‘Ni kwa hisia,...yaani macho ya hisia yanaona hicho kitu,.....yote hayo yanafanyika kihisia, kindoto-ndoto naona wanatenda...’akasema

‘Ok, ukaona nini cha ajabu....?’ akaulizwa

‘Maana mwanzoni nilikuwa nahisi kuwa wanaukata mwili wangu na kugawana nyama au vitu vya ndani, lakini sikuona hivyo vitu kama nyama au vitu vya ndani vikipewa hao waliokuwepo pembeni yangu...’akasema

‘Safari niliona kitu kikitolewa tumboni mwangu,...’akasema

‘Kitu gani ulikiona , utumbo, maini au kitu gani?’ akaulizwa

‘Niliona wametoa kiumbe cha ajabu...’akasema na nesi akashika mdomo kama anashuhudia uwongo wa huyo mama, lakini madocta walikuwa hawamuangalii yeye, wao walikuwa wanamuangalia huyo mama tu.

‘Kiumbe cha ajabu...?’ wakauliza mdocta wote kwa mshangao.

‘Ndio nasema kiumbe cha ajabu ,kwa uonekavu wake....kilikuwa kama mtoto mchanga, lakini ukubwa wake ndio ulinitisha...kama nilivyosema, kila kitu humo kilikuw akikubwa sana, kwahiyo hata huyo mtoto mchanga, alikuwa mkubwa...kupita hata mimi….’akasema

‘Kwa uoni wangu asingeliweza kukaa tumboni mwangu, ila kwa haraka nikajua ni mtoto wangu..kiumbe hicho kitakuwa kimetokea tumboni mwangu...na nikahisi kinafanana na mimi...hasa macho....’akasema

‘Kwanini macho...?’ akaulizwa

‘Hata sijui maana kilikuwa kimefumba macho...hadi kilipofikia ile hali ya kulia,...nikaona macho yakitembea kuonekana kuwa kipo hai...nikayaona macho yake kama yanafanana na macho yangu....kwasabbu ya ukubwa unaona kila kitu wazi..macho makubwa, pua kubwa…unaonaeeh…’akasema

‘Hebu nikuulize kwanza, je hapo ulipokuwepo ulijua kuwa una mtoto tumboni...au ndoto yako ilianza ghafla upo sehemu hujui kama upoje...kwani ulikuwa mja mnzito kabla?’ akaulizwa

‘Sikumbuki ya nyuma,..ninachokumbuka ni hivyo tu, kuwa nipo porini...nimezungukwa na hiyo mijitu...na hiyo mijitu ikatoa kiumbe cha ajabu tumboni mwangu....na kiumbe hicho kinafanana na mimi hasa macho....’akasema

‘Yule kiumbe, ambaye ni mtoto mchanga, mkubwa tu, lakini kwao wao kwa vile walikuwa wakubwa vile vile, walimshika kama vile unavyoshika kichanga..., na kichanga hicho kilikuwa na damu-damu hivi, niliogopa … ‘akasema

‘Kwa uoni wangu alikuwa mtoto wangu, lakini nilijiuliza aliwezaje kukaa tumboni mwangu maana ni mkubwa....’akasema

‘Huyu jamaa aliyekuwa muda mwingi akifanya jambo kwenye tumbo langu akawa kashika hicho kiumbe mkononi akawa anafanya jambo....akawa kama anakata kitu kama mnyororo mkubwa uliotokea chini, nilihisi utakuwa umetokea tumboni kwangu.....’akasema

‘Yule jamaa akawa kashika kile kiumbe kama mtoto anakata vitu fulani, sijui ni nyama zilizomzunguka yule mtu-kitoto au nini, halafu akamkabidhi mtu-jitu mwingine, ambaye alikuwa kashika mavitambaa makubwa, huyo mtu-jitu mwingine alikuwa ni mwanamke

‘Ulijuaje kuwa ni mwanamke....?’ akaulizwa

Nilimjua kuwa ni mwanamke kutokana na nguo zake japokuwa alikuwae kajifunika uso, lakini gauni....mavazi ya kike yalimtofautisha na hao wengine...na huyu mtu-jitu akakizungushia kile kitoto-mtu na kukiweka kwenye chombo kikubwa kama beseni kubwa, halafu wakaendelea kufanya wanalolifanya kwenye mwili wangu.

Na wale wengine wakawa wanahangaika na huyo mtoto.... Nilitamani kuwaambia wanirudishie hicho walichokitoa tumboni mwangu, ingawaje sikujua ni namna gani mtoto mkubwa hivyo aliweza kukaa tumboni mwangu na ukubwa wote ule...yaani ni mkubwa.... Nikataka kusema `nipeni mtoto –jitu wangu’ lakini mdomo haukuweza kufunguka!...’akasema akicheka.

‘Kwa bahati, yule mwanamke-jitu akafunua uso , sijui ilikuwaje nikamuona sura yake, halafu kwa haraka akajifunika, ni wakati anakipokea hicho kitoto –jitu kutoka kwa wale wengine waliokuwa wakifanya jambo kwa huyo mtoto.....na akawa kama anasikiliza jambo kwa wenzake, halafu akaondoka na hicho kitoto-jitu...nilitamani kuiga ukelele wanirudishie mtoto wangu...

‘Huyo mwanamke uliyemuona ni nani, unaweza kumkumbuka….?’ Akaulizwa

‘Ndio nikimuona nitamkumbuka tu…..hata huyo mwanaume, …nikimuona nitamjua…’akasema

‘Hujawahi kumuona hapa hospitalini tena?’ akaulizwa

‘Hapana tangia nije hapa sijawahi kumuona, ila nikimuona nitamtambua, anaonekana ni kijana kijana, japo pale walikuwa na maumbo makubwa…’akasema

‘Je na huyo mwanamke ni nani…?’ akaulizwa

‘Si ndio huyo nesi,….’akasema na docta wakasita walitaka kumtambulisha nesi ambaye alikuwa pembeni na kwa jinsi huyo mma alivyolala asingelwieza kumuona. Nesi alikuwa kimia, moyo akiomba huyo mama asije akasema ni yeye, na kukatokea mtafaruku mwingine,  akawa katulia, akiwasikiliza wakubwa wake watasema nini… na maneno ya huyu mama yalimchanganya, kuna muda naona kama katunga uwongo, lakini kuna muda anahisi …ngoja asubirie huko mbele atasema kitu gani..

‘Hapa hospitalini kuna nesi wengi….ni yupo huyo ambaye ulimuona?’ akaulizwa

Yule mama kwanza akajinyosha halafu akawa kama anataka kuinuka, na docta wakamuambia;

‘Wewe usiinuke, wewe tuambie ni yupi kwa sifa kwa jinsi alivyo…na kama ukimuona uanaweza kumtambua….’akaambiwa

NB: Tuachie hapa kwa muda,….kuna wazo muhimu la leo nataka kuliandika

WAZO LA LEO: Ajali za barabarani zimekuwa zikiongezeka, watu wengi wanapoteza maisha na wengine kuwa na vilema vya kudumu,…Tunapoteza nguvu kazi ya taifa, na ukiangalia sana na hili limekuwa ni tatizo sugu, …imeonekana kuwa tatizo kubwa ni madereva na mwendo kasi, ..pia miundo mbinu, barabara zetu bado ni ndogo.

Lakini pia kuna udhaifu wa watendaji wetu katika kusimamia sheria,…na ushahidi kuwa mdogo kuwabana hawa watu…. kama sheria ingelifuatwa vyema adhabu kali ikatolewa, madereva wangeliogopa….lakini pia kunahitajika utaalamu wa ziada ili kuwabana hawa wakosaji na wasimamizi wa sheria wasiowajibika vyema.

Sasa hivi kuna utaalamu wa kuona matukio kuna vifaa na tekinolojia hiyo,…vifaa hivyo vinawekwa majumbani na maofisini,… hili ni muhimu kuwepo kwenye haya magari pia…, kila gari lihakikishe lina hicho kifaa kwa hivi sasa. Kama simu inaweza kugundua wapi mtu alipo, kwanini haya magari yasiwekwe vifaa vinavyoonyesha wapi gari hili lipo,..kukawa na mitambo ya kunasia mienendo ya haya magari, utaalamu huo upo…


Ni kiasi cha kuhakikisha kuwa magari yote makubwa ya kwenda mikoani, yamewekewa hivi vifaa, na kuwe ni kitengo maalumu cha kuchunguza hizi safari, maana watu wanapoteza maisha na maisha ni bora kuliko hizo gharama za kuweka hivyo vifaa ….tujalini raia wetu kwa vitendo ili kuwe na maisha bora yenye usalama.Ni wazo langu la leo
Ni mimi: emu-three

No comments :