Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, February 2, 2015

NANI KAMA MAMA-27



 ‘Hodi hapa…’ Dada mtu na mdogo mtu wakashituka. Hawakushituka kwasababu  ya hodi walishituka kwasababu ya sauti waliyoisikia, mdogo mtu akamuangalia dada yake, na dada yake akawa kama katahayari,  akatikisa kichwa huku akifanya kama kutabasamu na mdogo wake akauliza;

‘Ni nani huyo…mbona kama sauti ya shemeji, na..na  dada, siulisema shemeji yupo ndani au sikukuelewa vyema..?’ akauliza mdogo mtu akijaribu kumfunika usoni yule mtoto mchanga..

Kitendo hiki cha kumfunika mtoto, kilitafsiriwa vibaya, na dada mtu, akili ilishaanza kujenga hisia nyingine udugu ukaanza kusogezwa mbali, akili ikawa inajiuliza;

‘Kwanini mdogo wake amfunike huyo mtoto, ….hataki mume wake amuone kwaninini anakuwa kama anamficha, hapa kuna jambo, kama mdogo wake hajaja na mwanaume mwingine anayefanana na mume wake, …basi lazima kuna jambo kati ya mdogo wake na mume wake…’akili ikawa inawaza hivyo

Kwa muda mfupu sana akili ilifanya mengi, akawa anamuangalai yule mtoto mchanga japokuwa alikuwa kafunikwa, lakini taswira ya yule mtoto mchanga  sura yake, ilikuwa imeshanata kichwani mwa dada mtu,;

‘Kwanza mtoto anafanana kabisa na mume wangu, halafu kwanini mdogo wangu hataki kuniambia ukweli,…kama kweli ana mume mwingine,  na wakati kwenye maisha yetu mimi nay eye huwa hatufichani jambo, kila kitu tuna-ambizana, hajawahi kunificha siri yake hata siku moja, …hapa kuna jambo, na kama ni kweli, sijui kama udugu utakuwepo tena..’akafikia kujiapiza moyoni, wivu ukatanda moyoni.

Wakati anawaza hayo, ..akili yake pia ilikuwa inawaza jambo jingine hasa alimposikia sauti ya mume wake, ikitokea nje, maana anachojua yeye ni kuwa mume wake yupo chumbani,…. kwani walijua kuwa hao waliofika ni maaskari, sasa anashanga kusikia sauti ya mumewe ikitokea nje.

‘Huyu mtu vipi…’akasema dada mtu, huku akichungulia mlango wa chumbani.

‘Kwani vipi dada….?’ Akauliza mdogo mtu naye akiangalia mlangoni na mlango wa chumba cha hao wanandoa wawili, akageuka kumuangalia dada yake kwa macho ya mshangao;

‘Vipi dada kuna nini kinaendelea, nakumbuka ulisema shemeji yupo chumbani…au?’ akauliza tena mdogo mtu

‘Ni kweli, shemeji yako alikuwa chumbani, hata mimi…oh, ngoja tuone, asije akawa ni mtu mwingine ana sauti sawa na shemeji yako….’akasema akisimama kuelekea chumbani, lakini kabla hajaufikia mlango wa chumbani, mlango wan je ukafunguliwa…




******

Mshangao….

Mke mtu akimuangalia mumewe kwa macho ya udadisi, akiwa anashindwa kuelewa, maana hakuna mlango mwingine wa nje wa kutokea ukiwa chumbani, sasa mume wake alitokea wapi….

Shemeji mtu akawa anamshangaa shemeji yake ambaye aliambiwa yupo chumbani sasa anatokea nje, akawa anajiuliza kuna nini kati ya shemeji yake na dada yake, lakini hakulitilia maanani sana, kwani alijua hayo ni mambo ya wanandoa hao.

Mume wa familia naye alikuwa akishangaa na huo ugeni, alitarajia kukutana na watu wenye sare pekee, polisi... wakiwa na shemeji yake...lakini alichokiona ni tofauti.


Alizidi kushikwa na mshangao pale alipomuona shemeji yake akiwa kabeba mtoto mchanga japokuwa kafunikwa, hakuweza kuiona sura ya huyo mtoto alipoingia kwa mara ya kwanza, akawa najiuliza,…sasa huyo mtoto ni wanani, na ujauzito huo aliubeba lini, mbona hakuwahi kuwaambia…lakini muda umepita, yawezekana kweli aliamua kujificha mpaka ajifungue…

‘Shemeji naye, umetushitua kweli…shikamoo shemeji…’ aliyeweza kuuvunja huo ukimia na mshangao alikuwa shemeji yake, lakini salamu haikuitikiwa, shemeji mtu akawa katoa macho akimtizama yule aliyebebwa mikononi….

‘Mhh, mtoto wa nani, nahisi nimeibiwa mke?’’ akauliza huku akimtizama shemeji yake, halafu akageuka kumuangalia mkewe. Mkewe alikuwa akimuangalia kwa macho ya udadisi, na huku kakunja sura. Mume mu alipoiona hiyo sura akahisi hakuna usalama, akasema;

'Kwani vipi...?' akauliza huku akiwa kama anamkonyeza mkewe, kuelekea kwa shemeji yake lakini mkewe akabakia vile vile.

‘Niambie kwanza umetokea wapi mume wangu , wewe si ulikuwa chumbani, sasa nakuona umetokea nje, unataka mimi nionekane muongo, na huko chumbani kuna mlango gani mwingine wa kutokea nje...’akasema mke wake.

‘Niliwahi kukuambia kuwa mimi nina miujiza, na niliwahi kupitia mafunzo ya ukomandoo..uamini sasa...’akasema akitabasamu, na kwa haraka akaelekea chumbani, na kuwaacha mke na mdogo wake wakiangaliana.

‘Nyie watu mna vituko…’akasema mdogo mtu akimfunua kidogo usoni yule mtoto mchanga, na dada mtu akamuuliza

‘Sasa kwanini unamfunika hivyo…huoni utamziba hata hewa ya kupumua…’akasema dada mtu.

‘Unajua nilitaka shemeji tumshitukizie tu…sikutaka amuone mapema hivyo,..lakini sio mbaya, ngoja akae hivyo,…’akasema nesi, na dada yake akawa anazidi kuingiwa na mashaka, na alitaka mumewe atoke haraka ili kijulikane mbicho na mbivu.

Mara wakasikia kukigongwa gongwa huko ndani…

‘Shemeji anafanya ukarabati huko chumbani…?’ akauliza mdogo mtu, na dada mtu akawa anasimama akitaka kuingia  chumbani kuona ni nini mume wake anakifanya, lakini mdogo wake akaanzisha mazungumzo yaliyomfanya asite kuondoka;

‘Sasa huyo mama niliyesikia akiimba huko nje, eti ‘nataka mtoto wangu...’ mliwahi kumuona sura yake, hamumufahamu kabisa….?’ Akauliza

‘Hakuna niliyesikia akisema anamfahamu…’akasema dada yake akiwa bado mawazo ake yapo huko ndani akisikia mume wake akiendelea kugonga gonga.

‘Dada, muwe makini, maana siku hizi kuna tatizo la kuibiwa watoto, na wanaofanya hivyo ni akina mama, huwezi hata kuamini kuwa akina mama hao wanaweza kuwa wezi ..tena wezi wa binadamu, …ni vitu vya ajabu huwezi hata kuamini ukisimuliwa…’ akasema mdogo mtu akimuangalia dada yake ambaye alionekana hajatulia

‘Ni kweli hata hapa kijijibi imetokea na kijiji cha jirani, watoto walipotea kiajabu, wenzao wakasema walichukuliwa na mama mmoja…kijiji cha jirani mwili wa mtoto aliyepotea ukapatkana maporibi ukiwa umekatwa sehemu za siri…lakini huyu mama hafanani kabisa na watu hao….’akasema

‘Una uhakika gani dada, dunia imebadilika, wanadamu wamegeuka chui, na kuvaa ngozi za kondooo-kondooo, yule uneyemuamini leo kama mtakatifu, mchangumungu, usiku anafanya mambo ya ajabu kabisa….’akasema

‘Kiukweli hakuna anayefahamu sura yake na wapi anapotokea , mara nyingu huwa kajifunika uso wake, sizani kama kuna mtu aliwahi kumuona sura yake...labda hao watoto ambao wanamfuatilia kila mahali….’akasema dada yake.

‘Na unasema hajawahi kuonekana hapa kijijini kabla, na kwanini hataki sura yake ionekane?’ akauliza mdogo mtu naye akiangalia mlango wa chumbani alipoingia shemeji yake, aliposikia kugongwa gongwa kukiongezeka.

‘Hatujawahi kumuona huyo mama kabla, huyo ni mgani kabisa...cha ajabu ni huo wimbo wake, na miujiza yake tu,...’akasema dada mtu

‘Miujiza gani kaifanya….?’ akaulizwa mdogo mtu pale alipoona dada yake katulia vyema kwa vile kule kugongwa ndani kulishapungua

‘Ni kama huo niliokuambia kuwa  anaweza kutoweka ghafla, unakuwa naye sambamba, ukigeuka hivi, ukija kuangalia pale alipokuwepo, anakuwa hayupo tena…katoweka…’akasema

‘Mhh, …anatoweka kabisa..?’ akauliza mdogo mtu.

‘Muulize shemeji yako maana nikiongea mimi mtasema ooh, nimetunga hadithi zangu, yeye ilimtokea kabisa ….alikuwa akimfuatilie, na wakati anaongea naye, akageuka kuwafukuza watoto, aligeuza uso kuangalia pale alipokuwa kasimama huyu mama akawa hamuoni, keshatoweka, alitafuta huku na kule hayupo…na sio yeye tu, wengi imewatokea hivyo…..’akasema.

‘Kuna jambo gani jingine analofanya huyo mama?’ akauliza mdogo mtu.

‘Kama unamfuatilia nyuma, anafahamu kabisa wewe unamfuatilia,.....wengine wanasema kuwa anatatua shida za watu, akikuombea unatatuliwa, ....na wengine wamefikia kusema kama una tatizo la kutokupata mtoto,...yeye...yeye....’akasita kwani mume wake alikuwa kajitokeza kutoka chumbani akiwa kachafuka na mavumbi. Na ndugu hawa wakawa wanaangaliana

‘Shemeji naye, umetushitua kweli…’ akasema shemeji mtu.

‘Huo ukarabati umeanza lini…?’ akauliza mkewe.

‘Aaah, we acha tu, maana hujafa hujaumbika….tuyaache haya, ngoja ninawe..kuondoa hili vumbi….’akasema na mkewe akawa kama anawaza jambo fulani, akatikisa kichwa na mdogo wake akawa anamuangalia kwa macho ya udadisi, kabla hajamuuliza kitu dada yake mara shemeji akaingia;

Walisaliamiana sasa kama ada na kuanza kuulizana hali za huko mjini,  na maongezi yakaanza, kuhusiana na kadhia ya hospitalini.

‘Haya hebu tuelezee yaliyotokea huko, maana umetuweka roho juu,  na hata sasa unataka kuifanya ndoa yangu iwe rehani…

‘Kwa vipi mimi niifanye ndoa yenu kuwa reheni..?’ akauliza

‘Muulize ndugu yako, …kama anafikia kunishuku mimi kuwa nina ajenda za siri na wewe unafikiri hapo ana maana gani,…mke wangu, hilo limenivunja nguvu kweli kweli, huyu shemeji tumemlea wenyewe, leo hii mimi ni….’akasindwa kumalizia.

‘Ina maana dada ulishafikia kufikiria hivyo,…dada…kweli hapo ulikosea,…’akasema

‘Sikilizeni niwaambie ukweli, mimi sio mtoto mdogo , mpaka kufikiria huko, nimechunguza na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Hebu niwaulize…’akasema akimfunua yule mtoto, akasema;

‘hebu niambieni , kiukweli huyu mtoto anafanana na nani…?’ akauliza

Mumewe akageuka kumuangalia yule mtoto kwa makini, halafu akasema;

‘Unajua kiukweli, watoto wakiwa wachanga wote hufanana…hapo sio rahisi ukasema moja kwa moja anafanana na mtu fulani, mke wangu wewe hujazaa, huwezi kutuambia kuwa una uzoefu huo,….kwanza hebu niambie, wewe unafikiri huyu mtoto anafanana na nani?’ akauliza mumewe.

‘Unaona..hutaki kusema ukweli, unakimbilia kuniambia `wewe hujazaa, wewe umezaa sio, ….’akasema sasa akiwa kakasirika.

‘Mume wangu wewe ni mwepesi sana kugundua kuwa huyu anafanana na huyu…umeishi pamoja na kila mara huwa hunaniambia kuwa sura za watu kwako unazijua, na kufanana kwao,..leo hii iweje ushindwe kuligundua hili, sio kwamba unafahamu ukweli, lakini hutaki kuuweka wazi…’akasema na mume wake akatabasamu kwa kebehi

‘Ukweli gani unafikiria wewe…hebu weka wazi, tusiyumbishane…’akasema mumewe

‘Muangalia vyema huyo mtoto, semeni ukweli wenu, huyu mtoto hafanani na wewe…’akasema na mdogo mtu akamfunua yule mtoto, naye kwa mara ya kwanza akaligundua hilo…hakuwa amelifikiria hilo kabisa, akiwa anaonyesha uso wa kushanga akasema;

‘Oh,…ni kweli, shemeji kweli anafanana na wewe…’akasema akimuangalia yule mtoto na shemeji yake kwa zamu, halau akamuangalia dada yake na kusema;

‘Dada naye mdadisi kweli..mimi kiukweli sikuwa na wazo hilo, …unajua kadhia hii ilinifanya nishindwe hata kufikiria, nilishaona maisha yangu yamedidimizwa kwenye shimo nzito la giza..nikajua sasa basi….yaani mpaka sasa sijui nitaokokaje…’akasema.

‘Si umejitakia mwenyewe…’akasema dada mtu, na kabla mdogo wake hajajibu, shemeji yake akasema;

‘Yaliotokea huko kazini ni kwasababu ya huyu mtoto….kwani baba yake yupo wapi?’ akauliza mume mtu, akimuangalai shemeji yake, na mkewe akawa anatabasamu kuonyesha kuwa hao watu wanamchezea akili.

‘Ndugu zanguni, naona wakati umefika niwaeleze ukweli wote…ili msije mkaweka dhana ambazo huenda hazipo, kuanzia sasa huyu mtoto ni wetu…huyu mtoto ni wenu, …’akasema

‘Mbona unauchanganya, mara huyu mtoto ni wetu, mara ni wenu, kwa vipi…tuambie kwanza baba yake yupo wapi?’ akauliza shemeji mtu.

‘Baba yake si wewe…hivi mume wangu unajifanya huelewi,…, unataka kuniona mimi mjinga au sio…huyu mtoto baba yake ni wewe…na mama yake…’akasema mkewe na kabla hajamalizia mumewe akadakia, huku akimuangalia yule mtoto mchanga.

‘Baba yake ni mimi, kwa vipi?’ akauliza

‘Ndio nataka niwaeleweshe vyema,…lakini kabla ya kuwalewesha hilo, najua mna dukuduku la kutaka kujua ni kitu gani kilitokea huko mjini,…’akasema mdogo mtu

‘Aaah, kwanza tulimaze hili…baba wa mtoto huyu ni nani..maana mke wangu anataka kunichefua…kauli yake hiyo sijaipenda, kwanini anafikia kunishuku vibaya,…kufanana na mtoto huyu isiwe ni kigezo cha kunipaka matope, wangapia wanafanana kutoka mabara tofaui kabisa…’mume mtu akawa anaongea kwa sauti ya kukasirika.

‘Unaonaeeeh,…kama sio kweli kwanini unaingiwa na jaziba…?’ akauliza mkewe.

‘Kwasababu wewe unanijaza hizo jaziba…ina maana mke wangu umefikia sehemu huniamini…?’ akauliza akimkazia mkewe macho

‘Kumbuka siku uliporudi ukasema una mazungumzo na mimi, ukasema, kuwa ‘kwani hatuwezi kupata mtoto kwa njia nyingine..’,

‘Kumbuka jinsi ulivyonipiga chenga kuniambia ukweli kuwa umeshaongea na mdogo wangu, wakati kumbe umeshaongea na mdogo wangu kuhusu yaliyotokea huko mjini, hukutaka kuniambia mapema ukweli…sasa mdgo wangu kafika…na ushahidi, utasema nini hapa…., ’akasema na wote wakawa wanamsikiliza yeye.

‘Hukutaka kuniambia ukweli …ukijua mimi ni ndugu yake, lakini wewe ukalichukulia kirahisi maana wewe ulishajua ukweli..sasa hakuna cha kuficha, ukweli ndio huu, mtoto anafanana na wewe sura kwa sura…utaniambia nini hapa..’akasema.

‘Dada….’mdogo wake akataka kuingilia kati, lakini dada yake, akanyosha mkono kumkatisha, na sasa alikuwa anasimama kutaka kuondoka.

‘Sasa unataka kwenda wapi…?’ akauliza mume wake.

‘Nataka niwaachie nafasi, mkae wenyewe, nyie wawili make, mliongelee hili, ili mjue jinsi gani ya kunihadaa, maana hapa mnajikanyaga, kila mtu anaongea lake, nataka ukweli, kama mlifanya hili kwa siri, ili tupate mtoto kwa njia hiyo, mimi hapa hatutaelewana …..’akasema

‘Dada…mbona hivi,….kupanga na nani….dada mbona sijaongea ukweli kuhusu huyu mtoto, subirini niwaambie….’akasema mdogo mtu akitaka kuingilia kati, lakini dada yake alishaanza kuondoka kuelekea nje.

‘Hebu muache aende, …akatulize hasira zake na ibilisi akimtoka tutaweza kuongea na kusikilizana…huyu namfahamu mimi, huwa akikasirika inakuwa hivyo,…’akasema mume mtu, lakini mdogo mtu hakukubalia, akasema;

‘Dada mtoto huyu ni moja ya chanzo cha yaliyotokea huko mjini…lakini pia ndiye muokozi wangu, kwani kama sio yeye ningelishafukuzwa kazi mapema…na ndio maana nimemleta hapa ili muweze kunisaidia, sasa kama hutaki kutulia nikawafahamisha kilichotokea huko kazini, basi,…ngojeni nikafungwe…’akasema na dada yake akasimama…

NB: Haya hebu tuone hii kadhia


WAZO LA LEO: Tuwe makini na taarifa, tuwe na uhakika na lile tunalotaka kuliongea kwa watu, kama hatuna uhakika nalo ni bora kukaa kimia, tuchunge sana ulimi, tuchunge sana `kalamu’…ulimi na kalamu vinaweza vikawa silaha ya wema au balaa…hivi vitu viwili vikitumiwa vyema, ni hazina yenye manufaa, lakini vikitumiwa vibaya, ni silaha yenye sumu mbaya sana. Tuweni sana makini katika matumizi ya hivi vitu.
Ni mimi: emu-three

Ni mimi: emu-three

No comments :