Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, October 13, 2014

DUNIA YANGU-47‘Ni shahidi gani huyo manataka afike hapa mbele?’ akaulizwa.

‘Ni Kigagula binti Mzimuni, mama wa mmiliki wa hoteli Ya Paradise….’a

'Kigagula, ni huyo mama anayeishi hapo Paradise Hoteli, lakini anafahamika na jamii inayomzunguka kuwa kachanganyikiwa, na unafahamu vyema sheria haimruhusu mtu wa namna hiyo kutoa ushahidi, unalielewa vyema hilo sitaki kukumbusha..’ .

‘Huyu mama hajachanganyikwa kihivyo, muheshimiwa hakimu….’akasema muendesha mashitaka

‘Mna uhakika na hilo, ni ajabu basi ….mnaweza kulithibitisha hilo?’ akauliza hakimu akionyesha wasiwasi na mshangao.

‘Ndio muheshimiwa, tunataka kulithibitisha hilo mbele ya mahakama yako tukufu muheshimiwa, na ndipo utakapojua njama za hawa watu, wapo tayari hata kuwaua wazazi wako kwa ajili ya tamaa ya mali…'


Tuendelee na kisa chetu..............


                                             ***********


Mahakama  ilikuwa kimiya…

Mara kikaingizwa kigari cha kukokotwa na mkono, na ndani yake akiwemo mama mzee, ambaye ndiye shahidi  aliyetakiwa kuhojiwa. Mama huyu  alionekana kutulia kwenye kiti chake akiwa kama kajiegemeza upande mmoja, na kofia pana kichwani lenye rangi sawa na gauni lake, 

Alivyokaa kwenye kle kigari, alikuwa kama kakaa upande upande, labda ni kutokana na matatizo alio nayo ya kiafya, na muda wote alikuwa kainama chini, hukuinua uso kuwaangalia watu hadi alipofikishwa mbele ya mahakama,  sehemu wanaposimama mashahidi wanapohojiwa.

Akainamisha kichwa kama kusalimia, na hapo watu wakacheka, hata hakimu akatabasamu, huku akimuangalia mama hayo kwa macho ya mshangao na alionekana kuwa na hamu kubwa kumsikia mama huyo atakachongea, maana amjuavyo yeye huongea kwa jaziba na matusi juu.

Akawa anamuangalia huyo mama , na pia kugeuza jicho kumuangalia muendesha amshitaka, huku kichwani akikumbuka siku ambazo aliwahi kukutana naye, japo kwa sio mara kwa mara lakini mara chache, alizokutana naye, alipofika kwenye hiyo hoteli kikazi na kufahamishwa kuwa huyo mama ni nani…

‘Huyu mama ni nani mbona namuona akitembea huku na kule na anaonekana mkali kweli?’ akauliza huyo hakimu siku ya kwanza kumuona.

‘Huyo mama inasadikiwa ni mama wa mtoto ambaye alikuwa mumiliki wa kwanza hoteli hii?’ akaambiwa na watu aliokuwa nao.

‘Anaonekana hayupo sawa….’akasema

‘Kachanganyikiwa, ..akianza kutukuana hapo utakimbia,….’akaambiwa, na mara mama huyo akawaona wakimuangalia.

‘Na nyie mnashangaa nini hapo, mumekuja kushangaa hapa, kwenu hakuna wazazi kama mimi,….au niwaonyeshe kuwa mimi ni mzazi na nimewaza nyie….’akawa kama anataka kuvua nguo, na walinzi wake wakamzuia.

‘Acheni niwaonyeshe wajue kuwa mimi ni nani, mijitu mizima ovyo,...eti hakimu , hakimuhata mimi naweza kuwa hakimu, hakimu watakuwa hawa bwana,... haya wasikilizeni waende zao huko juu wakafanyae ufusuka wako na kulewa, unafikiri kuna cha zaidi walichofuata hapa...'akasema akiwaangalia hao wageni.

'Waone kwanza, hivi kweli nyie mnaweza kunihukumu, mimi, nisimame mbele ya mahakamayenu mseme, utafungwa, thibutu, maweee...semeni mlichofuata hapa kama si hayo hayo, mmmh, ngoja ninyamaze maana mteja ni mfalme, yaani  hata kama ni mzinzi, anatakiwa awe mfalme..hahaha , karibuni ndani ya dunia…hahaha….’akawa anacheka na kujizungushazungusha, kipindi hicho alikuwa anaweza kutembea mwenyewe

'Mimi hata siku moja siwezi kusimama mahakamani kwako nikakusikiliza, mnasikia, kamwe, niikija huko mjue mimi ndio hakimu wenu,...haya nendeni wazinzi wenzenu wanawasubiria huko juu.....hata hamuoni haya, mumeacha wake zenu huko mnakuja kufuata maradhi...'akasema huyo mama

Hakimu alipokumbuka hayo akatabasamu, maana yule yule aliyekataa kuwa hawezi kuja kusimama mbele ya mahakama yake leo yupo mbele yake na yeye anatakiwa kuhakikisha haki inatendeka, .`.na sheria haimruhusu mtu ambaye kachanganikiwa kutoa ushahidi, ….lakini anayway, ngoja tuone..’ akawa anajisema kimoyo moyo.

Baadaye alipofika tena, akawa hamuoni, akawauliza watu wanaofika hapo mara kwa mara aliokuwa nao;

‘Yule mama aliyekuwa mkali kweli siku hizi yupo wapi?’ akauliza.

‘Yule mama anaumwa, wanasema alipatwa na kiharusi, na hata alipopona hajaweza kutembea mwenyewe, anatembea kwa msaada wa kigari cha kusukuma kwa mkono…’akaambiwa.

‘Oh, alikuwa maklo kweli na kila mtu alikuwa akimuogopa, niliona wafanyakazi humu ndani wakiwajibika kweli wakimuona yeye….sasa kumepooza…’akasema.

‘Nasikia anataka kuja hapa, lakini wanamzuia, wameamua kumfungia kwenye eneo la nyumba yao  iliyokuwepo hapo pembeni mwa hiyo hoteli…’muheshimiwa hakimu akaambiwa siku hizo.

Muheshimiwa hakimu akaondoa yale mawazo ya nyuma na kuendelea kumuangalia vyema, na akilini mwake akawaza;

‘Lakini leo mbona anamuona yupo tofauti, utafikiri sio huyo mama ninayemfahamu mimi…’akawa anawaza na hapo akawageukiwa wasaidizi wake kuaona na wao wana taswira gani usoni mwao kuhusu huyo mama, na wenzake walionekana kuwa kama yeye.

Baadaye hali ilipotulia vyema, na watu ambao walishaanza kunong’ona, na minong’ona  ya wengi hugeuka kuwaa ngurumo. Taratibu zikaanza, yule mama akawa anahojiwa na kulishwa kiapo,  na baadaye muendesha mashitaka akawa kasimama karibu na yule mama akaanza kumuhoji.

‘Tuambie tena jina lako ni nani mama yetu?’ akauliza huyo mama.

‘Hilo swali mnaniuliza mara ngapi, msinichezee akili yangu, mimi sio tahira kama mlivyozoea kuniita, mimi nina akili zangu timamu, ni hawa vichaa wachache wanaonidunga sindani za kunipoteza akili yangu ya asili….ole wao,…..’akasema akiwa kamkazia macho muendesha mashitaka.

‘Ndio maana nakuuliza jina lako tena tuone kama kweli unayosema ni kweli, kuwa wewe una akili zako timamu, wanafanya kukuzulia tu kuwa umechanganyikiwa….’akasema muendesha mashitaka.

‘Hahaha, na hata wewe pia, unanipima, hahaha, haya mimi naitwa Kigagula….’akasema huyo mama akiinua uso na kumuangalia muulizaji wa maswali, na watu wakacheka, na akageuka kuwaangalia watu, watu wakakatiza kucheka na kukaa kimiya utafikiri katamka neno la kuwanyamazisha.

‘Hilo ndilo jina lako halisi au una jina jingine ?

‘Hilo ndilo jina langu la urithi, majina mengine nimeshayaandika hapo mlipokuwa mkinihoji, sitaki kuyarudia tena, maana yana nuksi,  jina langu ni Kikagula binti  Mzimuni, hilo nilipewa na bibi yangu,na niliambiwa nisilje kulibadili, hayo majina mengine ya kisasa mimi siyataki kuyasikika kabisa…’akasema.

‘Kwanini wanakudunga sindani , huoni ni kwa vile wanahisi una matatizo ya kiakili?’ akaulizwa.

‘Wao ndio wana matatizi ya kiakili sio mimi, wamegundua kuwa ninataka kongea mambo wasiyotaka yaongelewe,..wakaona dawa ni kunimaliza kwa kunipiga madawa ya kulevya, lakini wameshindwa, wewe huoni, wapo wapi….wanacheza na Kigagula….watakwenda na maji,….wote, na hata huyo anayejifanya sasa kakua na kunizidi mimi mama naye, watajuta kuzaliwa….’akasema akitingisha kichwa.

‘Mama  kwani wewe una watoto wangapi?’ akulizwa.

‘Mimi nina mtoto mmoja tu, wa dawa….hahaha, wa dawa, na ana makarama yule mtoto, usiombe kukutana naye, ni jembe dunia yote kaiweka hapa….’akasema akionyesha kiganya cha mkono.

‘Na mume wako yupo wapi?’ akaulizwa.

‘Mume wangu, ….’hapo akatulia kidogo, halafu akasema.

‘Mume wangu hayupo duniani, alishafariki, ila sasa anajifanya kunijia na kudai eti na mimi nife nimfuate huko alipo, hahaha mimi sifi, nitadunda mpaka kieleweke…’akasema na kuanza kuangalia huku na kule.

‘Mume wako alipofariki, wewe na mtoto wako mlikuwa mkiishi wapi?’ akaulizwa

‘Hapo hapo ilipojengwa hiyo hoteli kubwa ya kitalii, unajua hapo mwanzoni hapakuwa hivyo, kulikuwa na nafasi kubwa ilikuwa wazi, mume wangu alikuwa mjanja, alinunua sehemu kubwa sana…sio kwamba alinunua, sehemu hiyo yote ilikuwa ya mababu na mababu zake…basi tena mambo ya pesa na serikali tena, basi, sehemu nyingne ilikuja kuchukuliwa na jiji, lakni hata hivyo bado kulikuwa na nafai ya kutosha, …’hapo akawa anaongea vizuri.

‘Una maana ni hapo kwenye hiyo hoteli ya Paradise?’ akaulizwa

‘Ndio hiyo hiyo pepo ya ndoto ya mwanagu, usiniulize maswali ya kijinga, uliza swali la moja kwa moja, kwani tulikuwa tunaongelea nini mwanzoni mpaka uulize ni hapo ni hapo..nyie vijana wa siku hizi akili zenu ni ndogo sana, mnashindwa kupambanua mambo, ndio  hapo hapo tunapopaongelea …..’akasema kwa sauti ya ukali.

‘Kwahiyo hiyo hoteli ilijengwa baada ya mume wako  kufariki?’ akaulizwa

‘Ilikuwa imeshaanzwa kujengwa bwana….’akasema akibenua mdomo, kama kikerwa, halafu kama vile amekumbuka yupo akasema;

‘Ilianzwa kujengwa zamani sana, … asikudanganye mtu, mimi mwenyewe niliwahi kusimamia nikiwahimiza mafundi,  na taratibu za ujenzi zilianza zamani sana,  lakini sio kwa ukubwa huo, hapo nakubali, ramani ya awali ilikuwa ndogo tu, wao ndio wakaongezea kwenye ramani yao na ndio ikawa hivyo....’akasema.

‘Ni akina nani waliongezea ukubwa huo,..?’ akaulizwa.

‘Ni mtoto wangu akishirikiana na wenzake, …wenzake sasa wanajifanya eneo hilo ni la kwao, eti na wao wa hisa, eti..eti… thubutu, nitawateketeza mmoja baada ya mwingine, nimewaambia sitaki kusikia kauli hiyo tena, ….sijui wapo wapi hao watu mbona hamjawakamata. Mmmh, ndio hao hapo, waulizeni , lakini wengine hawapo hapo….?’ Akauliza na kugeuka kuangalia huku na kule.

‘Kwani wale pale sio wenyewe, wadhamini wa hiyo hoteli,….?’ akaulizwa
.
‘Hao ni vibaraka wao tu, wapo wenyewe, matahira fulani, wanajifanya wana akili kupindukia,….vichwa maji kama mwanagu, wengine wanaishi nje, kuna mmoja tu yupo hapa, ananikera kwelikweli yule mtu,…yeye, anajifanya anajua sana, huyu ….hebu ?’ akageuka huku na kule kama kumtafuta mtu.

‘Ni nani huyo unayemtafuta?’ akaulizwa

‘Achana naye, mtamuona huko makaburini….’akasema

‘Makaburii!?’ akauliza muendesha mashitaka kwa mshangao

‘Huna maswali mengine ya maana…?’ akauliza huyo mama akionekana kukerwa.

‘Kwahiyo mtoto wako na hao unaowaita vichwa maji ndio waliobuni huo mradi wa hoteli hiyo kubwa ya aina yake katika bara hili la Afrika?’ akaulizwa

‘Yah, exactly muheshimiwa …..ndio ndoto yao, ndio wao waliobuni mradi huo mkubwa na matarajio yao iwe ndio hoteli kubwa duniani, watu wawe wanakuja kutoka mbali, kumtembelea mtawala……’akasema.

‘Huyo mtawala ndio nani?’ akauliza.

‘Mtamuona siku ikifika,…siwaambii, kamwe, uliza swali jingine….’akasema

‘Kwahiyo mume wako alikuwa tajiri sana, mali hiyo alipata wapi?’ akaulizwa

‘Mume wangu alikuwa mrithi wa utawala , utawala wa kijadi, na mtawala wakati huo alikuwa akipata ruzuku toka kwa watu wake, ila wao waliwahi kumuliki eneo lenye madini…siunajua madini yalivyo na pesa, wakawa matajiri kweli, enzi hizo, hata wazungu walikuwa wakiwaheshimu,…mababu hao wakapita, wakaja sasa enzi za mume wangu, mambo yakaanza kulega lega….’akatulia kidogo.

‘Unajua kuna mambo mengine ya kijadi hayana maana, mume wangu akawa anayapuuzia baadhi yao, na kuna mambo yakawa yanaharibika,…siwezi kuwaaambia yote hapa, maana nyie mtajifanya hamyaamini, ila kiukweli yalikuwa na nguvu sana na yanatisha….’akasema akimuangalia muendesha mashitaka.

‘Baada ya mume wako kufariki,  utajiri wote wa mume wako ulibakia mikononi mwa mtoto wako,kwani mume wako hakuwa na watoto wengine?’ akaulizwa.

‘Walikuwepo watoto wengine..ndio hivyo, usasa mume wangu hakutaka sana kuonekana ana nyumba ndogo nyingi, lakini mimi nilikuwa nazifahamu, kisiri,….unajua tena, yeye akijifanya mjanja, akakutana na mjanja mwenzake, lakini tukawa tunaenda hivyo hivyo,…ndio kifupi alikuwa na watoto wengine , kwa wanawake wengine…’akasema.

‘Sasa wao ikawaje, hawakupata urithi wa utajiri wa mume wako?’ akaulizwa.

‘Mhh, sasa wewe unanichimba, …waulize kwanini walikimbie, sijawakataza kuja kuchukua kile wanachoona ni chao, walikimbilia huko kijijini wakawahi mashamba, mimi sikuwafuta kuwanyang’anya, kama wao walichukua huko, basi huku na wao hawana chao, unasikia vyema…hata hivyo ni nani angeweza kushindana na  Kigagula …’akasema.

‘Labda wewe uliwatisha, ukawaambia waondoke?’ akaulizwa.

‘Waliondoka wenyewe kwa uwaoga wao,sikuwahi kuwaambia waondoke……’akasema

‘Ni kwanini walifanya hivyo, mpaka waogope, je walikuwa wakikuogopa wewe…..?’ akaulizwa.

WAZO LA LEO: Dhuluma inapozidi, watu hufikia kutokuogopa, na wengine bila aibu wanaweza hata kuchukua mali ya mayatima, mali ya watoto wanyonge ambayo wazazi wao walihangaika, na kwa vile wazazi hao hawapo, basi wadhalimu huichukua bila hata aibu. Hio ni dhuluma kubwa sana , na hilo deni lna mnafahamu hakimu wake ni nani, hakimu muadilifu anayefahamu undani wa kila jambo.

Ni mimi: emu-three

No comments :