Siku
ya kwanza ya kusikilizwa kesi ya mauji ya mke wa Inspecta, watu walijitokeza
kwa wingi, utafikiri ilikuwa kesi iliyotangazwa sana, na ilivyoonekana kujaa
kwa watu kulitokana na propaganda nyingi zilizotapakaa kwenye magezetini, na
kila mmoja alijua kuwa Inspecta ni muuaji asiyefaa kusamehewa, na baadhi ya magazeti
yaliandika hivi;
‘Hatimaye
haki itatendeka kuondoa uzalilishaji wa wanawake wanao zalilishwa na waume zao
hadi kufikia kuwawa…
Jingine
likaandika, ‘hatimaye serikali yasalimu amri na kumfikisha mmoja wa watendaji
wake mahakamani, baada ya kubainika ukweli wa kuzalilishwa kwa wanawake hadi
kuuwawa…
Haikutosha
jingine likaandika;
‘Kigogo
wa polisi aliyemuua mkewe kwa sababu ya wivu, atinga mahakamani,..
‘Kesi
iliyotaka kupindishwa ionekane kuwa mke kajiua mwenyewe, yatinga mahakamani
huku mshitakiwa wake akiwa mmoja wa wakuu wa idara ya usalama…
Ilimradi
kila gazeti liliandika kivyake, na hakuna gazeti liliweka bayana ukweli wa
tukio zima, au hata kumtetea Inspecta, habari zote zilionyesha kuwa Inspecta ni
mkosaji anayestahili hukumu nzito, na amekuwa akilindwa na wakubwa ndio maana
kesi yake ilicheleweshwa kufikishwa mahakamani.
Siku
kabla ya kesi hiyo, Inspecta alitembelewa na mtu asiyemtegemea kabisa na
hakutaka kabisa aje kuonana naye kwani ingelileta picha mbaya..na hata yeye
moyoni alimuona mtu huyo kama mmoja wa watu ambao wamechangia kumuharibia
mpangilio mzima wa maisha yake….alipoambiwa kuna mgeni, akajua ni rafiki Inspecta
amefika, akihitajia jibu lake, lakini alipotoka hakumuona huyo rafiki yake..na
akitaka kugeuka kuondoka mara akasikia sauti nyuma yake.
‘Baby,
pole sana…..’akashituka, akashindwa hata kugeuka, alichofanya ni kusema…
‘Ni
wewe umekuja kufuata nini hapa…?’ akauliza Inspecta.
‘Nimekuja
kukushauri jambo, na kupata jibu lako, maana nimekutana na rafiki yako, akasema
yupo mbioni kuhakikisha kuwa ukweli unabainika, kuwa mke wako alijiua yeye
mwenyewe, na mimi nikaona hakuna hilo halina ubaya akufaaye kwa dhiki ndiye
rafiki wa kweli, au sio…, sasa basi mimi, nimekuja kupata jibu lako, je upo
tayari tulifanyie kazi…?’ akauliza huyo mdada akionyesha uso wa huruma.
Inspecta
alipoambiwa hivyo,akakumbuka mazungumzo yake na rafki yake, siku alipokuja
kumtembelea, ambaye alisema anahitajia jibu kesho yake, lakini kesho yake
hakufika zikapita siku mbili, na siku ya kutajwa kesi ikawa anakaribia, na
Inspecta Moto, akajua mwenzake keshaghairi, kaona hana hoja.
‘Sitaki
kuongea na wewe, nataka kuongea na huyo aliyekutuma, nakuomba tafadhali uwe
mbali na mimi…’akasema bila kugeuka kumuangalia.
‘Sikiliza
kati ya watu wanaoweza kukuokoa katika hiyo kesi, mmojawapo ni mimi, mimi
naweza kukiri mambo mengi sana, na yakaja kukusaidia, mwenyewe unafahamu hilo,
na pia mimi ndiye ninaweza kukuangamiza, na hakuna ushahidi wowote utakaoweza
kukutetea kama nikiamua kufanya hivyo…kweli si kweli…’akasema
Inspecta
akageuka kuangaliana na huyo mdada, kwanza akakunja uso kwa hasira, lakini
macho yake yalipkutanana huyo mdada, akajikuta akinywea, …na kwa mbali akaiona
taswira ya mkewe akilia,…..alipoiona hiyo hali, akainama chini na kutulia.
‘Unakumbuka
mazungumzo yenu na rafiki yako, je umeshafikiria vya kutosha maana kesho kesi
inaanza kutajwa rasmi, na ukikubali tu, kila kitu kitageuka, hata hayo magazeti
unayoona yakiandika ubaya, yatagezwa na kukuandika wema, kuwa kweli kumbe, mkeo
alijiua….hilo niamini mimi…
Akasema
huyo binti, na Inspecta akakumbuka walivyokutana na raiki yake Inpsecta
mwenzake, japokuwa siku hiyo, hakupenda kabisa kukutana na huyo mtu, lakini baadaye
akaamua kwenda kuongea naye tu ili ajue ni kitu gani kilichomleta, na
mazungumzo yao yalikuwa hivi…
***********
‘Rafiki
yangu, najua utaona nimekutupa, hasa baada ya hili tukio, ni kweli sitakuwa
mbali na sheria, kwani ulichofanya hata mimi kimeniuma sana,…sikuamini hadi
nilipofanya upelelezi wa kina, nikagundua mengi na moja wapo eti wewe
ulinishuku kuwa huenda mimi natembea na mke wako, …siamini, na sutakusamehe kwa
shutuma hiyo..mimi rafiki yako nikusaliti, hivi imekuwaje hadi kufikiria hivyo….’akaanza
hivyo.
‘Ndicho
kilichokuleta hapa au kuna zaidi ya hilo?’ akauliza Inspecta Moto.
‘Kilichonileta
hapa ni upelelezi wa mauaji ya mke wako, nataka sheria ichukue mkondo wake,
lakini kwa haki,…sasa nataka kujua ukweli kwanini ulifanya hivyo, licha ya
madai yako kuwa hizo ni njama za sijui dunia
yangu, na porojo zisizo na maana, hivi kwanza ulikuwa na maana gani kusema
hivyo, ….’akasema Maneno
‘Nakuomba
kama huna la maana lililokuleta hapa, rudi kwa hao mabwana zako waliokutuma,
waambie nitapambana nao kwa kila hali,..nitahakikisha hadi tone la mwisho la
damu yangu linamwagika ..hadi nyote mlioshirikiana kuyafanya haya hadi kufikia
kumuua mke wangu na kunisingizia mimi, yanabainika,..hilo nakuhakikishia,
nafahamu unanifahamu vyema nilivyo , nikiahidi jambo ni lazima litendeke….’akasema
‘Unajua
mimi sikuelewi, kwanini unanishinikiza kwenye makosa yako, mimi nahusika vipi,
kwanza hebu tuwekane wazi, ilikuwaje hadi unishuku na mauchafu hayo, tumeishi
miaka mingi bila kusikia hilo imekuwaje sasa…hivi kama ningekuwa mtu wa
kukushuku kwanini mimi nisingelikushuku wewe uliyekuwa unatoka na mke wangu
hata bila ya mimi kujua, eeeh, acha wivu
usio na tija, na sasa unaona matokeo yake….’akasema
‘Nakufahamu
ulivyo siku zote ukiahidi jambo ni lazima ulitende, ndio maana ulivyoahidi
kumuua mke wako ukafanya hivyo, au sio….’akaongeza Inspecta Maneno
‘Pandikiza
fitina uwezavyo, ongeza na chuki juu yake, lakini nakuambia ukweli hutafanikiwa
kwangu mimi, najua kila jambo lilivyotengenezwa, ni swala la muda tu,
nakusikitikia kwa jinsi ulivyojiingiza kwenye mitandao ya kijasusi, na kuacha kazi
yako ya kuwatumikia wananchi…’akasema
‘Kwa
vipi maana sikuelewi unachoongea, hayo maneno yako, unayatoa wapi hayo, ….?’
Akauliza
‘Utakuja
kuyasikia mahakamani hatua kwa hatua,…..ngoja kesi ifike mahakamani, siwezi
kukuambia lolote kwa hivi sasa, haya niambie umekuja kufuata nini, au unataka
kujua nafahamu kiasi gani kutokana na njama zenu…’akasema
‘Nina
maswali nataka kukuuliza…’akasema, na Inspecta Moto akatulia, hakusema neno la
kukubali au kukataa
‘Ukinijibu
vyema huenda na mimi nikatafuta njia njema ya kukusaidia,…mimi nina njia ambayo
inaweza kukusaidia sana, lakini nataka kujua ukweli wako, niambie ulipofika
siku ile kwa mkeo, usiku, mliongea nini mpaka ukafikia kukasirishana kiasi
hicho?’ akauliza, na Inspecta moto akabakia kimiya
‘Wakati
mpo hotelini ya yule mpenzi wako, ulisikika ukisema , tena mbele ya wahudumu wa
mle ndani, kuwa utamuua mke wako,…kuna nini kilikushinikiza hadi kufikia kutoa
kauli kama hiyo nzito, tena ya kuapiza, na wewe kawaida yako ukiapiza kitu
hurudi nyuma, kwanini hadi kufikia kumuua mkeo,,..?’ akauliza lakini Moto akawa
kimiya
‘Je
wewe na mkeo mlikujaje mkawa hamuelewani, na kwanini hukuniambia , maana mimi
ndiye rafiki yako mkubwa ningelikusaidia kutoa muafaka, unakumbuka siku mkeo
alipofika kutoka kijijini kwa wazazi wake…wewe hukuwepo, nikajaribu kukusaidia
ili sijue kuwa upo na huyo mpenzo wako, kwa nia njema nikajaribu kumliwaza ,
maana alishafikia kukasirika,..’akasema
‘Kuliwaza
eeeh, nafahamu sana, unajua jinsi gani ya kuliwaza wake za watu…ndio ukamchukua
mkaenda naye hapo hotelini, na hiyo kumbe haikuwa mara yenu ya kwanza au sio?’
akauliza Inspecta Moto
‘Ndio
sio mara ya kwanza, na sio mara ya kwanza kutoka na shemeji kumpeleka popote
alipotaka, kama ilivyo kawaida ya wewe kumchukua mke wangu, na yote hayo
tuliyafanya kwa kuaminiana, au sio, sasa kuna kitu gani kilitokea hadi ukafikia
hatua ya kutokuniamini mimi?’ akauliza, na inspecta akabakia kimiya.
‘Nilipofika
usiku ule pale hotelini nilimkuta mke wako akiwa kalewa sana…sio kawaida ya
shemeji kulewa hivyo, mimi namfahamu sana, kafanya hivyo kutokana na wewe au
sio,… na alikuwa na wanaume, ambao sikuwaamini, nikaona nimchukue shemeji
kumrejesha nyumbani, ….nakueleza haya ili nikuondoe wasiwasi wako, kuhusu
mimi…’akasema na Inspecta akbakia kimiya.
‘Nilimshauri
sana shemeji kuwa anayofanya sio mazuri, ni vyema turudi nyumbani na mimi
nitakutafuta maana alisema wazi kuwa anafanya
yote hayo akikushuku kuwa upo na huyo mpenzi wako, kitu ambacho ni kweli, …au
unabisha hukuwa na mpenzi wako huyo binti mrembo Jembe…?’ akauliza
‘Umemaliza?’
akauliza Inspecta Moto.
‘Ni
hivi, nilipoona shemeji yupo katika ile hali, mimi nikamshauri na baadaye kwa
shingo upande akakubali, nikamchukua hadi kwenye gari, na ilikuwa vigumu sana,
hata hivyo kwa heshima aliyokuwa nayo kwangu,mwishowe alikubali, nikamchukua
hadi nyumbani…’akasema
‘Nilipofika
nyumbani kwako, akateremka kwenye gari, nikamuuliza kama anaweza kutembea
mwenyewe , maana alikuwa amelewa, akasema anaweza, na mlinzi akamsaidia
kumuingiza ndani, na mimi nikasubiri hadi mlinzi alipotoka , na kusema
ameshamfikisha ndani, …sikuwa na amani, nilitaka nihakikishe kuwa huyo mtu
kalala….nikampigia simu nikiwa hapo hapo nje…’akaema
‘Ushahidi
wa simu kuwa kweli nilimpigia upo, hata ukihitajia naweza kukuthibitishia hilo,…na
yeye alipokea simu yangu, akasema nisiwe na wasiwasi, ameshafika ndani, na muda
huo alikuwa akijindaa kulala, aliongea kwa sauti iliyo sahihi kabisa….kama
unataka kusikia sauti yake naweza kukusikilizisha…’akasema
‘Kwanini
ulirekodi yote hayo….huoni kuwa ilikuwa sehemu ya kujihami , ya kuwa ulkuwa na
njama, na kama ikitokea tatizo utoe ushahidi huo…’akasema
‘Mimi
nina kawaida ya kurekodi simu zangu zote zenye utata, na hali ilivyokuwepo siku
hiyo,nilijua wewe unaweza kuleta utata, nikajihami kihivyo, na utakuja kuona
kuwa siku hiyo nilikuwa nimerokodi simu zote nilizopiga maana hata hivyo
nilikuwa kazini kufanya uchunguzi wa kesi zinazoendelea..’akasema
‘Baada
ya kuhakikisha kuwa kweli shemeji kalala, baada ya kunihakikishia kwenye simu,
mimi nikaondoka, nikimuachia maagizo mlinzi kuwa kama kuna lolote litakalo tokea
anifahamishe, na mimi nikarudi hotelini kukutafuta wewe..’akasema
‘Niliporudi
hotelini nikakutana na hizo shutuma kutoka kwa muhudumu ambaye nilikutana naye
mlangoni akiwa anaondoka, na ilikuwa ni Bahati tu, vinginevyo nisingekutana
naye, alichelewa akiwa na shughuli nyingine, akaniambia kuwa wewe umetoka hapo
ukiwa na hasira, na umeapa kuwa utamfanya mke wako kitu kibaya ambacho hajawahi
kufanyiwa…..’akasema
‘Kwa
vile mimi nakufahamu sana, kuwa ukilewa wewe unakuwa mtata, ndio maaa hupendi
kulewa mara kwa mara, na sijui kwanini umeanza tena kulewa. Kiukweli nilianza
kuhisi vibaya, kuwa kama umelewa, lolote laweza kutokea, nikaona nifanye juhudi
kuhakikisha kuwa wewe na shemeji hamtazuriana.
‘Lakini
nikajiuliza nitafanyaje, maana kwa hali ilivyokuwa na huku umelewa, taswira ya
kibinadamu inaweza kugeuka, wema kuwa ubaya,hata hivyo sikukata tamaa, na kabla
ya kufanya lolote,nikataka kuhakiki, nikampigia simu mpenzi wako ili nijue
jinsi ulivyoachana naye je ulikuwa umelewa sana au la
‘Kauli
yake ilinikatisha tamaa kwani haa yeye alikuwa na wasiwasi sana kuhusu hatima
yako na familia yako. Yule binti anakupenda kweli, hata hivyo, hapeni kuvunja
ndoa yako kihivyo, alitaka wewe mwenyewe uje kuamua, unajua aliniambiaje…’akatulia
‘Nenda
kahakikishe kuwa kuna usalama, sitaki baya litokee mimi niwe sababu, sitaki
mpenzi wangu aingie matatani kwa mgongo wangu, nenda tafadhali….akanisishi
sana, nikamuuliza kwani kumetokea nini..akaniambia;
‘Rafiki
yako kalewa….na alipokumbuka yale aliyokuwa akifanya mkewe, kaondoka hapa kwa
hasira huku ukiapiza kuwa akifika nyumbani atamfanya kitu mbaya mke wako, nikamuuliza
kitu mbaya gani, akasema umetamka waziwazi kuwa utamuua mke wako,….sasa nakuuliza je
kauli hiyo hukuitamka, je umesingiziwa kusema maneno hayo?’ akauliza na
Inspecta Moto akabakia kimiya.
‘Unaweza
kusema kutamka ni jambo jingine na kutenda ni jambo jingine haya tuseme
hivyo,
twende hadi hapo ulipofika kwako, …ulifanyaje, kwa jinsi inavyoonekana ulifika,
na ukaanza kuzozana na mke wako, mkaanza kupigana, yeye akiwa na kisu ,
namfahamu sana shemeji pamoja na yote …ana hasira za haraka, licha ya kuwa
mwanamke mpole sana mwenye hekima, nitamkosa sana shemeji yangu….’akasema na
kuinama chini.
‘Umemaliza…’akauliza
Inspecta Moto.
‘Nataka
kukuonyesha uliyotenda, maana unaweza kusema unasingiziwa, kesi ya mauaji mara
nyingi watu hawakubali kuwa wamefanya mpaka ushahidi upatikane, maana ukikiri
basi hakuna jinsi ni kunyongwa tu…..’akasema
‘Na
ndio lengo lenu, mkijua kuwa mimi nikiondoka, basi hakuna kikwazo kwenye
mipango yenu, mumemuondoa mke wangu baada ya wewe kugundua kuwa kagundua
mengi unayoyafanya….au unafikiri hilo
sijui…’akasema Moto.
‘Samahani
sana, hayo ya kugundua, sijui mimi nahusika na kundi gani hayo ni yako, na sio
vizuri kumuhusisha shemeji ya hisia zako, shemeji wa watu yupo mbali kabisa na
hisia zako ..hajawahi hata siku moja kuniamboa lolote kuwa mimi ninahusika na
lolote…sijui hayao yanatoka wapi, ni kwa vile umeona nimebadilika, nimeamua
kujijanga, sasa wewe ulitaka nife masikini…..’akasema
‘Najua
kifo cha shemeji kilikuwa bahato mbaya, ni wakati mnapambana, akiwa na kisu,
ukitaka kumnyang’anya ndipo bahai mbaya kikamchoma,….sizani kama ulikusudia, na
hilo nimekutetea sana….kwahiyo itakuwa mauaji ya Bahati mbaya, …sina jinsi gani
nyingine ya kukusaidia…’akasema
‘Sawa
nimekusikia, unaweza kuondoka…..’akasema Moto.
‘Ila
kuna kitu kingine, hicho ni baina yangu mimi na wewe, tunaweza kufanya hivyo
japokuwa ni dhambi, ..wakati mwingine mtu akishakufa ndio basi tena, tugange
yaliyopo, hilo ni wazo langu tu, kama utaliafiki, basi mimi nitalifanyia kazi….’akasema
‘Unataka
kusema nini?’ akauliza Moto
‘Mkeo
kajiua mwenyewe….’akasema Maneno na kumuangalia Moto kwa makini
‘Hayo
unasema wewe…’akasema Moto.
‘Ni
uamuzi wako, ufe jela, kwa kifungo cha maisha au kunyongwa, au ukubaliane na
wazo langu, …’akasema
‘Hayo
ni mawazo yako, kama umemaliza unaweza kuondoka…’akasema Moto.
‘Ni
hivi mimi nimeshaanza kujenga hoja, na kukusanya ushahidi mwingine, ambao
utakusaidia wewe, nimeshaanzia huko hotelini, kusawazisha mambo, na wao wana
mitambo yao ya kuweka kumbukumbu, nitakachofanya ni kuhakikisha atukio yote
yanahakikiwa, ili ionekane kuwa shemeji, …alikuwa na dhamira ya kijiua mwenyewe….’akasema
‘Wewe
una kichaa, wameshakuharibu akili yako, na nikuambie ukweli sitakaa kimia hadi
nione haki inatendeka….’akasema Moto.
‘Sikiliza
rafiki yangu, hii dunia ina mambo, na ukijifanya wewe una huruma, mpole, mcha
mungu, wenzako wanatumia hayo kukudidimiza kwa masilahi yao…ukitaka kujietetea
wanakupeleka kwenye mistari, kuwa muogope mungu, usifanye hivyo, uwe na huruma,
wakijua kuwa ukifanya hivyo, wao wananeemeka…..’akasema
‘Sikiliza
rafiki yangu wakati umefika na wewe kula nao sahani moja…mnabanana hapo hapo…ukijifanya
mjanja, utaumia, na hutapata faida yoyote, hao watu unaotaka kupambana mimi
siwaoni, ni hisia tu, nilishafanya uchuguzi, mengi ni kuhangaika tu, huwezi
kupata lolote kwa hisia hizo, anyway…hilo
wazo langu tu, kaa fikiria hilo wazo
hadi kesho nikija unipe jibu, kwani, hata ufanye nini huwezi kumrejesha shemeji
duniani, au sio…’akawa kama anauliza
‘Ni
kweli tunatakiwa kuona haki inatendeka, lakini kwa hali hii ilivyo, ni wewe au
yeye, na yeye hawezi kuja kujitetea kuwa ulifanya wewe hivyo, kuwa ulimuua,
haiwezekani hilo, yeye keshaondoka, umebakia wewe,…kwanini umebakia ina maana bado
unahitajika duniani, …au sio…’akasema
‘Sasa
ukijifanya msamaria mwema, unakiri kosa haya, kwa vile ushahidi upo wazi, basi
wewe kiri kosa tujue moja, vinginevyo,mimi nakushauri kama rafiki yako .. tetea
shingo yako…hilo ni ushauri wangu tu, kama hutaki haya pambana na ukuta…’akasema
akisimama kuondoka.
‘Umemaliza…..’akauliza
Moto.
‘Ndio
hivyo, kama upo tayari nipe hiyo kazi, nitahakikisha kesi inafutika, na unardi
uraiani, uje tujiunge pamoja, ujijenge, uwe kama mimi , wekeza miradi, jiandae
vyema kwa familia yako, hizi kazi zina mwisho wake, utastaafu huna hata cha
kuanzia.nakuonea sana huruma…’akasema
Inspecta
Moto, akasimama na kuanza kundoka, akimuacha rafiki yake akiwa katulia na
alipofika mlangoni ambapo kasimama mlinzi akageuka, na akataka kusema neno….
WAZO LA LEO: Wakati wote
simamia kwenye haki na ukweli,…vikwazo, vishawishi na tamaa mbaya visikukwaze,
na kugeuka nyuma, ukasaliti haki, kwa jina la kuja kujitakasa baadaye, haki ina
masharti yake, mojawapo ni kuwa mkweli na mwanifu. Jijenge na tabia hiyo njema,
ya ukweli na uaminifu, kamwe hutajuta katika maisha yako.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Heʏ there! Someone in my Facebook group shaгed this website
ԝith us so I came to take a look. I'm definitely loving the infοrmɑtion. I'm bookmarking
and will be tweeting this to my followers! Wonderful blog and wonderfսl style and
design.
My weblоg: temp
An oսtstanding share! I have just forwarded this onto a coworker who had been doing a little homework on this.
And he actually bought me lunch because I discovered it for him...
lol. So let me reword this.... Thank YOU for the meal!! But yeah, thanks for spending time to talk aƄout this iѕsue here
on your internet site.
Revіew my homepаge :: clothes printables
Post a Comment