‘Hawa watu wanasema wana akili zaidi yangu kwa
vile wamekwenda kusoma Ulaya, Marekani, na wapi sijui, lakini hawajui mimi nina
akili zaidi yao, ngoja niwaonyeshe mimi nilivyo na akili zaidi yao,....’akasema
akikumbuka yeye alitaka kwenda kusoma nje, lakini baba yake alikataa, baba yake
alimwambia anatakiwa kuwa hapo kwani ana mambo mengi ya kujifunza kwanza
Lakini hata hivyo, alipelekwa kwenye shule ya
hali ya juu, akasoma, na darasani alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakifanya
vyema, hakumuangusha baba yake, na siku moja baba yake akamwambia;
‘Akili uliyo nayo najua baadaye utaitumia
vyema, nataka ujue utawala, ujue jinsi ya kuongoza watu, lakini pia nataka ujue
uchumi, ili uweze kuwa mzalishaji mnzuri, ...’akasema baba yake.
‘Nitajitahidi baba , lakini mimi nilitaka
kwenda kusoma nje, nijifunze mambo ya mitandao, napenda sana komputa...’akasema
‘Hayo yote utajifunzia hapahapa usijali, siku
pesa inaongea,...’akasema baba yake
Ni kweli pesa inaongea, elimu zote hizo
alizipata humu humu nchini, na japokuwa alikuwa na hali fulani ya ugumu, lakini
alipokuwa na komputa, aliweza kugundua mambo mengi, na baba yake akagundua kuwa
mtoto wake ana kipaji cha mambo hayo, lakini hakutaka kumuingiza huko moja kwa
moja,alitaka mtoto huyo awe mrithi wake..
Alipokuwa akiyawaza hayo, akakishika kile
kijitabu, na kufungua ule ukurasa ambao alishaanza kuandika kwa kifupi jinsi wazo
lake litakavyokuwa, jinsi gani anaweza kuyaweka mambo yake kwa
pamoja...akachora dunia, na kuiangalia kwa makini,halafu akachora mikono mingi,
ikiizunguka hiyo dunia, akaiangalia ile picha kwa makini , kwa muda
mrefu....halafu akatabasamu..
‘Ni ujanja mdogo tu ukiwa na akili kama zangu,
halafu tena uwe na pesa...hahahaha’akasema na kuanza kuandika mawazo yake
kwenye maandishi, aliandika kwa muda mrefu,...vidole vyake vilikuwa vyepesi
sana, kwa muda mfupi akawa amendika mambo mengi..
Baadaye akatulia, na akilni alijua kabisa licha
ya hayo mawazo yake, licha ya hayo malengo yake, licha ya kuwa ana
pesa,...lakini yeye peke yake hataweza, ...hata pesa alizo nazo, hazitatosha,
kunahitaji pesa nyingi zaidi...
‘Mmmh, kweli pesa hazitoshoi hata uwe na pesa
za kuijaza hii dunia,..lakini kianzio kipo...’akasema na kuanza kupiga mahesabu
yake, na alipofikia mwisho akajikuta anahitaji pesa mara mbili ya hizo
alizonazo...
‘Haiwezekani....’akasema,
‘Hata hivyo, hata nikiwa na pesa kuna tatizo
jingine,...nahitaji vichwa, nahitaji rasilimali watu, na watu hao wawe na
utashi wa hali ya juu, wawe na ujasiri...’akasema na kuandika hayo mawazo
‘Wakati mwingine, kama ikibidi, kutakuwa na
kumwaga damu..’alipowaza hivyo, akainua kichwa na kuangalia kile kisu, na rangi
nyekundu iliyokuwa kwenye kile kisu, ilionekana kama inavuja,...hizo ni hisia
zilizokuwa zikimjia akilini
‘Kwahiyo nahitaji watu ambao wapo tayari hata
kuua....hilo sio tatizo nitawajenga, kila kitu kinawezekana kama ukiwa pesa,
....’. Akatikisa kichwa na kusema;
‘Ukiwa na pesa, ukawa na utajiri kama huu huwezi
kushindwa kitu, sijui kwanini wazee hawa walikuwa wakiishi kwa shida, wakati
pesa wanazo, utajiri wanao lakini waliukalia, sasa mimi nitautumia, tatizo ni
muda, tatizo ni namna ya kuanza, tatizo ni hawa watu , rasisilimali watu
watakavyonielewa,...’akasema na kuanza kuandika mambo mengine kwenye hicho
kitabu, hadi ukurasa ule ukajaa tena....
Kabla
hajafungua ukurasa mwingine mpya, akaona afanye marejeo kidogo, akafungua
ukurasa ule wa mahesabu ya pesa, akaongeza mistari mingine na kuweka kiasi cha
pesa, na pesa anayohitajika ikazidi kuongezeka,...akaangalia kiasi cha pesa kilichopo benki, akakigawa mara
nne, kwanza fungu la kujiwezesha, pili
fungu la kuwezesha, tatu fungu la kuwekeza, nne, fungu la dharura...pesa
imekwisha....
‘Pesa haitoshi, mmmh, haiwezekani....’akasema
na kuguna
‘Ina maana pesa zote zimeisha kwa haya mambo
manne tu, haiwezekani, ....’akasema
‘Lakini huyu baba aliwezekaje kuwa na pesa nyingi
kama hizi...hii miradi aliwezeaje kuimudu mwenyewe, .....?’ akajiuliza
Alifungua ukurasa mwingine, ambapo kuna
watendaji wa kampuni za baba yake, akawaangalia hao watu, aliona wengi ni
wazee, akaanza kuangalia kisomo chao, akaguna, na kuanza kuandika mapendekezo
yake, alipomaliza akasema;
‘Hawa hawanifai...nataka vichwa
vingine,....hawa hawataweza kupokea mafunzo yangu, nataka watendaji wanaoweza
kubuni mambo mapya, wasiogope kuthubutu, hilo nitalifanyia kazi...’akasema na
kuandika maazimio, halafu akafungua ule ukurasa wake wa kwanza, lakini mara
akakumbuka jambo, akasema.
‘Kwanza lazima niongee na hawa mameneja wote,
pili nihakikishe hakuna kinachofanyika mpaka mimi nitoe idhini, na tatu pesa
zote kuanzia sasa zitaingia kwenye account yangu....’hapo akacheka na kuikuza
picha yake ya dunia ikiwa na mikono mingi...
‘Bila hivi wajanja watanizidi,...mmh, kwanza
niongee na huyu mhasibu wa mzee, mmh, hata yeye ni mzee, kwanini baba alipenda
kuwaweka watendaji wake wa karibu wazee, huyu nitamuondoa,...ngoja kwanza
niongee naye, nione kama kuna pesa nyingine zimeingia,.....’akampigia huyo
meneja fedha, na kumuuliza, na aliambiwa hakuna fedha iliyoingia tangu baba
yake afariki maana wawekezeja wengi, hawajakuwa na amani, na utawala mpya...
‘Kwanini, nyie sasa mnafanya nini maofisini?’
akauliza
‘Kazi zetu zipo kila siku kuwe na pesa au
kusiwepo na pesa, kuna mambo mengi tunafanya, ...’akasema huyo mzee
‘Naona, hamuwezi kazi...kama hakuna pesa,
sihitaji watendaji wengi...nataka uje ofisini kwangu na mahesabu yako yote,....na
uje na wazi jipya la kunihakikishia utendaji wako, kama huna wazo jipya, sizani
kama utanifaa...’akasema
‘Nitakuja tu kijana..mzee, bosi....’akasikia
huyo mzee, akishikwa na kigugumizi, na hapo Diamu akatabasamu na kusema;
‘Hivyo ndivyo nataka, nikiongea, watu
wanagwaya, mzee, sasa ananiita mzee,...hahahaha...’akacheka na huku akifungua
ule ukurasa wa mawazo yake, na akawa anakumbuka maneno ya mama yake;
‘Mwanangu uwe makini na hao wazee wa siku
nyingi, hao watakuwa kikwazo kwenye mambo yako, hao wanafahamu kila kitu kuhusu
mzee wako, kuna muda walihisi kuwa mzee , baba yako kauwawa, hao wazee wanaona
mbali sana, .. cha muhimu ni kwenda nao taratibu ukiweza waondoe mmoja mmoja,
ila uwe makini, wanaweza kukuharibu kabisa....’akasema mama
‘Mimi siogopi mtu...’akasema
‘Sio swala la kuogopa, ni swala la
kukuharibia...’akasema mama
‘Mimi nitajua jinsi gani ya kuwaweka sawa,
usijali mama, huyu mtoto wako haogopi kitu, baba alinijenga kuwa
jasiri...nitajua ni nini cha kuwafanya....’akasema
Wakati anawaza hivyo, mara mlango ukagingwa na
huyo mhasibu akaingia ni mzee , ni makamo ya baba yake, na wakasalimiana, na
wakaongea, na yule mhasibu alijaribu kumuelezea ni kwanini wawekezaji hawataki
kuwekeza, lakini ndani ya akili ya diamu, hakutaka kuelewa, alijua kila jambo
lina njia, haiwezekani, ...halafu akasema;
‘Ok, sasa naanza kuelewa, kumbe hilo nalo ni
tatizo, hapa sasa nahitajia kichwa kipya, cha ushawishi, ni lazima hawa watu
warudi kwenye mstari, ni lazima wote waje kwetu, sioni kwanini mzee, hebu
niambie kuna mbinu gani tunahitajika kutumia?’ akauliza
Yule mhasibu akajaribu kumuelezea kitaalamu,
kuwa yeye anahitajika kuonyesha kuwa kweli anaweza kusimamia mitaji yao, je
kweli anaweza kuhakikisha mitaji ya hao watu itakuwa salama, na kuna kikao
kitakaa kuamua kama wataendelea kuwekeza hapo kwenye kampuni au watakwenda
kuwekeza kwingin....blabla...., hakutaka hata kusikia zaidi.
‘Mzee, hivi ni mimi nahitajika kuwaonyesha au
wao waonyeshe kuwa wananotaka kuwekeza kwangu, hivi hawa watu hawajui kuwa mimi
nimeshikilia mpini,...kumbe eeh, lakini hivi kwanini wasumbue, kwanza hadi sasa
mimi nina mitaji yao tayari, mtu akisema hataki kuendelea na mimi, mtaji wake
hapati,...hilo nataka walielewe, pili, mitaji yao, nikuitumia mimi, bila wao kupata hata senti moja, watanifanya
nini?’ akauliza
‘Watakushitaki, kuna mikataba kisheria, hilo
kijana wangu usijaribu kufanya, watu hao wana mawakili wao, na kwanini ufanye
hivyo, muhimu ni kuwahakikishia tu, uwe na ushawishi, kivitendo, sisi tumeishi
miaka mingi kwenye miradi ya kampuni ya baba yako tutakusaidia,...’akasema mzee
‘Hahaha, mikataba kisheria...sheria, eeh, na
mwanasheria wetu ni nani, ni yule mzee, mmh,wazee, wazee kila kona wazee...nitataka
kuongea naye, usijali mzee, tupo pamoja, nitahitaji uzee wako kwa muda, lakini
baadaye, nitajua la kufanya ....’akasema akiandika kitu kwenye kijitabu chake.
‘Mzee, wewe niachie mimi hayo, ila nahitaji
mahesabu yote, nahitaji kila kitu ulichokuwa ukikifanya, kesho ukija hapa
tutakaa nataka kujua kila kitu ulichokuwa ukikifanya, usiache hata jambo moja,
...umenisikia mzee wangu...?’ akasema
‘Lakini utakuwa muda mfupi kuweza kufanya hilo,
nakushauri muhimu tuwe na ajenda ya kushawishi wawekezaji kwanza, tusianze
mambo ya ndani yatakayoleta sintofahamu, wakahisi kuna migongano...ni muhimu
sana hilo kibiashara...’akasema mzee
‘Mzee wewe, unaweza kwenda...mimi najua ni kitu
gani nafanya, wewe utaona mzee, hapa yupo kichwa, Diamu, unafahamu maana ya
jina hilo....’
‘Nakumbuka baba yako alipotaka kukupa hilo jina
nilikuwepo, akasema anataka jina tofauti, akasema atakuita jina la kipekee, na
mama yako ndiye akalitaja jina hilo, lakini wazee wengi walipinga, kwani sio
majina ya kifamilia,....’akasema
‘Basi mimi nafahamu maana ya jina hilo, jina
hilo maana yake ni damu ya shetani...hahaha...’akasema na kucheka, na yule mzee
akamwangalia kijana yule kwa mshangao na kusema
‘Mwanangu hiyo sio maana yake usijiumbie
ubaya....ujue jina linaweza kukufanya uwe na tabia hiyo hiyo unayofikiria
wewe,...’akasema mzee
‘Yah, mimi nahisi nipo hivyo, ....kwani hao
nikisema ndio nimekuwa, hata hivyo, sioni ajabu, mzee, wewe hunifahamu mimi
nipoje ndani, lakini ipo siku utanifahamu,...’akasema akimuangalia yule mzee
kwa macho makali, hadi yule mzee akakunja uso kuonyesha wasiwasi, akageuka na
kuanza kuondoka, na Diamu akamuangalia yule mzee wakati anatembea, akatikisa
kichwa na kabla yule mzee hajafunga mlango Diamu akasema;
‘Mzee, pia, natumai kwa muda uliokaa na mzee
wangu, umewekeza mahali,..nataka ukakae kwenye miradi yako, ujitegemee,
unalionaje hilo wazo, waachie vijana wawajibike, au nitakuwa nimekosea?’
akauliza na yule mzee, akasema;
‘Utakuwa umefanya haraka kuchukua maamuzi hayo,
sikatai, hata hivyo nilishaomba iwe hivyo kwa baba yako, baba yako akakataa,
akasema ananihitaji sana, sasa kama wewe unaona hivyo, basi lakini kwa kuanzia
sisi ni watu muhimu sana, maana tunafahamu wapi baba yako alipotoka hadi hii
leo, hujui siri ya mafanikio ya baba yako, huwajui maadui zake, kijana
unatuhitajia sana sisi ....’akasema mzee huyo kwa sauti ndogo ya kutia huruma.
‘Mimi nafanya hivyo kwa nia njema tu, sio
kwamba siwahitaji, nawahitaji sana, lakini yatakayotokea mnaweza mshindwe
kuvumilia,...sitaki kupata laana nyingine, hapana, hata hivyo, uongozi wangu
utakuwa wa mikikimikiki, sijui kama watu kama nyie mtauweza,...nataka
tusaidiane jambo kwanza utaniambia unahitaji kiasi gani cha kukuza mtaji wako, tuone
tutasaidiana vipi, ninaweza kukuhitaji tena na tena, maana mzee alisema wewe ni
muaminifu sana, umeishi naye kwa uaminifu mkubwa...’akasema
‘Hamna shida, ila kwa ushauri wangu wa mwisho
ni kuwa mageuzo unayotaka kuyafanya, usiyachukulie kwa pupa, hata nyumba
haijengwi kwa siku moja, ni vyema ukaenda hatua kwa hatua kidogo kidogo, mwishowe
utaweza kusimamia shughuli zote kwa makini zaidi,...wawekezaji ni muhimu sana
kwenye kampuni, ukiwakosa hali itakuwa mbaya...’akasema huyo mhasibu
‘Mzee, usijali, hakuna kitakachoharibika, ila
nawaonya wenye nia mbaya, kama kuna mtu ataanza kuleta balaa, akafanya fitina,
mimi nitamuona, nitahakikisha anakwenda kusikojulikana.....nimeshajiandaa kwa
hilo...’akasema na yule mzee akasema
‘Hakuna mwenye mawazo hayo, ni kusaidiana tu,
ila kwa hilo unalotaka kulifanya utajiharibia, na sisi wazee kama unatuona
hatufai kwenye ofisi yako tutaondoka tu, ila utakuja kutukumbuka...’akasema
‘Sawa mzee, cha muhimu ni kujua kuwa kila jambo
lina muda wake, umri nao unakushitaki, huoni mzee kuwa unahitajika kumpumzika,
ni muhimu wewe ukaa-kaa nyumbani,...nakushauri hivyo, kaa jipange nipa mahesabu
yako, ili upate kianzio cha uzeeni, au sio mzee...?’akasema na yule mzee, alifunga
mlango bila kusema neno.
‘Hahaha mzee kazeeka kupita kiasi kwa muda
mfupi tu,....mzee wangu kaondoka itakuwa yeye, ngoja kwanza, hata hivyo kanipa
wazo, wazo jipya, hapa ni lazima niwarejeshe hao wawekezaji kwenye mstari, ni lazima
kwanza nimtafute huyu mtu wa kushawishi, .....’akabponyeza kitufe kwenye simu
ya mezani, na mara sauti ikasema;
‘Bosi nakusikiliza...’ile sauti anayoipenda
kuisikiliza ikasema;
‘Njoo hapa mara moja kuna kazi nataka unifanyie
mara moja....’akasema
Yule binti akafika, na kusimama mlangoni,
akionyesha lile tabasamu lake analolijua mwenyewe, huwa akilitoa hilo tabasamu
watu kama akina Diamu, hawakatizi ni lazima watasema neno.
‘Ingia ukae hapa kwenye kiti, kuna mambo nataka
tuyafanyie kazi, nataka unisikilzie kwa makini, ukifika nyumbani leo nataka ukae,
upasue kichwa na ubuni mbinu na kesho nataka jibu,....unakumbuka
nilipokutoa....?’akauliza
‘Bosi nawe bwana, kwanini unasema hivyo...mpaka
uanze kuninyanyasa...’akasema huyo binti akijibaragua kimadoido.
‘Aaah, sio kukunyasa kama unavyofikiria wewe, mimi
ninachotaka ni kutumia vipaji, wewe una kipaji, au sio....?’ akawa anauliza
‘Kipaji gani bosi, mimi sio muimbaji....?’
akauliza
'Hicho ulichokuwa ukikifanyia kazi,nataka
ukumbuke zile mbinu za mitaani, jinsi gani ulivyoweza kuwapata watu wakubwa,
ambao walijifanya hawapatikani, jinsi ulivyoweza kuwaachanisha waume na wake
zao,....’aliposema hivyo, yule binti akacheka hadi bosi akabakia ameduwaa, na
baadaye bosi akauliza
‘Unacheka nini,...mimi nipo kikazi
zaidi...’akasema Diamu
‘Nimecheka maana sikutegemea bosi kama wewe
utafikiria hayo mambo yangu kama yana faida, ...’akasema
‘Hahaha, kila kipaji kina faida, watu
hawajui,...mimi nataka kufanya mambo ambayo hayajawahi kufanyika, vipaji,
akili, ujanja, umbeya,....ni rasilimali...’akatulia kidogo
‘Bosi...’akasema huyo binti
‘Nataka ufikirie, nakuhitajia kwa kazi maalumu,
kwanza nataka uelewe kuwa mimi nimekuchukua kwenye hii ofisi sio kwa ajili ya
kuangalia urembo wako tu, nataka huo urembo wako uwe ni mtaji, una kazi muhimu
sana,...kwa hivi sasa nahitajia sana mbinu zako za mitaani,nataka kuutumia
uzuri wako kifaida, unasikia, kaa uwaze uchanganue uje na wazo tofauti
...’akasema
‘Kweli bosi hata mimi nilikuwa na wazi kama
hilo lakini nilikuwa naogopa kukuambia, kama utakubaliana name, mimi nitafanya
lolote unalotaka maana wewe ndiye unayeniweka hapa mjini...’akasema akijerembua
‘Kuna watu nataka waingie kwenye mtandao wangu,
wamejifanya kutokuwekeza kwenye kampuni yetu, kisa hawaniamini, na sasa hivi tunahitaji
pesa nyingi sana, sio kwamba hatuna pesa, pesa zipo, lakini tunahitajia pesa zaidi,
kabla ya kuanza wazo langu nililo nalo kichwani ni lazima tutafute pesa,....’akasema
‘Wazo gani bosi, mbona kila siku unasema
unawazo, unawazo..ni wazo gani hilo?’ akauliza
‘Wazo hilo litakuja kutajwa wakati muafaka, ila
nataka wewe uwe mtu wangu wakaribu sana, maana tumetoka mbali, wewe ndiye
uliyenifundisha mambo fulani, ukanitoa tongo tongo za aibu, ukanijengea ujasiri
nisokuwa nao kabla, ...wewe na mama ni watu muhimu sana kwangu siwezi kukutupeni,
ila na wewe usiniangushe,...’akasema
‘Siwezi kukuangisha bosi wangu...’akasema huyo
binti
‘Ninachotaka nikutumia kipaji chako, nataka
nianze kwa hilo kwanza, vipaji, vipaji ni mtaji nyie hamjui tu,...mmh, hilo ni
muhimu sana kwasasa..., unasikia, jikumbushe, na pia kaa fikiria, unipe mawazo,
nataka mawazo yenye kujenga, unasikia, usikae tu hapa ukitegemea nikulipe, hapana,
ni lazima na wewe uonyeshe kipaji chako au sio, ...’akasema
‘Lakini....’akataka kusema neno baadaye akasita
‘Lakini nini, unajua wewe ulikuwa mitaani,
ukawa unakutana na watu mbali mbali, wengine wakubwa, uliniambia hata
waheshimiwa ulikuwa unakutana nao, na hao ndio walikufanya ung’are zaidi,ukajenga,
una gari la bei mbaya, ..mmmh, sasa
nataka tukae tupange, nina wazo jipya kwako, litaleta tofauti,isiwe gari tu,
nyumba tu, sasa fikiria zaidi ya hayo, wewe nenda ....ngoja nifikirie
kwanza...’akasema
‘Lakini bosi mawazo si mazuri, usiumize kichwa
sana, mbona una utajiri wa kutosha, utajiri ulio nao unaweza kula wewe na
wajukuu zako, kwanini uumize kichwa?’ akauliza yule msichana na yule jamaa
akamuangalia bila kusema kitu, baadaye akasema;
‘Nina wazo kubwa sana, na hilo wazo tukiliweka
kwenye matendo, likafanya kazi, dunia itaniheshimu, kila mtu ataniheshimu, hata
wewe mwenyewe utaniheshimu...’akasema
‘Bosi mbona hata hivyo mimi nakuheshemu sana
tu...’akasema
‘Bado,...sijapata heshima inayostahili,....’akasema
‘Kwahiyo bosi nifanye nini?’ akauliza
‘Hilo sasa ni tatizo, watu ninaowataka mimi, ni
kuwa nikiwaagiza jambo, wanajua ni nini cha kufanya, akili zao zinatakiwa ziwe
pana, ...naona kwanza unahitajia shule, nitakuepeka shule, shule maalumu,
ukitoka huko, sitapata maswali kama hiyo, ...nikisema fanya hiki, natarajia
matokeo, mimi nataka vichwa, watu wanaofikiria, wabunifu...’akasema.
‘Sawa nimekuelewa bosi,....’akasema yule binti
huku akitabasamu, alisubiri kidogo, alipoona bosi wake kazama kwenye mawazo,
akasimama akatembea kuelekea pale alipokaa bosi wake na kuanza kumkanda kanda
mgongoni,
Mhh, unaona hiki ni kipaji...sasa nataka haya
uyafanyie kazi, kila atakayeingia kwenye anga zetu, ni biashara...lakini zaidi
ya hayo, kila tunalolitaka tunapata, nataka wewe ukishaiva unakuwa mwalimi wa
wengine....unaona raha hii unayonipa, ukiwapata hawa waheshimiwa, hawa
matajiri, watakubali tu...inatosha, ...’akasema na yule binti akaacha na jamaa
akasema
‘Unaweze kwenda mrembo, lakini kumbuka, kesho,
nataka jibu, nataka unipe mipango yako,....kesho nataka wazee wote wafungashe
virago, kesho...., nataka kuanza kulifanyia kazi wazo langu, kesho, kesho.....’
NB: Hivi huyu jamaa vipi, hebu tuone mawazo ya
watu kama hawa, ambayo ndio yapo kila mahali kwa sasa,
WAZO LA LEO: Akili
aliyotupa mungu ni kwa ajili ya kutuwezesha kuishi kwa amani, vipaji alivyotupa
mungu, ni kwa ajili ya kutuwezesha tuweze kuyamudu maisha yetu ya kila siku, je
ni wangapi wanatumia vipaji vyao vyema, kwenye malengo mema. Kila mtu ana
kipaji chake, basi tufikiri njia njema yenye manufaa kwa mtu mwenyewe na kwa jamii.
nnmimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment