Marejeo: Turejee pale
Maua alipokuwa akiikimbia Simba iliyojeruhiwa, na baadaye akapoteza fahamu, na
alipozindukana akajikuta yupo kwenye kijumba, na harusi kali ya pombe
ikitawala, kuashiria kuwa hapo, kama sio kilabu ya pombe, basi kuna mnywaji
aliyebobea….Haya tuendelee na kisa chetu, tuyaone maisha ya mama huyu kwa huyo
mukozi wake.
‘Naona sasa umezindukana, una…bahati sa..ana wewe mwanamke,
ungakufa, sijui kwanini mwanamke mrembo kama wewe unaishi porini,…wewe
ulitakiwa uishi na sisi huku duniani. Sisi ndio, matajiri wa hiki kijiji,
….mimi watu wananiita mlevi, lakini…sijanywa pombe zao,….ooh, ngoja nicheua
kidogoooh, Bhoooh’ akawa anaongea kilevi na altulia pale alipokuwa akicheua na harufu iliyotoka hapo.
Mama alisema harufu ilitoka hapo, …hajawahi kuiskia katika
amsiha yake yote, ni harufu ya uozo,…na hapo hapo, akashikwa na kichefu chefu,
na kuanza kutapika, na yule mwanaume alipoona hivyo, akaanza kucheka, alicheka
sana, hadi akadondoka, na baadaye akaondoka zake huku akisema;
‘Unatapika…hujanywa, unatapika, je ukinywa itakuwaje,…usisumbuke,
matapishi nimeyazoea, naishi nayo, nashinda nayo,…ni kawaida tu, ..ngoja
nikadai pesa yangu, …’akaondoka hapo akiwa anapepesuka.
Baadaye walikuja
watoto wawili, wakamletea chakula, na alipowadadisi mama yao yupo wapi, mwanzoni
walisita kumwambia. Nafikiri walikuwa wakimugopa baba yao, au kuna jambo
limejificha hapo, na hawo watoto hawakupenda kuliongelea, ila baadaye mmoja wao
ambaye ni mdogo ukilinganisha na mwingine akasema;
‘Mama alimtoroka baba kwasababu …..’alipoanza kuongea
mwenzake akamfinya na kumwambia atapigwa na baba. Maua akawaangalia kwa muda, na walionekana
kujawa na huzuni kutokana na swali hilo, na akasema;
‘Mimi nilitaka tu kujua mama yenu yupo wapi, kama mnaogopa
kupigwa basi, ila nawashukuruni sana chakula huki kizuri ni nani kawapikia hiki
chakula?’ akawauliza. Kwanza waliangaliana na huku wakitabasamu, na hata
kucheka na yule mkubwa akasema;
‘Tumepika wenyewe, ….nani angetupikia, …sisi wenyewe tunajua
kupika, mama alitufundisha, ‘akasema huyo mkubwa.
‘Chakula kizuri kweli, inaonekana mama yenu alikuwa
akiwapenda sana’akasema Maua. Na swali hilo lilionyesha kuwagusa sana, kwani
sura zao zilionyesha huzuni, na Maua alizania huenda wangeliangua kilio, lakini
inaonekana walishazoa haya maisha na yule mdogo akasema;
‘Mama alitufundisha kupika kwasababu alikuwa hashindi
nyumbani,…’akasema yule mdogo ambaye alikuwa tayari kuelezea kuhusu mama yake,
na mwenzake akachukua vyombo na kuondoka navyo, na hapo Maua akaona amuulizie
vyema huyo mtoto kuhusu mama yao.
Huyo mtoto alikaribia miaka kumi au kumi na moja, ..na kaka
yake huenda ni kati ya kumi tatu, au kumi na nne, walionekana wakakamavu
mwilini kuonyesha kuwa wanafanya kazi nzito, au kazi za suluba, na nguo zao
zilichakaa sana, na chafu.
‘Mama alikuwa akifanya biashara ya pombe na walikuwa
wakishirikiana na baba, …lakini kila mara wakirudi nyumbani, wanaishia kugombana,
kila mmoja anamshuku mwenzake kuwa kachukua pesa za biashara yao, na wakianza
hivyo, hawalali mpaka wapigane..’akasema huyo mtoto.
‘Na nyie wakati huo mko wapi?’ akamuuliza.
‘Tupo hapa hapa nyumbani,..tunaangalia tu, maana ukitaka kuingilia
ugomvi wao, unakugeukia wewe, na unaweza ukachapwa mpaka uvimbe, …na mara
nyingi tukiwaona hivyo, tunajifungia hapa chumbani kwetu, tukiomba mungu
wasiumizane’akasema huyo mtoto.
‘Ina maana wanapigana hadi kuumizana?’ akauliza na yule
mtoto akacheka kicheko kidogo, na kusema
‘Kuumizana…Watu wanapigana na chochote kilichopo mbele yao,
kama kuna vyombo, wanarushiana,….kuna siku mama alipigwa hadi akapoteza fahamu
na kuvunjika mkono’akasema
‘Kwahiyo ndio akaondoka, na kuwaacha peke yenu?’ akamuliza.
Yule mtoto akatulia kwa muda kama anawaza jambo, halafu akasema;
‘Hapana hakuondoka siku hiyo hiyo…, kwani kesho yake, baba
alimsadia wakaenda hospitalini, na alikaa hadi akapona, na kipindi chote hicho,
mama alichokuwa akiumwa, baba hakuwa akilewa sana, alikuwa analewa kidogo, kwa
vile biashara yenyewe ilihitaji kuonja onja….lakini alionyesha kumuhurumia sana
mama, ….’akasema
‘Sasa kwanini mama aliondoka, inaonyesha walikuwa wakipenda
sana’akauliza Maua.
‘Baba mwanzoni walikuwa wakipendana sana, tukiwa wadogo,
walikuwa na maisha mazuri,…baadaye baba akaachishwa kazi huko alipokuwa
akifanya, akaanzisha biashara, ….lakini bishara haikudumu, ndio wakajiingiza
kwenye biashara ya pombe, hapo amani ikawa haipo tena.
‘Hebu niambie, mliwezeje kuishi katika hiyo hali, hakuna
chakula, …wazazi wanapigana?’ akauliza Maua akiwazia mbali, kuwa na yeye ana
mtoto, na huenda mtoto wake huko alipo atakuwa anateseka, hapo aakjikuta
machozi yakimlenga lenga…
‘Mwanzoni tulipata shida sana, tnalia njaa mama hana cha
kupika, inabidi wakati mwingine aende kufanya kibarua kwa watu, wanamsimanga,
na wanamuibia,…hadi walipoamua kuanzisha hiyo biashara ya pombe..lakini ikawa
ni tatizo jingine,…maana ule upendo wa wali ukaondoka, …mwanzoni walipokuwa
wakipigana tulikuwa tnalia sana,…hadi tukazoea…tutafanyaje tena….’akasema
akionyesha uso wa huzuni.
‘Wakati mwingine ni marafiki,…lakini tatizo ni wakilewa..’akasema
na kutuliwa..
‘Kwahiyo mama akaondoka?’ akauliza Maua akiwa keshazama
kwenye huzuni na mawazo
‘Siku mama alipoondoka, ni pale baba alipomshuku mama kuwa
kaiba pesa, na ana mwanaume mwingine, na mama akawa anakataa, lakini baba
aliendelea kumshuku hivyo, na kauli hiyo kila mara baba alikuwa akiiongea, na
mama hakupenda kusikia hivyo, kuwa ana mwanaume mwingine, Na siku hiyo ambayo mama
hakuweza kuvumilia tena hadi akaamua
kuondoka , na pale alipofika mwanaume mmoja akidai pesa zake…’akatulia.
‘Pesa gani hizi, ina maana huyo mwanaume alimkopesha mama
yako?’ akaulizwa.
‘Hapana sio kuwa alimkopesha mama hizo pesa zinazodaiwa,
huyo mwanaume alisema alinunua pombe, lakini hakupewa chenji yake, na mama
akasema hakumbuki kupokea pesa yake, labda kama baba ndiye alichukua. Wakawa
wanabishana na huyo mtu, ambaye alionekana kulewa, hadi kufika kuanza kupigana.
Wakati huo huo baba akatokea na kuwaona mama akiwa kashika
na yule mwanaume, wakiwa wanapiga, baba yeye alichukulia vingine , aliona kama
wapo kwenye….’ Yule mtoto pale akatulia na kuinama chini.
‘Sawa nimekuelewa endelea ikawaje?’ akauliza Maua.
‘Basi baba akaja kwa hasira na kuwavamia akaanza kupigana na
huyo mwanaume akidai kuwa ndiye anayemuibia mkewe…..na mama alipoingilia kati
ikaanza kupigwa yeye, ikawa baba anapiga na watu wawili, baba akazidiwa, na
aliumizwa kweli kweli..’akasema huyo mtoto.
‘Na ndio mama akaondoka?’ akaulizwa.
‘Walipigana sana siku hiyo na kesho yake, pombe
zilipowaishia, bado baba akasisitiza kuwa mama na huyo mwanaume ni marafiki, ndio
maana wamemhangia na kumuumiza, …mama hakukubali, ….akasema kama hamuamini basi
anaondoka,..…’akasema huyo mtoto.
‘Baba alipoambiwa hivyo alisema nini?’ Maua akauliza
‘Baba aliingia ndani na kukusanya nguo za mama akazitupia
nje, na kusema kuwa hataki kumuona tena mama hpo ndani, kwani keshawafuma na
mbaya wake, na mbaya zaidi wamemchangia na kumuumiza,…’akasema huyo mtoto.
‘Ina maana kumbe baba ndiye alimfukuza mama, na mama
alipoondoka hakurudi tena, au hakuna mtu aliyekuja kuwasuluhisha?’ akauliza
Maua.
‘Mama hakurudi tena, ..na hakuna mtu aliyekuja, ..nani
angekuja huku, wakati mama na baba wametengwa na jamii, kwasababu ya biashara
yao, na kulewa, watu wanawapiga vita, na kila mara maaskari huja hapa
kuwatafuta, na mara nyingi wanakwenda kujificha huko porini’akasema huyo mtoto.
‘Sasa nyie mnasoma shule?’ akamuuliza.
‘Shule tuliacha…mimi niliachia darasa la tano, na kaka naye
aliachia la saba, hakuwahi kufanya mitihani, …tunafanya vibarua, ….kupata pesa
ya kula’akasema huyo mtoto.
‘Ina maana hata pesa za matumizi baba yenu hawapatii?’
akauliza.
‘Kuna siku anatupatia, siku nyingine, ….kama ndio kakimbilia
porini, akitafutwa na maaskari, inabidi tujua wenyewe tutaishi vipi, sisi sio
watoto wadogo tena, tunajua kuishi, leo nikipiata kidogo, naleta tunapika
chakula…’akasema huyo mtoto.
‘Kwahiyo mama yenu hakuwahi kurudi hapa tena?’akamuuliza
‘Toka siku hiyo alipoondioka hajawahi kurudi tena, na
hatujui kabisa kaenda wapi, na baba ameapa kuwa akimuona atamchinja’akasema
huyo mtoto
‘Kwanini afikie hatua ya kusema hivyo?’ akaumuuliza.
‘Anasema mama alipoondoka aliondoka na pesa yake yote ya
mtaji, …’akasema huyo mtoto na mwenzake akawa keshafika. Na usiku ikaingia, na
kwa mbali wakasikia sauti ya mtu akiimba, …na watoto wakamwangalia huyo mgeni
wao pale kitandani, na mmoja akaguna na
kusema;
‘Baba huyo anakuja,….sijui kama kutakuwa na amani hapa ndani….’akajifunika
gubi gubi, na muda huo huo mlango ukagongwa kwa fujo…ulifunguka kama vile
unavunjwa, na huyo jamaa akadondokea ndani, huku akilalamika.
‘Mimi nagonga hamtaki kufungua…huyu mwanamke hajarudi eeh,
akija hapa ama zake ama zangu….na nasema siku nimuona kichwa chake ni halali
yangu…nyie watoto,..mmh, ooh, nimekumbuka, huyo mwanamke bado yupo humu,….?’ Akatulia
kidogo kama vile anasikiliza jibu.
‘Mnajifanya mumelala, su sio….mumeshakuwa madume, nyumba hii
dume ni mimi peke yangu…nyie bado watoto…kama mumekuwa madume, tafuteni nyumba
yenu…mnasikia, kesho mkatafute sehemu yenu,…sitaki presha hapa’akasema halafu
akatulia, ikawa kama amelala, na muda wote huo, alikuwa kalala pale sakafuni
alipoangukia.
‘Kwanza mumempa chakula huyo mgeni….aah, mgeni…ndio huyo
namuita mgeni, kwa leo,…nauliza mumempa chakula, …lakini mgeni siku ya kwanza,
ya pili, ya tatu, chukua jembe ukaafanye nini…..nimesema hivyooooooooh’
akatulia na kuanza kukoroma pale pale alipodondokea na baadaye akashituka na
kusema
‘Kesho wanakuja wageni…wageni wa mgeni, wanasema wanamleta
mtoto…nani atalea mtoto mchanga hapa, hilo nimelikataa…sikubali, unasikia wewe
mwanamke, …ooh, nisemehe, mgeni, aah, ngoja nilale, maana mnajifanya wote mume
lala, ila nata unielewe….’akatulia.
‘Wakilte huyo mtoto, eti mtoto mdogo,…sijui ana umri gani,…nani
atamlea….sitaki presha..utapanga mwenyewe kunyoa au kusuka, ukae hapa, usiwe na
mtoto, kama una mtoto, tafuta sehemu nyingine, kwanza nasikia ulitakiwa ufe….sasa
nimekuokoa, …mimi ndiye muokozi wako, unisikilize mimi..haya usiki mwema…’akaanza
kukoroma, kama radi.........
NB, Hayo ndio maisha ya mama Maua, tukutane sehemu ijayo
WAZO LA LEO:
Ukijiona umekuwa, ujue kuwa kuna wazazi waliokulea, na malezi mengine ni ya
taabu sana, …taabu hiyo aijuye ni huyo mzazi, kwani uchungu wa mwana aujuaye ni
mzazi,. Kwahiyo ni vyema, tukawakumbuka
wazazi watu, au walezi wetu ….kwasababu vyovyote iwavyo, bila wao, usingelikuwa
hapo ulipo.
Lakini wazo letu la leo linasema; Kuna watoto hawajui
kabisa ,mzazi wake ni nani, huyo hakupenda kabisa kutokuwa na wazazi, …alihitaji
pendo la wazazi kama wewe, lakini kwa sababu mbalimbali hamjui mzazi wake. Wewe na mimi
ndiye mzazi wake, ukila , ukasaza, ukatupa jalalani, ujue unafanya kosa kubwa
sana, ulitakiwa umkumbuke huyu mtoto…
Jamani tuwakumbuke mayatima na watoto
walio kwenye mazingira magumu.
Kwa hali ya sasa hivi watoto wanaopita mabarabarani wakiomba
wanaongezeka, hao ni wa mabarabarani tu, kuna watoto wapo mitaani tunapoishi, kuna watoto wapo
mjumbani, ambao hawajui leo au kesho watakula nini …hebu tujiulize
ungejisikiaje kama mtoto huyo ni wa kwako, ndio ni wa kwako, lakini fikiri katoka tumboni kwako, na ndio huyo yupo katika hali hiyo, yupo barabarania akiomba, au yupo
nyumbani lakini hana chakula, analilia chakula, lakini chakula hakuna, wewe
umejaliwa, unakula unasaza, unatupa,..mnaandaa masherehe ya mamilioni..…
Mimi na wewe ni mzazi wa huyo mtoto, …ukila ukisaza na
kutupa, au ukashinda kwenye baa na kunywa hadi kupitiliza, ukafanya sherehe ya
kufuru,….unafanya makosa kwani umemsahau mmoja wa mtoto wako….
********************************************************************
Kumbe tarehe 5-December ndio siku ya kuzaliwa kwa emu-three, ooh, jamani siku zinakwenda kama mchezo, nashukuru kwa kunikumbusha hili;
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Hii leo imeumiza imekata kabisa utumbo..maana ni kweli kuna watu wana maisha mazuri na watoto wao wanaangaika wanakula na kusaza ...hakika sisi binadamu sijui tumeumbwaje?:-(
Unanimaliza kabisa pale unapoweka wazo la leo, twakushukuru sana na kazi ya mikono yako ikuwezeshe ili uzidi kutupa zaidi. C.R
Inaumiza sana kwakweli, watoto wanahangaika hawana msaada, tunasahau kuwa ni malaika tu wasio na hatia, na hata ikitokea wamekuwa wezi au majambazi ni sisi watu wazima ndio tumesababisha hivyo kw akutojali familia zetu na watoto wasio na wazazi tunawatumikisha bila kujali nao wanastahili kuwa shule n.k tunawanyanyasa kijinsia na kimaumbile. Tusimame pamoja kuwatetea watoto jamani
Post a Comment