Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, December 5, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-57Hitimisho -1
`Maua , nimepewa muda mfupi sana na shangazi, na muda huo natakiwa nikusimulie kisa changu ili uondokane na hisia potofu , ambazo kila mmoja anajua hivyo, kuwa mimi nilishakufa,….mimi sijafa, na kisa hiki kitakuonyesha jinsi gani nilivyookoka na ajali ile. Nakuomba baada ya kisa hiki uwe huru kuamua kwa utashi wako mwenyewe bila shinikizo la hisia ambazo hazipo,au shinikizo la mtu mwingine, utoe uamuazi wako mwenyewe, je upo name au kutokana na hili tukio ulishabadilika, …je kama ungelikuwa wewe ungelichukua hatua hiyo uliyoichukua…siwezi kukulaumu, lakini cha muhimu, najua una haki ya kujua ni nini kilitokea hadi kuwepoleo hii.

‘Maua, mungu ndiye anayejua mwisho wa kila mtu, hata mimi siwezi kuamini kuwa bado nipo hai, nilijua sasa hivi ni meshakuwa nyama za samaki,…lakini mungu hakupenda iwe hivyo, nilishahisi kwa muda wa miaka miwili lolote linaweza kutokea, lakini niliona nije nikuone na nijue nini kinaendelea, …sasa ondoa hisia hizo kuwa mimi labda ni mzuka, au shetani, mimi ndiye yule yule, mume wako ambaye leo unataka kunikana, ..Maua sitaki kukulazimisha, sitaki kukuweka katika njia panda, kwani wahenga wanasema usilolijua ni sawa na usiku wa kiza, huenda yapi makubwa ambayo huyajui, lakini ni bora ukayajua yangu kwanza,,kadrri muda utakavyoruhusu.

‘Maua, kwanza, nimeamini ukweli wa hisia zangu, hisia zangu ziliniashiria toka awali, kuwa safari ile haitakuwa nzuri, unaweza ukasema, ningelijua ningelifuata hizo hisia zangu, nikaahirisha hiyo safari, kwani siku tuliyotakiwa kuondoka, nilikuwa sijiskii vizuri kabisa, nilitamani kabisa nisiondoke, nitakajipanga kuwapigia wenzangu, kuwa sitafika siku hiyo, lakini ikatokea kitu kingine nikajisahau…hata nilipoamuka asubuhi ya safari, nikawa na jivuta vuta kama sio msafiri, na sio kawaida yangu, na hutaamini nilichelewa hata kufika bandarini pale ziwani, lakini kwa vile ilikuwa ni maswala ya kikazi nilikimbilia pale ziwani na kujikuta nimechelewa, hata hivyo nikaruhusiwa kuingia ndani ya meli..

Kwa ujumla walikuwepo watu wengi siku hiyo na wote walitaka kusafiri, na kila waliokuja kuliruhusiwa kuingia kama mimi, kwa mahesabu yangu walikuwa ni zaidi ya mia sita. Nikaingia ndani ya meli na kuitizama, huku nikiwaza, kweli meli hii ni ya muda mrefu, ilionekana kuchoka kweli, lakini akilini nikasema ya kale ni zahabu.Nikiwa ndani ya meli, kila upande nilipokwenda nilikuta watu wamejaa isivyo kawaida, nilitafuta sehemu yangu nikakaa, na huwa mara nyingi sipendi kukaa sehemu moja,…lakini kwa kujisikia vibaya, nilitamani nilale tu, lakini nikasema siwezi kuvunja taratibu zangu, kabla ya kujilaza kwenye kiti changu nilamua kuzunguka zunguka kwanza huku na kule, nilitembea huku na kule, ili mradi kupoteza muda…na baadaye safari ikaanza nikarudi kwenye sehemu yangu na kujilaza.

Pale nilipokuwa nimejilaza nikawa nakuwaza wewe mke wangu, nilitafakari mengi, jinsi mambo ya safari yanavyoweza kuwatenganisha mke na mume, niliwaza, kwanini safari kama hizo tusingekuwa pamoja, lakini baada ya hilo tukio nikasema hapana, aheri nimesafiri peke,yangu maana waliosafiri na familia zao walizisahau wakati kila mtu alipokuwa akihamanika na roho yake. Jamani isikieni ajali tu, huwezi amini kuwa mtu atamshau mwanae, mke wake au mume wake, na kukimbilia kivyake kama hawajuani….

Tulipofika kisiwa cha Kariemo nilihisi kuna kitu kimetokea…, lakini sikuwa na uhakika, hisia zangu ziliniambia kuna tatizo,kwani meli ilikuwa haipo katika msimamo wake wa kawaida. Kwa muda huo nilikuwa najisomea kitabu nilichokuwa nimekinunua, kitabu hicho kiliandikwa juu `Titanic Tragedy’ sijui kwanini nilikichukua hicho kitabu, maana kilichokuwa kinaelezewa hapo kilikuja kufanana na tukio letu,…ingawaje hakukuwa na ile hadithi ya kimapenzi kama ilivyokuwepo kwenye hiyo kitabu, lakini lile tukio la kuzama na mihangaiko yake, ilifanana kabisa na nilichokiona ndani ya kile kitabu.

Wakati naanza kukisoma hicho kitabu, nilikuwa nakisoma kama vitabu vingine vya hadithi tu,…lakini nikikumbuka, kilikuwa kikitabiri ajali yetu,…kwahiyo baadaye sikukichukulia kama historia tu, nakichukulia kama kitu muhumi sana katika tukio letu hilo. Ndani ya hicho kitabu, pamoja na kile kisa cha mapenzi ya wapendwa wawili, lakini hata hivyo niligundua mengi ambayo nilikuwa siyajui kabla, …
.
Wakatu ninaendelea kukisoma, hicho kitabu ,…akili yangu nayo ilikuwa ikitingwa na wasiwasi, nilikuwa nimeanza kuhisi hali isiyo ya kawaida, licha ya kuwa mzoefu wa kusafiri kwenye hii meli, lakini kitu kama kichefuchefu na kutokujisikia vibaya vilisumbua sana,…nikjaribu kutafuta usingizi, na njia pekee niliyoijua ni kusoma kile kitabu kwa bidii. Na kweli kile kitabu kikanipeleka mbali na kuanza kusisimukwa na hilo tukio lililokuwa likieelzewa, na kisa hicho cha wapenzi wawili.

Niligundua kuwa meli hiyo ya Titanic ilikuwa kubwa sana,na kweney safari hiyo watu wengi walijumuika kusafiri, , ilielezewa kuwa , baada ya hiyo meli kupatwa na hiyo ajali, abiria wengi sana walipoteza maisha, watu 1500 hivi walipoteza maisha , na ni watu 705 tu waliookolewa, ilikuwa ni tukio lililotokea mwaka 1912. Hapo nikashikwa na kausingizi kakimang’amung’amu nikalala.

Nje vigelegele vilikuwa vimepamba moto, lakini ndani ya chumba hiki, kulikuwa kumetulia, na ni sauti ndogo ya mtu mmoja iliyokuwa ikiongea tena kwa kuhakikisha kuwa hakuna anayewasikia hicho wanachoongea humo ndani. Hata Maua ambaye mwanzoni hakuwa na shauku ya kusikiliza hicho kisa akijua huyo sio mwanadamu, lakini kila hatua alitamani kusikia zaidi nini kilitokea, akatulia kimiya akiwa muda mwingi kaangalaia chini, lakini akili yake ilikuwa inanasa kila neno.

‘Lakini huyu ni binadamu kweli, mbona kila anachozungumza kinaingia akilini, hapana, Mhuja alishakufa, miaka miwili mtu asikumbuke hata kupiga simu, nikupoteza gani kumbukumbu kwa muda wote huo…aah, ngoja nimsikiliza kwanza, halafu, …..Mawazo ya Maua yalikuwa yakihamanika na ujio huo wa mtu huyu, bado kabisa akili yake ilikuwa akimfikiria kama mzuka, haikuwa bado inamtambua kama miongoni mwa watu waliobahatika kuokoka katika ajali hiyo, ni muda mrafu kwa mtu kuamini hivyo, …Sura, mwili maongezi na kila kitu ni yule yule mpendwa wake, …’akawawa anawaza huku akisikiliza hicho kisa.

‘Maua sijui kama uliwahi kukisikia kisa hicho cha kuza kwa meli ya Titanic, au kuangalia picha yake, ilivyokuwa, ndivyo ilivyokuja kutokea kwetu sisi, nilikisoma hicho kitabu kwasababu ni kisa kizuri cha kihistoroa, lakini ni tukio ambalo kwangu litakuwa kama kumbukumbu ya tukio letu, na nitajitahidi kukitafuta tena hicho kitabu, kama kumbukumbu yangu ya safari yangu hiyo.…’akasema Mhuja, huku akiangalia saa, akijua kuwa muda aliopewa unakwisha na huenda mambo yanakaribia kuiva, lakini hata kama yataiva na Maua atakubali kuachana na hiyo ndoa, basi ndoa itakua haipo, lakini kama atakataa kwasababu zake, ataitimiza ahadi yake aliyoiweka kwa shangazi, na hata kwa Maua kuwa kauli yake ataiheshimu, kwani huwezi kulazimisha pendo, licha ya kuwa anampenda sana mkewe,..ndio anampenda sana mkewe, lakini miaka miwili ni mingi mengi yametokea, huweze jua….

`Wakati nimeshatekwa na usingizi, mara nikazindukana sikujua kuwa ni ndoto ama ni ukweli, lakini baadaye nikajua kuwa sio ndoto, ilikuwa ni ukweli, sauti ile niliyoisikia kama ndoto ikisema `meli inazama, niliisikia tena wakati nimefumbua macho yangu, …kilichokuwa kikiendela kwa wakati ule ilikuwa nikila kona ya meli, vilio , vilio, kelele, na mihamaniko ya kila mtu akitafuta jinsi gani ya kuokoka. Nikiwa ndani ya usingizi, niliota ninaogelea nikiwa nimepiga mbizi, …na naogeela ndani ya maji nikipishana na samaki, huku wale samaki wakisema kwa sauti yajuu `tunazama …’ nikawa najiuliza hawa samaki wanasema hivyo wakati majini ndio kwao, wanazama nini tena.
Nikazindukana na kufungua macho haraka huku nikiangalia huku na kule, kuwaangalia wenzangu …hapo nikaamini kuwa ile ilikuwa sio ndoto, kweli kulikuwa na tatizo, kila mmoja alikuwa akihangaika kivyake na sauti zilikuwa zilia huku na kule,. Sauti za vilio vilitanda hewani na sauti nyingi zilikuwa za ikina mama….

Na mara kweli tukasikia mtetemeko wa meli ukitikisika, na ukiangalia kwa nje, ilionyesha dhahiri kuwa meli ilikuwa imekaa upande, …tukahisi kabisa tukiwa tunapalekwa juu, na abiria wakawa wanajaribu kukimbilia upande wa pili ili kujaribu kuiweka sawa hiyo meli, lakini haikusaidia kitu, tukaanza kuzama kuserereka, kwani meli ilikuwa ikizama upende upande,kwahiyo watu walikuwa wakikusanywa sehemu moja..

‘Meli ikawa inazama…kilichofuatia hapo, ni kila mtu na roho yake…..kwani maji yalishaanza kuonekana ndani ya meli, . Mimi sikupoteza muda tena, …kwa ujumla nilipona hivyo nikajau hapa kinachotakiwa sio kusubiri, nilichofanya ni kuvamia sanduku moja kubwa nikalibeba na kutoka sehemu ili niliyokuwepo hadi upande ambao ulikuwa sehemu ya juu, sikupoteza muda zaidi kuangali nini na kwanini imekuwa hivyo, …mimi na sanduku langu, nikajitupa ndani ya maji,na kuanza kutumia ujuzi wangu wa kuogelea. Nipojitupa kwenye maji kwanza nilizama kwenda chini …na wakati natua kwenye maji kichwa change kiligonga chuma cha meli,…mwanzoni sikuyasiki hayo maumivu, lakini kila dakika iliyokuwa ikienda mbele, ilikuwa kama mtu anapigilia kiti kwenye kichwa changu.
Niliibuka kwenye maji toka na kuweka kichwa juu kuangalia, nyuma yangu, ilikuwa kama ziwa limechafuka kwani watu walikuwa wakijitupa ndani ya maji, makelele ya yakuomba msaada, …na kila kelele niliyosikia ilikuwa inaniongezea maumivu ya kichwa nikaona niogelee mbali zaidi , na huku nalitumia lile sanduku kama msaada, kwani kichwa kilikuwa hakinipi nafasi ya kupiga mikono kama makasia, …kwakweli kama isingelikwua yale maji, kuwa nipo ndani ya maji ningelipoteza fahamu,kichwa kilikuwa kinauma kuliko kawaida,hata nguvu za kuogelea zilianza kuniishia ….

Hutaamini kuwa meli kubwa kama hiyo, kulikuwa hakuna vyombo vya kujiokolea, hasa yale majaketi ya kuweza kuvaa na kuelea, na nilikumbuka wakati tupo humo ndani wengi walikuwa akijadili kuwa meli hiyo imekuwa kuku sana , haikuwa inastahili kuasafirisha abiria wengi, na vifaa vya uokozi vilikuwa vichache saba. Na siku hiyo kila mmoja alikiri kuwa abiria walikuwa wengi kupindukia.

Kwakweli wakati nhangaika ndani ya maji niliwaonea huruma sana wale akina mama na watoto, lakini nani angeliwajali wakati kama huo , kila mtu alikuwa kihangaika kivyake, mama au baba hamjui mtoto, kila mmoja analia mama…sasa sijui mama wa kila mtu ni nani….

‘Maua muda unakwisha, mumemalizana, niingie…’ilikuwa sauti ya shangazi.
‘Bado kidogo shangazi, …’akasema Maua huku akimwangalia Mhuja, …alishaanza kuhisi kuwa huyo kweli ndiye inawezekana akawa ndio yeye …kwanini shangazi aseme mumeshamalizana, na je afanyeje, kwani hali aliyo nayo inamweka katika njia panda,…akaangalia tumbo lake , na kupitisha mkono, na akainua kichwa kumwangalia Mhuja na moyoni akasema `samhani Mhuja…samahani….sijui nifanyeje, kwanini mimi….akajipweteka kwenye sofa na kuchukua mwanasesere ambaye alikuwa kampa jina la Mhuja, akimaanisha kuwa huyo mtoto akimza atampja jina hilo kama ni mwanaume.

'Maua muda unakwisha ....'shangazi akasema kwa nguvu.

NB. Je katika hali kama hiyo kama ingelikuwa wewe ungelichukua uamuazi gani?


Ni mimi: emu-three

3 comments :

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

lile sekeseke la hotelini limekwishaje?

Subira said...

Ingekuwa mimi ningevunja hiyo ndoa inayotaka kufungwa kwani kisheria mume yupo kwa hiyo hakuna ndoa nyingine hapo mpaka ya mwanzo ivunjike. Nae Mhuja hana haja ya kudai kasalitiwa kwani kama angekuwa amekufa kweli je angelitegemea mke wake akae hivyo hivyo? Alee tu huyo mtoto atakaezaliwa, mbona wanaume wengi wanalea watoto sio wao bila kujua (wink)?

emu-three said...

Mkuu lile sekeseke la kule hotelini linakuja, kwani mhusika mkuu aliyekuwepo kupambana na lile kundi yupo nchini, na atakupa kila kitu kilichotokea, sijui zaidi tususbiri hatua hiyo.

Subira ni kweli, ndoa ile ilikuwa `haijavunjwa' na wanandoa wenyewe, lakini kwasababu ambazo zilikuja kutokea tulikuta imekuwa hivyo, na Mhuja akakubali iwe hivyo, sasa ao kuna changamoto, ndio maana nilihitaji maoni ya watu, kuwa ikitokea hivyo, kidini , kimila inakuwaje?