Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, September 23, 2009

Serikali za Mitaa-Sio vyote ving'aavyo...

Lamgambo limelia, mwenye masikio asikie na mwenye kutafakari ang'amue. Tumesikia kwenye vyombo vya habari na hata mitaani kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa upo njiani. Wengi wetu tunauchukulia kirahisirahisi, kama tulivyozoea kuwa uchaguzi hapa kwetu ni kama kuwapa watu kula, kumbe ni makosa makubwa tunayofanya na madhara yake huturudia sisi wenyewe.

Serikali za mitaa ni sehemu zilizopo karibu yetu wananchi, na kwahiyo viongozi wake wanatakuwa wale tunaowafahamu na wanaojua shida zetu, wawe mstari wa mbele kuwatetea na kuwakilisha matatizo yetu serikalini. Kuna shida nyingi mitaani, miundo mbinu, mahospitali, mashule, masoko, viwanja vya wazi kwa michezo nk, hivi vyote ni muhimu kwa kushirikiana na huyo tutakayemchagua.

Katika pitapita yangu nikakutana na jamaa wanabishana kuhusu maswala ya uchaguzi,mmoja akadai kuwa yeye ingawaje kajiandikisha lakini hatahangaika kwenda kupiga kura, kisa ni kwamba achague asichague bado wanaopita kwenye uchaguzi ni walewale ambao yeye mwenyewe hawataki. Mwenzake akamuuliza, sasa unafikiri kwa nini ni hawo hawo wanapita kwenye uchaguzi,akasema wanapita kwa njama, rushwa na mengineyo ambayo hata kuyaandika hapa naona aibu. Hizi ni hisia za wengi wetu!

Mawazo haya yamewagubika wengi wetu, na hili linachangiwa na kutokufahamu nini hasa maana ya uchaguzi na zaidi ni nini hasa maana ya demokrasia kwa ujumla. Tunasahau kuwa chaguzi zilikuwepoenzi na enzi za mambau zetu na zilifuta utarabu maalumu kimila. Lakini sasa hivi tunaona kama ni kitu kigeni, cha kuiga au kisicho na maana.

Wapo pia wananchi wengi wanaopiga kura kutimiza wajibu tu, wanaogopa,au wamesukumwa na zawadi walizopewa, lakini kwanini wanampigia nani bado ni kufata mkumbo. Tunashindwa kuelewa kuwa kura zetu ni muhimu sana katika maendeleo ya mitaa yetu. Na kuipoteza kura yako ni kuchangia kurudisha maendeleo ya eneo lako,kwani wataendelea kuchaguliwa viongozi wasiofaa, na wewe utaendelea kuumia.

Naikumbuka sana hadithi ya babu, ambayo alinisimulia kuhusu jamaa mmoja ambaye alibahatika kusoma na kuishi mjini. Baada ya kumaliza masomo yake ikabidi arejee kijijini kwao ili awajibike na huko akapata kazi kama alivyoahidiwa. Ikafika muda wa kuoa, wazazi wake na wazee mbalimbali wakamshauri aoe wasichana wa hapo kijijini ambao waliwaona wanamfaa kitabia, kiuwajibikaji na mambo mengineyo. Yeye akakataa akisema wengi wa wasichana wa hapo kijijini ni washamba,hawataendana na elimu yake. Anataka msichana aliyesoma, anayejua Kiingereza na hasa kutoka mjini.

Basi bahati nzuri wakaja wageni toka mjini, wageni hao walikuja na binti yao, na huyo binti akapata bahati ya kuajiriwa kwenye miradi iliyowekwa hapo na serikali. Binti huyu alikuwa mrembo na kama unavyojua wasichana wa mjini, wanavyojua kujikwatua, tofauti na wakijijini ambao muda mwingi wapo katika mihangaiko ya kimaisha. Jamaa alipomuaona akasema huyu ndiye anayenifaa kwanza kasoma pili mrembo, tatu ni mtoto wa mjini.

Akaanza kukutana naye na urafiki ukanoga, na hatimaye jamaa akawasilisha ombi lake kwa wazee. Wazee wakamuuliza je unamfahamu vizuri huyu binti, huko alikotoka unapajua vizuri , familia zao na taratibu zao? Jamaa akajibu hayo yamepitwa na wakati. Wazee wakamwambia sisi hatuna kipingamizi ilimradi umeridhika naye sawa, lakini usidhani vyote ving'aavyo ni dhahabu.

Jamaa kaona, siku ya arusi vioja vikaanza, mila za kijiji hazikufuatwa, binti akawa anafanya mambo ya kimji, kumbusu bwana harusi mbele ya kadamnasi, na mbele ya wakwe. Binti hakuachia hapo, alisema yeye hataki ndugu wa mume kuishi kwenye nyumba yao.

Vituko viliongezeka kila siku, binti akawa hawaheshimu wakwe zake na wakija kutembelewa bila miadi hawakaribishwi, binti uvaaji wake ukawa hauendani na maadili ya hapo kijijini, hatimaye wazee wakawatenga na jamii ikawa haina radhi nao. Jamaa ikabidi ahamie mjini, lakini huko aliishia kubaya zaidi maisha yakawa magumu kwani binti anataka kuishi matawi ya juu lakini mume hana uwezo huo. Hatimaye ndoa ilivunjika kwa mizengwe na fadhaa kubwa.

Huu ni mfano tu,lakini unatufundisha mengi kuwa tuwe waangalifu katika kumchagua kiongozi wetu, tusigubikwe na mawazo mengine ambayo hayataleta maendeleo, tuangalie nini tunakitaka ili tujue nani anafaa kutuongoza, je tunamjua ipasavyo, je anauwezo wa uongozi, je anajua vyema matatizo yetu. Tusipoangalia tutaishia kuwachagua viongozi eti kwasababu tu `wanajulikana lakini hawana sifa ya uongozi' ni `ni wasomi wa wamjini lakini ni mafisadi' nk.

Tusipoangalia tutaishia kulalamika kumbe chanzo ni sisi wenyewe, na ndipo pale ardhi ambayo ni urithi wa vizazi vyetu ikiishia kuuzwa kwa kisingizio cha uwekezaji, ajira na biashara zitaishia kwa wageni sisi tukibakia kuwa vibarua na watumwa wa wawekezaji na baya zaidi hatutakuwa na muda wa kumuona kiongozi wetu wa mitaa kwasababu yeye amezoea kuonwa kwa miadi. Mwenye macho atizime na mwenye kuelewa atang'amua, kwani lakuvunda sasa, halina ubani.
From miram3

No comments :