Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, August 14, 2009

Adha ya Usafiri na diari yangu

Diary yangu inanikumbusha siku ile ya kashehe 30-09-2008, ambako simu yangu ilizimka kwahiyo sikuweza kuamushwa na `alarm’ Niligutuka kutoka kwenye ndoto ya kutisha ya kuumwa na nyoka. Cha ajabu hata kama upo usingizini ukimuota huyu mdudu, utazinduka tu. Kwa imani za watu wengine, ukiota ndoto kama hii, inaashiria kukumbana na wanga. Nashukuru, sikudhurika na nyoka huyo, kwani alitokea jamaa kwenye ndoto akanitibu jeraha, na kuniambia niko safi.
Nilizinduka na kuangalia nje `kweupeee’. Ilikuwa saa kumi na mbili na dakika chache, na saa kama hizo nilitakiwa niwe maeneo ya TAZARA. Ilikuwa bado na kigizagiza, ingawaje mionzi ya kupambazuka ilishapenya madirishani.
Nilivaa haraka na kukimbilia kituoni, cha ajabu nilikuta umati wa watu kituoni, kuonyesha kuwa hata wale waliowahi walikuwa hawajaondoka. Nini kilichoajiri siku ya leo ilikuwa swali la kila mtu, je madereva wamegoma, au kuna nini cha ajabu.
Kituo hiki cha Moshi Bar, kimejaza magari mabovu, magari ya vituo vyote utayakuta hapa, si Mwenge, Kimara, Kigogo,Temeke,na kila kituo unachokijua wewe utayakuta magari yenye nembo za maeneo hayo, lakini mwisho wake ni Mombasa.
`Kimvua hiki kidogo tu kimefanya magari yote yashindwe kufanya kazi, hawa wenye madaladala sijui wanaishi kibiashara kweli’ mmoja wa abiria alilalamika.
Ni kweli kwa vile usiku kulinyesha magari mengi yanaogopa maji na kunasa kwa tope, kwani barabara hii ya Moshi Bar hadi Mombasa inasifika kwa tope, makorono na vumbi kipindi cha jua kali.
Gari moja lilikuja kwa kasi utafikiri lipo kwenye mashindano likijifanya linapitiliza, na lilipofika umbali fulani likageuza ghafla na hamadi liligeuzia pale niliposimama na kunifanya niwe wa kwanza kuingia ndani ya gari. Nilishukuru Mungu kimoyomoyo.
Nikiwa nawashangaa watu wanavyogombea kuingia macho yangu yalikagua viatu nilivyovaa. Ilikuwa Bahati ya ajabu, sijui ingekuwaje kama nisingegundua makosa haya mapema.
Sikuamini macho yangu, sijui ni kwa sababu ya ile harakaharaka ya kuwahi au ni kwasababu ya tatizo la umeme, kwani asubuhi hii umeme ulikuwa umegoma. Hapa bongo kila kitu kina mgomo wake, bila hivyo hakueleweki kitu. Nilikagua tena viatu vyangu na nilipohakikisha kweli nimevaa viatu viwili tofauti, nilijicheka na kujiandaa kushuka ndani ya gari.
‘Vipi mzee unaenda wapi’ konda aliuliza akiwa tayari ameamurisha gari liondoke.
‘Nimesahau nauli..’ nilijibu haraharaka huku naruka nje ya gari. Kidogo nidondokee magoti, kwani gari gari lilishaanza mwendo.
Nilirejea kituoni baada ya kubadilisha viatu na umati ulikuwa umeanza kupungua nafikiri wengi wa abiria waliamua kutembea kwa mguu. Nami wazo hilo lilinijia na kuanza kutembea mwendo mdogo mdogo.
Nilipofika relini, gari moja lilokuwa linatengenezwa lilianza kusukumwa, nami nikajiunga kulisukuma na ikawa ndio ahueni yangu. Tulipofika Mazizini gari likasimama, na kuzima. Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu. Saa kama hizo mara nyingi ninakuwa maeneo ya Msasani au Magomeni.
Hali ilivyokuwa ilibidi abiria wote tutoke tusukume gari, na ndivyo ilivyokuwa, lakini gari halikuwaka, ikabidi tuanze mwendo wa mguu. Kwasababu tulikuwa wengi, mwendo ulikuwa wa haraharaka na tukawasili Mombasa kiasi cha saa moja na dakika kadhaa.
Sheria za kazini ni kuwa saa mbili kazi zimeanza, na ukichelewa utakuta daftari la mahudhurio limepelekwa kwa meneja utawala, na huenda ukaishia kupewa onyo kali. Lakini baya zaidi kampuni ilikuwa katika mchakato wa kupnguzwa wafanyakazi kwahiyo mchelewaji ananafasi kubwa ya kupewa barua hiyo.
Kijasho chembamba, kilinitoka licha ya kile cha kutembea mwendo mrefu, umati nilioukuta hapo Mombasa utafikiri watu wote waishio maeneo ya huku waliamua kusafiri siku hiyo. Niliamua kusubiri magari yatokayo mjini, ili niende nayo hadi Gongolamboto halafu nirudi nayo, manake nilipe nauli mara mbili. Na hii iliniashiria kuwa inabidi niamua kutokula mchana ili nipate nauli ya kurudia nyumbani jioni.
Wakati tunageuza kichwa huko na kule utafikiri tunaamurishwa na mjamaa fulani aliyejificha, macho yetu yalishuhudia mama akikoswakoswa na magurudumu ya basi moja la Msasani-Gongolamboto. Magari haya yanamtindo wa kuchukua abiria juu kwa juu. Yaani huku linatembea huku wanapakiza abiria. Yule mama alipoinuka pale, bado hakukubali alilikimbilia lila gari na bahari nzuri akafanikiwa kudandia. Ni hatari lakini atafanyaje?
Nilibahatisha basi lakini lilijaza kupita kiasi. Nilipokanyaga nilikuwa nimesimamia vidole, na kila nilipojaribu kushusha unyayo chini, nilisikia abiria akilalamika, `unanikanyaga, unaniumiza’ Kwahiyo ilibidi nisimame kwa mtindo huo hadi pale abiria walipoanza kupungua.
Nilifika ofisini saa tatu kasoro hivi, na hapo iliashiria kuchelewa kupita kiasi, na maana yake niende kwa meneja utawala kujieleza. Sipendi kabisa hii hali lakini ningefanyaje? Nilijiuliza bila majibu.
Niliwakuta wenzangu wanaoishi maeneo ya majirani wameshafika, na kila mmoja aliniangalia kwa jicho la huruma. Nilianza kunywea kwanini wananiangalia kwa jicho la huruma, kuna nini cha ajabu kimetokea.
Tutaendela baadaye.
NB. Jamani kutokana na tukio hili nikaamua kutunga kitabu cha `YOTE MAISHA’ Mungu akijalia nitakiweka hewani.
Na siku za nyuma niliandika maelezo mazuri kuhusiana na tatizo la Usafikiri njia ya kuelekea Gongolamboto na kuiepeleka kwa michuzi ikiwa na kichwa cha habari kero ya usafiri Gongolamboto.

From miram3.com

No comments :