Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, August 31, 2018

YOTE KWA MAPENZI YA MUNGU-40


‘Wewe mtu wa jamii mbona umetutoroka, kwanini unafanya hivyo..haya niambie…unafanya nini huku…’ilikuwa sauti ya mpelelezi, iliyotokea nyuma yangu…

Nilishtuka kidogo, maana sikutegemea hawa jamaa watanifuatilia kwa muda huo na mimi nilishakuwa na mipangilio yangu tayari, nikageuka na kuangaliana na mkuu huyu…

Tuendelee na kisa chetu….

*************

‘Hapana afande nilikuwa napoteza poteza muda huku, maana nijuavyo mimi , nyie watu msingelipenda  niwaingilie kwenye kazi zenu au sio…’nikasema

‘Najua ujanja wako…hapo kuna jambo umeligundua,…’akasema

‘Hahaha afande mbona huniamini….’nikasema

‘Ok, sawa, ilimradi usivunje sheria…unajua hivi sasa kutokana na muda, ..mimi nimeona, tushirikiane, sio kwamba tumeshindwa,kwahiyo ukigundua jambo,  usitufiche maana muda unakwenda, na hadi hivi sasa sijaona jambo linalohusiana na kesi yako, haya yanayotokea hivi sasa sioni uhusiano wake na hiyo kesi yako, kama ipo, tuambie…’akasema

‘Kama ni hivyo…afande, mimi naona  ni bora mniachie nifanye kazi yangu, ili nije kuwaonyesha uhusiano wa kesi yetu, na haya matukio..’nikasema

‘Kiukweli , huwezi kupewa ruhusa hiyo , maana hiyo kesi ipo mikononi mwetu, na sio kwamba hatuifanyii kazi, tunaifanyia,..na ..’kabla hajamaliza nikasema

‘Afande …kumbuka huyo mnayehangaikia sasa hivi ni Dalali, na Dalali ndiye kiini cha haya yote, nionavyo mimi,…sasa kwanini haya yanatokea, kwanini anatoroka, kwanini, anaumwa,…ukiuanganisha utagundua kuwa sabubu ni hilo deni…’nikasema

‘Inaweza ikawa hivyo, sitakai,..lakini ni ushahidi gani utakaoliwezesha hilo, unajua sio kwamba napinga, lakini kuna swala la muda hapa, wakili anahitajia ushahidi ili aweze kuweka pingamizi, ili mnada usifanyike, ili kesi iingie mahakamani, sasa kama kuna jambo umeligundua ni bora utuambie mapema, ili wakili awahi kufany kazi yake, sijui unanielewa…’akasema.

‘Kwahiyo kwa kauli hiyo umeshakubali kuwa na mimi naweza kuingilia kazi zenu…?’ nikauliza

‘Sio kuingilia bwana..wewe vipi…, ila kama una jambo la kusaidia tuambie, ukiingilia unakiuka sheria, na mimi sio mtungaji wa hizo sheria,..wewe ni raia tu, wenye kazi ya kupeleleza hilo jambo ni sisi, nyie mnatakiwa kutusaidia tu , unanielewa…’akasema

‘Mimi nionavyo hapo, kwa kifupi, hii kesi imeshawashinda…kwahiyo mnahitajia msaada kutoka kwetu sisi raia, ni sawa, hilo ni jukumu letu, lakini kwanini mnaniwekea vizingiti, ili niwasaidie, kama raia, nipeni nafasi,..kibali ili niweze kufuatilia baadhi ya mambo..…tusipoteze muda, kubali hilo…’nikasema

‘Wewe umetukimbia huko juu, ukaacha kuona vioja..dunia hii kuna mambo…’akasema kupotezea nilichomuulizia…najua ni kwanini mwenzake ndiye kikwazo.

‘Ehee, niambia kumetokea nini huko juu,…ila sio naingilia kazi zenu..?’ nikauliza

‘Ok…unajua…huyo mgonjwa kabadilika kabisa…alianza kujipiga piga, huku akipiga ukelele,..’moto, moto…’ lakini pale alipolala  hakuna moto…ikawa ni kazi kumshika, watu waliojaribu kumshika walirushwa kama mpira..mimi nikaona hayo ni mambo ya kienyeji, ngoja niwaachie wenyewe…’akasema

‘Ndio ukaondoka kuja huku…?’ nikauliza

‘Nilibakia kidogo, nikasikia akiongea…maana tokea awali, wanasema mtu huyo haongei, lakini hapo alianza kuongea , tena sauti sio ya kwake…na jinsi alivyoweza kusimama, akawa anawarusha watu, kwa nguvu za ajabu, ni kitu ambacho kilimshangaza docta…anasema hawajahi kuona, alikuwa akiongea sauti nyingine kabisa…’akasema.

‘Aliongea nini..?’ nikauliza.

‘Maajabu…, eti ni kaka yake kamtokea,…mimi ni kaka yake Dalali…hapo akataja jina lake, akianza na marehemu…akawa anasema;

‘Mimi nimekuja kufuatilia deni langu, nilishawaambia nimeondoka nikiwa nimeacha deni kubwa sana,…fanyeni mfanyavyo, hilo deni lilipwe,…kama mumeshindwa, waachieni benki wafanya wajuavyo wao, na familia yangu itajaliwa majaliwa mengine....’hiyo sauti ikasema hivyo.

‘Nyie hamukuiliza, kwanini nyumba iuzwe, je yeye, kama yeye, anakubaliana na hilo…’nikasema

‘Ninani angeliuliza hilo, sisi hatujui…tulibakia tumeduwaa, yeye akaendelea kusisitiza hilo, kuwa anahitajia deni hilo lilipwe haraka la sivyo…’akatulia hapo

‘Watu wangu wa karibu watadhurika…’akatulia kidogo na mimi nikaona nimuulize …

‘Kudhurika kwa vipi kwa jinsi , ulivyoelewa wewe…?’ nikamuuliza

‘Nahisi watu wake wa karibu labda ndio hao watoto, na akina Dalali…’akasema

‘Ehe…’nikasema

‘Aliendelea kuongea…;

‘Nyie mliniomba nitulie kwanza, ili watu wafuatilie jinsi gani ya kulilipa hilo deni, aliyeniomba, keshaondoka, sababu kubwa ni uwongo wake…sasa na nyie, mtafuatia mmoja baada ya mwingine…maana naona badala ya kufuatilia deni, nyie mnafuatilia mambo mengine…’sauti ikasema hivyo.

‘Kasema , mtaalamu, keshajiunga huko alipo, sasa bado wengine, wanahitajika…, kwahiyo anatuma huo ujumbe kwa wanaohusika, na ujumbe huo tayari ameshauwakilisha kwa mkewe…’akatulia

‘Kwa mkewe, kwa njia gani…?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui…labda uwasiliane naye kulihakiki hilo..’akasema na mimi nikaona nisipoteze muda, nikampigia huyo mama mjane.

‘Vipi huko kumetokea nini…?’ nikamuuliza.

‘Oh…jana..sikulala….niliota mambo ya ajabu ajabu,…tofauti na ndoto zile za kawaida…nilihisi majinamizi..na sauti ya kutisha, ikisema, natakiwa kuhakikisha deni la mume wangu limelipwa…’akasema.

‘Ulisikia sauti kwenye ndoto ukiwa umelala au sio…?’ nikauliza.

‘Ndio…hiyo ni ndoto ya kutisha…ilibidi usiku huo nisiweze kulala kabisa, baada ya kuota ndoto hiyo, ...maana kila nikijaribu kulala, hiyo hali inajirudia…’akasema.

‘Je watoto vipi…?’ nikauliza.

‘Kuna muda walipiga kelele…nikawasomea, na kumuomba mungu, wakatulia na kulala..ila hapa nilipo moyo wangu hauna amani, najiulize..je ni kweli deni hilo lipo, huenda labda…’akataka kusema

‘Dada achana na mawazo hayo…hayo ni mashetani,…hilo deni sio la mume wako, na hatua iliyofikia, …wewe ngoja tu, nahisi sasa hivi tunaendea mwishoni…’nikasema

‘Haya, hata mimi siwezi kuamini…ila najiuliza mbona awali sikuota hivyo..niliota mume wangu ananisaidia..sasa hivi , yeye tena anakuja kunikaba…’akasema

‘Mashetani hayo..yasikutishe,…hali halisi itakuja kujielezea, unasikia,..je hujapata chochote kingine,…?’ nikauliza

‘Una maana ushahidi,..kam hivyo…?’ akauliza

‘Ndio…’nikasema

‘Sijapata..nimefagia, nimekagua kila mahali, hakuna kitu …’akasema

‘Basi usijali…’nikasema na kukata simu.
‘Haya umesikia mwenyewe…’akasema mpelelezi…maana niliweka sauti kubwa , ili nay eye asikie nikiongea na huyo mama mjane.

‘Kwahiyo na wewe unaamini kuwa kweli hilo deni ni la marahemu…?’ nikamuuliza

‘Mimi siamini kitu bila ushahidi..ilivyo, ..ushahidi wa kuwa kweli hilo deni ni la marehemu upo..sasa kama sio lake, ushahidi upo wapi..unielewe hapo…’akasema.

‘Nini zaidi aliongea…hiyo sauti iliongea?’ nikauliza.

‘Kuna kauli …sauti ilisema, wote wanaojua siri ya hilo deni, kama wasipowajibika, kulilipa, nitawlipizia, kama nilivyofanya kwa mtaalamu..sasa..neno siri…’akasema mpelelezi.

‘Siri…ina maana hilo deni lina siri au sio, na siri hiyo anayeijua ni nani….?’ Nikauliza.

‘Ni hao watu wake wa karibu…’akasema

‘Ambao ni Dalali, mtaalamu na…’nikatulia hapo,..simu yangu iliingia ujumbe wa maneno

‘Ndivyo alivyosema…’yeye akasema huku mimi nikisoma huo ujumbe wa maneno, ni watu wangu, ..

‘Je kwenye hiyo sauti, hakuweza kuwataja hao watu wake wa karibu.?’ nikamuuliza

‘Hakutaja jina, zaidi ya kusema hayo niliyokuambia na zaidi akasema maneno haya ambayo ndiyo yalinifanya mimi nikutafute…’akasema

‘Maneno gani..?’ nikauliza

‘Na huyo moto,..sasa hivi, moto wake utazima..nilimuamini sana, kumbe hana maana, siku zake zinahesabika…’akasema.

‘Moto..?!!!’ nikauliza kwa mshangao.

‘Ndio…’moto’….una elewa ni kwanini nimekutafuta kwa kauli hiyo, si unakumbuka …?’ akaniuliza akiniangalia kwa mashaka.

‘Yaah…najiuliza tu, hilo neno nimelisikia mara nyingine tena…, na kwanini linajirudia…moto…moto…ni jina au ni …tendo..?’ nikauliza.

‘Yeye huyo, kasema hivyo, ‘na huyo moto, moto wake utazima…’..yaah, hata mimi nimeliwazia hilo, nilipokumbuka kauli yako, ndio maana nikaona nikutafute, wewe..je wewe ulimaanisha nini, au uligundua nini, kuhusiana na hilo…, ‘kwanini neno moto…limejirudia’…nikuulize wewe, je lina maana yoyote kwako…?’ akaniuliza

‘Nakumbuka sana, na nahisi lina maana kubwa sana, na kwa vile limetajwa hapo tena, nahis kuna kitu ndani yake, lakini je huyo mtoaji hilo neno au kauli, anaaminika, ana siri gani yenye manufaa kwetu, isije pia ikawa ni mtego…’nikasema.

‘Unakumbuka wakati tunafuatilia zile nyaraka zilizoungua, wewe ulisem kuwa neno moto, linaweza kuwa ni ujumbe…na..unajua nyie waandishi mna mambo, napenda sana fikira zako, ila nyingi ni maneno tu, sisi tunataka ushahidi wenye kushikika, je kwa kauli hiyo una lolote la kusema…’akatulia kama anawaza jambo.

‘Lakini natumai hadi hapo umeshaanza kuelewa ni kwanini nilisema hivyo na bado naona kuna haja ya kutafuta ni nini kipo nyuma ya hilo neno ‘moto’…umeona hapo, kuna ujumbe hapo, kama sio mtego au sio….?’ Nikamuuliza huku nikiwaza jambo.

‘Yah nilikuelewa…lakini mimi siwezi kukubali jambo mpaka nipate ushahidi.., na ndio maana kwangu mimi nashindwa kusema lolote, ila bado nalifanyia kazi,...kuna jambo jingine nalo nalifuatulia, kama nitagundua kitu, basi nitakuwa na wewe kwenye fikira zako, japokuwa ushahid wake bado ni finyu kusema lolote…’akasema.

‘Jambo gani…?’ nikamuuliza

‘Kuhusiana na wamiliki wa ile kampuni na hii hospitali…’akatulia akiniangalia moja kwa moja usoni.

‘Kwahiyo umegundua nini hadi hapo…?’ nikamuuliza

‘Nimeanza kupata picha fulani…nimejiuliza hapo,…ni.kwanini hao wamiliki wameficha majina yao halisi. Hata kwenye hati zao za biashara, ilikubalikaje hivyo, …ni kitu cha ajabu sana,…’akaangalia kama anawaza jambo.

‘Hii  ina maana gani, ya kuwa hata kwenye vitambulisho vyao watakuwa wameandika hivyo kwa kufupi,…hapana,  haiwezekani, nahisi kuna jambo hapo halipo sawa....ila  ngoja nilifanyie kazi..’akasema

‘Je hilo litasaidia kesi ya deni linalosemwa ni la marahemu...?’ nikauliza nikijikwangua kichwa kama kinawasha sana.

‘Mimi siangalii hivyo, mimi naangalia kwenye ukiukwaji wa sheria…sasa je ukiukwaji huo wa sheria ni kutokana na hilo deni, hilo ni swali jingine….na..kiukweli hadi hapa sijaona uhusiano wake na hilo deni…, zaidi ni kuvunjwa kwa sheria, udanganyifu..kujaribu kuua,..na ndio maana nataka mzee mtupe akamatwe, unanielewa hapo, lakini sio mimi niwe mvunjifu wa amri za mahakama,….’akasema

‘Moto..utaleta jibu…., niamini afande, moto, moto…kama ni jina au ni tendo, vyovyote iwavyo, kwa mapenzi ya mungu, tutapata jambo la kuieleleza mahakama wapi sheria ilitakiwa iende..na mahakama imetimiza wajibu wake ..je sisi watendaji,..tulitimiza wajibu wetu ili mahakama iamua itakiwavyo….sijui…..’nikasema

‘Moto utaleta jibu kwa vipi,…hizo nadharia zako hazitaweza kusaidia,..sana sana ni kupoteza muda,wewe hujui hali ilivyo kwa sasa, mimi naulizwa na wakubwa zangu, huku mahakama inatulaumu kwa kuzuia jambo, bila ya kuwa na ushahidi..haya yananiweka mimi mahali pa njia panda, na mwishowe unafikiria itatokea nini, siwezi kukubali kuharibu ajira yangu na kiapo changu, ’ akasema.

‘Labda nikueleze jambo moja, wakati najaribu namba za hao wamiliki wa hospitali na hizo kampuni..maana sio kampuni moja, hao jamaa wana zaidi ya kampuni moja…’nikasema

‘Ndio, hilo tumeliona…’akasema.

‘Sasa kila sehemu wana namba tofauti na kwingine, najua lengo lao ni kutaka kuonyesha kuwa hizo ni kampuni za watu tofauti…sasa…eeh, kuna namba mbili tofauti, kwa mtu huyo mmoja…kwenye kuhakiki,.nimegundua herufu  ya awali, ya ‘M’ inasimama kwa jina ‘Maozo..’ nikasema

‘Maozo, ni jina hilo…?’ akuliza hivyo, sikumjibu nikaendelea kuelezea.

‘Na kwenye ‘M’ ya mwisho, …kwenye hili jina… ‘M.AL.M.’…inasimama kwa jina ‘MOTO’…ina maana ‘moto ni nini..’nikasema

‘Namba ipi…?’ akauliza na mimi nikamuonyesha, akaijaribu kutuma pesa, na alipoona hilo jina, akasema

‘Oh….ina maana basi ‘moto ‘ ni jina la mtu, sasa huyu mtu  ni nani na yupo wapi….?’ akaniuliza.

‘Hiyo ni kazi yenu kumtafuta huyo mtu, sijui ni huyo wa huko nje,..au… au sio..au naweza kusaidia kama mnanihitajia, lakini kivywangu…je mtaniruhusu..?’ nikasema na kuuliza.

 ‘Yah…nalijua hilo, kuwa hiyo ni eeh… ni kazi yetu..na hili nitalimaliza hii leo, ili kieleweke, kwa wakubwa zangu..na hadi jioni nitakuwa nimepata jibu kuwa,, huo mnada uendelee au la….’akasema.

‘Natumai, hilo jina ‘Moto’ linaweza kuwa ufunguo, ..wa kuingia kwenye ukweli halisi, na kuupata ushahidi wa kulimaliza hili tatizo…’nikasema…nikiwa nimeshika kichwa nikiwaza mambo mengi.

‘Lakini awali ulisema Dalali, ndiye ufunguo wa kupata ukweli…’akasema

‘Ina maana ukweli haujajulikana kwa kupitia Dalali, afande, kuna mengi tumegundua kupitia kwake, au sio…?’ nikamuuliza

‘Ukweli upi sasa, utakaosaidia hii kesi, unanielewa lakini…?’ akauliza

‘Ukweli wa kuwa hilo deni sio sahihi kwa marehemu, cha muhimu kuanzia sasa ni kuutafuta ushahidi mnaoutaka nyie, au sio…kwangu mimi nimeshaliona hilo kinadharia, sasa kiushahidi wa kikwenu…ndio nataka mnipe kibali. Ili niweze kuutafuta,… ushahidi mnaoutaka nyie…’nikasema.

‘Tuzizungushane hapa…mimi nakuambia ukweli, kama ushahidi usipopatikana, aah, tusije kulaumiana,…’akasema

‘Leo,..tuombe mungu tu…’nikasema

‘Mimi nasema hivi, kama leo hakuna ushahidi, basi..amrii ya mahakama lazima itimizwe,...sasa hivi tunakimbizana na muda, ulielewe hilo…’akasema

‘Sasa utaniruhusu, niutafute huo ushahidi…maana kuna sehemu nataka kwenda , na  ni bora uniache niende mimi peke yangu,..’nikasema.

‘Wapi unataka kwenda…?’ akaniuliza.

‘Ni bora nisiseme kwa sasa, nisije kuwapotezea muda wenu…muhimu ujue kuwa kuna jambo nalifuatilia,…’nikasema.

‘Wapi, sasa, kwanini hutaki tushirikiane tulimalize hili mapema…’akasema kwa kulalamika

‘Afande, ngoja tusipoteze muda, …mimi naomba hivi.., nyie muendelee na Dalali…hakikisha hamumpotezi huyo mtu…kama mumeambiwa hivyo, kwa kauli ya shetani kuwa…wataondoka mmoja baada ya mwingine ..hiyo lugha ina ajenda ya siri hapo..’nikasema

‘Oh…siamini hayo, sasa eeh…ok, wewe nenda…na lolote utakalolipata nifahamishe haraka iwezekanavyo..unasikia…sitaki uje kuingia matatani..’akasema na kugeuka kurudi huko juu.

‘Sitaki uje kuingia matatani hahaha, usihofu afande…’nikayarudia yale maneno yake nikitizama saa ya ukutani,

‘Nitawahi tu…’nikasema

Hapo nikageuka huku na kule nikimtafuta yule mlinzi, alikuwa hajarudi,…taratibu nikatoka kwenye hilo jengo, akilini mwangu ilikuwa kuelekea huko baharini…ambapo nimeambiwa nitakutana na huyo jamaa….’chizi..’

Nilifika ufukweni…ila nilihis kama kuna mtu ananifuatilia kwa nyuma, na kila nikigeuka simuoni mtu, ila nahisi kuna mtu…sikujali, nikaendelea kutembea…nikafika sehemu niliyoelekezwa, nikaona, maboksi yamepangwa, kama meza, halafu kuna kiti kibovu..lakini hakuna mtu karibu...

Nikasogea eneo …nikahisi kitu…sijui, nikainama kidogo…nilichelewa,..kitu kigumu kiligonga kichwani…na kudondoka chini, sauti niliyosikia, ni…

‘Mkamate huyo…’nikapoteza fahamu.

NB….Sijaweza ku-edit vyema…


WAZO LA LEO: Tusikate tamaa , tupambane  na hali ilivyo…tutashinda tu. Yote maisha.
Ni mimi: emu-three

No comments :