‘Wewe mtu wa jamii mbona umetutoroka, kwanini
unafanya hivyo..haya niambie…unafanya nini huku…’ilikuwa sauti ya mpelelezi,
iliyotokea nyuma yangu…
Nilishtuka kidogo, maana sikutegemea hawa jamaa
watanifuatilia kwa muda huo na mimi nilishakuwa na mipangilio yangu tayari, nikageuka
na kuangaliana na mkuu huyu…
Tuendelee na kisa chetu….
*************
‘Hapana afande nilikuwa napoteza poteza muda huku,
maana nijuavyo mimi , nyie watu msingelipenda
niwaingilie kwenye kazi zenu au sio…’nikasema
‘Najua ujanja wako…hapo kuna jambo umeligundua,…’akasema
‘Hahaha afande mbona huniamini….’nikasema
‘Ok, sawa, ilimradi usivunje sheria…unajua hivi sasa
kutokana na muda, ..mimi nimeona, tushirikiane, sio kwamba tumeshindwa,kwahiyo
ukigundua jambo, usitufiche maana muda
unakwenda, na hadi hivi sasa sijaona jambo linalohusiana na kesi yako, haya yanayotokea
hivi sasa sioni uhusiano wake na hiyo kesi yako, kama ipo, tuambie…’akasema
‘Kama ni hivyo…afande, mimi naona ni bora mniachie nifanye kazi yangu, ili nije
kuwaonyesha uhusiano wa kesi yetu, na haya matukio..’nikasema
‘Kiukweli , huwezi kupewa ruhusa hiyo , maana hiyo
kesi ipo mikononi mwetu, na sio kwamba hatuifanyii kazi, tunaifanyia,..na
..’kabla hajamaliza nikasema
‘Afande …kumbuka huyo mnayehangaikia sasa hivi ni
Dalali, na Dalali ndiye kiini cha haya yote, nionavyo mimi,…sasa kwanini haya
yanatokea, kwanini anatoroka, kwanini, anaumwa,…ukiuanganisha utagundua kuwa
sabubu ni hilo deni…’nikasema
‘Inaweza ikawa hivyo, sitakai,..lakini ni ushahidi
gani utakaoliwezesha hilo, unajua sio kwamba napinga, lakini kuna swala la muda
hapa, wakili anahitajia ushahidi ili aweze kuweka pingamizi, ili mnada
usifanyike, ili kesi iingie mahakamani, sasa kama kuna jambo umeligundua ni
bora utuambie mapema, ili wakili awahi kufany kazi yake, sijui unanielewa…’akasema.
‘Kwahiyo kwa kauli hiyo umeshakubali kuwa na mimi
naweza kuingilia kazi zenu…?’ nikauliza
‘Sio kuingilia bwana..wewe vipi…, ila kama una jambo
la kusaidia tuambie, ukiingilia unakiuka sheria, na mimi sio mtungaji wa hizo
sheria,..wewe ni raia tu, wenye kazi ya kupeleleza hilo jambo ni sisi, nyie
mnatakiwa kutusaidia tu , unanielewa…’akasema
‘Mimi nionavyo hapo, kwa kifupi, hii kesi
imeshawashinda…kwahiyo mnahitajia msaada kutoka kwetu sisi raia, ni sawa, hilo
ni jukumu letu, lakini kwanini mnaniwekea vizingiti, ili niwasaidie, kama raia,
nipeni nafasi,..kibali ili niweze kufuatilia baadhi ya mambo..…tusipoteze muda,
kubali hilo…’nikasema
‘Wewe umetukimbia huko juu, ukaacha kuona
vioja..dunia hii kuna mambo…’akasema kupotezea nilichomuulizia…najua ni kwanini
mwenzake ndiye kikwazo.
‘Ehee, niambia kumetokea nini huko juu,…ila sio
naingilia kazi zenu..?’ nikauliza
‘Ok…unajua…huyo mgonjwa kabadilika kabisa…alianza
kujipiga piga, huku akipiga ukelele,..’moto, moto…’ lakini pale alipolala hakuna moto…ikawa ni kazi kumshika, watu
waliojaribu kumshika walirushwa kama mpira..mimi nikaona hayo ni mambo ya
kienyeji, ngoja niwaachie wenyewe…’akasema
‘Ndio ukaondoka kuja huku…?’ nikauliza
‘Nilibakia kidogo, nikasikia akiongea…maana tokea
awali, wanasema mtu huyo haongei, lakini hapo alianza kuongea , tena sauti sio
ya kwake…na jinsi alivyoweza kusimama, akawa anawarusha watu, kwa nguvu za
ajabu, ni kitu ambacho kilimshangaza docta…anasema hawajahi kuona, alikuwa akiongea
sauti nyingine kabisa…’akasema.
‘Aliongea nini..?’ nikauliza.
‘Maajabu…, eti ni kaka yake kamtokea,…mimi ni kaka
yake Dalali…hapo akataja jina lake, akianza na marehemu…akawa anasema;
‘Mimi nimekuja kufuatilia deni langu, nilishawaambia
nimeondoka nikiwa nimeacha deni kubwa sana,…fanyeni mfanyavyo, hilo deni
lilipwe,…kama mumeshindwa, waachieni benki wafanya wajuavyo wao, na familia
yangu itajaliwa majaliwa mengine....’hiyo sauti ikasema hivyo.
‘Nyie hamukuiliza, kwanini nyumba iuzwe, je yeye,
kama yeye, anakubaliana na hilo…’nikasema
‘Ninani angeliuliza hilo, sisi hatujui…tulibakia
tumeduwaa, yeye akaendelea kusisitiza hilo, kuwa anahitajia deni hilo lilipwe
haraka la sivyo…’akatulia hapo
‘Watu wangu wa karibu watadhurika…’akatulia kidogo na
mimi nikaona nimuulize …
‘Kudhurika kwa vipi kwa jinsi , ulivyoelewa wewe…?’
nikamuuliza
‘Nahisi watu wake wa karibu labda ndio hao watoto, na
akina Dalali…’akasema
‘Ehe…’nikasema
‘Aliendelea kuongea…;
‘Nyie mliniomba nitulie kwanza, ili watu wafuatilie
jinsi gani ya kulilipa hilo deni, aliyeniomba, keshaondoka, sababu kubwa ni
uwongo wake…sasa na nyie, mtafuatia mmoja baada ya mwingine…maana naona badala
ya kufuatilia deni, nyie mnafuatilia mambo mengine…’sauti ikasema hivyo.
‘Kasema , mtaalamu, keshajiunga huko alipo, sasa bado
wengine, wanahitajika…, kwahiyo anatuma huo ujumbe kwa wanaohusika, na ujumbe
huo tayari ameshauwakilisha kwa mkewe…’akatulia
‘Kwa mkewe, kwa njia gani…?’ nikamuuliza
‘Mimi sijui…labda uwasiliane naye kulihakiki
hilo..’akasema na mimi nikaona nisipoteze muda, nikampigia huyo mama mjane.
‘Vipi huko kumetokea nini…?’ nikamuuliza.
‘Oh…jana..sikulala….niliota mambo ya ajabu
ajabu,…tofauti na ndoto zile za kawaida…nilihisi majinamizi..na sauti ya
kutisha, ikisema, natakiwa kuhakikisha deni la mume wangu limelipwa…’akasema.
‘Ulisikia sauti kwenye ndoto ukiwa umelala au sio…?’ nikauliza.
‘Ndio…hiyo ni ndoto ya kutisha…ilibidi usiku huo nisiweze kulala kabisa, baada ya kuota ndoto hiyo, ...maana kila nikijaribu kulala, hiyo hali inajirudia…’akasema.
‘Je watoto vipi…?’ nikauliza.
‘Kuna muda walipiga kelele…nikawasomea, na kumuomba
mungu, wakatulia na kulala..ila hapa nilipo moyo wangu hauna amani,
najiulize..je ni kweli deni hilo lipo, huenda labda…’akataka kusema
‘Dada achana na mawazo hayo…hayo ni mashetani,…hilo
deni sio la mume wako, na hatua iliyofikia, …wewe ngoja tu, nahisi sasa hivi
tunaendea mwishoni…’nikasema
‘Haya, hata mimi siwezi kuamini…ila najiuliza mbona
awali sikuota hivyo..niliota mume wangu ananisaidia..sasa hivi , yeye tena
anakuja kunikaba…’akasema
‘Mashetani hayo..yasikutishe,…hali halisi itakuja
kujielezea, unasikia,..je hujapata chochote kingine,…?’ nikauliza
‘Una maana ushahidi,..kam hivyo…?’ akauliza
‘Ndio…’nikasema
‘Sijapata..nimefagia, nimekagua kila mahali, hakuna
kitu …’akasema
‘Basi usijali…’nikasema na kukata simu.
‘Haya umesikia mwenyewe…’akasema mpelelezi…maana
niliweka sauti kubwa , ili nay eye asikie nikiongea na huyo mama mjane.
‘Kwahiyo na wewe unaamini kuwa kweli hilo deni ni la
marahemu…?’ nikamuuliza
‘Mimi siamini kitu bila ushahidi..ilivyo, ..ushahidi
wa kuwa kweli hilo deni ni la marehemu upo..sasa kama sio lake, ushahidi upo
wapi..unielewe hapo…’akasema.
‘Nini zaidi aliongea…hiyo sauti iliongea?’ nikauliza.
‘Kuna kauli …sauti ilisema, wote wanaojua siri ya
hilo deni, kama wasipowajibika, kulilipa, nitawlipizia, kama nilivyofanya kwa
mtaalamu..sasa..neno siri…’akasema mpelelezi.
‘Siri…ina maana hilo deni lina siri au sio, na siri
hiyo anayeijua ni nani….?’ Nikauliza.
‘Ni hao watu wake wa karibu…’akasema
‘Ambao ni Dalali, mtaalamu na…’nikatulia hapo,..simu
yangu iliingia ujumbe wa maneno
‘Ndivyo alivyosema…’yeye akasema huku mimi nikisoma
huo ujumbe wa maneno, ni watu wangu, ..
‘Je kwenye hiyo sauti, hakuweza kuwataja hao watu
wake wa karibu.?’ nikamuuliza
‘Hakutaja jina, zaidi ya kusema hayo niliyokuambia na
zaidi akasema maneno haya ambayo ndiyo yalinifanya mimi nikutafute…’akasema
‘Maneno gani..?’ nikauliza
‘Na huyo moto,..sasa hivi, moto wake utazima..nilimuamini
sana, kumbe hana maana, siku zake zinahesabika…’akasema.
‘Moto..?!!!’ nikauliza kwa mshangao.
‘Ndio…’moto’….una elewa ni kwanini nimekutafuta kwa
kauli hiyo, si unakumbuka …?’ akaniuliza akiniangalia kwa mashaka.
‘Yaah…najiuliza tu, hilo neno nimelisikia mara nyingine
tena…, na kwanini linajirudia…moto…moto…ni jina au ni …tendo..?’ nikauliza.
‘Yeye huyo, kasema hivyo, ‘na huyo moto, moto wake
utazima…’..yaah, hata mimi nimeliwazia hilo, nilipokumbuka kauli yako, ndio
maana nikaona nikutafute, wewe..je wewe ulimaanisha nini, au uligundua nini,
kuhusiana na hilo…, ‘kwanini neno moto…limejirudia’…nikuulize wewe, je lina
maana yoyote kwako…?’ akaniuliza
‘Nakumbuka sana, na nahisi lina maana kubwa sana, na
kwa vile limetajwa hapo tena, nahis kuna kitu ndani yake, lakini je huyo mtoaji
hilo neno au kauli, anaaminika, ana siri gani yenye manufaa kwetu, isije pia
ikawa ni mtego…’nikasema.
‘Unakumbuka wakati tunafuatilia zile nyaraka
zilizoungua, wewe ulisem kuwa neno moto, linaweza kuwa ni ujumbe…na..unajua
nyie waandishi mna mambo, napenda sana fikira zako, ila nyingi ni maneno tu,
sisi tunataka ushahidi wenye kushikika, je kwa kauli hiyo una lolote la kusema…’akatulia
kama anawaza jambo.
‘Lakini natumai hadi hapo umeshaanza kuelewa ni
kwanini nilisema hivyo na bado naona kuna haja ya kutafuta ni nini kipo nyuma
ya hilo neno ‘moto’…umeona hapo, kuna ujumbe hapo, kama sio mtego au sio….?’ Nikamuuliza
huku nikiwaza jambo.
‘Yah nilikuelewa…lakini mimi siwezi kukubali jambo
mpaka nipate ushahidi.., na ndio maana kwangu mimi nashindwa kusema lolote, ila
bado nalifanyia kazi,...kuna jambo jingine nalo nalifuatulia, kama nitagundua
kitu, basi nitakuwa na wewe kwenye fikira zako, japokuwa ushahid wake bado ni
finyu kusema lolote…’akasema.
‘Jambo gani…?’ nikamuuliza
‘Kuhusiana na wamiliki wa ile kampuni na hii
hospitali…’akatulia akiniangalia moja kwa moja usoni.
‘Kwahiyo umegundua nini hadi hapo…?’ nikamuuliza
‘Nimeanza kupata picha fulani…nimejiuliza hapo,…ni.kwanini
hao wamiliki wameficha majina yao halisi. Hata kwenye hati zao za biashara,
ilikubalikaje hivyo, …ni kitu cha ajabu sana,…’akaangalia kama anawaza jambo.
‘Hii ina maana
gani, ya kuwa hata kwenye vitambulisho vyao watakuwa wameandika hivyo kwa
kufupi,…hapana, haiwezekani, nahisi kuna
jambo hapo halipo sawa....ila ngoja
nilifanyie kazi..’akasema
‘Je hilo litasaidia kesi ya deni linalosemwa ni la
marahemu...?’ nikauliza nikijikwangua kichwa kama kinawasha sana.
‘Mimi siangalii hivyo, mimi naangalia kwenye ukiukwaji
wa sheria…sasa je ukiukwaji huo wa sheria ni kutokana na hilo deni, hilo ni
swali jingine….na..kiukweli hadi hapa sijaona uhusiano wake na hilo deni…,
zaidi ni kuvunjwa kwa sheria, udanganyifu..kujaribu kuua,..na ndio maana nataka
mzee mtupe akamatwe, unanielewa hapo, lakini sio mimi niwe mvunjifu wa amri za
mahakama,….’akasema
‘Moto..utaleta jibu…., niamini afande, moto, moto…kama
ni jina au ni tendo, vyovyote iwavyo, kwa mapenzi ya mungu, tutapata jambo la
kuieleleza mahakama wapi sheria ilitakiwa iende..na mahakama imetimiza wajibu
wake ..je sisi watendaji,..tulitimiza wajibu wetu ili mahakama iamua itakiwavyo….sijui…..’nikasema
‘Moto utaleta jibu kwa vipi,…hizo nadharia zako
hazitaweza kusaidia,..sana sana ni kupoteza muda,wewe hujui hali ilivyo kwa
sasa, mimi naulizwa na wakubwa zangu, huku mahakama inatulaumu kwa kuzuia
jambo, bila ya kuwa na ushahidi..haya yananiweka mimi mahali pa njia panda, na
mwishowe unafikiria itatokea nini, siwezi kukubali kuharibu ajira yangu na
kiapo changu, ’ akasema.
‘Labda nikueleze jambo moja, wakati najaribu namba za
hao wamiliki wa hospitali na hizo kampuni..maana sio kampuni moja, hao jamaa
wana zaidi ya kampuni moja…’nikasema
‘Ndio, hilo tumeliona…’akasema.
‘Sasa kila sehemu wana namba tofauti na kwingine,
najua lengo lao ni kutaka kuonyesha kuwa hizo ni kampuni za watu tofauti…sasa…eeh,
kuna namba mbili tofauti, kwa mtu huyo mmoja…kwenye kuhakiki,.nimegundua herufu
ya awali, ya ‘M’ inasimama kwa jina ‘Maozo..’
nikasema
‘Maozo, ni jina hilo…?’ akuliza hivyo, sikumjibu
nikaendelea kuelezea.
‘Na kwenye ‘M’ ya mwisho, …kwenye hili jina…
‘M.AL.M.’…inasimama kwa jina ‘MOTO’…ina maana ‘moto ni nini..’nikasema
‘Namba ipi…?’ akauliza na mimi nikamuonyesha,
akaijaribu kutuma pesa, na alipoona hilo jina, akasema
‘Oh….ina maana basi ‘moto ‘ ni jina la mtu, sasa huyu
mtu ni nani na yupo wapi….?’ akaniuliza.
‘Hiyo ni kazi yenu kumtafuta huyo mtu, sijui ni huyo
wa huko nje,..au… au sio..au naweza kusaidia kama mnanihitajia, lakini
kivywangu…je mtaniruhusu..?’ nikasema na kuuliza.
‘Yah…nalijua
hilo, kuwa hiyo ni eeh… ni kazi yetu..na hili nitalimaliza hii leo, ili kieleweke,
kwa wakubwa zangu..na hadi jioni nitakuwa nimepata jibu kuwa,, huo mnada
uendelee au la….’akasema.
‘Natumai, hilo jina ‘Moto’ linaweza kuwa ufunguo,
..wa kuingia kwenye ukweli halisi, na kuupata ushahidi wa kulimaliza hili
tatizo…’nikasema…nikiwa nimeshika kichwa nikiwaza mambo mengi.
‘Lakini awali ulisema Dalali, ndiye ufunguo wa kupata
ukweli…’akasema
‘Ina maana ukweli haujajulikana kwa kupitia Dalali,
afande, kuna mengi tumegundua kupitia kwake, au sio…?’ nikamuuliza
‘Ukweli upi sasa, utakaosaidia hii kesi, unanielewa
lakini…?’ akauliza
‘Ukweli wa kuwa hilo deni sio sahihi kwa marehemu,
cha muhimu kuanzia sasa ni kuutafuta ushahidi mnaoutaka nyie, au sio…kwangu
mimi nimeshaliona hilo kinadharia, sasa kiushahidi wa kikwenu…ndio nataka mnipe
kibali. Ili niweze kuutafuta,… ushahidi mnaoutaka nyie…’nikasema.
‘Tuzizungushane hapa…mimi nakuambia ukweli, kama ushahidi
usipopatikana, aah, tusije kulaumiana,…’akasema
‘Leo,..tuombe mungu tu…’nikasema
‘Mimi nasema hivi, kama leo hakuna ushahidi, basi..amrii
ya mahakama lazima itimizwe,...sasa hivi tunakimbizana na muda, ulielewe hilo…’akasema
‘Sasa utaniruhusu, niutafute huo ushahidi…maana kuna
sehemu nataka kwenda , na ni bora
uniache niende mimi peke yangu,..’nikasema.
‘Wapi unataka kwenda…?’ akaniuliza.
‘Ni bora nisiseme kwa sasa, nisije kuwapotezea muda
wenu…muhimu ujue kuwa kuna jambo nalifuatilia,…’nikasema.
‘Wapi, sasa, kwanini hutaki tushirikiane tulimalize
hili mapema…’akasema kwa kulalamika
‘Afande, ngoja tusipoteze muda, …mimi naomba hivi..,
nyie muendelee na Dalali…hakikisha hamumpotezi huyo mtu…kama mumeambiwa hivyo, kwa
kauli ya shetani kuwa…wataondoka mmoja baada ya mwingine ..hiyo lugha ina
ajenda ya siri hapo..’nikasema
‘Oh…siamini hayo, sasa eeh…ok, wewe nenda…na lolote
utakalolipata nifahamishe haraka iwezekanavyo..unasikia…sitaki uje kuingia
matatani..’akasema na kugeuka kurudi huko juu.
‘Sitaki uje kuingia matatani hahaha, usihofu afande…’nikayarudia
yale maneno yake nikitizama saa ya ukutani,
‘Nitawahi tu…’nikasema
Hapo nikageuka huku na kule nikimtafuta yule mlinzi,
alikuwa hajarudi,…taratibu nikatoka kwenye hilo jengo, akilini mwangu ilikuwa kuelekea
huko baharini…ambapo nimeambiwa nitakutana na huyo jamaa….’chizi..’
Nilifika ufukweni…ila nilihis kama kuna mtu
ananifuatilia kwa nyuma, na kila nikigeuka simuoni mtu, ila nahisi kuna mtu…sikujali,
nikaendelea kutembea…nikafika sehemu niliyoelekezwa, nikaona, maboksi
yamepangwa, kama meza, halafu kuna kiti kibovu..lakini hakuna mtu karibu...
Nikasogea eneo …nikahisi kitu…sijui, nikainama kidogo…nilichelewa,..kitu
kigumu kiligonga kichwani…na kudondoka chini, sauti niliyosikia, ni…
‘Mkamate huyo…’nikapoteza fahamu.
NB….Sijaweza ku-edit vyema…
WAZO
LA LEO: Tusikate tamaa , tupambane na hali ilivyo…tutashinda tu. Yote maisha.
Ni mimi:
emu-three
No comments:
Post a Comment
Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com