Thursday, August 30, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-39


Wakati mpelelezi, anawapigia watu wake kuwaelekeza kazi, mara tukasikia kelele ikitokea ndani ya wodi aliolazwa mgonjwa, ...Dalali...

Tuendelee na kisa chetu...

************

Ile kelele ya kilio iliwafanya wapelelezi hao kukimbilia ndani, na mimi nikaona ndio nafsi yangu ya kucahana na hao watu,…kwa haraka nikashuka ngazi,…kabla sijafika kwenye ngazi, nikagundua chumba, mlango upo wazi, ndani yake kuna makabati, …ni kama masijala. Sehemu ya kuhifadhia kumbukumbu….

Nikaingia ndani ya hicho chumba…niliona meza, hakuna mtu, ila kuna dalili kuwa alikuwepo mtu humo ndani, …nikatoka nje kuhakikisha,…sikuona dalili ya  mtu karibu,..nikarudi ndani, nikaangalia huku na kule, nikaona sehemu kumeandikwa.

‘Kumbukumbu za wafanyakazi…’ nikasogelea na kuchukua dafutari kubwa, nikakagua, nikaona sehemu kuna majina ya wafanyakazi, na umri, na miaka ya kuajiriwa..hapo nikagundua, kitu nilichokuwa nikikitaka…

Kwa haraka nikatoka humo na kushuka ngazi hadi sehemu ya mapokezi. Nikamuendea yule binti wa mapokezi,…nilipomkaribia na kumuangalia usoni, nikagundua jambo,..huyu mdada...sio bint, kama unavyomuona kwa mbali, ukimkaribia ndio utafahamu kuwa huyu mdada ni mtu mnzima…

Bado  alikuwa kakaa pembeni,…kama alivyoamrishwa;

‘Samahani dada mpendwa, naomba nikuuliza jambo…?’ nikamwambia na hapo akanitupia jicho, akiwa kakunja uso kwa hasira.

‘Jambo gani, wewe uliza tu, lakini sio la kunifunga, maana leo mumeni..fanya nionekane kinyago…’akasema.

‘Nina hamu sana ya kufahamu hii hospitali…’nikasema na hapo akaonyesha uso wa kushangaa.

‘Kwani wewe haupo na hao watu…walioniharibia siku yangu…?’ akauliza akiniangalia moja kwa moja usoni...bila kupepesa jicho.

‘Kiukweli, sipo nao kikazi, …mimi ni mwandishi tu wa habari..nilikuja hapa kwa ajili ya kufanya utafiti fulani, wa kazi za hospitali, zinazowasaidia watu…, na hao nimekutana nao hapa, nikaona nitumie mwanya huo, ila kiukweli hapa mimi…sina nia mbaya kabisa…’nikasema.

‘Sasa unataka kuandika kuhusu nini, hakuna cha kuandika hapa,...usije kuniharibia kazi yangu, hii ni hospitali kama hospitali nyingime…’akasema

‘Najua..lakini tofauti na unavyofikiria wewe , mimi naweza kuandika mambo yakaisaidia hii hospitali kujulikana zaidi,...unalifahamu hilo, je ikujulikana kuwa kujulikana kwake kumeanzia zaidi kwako, unafikiri itakuwake.... na.., hopsitali hii ina bahati sana...'nikasema

'Bahati gani...?' akaniuliza akionyesha shauku.

'Kuwa na warembo wazuri..wakiongozwa na wewe...'nikasema kwanza akiniangalia kama haamini ninachoongea, halafu akatabasamu...tabasamu likaenda kwenye kicheko.

'Hahahahee....una maneno ..eti warembo wapo wapi hao...?' akauliza

'Wewe mwenyewe hapo unaongoza, watu wengi si wanakusifia hivyo...?' nikauliza

'Wananisifia,..lakini mbona hawanioi...naona sifa zao hazina maana, ni kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa,...sina haja nako...'akasema

'Kiukweli, sura yako ni ya mvuto..hivi kwanini hujagombea ulimbwende, nimekaa huko nikashindwa, nikaona hata, ngoja niongee nawe kidogo, huku nikifanya kazi yangu…’nikasema na hapo nikaona tabasamu likizidi mdomoni, nikaona nimefanikiwa.

‘Hahaheee…’akacheka mpaka watu wakageuka kumuangalia...alipoona hivyo akajibaragua, sasa akawa ananiangalia kwa shauku.

‘Mhhh naona wewe utaifanya siku yanguu iwe nzuri,..unajua kuharibiwa siku, leo hawa watu, sijui wamekuja kufanya nini hapa, wameniuzi sana…wameniharibiwa siku yangu, nilijiremba leo, nilijua ..aah, shida tupu…’akasema.

‘Usijali..mrembo kama wewe hustahiki kufanyiwa hivyo, ..pole sana…na hawajui kuwa wewe ni bosi wa hii kampuni maana unafahamu kila kitu,…wangekufanyia ihsani, wasingelisumbuka hivyo…’akasema.

‘Umejuaje…nimependa sana ongea yako….haya niambie unataka kujua nini…?’ akauliza.

‘Najua wewe ni kama mwanzilishi wa hii hospitali, hivi wewe uliajiriwa lini humu..?’ nikamuuliza, na akatabasamu..

‘Hehehe…yaani, isingelikuwa..hao watu, tungeongea mengi tu,..mimi hapa nimeajiriwa, tangu hospitali hii ianzwishe,  hao wengine wote, mabosi huko juu, wamenikuta mimi hapa, hata huyo mlinzi, …japokuwa hatukupishana sana, alinikuta mimi hapa..sasa mwenyewe utajua ni lini niliajiriwa …’akageuka huku na kule nahisi alikuwa akimtafuta mtu.

‘Usiwe na wasiwasi, wakuu wanongea na wakubwa zako huko juu,…hawakujua kuwa kuna mtu anafahahamu kila kitu hapa…mrembo wa hii hospitali…nimesikia kuwa wao wanamtafuta mgonjwa mmoja, aliyetoweka huko alipokuwa akitibiwa…’nikasema.

‘Mgonjwa huyu wa ajabu sana, si ndio huyo waliyeniulizia mimi, wajinga sana, wangeniuliza kwa ustaraabu , ningeliwaambia kila kitu…’akasema.

‘Kwanini ni mgonjwa wa ajabu…?’ nikauliza.

‘Mhh..hata siwezi kuliongea hili,…wengi hawawezi kuniamini…mmh, lakini mimi ninaona yasiyoonekana, ndio maana hata huyo aliyekuwa mkuu wa hii hospital, aliniajiri, kwa kuniamini, kuwa nitakuja kumsaidia sana,…’akasema

‘Ndio huyu yupo nchi za nje…?’ nikamuuliza
‘Hahaha,..hapana, kuna ambaye alisimamia kila kitu, yeye ni kama mwenye hii hospitali…’akasema.

‘Anaitwa nani…?’ nikamuuliza

‘Nani huyu mwenye kampuni, au huyu aliyesimamia…huyu wan je..jina lake gumu ..sijui nani vile..ila huyu wa hapa..japokuwa, hayupo,..ana matatizo yake binafsi, ..kwanini unataka jina lake..?’ akaniuliza, nikaona nisimkimbize huko, nikauliza swali jingine.

‘Niambie huyo mgonjwa…, ana maajabu gani..yeye si mgonjwa tu au jambo zaidi ya huo ugonjwa wake…?’ nikauliza.

‘Wagonjwa wengine wanakuja na nuksi zao, na huyo ni mmojawapo…’akasema

‘Mhh, sikuelewi…’nikasema hivyo.

 ‘Huyo mgonjwa ni mchawi…nuksi mkubwa, …sijui kwanini walimpokea…’huyo mdada akasema na kunifanya nishtuke kidogo.

‘Mchawi…!!! Kwanini, walimpokea akina nani, si wewe ndio unawapokea wagonjwa, kwa uoni wangu, huenda huo ugonjwa wake ndio umemchanganya kichwa, namuonea huruma sana...’nikasema.

‘Mimi nina mambo yangu kichwani mtu kama ana uchawi, au mambo yake mabaya ninamfahamu tu…’akasema.

‘Kwahiyo, unataka kusema nini…? ‘nikamuuliza.

‘Huyo mgonjwa…ni kweli ni mgonjwa sikatai…, lakini pia, ni mchawi..au anatumiwa na wachawi, niamini hilo,…….’akasema

‘Mhh…una uhakika gani na hayo maneno yako…?’ nikamuuliza, nikionyesha uso wa mshangao.

‘Usiku alitoka nje,…’akasema na hapo nikajikuta nashtuka.

‘Hapana,..naona umekosea, mgonjwa ninayemzungumzia mimi ni mgonjwa mmoja hawezi hata kujiinua kitandani,… atatokaje nje…?’ nikauliza.

‘Huwezi amini hilo…ila mimi nilimuona kwa macho yangu haya mawili, nilimuamboa bosi wangu lakini hakuniamini…’akasema.

‘Bosi yupi,…?’ nikauliza.

‘Bosi wangu mimi, sio huyo huko juu, kuna bosi wa utawala..mnoko kama nini..’akasema.

‘Yupo wapi…?’ nikauliza.

‘Katoka…na safari zake…’akasema.

‘Sasa kwanini hakukusikiliza…?’ nikamuuliza.

‘Mimi…sijui, …labda ni kwa vile haamini mambo hayo,…anajifanya msomi, kiingereza kingi mdomoni…hahaha..ila kwangu mimi kalewa, ndio nampendea hapo….’akasema.

‘Mimi siamini,..ulimuona kwa macho yako, akitoka nje…kwanza ilikuwa muda gani…?’ nikamuuliza.

‘Hahaha.hee…vijana bwana, dunia hii ina mambo,…mimi hawataki kunioa kwa sababu ya mambo yangu kichwani..amini hilo, alitoka,..na nilimuona kwa macho haya mawili, na ilikuwa usiku,kama  saa sita hivi….’akasema.

‘Usiku ulikuwa bado upo kazini…?’ nikamuuliza.

‘Umesoma hapo nje..hapa ni masaa 24, na mawili ya ziada,..tupo kazini…na mimi silali,..sina ugonjwa wa kulala…nilimuona akitoka…nikajifanya nimelala, sasa tembea yake ndio utachoka…’akasema.

‘Mhh, akitembeaje,..?’ nikamuuliza hivyo.., na hapo akawa anaigiza kutembea kule kwa kunyata, kama roboti…kwa mikono…karibu nicheke.

‘Unacheka…mimi nimeona mengi..unaiona hii sura yangu, bado mdada mbichi, lakin umri wangu, …huwezi amini…kwahiyo najua mengi, ya kale na mengi ya sasa..najua kuishi kischana na kiutu-uzima..’akasema.

‘Hongera, ndio maana bado mbichi….natamani nije kutoka na wewe mrembo wa aina yake..’nikasema hivyo, na hapo ndio akajirembua,…nikajua hapa nimempata.

‘Mhh..hehehehe…jaribu kama hutaumbuka, …wenzako wanakimbia, ..maana yakinipanda,…kila ninachotaka ni lazima nikipate…’akasema.

‘Nikuulize tu, kwanini sasa alikuwa akitembea hivyo, kama roboti..?’ nikamuuliza ,hapo akatabasamu, na kusema;
‘Nguvu za kichawi hizo,..ndio maana nahisi sio kwa uwezo wake, kuna mtu alimchezea undondocha…akawa anavutwa na hizo nguvu…akatoka nje..na kuondoka, lakini baadae alirudi…’akasema.

‘Hukujua alikwenda wapi..?’ nikamuuliza, hapo akatulia kidogo kama anawaza jambo.

‘Unajua pamoja na kazi hizi, bado nilijua ni wajibu wangu kuchunga wanaotoka na kuingia ndani, mimi nikikaa hapo mezani, macho na masikio yanafanya kazi yake..ndio maana nipo hapa hadi leo..silipwi vizuri, lakini nikiwa na shida ndogo ndogo napata ninachokitaka.., sina shida..’akasema.

‘Hongera…’nikasema.

‘Asentee,….ndio …nikamuamusha huyo mlinzi…jamani huyo mlinzi kwa kulala, amezidi..ipo siku atafumwa, asinitegemee mimi kila wakati nitakuwa namlinda, ..ni kaka yangu wa kikazi maana tumeanza naye hapa..namlinda, namsaidia, ana familia kubwa, kazaa kama kuku, ..’akasema

‘Huyu mlinzi ni yupi…?’ nikamuuliza

‘Si yule pale….sema kiukweli anawajibika sana,…na anapendwa, mimi nay eye tunapendwa, sio utani,…’akaangalia huku na kule kama anamtafuta mtu.

‘Basi……nilimuambia amfuatilie huyo mtu, na aliogopa sana, ..kwa vile alikuwa amelala na  mtu kampita bila ya yeye kumuona, …na kweli alimfuatilia, nashangaa badae anarudi jasho linamtoka hata kuongea hawezi akadondoka na kupoteza fahamu …’akasema.

‘Kwanini sasa..?’ nikamuuliza

‘Watakuwa waligundua kuwa kuna mtu anamfuatilia, huyo mtu wao… sema, hawakutaka kumuumiza…ila cha moto alikiona, isingelikuwa na mimi nafahamu baadhi ya madawa ya kuagua, jamaa tungemsahau…’akasema

‘Ok nitaongea nawe baadae, nimefurahi sana kuonana na mrembo wa hii hospitali, usisahau, …nitala nije tutoke wote..…’ nikasema nikiwa na hamu ya kufahamu wapi huyo mgonjwa alikwenda.

Haheheeeh, wewe, shauri lako…’akasema

‘Je naweza kuongea na yule mlinzi..?’ nikamuuliza

‘Ila usiseme ni mimi nimakuambia hayo, sitaki kabisa…., na sijui kwanini nimekuambia hayo, nahisi wewe sio mtu mwema…’akasema akitikisa kichwa.

‘Usijali…hujafanya jambo baya,….’nikasema na kumuendea huyo mlinzi,..nilimkuta anasinzia…nikatoa shilingi elifu tano, na kumsogezea usoni mwake, alipofungua macho akaona hiyo noti mbele yake. Akashtuka, na kuiangalia kwa macho yenye uchu.

‘Bosi naona una njaa…unaweza kwenda kununua chochote…’nikasema na ile noti nikiwa nimeishikilia mkononi, na yule mlinzi akawa anaendelea kuiangalia kwa macho ya tamaa.

‘Oh…nitashukuru…hapa nina njaa, nasubiria wanitume, angalau nami…mhhh.. huenda nitapata chochote,…haya maisha jamani…’akasema sasa akipiga miayo.

‘Lakini kabla hujaondoka kununua chochote nikuulize jambo…’nikasema

‘Jambo gani…?’ akauliza kwa mashaka.

‘Wewe jana ulimfuatilia yule mgonjwa, kwanini uliacha akatoka wakati unajua ni wajibu wako kuwalinda wagonjwa ..?’ nikamuuliza.

Mlinzi yule alibadilika sura, akaniangalia kama kaona jinamizi.

‘Ume-jua-aje..ni nani…ooh, hapana, haikuwa hivyo…’akasema.

‘Ilikuwaje…niambie ukweli maana kuna video ilikuona, ukilala na kuwacha mgonjwa atoke je angepatwa na matatizo ingelikuwaje…’nikasema.

‘Hapana, …naapa siku-ilitokea bahati mbaya tu,.sijui kwanini …hata sasa sielewi, muda mwingi nilikuwa macho, lakini muda aliopita huyo mtu,…sijui ilikuwaje, nisamehe tu…’akasema akitaka hata kupiga magoti.

‘Utawezaje kujitetea kwa bosi wako sasa, maana nataka kwenda kulalamika...’nikasema.

‘Oh…jamani,..usije kusema kwa bosi, nakuomba tafadhali…nina watoto na familia inanitegemea…’akaongea akitaka hata kulia.

‘Ok..usijali, muhimu uniambie ukweli, ilivyokuwa,…ehe..uliamuka ukakuta ameshatoka, ukamfuatilia, kwanini ulimfuatilia..?’ nikamuuliza na hapo akawa kama haamini anachosikia, na..akaangalia juu, kuangalia kama ataona kitu kilichochukua hayo matukio.

 ‘Ni kweli, nitakuambia, maana hata sijui ulitokeaje hivyo,..hadi sasa sijawa vizuri…’akasema akionyesha uso wa wasiwasi.

‘Hebu nikuulize hapa hospitalini,..uliajiriwa lini..?’ nikamuuliza.

‘Muda sasa..mimi inajengwa naiona, nikawa nalinda vifaa, ikakamilika na kuanza kazi, nikaendelea kuwa mlinzi, hadi leo, kwahiyo mimi hapa ni  mkongwe pamoja na yule dada, yule dada kanitangulia kidogo…’akasema.

‘Kwahiyo kumbe unamfahamu hata mwenye kumiliki hii hospitali..’nikasema.

‘Mhh…hapana…nasikia yupo nje ya nchi..ila kuna mtu analiyeishughulikia, hadi leo..japo, ….’akasema na kukatiza.

‘Mbona unajibu kwa kutokujiamini,….je nikimuambia bosi wako hayo yaliyotokea usiku, ndio hivyo utaongea, mbele yake …eeh..’nikasema.

‘Tafadhali usimwambie,..nitakuambia kila kitu…’akasema.
 ‘Sawa…niuliza tu…’akasema

‘Mwenye kampuni, ambaye mnamfahamu nyie, ndiye aliyakuajiri wewe…?’ nikamuuliza

‘Ndio…’akasema

‘Kwahiyo unamfahamu kwa ukaribu sana…?’ nikauliza

 ‘Yah…ni mtu mwema sana..’akasema.

‘Kwahiyo unalipwa vizuri…’nikasema hivyo sikuwa na maana ya kumuuliza
.

‘We acha tu,..hawa wageni waliokuja kuajiriwa, ndio wabaya,…kabisa kabisa nasema kutoka moyoni, ila sasa utasemaje, ukiongelea mshahara, ujue ndio siku yako ya kufukuzwa kazi,..unajua nikuambie kitu…siku moja nilimtembelea huyo jamaa..unajua keshakuwa chizi…’akasema

‘Nani huyo…?’ nikamuuliza

‘Huyo mumuliki,…ambaye tunamtambua sisi…’akasema

‘Oh…una uhakika…?’ nikamuuliza

‘Chizi , chizi..lakini cha ajabu hajanisahau…nilipofika kwake, alikuwa yupo vizuri, …tukakaa tukaongea…akaniuliza habari za kazi, naendeleaje, …., mara huyoo, mashetani yakampanda, akaanza kukimbia, mimi sijui hili wala lile,..jamaa zake wakaanza kumfukuza, nasikia walimkuta yupo ufukweni mwa bahari…’akasema,

‘Oh, imekuwa hayo, ni kwanini yupo hivyo..?’ nikamuuliza

‘Nilivyoulizia, watu wengine, …wanadai ni kutegana wao wenyewe kwa wenyewe..,..hizi biashara nyingine zimegubikwa na mambo haramu, mtu unataka utajiri kwa kupitia mambo kama hayo …fuuu’ akasema akupuliza kwenye mkono.

‘Una uhakika gani na hilo…?’ nikamuuliza

‘Mhh, kiukweli, sina uhakika na hilo..kiukweli tunaongea tu..nikuulize kwanza wewe ni nani, maana umenipatia kweli kweli..?’ akaniuliza.

‘Mimi ni mtu wa jamii, mara nyingi nikiona tukio, napenda kulifuatilia kujua ni kwanini limetokea hivyo, na kama kuna namna ya kusaidia,..nisaidie..ndio maisha yangu yalivyo, sasa mimi nafuatilia matibabu ya huyo mgonjwa,..’nikasema bado nimeshikilia ile noti.

‘Sasa ..unasemaje, maana hapa umenitega kweli,..nina njaa, na huku unanitishia …sikiliza ndugu yangu, ..nipe hiyo pesa nikanunue chochote..hapa tumbo linangurua kwa njaa…’akasema

‘Nitakupatia…ila bado kuna mambo sijayaelewa,..ukinielezea, basi mimi nitaachana na wewe, sina haja ya kwenda kuonana na bosi wako kukushitakia…’nikasema

‘Mambo gani hujayaelewa hapo eeh..?’ akauliza.

 ‘Usijali, mimi sina nia mbaya kama nilivyokuambia,…mimi kiujumla  nataka kuonana na huyo ;chizi..ili niweze kujua zaidi, nimefurahishwa na …hadithi hii’ ..nikasema

‘Hahaha,..hii sio hadithi ni ukweli mtupu…lakini kwa vile umenijali, mimi nitakuelekeza, lakini usije kusema ni mimi nimekuambia , hapa nimekueleza tu kwa vile…umenitega, na sijui kwanini…nimekuamini kiasi hicho, mmh, uwe makini, usije kunilaumu…’akasema.

‘Hapana, siwezi kukulaumu, ila maneno yako ya kwanza, kuwa niwe makini, nahisi unajua jambo…hutaki mimi niwe rafiki yako..?’ nikauliza

‘Rafiki !!.....hahaha, ukinijali tumbo langu na watoto wangu, huna haja ya kuliuliza hilo…nipe hiyo pesa basi…..’akasema na mimi nikawa kama nataka kumpa, ila sikumpatia, nikasema

‘Hii ni yako usijali…lakini ….bado nahitajia msaada wako, nataka kujua zaidi...’nikasema

‘Wataka kujua nini..?’ akauliza

‘Huyo mgonjwa alitokaje..hadi usimuone..?’ nikamuuliza na hapo akaonyesha uso wa mashaka.

‘Huyu mgonjwa,…kachanganyikiwa, na alivyotoka hapa mlangoni,..sikumuona kabisa.. siamini..mimi kiukweli wakati mwingine napitiwa na usingizi..lakini ukisogea karibu yangu, nitaamuka tu, nalala kama paka..king’amu ng’amu, mimi nilikuwa askari. Mpiganaji, nikaacha kazi, nilikuwa naumwa umwa, lakini bado uaskari upo kweney damu…sasa sijui alinifanya nini…’akatulia

‘Alikupilizia madawa labda…’nikasema

‘Hapana..na dada yeye kasema huyo mgonjwa  ni mwanga… yule dada ana mashetani, wanamlinda,…na hao wadudu wake huwa wanampa habari..basi, unjua tena, nilishaharibu, kulala..kuliponza,..njaa tena…mdada akaniambia nimfuatilie huyo mgonjwa..’akatulia

‘Kwa haraka nikamfuatilia…nilimuona kwa mbali, ile tembea ya kinyonga, lakini kwa haraka kweli…nikajitahidi wee, sikuweza kumkaribia,…nikajitahidi kukimbia , lakini sikuweza…mara kwa mbele nikaona…jitu-mtu refu,...'akasema sasa akionyesha wasiwasi kama kweli analiona

'Unajua urefu wake..mimi pale nilipo, niliona .. miguu na kiwili wili, kichwa sikubahatika kukiona, maana ni refu, ingelinibidi niinue kichwa hivi...kuangalia juu, ili nimuone kichwa chake..lakini wewe ni nani angalifanya hivyo, nilipoona hivyo,…wee, nikageuka, …hata sijui nilifikaje hapa..’akasema sasa akionyesha uso wa mashaka.

‘Una uhakika, uliona hivyo, sio ni huo uwoga wako tu…?’ nikamuuliza na mara huyo mlinzi akaitwa…

 ‘Mlinzii….’sauti ikaita..na hapo jamaa huyo, akasimama

‘Bosiii….nakuja…’akasema, haya nipe basi, maana ndio hivyo, nimeanza kutumwa hivyo, wakianza kunituma hapa ..ndio hivyo, mlinzi, mlinzi.... hakuna kukaa…’akasema.

‘Ikawaje,..malizia kwanza. kwa haraka....’nikasema.

‘Ikawaje ...hahaha...! Nakuambia sijui mimi nilifikaje hapa...maana ninachokumbuka,..ni kujigomba mlangoni, nikitaka kuingia, ..na mlango unafunguliwa na mdada... nikadondoka,…yaliyotokea baadae alikuja kunihadithia dada…namshukuru sana, sijui nitamlipa nini…’akasema.

‘Hakuna mtu mwingine uliyemuona…wakati unamfuatilia huyo mgonjwa…?’ nikamuuliza.

‘Hapa—na…ooh, ndio, wakati nakimbia, nilimuona mzee mmoja, sasa cha ajabu, nimekuja kumkumbuka, … huyo mzee alikuja hapa, ndio nikakumbuka ndio yeye niliyemuona usiku...’akasema.

‘Ulimgunduaje kuwa ndio yeye…?’ nikamuuliza.

‘Kama askari unaweza kumjua mtu kwa haraka, tembea, alivyo…ndio yeye sina shaka ya hilo…’akasema.

‘Unamfahamu huyo mzee vyema, hajawahi kufika hapa kabla.?’ Nikamuuliza.

‘Mhh…kama kufika hapa labda akija kutibiwa lakini sikumbuki …yawezekana, unajua wanakuja watu wengi, ila sura yake sio ngeni kwangu…’akasema na kuelezea jinsi alivyo.

‘Atakuwa ni mzee  mtupe,…. hahaha hana lolote yule, ndiye ulimuogopa…’nikasema.

‘Sio yeye niliyemuogopa bwana, mimi niliona sheteni,…jitu refu, limevaa manguo meupe,..usitake nikumbuke…’akasema.

‘Lakini baadae si umesema ulikuja kumuona huyo mzee, alikuwa kasimama au anatembea…?’ nikamuuliza.

‘Kasimama ananiangalia….na alipoona nakimbia, akageuka kurudi alipotoka, huyo mzee ni Kigagula…’akasema.

‘Kwanini unafikiria hivyo…?’ nikamuuliza.

‘Hebu jiulize, yaliyotokea , halafu umuone mtu kasimama anaangalia muelekeo wenu, baadae ageuka kurudi alipotoka…’akasema sasa akigeuka kule alipoitiwa.

‘Haya chukua pesa…ila mimi nataka kuonana na huyo chizi, uliyemtaja nitampataje…?’nikauliza.

‘Ukitaka urahisi nenda kamvizie baharini, nasikia ni lazima kila siku afike huko..sijui kwanini anakwenda huko….kuna sehemu anapenda kukaa, ..katengeneza kama ofisi ya kichizi, ukifika utafikiri yupo ofisini…’akasema na kundoka haraka.

Hapo shauku ya kuonana na huyo Chizi...kama alivyomuita huyo mlinzi, ikanijia...lakini nikajiuliza, iweje, na nitawezaje kwenda bila kuwashirikisha hao wapelelezi...kiukweli sikupenda kuwashirikisha...lakini je...likitokea lolote...na kwanini litokee.

'Chizi...'nahisi huyu chizi..atanisaidia jambo, hata kama ni chizi...nikawa nawaza na mara, sauti ikatokea nyuma yangu...

************

‘Wewe mtu wa jamii mbona umetutoroka,…unafanya nini huku…’ilikuwa sauti y mpelelezi, ikutoka nyuma yangu…nilishtuka kidogo, maana sikutegemea watanifuatilia na muda huo nilishaanza kutembea kutaka kutoka nje…

NB: Je mtu wa jamii atakwenda huko peke yake kumtafuta huyo ‘chizi…’? Huyo chizi ni nani,…

WAZO LA LEO: 

Usipende kuwazarau wengine, au kuzarau kila jambo kwa vile wewe unajua zaidi, …

 Kuna watu walio soma, na mara nyingi wakikaa na wengine wasio na elimu zaidi yao, hupenda kuwazarau wenzi wao…, hata hawapendi kusikiliza wenzao wanachoongea, kisa wao wamesoma zaidi.

 Ni kweli aliyesoma ‘elimu’ sio sawa na yule aliyesoma kidogo, au chini ya hapo…lakini tukumbuke kufahamu mambo kunaweza kukatofautiana, kuna elimu nyingine sio za darasani, kuna elimu za mazingira watu wanavyoishi nk, una elimu za aina mbali mbali, huwezi kuzisomea zote.

Wanasema hivi… Hata usome vipi, hutaweza kufahamu kila jambo.
Ni mimi: emu-three

No comments:

Post a Comment

Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com