Haraka tulifika hospitali ambayo mpelelezi
alielekezwa na huyo mtu wake,..ambapo kwa maelezo aliyoyapata, kagundua wapi Dalali,
kalazwa…lakini taarifa nyingi mitaani kwa hivi saa ni kuwa Dalali keshafariki,
ndugu zake wanaficha ukweli.
‘Mtu wangu kanipigia simu kagundua wapi
walipohifadhiwa Dalali…’akasema mpelelezi.
‘Kuhifadhiwa kwa vipi, …maiti yake au…?’ nikauliza.
‘Maiti!!!..hahaha, hapana bwana, usisikilize uvumi wa
watu, hatujapata taarifa zozote kuwa Dalali kafariki…’akasema.
‘Watu wangu,..waliona watu wakiwa wamebeba mgonjwa,
…wakimuingiza kwenye hiyo hospitali, na walipochunguza wakagundua kuwa ni
Dalali...’akasema sasa tukiwa safarini kuelekea huko.
Tulifika hilo eneo, na kukutana na jamaa moja, akasema;
‘Kwenye hilo jengo hapo, hilo jengo ni la hospitali,
japokuwa haifahamiki sana,..ila ni hospitali kubwa, ina wataalamu kweli…’akasema
mtu wa mpelelezi, akituonyesha kwa kidole.
Tukawa
tunatembea kuelekea kwenye hilo jengo, tuliacha gari mbali kidogo, ili tusije
kuleta namna ambayo huyo mtu wetu atatoroka, au kutoroshwa,….mimi nikawa
nafuatilia nyuma.
‘Huko juu kuna ofisi za watendaji …’akasema huyo mtu
wa mpelelezi…mapokezi ni hiyo hapo mbele..’akasema huyo mtu. Wapelelezi hawa
wawili wakateta kidogo, halafu mmoja akiongozana na huyo jamaa aliyetuleta
hapo, akaondoka na mpelelezi, sijui wanaenda wapi.
Mimi nikabakia na huyu mpelelezi mmoja, ambaye
alisogea hadi sehemu ya mauliza, na mimi nikawa nyuma yake..
‘Nani mumiliki
wa hii hospitali…?’ akauliza afande, akimuuliza mdada mmoja aliyekaa kwenye
meza ya mapokezi.
‘Kwani nyie ni nani, na mnataka nini, nyie sio
wagonjwa…?’ akauliza na mpelelezi akatoa kitambulisho chake na kujitambulisha.
Yule mdada akataka kupiga simu, na huyo mpelelezi, akasema;
‘Sogea huku, uwe mbali na hiyo simu..’akaambiwa na
huyo mdada akafanya hivyo akionyesha wasiwasi…
‘Haya niambie ni nani mwenye mamlaka na hii
hospitali..?’ akaulizwa, na pale nikawa najiuliza yule mpelelezi mwingine
kaenda wapi, maana nilikuwa na mashaka, hawa watu wakigundua kuwa kuna watu wa
usalama, huenda wakakimbilia kumfica huyo mtu tunayemtafuta.
.
‘Hayupo, yupo nchi za nje…’akasema huyo dada
‘Kwahiyo ni nani mwenye mamlaka na hii hospitali kwa
hivi sasa, bosi wenu ni nani…?’ akauliza
afande.
‘Ni…yupo ofisini kwake huko juu,…’akasema huyo mdada
akiangalia huku na kule kwa mashaka.
‘Haya hebu niambie, kuna mgonjwa mwenye jina la
….alimaarufu Dalali…?’ akauliza
Yule mdada akachukua daftari, lenye orodha ya
wagonjwa,akaanza kutafuta hilo jina,..baadae akasema;
‘Hakuna mwenye jina kama hilo…’akasema akiendeela kupekua
orodha ya majina.
‘Una uhakika..?’ akaulizwa
‘Ndio angalia orodha ya wagonjwa waliofikishwa hapa
…’akasema akitoa hicho kitabu cha wagonjwa walioingia hapo hospitalini, na wakati
wanaendelea ndio akaja yule jamaa aliyeondoka na mpelelezi, akasema;
‘Afande yupo huko juu, afande ameshamuona, ndio yeye…’akasema
huyo jamaa.
‘Sawa nakuja…’akasema mpelelezi, na akamwambia askari
mwingine aliyevalia sare rasmi,
‘Hakikisha huyu mdada hashiki simu…’akasema
mpelelezi,
‘Ofisi ya kiongozi wa hii hospitali yupo chumba
gani..?’ akamuuliza huyo mdada, kabla hatujaachana naye na huyo mdada akaongea
kwa sauti ya uwoga akitaka namba ya hicho chumba mbacho bosi wake yupo.
‘Usiwe na wasiwasi, hatua nia mbaya na bosi wako,…sis
kuna mgonjwa tunamtafuta, unasikia, hutafukuzwa kazi…’akasema
mpelelezi,…tukaelekea juu, kwa kupitia kwenye ngazi,..tulipofika sehemu ya juu,
tukageuka kushoto na kulia, na mbele yetu tukaiona hiyo ofisi ya mkuu wa hiyo hospitali.
Tukafika na kugonga mlango.
‘Ingia…’sauti nzito ikasema kutoka ndani.
Akaanza kuingia mpelelezi na kujitambulisha, na
baadae tukaingia sisi wengine, …jamaa sasa nikaona kijashi kikimtoka,.
‘Niwasaidie nini wakuu..’akasema, akijikaza kutokuonyesha
wasiwasi.
‘Tunakuomba tuongozane na wewe kuna mgonjwa tunataka
kuonana naye…’akaambiwa.
‘Kwa-kwani..kuna tatizo gani..?’ akauliza.
‘Wewe twende tu, utajua tatizo ni nini, tukionana
naye…’akaambiwa na tukatoka hapo hadi kwenye chumba kingine, anayetuongoza ni
yule askari kanzu
‘Chumba cha
wagonjwa maalumu…’ akasoma mpelelezi kwa nguvu.
‘Humu mnalaza watu wa namna gani..?’ akaulizwa
‘Wagonjwa waliozidiwa, au wagonjwa wanaohitajia
huduma maalumu..’akasema
‘Orodha yake pia iko kwenye kile kitabu cha mapokezi..?’
akaulizwa
‘Wakati mwingine inasahaulika, maana wagonjwa kama
hao, wakiletwa hapa, huwa wamezidiwa, kwahiyo kwa haraka wanakimbizwa kupata matibabu ya haraka, ndio
tunaita matibabu maalumu…, lakini baadae jina la huyo mgonjwa aliyewahishwa huku,
ni lazima liingizwe kwenye kile kitabu.
‘Mgonjwa gani kaingizwa humu ambaye jina lake
halijaandikiwa kule..?’ akaulizwa
‘Siwezi kujua, kwakweli,…maana mimi ni mkuu wa hii
hospitali, naletewa taarifa muhimu tu..ila orodha hizo zinaletwa jioni, au nikihitajia,
sio lazima kila siku nizipitie…’akasema.
Basi wapelelezi hao wakaingia humo ndani, na tukamkuta
yule mpelelezi mwingine yupo anaongea na docta mmoja,..na pembeni kabisa kwenye
kitanda, tukamuona mgonjwa kalazwa…akiwa kawekewa chupa za kuongeza maji..
‘Yule pale ni nani..?’ akaulizwa
‘Siwezi kujua mpaka nisome kadi yake…’akasema na
wakasogea hadi pale alipolazwa mgonjwa, na jina likabainika, jina la kama bandia..ila
kwa herufu za mwanzo kwa kifupi.
‘Una uhakika hujui lolote kuhusu huyu mgonjwa..?’
akaulizwa.
‘Ki-kiukweli mimi sijui…kama nilivyosema mimi ni
msimamizi, meneja wa hii hospitali, majukumu ya wagonjwa, yanafanywa na
wenzangu walio chini yangu…’akasema
‘Ni nani sasa anayhusika hapa..?’ akauliza afande
‘Ni huyo hapo…’akasema akimuonyeshea docta mmoja
aliyekuwa akiongea na yule mpelelezi mwingine.
Wakateta, kidogo wakuu hawa wawili,…na baadae huyu
mpelelezi tuliyekuja naye akaendelea kuhoji….
‘Tuambie kuhusu huyu mgonjwa aliletwa na nani hapa.?’
afande akamgeukia huyo jamaa mwingine.
‘Kama nilivyomuambia huyu mwenzako,..kuna jamaa
walifika usiku..na kusema huyu mtu kazidiwa, na hali kama ilivyo hivyo, hawezi
hata kuongea, ndio tukampokea,..kwasababu hatuna taarifa za kuwa ni muhalifu au
kaumia, tukaanza matibabu yake,…ni hivyo kama unavyomuona, hatua tuliyoifanya
ni kumwekea hayo maji…’akasema huyo jamaa.
‘Ndugu zake tokea wamlete walishafika tena kumuona
..?’ akaulizwa
‘Hapa-na..ila ..ndio…alifika mzee mmoja …eeh,…, akiwa na haraka , anasema anasafiri,
alipokuja akamuangalia tu kwa mbali, halafu akaondoka…’akasema.
‘Huyo mzee yupoje…?’ akaulizwa na akamuelezea jinsi
alivyo.
‘Mzee mtupe…’akasema mpelelezi.
‘Je mlivyompima anaonekana ana tatizo gani..na hakuna
taarifa nyingine mliyoipata kuwa huyo mgonjwa alikuwa akitibiwa sehemu
nyingine..?’ akaulizwa.
‘Ha-hapana, ndio..walisema huyu mgonjwa alikuwa
akitibiwa sehemu nyingine, lakini akaruhusiwa, kwa ushauri kuwa akatibiwe
nyumbani, lakini hali yake ikazidi kuwa mbaya, ndio wakaona wamlete
hapa..’akasema.
‘Nyie mna taratibu gani za kupokea wagonjwa, …hamna
jinsi ya kuhakiki, kama mgonjwa ni mhalifu au la…?’ akaulizwa.
‘Sisi kazi yetu ni kupokea wagonjwa, ..mara nyingi
mtu kama kaumia, kapigwa, kagongwa na gari…hapo ndio tunaweza kumtilia mashaka,
lakini mgonjwa kama huyu, huwezi kufikiria lolote…’akasema
‘Hukusikia lolote kutoka kwa waliomleta..?’ akaulizwa
‘Zaidi nilichosikia ni wao kuongea, wengine wakisema,
huyu mgonjwa kutokana na maradhi yake…, hatakiwi kupigwa sindano…lakini baadae,
tulivyowaambia kwua ni muhimu awekewe maji, wakakubaliana na sisi, ndio
tukaanza taratibu za kumtibia, na hao jamaa zake wakaondoka, na kutuachia
tukiendelea na kazi,..na ni baada ya kulipa pesa…’akasema.
‘Sawa tuna imani hayo unayoongea ni ya kweli, kama
tutagundua kuna jambo unatuficha, ujue wewe utawajibika..’akaambiwa
‘Afande mimi sijui lolote zaidi ya hayo
niliyowaelezea..’akasema
Wapalelezi hao wakasogea pembeni wakashauriana jambo,
baadae wakarudi na kusema;
‘Kwahiyo nyie kwenye hospitali hii,mna imani kuwa
mtaweza kumuhudumia huyu mgonjwa, maana wenzenu walishindwa, wakataka
ahamishiwe Muhimbili…’akaambiwa
‘Hata sisi tulishafikia maamuzi hayo, kutokana nahali
yake tuliona hapa hapatamfaa, na ndio nilikuwa naandika uhamisho huo ili jamaa
zake wakifika niwaarifu kuwa huyu mgonjwa anastahiki kupelekwe hospitali za
juu, na ndio nyie mkatokea…hii ndio fomu yake ya kuhamishwa hapa kuelekea
hospitali ya juu…’akasema akionyesha karatasi iliyoandikiwa.
Wakati wakiendelea kuhojiana ….
Mimi nikamsogelea Dalali, nikawa namchunguza,
kiukweli alikuwa kama kalala, mapigo ya moyo yanafanya kazi …lakini…moyoni
nikawa namashaka na huyu mtu, sikuamini
kama anaumwa kiasi hicho, sijui kwanini nilihis hivyo.
Nikamuinamia Dalali na kumuongelesha sikioni…
.
‘Dalali…wakati umefika wa wewe kusema ukweli, najua
huenda umeingizwa kwenye majanga haya kwa tamaa tu, ila nakuonya, hali ilivyo
ni mbaya, kumeshatokea mauaji tayari, sasa je upo tayari kuwa muuaji,…ujanja
ujanja hautakusaidia
‘Mimi kama jamaa yako nakushauri ufunguke, kabla hali haijafikia kubaya, funguka
ujiokoe, mtetezi wako keshafariki, na …’nikajikuta nimesema hivyo..wakat huo
wapelelezi hao wanahojiana na hao wakuu wa hiyo hospitalini.
Nilikarejea hayo maneno na mara nikahis mkono wa
Dalali ukitikisika, nikasogea karibu, na ule mkono..nikaona ule mkono
umefumbata kitu..nikajaribu kuufungua ule mkono, nikaona karatasi ndogo,
nikaitoa mkononi mwake, .nikaikunjua,...kulikuwa na namba ya simu.
Nikawaangalia
wenzangu, niliwaona bado wanawahoji wahusika wa hiyo hospitali,..nikakariri ile
namba,..na kuiandika kwenye simu yangu, halafu nikakirejesha kile kikaratasi
mkononi mwa huyo mgonjwa, ..nikasogea pembeni nikaweka ile namba kwenye simu
yangu..
Nikajaribu kuipiga ile namba, na nikasikia, ikiita….
Baadae sana ikapokelewa, lakini mpokeaji hakusema
neno,akawa kimia, nikawa nahisi muhemo wake tu, kuashiria yupo hewani…nilipoona
haongezi, .. nikakata,..nikachukua ile namba nikajaribu kutuma pesa, ili kuona
mwenye jina ni nani..
Jina
likatokea…
‘M.AL.M.’
‘Kwanini inatokea kwa ufupi hivi…?’ nikajiuliza, ina
maana aliyejisajili huenda hakutumia kitambulisho rasmi..nikawa na hamu sana
kufahamu zaidi nikaituma hiyo namba kwa jamaa yangu mmoja anayefanya kazi
sehemu za simu, na akasema ataifanyia kazi.
‘Mtu wa jamii umegundua nini..?’ nikashtuka sauti ikiongea
nyuma yangu ..alikuwa ni mpelelezi, kwa haraka
nikasema;
‘Aaah, bado najaribu kuwasiliana na watu …na, sijui
kwanini, huyu mgonjwa ni kama kalewa madawa..’nikasema
‘Hapana hajalewa madawa,… sisi hapa hospitalini, tuna
utaratibu wetu, mgonjwa akija ni lazima tupate vipimo vyake kwanza…ila kwa hali
ya huyu mtu,..tuliona aanze na dripu hizo za maji za kumpa nguvu..huku
tukiendelea kuchukua vipimo vyake…’akasema.
‘Lakini si umesema, mumeona kuwatatizo lake lipo juu
ya uwezo wenu, sasa mumechukua vipimo vyake vya kazi gani..?’ akaulizwa
‘Tulianza na vipimo vyake vya kawaida,..tukaona
hakuna tatizo..swali likawa, ni kwaniniyupo hivyo, kwanini mwili
umepooza,…tukahis huenda kapatwa na kiharusi, sasa kiharusi chahitajia vipimo
vya ubongo…na…’kabla hajamaliza, mpelelezi akauliza swali jingine.
‘Kwahiyo tangu huyu mgonjwa aletwe hapa, hajaweza
kutoa sauti, au kuonyesha dalili ya kuongea..?’ akaulizwa.
‘Ni kama unavyomuona hivyo…anaweza akafumbua macho
kwa shida,…sijui ni tatizo gani kwakweli…’akasema .
Mpelelezi akasogelea pale kitandani akawa anamkagua,
akachunguza mkono wake, na hata kufumbua viganya vya mikono……cha ajabu sasa
hivi mikono imefunguka viganja vya mikono vipo wazi, lakini kile kikaratsi
hakipo tena.
Hapo nikaingia na mashaka..kile kikaratasi alichokuwa
nacho awali, maana nilikirejesha mkononi mwake, kimeenda wapi…nikasogea pale
kitandani nikawa nakagua,..hakipo..
‘Unatafuta nini…?’ akaniuliza mpelelezi.
‘Hapana..niliona kitu hapa, nikawa nakagua ni kitu
gani..’nikasema
‘Wewe mtu wa jamii wewe, nahisi kuna kitu umekigundua
lakini hutaki kutueleza, ila nakuonya, usije ukafanya mambo kivyako, hili
tatizo ni kubwa…na ni tatizo lipo mikononi mwetu…’akasema mpelelezi.
‘Najua afande..siwezi kufanya hivyo,..lazima niwe
makini sana..’nikasema.
Wakati namuamia hivyo, akili yangu ilikuwa mbali,..ina
maana Dalali anaigiza, huenda huyu mtu ni mnzima,..sivyo kama inavyoonekana…,
lakini kwanini afanye hivyo, na kwanini docta waseme yupo hivyo kama alivyo…ina
maana…sasa nifanyeje...nikawa najiuliza na mara yule mtu niliyempa hiyo namba
akapiga simu.
Nikasogea pembeni na kuanza kusikiliza
‘Hiyo namba ni ya….’akataja yale majina kwa kufupi
kama nilivyoona, ila akaongeza kusema;
‘Huyo mtu ana namba nyingi, kutokana na taarifa zetu…kwenye
namba hiyo kafupisha majina yake tu..sijui kwanini ilitokea hivyo,…’akasema.
‘Ni nani,..umeweza kufahamu hayo majina yake kwa
kirefu chake..?’ nikauliza
‘Ndio..’akasema na kunitajia, jina la mwisho ndio
likanifanya mwili usisimukwe.
‘MOTO…’nikasema kwa sauti, na kuanya mpelelezi ageuke
kuniangalia.
‘Atakuwa ni nani huyu..?’ nikauliza, jamaa akasema
hivyo ndivyo inavyoonekana kwenye namba nyingine…zaidi hajui.
Sasa hapo
nikawa najiuliza, je niwashikirishe hawa wapelelezi au nifuatilie mimi mwenyewe
kwanza, tatizo nikiwashirikisha hawa watu…, watakimbilia kunizuia, na kwa namna
hiyo sitaweza kupata taarifa kamili.
Baadae nikaamua, nifuatilie mimi mwenyewe kwanza..,
nikawa natafuta namna ya kutoka humu ndani, na kuachana na hawa watu kwa muda..maana
muda ni muhimu sana.
‘Sasa mtu wa jamii, unashauri nini, maana hatutaki
tena uje kuingilia hii kazi, , sasa hivi tumeshagundua kuwa kuna uhalifu, na
kazi inafanyika…usione sisi tupo hapa, kuna watu tumewatuma kila sehemu muhimu…,
hawa watu wote watafikishwa mahakamani…’akasema.
‘Sawa watafikishwa mahakamani, kwa kosa gani..?’
nikauliza.
‘Utakuja kulifahamu,..ila hadi hapo hatujaona
mahusiano yoyote na hilo deni,..unalolifuatilia wewe, au ile ajali…hapa ni kesi
ya udanganyifu,…na kujaribu kuua kwa sumu…je hayo yanaingiliana na kesi yako,
bado hilo tunalifanyia kazi…’wakasema.
‘Kama hamjaona mahusiano yoyote na hiyo kesi, basi
nahisi nyie bado mpo mbali na ukweli, mimi niwashauri jambo… huyu mtu..anayejifanya
mgonjwa, muwe na ulinzi naye
mkali,..mtakosa ushahidi wa maana sana mkimpoteza huyu mtu..’nikasema.
‘Atalindwa sasa kama muhalifu, na sijui kwanini
unafikiria hivyo, yeye zaidi ya kutoroka hospitalini, bado hahusikani na
…makosa haya mengine..lakini nimekuelewa, usijali, sasa kama kuna jambo
unalifahamu zaidi ni bora uliseme hapa hapa,…’akasema huyo mpelelezi.
‘Kwa hivi sasa hakuna, ..naaah, mimi naweza
kuondoka..?’ nikauliza
‘Unataka kwenda wapi..hatujamalizana na wewe bado, ni
lazima turudi ofisini tukakutane na wakili, kesi yako, ni vyema ieleweke..bila
ushaidi zoezi lile la mnada linaweza kuendelea tu....’akasema na aliposema
hivyo, nilihisi kama kuna namna ya mtikisiko kwenye kitanda cha Dalali,…na mara
simu yangu ikaita.
‘Ni nani..?’ nikauliza, na nikasikiliza kwa makini,
baadae nikasema.
‘Una uhakika ndio yeye…?’ nikauliza na kusikiliza kwa
muda, baadae nikageuka kumuangalia Dalali, wakati huo wapelelezi wanatembea
kutaka kutoka nje, walikuwa wakiongea na mkuu wa hiyo hospitali.
Unajua nilipata mshutuko, kama vile unaambiwa mtu
kafa, halafu unamuangalia unaona macho yake yanakuangalia..ndivyo hisia za
mshutuko nilioupata mimi…
Pale nilipogeuka na kumuangalia Dalali, nilijikuta
tunaangalia na Dalali,…na kwa haraka akayafunga macho yake..ilinibidi nicheke
kidogo.Sikutaka kumsogelea tena Dalali, akili yangu ilishaanza kujenga hisia
nyingine.
Nikasogea ukutani, nikawa nasoma maelezo ya hiyo hospitali, nikaangalia wamiliki
wa hiyo hospitalini na tarehe ilipofuinguliwa,..na pale nikaona majina matatu na kifupi chake,…yawezekana
hivyo, lakini jina la pili yake ndilo linakinifanya niwaze kuchukua hatua
nyingine..nikaibandua ile karatasi na kuwa nayo ..
Nikamsogelea mpelelezi, nikamwambia nataka kuongea
naye lakini nje ya hiyo hospitali,
‘Ila kwa hali ya Dalali ilivyo kunahitajika kuwepo
mlinzi wa kuaminika,sana’ nikasema.
‘Yupo,…wale wale vijana wangu nawaamini
sana..’akasema.
‘Sawa…tusije kupoteza ushahidi, nahisi humu ndani
..kuna ushahid mwingine muhimu sana..’nikasema.
‘Haya niambie..kuna nini ambacho umetaka tuongelee
huku nje,..?’ akaniuliza akiniangalia machoni.
‘Umeshafahamu anayemiliki hii hospitali…?’
nikamuuliza.
‘Wanasema ni jamaa mmoja ambaye kwa hivi sasa yupo
nchi za nje…’akasema.
‘Ni mtu mmoja tu, anayemiliki hii hospitali,…nahis
kam a wapo zaidi ya mmoja,..?’ nikauliza.
‘Wanasema huyo mtu mwingine alishafariki, na mwingine
kawekwa tu , ila mwenye mamlaka na hisa kubwa ni huyo ambaye yupo nchi za nje…’akasema.
‘Ni nani…?’ nikauliza na yeye akamtaja jina lake.
‘Umeamini hayo maneno, unawaamini hao waliokuambia
hivyo..?’ nikamuuliza
‘Kwanini nisiwaamini, au kwanini unauliza hivyo,
ongea kwa uawazi muda umekwisha..?’ akaniuliza
‘Nahisi hapa tunachezewa ujanja, na huu ujanja wao
nahis sasa umefikia mwisho…’nikasema.
‘Kwanini…?’ akaniuliza
Mimi nikatoa ile karatasi, na kumuonyesha,…
‘Ya nini hii…?’ akauliza ,naona alikuwa na haraka .
‘Angalia haya majina, ya wamiliki wa hii hospitali,…hawa
watu wameandika majina yao kwa kifupi..huyu hapa, labda ndiye huyo mumiliki
ambaye yupo nje….sina uhakika na kauli hiyo, ila hebu angalia hili jina la
pili…ni kifupi cha majina gani..?’ nikamuuliza
‘Siwezi kujua…’akasema
‘Nikatoa kadi moja ambayo niliwahi kuipata
mahali…nikamuonyesha, unaifahamu hii kampuni..?’ nikamuuliza
‘Mhh…ni kama naifahamu…’akasema
‘Ni nani mumiliki wake…?’ nikamuuliza
‘Sijui…’akasema
‘Hebu angalia hapa chini, kwenye hii kadi..uzuri
wametaja majina ya wamiliki wa hiyo kampuni, japokuwa wameweka harufu za majina
kwa ufupi… hii kampuni inamilikiwa na watu watatu….na uje uangalia haya majina
ya ufupisho kwenye hii karatasi hapa..’nikasema
‘Ndio yanafanana…’akasema
‘ Sasa angalia hizi namba zao za simu…zijaribu, kama
unawatumia pesa, ili upate majina yao halali..japokuwa huku kwenye kazi kuna namba
tofauti, na namba za hapa hospitalini…lakini wewe zijaribu hizi
namba..’nikasema.
‘Unataka kuhakiki kitu gani, tusipoteze muda
hapa…’akasema
‘ZIJARIBU KWANZA..’Nikasema kwa ukali, mpaka
akashtuka, na kuanza kuzijaribu, nikamuona uso ukibadilika kwa mshangao
‘Umegundua kitu..?’ nikamuuliza
‘Ina maana, …haiwezekani…’akasema
‘Sasa kama umegundua kitu, hakikisha unaongeza ulinzi
wa hali ya juu kwa huyo mgonjwa, hakikisha unawatuma vijana wako wamtafute kila
kona, huyo mumiliki mwingine ..’nikasema
‘Wamesema yupo nchi za nje,…’akasema
‘Unaamini hivyo…mimi siamini,…watume vijana wako
wamtafute, hiyo sasa ni kazi yako, tumalize hii kazi, na najua itakuwa ushahid
wetu wa kuimaliza hii kesi..’nikasema na jamaa kwa haraka akachukua simu yake
na kuanza kuwapigia watu wake.
Wakati analifanya hilo, … mara tukasikia kelele ndani
ya hiyo wodi, alipolazwa Dalali…
NB: Oh, kidole kinauma, njaa inauma…
WAZO
LA LEO: Ukipatwa na mitihani ya kimaisha,..iwe ni hali
ngumu, iwe ni maradhi, iwe ni kukosa kazi, …au jambo lolote la kukukwaza,
kimaisha…
Na wakati mwingine mitihani hiyo inaweza ikawa ni sababu y a watu wengine tu,
wanataka kukuharibia maisha yako. Ukijikuta upo katika hali hiyo usikimbilie
kulalamika, au kuchukua hatua ambazo huna uhakika nazo, ukatumia hasira.
Ukifanya hivyo, unaweza usifanikiwe.
Muhimu uwe na
subira,huku ukitenda yaliyo mema, na dai
haki zako katika utaratibu sahihi..mafanikio yake yanaweza kuwa makubwa zaidi
ya unavyofikiria, maana mola huwasaidia na kuwaongoza wale wenye kusubiri , na
wakawa wanatenda yaliyo mema.
No comments:
Post a Comment
Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com