Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, August 28, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-38


 Haraka tulifika hospitali ambayo mpelelezi alielekezwa na huyo mtu wake,..ambapo kwa maelezo aliyoyapata, kagundua wapi Dalali, kalazwa…lakini taarifa nyingi mitaani kwa hivi saa ni kuwa Dalali keshafariki, ndugu zake wanaficha ukweli.

‘Mtu wangu kanipigia simu kagundua wapi walipohifadhiwa Dalali…’akasema mpelelezi.

‘Kuhifadhiwa kwa vipi, …maiti yake au…?’ nikauliza.

‘Maiti!!!..hahaha, hapana bwana, usisikilize uvumi wa watu, hatujapata taarifa zozote kuwa Dalali kafariki…’akasema.

‘Watu wangu,..waliona watu wakiwa wamebeba mgonjwa, …wakimuingiza kwenye hiyo hospitali, na walipochunguza wakagundua kuwa ni Dalali...’akasema sasa tukiwa safarini kuelekea huko.

Tulifika hilo eneo, na kukutana na jamaa moja, akasema;

‘Kwenye hilo jengo hapo, hilo jengo ni la hospitali, japokuwa haifahamiki sana,..ila ni hospitali kubwa, ina wataalamu kweli…’akasema mtu wa mpelelezi, akituonyesha kwa kidole.

 Tukawa tunatembea kuelekea kwenye hilo jengo, tuliacha gari mbali kidogo, ili tusije kuleta namna ambayo huyo mtu wetu atatoroka, au kutoroshwa,….mimi nikawa nafuatilia nyuma.

‘Huko juu kuna ofisi za watendaji …’akasema huyo mtu wa mpelelezi…mapokezi ni hiyo hapo mbele..’akasema huyo mtu. Wapelelezi hawa wawili wakateta kidogo, halafu mmoja akiongozana na huyo jamaa aliyetuleta hapo, akaondoka na mpelelezi, sijui wanaenda wapi.

Mimi nikabakia na huyu mpelelezi mmoja, ambaye alisogea hadi sehemu ya mauliza, na mimi nikawa nyuma yake..

 ‘Nani mumiliki wa hii hospitali…?’ akauliza afande, akimuuliza mdada mmoja aliyekaa kwenye meza ya mapokezi.

‘Kwani nyie ni nani, na mnataka nini, nyie sio wagonjwa…?’ akauliza na mpelelezi akatoa kitambulisho chake na kujitambulisha. Yule mdada akataka kupiga simu, na huyo mpelelezi, akasema;

‘Sogea huku, uwe mbali na hiyo simu..’akaambiwa na huyo mdada akafanya hivyo akionyesha wasiwasi…

‘Haya niambie ni nani mwenye mamlaka na hii hospitali..?’ akaulizwa, na pale nikawa najiuliza yule mpelelezi mwingine kaenda wapi, maana nilikuwa na mashaka, hawa watu wakigundua kuwa kuna watu wa usalama, huenda wakakimbilia kumfica huyo mtu tunayemtafuta.
.
‘Hayupo, yupo nchi za nje…’akasema huyo dada

‘Kwahiyo ni nani mwenye mamlaka na hii hospitali kwa hivi sasa, bosi wenu  ni nani…?’ akauliza afande.

‘Ni…yupo ofisini kwake huko juu,…’akasema huyo mdada akiangalia huku na kule kwa mashaka.

‘Haya hebu niambie, kuna mgonjwa mwenye jina la ….alimaarufu Dalali…?’ akauliza

Yule mdada akachukua daftari, lenye orodha ya wagonjwa,akaanza kutafuta hilo jina,..baadae akasema;

‘Hakuna mwenye jina kama hilo…’akasema akiendeela kupekua orodha ya majina.

‘Una uhakika..?’ akaulizwa

‘Ndio angalia orodha ya wagonjwa waliofikishwa hapa …’akasema akitoa hicho kitabu cha wagonjwa walioingia hapo hospitalini, na wakati wanaendelea ndio akaja yule jamaa aliyeondoka na mpelelezi, akasema;

‘Afande yupo huko juu, afande ameshamuona, ndio yeye…’akasema huyo jamaa.

‘Sawa nakuja…’akasema mpelelezi, na akamwambia askari mwingine aliyevalia sare rasmi,

‘Hakikisha huyu mdada hashiki simu…’akasema mpelelezi,

‘Ofisi ya kiongozi wa hii hospitali yupo chumba gani..?’ akamuuliza huyo mdada, kabla hatujaachana naye na huyo mdada akaongea kwa sauti ya uwoga akitaka namba ya hicho chumba mbacho bosi wake yupo.

‘Usiwe na wasiwasi, hatua nia mbaya na bosi wako,…sis kuna mgonjwa tunamtafuta, unasikia, hutafukuzwa kazi…’akasema mpelelezi,…tukaelekea juu, kwa kupitia kwenye ngazi,..tulipofika sehemu ya juu, tukageuka kushoto na kulia, na mbele yetu tukaiona hiyo ofisi ya mkuu wa hiyo hospitali.

Tukafika na kugonga mlango.

‘Ingia…’sauti nzito ikasema kutoka ndani.

Akaanza kuingia mpelelezi na kujitambulisha, na baadae tukaingia sisi wengine, …jamaa sasa nikaona kijashi kikimtoka,.

‘Niwasaidie nini wakuu..’akasema, akijikaza kutokuonyesha wasiwasi.

‘Tunakuomba tuongozane na wewe kuna mgonjwa tunataka kuonana naye…’akaambiwa.

‘Kwa-kwani..kuna tatizo gani..?’ akauliza.

‘Wewe twende tu, utajua tatizo ni nini, tukionana naye…’akaambiwa na tukatoka hapo hadi kwenye chumba kingine, anayetuongoza ni yule askari kanzu

‘Chumba  cha wagonjwa maalumu…’ akasoma mpelelezi kwa nguvu.

‘Humu mnalaza watu wa namna gani..?’ akaulizwa

‘Wagonjwa waliozidiwa, au wagonjwa wanaohitajia huduma maalumu..’akasema

‘Orodha yake pia iko kwenye kile kitabu cha mapokezi..?’ akaulizwa

‘Wakati mwingine inasahaulika, maana wagonjwa kama hao, wakiletwa hapa, huwa wamezidiwa, kwahiyo kwa haraka  wanakimbizwa kupata matibabu ya haraka, ndio tunaita matibabu maalumu…, lakini baadae jina la huyo mgonjwa aliyewahishwa huku, ni lazima liingizwe kwenye kile kitabu.

‘Mgonjwa gani kaingizwa humu ambaye jina lake halijaandikiwa kule..?’ akaulizwa

‘Siwezi kujua, kwakweli,…maana mimi ni mkuu wa hii hospitali, naletewa taarifa muhimu tu..ila orodha hizo zinaletwa jioni, au nikihitajia, sio lazima kila siku nizipitie…’akasema.

Basi wapelelezi hao wakaingia humo ndani, na tukamkuta yule mpelelezi mwingine yupo anaongea na docta mmoja,..na pembeni kabisa kwenye kitanda, tukamuona mgonjwa kalazwa…akiwa kawekewa chupa za kuongeza maji..

‘Yule pale ni nani..?’ akaulizwa

‘Siwezi kujua mpaka nisome kadi yake…’akasema na wakasogea hadi pale alipolazwa mgonjwa, na jina likabainika, jina la kama bandia..ila kwa herufu za mwanzo kwa kifupi.

‘Una uhakika hujui lolote kuhusu huyu mgonjwa..?’ akaulizwa.

‘Ki-kiukweli mimi sijui…kama nilivyosema mimi ni msimamizi, meneja wa hii hospitali, majukumu ya wagonjwa, yanafanywa na wenzangu walio chini yangu…’akasema

‘Ni nani sasa anayhusika hapa..?’ akauliza afande

‘Ni huyo hapo…’akasema akimuonyeshea docta mmoja aliyekuwa akiongea na yule mpelelezi mwingine.

Wakateta, kidogo wakuu hawa wawili,…na baadae huyu mpelelezi tuliyekuja naye akaendelea kuhoji….

‘Tuambie kuhusu huyu mgonjwa aliletwa na nani hapa.?’ afande akamgeukia huyo jamaa mwingine.

‘Kama nilivyomuambia huyu mwenzako,..kuna jamaa walifika usiku..na kusema huyu mtu kazidiwa, na hali kama ilivyo hivyo, hawezi hata kuongea, ndio tukampokea,..kwasababu hatuna taarifa za kuwa ni muhalifu au kaumia, tukaanza matibabu yake,…ni hivyo kama unavyomuona, hatua tuliyoifanya ni kumwekea hayo maji…’akasema huyo jamaa.

‘Ndugu zake tokea wamlete walishafika tena kumuona ..?’ akaulizwa

‘Hapa-na..ila ..ndio…alifika mzee mmoja  …eeh,…, akiwa na haraka , anasema anasafiri, alipokuja akamuangalia tu kwa mbali, halafu akaondoka…’akasema.

‘Huyo mzee yupoje…?’ akaulizwa na akamuelezea jinsi alivyo.

‘Mzee mtupe…’akasema mpelelezi.

‘Je mlivyompima anaonekana ana tatizo gani..na hakuna taarifa nyingine mliyoipata kuwa huyo mgonjwa alikuwa akitibiwa sehemu nyingine..?’ akaulizwa.

‘Ha-hapana, ndio..walisema huyu mgonjwa alikuwa akitibiwa sehemu nyingine, lakini akaruhusiwa, kwa ushauri kuwa akatibiwe nyumbani, lakini hali yake ikazidi kuwa mbaya, ndio wakaona wamlete hapa..’akasema.

‘Nyie mna taratibu gani za kupokea wagonjwa, …hamna jinsi ya kuhakiki, kama mgonjwa ni mhalifu au la…?’ akaulizwa.

‘Sisi kazi yetu ni kupokea wagonjwa, ..mara nyingi mtu kama kaumia, kapigwa, kagongwa na gari…hapo ndio tunaweza kumtilia mashaka, lakini mgonjwa kama huyu, huwezi kufikiria lolote…’akasema

‘Hukusikia lolote kutoka kwa waliomleta..?’ akaulizwa

‘Zaidi nilichosikia ni wao kuongea, wengine wakisema, huyu mgonjwa kutokana na maradhi yake…, hatakiwi kupigwa sindano…lakini baadae, tulivyowaambia kwua ni muhimu awekewe maji, wakakubaliana na sisi, ndio tukaanza taratibu za kumtibia, na hao jamaa zake wakaondoka, na kutuachia tukiendelea na kazi,..na ni baada ya kulipa pesa…’akasema.

‘Sawa tuna imani hayo unayoongea ni ya kweli, kama tutagundua kuna jambo unatuficha, ujue wewe utawajibika..’akaambiwa

‘Afande mimi sijui lolote zaidi ya hayo niliyowaelezea..’akasema

Wapalelezi hao wakasogea pembeni wakashauriana jambo, baadae wakarudi na kusema;

‘Kwahiyo nyie kwenye hospitali hii,mna imani kuwa mtaweza kumuhudumia huyu mgonjwa, maana wenzenu walishindwa, wakataka ahamishiwe Muhimbili…’akaambiwa

‘Hata sisi tulishafikia maamuzi hayo, kutokana nahali yake tuliona hapa hapatamfaa, na ndio nilikuwa naandika uhamisho huo ili jamaa zake wakifika niwaarifu kuwa huyu mgonjwa anastahiki kupelekwe hospitali za juu, na ndio nyie mkatokea…hii ndio fomu yake ya kuhamishwa hapa kuelekea hospitali ya juu…’akasema akionyesha karatasi iliyoandikiwa.

Wakati wakiendelea kuhojiana ….

Mimi nikamsogelea Dalali, nikawa namchunguza, kiukweli alikuwa kama kalala, mapigo ya moyo yanafanya kazi …lakini…moyoni nikawa namashaka na  huyu mtu, sikuamini kama anaumwa kiasi hicho, sijui kwanini nilihis hivyo.

Nikamuinamia Dalali na kumuongelesha sikioni…
.
‘Dalali…wakati umefika wa wewe kusema ukweli, najua huenda umeingizwa kwenye majanga haya kwa tamaa tu, ila nakuonya, hali ilivyo ni mbaya, kumeshatokea mauaji tayari, sasa je upo tayari kuwa muuaji,…ujanja ujanja hautakusaidia

‘Mimi kama jamaa yako nakushauri  ufunguke, kabla hali haijafikia kubaya, funguka ujiokoe, mtetezi wako keshafariki, na …’nikajikuta nimesema hivyo..wakat huo wapelelezi hao wanahojiana na hao wakuu wa hiyo hospitalini.

Nilikarejea hayo maneno na mara nikahis mkono wa Dalali ukitikisika, nikasogea karibu, na ule mkono..nikaona ule mkono umefumbata kitu..nikajaribu kuufungua ule mkono, nikaona karatasi ndogo, nikaitoa mkononi mwake, .nikaikunjua,...kulikuwa na namba ya simu.

 Nikawaangalia wenzangu, niliwaona bado wanawahoji wahusika wa hiyo hospitali,..nikakariri ile namba,..na kuiandika kwenye simu yangu, halafu nikakirejesha kile kikaratasi mkononi mwa huyo mgonjwa, ..nikasogea pembeni nikaweka ile namba kwenye simu yangu..

Nikajaribu kuipiga ile namba, na nikasikia, ikiita….

Baadae sana ikapokelewa, lakini mpokeaji hakusema neno,akawa kimia, nikawa nahisi muhemo wake tu, kuashiria yupo hewani…nilipoona haongezi, .. nikakata,..nikachukua ile namba nikajaribu kutuma pesa, ili kuona mwenye jina ni nani..

 Jina likatokea…

‘M.AL.M.’

‘Kwanini inatokea kwa ufupi hivi…?’ nikajiuliza, ina maana aliyejisajili huenda hakutumia kitambulisho rasmi..nikawa na hamu sana kufahamu zaidi nikaituma hiyo namba kwa jamaa yangu mmoja anayefanya kazi sehemu za simu, na akasema ataifanyia kazi.

‘Mtu wa jamii umegundua nini..?’ nikashtuka sauti ikiongea nyuma yangu ..alikuwa ni mpelelezi, kwa haraka  nikasema;

‘Aaah, bado najaribu kuwasiliana na watu …na, sijui kwanini, huyu mgonjwa ni kama kalewa madawa..’nikasema
‘Hapana hajalewa madawa,… sisi hapa hospitalini, tuna utaratibu wetu, mgonjwa akija ni lazima tupate vipimo vyake kwanza…ila kwa hali ya huyu mtu,..tuliona aanze na dripu hizo za maji za kumpa nguvu..huku tukiendelea kuchukua vipimo vyake…’akasema.

‘Lakini si umesema, mumeona kuwatatizo lake lipo juu ya uwezo wenu, sasa mumechukua vipimo vyake vya kazi gani..?’ akaulizwa

‘Tulianza na vipimo vyake vya kawaida,..tukaona hakuna tatizo..swali likawa, ni kwaniniyupo hivyo, kwanini mwili umepooza,…tukahis huenda kapatwa na kiharusi, sasa kiharusi chahitajia vipimo vya ubongo…na…’kabla hajamaliza, mpelelezi akauliza swali jingine.

‘Kwahiyo tangu huyu mgonjwa aletwe hapa, hajaweza kutoa sauti, au kuonyesha dalili ya kuongea..?’ akaulizwa.

‘Ni kama unavyomuona hivyo…anaweza akafumbua macho kwa shida,…sijui ni tatizo gani kwakweli…’akasema .

Mpelelezi akasogelea pale kitandani akawa anamkagua, akachunguza mkono wake, na hata kufumbua viganya vya mikono……cha ajabu sasa hivi mikono imefunguka viganja vya mikono vipo wazi, lakini kile kikaratsi hakipo tena.

Hapo nikaingia na mashaka..kile kikaratasi alichokuwa nacho awali, maana nilikirejesha mkononi mwake, kimeenda wapi…nikasogea pale kitandani nikawa nakagua,..hakipo..

‘Unatafuta nini…?’ akaniuliza mpelelezi.

‘Hapana..niliona kitu hapa, nikawa nakagua ni kitu gani..’nikasema
‘Wewe mtu wa jamii wewe, nahisi kuna kitu umekigundua lakini hutaki kutueleza, ila nakuonya, usije ukafanya mambo kivyako, hili tatizo ni kubwa…na ni tatizo lipo mikononi mwetu…’akasema mpelelezi.

‘Najua afande..siwezi kufanya hivyo,..lazima niwe makini sana..’nikasema.

Wakati namuamia hivyo, akili yangu ilikuwa mbali,..ina maana Dalali anaigiza, huenda huyu mtu ni mnzima,..sivyo kama inavyoonekana…, lakini kwanini afanye hivyo, na kwanini docta waseme yupo hivyo kama alivyo…ina maana…sasa nifanyeje...nikawa najiuliza na mara yule mtu niliyempa hiyo namba akapiga simu.

Nikasogea pembeni na kuanza kusikiliza

‘Hiyo namba ni ya….’akataja yale majina kwa kufupi kama nilivyoona, ila akaongeza kusema;

‘Huyo mtu ana namba nyingi, kutokana na taarifa zetu…kwenye namba hiyo kafupisha majina yake tu..sijui kwanini ilitokea hivyo,…’akasema.

‘Ni nani,..umeweza kufahamu hayo majina yake kwa kirefu chake..?’ nikauliza

‘Ndio..’akasema na kunitajia, jina la mwisho ndio likanifanya mwili usisimukwe.

‘MOTO…’nikasema kwa sauti, na kuanya mpelelezi ageuke kuniangalia.

‘Atakuwa ni nani huyu..?’ nikauliza, jamaa akasema hivyo ndivyo inavyoonekana kwenye namba nyingine…zaidi hajui.

 Sasa hapo nikawa najiuliza, je niwashikirishe hawa wapelelezi au nifuatilie mimi mwenyewe kwanza, tatizo nikiwashirikisha hawa watu…, watakimbilia kunizuia, na kwa namna hiyo sitaweza kupata taarifa kamili.

Baadae nikaamua, nifuatilie mimi mwenyewe kwanza.., nikawa natafuta namna ya kutoka humu ndani, na kuachana na hawa watu kwa muda..maana muda ni muhimu sana.

‘Sasa mtu wa jamii, unashauri nini, maana hatutaki tena uje kuingilia hii kazi, , sasa hivi tumeshagundua kuwa kuna uhalifu, na kazi inafanyika…usione sisi tupo hapa, kuna watu tumewatuma kila sehemu muhimu…, hawa watu wote watafikishwa mahakamani…’akasema.

‘Sawa watafikishwa mahakamani, kwa kosa gani..?’ nikauliza.

‘Utakuja kulifahamu,..ila hadi hapo hatujaona mahusiano yoyote na hilo deni,..unalolifuatilia wewe, au ile ajali…hapa ni kesi ya udanganyifu,…na kujaribu kuua kwa sumu…je hayo yanaingiliana na kesi yako, bado hilo tunalifanyia kazi…’wakasema.

‘Kama hamjaona mahusiano yoyote na hiyo kesi, basi nahisi nyie bado mpo mbali na ukweli, mimi niwashauri jambo… huyu mtu..anayejifanya mgonjwa,  muwe na ulinzi naye mkali,..mtakosa ushahidi wa maana sana mkimpoteza huyu mtu..’nikasema.

‘Atalindwa sasa kama muhalifu, na sijui kwanini unafikiria hivyo, yeye zaidi ya kutoroka hospitalini, bado hahusikani na …makosa haya mengine..lakini nimekuelewa, usijali, sasa kama kuna jambo unalifahamu zaidi ni bora uliseme hapa hapa,…’akasema huyo mpelelezi.

‘Kwa hivi sasa hakuna, ..naaah, mimi naweza kuondoka..?’ nikauliza


‘Unataka kwenda wapi..hatujamalizana na wewe bado, ni lazima turudi ofisini tukakutane na wakili, kesi yako, ni vyema ieleweke..bila ushaidi zoezi lile la mnada linaweza kuendelea tu....’akasema na aliposema hivyo, nilihisi kama kuna namna ya mtikisiko kwenye kitanda cha Dalali,…na mara simu yangu ikaita.

‘Ni nani..?’ nikauliza, na nikasikiliza kwa makini, baadae nikasema.

‘Una uhakika ndio yeye…?’ nikauliza na kusikiliza kwa muda, baadae nikageuka kumuangalia Dalali, wakati huo wapelelezi wanatembea kutaka kutoka nje, walikuwa wakiongea na mkuu wa hiyo hospitali.

Unajua nilipata mshutuko, kama vile unaambiwa mtu kafa, halafu unamuangalia unaona macho yake yanakuangalia..ndivyo hisia za mshutuko nilioupata mimi…

Pale nilipogeuka na kumuangalia Dalali, nilijikuta tunaangalia na Dalali,…na kwa haraka akayafunga macho yake..ilinibidi nicheke kidogo.Sikutaka kumsogelea tena Dalali, akili yangu ilishaanza kujenga hisia nyingine.

Nikasogea ukutani, nikawa nasoma  maelezo ya hiyo hospitali, nikaangalia wamiliki wa hiyo hospitalini na tarehe ilipofuinguliwa,..na pale nikaona  majina matatu na kifupi chake,…yawezekana hivyo, lakini jina la pili yake ndilo linakinifanya niwaze kuchukua hatua nyingine..nikaibandua ile karatasi na kuwa nayo ..

Nikamsogelea mpelelezi, nikamwambia nataka kuongea naye lakini nje ya hiyo hospitali,

‘Ila kwa hali ya Dalali ilivyo kunahitajika kuwepo mlinzi wa kuaminika,sana’ nikasema.

‘Yupo,…wale wale vijana wangu nawaamini sana..’akasema.

‘Sawa…tusije kupoteza ushahidi, nahisi humu ndani ..kuna ushahid mwingine muhimu sana..’nikasema.

‘Haya niambie..kuna nini ambacho umetaka tuongelee huku nje,..?’ akaniuliza akiniangalia machoni.

‘Umeshafahamu anayemiliki hii hospitali…?’ nikamuuliza.

‘Wanasema ni jamaa mmoja ambaye kwa hivi sasa yupo nchi za nje…’akasema.

‘Ni mtu mmoja tu, anayemiliki hii hospitali,…nahis kam a wapo zaidi ya mmoja,..?’ nikauliza.

‘Wanasema huyo mtu mwingine alishafariki, na mwingine kawekwa tu , ila mwenye mamlaka na hisa kubwa ni huyo ambaye yupo nchi za nje…’akasema.

‘Ni nani…?’ nikauliza na yeye akamtaja jina lake.

‘Umeamini hayo maneno, unawaamini hao waliokuambia hivyo..?’ nikamuuliza

‘Kwanini nisiwaamini, au kwanini unauliza hivyo, ongea kwa uawazi muda umekwisha..?’ akaniuliza

‘Nahisi hapa tunachezewa ujanja, na huu ujanja wao nahis sasa umefikia mwisho…’nikasema.

‘Kwanini…?’ akaniuliza

Mimi nikatoa ile karatasi, na kumuonyesha,…

‘Ya nini hii…?’ akauliza ,naona alikuwa na haraka .

‘Angalia haya majina, ya wamiliki wa hii hospitali,…hawa watu wameandika majina yao kwa kifupi..huyu hapa, labda ndiye huyo mumiliki ambaye yupo nje….sina uhakika na kauli hiyo, ila hebu angalia hili jina la pili…ni kifupi cha majina gani..?’ nikamuuliza

‘Siwezi kujua…’akasema

‘Nikatoa kadi moja ambayo niliwahi kuipata mahali…nikamuonyesha, unaifahamu hii kampuni..?’ nikamuuliza

‘Mhh…ni kama naifahamu…’akasema

‘Ni nani mumiliki wake…?’ nikamuuliza

‘Sijui…’akasema

‘Hebu angalia hapa chini, kwenye hii kadi..uzuri wametaja majina ya wamiliki wa hiyo kampuni, japokuwa wameweka harufu za majina kwa ufupi… hii kampuni inamilikiwa na watu watatu….na uje uangalia haya majina ya ufupisho kwenye hii karatasi hapa..’nikasema

‘Ndio yanafanana…’akasema

‘ Sasa angalia hizi namba zao za simu…zijaribu, kama unawatumia pesa, ili upate majina yao halali..japokuwa huku kwenye kazi kuna namba tofauti, na namba za hapa hospitalini…lakini wewe zijaribu hizi namba..’nikasema.

‘Unataka kuhakiki kitu gani, tusipoteze muda hapa…’akasema

‘ZIJARIBU KWANZA..’Nikasema kwa ukali, mpaka akashtuka, na kuanza kuzijaribu, nikamuona uso ukibadilika kwa mshangao

‘Umegundua kitu..?’ nikamuuliza

‘Ina maana, …haiwezekani…’akasema

‘Sasa kama umegundua kitu, hakikisha unaongeza ulinzi wa hali ya juu kwa huyo mgonjwa, hakikisha unawatuma vijana wako wamtafute kila kona, huyo mumiliki mwingine ..’nikasema

‘Wamesema yupo nchi za nje,…’akasema

‘Unaamini hivyo…mimi siamini,…watume vijana wako wamtafute, hiyo sasa ni kazi yako, tumalize hii kazi, na najua itakuwa ushahid wetu wa kuimaliza hii kesi..’nikasema na jamaa kwa haraka akachukua simu yake na kuanza kuwapigia watu wake.

Wakati analifanya hilo, … mara tukasikia kelele ndani ya hiyo wodi, alipolazwa Dalali…

NB: Oh, kidole kinauma, njaa inauma…

WAZO LA LEO: Ukipatwa na mitihani ya kimaisha,..iwe ni hali ngumu, iwe ni maradhi, iwe ni kukosa kazi, …au jambo lolote la kukukwaza, kimaisha…

Na wakati mwingine mitihani hiyo  inaweza ikawa ni sababu y a watu wengine tu, wanataka kukuharibia maisha yako. Ukijikuta upo katika hali hiyo usikimbilie kulalamika, au kuchukua hatua ambazo huna uhakika nazo, ukatumia hasira. Ukifanya hivyo, unaweza usifanikiwe.


 Muhimu uwe na subira,huku  ukitenda yaliyo mema, na dai haki zako katika utaratibu sahihi..mafanikio yake yanaweza kuwa makubwa zaidi ya unavyofikiria, maana mola huwasaidia na kuwaongoza wale wenye kusubiri , na wakawa wanatenda yaliyo mema. 

Ni mimi: emu-three

No comments :