Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, September 3, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-41



Ilikuwa natembea, nawahi sehemu, sijui nilikuwa naelekea wapi,

Lakini yaonekana…kuna mvua, na jua kwa wakati mmoja,… 

Lakini nina haraka sana, sijali mvua hiyo au jua hilo…niliwapita watu na wengine wakikimbilia sehemu ili wasilowane..kwahiyo tukawa tunapishana, bila hata kusalimiana, wengine nawafahamu, lakini hata wao hawakuwa na habari na mimi, kila mtu anatafuta usitiri wake asilowane, lakini cha ajabu pia jua linawaka.

Na mara nikaguswa na wimbo…

‘Matatizooo. Matatizo, sijui yatakwisha lini…mimi mama mjane, na watoto wangu yatima…matatizo , matatizo sijui yatakwisha lini…kila anionaye, hanithamini…watu wananipita kama hawanijui…matatizo, matatizo sijui yatakwisha lini…’ilikuwa ni wimbo, wenye sauti ya huzuni. Wimbo ule, ...ukanifanya nisimame.

Nikageuka kushoto hakuna mtu, nikageuka kulia..namuona huyo mama, kakaa huku kajikunyata, kalowana, na watoto wake pia,..lakini jua lipo , nalo ni kali kweli, watoto wanatetemeka baridi..jua,...kuna jua lakini haliwasaidii kitu…watoto wanalia…hakuna anayewajili.

‘Mama njaa…mama, tunalowana…’ilikuwa kilio cha watoto, na mama anawaimbia wanawe…

‘Wewe mama toka hapo , mvua hiyo, itakupatia maradhi, na hao watoto wanashikwa na homa..’nikasema na huyo mama akageuka, ..na kuniangalia, huku anatoa  machozi, akasema. Machozi yana rangi, kutofautisha na maji ya mvua, ambayo ilikuwa kitengeneza mifereji usoni mwa huyo mama.

‘Wewe waongelea mvua…hulioni na hili jua, vyote hivyo ni vyetu..ni nani atatusitiri sisi, kwenye mvua, na kwenye jua…ni nani atatusitiri kwenye njaa na shida…hakuna, nyie mna haraka zenu, hamuwakumbuki watu kama sisi, hata kinga ya mvua na jua, hatuna tena…’akasema na kuangalia watu wanavyokimbizana kutafuta sehemu ya kujikinga na mvua.

‘Lakini huwaoni hao watu…wao wanahangaika kukimbilie kwenye kinga ya mvua…na wewe fanya hivyo…’nikasema

Na yeye, kama kunionyesha, akainua mikono yake, hauinuki, kumbe kafungwa na  mnyororo, nikaona ajabu, kwanini afanyiwe hivyo..

‘Ni nani kakufunga hivyo..?’ nikauliza

‘Ni walimwengu…ni wanajamii…’akasema

'Oh..wanajamii, haiwezekani...'nikasema sasa najitutumua kumsogelea, ..kumbuka awali nilikuwa natembea kwa haraka...ajabu sasa nataka kwenda kwake, siwezi...miguu minzito, na sio miguu...mchanga, utelezi..mvua...

‘Oh..ngoja nije nikufungue…’nikasema nikijaribu kumsogelea pale walipo, lakini mchanga, unanifanya nitembee kwa shida, maji…na mara...

Kitu kikali kikinigonga kichwani kwa nyuma, ..na maumivu yake yakanifanya nisiweze kuhimili nikadondoka…nikaanza kuona giza, huku yule mama akiendelea kuomba msaada..sasa akisema;

‘Amuka…ukilala wewe ni nani atatusaidia, ukipotea wewe ni nani atatusaidia,…kwanini nakutana na mitihani hii jamani…amuka , muka jamani...’sauti hiyo ilinifanya niingiwe na nguvu, nikajitutumua, kichwa kinauma…maumivu makali..na mara, nikahisi mwanga mkali ukipenya machoni..

Nikazindukana..lakini huku nalia...

‘Kichwa kichwa…’

‘Docta, docta, kaamuka, analalamika kichwa..'nikasikia sauti kwa mbali.

Ilikuwa suti iliyoashiria kuwa nipo mahali gani, lakini akili yangu bado ilikuwa haijawa sawa, sijitambui, …naona watu marue rue, na hali hiyo ikaendelea na baadae ikawa sawa, nikawa naweza kuona vyema.

‘Nipo wapi, ooh, kichwa…’nikasema

***************

Nilizindukana na kujikuta nipo hospitalini, kichwa kimewekwa bandeji kwa nyuma, niliangalia huku na kule, sikumuona mtu ..baadae akaingia mama mjane…akiwa kaongozana na docta.

‘Oh, pole..unajisikiaje kaka..?’ akaniuliza na docta akawa ananiweka sawa, akawa ananikagua kichwani.

‘Kwanini hutulii, umeona umejitonesha sasa…’akasema docta.

‘Kichwa kinauma…’nikasema

‘Kwasababu umejitonesha, tulia hivi hivi…’akasema akiniweka sawa.

‘Ni kosa langu docta, nilipitiwa na usingizi…’akasema huyo mama.

‘Lakini ulikuwa unaimba…’nikasema

‘Umenisikia…?’ akauliza kwa mshangao

‘Nilikuwa naota…’ nikasema

‘Lakini niliimba muda, halafu nikapitiwa na usingizi, nilipoamuka nikakuta unachezesha kichwa,…unalalamika, ..kichwa kichwa…’akasema.

‘Oh…’nikaguna hivyo na docta akawa ameniwekea dripu ya maji,..na kusema.

‘Sasa tulia…ukitaka upone utulie hivyo hivyo..’akasema docta na kundoka, nikabakia mimi na huyo mama mjane..

‘Watoto wapo wapi…?’ nikamuuliza.

‘Watoto…!!!, watoto wapo nyumbani…vipi kwani…?’ akaniuliza sasa akionyesha uso wa kushangaa…na kutulia kimia, nikiwaza hiyo ndoto.

‘Kwani unajisikiaje sasa…?’ akaniuliza

‘Sasa kidogo, sijambo, ila kichwa bado kina maumivu kwa mbali…nimefikaje hapa..?’ nikauliza.

‘Nasikia waliokuleta hapa hospitalini ni …askari…’akasema.

‘Askari, askari gani hao,…mi-mi nakumbuka, eeh, kichwa kinauma, kwa nyuma,..ndio..nilipigwa na kitu kigumu kichwani, si ndio hivyo….nikapoteza fahamu, si ndio hivyo....’nikasema nikitaka uhakika.

‘Nlivyoambiwa ni kuwa, hao maaskari walikuokoa, ukitaka kuuliwa na mtu..lakini hawajasema ni mtu gani…’akasema

‘Mhh..ni huyo chizi nini..’nikasema.

‘Chizi, chizi gani…?’ akauliza

‘Mhh, hata simjui…’nikasema

‘Maana, kuna mtu namfahamu wanamuita hivyo. Chizi, lakini ni msafi kweli, ..uchzi wake ni waajabu sana,…’akasema

‘Ni nani huyo..?’ nikamuuliza

‘Mhh, niliwahi kumuona mara moja,..huwezi amini kuwa kachanganyikiwa, ila wanasema kikicharuka, inabidi watu wakimbizane, maana anaweza hata kuua, analalamika, ‘moto, moto..’ nikama anaungua vile…’akasema

‘Oh…moto…?’ nikauliza hivyo.

‘Ndio , kwani unamfahamu…?’ akauliza

‘Kama ndio huyo,..basi ndiye nilikuwa namtafuta, ..’nikasema.

‘Wanini, kujitafutia matatizo, unaona alivyokufanya…’akasema

‘Unajua…huyo ndiye anaweza kuwa ni msaada wa kesi yetu…’nikasema

‘Umechanganyikiwa, mtu ni kichaa, ..atasikilizwa na nani, na hata hivyo, yeye atautsaidiaje…?’ akauliza mama mjane

‘Kwanza niambie, huko baharini, ulikwenda kufanya nini huko, ndio kumtafuta huyo chizi…..?’ akaniuliza mama mjane.

‘Oh…hata sijui,…itakuwaje,..’nikasema hivyo.

‘Jamani mimi nilishakuambia, haya yote yanayotokea, yanatokea kwa mapenzi ya mungu,kama kapanga iwe hivyo, itakuwa hivyo, na yeye akitaka, yote yatakwisha, sio kwa ujanja wetu, sio…sasa mpaka wanataka kukua,,…’akasema mama mjane.

‘Haya...vipi wanasemaje kuhusu mnada..imefikia wapi..?’ nikauliza bila kumjali maneno yake.

‘Mhh…sijasikia lolote kwa leo….jana ndio ilikuwa wafike, lakini hawakutokea, japokuwa watu walifika kwa ajili ya huo mnada..baadae nikasikia, wameahirisha , sasa sijui hadi lini, labda leo mimi sijui, nimeshakata tamaa..’akasema

‘Mhh…usikate tamaa..nataka nionane na huyo mtu tu…’nikasema

‘Jana ilibidi niache kila kitu, niliposikia kuwa umeletwa huku hospitalini, …nikaja na kukuta kwenye hiyo hali..kiukweli nililia sana, hata waliposema niondoke, sikukubali, nikasema nitakaa hapa hapa,…sasa nikapitiwa na usingizi,..unisamehe tu…’akasema.

‘Ahsante kwa kunijali, dada yangu…’nikasema

‘Kwani mliponipigia simu, …ukaniuliza ..nikakuelezea nilivyota, majinamizi, mlikuwa mnafanya nini,…?’ akaniuliza

‘Mhh…sijui…kwa mara ya mwisho niliongea na mpelelezi, akasema anafuatilia kuhusu kuzuia huo mnada usifanyike, lakini walikosa ushahidi wa kuweka pingamizi,..ndio nikawa nafuatilia, nipata huo ushahidi,…sasa siwezi kuwa na uhakika,..nahisi kuna kitu kimetokea, vipi watoto lakini…?’ nikauliza

‘Hawajambo, zaidi ya…hilo tukio..hakuna kibaya…’akasema alionekana kama ananificha kitu.

‘Docta yupo wapi, ,maana kuna jambo muhimu ni lazima nilifuatilie,..kabla hawaja….mhh...kichwa jamani, hakitaka nifikiria jambo, sasa kinaanza kuuma tena.., sijui walinipiga kwa nyundo,..lakini ni lazima nionane na huyo mtu…’nikasema.
Nikawa nataka kama kujiiunua

‘Unataka kwenda wapi, na hali hiyo…’ sauti ikatokea mlangoni

***********

Ilikuwa ni sauti ya mpelelezi. Nilitaka kujiinua nimuangalia lakini kwa jinis nilivyolala, nikashindwa.

‘Mtu wa jamii…hahaha, umeionja joto ya jiwe eeh…, nilikuambia hizi kazi zina wenyewe, ukajifanya na wewe mpelelezi…hahaha, pole sana…, je nisingelifika kwa wakati muafaka, unafikiri ingelikuwaje…’akasema.

‘Ulifika tu, kwa mapenzi ya mungu, wala sio kwa ujanja wako afande..hata hivyo nashukuru sana kama ni wewe ulini-okoa, ilikuwaje kwani, na huyo jamaa aliyefanya hivi ni nani, alitaka kuniua, au…?’ nikauliza.

‘Hahaha, haya bwana, ni mapenzi ya mungu kweli…maana huyo jamaa alidhamiria kukua kweli…nilimuwahi kwa risasi,…’akasema.

‘Ina maana umemuua…oh , sasa si umehribu ushahidi wote..?’ nikauliza.

‘Hapana, sikutaka kumuua, nilimjeruhi  mkononi, akiwa tayari anataka kukutwanga nyundo ya pili kichwani..nisingelifanya hivyo, sasa hivi ungelitw jina jingine…’akasema.

‘Oh…ina maana kweli alikuwa na lengo la kuniua..ni nani huyo lakini..?’ nikamuliza.

 ‘Wewe ulikuwa unakwenda kuonana na nani kwani..?’ akaniuliza swali bila kunijibu swali langu. Na ili kuwaza kidogo, kichwa kikaanza kuniuma.

‘Mhh…kichwa kinauma sana afande…lakini lazima nitoke,..nataka nitoke , docta yupo wapi kwani, muda unakwisha au, unakumbuka wanataka kuufanya huo mnada…’nikasema nikijaribu kujiinua.

‘Unataka kwenda wapi wewe…sikiliza, huyo mtu uliyekuwa ukimfuata, keshapatikana kama ndio yeye unayetaka kwenda kuonana naye,…’akasema na mimi hapo nikabakia kimia.

‘Tumempata …’akasema kwa msisitizo bila kumtaja huyo mtu.

‘Ndio nani huyo, maana sikumbuki kukuambia ni nani nilikuwa namfuata..?’ nikamuuliza.

‘Si ndiye huyo uliyekuwa ukimfuata,…ameniambia yule mlinzi wa pale hospitalini…na na ndio nikajua umeelekea wapi…’akasema.

‘Kwani ilitokeaje hadi huyo mlinzi akakuambia, maana nijuavyo, wao hawakutaka kuliongelea hilo,..?’ nikamuuliza

‘Kuna mambo niligundua wakati nimekuacha pale uondoke, nilitaka kuwafahamu watu wa zamani wa humo…nikagundua kuwa mmojawapo ni huyo mlinzi na yule mdada wa mapokezi…nilipomuuliza mlinzi, akasema nimemuuliza maswali kama uliyomuuliza wewe…na ndio akaniambia wewe umemfuatilia huyo ‘chizi’ na mtu huyo hafuatiliwi ovyo.

‘Oh…lakini kitendo cha kumuhoji,..mpaka kufikia hapo, ilichukua muda, au sio…hadi kuamua kunifuatilia na kufika kwa wakati muafaka..naona kama…’nikasema bila kumalizia.

‘Nilichukua pikipiki, nikitaka nikuwahi….wewe ulitumia usafiri gani,…?’ akaniuliza

‘Bajaji…nilikodi bajaji…likaniacha mbali kidogo na ufukweni…, nikawa natembea nikiitafuta hiyo sehemu…, sikutaka huyo mtu anishuku…’nikasema.

‘Ndio maana nikafika wakati muafaka kwa pikipiki…’akasema.

‘Kwahiyo huyo aliyeniumiza mimi kichwani ..ndio huyo Chizi…?’ nikauliza.

‘Hapana…’akasema na kunifanya nibakia na mshangao

‘Sasa ni nani huyo…?’ nikauliza
‘Unajua yaonekana huyo mtu kwa muda mwingi alikuwa akikufuatilia, kila unapokwenda, na hukuwa makini kwa hilo…’akasema

‘Haiwezekani,…ni nani huyo anifuatilie…?’ nikauliza

‘Huwezi amini , ni babu yako….’akasema.

‘Mzee mtupe, kwa nini afanye hivyo ..?’ nikauliza.

‘Ni hadithi ndefu, wewe malizana na matibabu, maana hivi sasa sisi tunakimbizana na watu wa benki, leo ndio siku yao ya mwisho, tusipowakilisha ushahidi wetu, basi, hakuna jinsi, ni lazima mnada ufanyike….’akasema.

‘Kwahiyo ushahidi mnao, au....?’ nikauliza na huyo mpelelezi, akatabasamu tu, na muda huo akaingia docta,, akingia na mwingine na kigari cha kukukota

‘Tunataka kumchukua mgonjwa wetu, tunaomba mtoke…’akasema docta

‘Kunichukua kwenda wapi..?’ nikauliza

‘Chumba cha upasuaji…’akasema docta
Hapo nikaanza kuhisi vibaya, ni heri wasingeliniambia, nikahis huenda tatizo hilo ni kubwa sana…labda kichwa imepasuka hadi kuathiri ubongo..nikawa nawaza sana.

‘Usiogope…hilo tatizo sio la ndani…’akasema docta

‘Oh, sasa kwanini upasuaji…?’ aliyeuliza ni mama mjane.

‘Samahanini, naombeni mtoke nje…’akasema docta, akiwaambia mpelelezi na  mama mjane, na wawili hao wakatoka nje.., kiukweli sikuwa na amani kabisa…niliona nina jukumu kubwa la kufanya.

‘Docta, kwani haya maumivu hayawezi kupata dawa, yakatulia, ili nikafanya kazi moja muhimu sana, kwanini mpaka nifanyiwe upasuaji, kuna nini , niambieni…?’ nikamuuliza

‘Kuna tatizo kidogo…kuna damu zimevilia kwa ndani..ni kidogo tu, kwa juu, , tunahitajika kufanya upasuaji kidogo…ni sehemu nyeti, tukiachia hivyo, inaweza kulete matatizo..’akasema na muda huo tulishafika chumba cha upasuaji.

‘Nini…haiwezekani docta..hapana…hamuwezi kuahirisha, mimi nina ushahidi muhimu wa mahakamani, nisipokuwepo, kesi …tutashindwa na haki za watu zitapotea bure, hao wapelelezi hawajui kitu bado…,’ nikasema na sikuweza kumalizia, mara nikazama kwenye usingizi mnzito , kumbe alishaweka dawa ya nusukaputi.

**************

Ilikuwa sasa nipo chumba cha wagonjwa wa kawaida,..bahati nzuri siku hiyo alikuja mpelelezi kunitembelea….tukasalimiana, baadae akasema

‘Leo tunakueleta mgeni maalumu …docta anasema hali yako ni nzuri, ila bado huwezi kupewa ruhusa…’akasema

‘Mgeni gani..lakini kwanza nataka kujua kinachoendelea,…?’ nikauliza

Na wakati huo mpelelezi alikuwa akiangalia mlangoni, kwani mlango ulifunguliwa, na wakaingia askari wawili wakiwa wamemshikilia jamaa kati kati…huku kafungwa mnyororo…huku na huku…

‘Aaah…naumia ..naumia, nitasema ..nitasema kila kitu…’huyo jamaa akawa analalamika , akionyesha dalili za kupata maumivu, na aliponiona tu, akaacha kulia, na kusema;

‘Ni wewe….hahaha…aaah,…ila..ooh,  naumia jamani, wewe ndio tiba yangu ,unaona sasa nafuu, ..aah, imeanza tena,…, hapana,…niacheni, .. nisamehe..nisamehe..ni kweli..ni mimi, ni mimiii…’jamaa akawa anahangaika, lakini askari wake walimshika imara, huku wamemfunga na mnyororo.

‘Vipi mbona mnamfanya hivyo,..hamuoni kuwa mnamuumiza…’nikasema.

‘Tukimuachia hapa, ataumiza watu….na tumemleta hapa kwasababu anasema bila ya kukuona wewe na mama mjane, hataweza kupona, nyie ndio tiba yake….’akasema.

‘Kwanini….mbona mimi simjui huyu mtu, …kwani yeye  ni nani …?’nikasema, nikiuliza.

‘Mimi nakujua sana wewe, nakujua, akufahamu, nakuelewa, na najua unachokitaka…niakuambie, hapo ulipo unawaza nini…unajiuliza mimi ni nani, au sio, hahaha, najua mimi kweli si kweli……’akasema akihema kama mtu aliyekuwa anakimbia, sasa akiwa kanikodolea macho.

‘Uliniona wapi..?’ nikamuuliza nikionyesha ishara ya mshangao.

‘Siku ya kwanza ulipofika kwa mama mjane, mimi nilikuona, unajua, ulifika, kwa mapenzi ya mungu, ila mimi nikajua..…hahaha na mama mjane…, mama mjane yupo wapi sasa…nimewaambia nini…?’ akauliza akimuangalia  mpelelezi,
Mpelelezi.. akasema

‘Muiteni mama mjane aingie ndani…’akasema mpelelezi.

Mara mama mjane akaingia…alionekana alikuwa analia…nikataka kumuuliza analia nini, lakini huyo mjamaa akaniwahi

‘Mama mjane…haaaa …nisamehe jamani…’, sasa akawa kama anamfuata huyo mama wale maaskari, wanaonekana wana nguvu, walivyojazia, .. wakawa wamemshikilia imara. Nilitamani kuwaambia wamuachilie tu,  lakini huenda ni kwa usalama. Baadae huyo mtu akanigeukia,…

‘Wewe mimi nakufahamu sana…, nilikuona, kila siku mimi nakuona,…ulivyojiingiza kwenye mambo yasiyokuhusu…ungeshakuwa maiti wewe….hahahaha… ila..hahaha, wewe ni mjanja , unajua mimi mungu kanipatia kipaji, cha kuona hata visivyoonekana,  na kusikia, saana, lakini sasa..’akageuka kumuangalia mama mjane, halafu mimi..

‘Nimegeuka kuwa shetani…nimevitumia vibaya…sasa nakula jeuri yangu….hahaha, jamani,….mama mjane nisamehe…sina uwezo tena, wa kumrejesha….duniani, oooh, nitakwenda kukutana naye…nina uhakika atanisamehe….khaaah, …khaaah…’akawa kama anakabwa, na mdomoni kunatoa damu.

Baadae akatulia.. docta akachukua kitambaa na kumfuta mdomoni, na akawa kama hataki, baadae docta, akamuacha, jamaa akasema;…akiniangalia mimi…

‘Wewe kwa mara ya kwanza nilikuona, ukiingia kwa mama mjane nikajua wewe utakuwa ni adui yangu namba moja, wewe ni mjanja sana, , …hahaha, hapana nitasema,…kila kitu, msiniunguze jamani… naungua, moto, moto…haah, msininunguze nitasema..’akawa analalamika hivyo kuashiria  anateseka kweli...

‘Mama mjane…naomba unisamehe..’akasema akimuangalia mama mjane ambaye alikuwa kimia, kakaa pembeni ya kitanda, nilicholala mimi…, nikamuangalia mama mjane, mama mjane alikuwa akimuangalia huyo jamaa kwa uso wa huruma…chuki, machozi yanamtoka…hata huwezi kujua lipi ni lipi.

‘Najua nimewakosea sana…kwa ujumla wenu,…nawaombeni mnisamehe, ili nife kwa amani…sistahiki kuishi tena …mimi sio binadamu wa kawaida,..mimi ni shetani…’akasema akionyesha meno nje.

‘Mhh, haya niambie,..kama kwa kuniambia hayo unayotaka kunieleza inaweza kusaidia ….wewe kutokupata taabu hiyo uliyo nayo…maana bado mimi sijajua unataka kuniambia nini, na kipi kilichokusubi, na wewe ni nani…..je ni kuhusu deni la marehemu.’nikasema, na kuuliza.

‘Wewe ulinifuata nini kule ufukweni, kwanini, eeh, ulitaka ninywe damu yako, nimechoka kunywa damu za watu, eeh, niambie wewe,..…eeh, ?’ akaniuliza akinikodolea macho

‘Ina maana ni wewe …’nikakatisha maana niliona akitolea macho kama kaona kitu cha kutisha..halafu ghafla…

‘Hahahaha…eti wao wananiita mimi nani vile.....mimi sio hivyo, wanavyoniita, hawa wanaonitesa sasa ndio mizimu halisi...ndio nyie ndio halisi...yaah, ni kweli , mimi  ni …ni mtaalamu, ndio jamani ndio mimi...'akatulia kama anasikiliza


'Ndio, nawaambia kuwa…mimi ndiye mtaalamu halisi,..hahaha, …ni ni…ba-ba-bu, mimi sina baba, yeye si alinikataa,....ndio...ba-ba-bu... mlitaka mimi nifanye nini sasa…hahaha,….niache, haya niunguzeni nife kabisa..., kwanini mnanitesa hivi,….ni ba-ba, mbona hamsemi ma-ma, alimfanya nini mama, ndi-ndio…….…hahaha, …hahahaha…hahaha…’jamaa, akaendelea kucheka kucheka, kucheka…mpaka anaishiwa nguvu.

Ikapita muda, ..jamaa akafungua macho, mdomo, upo wazi kwa jinsi alivyokuwa akicheka, nikama mdomo umaganda…hauwezi kurejesheka tena.

‘Ndio hivyo, anateseka kweli…’aliyesema hivyo alikuwa ni mpelelezi

Docta akasogea pale na kujaribu kuufunga mdomo wa huyo jamaa, akawa anaukwepesha huyo jamaa, na docta akafanikiwa kuufunga huo mdomo, jamaa sasa akawa anajinyonga nyonga kuashiria maumivu…

Ukimuangalia utamuonea, huruma nikaona nipoteze mawazo, nikamgeukia mpelelezi..

‘Sasa ..mumefikia wapi…?’ nikauliza

‘Hawawezi kushinda hiyo kesi bila ya mimi….nimewaambia….haaah, hapana, nitasema kila kitu..yayayaya, naungua jamani….nitasema, ndio..wapi, mahakamani, ndio..nitasimama, na nani, …mtaalamu, …kafa ndio…nimebakia mimi, na nani, hapana hahusiki...nani, ba-ba-bu…ndio mleteni, na nani mwingine,.haya, nitasema, nipeni nafasi hiyo,..yaaah, siwadanganyi tena,..sawa...sawa...ndio..aakkaaaaa …hahaha, ..’sasa akawa anajinyonga, ..na ghafla, akatulia, akalegea,…anataka kudondoka, ikabidi wamshikilie…

Ikapita muda, jamaa sasa wanashindwa kumshikilia huyo jamaa, maana kalegea..docta akamsogelea, akamshika kumpima….akasema;

‘Kapoteza fahamu…’akasema docta

NB: Ni NINI HIKI TENA…

WAZO LA LEO: Ogopeni sana duwa ya mwenye kudhulimwa, ole wenu,…yule anayemdulumu mja wa mungu, …huwezi jua ni nini kisasi cha duwa hiyo kitakuandama, na mola wetu, huwa anatupatia nafasi nyingi sana za kutubia, lakini tunapuuzia, tunajiona sisi ni wajanja…Haah, ujanja kwa jasho la mtu, ujanja kwa haki ya mtu,…halafu unadhulumu hata mayatima,…

Tumuombe mola wetu, atuongoze kwenye njia sahihi, tuwe waadilifu, tuishi kwa jasho letu, …
Ni mimi: emu-three

No comments :