Friday, September 7, 2018

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-45


Mimi bado nikawa hospitalini, na nilikuwa nasubiria vipimo vya mwisho, ili niruhisiwe,…kichwa kilikuwa bado kinanisumbua, na docta ndio akaamua nichukuliwe vipimo vingine waone tatizo lipo wapi.

Na muda huo nikiwa hapo hospitalini, akili yangu ilikuwa haitulii, kwani nilikuwa nasubiria maelezo ya kesi ilivyokuwa, lakini siku hiyo hakuna aliyetokea, baadae nikapata ujumbe wa simu kutoka kwa mama mjane kuwa hali yake sio nzuri, kashindwa, kuja..

‘Nisamehe sana kaka, lakini nahisi sipo vizuri, ila siumwi tu, naona nikija hapo hospitalini nitaishia kulia, nikiwa mbele yako nadeka sana…’akaandika, hivyo, ikabidi nimpigie simu, alipopokea nikahisi kama anataka kulia, kabla sijasema kitu akaanza kwa kusema;

‘Kwani nini umenipigia, waona sasa natakani kulia…’akasema kweli akiwa kama anataka kulia.

‘Kwani imekuwaje huko mahakamani, leo naona nyote hakuna hata mmoja aliteyaka kuja kunielezea, kulikoni..?’ nikamuuliza.

‘Hakuna tatizo, ni kuchoka tu,..na jinsi ninavyojisikia, nikaona nipumzike kwanza, nitakuja kesho tukijaliwa, na wale maaskari, kuna vitu wanafuatilia, nahis ndio maana wameshindwa kuja huko…’akasema.

‘Najua wewe haupo vizuri kutokana na hiyo kesi, au sio..?’ nikamuuliza.

‘Aaah ,… hayo ya kesi sasa aah…, nimeshamuachia mungu,…wao wanafikiri wakimsingizia mume wangu uwongo ndio wameshinda, hawawezi kushinda kihivyo, na hata kama watashinda kesi, basi hawajashinda mbele ya mungu,…’akasema
‘Ni kweli, hata hivyo mimi sizani kama watashinda hiyo kesi,..usijali, kesi safari hii itahukumu kwa haki, …’nikasema.

‘Hahaha, Usijali,…utafikiri nacheka kufurahi, unajua alichosema hakimu, ..hadi sasa hajaona ushahidi wa kumshawishi, kuwa hilo deni sio sahihi kwa marehemu, ..ina maana ushahidi wa benk bado una nguvu..’akasema.

‘Ni nani aliongea jana..?’ nikamuuliza.

‘Si huyo chizi wanayemuita chizi, sijamuelewa bado , yeye ni nani..lakini kila hatua naanza kumfahamu…sasa sijui kama ni kweli aliyoyaelezea au kajitungia…’akasema

‘Alisemaje kwani..?’ nikauliza.


‘Eti deni hilo deni, ni la kweli na ni deni la marehemu..’akasema.

‘Alitamka hivyo hivyo ulivyotamka wewe…?’ nikauliza.

‘Hata kama katamka vingine lakini alikuwa na maana hiyo..’akasema.

‘Unaweza kurejea maneno , kwa jinsi alivyotamka yeye…?’ nikamuuliza na hapo akatulia kidogo kama anawaza, halafu akasema;

‘Aliulizwa hilo deni ni la marehemu, yeye akasema hivi… ‘Kwa jibu la haraka ni KWELI…’akasema.

‘Hivyo tu..?’ nikauliza.

‘Ndio, mengine ni mawakili waliongezea wakikariri kauli yake hiyo…’akasema.

‘Kwa neno hilo …’kweli’  bado sio uthibitisho kamili, kuwa kweli kakubali kuwa ..hilo deni ni la marehemu,…yategemea ni nini atakuja kuongea baadae, bado, nategemea mengi kutoka kwake kama kweli anaongea kwa nia ya kutubia…’nikasema.

‘Mhh, mimi nimeshakata tamaa…’akasema.

‘Kwanini ukate tamaa, sib ado kesi inandelea, bado Dalali, hajaitwa, hujui atakuja kusema nini,..vipi mzee Mtupe, hakuitwa kuendelea kuhojiwa…?’ nikauliza.

‘Hapana..nashangaa maana alikuwa hajamaliza…’akasema.

‘Unaona, huo ni mtindo wa huyo wakili, atarejeshwa tena, kukubali, baadhi ya mambo, na baada ya hapo, itakuwa ni nafasi ya hakimu kuunganisha ushahid wote ili aweze kuhukumu…’nikasema.

‘Haya …ni kwa vile wewe hukuwepo mahakamani..ungelikuwepo ukasikia …hasa kauli ya hakimu, ungelijua kuwa kweli kesi, hapo upande wetu,..nahis itakuwa kama ile safari ya kwanza…’akasema

‘Ni kuulize wewe, kutokana na hayo maelezo ya huyo shahidi, bado unaamini kuwa deni kweli sio la marehemu..?’ nikauliza.

‘Mimi licha ya….sisemi kwa vile nataka nyumba, hapana naongea kutoka moyoni, hilo deni sio la marehemu mume wangu…nahis kuna njama zimepangwa…na najiuliza kumbe ni njama za wanandugu..’akasema.

‘Ukiwa na maana mzee mtupe, mtaalamu na yule mtoa vibali,..lakini wao, hawajaongelewa kuhusiana na hilo deni au sio, wao waliongelewa kuonyesha jinsi gani watumisi waliopewa dhamana wanavyoweza kugushi, ..au kutoa vibali isivyo haki, au sio…’nikasema.

‘Lakini hapo tunazungumzia benki,…’akasema mama mjane.

‘Enzi hizo, hiyo benk, ilitawaliwa na watu wasio waaminifu…kama watu wa vibali, kama watu waliopewa dhamana wameweza kufanya hivyo, ..hata huko benki kunawezekana, na imethibitishwa kuwa walikuwepo watu wasio waaminifu, ndio maana wakawafukuza..huo ushahidi kuwa lolote liliwezekana kutendeka, kwanini walifukuzwa…’nikasema.

‘mhh..banki wao wanataka ushahid wa makaratasi,…’akasema.

‘Na hakimu je…?’ nikauliza.

‘Sijui yeye, atasimamia wapi…’akasema.

‘Yeye atasimamia kweli ukweli na haki…ataunganisha ushahdi wote, na kuliangalia tukia zima…na…nikuulize tu, huyo shahidi aliongea nini zaidi…?’ nikamuuliza.

‘Alielezea maisha yake, yeye alipotokea, na sana sana alimuelezea mama yake,  kumbe mama yake alizalilishwa, na kubakwa, ..na yeye ni matokea ya huko kubakwa,…’akasema

‘Oh…inasikitisha si ndio hivyo…?’ nikauliza.

‘Kiukweli inasikitisha sana, lakini mume wangu anaingizwaje huko, yeye sio aliyemzalilisha huyo mama yake, na …nakumbuka mume wangu aliwahi kuongea kitu kama hicho…’akasema.

‘Alikuambiaje..?’ nikauliza

‘Yeye alikiri kuwa zamani, mdogo wake huyo aliwahi kufungwa, kisa ni kwa vile alisadikiwa kuwa alimbaka mfanyakazi wa ndani, lakini kumbe mfanyakazi huyo wa ndani alikuwa muhuni…sasa hivyo ndivyo mume wangu alivyokuwa akifahamu,..alikuwa hajui undani wa tukio lenyewe..’akasema.

‘Ilitokeaje mpaka akaongea kuhus mdogo wake kufungwa…?’ nikauliza

‘Nakumbuka tulikuwa tunaongea maswala…mmh, ndio..ilikuwa kipindi namuonya kuwa asimuamini sana ndugu yake kwenye maswala ya benki, na yeye akawa anamtetea sana…’akasema.

‘Ilikuwaje mpaka ukaongea hilo…nahis hapo kuna jambo, hebu kumbuka vyema…?’ nikauliza

‘Ilikuwa tunahitajia pesa,…na ilikuwa ni jambo la haraka, akasema, ndugu yake akimbie benki akamchukulie, na ..muda ulishapita,…akasema yeye ndugu yake akienda, kama bado wafanyakazi wapo ndani, akimpigia simu..mtu mmoja, atamruhusu ..na atachukua hizo pesa…’akasema.

‘Huyu mtu ni nanii…?’ nikamuuliza.

‘Hakumtaja, ila alisema huyo ndugu yake ana namba yake…’akasema.

‘Ok..ok…sasa kwanini wewe ukaingiza maneno ya kumtahadharisha mumeo dhidi ya ndugu yake…?’ nikamuuliza.

‘Kuna mambo mengi…yakitaka uwepo wake, anasema ndugu yake amfanyie…’akasema.

‘Mhh..na sahihi yake je…?’ nikauliza.

‘Anaweza kumwambia lete hapa niweke sahihi, anaweka sahihi hata bila kusoma kilichoandikwa,…’akasema.

‘Lakini …hata kama hakusoma kilichoandikwa, lakini yeye si anafahamu ni jambo gani, linalohitajika labda, ..hata akiweka sahihi yake, bila kusoma haitamuathiri kitu…’nikasema.

‘Hapo nimechukulia mfano tu,,….wakati mwingine aliongea na watu wa benki, huyo ndugu yake akachukua pesa, na yeye mume wangu ndio akaenda au akaja kujaza karatasi ya kuchukulia pesa,…kifupi ni kuwa alimuamini sana ndugu yake…’akasema.

‘Hebi nikuulize wewe, kwanini wewe ukatilia shaka hilo,…wewe si umeishi naye huyo shemeji yako..unamfahamu matendo yake, kwanini ukamtilia shaka..?’nikamuuliza.

‘Kiukweli kuna matendo ..ya uhuni, anayo tu..uwongo ..anao tu..lakini anajua kuigiza, hasa akiwepo kaka yake, anajiigiza unyenyekevu, uaminifu, utafikiri mcha mungu fulani, lakini kwa mimi ninayemfahamu kwa vile nipo naye karibu …na mara nyingi, naona matendo yake…simuamini kama anavyomuamini kaka yake…’akasema.

‘Samahani lakini…ulisema aliwahi kukutaka kimapenzi, ukagombana naye,..je hiyo yaweza kuwa ni sababu ya kutokumuamini, kivile…au?... maana kama anataka kumuibia hata ndugu yake..mkewe, atakuwaje muaminifu si ndio hivyo..?’ nikamuuliza.

‘Hiyo kwangu niliidharau..nilijua ni ujana tu..sema niliposikia hayo maelezo ya huyo shahidi ndio nime..mshusha sana, naamini sio ujana tu……kama ndio yeye alimfanyia mama yake huyu shahdii matendo hayo machafu, ..sitaweza kumuamini tena…’akasema.

‘Ok…sasa, huyo shahidi kwanini alipize kisasi kwa mume wako…kwa jinsi ulivyonielezea awali, ni kama huyo shahidi alifanya mambo kwa kulipiza kisasi, japokuwa hatujaona ni nini alikuja kufanya…na..huyu mtu ni nani …nikiwa na maana…’nikatulia nikiwaza.

‘Anasema katika sehemu ya pili ndio ataelezea jinsi ya hilo deni….’akasema mama mjane

‘Sawa, ngoja tuone ukweli wake…lakini mhh…bado sijamuelewa,…yeye alikuwa akifanya kazi wapi…maana nijuavyo mimi, mtu ambaye …nahisi …aliyekuwa banki, ni huyo ambaye hadi leo hajapatikana..sasa huyu mtu..kichaa ni nani…?’ nikauliza.

‘Hadi hapo alipofikia, hajajifichua vyema, sijui kwanini mawakili hawajataka kumfichua, nahisi ni katika namna ya kujilinda au kumlinda huyo shahidi maana kesi inaendelea, je wakimuua, …au wanafanya hivyo,… kulinda ushahid mkuu, ambao, nahisi watakuja kuutoa baadae..’akasema

Exactly…upo sahihi…japokuwa mimi bado, namuweka Dalali mbele, kama mshukiwa mkuu, sijui kwanini..’nikasema.

‘Mshukiwa mkuu wa nini..?’akauliza mama mjane.

‘Wa hilo deni, ajali iliyosababisha kifo cha mumeo,…ikiwa na maana, yeye anafahamu undani wake..hiyo hali ya kuigiza anaumwa,..hawezi kutembea, kwanini afanye hivyo…unaona, kwanini, kwanini… hizi ‘kwanini’ bado zinanifanya nimuone mshukuwa ni yeye, akisimamishwa, kesi itakuwa…’nikatulia maana simu yangu iliashiria, mtu anapiga.

‘Kuna nini…?’ akauliza mama mjane.

‘Kuna mtu ananipigia, tutaongea baadae, ..’nikakata simu na kuangalia mpigaji wa simu,…ilikuwa ni namba ya yule mdada wa kule alipolazwa Dalali…

Nikasita kumpigia, sikutaka kuingiza mambo mengi kichwani, na hapo tu, kichwa kilishanza kuuma, na wakati nataka kuiweka simu nipumzike,… mara hiyo simu ikaanza kuita tena,… nikapokea tu,namba ilikuwa ni ile ile…

‘Pole sana, nasikia bado unatibiwa, vipi unaendeleaje..?’ akauliza.

‘Sijambo, huenda nikaja kuruhusiwa,…’nikasema

‘Mhh…vipi kuhusu hiyo kesi yenu inaendeleaje..?’ akauliza.

‘Bado inaendelea,…mimi sijawahi kufika huko,… vipi kwani kuna ushahidi unataka kuutoa au…?’ nikamuuliza.

‘Nataka nikutumie picha ya video, kuthibitisha kauli yangu,…’akasema.

‘Kuthibitisha kauli yako, ipi hiyo…?’ nikamuuliza.

‘Kuwa mtu wako anaweza kutembea, na ni mwanga, mchawi, nilikuambia hivyo..’akasema.

‘Lakini hadi sasa akitembea si ndio anachukua mazoezi, kwani hadi sasa hajaweza kuinuka, au kutembea..?’ nikamuuliza

‘Kwa maelezo ya madocta, bado…bado hawezi kutembea na madocta wanasema hivyo hivyo kuwa huyo mtu ni wa kuhudumia kitandani, hawezi hata kuinuka mwenyewe…’akasema.

‘Alitembea akienda wapi, ulivyomuona….?’ Nikamuuliza.

‘Kama siku ile….na nikaamua kumfuatilia mimi mwenyewe…’akasema.

‘Wewe haikukutokea kama ilivyotokea kwa mlinzi..?’ nikauliza.

‘Mimi hawaniwezi…nilimfuatilia,…akawa anatembea hadi barabarani, hapo akaita pikipiki, ikamchukua hadi baharini..’

‘Hadi baharini, kufanya nini…!!!?’ nikamuuliza

‘Mimi nikachukua pikipiki pia, tukawa tunamfuatilia, huyo dereva wa pikipiki akafika sehem akaniambia anaona maajabu, nikamwambia aniachie mimi niendeshe,…’akasema

‘Ndio mkafika baharini, ikawaje..?’ nikamuuliza

‘Yeye….akafika sehemu pale alipokuwa anakaa chizi…akaangalia huku na kule,…alipoona hakuna mtu, akaanza kuondoa maboksi yaliyokuwa yamelazwa aridhini, kama kitanda…sasa kwa bahati, kukatokea watu…akayarudisha kwa haraka, …baadae akaanza kurudi…’akasema.

‘Hiyo sehemu waweza kuikumbuka vyema…?’ nikauliza.

‘Ni pale ofisi kwa yule Chizi, unajua watu wanaogopa kufika eneo hilo,..kila aliyefika hapo anakutwa na majanga, kwahiyo ni sehemu imejitenga kihivyo…’akasema.

‘Wewe je…?’ nikamuuliza
‘Nifuate nini sasa…mimi nilitaka kuhakiki hilo jambo, kuwa huyo mtu anatembea lakini anakwenda wapi, mengina hayanihusu, ..sasa waitaka hiyo video nikutumie au niache tu, maana sijui kama itasaidia kitu…’akasema.

‘Nikuulize tena,..ni nani bosi wa hiyo hospitali..na je ni kweli yupo nchi za nje..?’ nikamuuliza.

‘Nakutumia…’akakata simu na haikupita muda,aakatuma hiyo video..

************
Kesi likuja kuanza siku nyingine, na shahidi yule yule akaitwa,…

‘Vipi khali yako…?’ akaulizwa na hakimu mwenyewe

‘Naendelea vizuri, haijatokea tena ile hali, nahisi naelekea kuzuri…’akasema

‘Unahisi ni kutokana na jinsi ulivyoongea huo ukweli,..?’ akaulizwa

‘Ndio muheshimiwa hakimu, nataka niongee kila kitu ili haki iweze kutendeka..’akasema

Hakimu akawageukia mawakili,…

‘Je bado mna maswali ya kumuuliza..huyo shahid kabla hajaingia sehemu ya pili ya maelezo yake, ila..shahdi usipoteze muda na maelezo mengi ya maisha yako, sisi tunataka kile kinachohusiana na hii kesi…’akasema hakimu.

Mawakili wakasema aendelee tu na sehemu ya pili, lakini kabla hajaendelea wakili wa kutetea madeni akasema;

‘Samahani kidogo…nataka kufahamu, jambo moja kabla hujaanza maelezo yako,.. wewe unasema kuna mmoja wapo wa watu ambao hukutaka kuwataja, ulidai yeye alitumia pesa zake kuwarubuni watu watoe ushahdi dhidi ya mama yako…’akasema na kabla hajauliza hilo swali shahidi akasema;

‘Mimi nimenukuu alivyoandika mama, kuwa, huyo jamaa ndiye alitumia pesa zake kumtetea ndugu yake, huku akijua kakosea, huku akijua kuwa ndugu yake alimpa mimba huyo mfanyakazi wao wa ndani....hakutaka kuulizia zaidi kuufahamu ukweli, hta pale mama alipotaka kujielezea…’akasema.

‘Wewe mwenyewe unamfahamu vyema huyo mtu, marehemu…?’ akaulizwa.

‘Ndio…nimewahi kukutana naye na hata kuongea naye…’akasema.

‘Alikutambua kuwa wewe ni mtoto wa huyo mama…?’ akaulizwa

‘Hapana..nilipokwenda kusoma, nilihakikisha narudi kivingine,..hata sura yangu ilibadilika, na hata hawa wazee, yule msamaria wa kwanza muuza dawa,, ..ambaye sasa ni marehemu alikuja kunifahamu baadae sana, baada ya kuamua kumwambia,..ndio hapo akaanza kujipendekeza kwangu,. Akasema yupo tayari kunisaidia kulipiza kisasi..’akasema.

‘Lakini wengine hadi leo hawajakutambua..au na wao walishakutambua?’ akauliza.

‘Mhh…nitakuja kuliongea hili, kwenye sehemu ya pili kama hutojali…’akasema

‘Nataka kuwa na uhakika tu, ..jinsi ulivyomuona huyo unayesema alitumia pesa zake kumtoa ndugu yake, na akafanya hadi ndugu yake ashinde kesi, je kweli anaweza kufanya tendo kama hilo..?’ akauliza

‘Najua una maana gani, lakini nataka kauli yako isikike..una maana tendo gani hasa..?’ akauliza.

‘La kuwarubuni watu ili watoe ushahidi wa uwongo..?’ akaulizwa.

‘Kiukweli..hafanani hivyo, na sijasema yeye aliwarubuni, hapo sina uhakika hata mama hakuandika hivyo, aliandika kuwa, yeye alikuwa tayari kutoa pesa zake, ushahdi upatikane, bila kujali kuwa ushahid huo ni wa halali au la…kwa kipindi nilichomfahamu mimi,..huyo jamaa, marehemu,..ni mtu mwema, mkweli..na watu wanamsema hivyo …’akasita wakili wa benk aliingilia kati.

‘Usiseme hisia zako, ongea ukweli ulivyo..’akaambiwa

‘Ukweli ndio huo…yupo hivyo ni ,mwema, sasa ni kwanini alijiingiza huko, mimi hapo siwezi kuelewa…’akasema.

‘Watu wanasema yeye hakufahamu lolote lililotokea kati ya mama yako, na huyo baba yako..yeye alielezewa kivingine, ..unavyomfahamu baba yako, yeye ni mjanja sana, yeye alitunga maneno ambayo yalimjaza hasira huyo kaka yake na kuamini kuwa mama yako alikuwa hivyo…’akaambiwa.

‘Mimi nategemea sana alichoandika mama yangu, mama yangu namuamini sana, sio muongo, waliomfahmu vyema wanaweza kulithibitisha hilo..sasa kama alichoandika kina uwalakini,..mim sijui..kwangu mimi huyo na mdogo wake, wote sawa tu…’akasema

‘Katika maelezo yako..aliyefanya hivyo, kumdhulumu mama yako na hadi akafikia huko, ni huyo baba yako, lakini hadi sasa tunayeona kuathirika na kisasi chako, ambacho japo hujaanza kukuilezea, ni ..kaka mtu,…’akaambiwa.

‘Hahaha, huyo baba yupo wapi…?’ akauliza.

‘Hujatuambia baba yako ni nani…’akaambiwa

‘Kutokana na maelezo, yangu, nisingelipenda kuwataja hao watu majina kwa hivi sasa, ila..huyo baba,..kwangu mimi sio baba, kwani alinikataa, alimtesa mama yangu,…atapata taabu sana ,..na yeye mwenyewe atahitajika kuja kutubia hapa mbele..najua hadi sasa anakana…anasema sio kweli, sio yeye…ngoja tuone,…’akasema

 ‘Je hiyo sehemu ya pili, itaeleza lolote kuhusu hilo deni, maana wewe haujathibitisha kuwa kweli hilo deni ni la marehemu au …la…’kabla hajamaliza wakili wa benki akasema;

‘ Keshasema bwana…na tunaimani hiyo sehemu ya pili utaelezea, jinsi deni lilivyotoka kisheria,…hapo ndio tutajua kuwa kweli umepona..na ushahdii wako hapa una uzito..’akasema wakiliw a benki

‘Naombeni mnipatie nafasi…kwani nahisi hali si nzuri sana..nahisi kuna kitu kina..kuna matu anataka kuharibu ..lakini hataweza…’akasema

‘Mtu gani…?’ akauliza

‘Mhh…, sehemu ya pili,..nitakayo elezea hapa,.. itatoa ushahidi wangu…ambao ndio ukweli kuhusu hilo deni…’akasema shahidi.

‘Kuwa ni la marehemu au sio…’akasema wakili wa benk.

‘Kuwa kweli limepewa marehemu kwa kulipiza kisasi,…’akasema wakili wa kutetea madeni na huyo shahidi akatabasamu kidogo, halafu akasema;

‘Wote mpo sahihi,..naomba niendelee…’akasema.

‘Endelea, jaribu kwenda kwa haraka…’akasema hakimu.


NB: Je hilo deni ni la kweli kwa marehemu..….TUTAENDELEA

WAZO LA LEO: Toba ya kweli ni tiba,...tiba ya maradhi ya nafsi, na hata maradhi ya mwilini, na pia ni tiba ya matatizo...kuna matatizo mengine,sababu yake kubwa ni dhuluma. 

Ni mimi: emu-three

3 comments:

  1. Do you have any video of that? I'd want to find out more details.

    ReplyDelete
  2. For most recent news you have to visit web and on world-wide-web I found this web page as a most
    excellent site for latest updates.

    ReplyDelete
  3. This is a great tip particularly to those new to the blogosphere.
    Brief but very accurate information… Thanks for sharing this one.
    A must read article!

    ReplyDelete

Changia hoja kwa kutoa maoni yako hapa: Au tuma kwa e-mail> miram3.com@gmail.com